Monday

NOTES ZA MIHADHARA YA KI 107 ISIMU

0 comments

YALIYOMO 


FonetikiTaaluma inayochunguza sauti zote ambazo zinaweza kutumika katika lugha yoyote ile na kutoa sifa za sauti hizo bila kujali zinatumika katika lugha gani na kwa njia gani.

(i)     FonolojiaTaaluma inayofafanua mfumo wa sauti zitumikazo katika lugha mahsusi na jinsi sauti hizo zinavyotumika. Katika Fonolojia kinachoshughulikiwa ni mifumo sauti ya lugha maalum. Wanafonolojia wameunda vipashio maalum vya kujadilia mfumo sauti kv. Fonimu na alofoni. Mfumo sauti wa lugha unajumuisha vitamkwa vya lugha pamoja na mfuatano wa vitamkwa unaunda silabi na muundo wake, kanuni za kifonolojia, toni, kiimbo, nk.

(ii)   MofolojiaTaaluma inayochunguza maumbo ya maneno katika lugha. Taaluma inayochambua na kuweka kanuni za jinsi maumbo tofauti ya maneno yanavyohusiana katika sarufi ya lugha husika. Vipashio vidogo kabisa vya lugha vinavyounda maneno ya lugha vinaitwa mofimu mfano m-tu   wa-tu. Mofimu ni vipashio vinavyoonyesha uhusiano uliopo kati ya sauti msingi za lugha (yaani fonimu) na maana katika sarufi ya lugha. Maumbo toauti ya mofimu moja yanajulikana kama alofoni za mofimu hiyo, mfano mtotowatotohapa m na wa ni alomofu.

(iii) SintaksiaTaaluma inayojihusisha na uchambuzi na ufafanuzi wa muundo wa sentensi za lugha. Inaendelea pale ilipoishia mofolojia. Uchambuzi wa kisintaksia unaonyesha uhusiano wa maneno na vipashio vingine vinavyojenga sentensi za lugha.

(iv) SemantikiTaaluma inayojihusisha na ufafanuzi wa maana katika lugha (yaani maana ya maneno na sentensi).

(v)   PragmatikiTaaluma inayojihusisha na ufafanuzi wa maana katika lugha kwa muktadha mahususi (yaani muktadha wa matumizi).

 

 

2 Isimu Tumizi

Ni uwanja wa Isimu unaohusika na utumiaji wa matokeo ya tafiti za kiisimu katika nyanja mbalimbali kwa lengo la kutatua matatizo yahusuyo lugha. Taaluma hii ilianza baada ya Vita Vikuu vya Pili vya Dunia wakati huo ilihusika na ufundishaji wa lugha kwa wageni, mfano Kiarabu, Kichina, Kirusi, nk. Baadaye katika miaka ya 19501960 ulizuka uwanja mpya wa utafiti wa lugha kwa kutumia mashine. Kwa hali hiyo isimu tumizi ilipanuka na kujumuisha nyanja zifuatazo:

(a) Ufundishaji wa lugha kwa wageni.

(b) Tafsiri kwa kutumia mashine

(c) Eneo la sera ya lugha na upangaji wa lugha.

(d) Lugha na elimu.

(e) Lugha na siasa (Propaganda katika siasa).

 

3 Isimu Nafsia (Saikolojia)

Ni taaluma inayohusika na mambo yanayowezesha watu kujifunza lugha mama. Inamwezesha kutumia na kuelewa lugha. Isimu nafsia mamboleo hutumia matokeo ya taaaluma mbalimbali, mfano elimu viumbe, sayansi ubongo, sayansi utambuzi, isimu ubongo, nk.

 

Isimu nafsia hutumia matokeo ya isimu ubongo, isimu utambuzi, elimu viumbe ili kutambua jinsi ubongo unavyochakata lugha (language processing). Isimu nafsia ya ujifunzaji lugha huhusika na uwezo wa watoto kujifunza lugha.

 

4  Isimu Ubongo

Sayansi inayochunguza utendaji wa ubongo na utendaji unaohusiana na mambo ya uelewa, uzalishaji na ujuzi dhahania wa lugha. Utendaji huu unachunguzwa katika hali mbalimbali za lugha, mfano uneni, maandishi, alama au ishara.

Isimu ubongo inashirikisha nyanja zifuatazo za taaluma:

a) Biolojia

b) Sayansi ya kompyuta

Afasiolojia (aphasiology)Taaluma inayochunguza matatizo ya lugha wayapatayo watu wenye matatizo ya ubongo.

 

5 Isimu Ujifunzaji Lugha

Taaluma inayochunguza jinsi mtoto anavyojifunza lugha ya mama kwa kuzingatia:

a) Mazingira anayopitia mtoto.

b) Hatua anazopitia katika kujifunza lugha.

MazingiraLazima mtoto awe katika jamii ya wanalugha na atagusane nao.

HatuaHuangalia hatua za mtoto katika kujifunza lugha.

 

 

6 Isimu Historia

Taaluma inayotalii jinsi lugha zinavyobadilika kwa kuchunguza lugha zinazoingiliana kimsamiati, kisintaksia na kimofolojia. Uchunguzi huo hufanywa kwa kulinganisha lugha mbalimbali na kuziainisha. Wanaisimu wanaangalia hali ya kufanana na kutofautiana kimuundo kwa lugha za wanadamu hata kuzitofautisha.

 

7 Isimu Jamii

Taaluma inayochunguza athari za vipengele vya kijamii jinsi lugha inavyotumika katika jamii. Pia wanaisimu wanachunguza jinsi lugha tofauti zinavyoathiriana wakati wazungumzaji wa lugha hizo wanapokutana.

 

8 Isimu Kompyuta

Taaluma inayohusika na utumiaji wa mbinu za kikompyuta na kimantiki katika kuchakata lugha.

 

 

 

Tuangalie kwa undani juu ya Fonetiki

Fonetiki

 

FONETIKI

Fonetiki ni taaluma inayoshughulika na kuchunguza sauti za lugha. Inachunguza sauti hizo zilivyo, zinavyotolewa, zinavyomfikia msikilizaji, nk. Fonetiki inachunguza sauti zote ambazo zinaweza kutumika katika lugha yoyote ile na kutoa sifa za sauti hizo bila kujali zinatumika katika lugha gani au kwa njia gani.

Kwa kusikiliza sauti hizo, wanafonetiki wanaweza kuzipanga sauti hizo katika makundi na kuzipa au kuzitolea sifa ambazo zinaweza kutofautisha sauti moja na nyingine.

 

Matawi ya Fonetiki

Fonetiki imegawanyika katika makundi makuu matatu Fonetiki matamshi, fonetiki safirishi na fonetiki masikizi.

a) Fonetiki matamshi (articulatory phonetics)

Huchunguza jinsi sauti za lugha zinavyotolewa na viungo vya sauti vya mwanadamu na kuziweka katika matabaka. Huangalia viungo vinavyohusika katika utoaji wa sauti fulani, pia huchunguza sifa za sauti hizo na kuangalia zinatofautianaje na zinafananaje.

 

b) Fonetiki safirishi au fonetiki akustiki (acustic phonetics)

Huchunguza jinsi sauti za lugha zinavyosafiri kutoka kwa msemaji hadi kumfikia msikilizaji husika na jinsi mawimbi ya sauti yanavyotengenezwa na jinsi yanavyosafirishwa hewani hadi kufikia sikio la msikilizaji.

 

c) Fonetiki masikizi (auditory phonetics)

Huchunguza lugha zinavyopokelewa na msikilizaji na jinsi zinavyotafsiriwa na sikio na akili ya msikilizaji, hivyo kuwezesha kuwepo masikilizano kati ya msemaji na msikilizaji.

 

Fonetiki Matamshi

Fonetiki matamshi inachunguza mambo yafuatayo:

i)                   Ala za sauti

ii)                 Mahali pa kutamkia

iii)               Namna ya utamkaji

iv)               Mikondo ya hewa

v)                 Aina za vitamkwa

vi)               Sifa bainifu za toni

vii)             Unukuzi wa toni

 

Ala za sauti

Ala za sauti ni viungo vya mwali wa binadamu vinavyotumika kumwezesha mwanadamu kutoa sauti. Pamoja na kutumika kutolea sauti, viungo hivi pia vina kazi nyingine za kibiolojia k.m. mapafu hufanya kazi ya kupeleka hewa kwenye damu; nyuzi sauti katika koromeo hufanya kazi ya kufunga koo wakati wa kula ili kuzuia chakula kisipite kwenye mrija hewa; ulimi na meno hutumika kuonja na kula chakula.

 

Ala za sauti

Ala za sauti ni viungo vya mwanadamu vinavyotumika katika kutoa sauti mbalimbali.

Viungo vifuatavyo ni ala za sauti ambavyo hushiriki katika utoaji wa sauti

1.                 Midomo

2.                 Meno

3.                 Ufizi

4.                 Kaakaa gumu

5.                 Kaakaa laini

6.                 Uvula (kidaka tonge)

7.                 Pua

8.                 Ncha ya ulimi

9.                 Pembe ya ulimi

10.             Ulimi sehemu ya mbele

11.             Ulimi sehemu ya nyuma

12.             Shina la ulimi

13.             Koromeo

14.             Chemba cha pua

15.             Chemba cha kinywa

16.             Kongomeo

17.             Kimio

18.             Nyuzi sauti

 

Ala za sauti zinaweza kugawanywa katika makundi makubwa mawili ambayo ni:

i)                   Ala sogezi

ii)                 Ala tuli

 

Ala sogezi ni zile ambazo husogea sogea wakati mtu anapozungumza, mfano ulimi, midomo, nk.

 

Ala tuli ni zile ambazo huwa zimetulia tu hazisogeisogei wakati mtu anapozungumza, mfano ufizi, kaakaa, meno, nk.

 

Meno ni miongoni mwa ala tuli. Meno hushiriki katika kutamka baadhi ya foni za lugha, mfano mtu anapotamka [s] na [z] hewa huruhusiwa kupenya kati ya meno na kwa hali hiyo meno hushiriki katika kuzitamka foni hizo.

 

Midomo ni ala sogezi ambazo mtu anapozungumza huwa hazitulii bali husogeasogea. Midomo hushiriki kiasi cha kutosha katika utamkaji wa vitamkwa vya lugha. Vitamkwa ambavyo hutamkiwa katika midomo ni kama vile [m], [p], na [b].

 

Ufizi ni kiungo kinachoshiriki kutamka baadhi ya foni. Ufizi ni ala tuli, hivyo hausogeisogei wakati wa kutamka foni. Baadhi ya foni za Kiswahili zinazotamkwa kwenye ufizi ni pamoja na [n], [t], [d], [z], [l] na [r]. Foni nyingi za Kiswahili hutamkiwa kwenye ufizi kuliko mahali pengine popote. Ufizi unaoshiriki zaidi ni ule wa juu.

 

Kaakaa gumu  hii ni sehemu tuli inayopakana na ufizi. Hii ni sehemu mojawapo inayotumika kutamka foni kama vile [ts], [j].

 

Kaakaa laini  hii ni sehemu tuli inayopakana na kaakaa gumu. Hutumiwa kutamka baadhi ya foni kama vile [k], [g], ng'].

 

Koromeo  huu ni uwazi unaoanzia kwenye kongomeo (kisanduku cha sauti) linapokomea hadi chemba cha pua kinapoanzia. Uwazi huu hupokea sauti inapotoka kwenye kisanduku cha sauti.

 

Ulimi  Mojawapo ya ala sogezi muhimu sana katika mfumo mzima wa uzungumzaji. Ulimi umegawanyika katika sehemu kuu tatu:

-                   Sehemu ya mbele (ncha ya ulimi)

-                   Sehemu ya kati (ubapa)

-                   Sehemu ya nyuma

 

Sehemu ya mbele (ncha ya ulimi)  hutumiwa kutamka vitamkwa mbalimbali kwa mfano, [n], [t], [d], nk.

 

Sehemu ya kati ya ulimi (bapa) hutumika kutamka vitamkwa kama vile [ts]

 

Sehemu ya nyuma ya ulimi (mzizi wa ulimi)  huenda juu au chini, mbele au nyuma wakati wa kutamka vitamkwa. Kusogea huko huathiri umbo la chemba cha kinywa na hii huathiri sauti zinazotamkwa.

 

Kidakatonge  huwa hakitumiki kutamka vitamkwa, lakini huzuia chakula kisipitie kwenye njia ya hewa hasa wakati mtu anapokula akiwa anaongea.

 

Nyuzi sauti  ni misuli miwili yenye uwezo wa kunyumbulika ambayo huwepo kwenye kongomeo. Misuli hii huumba sura mbalimbali za glota. Wakati mwingine hufunga kabisa njia na kufungua kwa ghafla. Wakati mwingine hukaa kwa namna ambayo sauti itokayo huwa ghuna au sighuna. Nyuzi sauti huibadilisha hewa inayotoka mapafuni kuwa sauti ya kusikika. Urefu na ukubwa wa nyuzi sauti huathiri sauti inayotolewanyuzi fupi na nyembamba hutoa sauti ya juu (kali) na nyuzi nene na ndefu hutoa sauti nzito.

 

Kongomeo (kisanduku cha sauti)  hii ni sehemu ambapo nyuzi sauti huhifadhiwa. Makongomeo yanatofautiana kati ya mtu na mtu. Kuna wengine wana makongomeo makubwa na wengine madogo.

 

Koo  hili ni bomba lenye uwazi ambapo hewa inayotoka mapafuni hupitia kwenda kwenye mapafu au kurudi kutoka mapafuni. Uwazi huu huanzia mapafuni hadi kwenye kongomeo.

