Monday

maudhui ya kazi za kifasihi husawiri jamii halisi

0 comments

 

FASIHI HUCHOTA MAUDHUI YAKE KUTOKA KATIKA HALI HALISI ZA JAMII. JADILI KAULI HII KWA KUREJELEA HADITHI TEULE.

Maudhui katika kazi ya fasihi ni jumla ya mawazo yote yanayozungumzwa pamoja na mtazamo wa mwandishi juu ya mawazo hayo. Maudhui hujumuisha mawazo pamoja na mafunzo mbalimbali yaliyomsukuma msanii hadi akatunga na kusanii kazi fulani ya kifasihi. Vipengele vya maudhui ni pamoja na dhamira, migogoro, falsafa ujumbe na msimamo.

 

Mwandishi wa kazi ya fasihi huwa na jukumu kubwa la kuichuja, kuiongoza, kuielekeza au kuikashifu jamii bila kusahau kuisifu mahali pafaavyo. Ikumbukwe kuwa mwandishi yuyu huyu wa kazi ya fasihi huwa kioo cha jamii kiasi kwamba kupitia kwake tunaweza kufahamu hali halisi inayoikumba jamii husika. Hii ni kwa sababu yale yote ambayo mwandishi huyaandika, msingi wake huwa ni jamii ambapo yupo au ameshuhudia swala husika likitendeka.

Maudhui haya huwa ni picha halisi ya matukio au matendo katika jamii inayomhusu mwandishi hivyo basi huitumia kazi yake kama kielelezo au kipiga-debe huhusu hali husika. Katika kazi hii tutazama katika tamthilia ya Mstahiki Meya iliyoandikwa na Timothy Eregi. Yafuatayo ni maudhui ambayo yamebainika wazi katika tamthilia ya Mstahiki Meya na ambayo yanadhihirika wazi kati jamii zetu ni yafuatayo:

(i)                 Uongozi mbaya

(ii)               Umaskini

(iii)              Ukoloni mamboleo

(iv)              Ufisadi

(v)               Ufeministi/Nafasi ya mwanamke.

 

v  Uongozi mbaya.

Uongozi mbaya ni hali ambapo aghalabu kiongozi anatumia mamlaka yake visivyo kwa kujinufaisha na kunufaisha vibaraka wake badala ya kuwatumikia raia wan chi au eneo husika kwa kuendeleza sera potovu na hata kutozingatia sheria za nchi. Viongozi wanaotekeleza sera za kiutawala zinazokandamiza au kurudisha nyuma maendeleo ya watawaliwa huwa ni viongozi wabaya. Maudhui mengi katika tamthilia hii yamejitokeza kutokana na maudhui makuu ya uongozi mbaya. Maudhui ya uongozi mbaya yamejitokeza katika tamthilia hii ya Mstahiki Meya pakubwa.

·         Uongozi wa Baraza la Cheneo unaoongozwa na Meya Sosi ni mbaya kwa kuwa unapalilia ufisadi. Meya Sosi anatumia mamlaka yake kunyakua ardhi ya umma, kuwaongeza mshahara wafuasi wake kiholela. Kuwapa marupurupu na kuwaajiri watu kazi bila kuzingatia ufaafu wao bali kwa kuzingatia mapendeleo ya kifisadi.

·          Usugu wa viongozi wa Cheneo hasa Meya Sosi kuvunja sheria bila kuhofia adhabu yoyote ni dhihirisho la uongozi mbaya. Licha ya kuwa Meya Sosi amefilisi barasa la Cheneo, anamzungumzia Daktari Siki kwa ujeuri na kusuma kuwa raia wangemchagua hata mara nne akitaka kwa kuwa tayari walikuwa wamemchagua mara mbili.

·         Uongozi mbaya pia unaonekana katika baraza la Cheneo pale tunaona ule ukatili na unyama unaotendewa raia hao. Wanayimwa haki yao ya kugoma wakipigania nyongeza ya mishahara na kutuma polisi wawatawanye na hata kuwaua.

