Dhana
ya kategoria imejadiliwa kwa namna tofauti tofauti. Khamisi na Kiango (2002) wamegawa kategoria katika mitazamo miwili; Wanamapokeo na
Wanausasa, ambapo Wanamapokeo walitumia dhana ya kategoria kumaanisha sifa
bainifu ya vitu na wanausasa wanaona kategoria kuwa ni “zile aina za maneno
kama vile nomino, vivumishi, vielezi, viunganishi, vihusishi na vitenzi”
Massamba,
(2009) anatoa maana ya kategoria kwa kusema kuwa “Ni jumla ya maumbo, faridi au
vipashio vingine ambavyo huchangia sifa fulani au ambavyo viko katika kiwango
kimoja. Maana hii ni ya jumla kwani imeeleza dhana ya kategoria kwa ujumla bila
kujikita katika kategoria miundo ambayo ndiyo sintaksia.
Massamba
(khj)[1]
anasema kuwa kategoria miundo ni“kategoria za mpangilio wa maneno ambazo ni
muhimu katika tungo kama vile kirai nomino(KN), kirai kitenzi(KT), kirai
kivumishi(KV) na kirai kielezi (KE).”
Fromkin
na Rodman (1993) wanataja aina mbili za kategoria; phrasal categories and lexical categories (kategoria za virai na
kategoria za kileksika-tafsiri ni yetu). Hivyo basi kulingana na nukuu hii
kategoria za kisintaksia zinaweza kutazamwa katika viwango viwili; kategoria za
kileksika na virai. Katika kazi hii aina zote mbili za kategoria za kisintaksia
zitajadiliwa.
Kwa
kuanza na kategoria ya kileksika, Kuna vigezo vya kiisimu ambavyo hutumiwa
katika kuainisha aina za maneno. Besha, (2007) anasema kuwa “kumekuwa na
mijadala mikali juu ya vigezo vinavyotumika kuainisha maneno ya lugha” hii
inaonyesha kwamba hata vigezo ambavyo vipo sio vya kuaminika sana. Vigezo hivyo
ni kama vile kigezo cha kifonolojia, kimofolojiakisintaksia na kisemantiki.
Kutokana
na vigezo hivyo wataalamu mbalimbali wametofautiana katika idadi yake. Kwa
mfano: “ Kapinga (1983), Nkwera (1978), Mohamed (1986), na Massamba na wenzake
(1999) wameainisha aina saba ilhali Msokile (1992), Mgullu, R (1999), Mbaabu
(2000), Rubanza (2003), Habwe na Karanje (2004) na Mdee na wenzake (2011)
wameainisha aina nane za maneno katika lugha ya Kiswahili”(Matinde 2012:124).
Katika
kazi hii aina za maneno ambazo zimejadiliwa ni: Nomino, Viwakilishi, Vitenzi,
Vivumishi, Vielezi, viunganishi, vihusishi na viingizi.
Nomino
(N) hii ni aina ya neno ambayo hutaja mtu,kitu, hali na dhana. Khamisi na
Kiango(khj.28) wanasema kuwa “seti ya nomino iko wazi kwa kuwa milango yake iko
wazi kupokea nomino mpya kadri zinavyojitokeza”. Matinde, (khj.125) anathibitisha kuwa
“kisintakisia nomino ni kategoria ya kileksika” nomino ziko za aina nyingi.
Mfano wa nomino ni kama vile Tanzania,
Juma, wadudu, kuimba na upendo.
Vivumishi
(V), ni neno linalotokana na kitenzi ‘vuma’ kumaanisha kutoa sauti, kujulikana
au kufahamika (Ndalu, A.E na wenzake 2014:760). Hivyo basi kivumishi ni neno
linalotoa taarifa zaidi kuhusu nomino. Mifano ya vivumishi ni _refu, mamia, _angu na yupi.