 

Pua  Husaidia kuchuja sauti inayotoka. Watu wenye mafua au walioumia pua sauti zao huwa hazichujwi. Baadhi ya vitamkwa kama vile nazali, hutamkwa kwa kupitishia mawimbi mengi zaidi ya sauti kwenye chemba cha pua na pua.

 

Chemba cha pua ni uwazi ambao upo kuanzia kwenye pua kuelekea ndani hadi kwenye koromeo. Husaidia kusafirisha na kuchuja sauti.

 

Chemba cha kinywa kuna sehemu nyingi katika chemba cha kinywa ambazo hutumika kutamkia sauti mbalimbali.

 

Mahali muhimu pa kutamkia foni za konsonanti ni pamoja na ala zifuatazo za sauti:

 

i)        Midomo miwili wa juu na chinisauti hutamkwa kwa kuikutanisha midomo yote miwili (wa juu na wa chini) na kupata sauti [b], [m], [p], nk.

ii)      Mdomo na menosauti hutamkwa wakati mdomo wa chini unapokuwa umeyagusa meno ya juu, mfano [f] na [v].

iii)    MenoBaadhi ya foni hutamkiwa kwenye meno. Vitamkwa vya kwenye meno huitwa foni za meno. Wakati wa kutamka ulimi huwekwa katikati ya meno ya juu na chini na hususan hugusa meno ya juu, mfano [th]

iv)    UfiziWakati wa kutamka foni za ufizi ncha ya ulimi hugusa ufizi, mfano [t].

v)      Kaakaa na ufiziWakati wa kuzitamka foni sehemu ya mbele ya ulimi hugusa sehemu ya kati ya ufizi na kaakaa gumu, mfano [s].

vi)    Kaakaa gumuFoni nyingine hutamkiwa kwenye kaakaa gumu. Wakati wa kutamka foni hizi sehemu ya kati ya ulimi huinuliwa na kugusa kaakaa gumu, mfano [ts] na [j].

vii)  Kaakaa lainiWakati wa kutamka foni, sehemu ya kati au nyuma ya ulimihuinuliwa hadi kukaribia au kugusa sehemu hiyo ya kaakaa laini, mfano [k], [g], [kh].

viii)                        Midomo na kaakaa lainifoni chache katika lugha hutamkiwa katika sehemu mbili tofauti na ambazo hazipo karibu yaani midomo na kaakaa laini, mfano [w].

ix)    KoromeoWakati mwingine baadhi ya foni katika lugha hutamkiwa kwenye koromeo. Wakati wa kuzitamka foni hizi koromeo hubanwa kiasi fulani ili kuruhusu sauti kutoka.

x)      GlotaUwazi ulio kati ya nyuzi sauti zilizopo katika kongomeo. Uwazi huu hubadilikabadilika kutegemea kile kinachotamkwa. Sauti za glota hutokea wakati nyuzi sauti zinapokutanishwa kwa muda mfupi. Sauti hizi ni chache katika lugha, mfano [h].

 

 

UAINISHAJI WA SAUTI: IRABU NA KONSONANTI

 

Sauti za lugha zimegawanyika katika makundi makubwa mawili: konsonanti na irabu.

 

Tofauti kati ya konsonanti na irabu inaonekana katika utamkaji wake. Wakati wa kutamka irabu hewa haizuiwi au kubanwa mahali popote, yaani hewa hupita kwa urahisi bila kuzuiliwa.

 

Uainishaji wa irabu

 

Katika uainishaji wa irabu wanafonetiki wameangalia na kubainisha sifa mbalimbali . Mojawapo ya sifa zinazoangaliwa ni pamoja na mkao wa ulimi katika kinywa wakati wa utamkaji, mkao wa mdomo wakati wa utamkaji na  mahali pa kutamkia irabu.

 

Mahali pa kutamkia irabumahali pa kutamkia irabu ni sifa inayozingatia mahali ambapo ulimi huwapo wakati wa kuzitamka irabu husika. Wanafonetiki wamebainisha sehemu tatu za kutamkia, yaani sehemu ya ulimi inayohusika wakati wa kutamka. Sehemu ya ulimi inayohusika katika utamkaji ni ile ya mbele, kati na nyuma ya ulimi. Kwa mfano katika Kiswahili irabu [i] na [e] hutamkwa kwa kutumia sehemu ya mbele ya ulimi, kwa hali hiyo hizi huitwa irabu za mbele. Irabu [u] na [o] hutamkwa kwa kutumia sehemu ya nyuma ya ulimi nazo huitwa irabu za nyuma. Irabu [a] hutamkwa kwa kutumia sehemu ya kati ya ulimi, hivyo huitwa irabu ya kati.

 

Sifa ya mkao au mwinuko wa ulimi inatumika kuangalia ulimi unakuwa chini, umeinuka juu kiasi au juu kabisa wakati wa utamkaji wa irabu. Kutokana na sifa hii ya mwinuko wa ulimi, irabu zinaweza kuainishwa katika makundi matatu ambapo [i] na [u] hutamkwa wakati ulimi ukiwa juu na [e] na [o] hutamkwa ulimi ukiwa katikati na [a] hutamkwa wakati ulimi ukiwa chini.

 

Kutokana na sifa hizo zilizotajwa, irabu zinaweza kuainishwa kwa kufuata vigezo vitatu:

  1. Kuangalia mkao wa ulimi kama umeinuka juu au upo chini.
  2. Kuangalia kuwa sehemu gani ya ulimi imehusika katika kutamka irabu.
  3. Kuangalia midomo ikoje wakati wa utamkaji.

 

a) Kwa kutumia kigezo cha mkao wa ulimi kuwa juu au chini irabu zinaweza kuainishwa kama ifutavyo:

Irabu juu [i, u] ulimi unakuwa umeinuka juu.

Irabu chini [a] ulimi unakuwa chini.

Irabu kati [o, e] ulimi unakuwa umeinuka hadi katikati.

 

b) Kwa kuangalia kigezo cha sehemu ya ulimi iliyoinuliwa juu au kushushwa chini tunaweza kuziainisha irabu kama ifuatavyo:

Irabu mbele [i, e] ulimi unakuwa umeinuliwa na kupelekwa mbele

Irabu nyuma [u, o] ulimi unakuwa umerudishwa nyuma

Irabu kati [a] ulimi hauwi nyuma wa mbele bali katikati.

 

Mkao wa midomowakati wa kutamka irabu midomo inaweza kuwa imeviringwa au haikuviringwa.

-        wakati wa utamkaji wa irabu, midomo inaweza kuwa imeviringwa na irabu zitakazotamkwa zitakuwa viringo, mfano [o, u].

-        midomo inaweza kuwa imesambazwa au kupanuliwa wakati wa utamkaji na kutoa irabu siviringo, mfano [i, e, o].

 

 

Kutokana na vigezo tulivyoangalia vya uainishaji wa irabu tunaweza kupata sifa bainifu za kila irabu kama ifuatavyo:

[i] irabu juu mbele siviringo.

[u] irabu juu mbele viringo

[e] irabu kati mbele siviringo

[o] irabu kati nyuma viringo

[a] irabu chini kati siviringo

 

 

 

Uainishaji wa konsonanti

 

Konsonanti ni sauti au foni ambazo wakati wa kutamkwa hewa huzuiwa kwa namna fulani. Wakati mwingine hewa huzuiwa kabisa na wakati mwingine huzuiwa kiasi mahali fulani baada ya kupita kongomeo.

Katika kuainisha konsonanti zimeangaliwa sifa za jumla za konsonanti ambazo ni jinsi konsonanti hizo zinavyotamkwa na mahali konsonanti hizo zinapotamkiwa.

 

Namna ya utamkaji

Kwa kuzingatia namna konsonanti zinavyotamkwa konsonanti zimegawanywa katika aina kuu sita ambazo ni:

  1. vizuiwa au vipasuo
  2. vikwamizwa au vikwamizi
  3. vizuiwa-kwamiza
  4. vitambaza
  5. vimadende
  6. nazali

 

Vizuiwa au vipasuo

Foni hizi zinapotamkwa kwanza hewa kutoka mapafuni husukumwa nje kwa nguvu na kuzuiwa kabisa kabla ya kuachiliwa ghafla na kutoa sauti ambayo hufanana na sauti inayosikika wakati kitu kinapolipuka. Kutokana na hali hiyo ya kutoa sauti ya mpasuko wanafonetiki wengine wameziita konsonanti hizi vipasuo. Katika Kiswahili kuna vizuiwa vifuatavyo: [p], [b], [t], [d], [k] na [g].

 

Vikwamizwa au vikwamizi

 Wakati wa kutamka foni hizi ala za sauti hukaribiana kiasi cha kutosha kuweza kusikia mkwaruzo

unaotokea wakati hewa inapopita kati ya ala hizo. Katika Kiswahili kuna vikwamizwa kadhaa ambavyo ni kama vifuatavyo: [f], [v], [s], [z], [Ɵ], [Ɣ], [ʃ], [h], [x] na [dh]

 

Vizuiwa-kwamiza

Wakati wa kutamka konsonanti hizi hewa husukumwa nje kwa nguvu, huzuiwa kisha nafasi ndogo huachwa ili hewa ipite ikiwa na mkwaruzo. Katika Kiswahili vizuiwa-kwamiza ni [ts] na [j].

 

Vitambaza

Wakati wa kutamka vitambaza hewa husukumwa nje, huzuiwa na kuruhusiwa ipite pembeni bila mkwaruzo mkubwa sana. Katika Kiswahili kitambaza ni kimoja tu ambacho ni [l].

 

Vimadende

Ni konsonanti ambazo wakati wa kutamka ncha ya ulimi huwa inakuwa imeugusa ufizi lakini kutokana na nguvu ya hewa inayopita kati ya ncha ya ulimi na ufizi, ncha ya ulimi hupigapiga kwa harakaharaka kwenye ufizi. Katika Kiswahili kipo kimadende kimoja ambacho ni [r].

 

Nazali

Konsonanti ambazo hutamkwa kwa kukishusha kimio kwa namna ambayo hewa nyingi kutoka mapafuni huelekezwa kupitia kwenye chemba cha pua. Katika Kiswahili kuna nazali zifuatazo:

[n], [m], [ng'] na [ny].

 

Mahali pa Kutamkia

Sifa hii inahusu ala za sauti zinazohusika katika kuzuia mkondohewa katika bomba la sauti. Wakati wa kutamka sauti za konsonanti, alasogezi husogea kuelekea kwenye alatuli au wakati mwingine alasogezi husogeleana kama vile mdomo wa juu na wa chini inaposogeleana. Aghalabu mara nyingi sauti huainishwa kwa kuzingatia alatuli iliyohusika isipokuwa kama hakuna alatuli iliyohusika. Kulingana na sifa ya mahali pa kutamkia sauti za konsonanti za Kiswahili zinaweza kugawanywa katika makundi nane makuu ambayo ni:

  1. Sauti za midomo
  2. Sauti za mdomo na meno
  3. Sauti za meno
  4. Sauti za ufizi
  5. Sauti za kaakaa gumu
  6. Sauti za kaakaa laini
  7.  Sauti za midomo na kaakaa laini
  8. Sauti za glota

 

Sauti za midomo

Hizi ni sauti ambazo hutamkwa kwa kuikutanisha midomo yote miwili, yaani mdomo wa juu na chini. Midomo yote ni alasogezi ambazo hukutana kutamka sauti kama vile [p], [b], [m], nk.

 

Sauti za mdomo na meno

Utamkaji wa sauti kwa kushirikisha ala hizi za sauti hufanyika kwa kukutanisha mdomo wa chini na meno ya juu. Mdomo wa chini ambao ni alasogezi husogelea meno ya juu ambayo ni alatuli na kutamka sauti kama vile [f], [v].

 

Sauti za meno

Sauti zenye sifa hii hutamkwa huku ncha ya ulimi ikiwa katikati ya meno ya juu na chini. Vitamkwa vinavyotamkiwa kwenye meno hujulikana kama foni za meno. Foni za meno ni pamoja na [ȶ], [ɵ].

 

Sauti za ufizi 

Ufizi ni mahali ambapo foni za lugha hutamkiwa. Ulimi kama alasogezi huinuka na kugusa sehemu ya ufizi. Katika lugha ya Kiswahili ufizi ndipo mahali ambapo foni nyingi zaidi hutamkiwa. Foni za ufizi ni kama vile, [t], [d], [n], [s], [z], [l], [r].

 

Sauti za kaakaa gumu

Kaakaa gumu ni mahali ambapo baadhi ya foni hutamkiwa. Wakati wa kuzitamka foni hizi sehemu ya kati ya ulimi (bapa) huinuliwa hadi kugusa kaakaa gumu. Foni zinazotamkiwa mahali hapa ni kama vile [ʦ], [Ɉ].

 

Sauti za kaakaa laini

Baadhi ya foni hutamkiwa katika kaakaa laini. Wakati wa kuzitamka foni hizi sehemu ya kati au nyuma ya ulimi huinuliwa hadi kukaribia au kugusa sehemu ya kaakaa laini. Foni zinazotamkiwa katika kaakaa laini ni kama vile [k], [g], [x] na [ɣ].

 

Sauti za midomo na kaakaa laini

Foni hizi ni chache katika lugha ya Kiswahili ambazo hutamkiwa katika sehemu mbili tofauti ambazo hazipo karibu. Mdomo na kaakaa laini ni sehemu zilizo mbali baina yao. Foni zinazotamkiwa katika sehemu hizo ni [w].

 

Sauti za glota

Glota ni sehemu ambayo hutumika kutamkia konsonanti za aina mbalimbali. Glota ni uwazi ulio kati ya nyuzi sauti zilizo katika kongomeo. Uwazi huu huweza kubadilika kulingana na kile kinachotamkwa. Foni za glota hutamkiwa katika glota bila kuvihusisha viungo vingine. Katika lugha ya Kiswahili foni ya glota ni moja ambayo ni [h].