·         Utawala wa Cheneo chini ya Meya unavunja kanuni za Baraza hasa pale anapokataa kuzizingatia na badala yake kusikiza Bili na ushauri wake kuhusu utoaji wa kandarasi za Baraza. - Ukosefu wa sera mwafaka na utaratibu wa kutatua matatizo

·         ukosefu wa dawa ni dhihirisho kuwa hakuna mikakati madhubuti ya kuhakikisha hali kama hizi zinashughulikiwa. - Mishahara ya wafanyakazi wa Baraza kucheleweshwa na vilevile kulipwa nusunusu (uk. 23).

·         Licha ya kuwa baadhi ya madiwani wanasema uchumi wan chi umeimarika lakini haumnufaishi mwananchi wa kawaida (uk. 23).

Uongozi wa mabavu au wa ki imla (Autocratic Leadership) unaweza kuwa mfano mzuri wa uongozi mbaya. Uongozi wa aina hii kiongozi hujiona kwamba ni yeye tu ndiye ajuaye kila kitu. Hasikilizi wala haombi mawazo au mawaidha kutoka kwa walio chini yake. Maamuzi yote huyafanya yeye. Yeye ni mtu wa kutoa amri na maelekezo tu. Hajali mawazo na fikira za mwenzake.Inaaminika kuwa huenda mwandishi wa tamthilia hii kwa njia moja au nyingine ameaathiriwa na utawala wa aina huu ambao unampamsukumo wa kutaka kupiga vita uozo huu wa uongozi katika jamii zetu.

Swala uongozi mbaya limeyakumba mataifa mbalimbali ulimwenguni. Uongozi hu mbaya umekuwa chanzo cha matukio yanayodamamiza maendeleo katika mataifa husika. Bara la Afrika limekumbwa pakubwa na swala hili la uongozi mbaya. Kiongozi wa upinzani nchini Kenya Mh.Raila Odinga. Akiongea na Sauti ya Amerika (Mei 26, 2009) muda mfupi kabla ya kutoa hotuba yake katika chuo kikuu cha Buffalo, New York, Odinga alisema kuwa mfumo mbaya wa uongozi umewanyima Waafrika haki ya kupanga namna ya kujiletea maendeleo yao wenyewe.

Mh.Odinga alisema kuwa Afrika inahitaji mabadiliko yatakayosaidia kupunguza mamlaka kupita kiasi yaliyowekwa katika taasisi za urais. Alisema hili litasaidia kuondokana na mifumo ya kidikteta, na kuingia mfumo wa uongozi wa kidemokrasia utakao wapatia mamlaka wananchi.Isitoshe ,viongozi wa nchi za Afrika wakiwa kwenye makongamano yao mbalimbali ya uongozi  wanakiri kwa vinywa wazi kuwa , uongozi mbaya wa watawala wa bara hili ndio unaoitishwa Afrika mgogoro wa wakimbizi.Haya yalitokea wazi wakiwa mjini Kampala, Uganda na kuongeza kuwa, utawala mbaya, uongozi usiofaa na dhaifu ndiyo sababu kuu ya kuvamiwa nchi hizo na wimbi kubwa la wakimbizi kutoka maeneo mengine.

Rais Yoweri Museveni wa Uganda alisikika akinadi hivyo  kwenye "kikao cha mshikamano" na kuongeza kuwa, taasubu za kikabila na kukosekana wapinzani wa kuaminika ni katika mambo yanayozusha mapigano ya umwagaji wa damu katika baadhi ya nchi za Kiafrika ambayo yanawalazimisha wakazi wa nchi hizo kuyakimbia makazi yao. Ukitoa Uturuki na Pakistan, Uganda ni nchi ya tatu yenye wakimbizi wengine duniani na ni ya kwanza barani Afrika. Hivi sasa kuna wakimbizi karibu milioni moja wa Sudan Kusini pekee nchini Uganda.

Uongozi mbaya huathiri uchumi swala ambalo linajitokeza katika mataifa mengi ya bara la Afrika. Mengi ya mataifa ya bara hili yamedidimia kiuchumi kwa kutokuwa na uongozi ufaao. Mfano mzuri ni kuporomoka kwa uchumi wa Uganda wakati wa utawala mbaya wa Iddi Amin Dada. Uongozi wake duni ulipelekea shilingi ya taifa la Uganda kukosa thamani ambapo kufufuka kwayo ni muhali sana.  Waaidha uongozi mbaya katika jamii zetu huwa kizuizi kikubwa sana kwa utangamano kiasi kwamba kundi moja hujiona kuwa bora zaidi kwa kufyonza mirija ya uchumi na mali huku kundi jingine likijiona kuwa bure kabisa. Hili pia huwa kikwazo na uwiano katika jamii teule huwa mtihani mgumu sana.

