UTANGULIZI
Lugha ya Kiswahili ni moja ya lugha zenye asili ya Afrika ambazo zimefikia upeo wa kutumiwa kama lugha za kiutandawazi ndani na nje ya bara la Afrika. Kiswahili kinatumika kama lugha ya taifa katika mataifa mawili ya Afrika Mashariki; Tanzania na Kenya.Katika ulimwengu wa teknolojia pia Kiswahili kinatumika kama lugha ya kiteknolojia. Kwa ujumla, Kiswahili kimepaa na kuwa lugha yenye watumiaji wengi zaidi kuliko lugha nyingine yenye asili ya kiafrika.
Chimbuko ni neno linalorejelea mahala kitu kilipoanzia. Tunapoangazia chimbuko la Kiswahili tunajikita kutaka kujua ni wapi hasa (kijiografia) Kiswahili kimetokea.
Neno asili lina maana ya jinsi au namna kitu kilivyotokea. Tunapoangalia asili ya Kiswahili tutakuwa tunazingatia namna Kiswahili kilivyoanza.
KUNA NADHARIA NNE (4) ZA CHIMBUKO NA ASILI YA KISWAHILI
1. KISWAHILI NI KIKONGO
Wanahistoria wanasema wabantu walihama kutoka katika misitu ya Kongo ambako ndio chimbuko lao. Inasemekana kuwa walikuja na lugha yao ambayo ndicho Kiswahili. Wabantu kutoka Kongo walisambaa katika sehemu mbalimbali za Afrika ikiwemo Afrika Mashariki hadi wakatika pwani. Shughuli za kibiashara,ufugaji,kilimo na vita ndio sababu za kuhama kwao.
UDHAIFU WA NADHARIA HII
ü Hakuna uthibitisho wa lini hasa wabantu hawa walihama kutoka Kongo kuja pwani ya Afrika Mashariki.
ü Lugha huwa imara na thabiti zaidi kule ilikoanzia kuliko kule ilikopelekwa.
ü Kiswahili cha Kongo ni dhaifu kimatamshi na kimsamiati ukilinganisha na kile cha pwani ya Afrika Mashariki.
Hii inathibitisha kuwa Kiswahili hakikuanzia Kongo bali kilipelekwa.
2. KISWAHILI NI PIJINI NA KREOLI
Pijini ni lugha ya kati inayozuka baada ya lugha mbili zenye asili tofauti zinapokutana kimatumizi. Pijini huweza kuzuka mahala ambapo kuna makundi mawili au zaidi na kila kundi likiwa na lugha yake. Ili kurahisisha mawasilano lugha hizi huchanganyika na kuingiliana. Jambo hili huweza kusababisha kuzuka kwa lugha ya mchanganyiko ambayo inaeleweka na makundi yote mawili. Hivyo pijini huwapa watu hao uwezo wa kuwasiliana.
Kreoli hutokea pale ambapo watu wanaozungumza pijini wameishi pamoja, wamezoeana na kuoana, kisha wamezaa watoto. Sasa watoto wanakuta pijini ikizungumzwa kama lugha ya wazazi wao. Kwao hao watoto hii itakuwa lugha ya kwanza. Ikifika hatua hii, lugha hii huitwa krioli.
Wanaoshikilia nadharia hii wanadai kuwa Kiswahili ni Pijini ambayo ilikoma na kuwa Kreoli. Wanasema, ujio wa Waarabu katika pwani ya Afrika Mashariki ulipelekea kuundwa kwa lugha ya kati (pijini) ambayo ilichanganya Kiarabu na Kibantu. Baada ya maingiliano ya kiutamaduni ikiwemo kuoana baina ya waarabu na wabantu vizazi vilivyofuata vilitumia pijini hiyo kama lugha yao ya kwanza. Ikawa Kreoli. Hivyo ndivyo Kiswahili kilivyoanza. Kwa hiyo Kiswahili ni Pijini na Kreoli ya Kibantu na Kiarabu.
UDHAIFU WA NADHARIA HII
ü Mtazamo huu umeshindwa kuitaja kinaganaga hiyo lugha ya kibantu iliyochangamana na Kiarabu kuunda Kiswahili. Na kama ipo ndio Kiswahili chenyewe.
ü Mtazamo huu umesisitiza zaidi juu ya msamiati wa kiswahili wenye asili ya kiarabu kama kigezo chake na kutupilia mbali vipengele kama vile matamshi,maumbo na miundo ya sentensi.