 

Sifa ya Hali ya Glota

Sifa hii hutumika kutofautisha foni ambazo zinatamkwa wakati nyuzi sauti zikiwa zinatetema na zile ambazo hutamkwa huku nyuzi sauti zikiwa hazitetemi. Foni zile ambazo hutamkwa nyuzi sauti zikiwa zinatetema huwa ghuna (yaani hutoa sauti kubwa) na zile ambazo hutamkwa nyuzisauti zikiwa hazitetemi huwa si ghuna (yaani sauti haiwi kubwa). Sauti ghuna ni kama vile [z], [b], [d], [g], [v], [ɣ]. Na foni ambazo si ghuna ni kama vile [s], [p], [t], [f], [k], nk.

 

Namna ya kutamka

Mahali pa kutamkia

 

 

Midomo

Midomo-meno

Ufizi - meno

Ufizi

Kaakaa gumu

Kaakaa laini

Koromeo (glota)

Vipasuo

Ghuna

b

 

 

d

 

g

 

Si ghuna

p

 

 

t

 

k

 

Vizuio Kwamiza

Ghuna

 

 

 

 

Ɉ

 

 

Si ghuna

 

 

 

 

ʦ

 

 

Vikwamizi

Ghuna

 

v

ȶ

z

 

ɣ

h

Si ghuna

 

f

ɵ

s

 

 

 

Nazali

 

m

 

 

n

ɲ

ŋ

 

Vitambaza

 

 

 

 

l

 

 

 

Vimadende

 

 

 

 

r

 

 

 

Viyeyusho

 

w

 

 

 

j

 

 

  

 

 

Unukuzi

Unukuzi ni uwakilishaji wa sauti ya lugha kwa kutumia alama. Data ya aina moja inaweza kunukuliwa kwa njia zaidi ya moja. Kuna mifumo mbalimbali ya unukuzi inayotumika kwa madhumuni ya aina mbalimbali. Madhumuni hayo yanaweza kujumuisha ufafanuzi wa kifonetiki, nadharia ya Fonolojia, ufundishaji wa lugha, leksikografia, nk.

Mnamo mwaka 1886 kikundi cha waalimu wa Kifaransa na Kiingereza, wakiongozwa na mwanaisimu Paul Passy, waliunda kilichojulikana baadaye kuanzia mwaka 1887 kama Chama cha Kimataifa cha Fonetiki. Alfabeti yao ya kwanza ilitokana na marekebisho ya tahajia kwa Kiingereza ilijulikana kama alfabeti ya Kirumi, lakini ili iweze kutumika katika lugha nyingine, iliruhusiwa kubadili kutoka lugha moja hadi nyingine. Hivyo, wanafonetiki walibuni alama za kifonetiki za aina mbalimbali zinazotumika kuwakilisha sauti mbalimbali. Alama hizi maalum zinajulikana kama alfabeti ya kifonetiki ya kimataifa (IPA). Hii ni seti ya alama za alfabeti zipatazo karibu mia moja pamoja na alama nyingine zisizo za alfabeti.

Ingawa alama hizi nyingi zinafanana na herufi za kawaida za tahajia ya kirumi, lakini kuna baadhi yao zinatofautiana na herufi hizo.

 

Orodha ya alama hizo:


a[a]

b[b]

ch[ʦ]

d[d]

e[ɛ]

dh - [ȶ]

f[f]

g[g]

gh[ɣ]

h – [h]

i – [i]

j – [Ɉ]

k- [k]

kh – [x]

l – [l]

m – [m]

n – [n]

ng' [ŋ]

ny – [ɲ]

o – [ɔ]

p – [p]

r – [r]

s – [s]

sh – [ʃ]

t – [t]

th – [ɵ]

u – [u]

v – [v]

w – [w]

y – [j]

z – [z]

 


 

 

Sifa Bainifu za Sauti

 

Sifa bainifu ni sifa ambazo hutumiwa kuzibainisha sauti mbalimbali za lugha. Kila sauti huweza kupambanuliwa kwa kutumia sifa maalum za sauti fulani na jumla ya sifa hizo ndizo ambazo huipambanua sauti hiyo na pia kuitofautisha na sauti nyingine.

Irabu zina sifa bainifu tofauti na sifa bainifu za konsonanti.

 

Sifa bainifu za irabu

Irabu hubainishwa kwa kutumia sifa kuu tatu ambazo ni:

  1. Mahali pa kutamkia
  2. Mwinuko wa ulimi
  3. Mkao wa midomo

 

 

Mahali pa kutamkia

Sifa hii inaweza kutumiwa kuzinainisha na kuzitofautisha irabu. Zipo sehemu tatu za kutamkia irabu ambazo ni

-        Sehemu ya mbele ya ulimi – sauti zinazotamkwa ni [i], [e]

-        Sehemu ya kati ya ulimi – sauti inayotamkwa ni [a]

-        Sehemu ya nyuma ya ulimi – sauti zinazotamkwa ni [0], [u]

 

Mwinuko wa ulimi

Sifa hii pia hutumika kuzipambanua irabu kwa kuangalia mwinuko wa ulimi kama ulimi umeinuka au upo chini. Kutokana na sifa hii ulimi unaweza kuwa umeinuliwa juu kabisa, nusu juu au chini.

Mwinuko wa ulimi unapokuwa juu sauti zinazotamkwa ni [i], [u]

Mwinuko wa ulimi unapokuwa kati sauti zinazotamkwa ni [a]

 

Mkao wa midomo

Hii ni sifa mojawapo inayotumika kuzipambanua irabu. Imeonekana kuwa wakati wa kuzitamka irabu midomo huwa katika namna kuu mbili za mkao ambazo ni:

Mkao wa mviringo na mkao wa mtandazo.

Inaonekana kuwa irabu zote zinazotamkiwa mbele wakati wa utamkaji wake midomo huwa imetandazwa na irabu zote za nyuma hutamkwa wakati midomo ikiwa mviringo.

 

 

Sifa Bainifu za Konsonanti

Konsonanti zinaweza kubainishwa kwa kutumia sifa mbalimbali. Sifa hizo bainifu zinaweza kuwa kimatamshi, kiakustika au kimasikizi. Wanaisimu mbalimbali wameeleza sifa mbalimbali zinazopambanua konsonanti. Mfano Jacobson na Halle (1950) walizipambanua konsonanti kwa kuonyesha sifa bainifu za kiakustika na walizigawa sifa hizo katika makundi matatu ambayo ni:

-        Sifa ya usonoranti

-        Sifa ya uprotensi

-        Sifa ya utoni

 

 

Sifa za usonoranti

Sauti zenye sifa ya usonoranti ni zile ambazo utamkaji wake hewa hupita bila kizuizi au huzuiwa kidogo sana kupitia chemba cha pua.

Sifa za usonoranti ni sifa bainifu zinazotumika kutofautisha sauti kama vile:

-        Sauti za irabu na zisizo irabu – katika ubainishaji wao irabu huonyeshwa kuwa na usonoranti [+usonoranti] na konsonanti huonyeshwa kuwa haina usonoranti [-usonoranti]. Pamoja na irabu kuwa na usonoranti pia zipo baadhi ya konsonanti ambazo zina sifa ya ukonsonanti.

-        Sauti za konsonanti na zisizo konsonanti – wakati wa kuzibainisha sauti za konsonanti zitaonyeshwa kuwa na ukonsonanti [+ukonsonanti] na zile sauti zisizo za konsonanti zitaonyeshwa kuwa hazina ukonsonanti [-ukonsonanti]

-        Sauti zenye unazali na zisizo na unazali – Wakati wa kuzibainisha sauti za nazali zitaonyeshwa kuwa na unazali [+unazali] na zisizo na unazali zitaonyeshwa kutokuwa na unazali [-unazali]

-        Sauti ghuna na sauti zisizo ghuna – katika kuzibainisha sauti hizi zile zilizo ghuna zitaonyeshwa kuwa ghuna [+ghuna] na zile zisizokuwa ghuna zitaonyeshwa kuwa si ghuna [-ghuna]

 

Sifa ya Uprotensi

Sifa ya uprotensi ilitumiwa kutofautisha sauti ambazo zina mkazo zaidi na zile ambazo ni hafifu.

 

Sifa ya utoni

Ilitumiwa na wanaisimu kuzitofautisha sauti ambazo ni

-        shadidi na zile ambazo ni kali

-        kali na ambazo si kali

 

Baadaye wanaisimu Morris Halle na Noam Chomsky walizigawa upya sifa hizo katika makundi matano:

 

  1. Sifa za makundi makuu
  2. Sifa za chemba
  3. Namna ya kutamka
  4. Sifa za chasili
  5. Sifa za kiarudhi

 

Sifa za makundi makuu

Zilitumiwa kuzitenganisha sauti ambazo zinatofautiana mno. Hapa walitenganisha irabu na konsonanti na pia walitenganisha aina mbalimbali za konsonanti.

Hapa zilitumiwa sifa za 1 usonoranti na 2 ukonsonanti.

 

 

Sifa za chemba

Sifa za chembe zilitumika kueleza mkao wa chemba cha kinywa na pia mahali kitamkwa fulani kinapotamkiwa katika chemba cha kinywa kama ni sehemu ya mbele, kati au nyuma ya kinywa. Hapa sifa mbili ziliangaliwa 1. korona 2 anteria.

 

 

Sifa ya Korona

Sifa ya korona ilitumiwa kuzipambanua zile sauti ambazo wakati wa kuzitamka bapa la ulimi huwa limeinuliwa kutoka nafasi yake ya kawaida chini kuelekea juu kwenye kaakaa gumu. Ulimi unaweza kuwa nusu chini au nusu juu alimradi haupo chini.

 

Sifa ya Anteria

Sifa ya anteria hutumiwa kuzipambanua sauti zote zinazotamkiwa mbele ya kaakaa gumu, kwa ujumla zinazotamkiwa sehemu ya mbele ya kinywa kwa kuzitofautisha na zile zinazotamkiwa baada ya kaakaa gumu ambazo zinatamkiwa nyuma ya chemba chembe cha kinywa. Sauti hizi hupewa sifa ya [+anteria] na zile za nyuma hupewa sifa ya kutokuwa za mbele [-anteria].

 

 

Sifa za namna ya utamkaji

Sifa za namna ya utamkaji zilitumika pia kupambanua sauti mbalimbali za lugha. Sifa hizi zilizotumika ni pamoja na:

-        Sifa za kuwa vifulizwa au la. Vifulizwa ni vitamkwa ambavyo hutamkwa kwa mwendeleo mfano [l, r, f au s]. Sauti zote ambazo zilitamkwa kwa kuendelea zilipewa sifa ya ya [+ kifulizwa] na zile ambazo hazitamkwi kwa kuendelea zilipewa sifa ya kutokuwa vifulizwa [-kifulizwa]

-        Sifa nyingine za namna ya kutamka zilizoangaliwa ni zile zinazotofautisha sauti kali na zile hafifu. Sauti kali ni zile ambazo wakati wa utamkaji nyuzi sauti huwa zimekaza na hafifu huwa nyuzi sauti zinakuwa zimelegea.

 

 

Sifa za chasili

Katika sifa ya chasili ziliangaliwa sifa kuu mbili ambazo ya kwanza ni sifa ya ughuna na pili ni sifa ya stridenti na melo

 

-        Sifa ya ughuna imetumika kuzibainisha sauti ambazo hutamkwa wakati nyuzi sauti zinapokuwa zinatetema. Sauti ghuna hupewa sifa hiyo kwa kuwekewa alama ya [+ghuna] ambayo huzitofautisha na sauti zile ambazo si ghuna kwa kuziwekea alama [-ghuna] kuonyesha kuwa si ghuna. Sauti ambazo ni ghuna wakati wa kuzitamka nyuzi sauti zinakuwa zinatetema na sauti si ghuna wakati wa kuzitamka nyuzi sauti huwa hazitetemi.

-        Sifa za Stridenti imetumika kuzitofautisha zile sauti ambazo hutamkwa zikiwa na nguvumkazo za juu na pia kuwa na kasimawimbi ya juu kiasi kuwa kasimawimbi ya chini huzidiwa. Mfano ni kama vile f, v, th, dh, s, z. sh, zh, h.

-        Sifa za  Melo zimetumika kuzibainisha sauti ambazo zimetulia zaidi na hazina nguvumkazo za juu sana na kasimawimbi ni ya chini. Sauti zenye sifa ya melo huwekewa alama [+melo]

 

 

Sifa za kiarudhi

Sifa bainifu za kiarudhi ni zile sifa ambazo huwekwa kwenye vipashio vikubwa kuliko sauti au foni. Sifa hizo zinaweza kuwekwa kwenye silabi, neno, kirai au sentensi. Baadhi ya sifa za kiarudhi zilizotumiwa ni pamoja na mkazo, kidatu, kiimbo na toni.

 

Mkazo ni sifa ya kiarudhi inayohusu jinsi watu wanavyotamka maneno kwa nguvu zaidi katika sehemu fulani fulani. Kwa kawaida lugha nyingi huwa na mikazo ya aina kuu mbili ambayo ni mkazo katika sentensi na mkazo katika neno.

 

Mkazo katika sentensi huwekwa mahali fulani katika sentensi kulingana na aina ya sentensi. Kwa mfano mkazo katika sentensi ya maelezo ni tofauti na mkazo katika sentensi ya kuuliza.

 

Mkazo katika neno huwekwa katika silabi fulani kwenye neno. Kila lugha huwa na utaratibu wake wa kuweka mikazo katika maneno ya lugha hiyo. Lugha nyingine mahali pa mikazo katika neno hapabadiliki lakini kuna lugha nyingine ambazo mahali pa mikazo hubadilika badilika. Mfano katika Kiswahili mkazo huwekwa katika silabi ya pili kutoka mwisho.