Viwakilishi
(W), Ndalu, A.E na wenzake (khj) wanasema kuwa maneno yote ambayo yanasimama
badala ya nomino yanajulikana kama kiwakilishi, yaani yanawakilisha nomino fulani.
Mfano wa maneno yanayosimama kama viwakilishi ni kama vile mimi, yule, wangapi, chake, kizuri, wengi na maelfu.
Vielezi
(E), hii ni aina nyingine ya maneno ambayo huelezea zaidi kuhusu kitenzi.
Katika lugha ya Kiswahili vitenzi hutokea katika sehemu ya kiarifu baada ya
kitenzi. Kitenzi hujaribu kujibu maswali kama vile tendo lilifanyika wapi?
Kivipi?Lini? Na mara ngapi.? Mifano yake ni kama vile; alfajiri, sanasana, harakaharaka, jana, nyumbani, mara kwa mara na polepole.
Vitenzi
(T), hii ni aina nyingine ya maneno ambayo kazi yake ni kutoa taarifa ya
tendeka kwa nyakati zote. Hii inamaanisha kwamba hutoa taarifa ya tendo
linavyotendeka, lilivyotendeka na litakavyotendeka. Kwa mfano: kulima, kula, kulala, kusoma, kuimba, ni,
aliyekuwa, alikuwa na si
Viunganishi
(U), hii ni aina ya maneno ambayo yanaunganisha neno moja na lingine, kirai
kimoja na kingine na sentensi moja na nyingine. Mara nyingi vimeundwa kwa mfumo
ufuatao:-Viongezi, hivi ni viunganishi ambavyo huonekana kuongeza idadi na
hutumika kuunganisha nomino, virai na sentensi. Kwa mfano: Maduhu anakula na kuongea.Viunganishi visababishi,hivi hudokeza
usababisho wa hali fulani kwa mfano alifaulu
kwa sababu alisoma sana.
Viingizi,
ni aina ya maneno ambayo uamilifu wake huonyesha hisia za watu. Baadhi ya
watalaamu wameviita vihisishi. Mfano Matinde (khj) yeye anatumia istilahi
‘vihisishi’. Viingizi hutofautiana kutegemea hisia za wazungumzaji na viko vya
aina nyingi kutegemea na muktadha. Kuna vile vya mwitiko kwa mfano naam! Abee! Labeka! Vipo vinavyohusu
shukrani kwa mfano alhamdulilah!Ahsante!,
Kuna vingine vinahusu furaha kwa mfano oyeee!
Haleluya!
Vihusishi
(H), ni aina ya maneno ambayo huonyesha uhusiano baina ya matukio au matendo
fulani ambapo tendo moja hukamilika baada ya lingine kutokea. Mifano yake ni
kama vile; ‘walikimbia kwa amri ya
jeshi.’
Kategoria ya virai,dhana
ya virai imefasiriwa na wataalamu mbalimbali kwa namna tofauti tofauti. Baadhi
ya wataalamu hutumia neno kikundi badala ya kirai. Mfano wataalamu kama
Mohamed, M.A (1986:62), Mkude, D.J (2010:228-229) na Besha, R.M (2007:84)
wametumia ‘kikundi’ badala ya ‘kirai’.
Hata hivyo kuna wataalam kama vile Massamba na wenzake (1999:84-118),
Khamisi, A.M na Kiango, J.G (2002) na Matinde, R.S (2012:169) wametumia neno
‘kirai’ badala ya ‘kikundi’. Katika kazi hii neno ‘kirai’ litatumika kwa sababu
kirai kinaweza kuwa neno moja au zaidi ilhali kikundi kinamaanisha neno zaidi
ya moja.
Maana
ya kirai imejadiliwa na wataalam mbalimbali, hata hivyo katika kazi hii maana
ya Massamba na wenzake (khj)wanasema kuwa “kirai ni kipashio cha kimuundo
chenye zaidi ya neno moja lakini ambacho hakina muundo wa kiimakiarifu”. Udhaifu
wa tafsiri hii ni kwamba si lazima kirai kiwe zaidi ya neno moja bali kinaweza
kuwa hata neno moja na kuendelea.