Waaidha uongozi kama huu huwagandamiza waandishi wengi hasa mashuhuri ambao kwa njia moja au nyingine huonekana kuipa hali halisi jamii ya uongozi uliopo ambao huwa kikwazo kikubwa kwa maendeleo ya taifa. Wengi wa waandishi hawa hukimbilia uhamishoni hadi hali inayowakubali inapofika katika mataifa yao ndipo wanaporudi. Mfano wa wale walioathirika ni pamoja na Ngugi wa Thiong’o(nyakati za utawala wa rais mustaafu Moi) wa hapa Kenya ,Wole Soyinka wa kutoka taifa la Naijeria na Nawal El Saadawi wa taifa la Misri ambaye alisumbuliwa na kunyanyaswa mno  na serikali dhalimu aliposimama kidete kumtetea mtoto wa kike.


Kama hali ilivyo sasa, umefika wakati ambapo viongozi wa sasa wa mataifa ya barani Afrika kuheshimu dhamana walizopewa kwa kuhakikisha wanazingatia misingi ya uongozi bora wenye manufaa kwa wananchi waliowapatia ridhaa ya kuongoza.
Viongozi wetu watambue kwamba uongozi wa kibabe, kidikteta na kidhalimu hautaishia kuwakosesha tu matakwa yao ya kibinafsi , bali utawaweka katika hatari ya kuadhibiwa na nguvu ya umma, lakini pia wataonekana wakosefu hata mbele za Mwenyezi Mungu.

 

Bara la Afrika limejaaliwa na Mwenyezi Mungu utajiri wa rasilimali lukuki, zinazopaswa kutumiwa vizuri na viongozi wetu ziweze kutuendeleza sote katika nyanya mbalimbali zikiwamo za kielimu, kiuchumi na kijamii kwa jumla kulifanya bara hili kuwa mahali pazuri pa kuishi duniani.



Waafrika wengi tungependa kama si kutamani kuona viongozi wetu wanauenzi utukufu huo wa Mungu, kwa kuonesha uongozi bora unaojali maslahi ya wengi badala ya kujikita katika kujitafutia maslahi binafsi kiasi cha kukosa sifa za utu na kukaa kama vitu tu vyenye kutu.

v  Ufisadi

Ufisadi ni kule kujipatia mali au kuwezesha hali fulani kufaulu/kufanikiwa kwa kutumia njia za mkato na zisizo za kimaadili kama ushawishi wa hela, mapendeleo ya kinasaba/kikabila au hata msukumo wa cheo kwa minajili ya kujinufaisha. Waaidha, ufisadi ni ulaji rushwa au matumizi ya hongo au mlungula. Ufisadi ni maudhui ambayo yamejitokeza kwingi katika tamthilia ya Mstahiki Meya.

Ipo mifano kadha wa kadha kutoka kwenye tamthilia hiyo. Hii ni pamoja na ifuatayo:-

v  Panapotokea shida Meya huunda kamati za utatuzi japo hazina umuhimu kwa Baraza la Cheneo. (uk.22 Diwani III) kamati hizi hutumiwa kudhibiti uongozi dhalimu wa Mstahiki Meya. Wanakamati hawa hulipwa kwa huduma zao.

v  Pendekezo la Diwani I kuwa vijana watunukiwe zawadi na waonyeshwe katika vyombo vya habari kama fursa ya kuonyesha uzalendo wao. (uk.20). Hii ilikuwa mbinu mojawapo ya kuwasahaulisha hali duni ya maisha yao.

v   Nakisi ya milioni mia moja na ishirini katika Baraza la Cheneo na Meya asema watafidia.

v  Madiwani kujiondolea kodi ilhali watu wote hatamuuza ndizi anatozwa kodi (uk.22)

v  Meya anapoelezwa kuhusu nakisi anasema si neno akidai kuwa anajua diwani wana njaa hivyo wasilipwe kodi.