 

Kidatu ni sifa ya kiarudhi ambayo inahusu kasi ya mitetemo ya nyuzi sauti. Wanafonetiki hupima kidatu kwa kuhesabu mizunguko ambayo nyuzi sauti huifanya katika nukta moja. Mizunguko inahesabiwa kwa kuangalia idadi ya mitetemo ambayo hufanywa na nyuzi sauti kwa nukta moja. Nyuzi sauti zitakapofanya mizunguko mingi zaidi basi sauti itakayotoka huwa ya kidatu cha juu, yaani ni kali, lakini nyuzi sauti zikifanya mizunguko michache katika nukta sauti inayotoka huwa ya kidatu cha chini kwa maana inakuwa sauti ya chini. Kidatu kinaweza kuwa cha juu, cha kati au cha chini. Hivyo kidatu kinahusiana moja kwa moja na kiwango cha sauti inayosikika. Mtu akiwa anazungumza hubadilisha vidatu kutokana na hali aliyo nayo, mfano kama akiwa na furaha, huzuni, hofu, hasira anaweza kubadilisha vidatu vyake ili kuonyesha hali hiyo.

 

 

Toni ni kiwango cha kidatu pamoja na mabadiliko yake ambayo hutokea wakati mtu anapotamka silabi au maneno. Katika lugha za toni mabadiliko ya toni hubadili maana ya yale yanayosemwa. Katika lugha hizo toni ni miongoni mwa sifa bainifu za lugha hizo. Kiswahili si lugha ya toni hivyo toni si sifa bainifu katika lugha hii.

 

Kiimbo ni utaratibu wa upandaji na ushukaji wa mawimbi ya sauti katika usemaji wa lugha. Kiimbo ni umbile zima la uzungumzaji wa mtu au kundi la watu. Kiimbo kinahusisha mambo yote yanayohusiana na uzungumzaji. Katika kiimbo kuna kidatu, mkazo, toni, uzuri wa sauti na sifa nyingine zote za uzungumzaji. Kiimbo kinatusaidia kutambua lengo la usemaji uliokusudiwa na mzungumzaji, tunaweza kutambua kama mzungumzaji anatoa maelezo, anauliza swali au anatoa amri.

Kutokana na mabadiliko ya kiimbo ambayo yanaonyesha lengo au maana anayokusudia mzungumzaji, tunaweza kupata aina kuu nne za viimbo ambavyo ni kiimbo cha maelezo, kiimbo cha maulizo, kiimbo cha amri na kiimbo cha mshangao.

Katika kiimbo cha maelezo mawimbisauti ya usemaji wake kwa kawaida huwa yanakuwa yamelingana.

Katika kiimbo cha maulizo vidatu huwa tofauti kutegemea aina ya swali linaloulizwa na kawaida mwishoni msemaji hupandisha kidatu.

Katika kiimbo cha amri, mzungumzaji hutumia kidatu cha juu zaidi kuliko ilivyo kwenye kiimbo cha maelezo.

Mawimbisauti ya kiimbo cha mshangao hutolewa huku yakiambatana na kupandisha, kushusha na kupandisha kidatu katika silabi za mwishoni mwa neno.

 

Wakaa ni sifa ya kiarudhi ambayo hujidhihirisha katika lugha nyingi. Wakaa ni ule muda ambao hutumika kutamka sauti fulani. Mara nyingi sauti huwa na wakaa wa aina tatu: wakaa wa kawaida, wakaa mfupi kuliko kawaida na wakaa mrefu kuliko kawaida. Katika baadhi ya lugha wakaa huwa ni sifa bainifu, hivyo watumiaji huteua wakaa unaofaa. 

 

 

 

 

FONOLOJIA

Fonolojia ni nini?

Fonolojia kama taaluma inayohusu lugha ni tawi la Isimu linaloshughulikia uchambuzi wa mfumo wa sauti za lugha fulani.

Fonolojia ni tawi la isimu ambalo hujishughulisha na uchunguzi, uchambuzi na uainishaji wa sauti pambanuzi ambazo hutumika katika mifumo mbalimbali ya sauti za lugha za binadamu (FOKISA).

Fonolojia hujishughulisha hasa na zile sauti ambazo hutumika katika kutofautisha maana za maneno katika lugha mahsusi.

Fonolojia hujihusisha na sheria au kanuni zinazoandamana na utoaji na utumiaji wa sauti hizo pambanuzi.

Fonolojia hujishughulisha na vipengele mbalimbali ambavyo vinahusiana na sauti na mpangilio wake wa uundaji wa maneno katika lugha mbalimbali. Vipengele hivyo ni kama vile matamshi, kiimbo, mkazo, lafudhi, toni, mfuatano wa sauti katika kuunda silabi, mfuatano wa sauti katika kuunda mofimu, mfuatano wa mofimu katika kuunda maneno na otografia.

 

Tofauti kati ya Fonetiki na Fonolojia

Fonetiki na Fonolojia ni matawi mawili ya isimu yaliyo jirani sana na wakati wote matawi haya hutegemeana na kukamilishana.

 

Matawi yote mawili yanachunguza kitu kimoja ambacho ni sauti za lugha.

Hata hivyo, ingawa taaluma hizi huchunguza sauti za lugha, lakini Fonetiki huzichunguza sauti bila kuzingatia mfumo ambamo sauti hizo hutumika, huchunguza sauti zote za lugha kwa ujumla, lakini Fonolojia huzichunguza sauti zilizo katika mfumo mmoja yaani lugha mahsusi. Kwa hali hiyo taaluma ya fonetiki ni moja tu, lakini Fonolojia ni nyingi kama ilivyo idadi ya lugha duniani. Hivyo tuna fonolojia za lugha mbalimbali kama vile fonolojia ya Kiswahili, fonolojia ya Kihehe, fonolojia ya Kichaga, Fonolojia ya Kifaransa, nk. Ina maana kila lugha ina fonolojia yake ambayo ni tofauti na fonolojia ya lugha nyingine.

 

Wanafonetiki wamekusanya sauti nyingi kutoka katika lugha mbalimbali duniani na bado wanaendelea kukusanya. Fonolojia ya lugha fulani hutumia sehemu ndogo tu ya sauti hizo zilizokusanywa. Fonetiki ni sawa na seti kuu ambamo sauti za lugha mbalimbali duniani hutunzwa na Fonolojia ya lugha ni sehemu ya seti hiyo.

 

Seti kuu (Fonetiki) ni seti isiyo na kikomo, lakini Fonolojia zote zina kikomo. Inaaminika kuwa lugha nyingi duniani hutumia wastani wa sauti kati ya ishirini na arobaini tu. Kiswahili kina fonimu thelathini na moja tu.

 

Katika kiwango cha Fonetiki sauti zote huorodheshwa na kutolewa ufafanuzi makini ambao huonyesha tofauti zote za kifonolojia katika foni. Ufafanuzi wa kifonolojia huzionyesha zile sifa bainifu ambazo ni bainifu katika lugha mahsusi inayoshughulikiwa, yaani sifa ambazo si bainifu katika lugha fulani si lazima zitumike kuzifafanua fonimu za lugha hiyo.

 

Kipashio cha ufafanuzi wa kifonetiki ni foni, ambacho ni kipande kidogo kabisa cha sauti ambacho hakihusishwi na lugha yoyote. Kipashio kidogo kabisa cha ufafanuzi wa kifonolojia ni fonimu.

 

Uchambuzi wa kifonetiki hauzingatii mfumo maalum wa lugha, lakini uchambuzi wa kifonolojia huzingatia mfumo maalum wenye taratibu maalum na hauishii katika kuzichambua fonimu tu, bali huchunguza mambo mengine pia kama vile mfuatano wa fonimu katika kuunda silabi, neno, nk.

 

Katika sifa za kiarudhi, fonetiki huzibainisha na kuzieleza sifa hizo kama zinavyotokea katika lugha mbalimbali. Fonolojia hushughulikia zile sifa za kiarudhi ambazo ni bainifu katika lugha inayoshughulikiwa na kuziacha zile ambazo si sifa bainifu katika lugha mahsusi inayochunguzwa.

Fonetiki na Fonolojia hutegemeana na kukamilishana. Uchambuzi wa kifonetiki husaidia uchambuzi wa kifonolojia na uchambuzi wa kifonolojia husaidia uchambuzi wa kifonetiki.

 

Fonetiki ni msingi imara ambao husaidia uchambuzi wa kifonolojia. Mtu asipokuwa na ujuzi wa Fonetiki atapata shida kufanya uchambuzi wa kifonolojia, mfano kuziorodhesha sauti mbalimbali anazosikia katika lugha fulani kwa kutumia alama maalum zinazowakilisha sauti na kuzifafanua sauti hizo kwa kutumia sifa bainifu.

 

Fonetiki huzipata foni zote kutoka lugha mbalimbali, yaani kutoka fonolojia za lugha mbalimbali, hivyo inaaminika kuwa kama zisingekuwepo fonolojia za lugha mbalimbali, wanafonetiki wasingekuwa na cha kuchunguza. Hivyo uchunguzi wa kifonolojia hutarajiwa kuwa nyenzo ya uchambuzi wa kifonetiki ambao hutuwezesha kuelewa muundo wa lugha inayochunguzwa.

 

Dhana ya fonimu

Fonimu zimeshughulikiwa na wanaisimu mbalimbali na baada ya uchunguzi wa muda mrefu wamefikia kuifafanua dhana ya fonimu kwa mitazamo mitatu:

-        Fonimu ni tukio la kifonetiki

-        Fonimu ni tukio la kisaikolojia

-        Fonimu ni tukio la kifonolojia

 

Fonimu kama tukio la kifonetiki

Fonimu ni kundi la sauti katika lugha fulani lenye sauti muhimu (fonimu yenyewe) pamoja na sauti zinazohusiana nayo na ambazo hutumiwa mahali pake katika miktadha maalum (alofoni). Ina maana kuwa fonimu zinaweza kutambuliwa na kutofautishwa na fonimu nyingine kwa kuangalia sifa za kifonetiki za fonimu hizo.

 

 

Fonimu kama tukio la kisaikolojia

Mtazamo huu unaoangalia fonimu kama tukio la kiasikolojia unaungwa mkono na wanaisimu wa Sarufi Zalishi. Mwasisi wa Sarufi Zalishi alikuwa Noam Chomsky akidai kuwa lugha ina mambo makuu mawili yaani umilisi na utendaji. Anadai kuwa mtu anapojifunza lugha huanza na umilisi. Anaendelea kuwa umilisi ni ule ujuzi wa lugha walio nao wazawa wa lugha fulani.

Mwanaisimu mwingine Boduin de Courtney anadai kuwa fonimu ni tukio la akilini ambalo huwa na nia ya mzungumzaji au jinsi anavyomwelewa mzungumzaji au vyote kwa pamoja. Ina maana kuwa watumiaji wa lugha fulani huzijua fonimu zote za lugha yao.

Pia wanaeleza kuwa fonimu ni dhana ya kisaikolojia kwa kuwa ni kipandesauti ambacho picha yake huwa akilini mwa mtu ambaye hukusudia aitoe wakati anapoongea.

Watetezi wa mkabala huu wanadai kuwa kila fonimu ina sifa zake katika lugha inamotumika na sifa hizi zote hufahamiwa na watumiaji wa lugha husika – kisha huwekwa akilini mwao. Wakati wa kuzungumza au kusikiliza mtu mwingine akiongea picha hiyo ya akilini ndiyo ambayo humwongoza aseme kile anachosema na aelewe kinachosemwa na wengine. Hii ndiyo sababu inayofanya fonimu ionekane kama tukio la kisaikolojia.

 

Fonimu kama tukio la kifonolojia

Mtazamo huu unawakilishwa na kikundi cha wanaisimu wa Prague chini ya mwanaisimu maarufu kwa jina Trubetskoy (1890-1938). Wanaisimu wa kundi hili walisisitiza mkabala wa kuangalia aumilifu wa vijenzi mbalimbali vya lugha. Walidai kuwa fonimu ni kipashio cha kifonolojia ambacho ni lazima kitazamwe ndani ya mfumo wa fonolojia kinamotumika. Ili kuielewa fonimu ni lazima kuchunguza uamilifu wa fonimu hiyo katika mfumo mzima wa fonolojia inamotumika.

Hapa mkazo unawekwa kwenye kazi mbalimbali ambazo hufanywa na fonimu fulani katika lugha maalumu.

Mtazamo huu haukatai kuwa kuwa kila fonimu ina sifa zake za kifonetiki, bali mtazamo huu unadai kuwa ingawa fonimu zote zina sifa za kifonetiki lakini sifa hizo za kifonetiki sizo zinazoifanya fonimu ya lugha fulani iwe fonimu, bali uamilifu wa fonimu ya lugha fulani huifanya kuwa fonimu.

Pia wanadai kuwa ili fonimu iweze kuwa fonimu katika lugha fulani lazima iwe bainifu kwa maana kwamba kama fonimu hiyo ikiwekwa mahali ambapo palikuwa na fonimu nyingine, maana ya neno jipya lazima ibadilike au ipotee. Mfano:

/p/ + /a/ +/k/ + /a/ - paka

/t/ + /a/ +/k/ + /a/ - taka

/s/ + /a/ +/k/ + /a/ - saka

/d/ + /a/ +/k/ + /a/ - daka

Kwa mifano hiyo tunaweza kusema foni [p], [t], [s], [d] ni fonimu katika lugha ya Kiswahili kwa sababu ni bainifu, yaani zinaweza kutofautisha maana katika maneno.