ü Kiswahili kingekuwa pijini au krioli inayotokana na lugha ya kibantu na kiarabu, basi sintaksia yake ingefanana na ile ya kiarabu
ü Pia, kama Kiswahili kingekuwa ni zao la uchangamano wa Kiarabu na lugha ya Kibantu basi asilimia hamsini ya misamiati ya kiswahili ingekuwa na asili ya kiarabu. Tofauti na ilivyo ambapo: Msamiati wa kibantu- 60% Msamiati wa Kiarabu-30% Lugha nyingine -10%
3. KISWAHILI NI KIARABU
Wapo baadhi ya wataalamu waliopendekeza kuwa Kiswahili ni lugha ya kiarabu. Wao wanatoa hoja kwamba maingiliano baina ya waarabu na wabantu yalipelekea kufifia na kufa kwa vijilugha vyote vilivyokuwako katika upwa wa Afrika Mashariki na kiarabu kikashika hatamu. Wanathibitisha hoja yao kwa uwepo wa msamiati wenye asili ya Kiarabu kwa asilimia 30 katika lugha ya Kiswahili. Pia hudai kuwa watu wengi waishio pwani ni waislaimu, na kiislamu kililetwa na Waarabu, lugha wanayozungumza ni Kiswahili hivyo inawezekana kabisa kuwa Kiswahili ni Kiarabu.
UDHAIFU WA NADHARIA HII
ü Mtazamo huu umesisitiza zaidi juu ya msamiati wa kiswahili wenye asili ya kiarabu kama kigezo chake na kutupilia mbali vipengele kama vile matamshi,maumbo na miundo ya sentensi.
ü Kiswahili kama lugha nyingine kimekopa msamiati kukidhi mawasiliano. Hiyo haiwezi kuwa sababu ya chenyewe kuwa Kiarabu.
4. KISWAHILI NI KIBANTU
Nadharia hii inashikilia msimamo kuwa Kiswahili si kiarabu, pijini au kreoli na wala si Kikongo bali Kiswahili ni lugha ya kibantu. Lugha za Kibantu ni lugha zenye asili ya Kiafrika, hasa zile zinazopatikana kusini mwa jangwa la sahala. Wataalamu wanoshikilia nadharia hii wanasema Kiswahili ni moja ya lugha hizo. Kuthibitisha hoja yao wanatoa ushaidi wa Kihistoria na Kiisimu.
USHAHIDI WA KIHISTORIA
i. UGUNDUZI WA ALI – IDRISI
Huyu ni mwana Jeografia aliyepata kuzunguka sehemu kubwa ya Bahari ya Hindi katika karne ya 10. Katika maandiko yake yaliyogunduliwa huko Sicily, katika mahakama ya Mfalme Roger II yanaonesha kuwa alipata kufika katika upwa wa Afrika Mashariki. Amevielezea visiwa vya Zanzibar kwa jina la “UNGUJA” Huu ni ushahidi kuwa kabla ya ujio wa Waarabu walioleta neno Zanzibar, Visiwa hivi vilikuwa na jina ‘Unguja’. Hii ni wazi kwamba wakazi wa visiwa hivi walikuwa na lugha yao. Lugha hiyo ndicho Kiswahili. Kwa hiyo Kiswahili si Kiarabu wala si pijini bali ni Kibantu
ii. USHAHIDI WA MARCO-POLO
Huyu ni mwanajeogarfia wa Kizungu aliyepata kusafiri sehemu mbalimbali duniani. Katika maandiko yake anaonesha kuwa alipata kutembelea Afrika Mashariki katika karne ya 10 na kuendelea. Katika maandishi yake anazungumzia asili ya watu aliowakuta Afrika Mashariki, lugha, dini na vyakula vyao. Maelezo ya Marco Polo yanakiri uwepo wa lugha ya watu wa Afrika Mashariki. Hakusema kuwa lugha hiyo Kiarabu bali lugha ya kibantu. Lugha hiyo ndicho Kiswahili. Hivyo Kiswahili ni Kibantu wala si kiarabu.
iii. USHAHIDI WA AL-MASUDI
Huyu ni mwanajeografia na historia wa Kiarabu. Naye alipata nafasi ya kufika katika Pwani ya Afrika Mashariki katika karne ya 10. Katika maandiko yake amefafanua majina ya viongozi wa pwani ya Afrika Mashariki kuwa ni Wakilimi. Pia, alistaajabishwa kusikia kuwa watu Waafrika waliitwa Wazanji na nchi yao Zanjibar. Ushahidi huu wa Al-Masudi unatudhihirishia kuwa hata waarabu wenyewe waliotembelea Afrika Mashariki walikuta waafrika wakitumia lugha yao ingawa ilikuwa na jina la Kiarabu. Hivyo Kiswahili si Kiarabu bali ni Kibantu.
iv. HISTORIA YA MJI WA KILWA
Katika historia, habari zinaeleza kuwepo kwa masultani wa Kilwa waliopewa majina kama Mkoma watu Nguo Nyingi Hasha Hazifiki. Majina haya yanathibitisha kuwepo kwa matumizi ya Kiswahili kabla ya ujio wa utawala wa Mwarabu. Hivyo Kiswahili si Kiarabu wa Pijini bali ni lugha yenye asili ya Kibantu.