v  Meya kutaka walinzi wa Baraza waongezwe mshahara kulifaa zaidi kama hospitalini, kiwanja cha ndege na wanaozoa taka hawalipwi mshahara, wacha nyongeza.

v  Ushauri wa Bili kwa Meya alipotaka kumpokonya aliyepewa kandarasi unaashiria ufisadi. Anampendekezea Meya asikilizane na aliyepewa kandarasi kuwa waikatize kandarasi yake, halafu mtu huyo amshitaki Meya. Korti ikiamua alipwe kulingana na

mkataba wa kandarasi basi mwenye kandarasi ampe Meya sehemu yake. Asemavyo,

Dawa ya adui ni kummegea unachokula  hakudhuru tena’. (uk.29).

Kwa yakini swala la ufisadi limekuwa donda sugu katika jamii zetu. Kwa kiwango

kikubwa sana. Swala hili  limeathiri pande zote za mataifa ulimwenguni kuanzia mashinani hadi kitaifa.

Kufikia March 15, 2016 Ufisadi nchini Kenya ulikuwa umeongezeka na kufikia asilimia 73.9 mwaka wa 2015  ikilinganishwa na asilimia 67.7 mwaka wa 2012.Kwa mujibu wa ripoti kuhusu rushwa iliyotolewa na EACC, kulingana na ripoti hiyo, wizara ya usalama wa ndani ikifuatiwa na ile ya afya na ardhi ndizo zinazoongoza kwa ufisadi. Utafiti huu uliofanywa kuanzia agosti hadi octoba 2015 inaonyesha kaunti ya Murang’a inaongoza kwa ufisadi ikifuatiwa na embu na Bomet.

Aidha asilimia 58 ya wakenya walitoa hongo ikilinganishwa na asilimia 53 mwaka wa 2015.
Mwenyekiti wa tume hiyo philip kinisu anasema kuwa miongoni mwa huduma za kitaifa ambazo wakenya wamekuwa wakiitishwa hongo ni ile ya matibabu, upeanaji wa vitambulisho na vyeti vya kuzaliwa,vile vile wamesisitiza umuhimu wa kila mkenya kuwajibika ili kukabili ufisadi nchini.Kulingana na EACC kuna kesi takriban 400 zinazoshughuliwa kwa sasa.

Kwa kurejelea hapo ni kuwa ni swala ambalo mwandishi analifahamu na kulishuhudia kwa macho yake hapa nchini Kenya na ulimwengu kwa jumla.Vipovisa mbalimbali hapa Kenya ambavyo vinatokea kiasi kwamba nchi inapoteza pesa nyingi sana. Hizi ni pamoja na kashfa nyinyi ambazo taifa la Kenya limekumbana nazo tangu utawala wa Raisi mstaafu  Moi, akaja Kibaki kisha sasa yupo Rais Uhuru Kenyatta. Kashfa hizi zimefanya Kenya ikapoteza mabilioni ya pesa kwa njia zisizoeleweka kabisa. Kashfa hizi zitabaki ndonda sugu kwa wakenya.

·         Goldenberg

·         Anglo leasing

·         NYS

·         Eurobond 

Mbali na kashfa hizi inaonekana wazi kuwa walio na nguvu za serikali wana nafasi kubwa ya Kuhakikisha kuwa ajira zile nzuri zinawafikia watu wao pekee huku wengine hata kama wanafuzu wakibaki wakiguguna mifupa. Ukitazama katika Mstahiki meya utapata kuwa Bili anajitokeza kuwa mshauri na mshirika mkuu wa Meya ingawa hayupo popote katika utawala wa Baraza la mji wa Cheneo.

Migomo nchini imekuwa jambo la kawaida kana kwamba serikali haina macho. Madaktari , wauguzi , wahadhiri na wengine wengi wamekuwa kucha kutwa wakilalamikia haki yao ambapo kuwalipa mishahara kulingana na mikataba inayowekwa ni ngumu sana. Hii ni kwa sababu serikali inaelekeza hazina iliyopangiwa kwa maslahi ya wachache serikalini.

Bili ni kioo cha wengi ambapo utagundua kuwa wameamua kuwateua watu maalum kuwa washirika wao katika maswala ya uongozi na utawala.Miradi serikalini ina upendeleo wa kutaka kuona kuwa faida ni kwa “vipenzi” wa watawala tu bali wasiotambulika hubakia midomo wazi kabisa kwa kumeza tu mate. Vituko hivi na vingine vingi vilifanya Kenya kuorodheshwa ya tatu fisadi duniani kulingana na gazeti la standard la Tarehe 27/02/2016. 