Trubetzkoy alitoa fasili ya fonimu kuwa ni kipashio kidogo kabisa katika lugha chenye uamilifu wa kutofautisha maana katika maneno.

 

Kila lugha ina namna yake ya kuziweka fonimu pamoja ili kupata vipashio vikubwa zaidi, kama vile silabi, maneno, nk. Kwa maneno mengine ni kuwa kila fonimu ina nafasi yake maalum katika kushirikiana na fonimu nyingine katika lugha inamotumika. Mfano /i/ katika Kiswahili ina uamilifu tofauti na /i/ katika Kiingereza. Kwa hali hiyo utaona wazi kuwa sauti za lugha mbalimbali huweza kufanana kifonetiki lakini matumizi ya sauti hizo yanaweza kutofautiana baina ya lugha moja na nyingine.

 

Fonimu katika lugha tofauti zina uamilifu tofauti haufanani na uamilifu wa fonimu ya lugha nyingine yenye sifa zinazofanana kifonetiki. Sababu mojawapo ya lugha kutofautiana ni kutokana na kuwa na fonimu tofauti na pia sababu nyingine ni kuwa uamilifu wa fonimu katika lugha mbalimbali hutofautiana. Ili kuielewa vizuri fanimu inabidi kuangalia uamilifu wa fonimu hiyo katika fonolojia ya lugha inamotumika fonimu hiyo (ndiyo maana likaitwa tukio la kifonolojia). 

 

Baada ya kuangalia mitazamo hiyo mitatu tutaona kuwa yote inaeleza mambo yanayofaa na mazuri, tofauti zipo katika mambo yanayotiliwa mkazo.

Mtazamo wa kwanza wa kifonetiki unasisitiza kuwa kila fonimu lazima iwe na sifa zake za kifonetiki kwa kuwa fonimu ni sauti ambayo hutamkwa ikasikika.

Mtazamo wa kisaikolojia unasisitiza umilisi na utendaji kwa maana kwamba watumiaji wa lugha huzifahamu fonimu za lugha yao na ufahamu huo ndiyo sehemu ya umilisi au ujuzi wa lugha. Ujuzi huu hukaa akilini mwao ambao unajumuisha  kujua sifa za kifonetiki za fonimu na sifa za kifonolojia za fonimu zote na   namna fonimu hizi zinavyotumika katika lugha.

Mtazamo wa kifonolojia unaosisitiza uamilifu wa fonimu unaeleza kuwa ili kuijua fonimu fulani lazima ujue matumizi yake. Na ili ujue matumizi yake ni lazima ujue sifa za kifonetiki za fonimu hiyo.

 

Sifa za Fonimu

Fonimu zina sifa za jumla zifuatazo:

  1. Kila fonimu inazo sifa zake za kifonetiki zinazoweza kuelezwa ili kuifafanua fonimu hiyo.
  2. Kila fonimu inazo sifa zake za kifonolojia ambazo huonyesha uamilifu wa fonimu hiyo katika lugha mahsusi.
  3. Watumiaji wa lugha fulani huzielewa sifa zote za fonimu za lugha yao ikiwa ni sehemu ya umilisi wao wa lugha hiyo.
  4. Kila fonimu hushiriki kujenga na kutofautisha maana katika maneno.
  5. Fonimu moja peke yake haina maana, yaani si kiashiria cha kiashiriwa chochote.
  6. Ukibadili fonimu katika neno bila shaka maana ya neno hilo itabadilika.
  7. Ukiongeza fonimu katika neno lolote maana ya neno hilo itabadilika au kupotea.
  8. Ukipunguza fonimu katika neno lolote maana ya neno hilo itabadilika au kupotea.
  9. Ukipangua mpangilio wa fonimu katika neno maana ya neno hilo itabadilika au kupotea.
  10. Kila lugha ina fonimu zake na fonimu za lugha tofauti hazifanani katika uamilifu wake.

 

 

Alofoni

Sauti mojawapo miongoni mwa sauti kadhaa zinazoiwakilisha fonimu moja. Alofoni hutokea katika mazingira mahsusi (Hartman 1972).

 

Alofoni ni sura au maumbo mbalimbali ya fonimu moja yanayotokea katika mazingira tofauti. Fonimu za lugha moja huweza kupata sura tofautitofauti kulingana na mazingira ambamo hutokea. Ina maana kuwa fonimu inaweza kubadilika na kuchukua umbo moja kutokana na kutokea kwake katika mazingira fulani na inaweza kubadilika na kuchukua umbo jingine kutokana na kutokea kwake katika mazingira mengine tofauti. Mfano katika Kiswahili tunaweza kupata alofoni za fonimu zifuatazo:

ki + ti ki + refu [kiti kirefu]

ki + ti ki + eusi [kiti cheusi] fonimu /k/ inapofuatiwa na irabu kukawa na mpaka wa mofimu, kisha kufuatiwa na irabu e hubadilika kuwa ch /tʃ/ kieusi – cheusi. Mfano wa maneno mengine ni kama kioo kieupe – kioo cheupe.

U + limi m + refu [ulimi mrefu]

n + limi  n + refu [ndimi ndefu]

fonimu /l/ inapotanguliwa na nazali n hubadilika na kuwa d (n + limi = ndimi). Hii ina maana kuwa katika mazingira haya sauti ch ni alofoni ya fonimu /k/ na d ni alofoni ya fonimu /l/.

 

Mbinu za kuzitambua Fonimu

 

Njia mbalimbali zinaweza kutumika kuzibainisha fonimu za lugha. Njia hizo ni pamoja na:

-        Kufanana kifonetiki

-        Jozi za mlinganuo finyu

-        Mgawanyo wa kiutoano

-        Mpishano huru

 

Kufanana kifonetiki

Sauti zinazofanana kifonetiki ni sauti zilizo na sifa bainifu zinazofanana. Sifa bainifu tumeshazijadili katika vipindi vilivyotangulia. Tuliona kuwa irabu zina sifa bainifu zao na konsonanti zina sifa bainifu zao. Kila lugha huteua baadhi ya sifa bainifu zinazotumika kubainisha foni katika kiwango cha fonetiki na kuzitumia kuzifafanua fonimu za lugha hiyo.

Sauti zinazoweza kufikiriwa kuwa ni fonimu moja lazima zifanane sana kifonetiki. Mfano hatuwezi kufikiria kuwa [i] na [a] ni fonimu moja kwa sababu zinatofautiana sana kifonetiki yaani sifa bainifu zao ni tofauti sana. [i] +irabu, +mbele, +juu, -mviringo na [a] +irabu, +mbele, +chini, -mviringo. Kwa kuangalia sifa za irabu hizi utaona kuwa hizi ni irabu tofauti kwa kuwa hazifanani kwa sifa zote za kifonetiki, na kwa hali hiyo haziwezi kuwa sauti za fonimu moja.

Hii ni mbinu mojawapo inayosaidia kutambua sauti za fonimu moja ni kufanana kwao kifonetiki.

 

Jozi za mlinganuo finyu

Mlinganuo finyu ni tofauti ndogo kabisa ya kifonolojia iliyopo baina ya maneno fulani. Maneno hayo mara nyingi huwa na:

-        idadi sawa ya fonimu,

-        fonimu zinazofanana isipokuwa moja,

-        mpangilio wa fonimu ulio sawa.

Mfano wa mlinganuo finyu ni kama vile maneno /pita/ na /piga/ maneno haya yana tofauti ya mlinganuo finyu kwa sababu:

-        Yana idadi sawa ya fonimu (yote yana fonimu nne).

-        Fonimu zilizopo zinafanana isipokuwa moja, yaani maneno yote yana fonimu /p/, /i/ na /a/. tofauti ni katika fonimu /t/ na /g/.

-        Mpangilio wa fonimu unafanana kwa kuwa /p/ na /i/ zinaanza na fonimu /t/ na /g/ zipo kwenye nafasi ya tatu na hizi ndizo zinazotoautiana kisha mwishoni kuna /a/.

Baada ya kuona mlinganuo finyu utaona unapatikana kwa kulinganua maneno mawili yenye tofauti ndogo. Hivyo jozi ya mlinganuo finyu ni maneno mawili au orodha mbili za maneno ambayo tofauti zao ni ndogo.

Kigezo hiki cha mlinganuo finyu ni cha kiuamilifu kwasababu ingawa maneno hayo yana tofauti ndogo lakini baada ya kuweka fonimu yenye sifa tofauti za kifonetiki neno linalopatikana lazima liwe la lugha husika na pia neno linalipatikana liwe na maana tofauti na neno la awali.

 

Mgawanyo wa kiutoano

Hii ni mbinu nyingine ya kutambua fonimu. Mbinu hii hutumiwa kuonyesha uhusiano uliopo baina ya sauti mbili au zaidi za fonimu moja ambazo haziwezi kutokea katika mazingira yanayofanana. Sauti ina mazingira maalum ambayo hayawezi kukaliwa na sauti nyingine. Mbinu hii inatuwezesha kutofautisha fonimu na alofoni. Tuangalie mfano ki + eusi = ch + eusi pale k ilipofuatiwa na i kwenye mpaka wa mofimu na kufuatiwa na e ilibadilika kuwa ch.

 

 

Mpishano huru

Maneno mawili yanaweza kuwa  na tofauti ya fonimu moja tu lakini ukiangalia fonimu hizo zilizo tofauti utaona kuwa fonimu hizo kwanza zinatofautiana sana kifonetiki na haziwezi kuwa alofoni za fonimu moja. Pili, utaona fonimu hizo zinazotofautiana kifonetiki hazipo kwenye uhusiano wa kiutoano yaani zinaweza kutumika katika mazingira yaleyale kwenye neno lakini ingawa fonimu hizi ni tofauti hazisababishi tofauti za maana katika maneno zinamotokea.

Katika mpishano huru fonimu mbili ambazo ni tofauti kabisa zinaweza kubadilishana, yaani kila moja inaweza kutumiwa badala ya nyingine bila kubadili maana katika maneno hayo.

Hii ni kinyume na hoja ya msingi ya fonimu inayosema kuwa ukibadili fonimu yoyote katika neno maana ya neno itabadilika.

Tofauti kati ya mpishano huru na mgawanyo wa kiutoano:

-        Mpishano huru unahusisha fonimu mbili au zaidi zilizo tofauti kabisa, wakati mgawanyo wa kiutoano huzihusisha alofoni mbili au zaidi za fonimu moja zinazofanana sana kifonetiki; za aina moja na zinazotamkiwa sehemu moja.

-        Mpishano huru unhusisha fonimu mbili zinazobadilishana nafasi moja katika neno, wakati mgawanyo wa kiutoano unahusisha alofoni ambazo zimegawana mahali tofauti pa kutokea. Kila moja ina muktadha wake maalum ambao alofoni nyingine haiwezi kutokea.

-        Kufanana: katika mpishano huru na mgawanyo wa kiutoano maana za maneno hazibadiliki.

 

Mifano ya mpishano huru:

angalau – angalao /u/ na /o/

wasia – wosia  /a/ na /o/

badili – badala /i/ na /a/

amkia – amkua /i/ na /u/

baibui – buibui /a/ na /u/

 

 

Fonimu za Kiswahili

Fonimu za Kiswahili zinaweza kugawanywa katika aina kuu tatu ambazo ni:

  1. Fonimu za irabu
  2. Fonimu za nusu irabu au viyeyusho
  3. Fonimu za konsonanti

 

Sifa za bainifu za fonimu ni sawa na sifa za foni zilizojadiliwa katika vipindi vilivyotangulia.

SILABI

Silabi ni kipashio cha kifonolojia ambacho kwa ukubwa kipo kati ya fonimu na neno. Silabi ni ndefu zaidi kuliko fonimu na fupi kuliko neno.

Kipashio cha kifonolojia kinachohusu matamshi ambacho sauti za lugha hutamkwa mara moja kwa pamoja kama fungu moja la sauti.

Kwa hali hiyo maneno ya lugha hutamkwa kwa kufuata utaratibu wa silabi.

Ingawa maneno ya lugha hutamkwa kwa kufuata utaratibu wa silabi, lakini kila lugha ina muundo wake wa silabi na namna ya utamkaji wake. Fonimu zinapokaa pamoja hujenga silabi ambazo huweza kutamkwa kama kitu kimoja.

 

Aina za silabi

Wanaisimu wamegundua kuwa zipo aina mbili za silabi katika lugha:

-        Silabi huru au wazi

-        Silabi funge

 

Silabi huru au wazi

silabi huru ni silabi ambazo mara nyingi huishia na irabu. Sauti za silabi huru huwa na msikiko au mvumo wa juu. Kutokana na kuishia na irabu silabi huru huwa zinakuwa na msikiko mkubwa zaidi. 

 

Silabi funge

Ni silabi ambazo huishia na konsonanti. Silabi funge kwa kawaida huwa na msikiko ambao ni hafifu. Kutokana na kuishia na konsonanti msikiko wake huwa na mvumo hafifu.

Wanafonolojia walio wengi wanaamini kuwa kwa kawaida silabi ina sehemu kuu tatu ambazo ni

-        mwanzo wa silabi

-        kilele cha silabi

-        mwisho wa silabi

Sehemu ya mwanzo na mwisho wa silabi ni sehemu ambazo husaidia kuweka mipaka ya kati ya silabi zinazofuatana

Sehemu ya mwanzo wa silabi hujulikana kama kilele au kiini cha silabi huwa katikati ya silabi na husikika kwa nguvu zaidi kuliko sehemu ya mwanzo na sehemu ya mwisho. Katika lugha nyingi irabu hukaa kwenye kiini cha silabi.

Mara nyingi kila silabi inakuwa na irabu kama kilele chake, iwe silabi huru au silabi funge.

Irabu ikiwa peke yake au miongoni mwa sauti nyingine zinazounda silabi, irabu husikika kuwa kilele cha silabi.