v. UTENZI WA FUMO LIYONGO
Kisa cha shujaa Lyongo kilikuwa kikighaniwa kama ushairi kwa karne nyingi kabla hakijarekodiwa kwenye maandishi mnamo karne ya 13. Uwepo wa kisa hiki katika utenzi kinadhihirisha kuwepo kwa lugha ya Kiswahili kabla ya ujio wa waarabu. Mfano wa beti zake: “Liyongo Kitamkali, Akabalighi vijali, Akawa mtu wa kweli, Na hiba huongeya.” Utenzi huu unathibitisha kuwa Kiswahili ni lugha yenye asili ya Kiafrika.
Kama tulivyoona hapo katika shahidi hizo. Historia inathibitisha kuwa Kiswahili ni lugha yenye asili ya Kibantu. Watu mashuhuri waliopata kuitembelea Afrika Mashariki wanaafiki katika maandishi yao kuwa Kiswahili kilipata kuwapo na kuongelewa kabla ya ujio wa wageni. Hivyo Kiswahili ni Lugha yenye asili ya Kibantu.
USHAHIDI WA KIISIMU
i. MISAMIATI
Msamiati ni sehemu ya msingi ya lugha. Sehemu kubwa ya msamiati wa Kiswahili unafanana na ule wa lugha za kibantu. Hii inamaana kwamba, misamiati katika lugha ya Kiswahili inaelekea kuwiana kimatamshi na hata katika viambishi vichache.
Mfano:
KISWAHILI | KISAMBAA | KIKURYA | KIJITA |
mtu | mdhu | omonto | omontu |
Maji | mazi | amanche | amanji |
Moto | moto | omoro | omulilo |
ii. TUNGO ZA KISWAHILI
Muundo wa tungo sentensi katika Kiswahili unafanana na muundo wa sentensi katika lugha nyingine za kibantu. Sentensi katika Kiswahili zinazingatia muundo wa KIIMA na KIARIFU, kadharika sentensi katika lugha nyingine za kibantu. Kufanana kwa muundo wa tungo kati ya Kiswahili na lugha nyingine za kibantu kunathibitisha kuwa Kiswahili ni moja ya lugha zenye asili ya kibantu.
KIIMA | KIARIFU | |
KISWAHILI | Juma | anakula ugali |
KIZIGUA | Juma | adya ugali |
KISUKUMA | Juma | alelya bugali |
KINDALI | Juma | akulya ubhughali |
iii. UPATANISHO WA KISARUFI
Katika kigezo hiki tunazingatia uhusiano uliopo kati ya NOMINO (viwakilishi) na viambishi awali vya nafsi katika vitenzi vya Kiswahili tukifananisha na lugha nyingine za kibantu. Ukichunguza kwa makini utagundua kuwa viambishi katika vitenzi vya Kiswahili hubadilika kutokana na maumbo ya umoja na wingi wa nomino au kiwakilishi katika sentenis. Tabia hii pia inajidhihirisha katika lugha nyingine za kibantu.
Mfano:
UMOJA | WINGI | |
KISWAHILI | Baba analima | Baba wanalima |
KINDALI | Utata akulima | Abhatata bhakulima |
KIKURYA | Tata ararema | Batata bararema |
KISAMBAA | Tate ataima | Tate wataima |
iv. MPANGILIO WA VIAMBISHI
Vitenzi katika lugha za kibantu huundwa na MZIZI ambao huambikwa viambishi ili kukamilisha maana yake. Kiswahili pia hufuata utaratibu huu. Vitenzi vyake huundwa na mzizi kisha kuambikwa viambishi.
Mfano:
KISWAHILI analima a-na-lim-a
KISAMBAA ataima A-ta- im-a
KIKURYA arerema A-re-rem-a
Katika mfano hapo juu utagundua kuwa mbali na kuthibitisha kuwa vitenzi vya Kiswahili na vile vya lugha za kibantu vinaundwa na mzizi na viambishi lakini pia utagundua vyote vinampangilio sawa. Yaani viambishi vya nafsi huanza kisha vinafuata vya njeo kisha mzizi. Hii inathibitisha kuwa Kiswahili ni moja ya lugha za kibantu.
v. IDADI YA IRABU
Kiswahili na lugha nyingine za kibantu, zote zina irabu ambazo ni: a , e , I , o , u. Hii inathibitisha kuwa Kiswahili ni Kibantu na wala si Kiarabu.
Kama tulivyoona katika ushahidi wa kiisimu,
Kiswahili kina sifa sawa za kiisimu na lugha nyingine kusini mwa jangwa la sahara.
Hii inathibitisha kuwa Kiswahili ni KIBANTU.