Kirai
kimeundwa na sehemu kuu mbili: neno kuu ambalo ndilo linalotawala kirai chote,
mfano ‘babu analima’ neno kuu ni
‘babu’ kwani ndilo linalotawala kirai na kijalizo ambayo ni maneno yanayojaliza
neno kuu, kwa mfano ‘babu analima’
neno ‘analima’ ndilo kijalizo cha neno kuu.
Massamba
na wenzake (khj) wanasema kuwa katika lugha ya Kiswahili kuna aina tano ya virai
ambavyo ni virai-nomino, virai-vitenzi, virai- vivumishi, vira-vielezi na virai
viunganishi. Hata hivyo Matinde, R.S (2012:169) ametabanaisha aina sita ya
virai, ambapo kutoka kwa Massamba na wenzake ameongeza kirai kihusishi. Katika
taaluma hii aina sita ya virai itajadiliwa:-
kirai-nomino,
ni kirai ambacho ama kwa hakika muundo wake uko katika nomino. Hujengwa kwa
nomino moja au zaidi au viwakilishi vya nomino, hudokeza taarifa inayohusu
nomino au kiwakilishi cha nomino. Kirai nomino kina miundo tofauti tofauti:Nomino
pekee kwa mfano;Mushi amekuja. Nomino
mbili au zaidi zinazounganishwa na kiunganishi. Kwa mfano babanamama wanaishi.Nomino
na kivumishi kimoja. Kwa mfano lori kubwa limeharibika.Kivumishi na nomino, kwa mfano;Yule jamaa aliumia. Pia kuna miundo mingine mingi
ambayo ama kwa hakika si rahisi kuiweka yote katika kazi hii.
Kirai
kivumishi, hiki ni kirai ambacho kimekitwa kwenye kivumishi, yaani neno kuu
katika kirai hiki ni kivumishi. Muundo wake huwa ni wa kivumishi pekee yake au
kivumishi na maneno mengine yanayoandamana nacho. mifano ya virai vivumishi ni
kama vile: ile chai ni tamu sana, lile duka ni kubwa sana na Yule tajiri ni mkali vibaya!
Kirai
kitenzi, hiki ni kirai ambacho huundwa kwa kitenzi na maneno mengine
yanayohusiana na kitenzi chenyewe. Kirai kitenzi chaweza kuundwa na kitenzi
kimoja kwa mfano; tumefika, kitenzi,
nomino na kitenzi, kwa mfano; tunaomba
wakuu kuwajibika, kitenzi na kielezi, kwa mfano; moto umewaka sana.
Kirai-kielezi,
ni kirai ambacho muundo wake haukitwi kwenye neno kuu, yaani kielezi bali
hukitwa kwenye baadhi ya maneno yanayofanya kazi pamoja na kielezi husika. Mara
nyingi huchukuliwa kwamba kina miundo ya aina nyingi ambapo sasa si rahisi kuwa
na kiini kimoja cha umiliki wa vipashio. Hivyo hakutakuwepo na miundo ya
virai-vivumishi ila mifano yake ni kama ifuatavyo; leo asubuhi Sofia ataimba, Mzee hukoroma mara kwa mara.
Kirai-kiunganishi,
hiki ni kirai ambacho muundo wake umekitwa kwenye uhusiano baina ya jina na
kiunganishi. Neno kuu lake ni kiunganishi. Uhusiano wa kiunganishi na jina
hudokezwa na matumizi ya: kwa,na, katikana
kwenye. Katika lugha ya Kiswahili
virai viunganishi huwa na muundo wa kiunganishi na kikundi jina. Kwa mfano:
ilibidi aondoke kwa amri ya jeshi, walikula chakula katika hoteli ile, aliingia kwenye
krabu, na alikamatwa na meno ya tembo.