Kuna baadhi ya lugha ambazo hutumia baadhi ya konsonanti pekee kama silabi, mfano nazali [m] na [n] na kitambaza [l]. Katika Kiswahili nazali [m] na [n] huweza kusimama peke yake kama nazali, mfano /m-tu/, /m-ka-te/.

 

Miundo ya silabi za Kiswahili

Lugha ya Kiswahili inayo miundo kadhaa ya silabi. Miundo hiyo ni kama hii ifuatayo:

  1. silabi za irabu
  2. silabi za konsonanti
  3. silabi za konsonanti + irabu
  4. silabi za konsonanti + konsonanti + irabu
  5. silabi za konsonanti + nusu irabu +irabu
  6. silabi za konsonanti + konsonanti + nusu irabu + irabu
  7. silabi za konsonanti + konsonanti + konsonanti + irabu
  8. silabi za konsonanti + irabu + konsonanti (silabi funge)

 

Silabi za irabu

Kiswahili kina irabu tano ambazo kila moja huweza kuwa silabi katika miundo ya maneno mbalimbali mfano:

u + a = ua

o+ a = oa

a + u + au

pa + u + a = paua

te + u + a = teua

 

silabi za konsonanti

Lugha ya Kiswahili huziruhusu naadhi ya konsonanti kuwa silabi katika maneno. Konsonanti zinazoweza kuwa silabi katika Kiswahili ni nazali /m/ na /n/ tu. Konsonanti hizi huwa silabi katika mazingira maalum na mara nyingi huwa zinakuwa katika nafasi ya mwanzoni au katikati ya neno. Mifano ni maneno kama:

m+ pa + ka = mpaka

m + ga + nga = mganga

n + chi = nchi

n + ta = nta

na + m + na = namna

n + ne = nne

pa + m + pu = pampu

pa + n + cha = pancha

 

silabi za konsonanti + irabu

Muundo huu wa silabi wa konsonanti + irabu ndio ulioshamiri zaidi si katika Kiswahili pekee, bali katika lugha nyingi duniani. Katika muundo huu maneno huweza kuwa na silabi moja, silabi mbili au zaidi.

Mfano:

pa

la

ka + ka = kaka

da + da = dada

sa + ma + ki = samaki

ta + pa + ta + pa = tapatapa

ta + ka + ta + ka = takataka

 

silabi za konsonanti + konsonanti + irabu

Katika Kiswahili konsonanti za mwanzo katika muundo huu wa silabi huwa ni vitamkwa vya nazali /m/ na /n/. Vitamkwa hivi huwa vinafungamana na konsonanti inayofuata ili kuunda muundo huu. Mfano:

pe + nda = penda

u + nga = unga

nja + ma = njama

mba + li = mbali

mbe + ya = mbeya

Pamoja na muundo huu wa nazali kutangulia, pia kuna baadhi ya silabi zenye kuanza na vitamkwa visivyo nazali. Muundo huu pia unahusisha konsonanti zisizo nazali. Konsonanti zinazokabiliana katika muundo huu wa silabi huwa hazikubaliani katika muundo wa lugha za kibantu. Mfano:

la + bda = labda

da +fta +ri = daftari (mgulu ameiita funge)

fa + ksi = faksi

se + kta = sekta

sto + o = stoo

 

 

silabi za konsonanti + nusu irabu (kiyeyusho) +irabu

Kiswahili kina muundo mwingine wa silabi za konsonanti + kiyeyusho + irabu. Muundo huu hushirikisha vitamkwa /w/ na /y/ na kawaida konsonanti huwa mwanzoni zikifuatiwa na kiyeyusho, mfano:

mwa + nga = mwanga

a + fya = afya

pwe + za = pweza

m + pya = mpya

kwa + ni = kwani

 

silabi za konsonanti + konsonanti + konsonanti + irabu

Muundo huu unatumika zaidi kwa maneno ambayo yamekopwa kutoka lugha nyingine. Mfano:

skru + bu = skrubu

spri + ngi = springi

 

 

silabi za konsonanti + irabu + konsonanti (silabi funge)

Kiswahili kinazo pia silabi chache ambazo huishia na konsonanti, na zinajulikana kama silabi funge. Silabi funge zinapatikana zaidi katika maneno yasiyo ya kibantu, au maneno ya mkopo. Kumekuwa na utata mara nyingi kuhusu mahali pa kuweka mpaka wa silabi, yaani konsonanti ya mwisho ikae wapi? Mfano:

lab + da = labda

al + ha + mi + si = alhamisi

il + ha + li = ilhali

tek + no + lo + ji + a = teknolojia

 

 

 

MOFOLOJIA

Mofolojia ni nini?

Tawi la Isimu ambalo huchunguza maneno na aina za maneno.

Tawi la Isimu linalochunguza maumbo ya maneno na hususani maumbo ya mofimu.

Mofolojia huchunguza mofimu na alomofu zake na jinsi ambavyo hukaa pamoja kuunda maneno mbalimbali katika lugha zinamotumika.

Mfumo kamili wa mofimu katika lugha fulani. Hapa mofolojia inahusika na uchunguzi wa mofimu za lugha moja, yaani mofolojia ya lugha husika.

 

Mofolojia kama taaluma ya Isimu inalo jukumu la kuchunguza maneno ili kuelewa maumbo yao.

Mofolojia kama kiwango kimojawapo cha kila lugha, inatofautiana na viwango vingine vya lugha ambavyo ni fonolojia, sintaksia na semantiki.

 

Mofimu, mofu na alomofu

Mofimu ni kipashio kidogo amilifu katika maumbo ya maneno.

Mofimu ni kipashio kidogo kabisa cha kisarufi kilicho na maana.

Mofimu ni kipashio kidogo kabisa katika lugha chenye maana na zaidi ya hayo, maana hiyo hutofautiana na mofimu nyingine katika lugha hiyo.

Kipashio kidogo kina maana umbo la neno au umbo katika neno lisiloweza kugawanyika katika sehemu nyingine ndogo zaidi. Udogo wa kipashio si udogo wa kiumbo bali ni kiwango ambacho mofimu hiyo haiwezi kugawanywa zaidi na kulete maana. Hivyo mofimu inaweza kuwa kubwa kiwango cha neno mfano maneno dawa, moshi, jiwe, nk. na mofimu inaweza kuwa na kipashio kimoja kidogo kabisa kiumbo kama vile m katika umbo m-tu.

Kipashio kuwa amilifu maana yake ni kwamba kina kazi maalum kisarufi. Kazi hizo ni kama ile ya kuwa kiini kinachobeba maana ya msingi katika neno au kuwa kiambishi kinachowakilisha dhana au kipashio cha kisarufi. Mfano umbo m-toto, kipashio m ni mofimu inayofanya kazi kuonyesha umoja, na kubainisha kundi la nomino ambamo nomino hiyo imo na kipashio toto ni mofimu inayobeba maana ya msingi.

Mofimu inazo sifa kadhaa zinazoibainisha, na tatu kati ya hizo ni muhimu. Sifa hizo ni kama vile:

-        Mofimu ni kipashio chenye umbo halisi

-        Mofimu huwa na maana

-        Kila mofimu huwa na nafasi yake ya kisintaksia katika kushirikiana na vipashio vingine kuunda vipashio vikubwa zaidi.

Ubainishaji wa mofimu hufanyika kwa kuzingatia kuwa neno linaweza kugawanyika katika vipande. Mfano,

mtu – m+tu

mto – m+to

kitabu – ki-tabu

 

Katika lugha pia yapo maneno ambayo maumbo yake hayawezi kugawanyika katika vipande amilifu. Mfano katika Kiswahili ni kama vile:

panga, kisu, suruali, tunda, papai, godoro, nk.

Mofimu zinaweza kugawanyika katika makundi mawili, kundi la kwanza ni zile mofimu ambazo zinatokana na kugawanyika kwa umbo la neno na kuna mofimu ambazo ni sawa na neno kamili.

 

Mofu

Kipashio cha kimofolojia kinachowakilisha mofimu.

Mofu ni umbo la neno ambalo huwakilisha mofimu na ambalo hudhihirika kifonolojia na kitahajia. Mofimu ambazo ni elementi dhahania huwakilishwa na mofu ambazo hudhihirika ama kifonolojia kama sauti za kutamkwa au kitahajia zikiwa ni alama za kuandikwa. Mfano /f/, /l/, /n/, /p/ au d, g, m, t.

Tunaweza kusema

Mofu ni maumbo halisi ya maneno ambayo hutamkwa wakati watu wanapozungumza au kuandikwa wakati watu wanapoandika maneno.

 

Mofu hudhihirika kifonolojia na kitahajia – mofu mbalimbali hudhihirika kifonolojia zinapotamkwa na pia kimaandishi zinapoandikwa.

 

Mofu huwakilisha maana – katika neno lolote katika lugha yoyote kuna maana na maana hiyo imehifadhiwa katika mofu zilizo katika neno hilo.

 

Mofu ni kipashio kidogo kabisa cha neno chenye maana – mofu ni sehemu ndogo kabisa ambayo hubeba maana na sehemu hiyo haiwezi kugawanywa katika sehemu ndogo zaidi zenye maana.

Kiumbo mofu huweza kulingana sawa na fonimu na wakati mwingine huweza kulingana na neno zima. Mofu inaweza kuwa kiambishi cha neno na pia mofu inaweza kuwa mzizi wa neno, mfano: m-toto, m-ti, mbwa, baba, samaki, nk.

 

Alomofu

Umbo mojawapo kati ya maumbo kadhaa tofauti yanayowakilisha mofimu moja.

Ni viwakilishi viwili au zaidi vya mofimu moja lakini ambavyo hujitokeza katika mazingira tofauti ya mtoano. Mfano katika Kiingereza kiambishi tamati /s/ cha wingi kina alomofu zifuatazo:

/s/ katika maneno cats, books, cakes, nk.

/z/ katika maneno dogs, bags, tables

/iz/ katika maneno classes, boxes, boys

Katika Kiswahili mofimu kiambishi m, mw, mu hujitokeza, mfano:

m-tu

m-ti

m-toto

mw-ana

mw-angaza

mu-uguzi

m hujitokeza kabla ya mashina ya maneno yanayoanza na konsonanti wakati mw hujitokeza kabla ya mashina yanayoanza na baadhi ya irabu na mu hutokea kabla ya mashina yanayoanza na irabu u. Hivyo m, mu, mw ni alomofu za mofimu mu katika mazingira tofauti.

 

Hivyo mofimu inapokuwa na umbo moja tu, umbo hilo linaitwa mofu na wakati mofimu moja inapokuwa na maumbo zaidi ya moja yanayoiwakilisha mofimu hiyo, maumbo hayo yataitwa alomofu za mofimu hiyo. Tunaweza kusema kuwa alomofu ni mofu mojawapo miongoni mwa mofu za mofimu moja.

 

Aina za mofimu

Mofimu zinaweza kugawanyika katika aina mbili – mofimu funge na mofimu huru.

Mofimu funge ni vipande vya maneno ambavyo haviwezi kusimama kila kimoja peke yake kisarufi. Mofimu funge ikiondolewa kwenye muktadha wake hukosa maana na ni vigumu kujua maana yake bila kuiweka katika muktadha wake.

Mofimu funge zinaweza kutokea kama mizizi ya maneno mfano:

kat-

imb-

pot-

Pia mofimu funge inaweza kutokea kama kiambishi, mfano:

m-

ki-

-ish-

-ik

 

Mofimu huru ni maumbo yanayoweza kusimama peka yake kimaumbo, kileksika na kisarufi.

Ni mofimu ambazo zinaweza kusimama peke yao kama maneno kamili, mfano ni kama:

baba, mama, samweli, kuku, jani, safi, nk.

Mofimu ni kipashio dhahania cha umbo fulani ambacho kinaweza kuwakilishwa na mofu tofautitofauti katika mazingira anuwai.

 

 

Mofolojia kama taaluma inaweza kugawanywa katika matawi makuu mawili ambayo ni:

-        Mofolojia ya minyambuliko ya maneno

-        Mofolojia ya uundaji wa maneno

 

Mofolojia ya minyambuliko ya maneno hushughulikia zaidi minyambuliko ya maneno ambayo huwekwa kwenye mizizi ya maneno kuwakilisha maana mbalimbali lakini minyambuliko hiyo haibadili aina ya neno hilo. Mfano katika Kiswahili mzizi wa neno -toto unaweza kuwekewa viambishi m-, ka-, wa- kupata maneno m-toto, ka-toto, wa-toto, nk. Hapa utaona aina ya neno haikubadilika baada ya kunyambulishwa.

 

Mofolojia ya uundaji wa maneno hushughulikia uundaji wa maneno kwa kuweka viambishi kwenye mizizi ya maneno na kiambishi nyambuaji huweza kubadili aina ya neno.  Wakati viambishi mbalimbali vinapopachikwa kwenye mzizi wa neno, huwa linapatikana neno jipya na neno jipya linalopatikana si lazima liwe la aina moja na neno la awali na pia si lazima liwe la aina tofauti na neno la awali. Mfano katika Kiswahili: mzizi wa neno piga ni pig- tunaweza kuweka viambishi na kupata maneno kama ifuatavyo

pig-o

ma-pig-ano

m-pig-aji

 

Tofauti iliyopo kati ya mofolojia ya minyambuliko na mofolojia ya uundaji wa maneno ni kuwa katika mofolojia ya minyambuliko ya maneno hakuna maneno mapya yanayoundwa, lakini katika mofolojia ya uundaji wa maneno ni kuwa maneno mapya huweza kuundwa tofauti na maneno ya awali.

 

Maneno katika lugha mbalimbali yanaweza kugawanywa katika aina kuu mbili, ambazo ni:

-        maneno yasiyoambishwa au yasiyoweza kuwekewa viambishi

-        maneno yanayoambishwa au yanayoweza kuwekewa viambishi

 

Maneno yasiyoambishwa na yanayoambishwa huweza kutokea kwa viwango tofauti katika lugha mbalimbali. Baadhi ya lugha huwa na maneno yasiyoambishwa mengi zaidi kuliko yale yanayoambishwa, na lugha nyingine huwa na maneno mengi zaidi yasiyoambishwa kuliko yale yanayoambishwa.

 

Maneno yasiyoambishwa ni maneno yale ambayo hayawekewi viambishi vyovyote wakati wote yanapotumika, na mara nyingi maneno haya huwa ni mizizi. Mfano majina ya watu, Juma, Ali, Samweli; majina ya miji kama vile Moshi, Kibaha, Kisarawe; majina ya nchi kama vile Tanzania, Uganda, Kenya, nk.

 

Maneno yanayoambishwa ni yale maneno ambayo mizizi yao inaweza kuwekewa viambishi mbalimbali vinavyobeba maana mbalimbali. Katika Kiswahili yapo maneno mengi yanayoweza kuambishwa. Tunaweza kuweka viambishi kabla ya mzizi wa neno au baada ya mzizi wa neno. Mfano ki-tabu, vi-tabu, m-tu, pig-a

CCCCCCCCCCCCCCCCCCCCCCCCCCCCCCCCCCCCCCCCCCCCCCCCC

Mizizi, Viambishi na Mashina

 

Mzizi ni nini?

Mzizi ni umbo msingi la neno ambalo haliwezi kuchanganuliwa zaidi tena katika sehemu nyingine ndogo bila kupoteza uamilifu wake na utambulisho wake wa kisemantiki.

Mzizi ni mofimu katika neno ambayo huwakilisha taarifa ya kileksika.

Mzizi sehemu ya neno baada ya kuondoa viambishi vyote.

 

Aina za mizizi

Lugha nyingi duniani zina aina mbili za mizizi ambayo ni:

mizizi funge na mizizi huru.

 

Mzizi funge

Mzizi funge ni mzizi ambao hauwezi kujitegemea wenyewe, yaani hauwezi kusimama peke yake kama neno.

Mfano:

paka – pak + a

pakia – pak + i + a

mpaka – m + pak + a

mpako – m + pak + o

upakaji – u + pak + a + ji

 

Hapa umbo la msingi ni pak na utaona kuwa halibadiliki wakati wote bali linaongezewa viambishi, huu ndio mzizi wa neno. Utaona kuwa mzizi kama umbo la msingi huwa halibadilikibadiliki.

Katika lugha yoyote maneno yanayohusiana kimaana, huwa yanakuwa na umbo moja la msingi au mzizi ambalo linalojitokeza mara kwa mara.

Mzizi ambao ni umbo la msingi lina kawaida ya kutobadilikabadilika katika maneno yote yanayohusiana nalo, lakini maumbo mengine yote yanayobakia katika kila neno huweza kubadilikabadilika. Kubadilika kwa maumbo hayo mengine mara nyingi huongezea maana za ziada zinazohusiana na maana ya msingi inayobebwa na mzizi.

 

Mzizi huru

Mzizi huru ni mzizi ambao unaweza kusimama peke yake kama neno kamili. Umbo la mzizi huu haliwezi kuchanganuliwa katika sehemu ndogo zaidi bila kuathiri maana yake ya msingi. Mfano:

panga, godoro, bega, redio, jengo, gereza, mbwa, chui, ng'ombe, nk.

maneno hayo yote utaona kuwa yanajitegemea kimaana. Maneno hayo hayawezi kuchanganuliwa zaidi katika vipande vidogo zaidi bila kupoteza maana ya msingi.

 

Viambishi

Viambishi ni mofimu zinazoambatishwa kwenye mzizi wa neno ili kuwakilisha hali au dhana mbalimbali zinazofungamana na neno pamoja na mofimu hizo.

Viambishi ni mofu ambazo huongezwa kwenye mizizi ya maneno mbalimbali na viambishi hivyo huwakilisha maana fulani.

Viambishi mara nyingi huwa na maana za kisarufi zaidi na havina maana za kileksika.

Kulingana na nafasi katika neno viambishi vipo vya aina tatu:

-        viambishiawali

-        viambishindani au viambishikati

-        viambishitamati

Kulingana na majina yao, viambishi vinaweza kuwekwa mwanzoni, katikati au mwishoni mwa neno. Katika lugha nyingi viambishi huwekwa mwanzoni na mwishoni mwa mzizi, Kiswahili ikiwa moja ya lugha hizo.

 

Viambishiawali ni aina ya viambishi ambavyo huwekwa kabla ya mzizi wa neno. Viambishi hivi hutamkwa kabla ya mzizi wa neno wakati wa mazungumzo. Mfano m-toto; wa-toto; m-paka; ma-daftari

  

Viambishindani au viambishikati ni aina ya viambishi ambavyo huwekwa katikati ya mzizi wa neno. Mfano wa viambishi hivi tunaweza kuipata katika lugha nyingine, kama vile Kihaya, mfano neno a-bon-a (amepata) – a-b-o-i-n-e (alipata). Lugha ya Kiswahili haina viambishi vya aina hii.

 

Viambishitamati ni viambishi ambavyo huwekwa baada ya mzizi wa neno. Mifano:

kat-a; sak-a; saf-ish-a; pig-a-n-i-a; njoo-ni; imb-i-a

 

Kwa kawaida viambishi vyote ni maumbo tegemezi ambavyo hufanya kazi mbalimbali za kisarufi. Viambishi huwa havina maana vinapokuwa peke yao.

Lugha ya Kiswahili inatumia viambishi vya aina mbili tu ambavyo ni viambishiawali na viambishitamati.

 

Shina

Shina ni sehemu ya neno yenye mzizi na viambishi ambapo hakuna neno jipya linaloundwa bali huleta mabadiliko ya kisarufi katika neno hilihilo moja. Ni sehemu ya neno ambayo ikiambishwa haisababishi kuundwa kwa neno jipya, mfano: piga; piga-ni-a; piga-n-ik-a; a-li-piga.

Neno la msingi linabaki kuwa lilelile na maana ya msingi pia inabaki kuwa ileile.

Piga ni shina ambalo kutokana nalo tunapata hayo maumbo mengine bila kubadili maana ya msingi.

Mifano mingine ni baadhi ya mashina ya nomino ambayo pia huweza kuwekewa viambishi na kusiwe na neno jipya lililoundwa, mfano:

godoro; ma-godoro; ki-ji-godoro; gari; ki-gari; kongamano; ma-kongamano

 

Kuna maneno ambayo hayawezi kuwa mashina kwa sababu yakiwekewa viambishi huunda maneno mapya, mfano:

taifa – utaifa, taifisha, utaifishaji

shamba – ushamba, mshamba, kishamba

 

Tofauti nyingine kati ya mzizi na shina ni kuwa mzizi huundwa na mofimu moja tu wakati shina linaweza kuundwa na mofimu moja, ambayo ni mzizi, mfano mbegu, sahani, jembe; pia shina linaweza kuundwa na mzizi na kiambishi, mfano pig-a, kat-a; na vilevile shina linaweza kuundwa na mofimu mbili ambazo zote ni mizizi, mfano bata-mzinga, nguruwe-mwitu.

Ingawa mzizi unaweza kuwa shina, lakini si kila shina linaweza kuwa mzizi.

 

Viambishi

Viambishi ni mofimu zinazoambatishwa kwenye mzizi wa neno ili kuwakilisha hali au dhana mbalimbali zinazofungamana na neno pamoja na mofimu hizo.

Viambishi vya lugha ya Kiswahili huweza kupachikwa mwanzoni au mwishoni mwa mzizi tu.

Upachikaji wa kiambishi kwenye mzizi au shina la neno hujulikana kama uambishaji, mfano, k-isu, safi-sh-a, tend-a, imb-ik-a, m-toto

 

Viambishi vinaweza kuainishwa kwa namna mbili tofauti.

-        Vinaweza kuanishwa kwa kuzingatia na nafasi vinamotokea katika neno.

-        Vinaweza kuinishwa kwa kuzingatia uamilifu wao.

 

Uainishaji kwa kuzingatia nafasi vinamotokea

Uainishaji huu unaangalia mahali viambishi hivyo vinapopachikwa katika mzizi wa neno.

 

Uainishaji kutokana na nafasi vinamotokea

Katika lugha ya Kiswahili viambishi vinaweza kupachikwa mwanzoni na mwishoni mwa mzizi wa neno. 

Viambishi vinavyojitokeza mwanzoni vinajulikana kama viambishi awali, mfano, m-zee, ma-chungwa, m-som-i, a-pat-e, nk

Viambishi vinavyojitokeza mwishoni mwa mzizi wa neno vinajulikana kama viambishi tamati, mfano, chek-a, kimbi-a, tembe-a, safi-sh-a.

 

Uainishaji wa Kiuamilifu

Uainishaji huu unazingatia kazi za kisarufi zinazofanywa na viambishi hivyo. Katika Kiswahili viambishi vina maumbo mbalimbali na kila kimoja kina kazi ya kisarufi.

Kazi hizi hutegemea mahali kiambishi kilipo katika umbo la neno na vilevile aina ya neno kinamojitokeza.

Baadhi ya kazi za viambishi ni kama vile upatanishi wa kisarufi, unyambulishi, uwakilishi wa njeo, uwakilishi wa hali na ukanushi.

Viambishi katika nomino

Viambishi katika nomino hufanya kazi ya kuwakilisha ngeli, idadi na upatanishi wa kisarufi.

 

Ngeli na idadi

Viambishi vinavyoonyesha idadi na ngeli katika nomino aghalabu hutokea mwanzoni kabla ya mzizi wa neno. Viambishi vya aina hii vinafanya kazi za aina mbili, ya kwanza ni kuwa vinawakilisha idadi (umoja na wingi) na pili vinawakilisha ngeli za nomino, yaani makundi ya nomino. Mfano ni kama ifuatayo:

m + tu – wa + tu

ki + tu – vi + tu

ji + cho – ma + cho

n+guo – n + guo

m + ti  - mi + ti

 

Upatanishi wa kisarufi

Viambishi vya nomino vinahusiana na vingine vinavyojitokeza katika sehemu za mwanzo katika aina nyingine za maneno katika sentensi.

Viambishi hivyo hufanya kazi ya upatanishi wa kisarufi.

Upatanishi wa kisarufi ni kukubaliana kwa viambishi vya nomino na vile vya kitenzi au kivumishi, mfano,

ki-su ki-moja ki-me-pote-a

wa-toto wa-wili wa-mefik-a

ma-we ma-wili ya-me-baki

 

Viambishi vya unyambulishi

Viambishi nyambulishi katika Kiswahili huambikwa kwenye mizizi ya nomino ili kuunda maneno mapya. Viambishi hivi hufanya kazi pamoja na viambishi vya ngeli na idadi kuunda nomino mbalimbali mfano:

-        kiambishi nyambulishi -e mwishoni mwa umbo la jina huonyeshwa kitendwa, yaani kile ambacho tendo hukifikia, km. tum-a – tum-e, ham-a  ham-e

-        kiambishi nyambulishi -o huonyesha kitumizi au kitendo, matokeo ya tendo au mahali tendo linapotukia, mfano, pig-a pig-o; siki-a siki-o;  zib-a ki-zib-o; som-a ki-som-o

-        kiambishi nyambulishi -ji huonyesha hali ya mazoea au ya kurudiwarudiwa

kwa tendo, mfano sem-a m-sem-a-ji; ku-nywa ki-nywa-ji

-        viambishi nyambulishi -vu na -fu hunyesha umbile au sifa inayostahiki kwa kile kinachohusika na tendo, mfano, oko-a w-oko-vu; chaka-a u-chaka-vu; pungu-a u-pungu-fu

-        kiambishi nyambulishi -a huonyesha maana maalum kuhusika na tendo, mfano, wi-a; m-wi-a; wi-w-a m-wi-w-a

-        kiambishi nyambulishi -i kinaonyesha weledi wa mtu, mfano som-a m-som-i; pik-a mpish-i;

-        kiambishi nyambulishi -zi huonyesha matokeo ya moja kwa moja ya tendo, mfano, poke-a ma-poke-zi; tum-i-a ma-tumi-zi; poke-a ma-poke-zi.

 

Maumbo yenye kiambishi tamati -o yanakuwa na viambishi awali ki-, vi, u na m hubeba dhana ya kitumizi mfano, ki-zib-o, ki-funik-o, u-fung-u-o, m-teg-o.

Maumbo hayo huwa na dhana ya matokeo yanapokuwa yametanguliwa na viambishi awali m-, mi-, ji-, ma-, w-, au n-, mfano, m-sem-o, nen-o, pig-o, ny-imb-o, m-chez-o, w-it-o. Nomino zinazoundwa kutokana na viambishi hivi mara nyingi hutokana na vitenzi, yaani yanatokana na mizizi ya vitenzi.

 

Kiambishi tamati -ni ni kiambishi ambacho si nyambulishi kinachotokea kwenye maumbo ya nomino za Kiswahili. Kiambishi hiki kinaweza kuambikwa kwenye nomino zote isipokuwa nomino mahsusi zinazohusu majina ya watu mfano, Ali, Yakobo, Yusufu; majina ya mahali, mfano, Bagamoyo, Tanzania, Kilwa; wakati, mfano, Jumamosi, Machi. Kiambishi hiki kikiambikwa kwenye nomino hubeba dhana ya mahali au ndani yake, mfano, chumba-ni, mji-ni, kanisa-ni, shule-ni, nk.