Kirai-kihusishi,
hiki ni kirai ambacho hudokeza uhusiano kati ya vitu vitu viwili au zaidi.
Virai hivi hujikita zaidi katika vihusishi vya ‘a-unganifu. Hutumika pamoja na
nomino ya mahali, nomino ya wakati au nomino dhahania. Kwa mfano: chukua simu juu ya meza, panya waliingia ndani
ya shimo, hutaruhusiwa kuzungumza wakati
wa kula
Kuna
faida nyingi za kuwa na kategoria katika lugha; yaani kategoria za kisintaksia
ambazo zimejadiliwa hapo juu kuwa ziko katika makundi mawili; kategoria za
kileksika na virai. Mojawapo ya faida za kuwa na kategoria hizo ni pamoja na:-
Inasaida
kupata sarufi inayojitoshereza kwa usahihi katika lugha. Lengo la uchambuzi wa
kisitaksia ni kutafuta ukubalifu na usokubalifu wa tungo zisizo sahihi. Katika
kujaribu kuchambua miundo ya lugha kwa kutumia mmilisi wa lugha fulani,
mwanasarufi hujikuta ameshapata maarifa na kubaini ni miundo ipi iliyo sahihi
na isiyo sahihi.
Vile
vile inasaidia kuunda nadharia mbalimbali za kisintaksia. Kutokana na uchambuzi
wa kategoria za kisintaksia kumepatikana nadharia kama vile sarufi miundo
virai, sarufi geuza maumbo zalishi.
Inasaidia
pia kujua aina za maneno. Mwanagenzi anapofanya uchambuzi wa kisintaksia
inamsaidia kujua aina mbalimbali za maneno katika lugha husika. Kwa mfano
nomino, Vitenzi, Vivumishi, vielezi, viunganishi na vihusishi ambayo pia
anaweza kutumia katika taaluma nyingine za isimu.
Ukiachilia
kujua aina za maneno faida nyingine ni kujua aina mbalimbali ya virai kwa mfano
kirai nomino, kirai kitenzi, kirai kihusishi na kirai kiunganishi.
Kwa
ujumla kategoria za kileksika na kategoria za virai zinahitaji kufanyiwa
uchunguzi wa ndani zaidi na kuweza kubainisha vigezo vinavyotumika katika
kuainisha. Hii inatokana na kwamba kuna baadhi ya maneno ambayo yanakuwa hayana
maalum pa kuyaweka mpaka hapo tu utakapoyakuta katika tungo. Kwa mfano maneno
yenye maana zaidi ya moja mfano ua linaweza kuwa kitenzi na linaweza pia kuwa
nomino, hivyo inakuwa vigumu kwamba liwekwe katika kundi gani hasa
linalositahili.
Marejeleo
Besha, R.M.(2007). Utangulizi wa Lugha na Isimu: Dar es
salaam. Macmillan Aidan
Fromkin,V na Rodman, R
(1993).An Introduction to Language:
Florida. HBJC publisher
Khamisi, A.M na Kiango,
J.G (2002). Uchanganuzi wa Sarufi ya
Kiswahili. Dar es salam: Chuo Kikuu Huria cha Tanzania.
Massamba, D.P.B.
(2009). Kamusi ya Isimu na Falsafa ya
Lugha. Dar es salaam: TUKI
Massamba, D.P.B. na
wenzake (1999). Sarufi Miundo ya
Kiswahili Sanifu (SAMIKISA): Dar es salaam: TUKI
Matinde, R.S (2012). Dafina ya Lugha: Isimu na Nadharia:
Mwanza: Serengeti Educational publishers.
Mkude, D.J. (2010).
Makala za Semina ya Kimataifa ya Waandishi wa Kiswahili: Uchambuzi wa Sentensi za Kiswahili.Dar es salaam: TUKI
Mohamed, M.A (1986). Sarufi Mpya: Dar es salaam: Press and
publicity center.