 

Viambishi katika vitenzi

Vitenzi katika Kiswahili hubeba viambishi vingi kuliko vipengele vingine vya kisarufi.

 

Viambishi vya unyambulishi katika vitenzi

Unyambulishaji – ni upachikaji wa viambishi kwenye mzizi ili kuunda maneno mapya. Katika Kiswahili kuna viambishi nyambulishi ambavyo hutumika katika uundaji wa vitenzi vipya, mfano,

tembe-a

tembe-le-a

tembe-le-a-n-a

tembe-l-e-wa

tembe-l-e-k-a

 

Katika Kiswahili kuna viambishi tamati nyambulishi vinane ambavyo huambikwa kwenye mizizi ya vitenzi kama vifuatavyo:

1.      -w-

2.      -ik-/-ek-

3.      -ish-/-iz-/-esh-/-ez-

4.      -il-/-el-

5.      -o-/-u-

6.      -am-

7.      -an-

8.      -at-

 

Viambishi vya nafsi

Viambishi vya nafsi huambatana na vitenzi. Viambishi hivi ni pamoja na ni-, u-, a-, tu-, m-, wa-, -ku-, -wa-, -tu-, nk, mfano ni-na-kuja, u-ta-pit-a, ni-me-wa-on-a, nk.

Viambishi vinavyotangulia mwanzoni kabisa mwa neno vinawakilisha nafsi katika nafasi ya kiima (mtenda)

Viambishi vinavyokabiliana na mizizi ya kitenzi ni viambishi vya nafsi katika nafasi ya yambwa (yaani ile inayopokea tendo).

Kiambishi tamati -ni kinapoambikwa mwishoni mwa vitenzi vya Kiswahili hubeba dhana ya idadi hasa nafsi ya pili wingi, mfano, ka-e-ni, kimbi-e-ni, njoo-ni, siki-e-ni.

 

Viambishi vya njeo

Viambishi vya njeo ni viambishi vinavyowakilisha dhana ya wakati. Kuna vinavyowakilisha wakati uliopita, ambavyo ni viambishi, -li-, -me-, mfano ni kama a-li-kuja, a-me-kuja. Kiambishi -li- huwakilisha wakati uliopita (kukubali) na kiambishi -me- wakati uliopita hali timilifu

Kiambishi -na-, mfano ni-na-kuja, a-na-enda kinawakilisha wakati uliopo (kukubali)

Kiambishi -ta- kinawakilisha wakati ujao (kukubali), mfano wa-ta-rudi, ni-ta-lima

Kiambishi -ku- kinawakilisha wakati uliopita (kukanusha), mfano, ha-ku-ja, si-ku-wa-ona.

Kiambishi -ja- kinawakilisha wakati uliopita hali timilifu (kukanusha), mfano, ha-ja-rudi, si-ja-fika, ha-tu-ja-mw-ona

Kiambishi awali hu- kinawakilisha hali ya mazoea (kukubali), mfano hu-enda, hu-tembea, hu-la, nk.

 

Viambishi vya hali

Viambishi vya hali ni vile vinavyoonyesha dhamira ya maelezo. Viambishi mbalimbali vinawakilisha dhana mbalimbali kama ifuatavyo:

Kiambishi -a ni kiambishi cha dhamira dhahiri, mfano kat-a, som-a, pak-a.

Kiambishi -e ni kiambishi cha dhamira ya matilaba, yaani kuonyesha nia ya kutenda jambo, mfano a-sem-e, a-kimbi-e, a-tembe-e.

Kiambishi -po- ni kiambishi (cha sharti) cha kuonyesha mahala au muda, mfano, ali-po-kuja, ali-po-fika.

Kiambishi -ki- ni kiambishi cha sharti, mfano a-ki-rudi, wa-ki-fika, tu-ki-ja

Kiambishi -ki- ni kiambishi cha tendo kuendelea, mfano alikuwa a-ki-tembea, tulikuwa tu-ki-imba

Kiambishi -li- ni kiambishi cha hali ya kuwa na, mfano a-li-ye na jembe.

Viambishi -nge-/-ngali-/-ngeli- ni viambishi vya kudadisi tendo, mfano, wa-nge-kuona, tu-nge-tembea

 

 

Viambishi virejeshi

Viambishi virejeshi ni viambishi vinavyowakilisha kitajwa katika umbo la vitenzi. Viambishi hivi mara nyingi huungana na na kiambishi -li- kuunda aina nyingine ya viambishi amilifu katika Kiswahili, mifano ni kama vile:

wa+o mfano, wa-li-o-kimbia

u+o mfano, u-li-o-dondoka

li+o mfano, li-li-lo-pasuka

ch+o mfano, ki-li-cho-katika

i+o mfano, i-li-yo-anguka

vy+o mfano, vi-li-vyo-letwa

zi+o mfano, zi-na-zo-tofautiana

Viambishi virejeshi vinapojitokeza katika maumbo ya vitenzi huwa vinarejelea kitajwa, yaani nomino inayohusika na tendo.

 

 

Uundaji wa maneno

Kila lugha ina kanuni zake za uundaji wa maneno. Katika lugha ya Kiswahili taratibu za aina mbili hutumika katika uundaji wa maneno. Taratibu hizi zinajulikana kama uambishaji na unyambulishaji.

 

Uambishaji

 

Uambishaji ni utaratibu wa kuweka kiambishi kabla, katikati au baada ya mzizi wa neno.

Katika Kiswahili viambishi huweza kujitokeza mwanzoni na mwishoni tu mwa mzizi, mfano:

m-toto; m-ti; pig-a; fuat-a; pat-a, simam-ia

Mifano hiyo inaonyesha kuwa viambishi vya Kiswahili vinaweza kutokea mwanzoni au mwishoni mwa mzizi.

Inawezekana kuwepo mpangilio wa viambishi viliwili kutokea kabla ya mzizi, mfano, a-na-som-a, tu-ta-temb-ea.

Hivyo, uambishaji ni utaratibu wa kuweka pamoja viambishi na mizizi katika maumbo mbalimbali ya neno. Hivyo, uambishaji katika lugha ni uwekaji pamoja wa viambishi na mzizi kwa namna mbalimbali bila kujali aina ya maumbo yanayopatikana. 

 

Unyambulishaji

Unyambulishaji ni utaratibu wa kuweka pamoja viambishi na mizizi au mashina ili kuunda maneno. Utaratibu huu unaruhusu viambishi nyambulishi (undaji) kuwekwa pamoja na mizizi au mashina ya maneno. Mifano ni kama vile maneno, umb-a umb-o; pig-a pig-o; safi saf-isha; fupi fupi-sha; pika-mpishi-mpikaji, mapishi.

Matokeo ya unyambulishaji ni kupatikana kwa maneno mengine. Katika mifano hiyo inaonekana kuwa umbo lenye viambishi huweza kiuwa na kambishi kimoja au zaidi. Mizizi inayobeba viambishi nyambulishi mara nyingi huwa ni mizizi funge.

 

 

Muundo wa nomino

Nomino ni nini?

Neno linalotaja kitu, kiumbe, hali, dhana au tendo lolote.

Lugha mbalimbali huainisha nomino kwa njia tofauti. Kiswahili huziainisha na kuzipanga nomino katika makundi mbalimbali yanayojulikana kama ngeli.

Ngeli ni nini?

Utaratibu wa taaluma ya sarufi ya lugha katika kupanga aina za nomino katika makundi. Utaratibu huu husaidia kuzigawa nomino katika makundi mbalimbali kwa kuzingatia uwiano uliopo baina ya nomino hizo na vipengele vingine vya kisarufi katika lugha.

Ngeli hutambuliwa kwa kuangalia viambishi vya mwanzo vya nomino na upatanishi wake wa kisarufi. Uainishaji wa nomino kwa kuzingatia viambishi awali hujulikana kama uainishaji wa kimofolojia.

Mfano msomi kiambishi awali ni m- na mzizi som- na kiambishi tamati -i ambacho hutumika kuundia nomino kutokana na kitenzi.

Kiambishi awali kinajulikana kama kiambishi ngeli

Ngeli za Kiswahili zimeainishwa katika makundi mbalimbali kwa kuangalia hali ya umoja na wingi wa nomino hizo.

Kila kiambishi ngeli kimepewa namba ya kukitambulisha. Kwa kutumia kigezo cha kimofolojia, nomino za Kiswahili zimegawanyika katika ngeli kumi na nane kama ifuatavyo:

 

Ngeli 1 mu-

Ngeli hii huchukua nomino zenye kiambishi ngeli mu-, pamoja na mw-, m- mfano muuguzi, mwalimu, mtoto. Kiambishi hiki hupata tofauti zinazosababishwa na mabadiliko ya kifonolojia. Mabadiliko hayo hutegemea muundo wa shina la nomino husika. Hii huweza kuathiri /u/ iliyo katika kiambishi ngeli mu- inapokuwa imekaribiana na fonimu ya kwanza ya shina.

U hugeuka kuwa w inapokaribiana na vokali isiyo u. Hali hii husababisha mofimu ngeli  mu- kuwa na alomofu tatu ambazo ni mu-, mw- na m-.

 

Ngeli 2 wa-

Hii huwalikisha wingi wa ngeli ya kwanza. wa- ni kiambishi ngeli cha ngeli hii, mfano wa-toto, wauguzi, nk. Kiambishi ngeli cha ngeli hii ya pili pia hupata mabadiliko ya kifonolojia ambapo wa- huwa na alomofu w-, mfano wa-limu.

 

Ngeli 3 mu-

Nomino katika ngeli hii huchukua kiambishi mu-, mfano muundo. Hata hivyo mofimu hii huwa na alomofu mu-, mw- m-. mu- huwa mw- iwapo mzizi wa neno utaanza na vokali isiyo u, mfano mw-embe.

mu- huwa m- iwapo mzizi wa neno utaanza na konsonanti, mfano m-ti.

 

Ngeli 4 mi-

Ngeli hii ni ya wingi wa nomino za ngeli ya tatu mofu ngeli yake ni mi-, mfano mi-ti, mi-embe. Mofu hii huwa haina alomofu.

 

Ngeli 5 ji-/ø

Nomino katika ngeli hii huchukua kiambishi ji-, mfano ji-we, ji-tu, nk. Hata hivyo kuna nomino nyingine ambazo huingizwa katika kundi hili la ngeli kwa kuzingatia upatanisho wao wa kisarufi ingawa hazina kiambishi ngeli ji-. Mfano goti.

 

Ngeli 6 ma-

Ngeli hii huwakilisha wingi wa ngeli ya tano. Mofu ngeli ya ngeli hii ni ma-, mfano ma-cho, ma-goti, ma-we.

 

Ngeli 7 ki-

Nomino katika ngeli hii huchukua kiambishi awali ki-. Mfano ki-tu, ki-atu, kikombe.

 

 

Ngeli 8 vi-

Nomino za ngeli hii huchukua kiambishi ngeli vi-. Hii huwakilisha wingi wa ngeli ya saba. Mfano vi-ti, vi-atu.

 

Ngeli 9 n/ø

Hakuna kiambishi ngeli maalum kinachowakilisha ngeli hii. Nomino za ngeli hii huendelezwa sawa katika umoja na wingi wake katika ngeli ya kumi. Mfano nyumba, kalamu, nyama, meza.

 

Ngeli 10 n/ø

 Ngeli hii huwakilisha wingi wa ngeli ya tisa. Kiambishi ngeli cha ngeli hii ni sawa na kile cha ngeli ya tisa. Tofauti kati ya ngeli ya tisa na kumi hudhihirika katika upatanisho wa kisarufi. Mfano nyumba inaungua – nyumba zinaungua.

 

Ngeli 11 u-

Nomino zinazoingia katika ngeli hii huwa na kiambishi ngeli u-, mfano u-limi, u-bao, u-jia.

 

Ngeli 12 ka-

Nomino za ngeli hii huwa na kiambishi ngeli ka-. Mfano ka-toto, ka-gari.

 

Ngeli 13 tu-

Ngeli hii inawakilisha wingi wa ngeli ya 12. Kiambishi cha ngeli hii ni tu-. Mfano tu-toto, tu-gari.

 

Ngeli 14 u-

Nomino za ngeli hii huchukua kiambishi ngeli u-, mfano u-tukufu, u-gonjwa, u-chungu, u-zuri.

 

Ngeli 15 ku-

Nomino za ngeli hii huchukua kiambishi ngeli ku-. Nomino za ngeli hii huundwa kutokana na vitenzi. Hizi ni nomino zinazoelezea vitendo. Mfano ku-piga, ku-tembea.

 

Ngeli 16 pa-

Nomino za ngeli hii hurejelea hali mbalimbali za mahali. Kiambishi ngeli ni pa-. Ngeli hii huonyesha mahali mahsusi. Mfano pa-le, ha-pa.

 

Ngeli 17 ku-

Nomino za ngeli hii huonyesha mahali kwa jumla. Mfano ku-le, hu-ku.

 

Ngeli 18 mu

Nomino za ngeli hii huonyesha undani wa mahali. Mfano hu-mu.

 

 

Kanuni za uundaji wa maneno

Maneno ambayo uundaji wake kwa kiasi kikubwa hutegemea miunganiko ya viambishi na mizizi ni nomino na vitenzi.

Unyambulishaji unaofanyika kwa kupachika viambishi kabla ya mzizi unahusu zaidi nomino.

Unyambulishaji unaofanyika kwa kupachika viambishi baada ya mzizi unahusu vitenzi.

 

Kanuni za uundaji wa nomino

Nomino za Kiswahili zina viambishi mbalimbali mfano:

m-/wa-

m-/mi-

ji-/ma-

ki-/vi-

Uundaji wa nomino kutokana na mizizi ya aina nyingine za maneno unajulikana kama unominishaji.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 


No comments:

Post a Comment