Ufisadi unaathiri taifa au jamii vibaya sana. Tukutazama wakazi wa Cheneo hawapati huduma ya kufaa kwa kuwa viongozi wanajilimbikizia mali bila kuwajali watawaliwa.

Ufisadi katika serikali umefafanuliwa kuwa matumizi mabaya ya mamlaka ili kujinufaisha kibinafsi. Ufisadi ulianza zamani. Kwa mfano katika Biblia, kuna sheria iliyowakataza watu kula rushwa walipokuwa wakishughulikia kesi, kuonyesha kwamba zoea hilo lilikuwepo zaidi ya miaka 3,500 iliyopita. (Kutoka 23:8) Bila shaka, ufisadi unahusisha mambo mengi, si kula rushwa tu. Nyakati nyingine maofisa wa umma huiba mali, hukubali kupokea huduma ambazo hawastahili, au hata kuiba pesa. Hata wakati mwingine wao hutumia vibaya vyeo vyao kuwanufaisha marafiki na pia watu wao wa ukoo.

Ingawa ufisadi unaweza kutendeka katika shirika lolote lile la kibinadamu, inaonekana kwamba ufisadi katika serikali umeenea zaidi. Ripoti ya mwaka wa 2013 ya Kipimo cha Ulimwenguni Pote cha Ufisadi (Global Corruption Barometer) iliyochapishwa na shirika la Transparency International, ilisema kwamba ulimwenguni pote watu huviona vyama vya kisiasa, polisi, maofisa wa umma, bunge, na mahakama kuwa taasisi zenye ufisadi mwingi zaidi. Acheni tuchunguze ripoti kadhaa zinazozungumzia tatizo hilo.

·         AFRIKA: Mwaka wa 2013, maofisa wapatao 22,000 wa umma nchini Afrika Kusini walishtakiwa mahakamani kwa sababu ya kujihusisha na ufisadi.

 

·         AMERIKA KUSINI: Mwaka wa 2012, nchini Brazili, watu 25 walipatikana na hatia ya kutumia pesa za umma kuwashawishi wapiga kura wawaunge mkono. Miongoni mwa watu hao alikuwa waziri mkuu wa zamani, mtu wa pili mwenye cheo kikubwa nchini humo.

 

 

·         ASIA: Mwaka wa 1995, watu 502 walifia ndani ya duka moja kubwa jijini Seoul, nchini Korea Kusini. Wachunguzi waligundua kwamba wajenzi waliojenga jengo hilo walijenga kwa saruji ya hali ya chini na walipuuza viwango vya usalama. Walifanya hivyo kwa kuwa maofisa wa jiji walikuwa tayari wamehongwa.

 

·         ULAYA: Cecilia Malmström, Kamishna wa Mambo ya Ndani wa Tume ya Ulaya anasema, “Inastaajabisha sana kuona jinsi tatizo hilo [ufisadi] lilivyoenea Ulaya. Viongozi wa kisiasa wameshindwa kulikomesha.”

Si rahisi hata kidogo kwa wanadamu kukomesha ufisadi katika serikali. Profesa Susan Rose-Ackerman, mtaalamu wa kupambana na janga la ufisadi aliandika kwamba ili mabadiliko yapatikane serikali inapaswa izingatie “kufanya mabadiliko makubwa kuhusu utenda-kazi wake.” Ingawa huenda likaonekana kuwa jambo lisilowezekana kupambana na ufisadi, Biblia inatuhakikishia kwamba kuna mabadiliko makubwa yanayokuja, na hakika yatatimia.

v  Umaskini

Umaskini (kutoka neno la Kiarabu) ni hali ya ukosefu wa mahitaji ya msingi ya binadamu kama vile chakulamaji salamahuduma za afyamavazi na nyumba kutokana na kukosa uwezo wa kuvinunua. Hii pia inajulikana kama umaskini uliokithiri au ufukara.

Umaskini wa kadri ni kuwa na raslimali chache zaidi au mapato madogo zaidi kulingana na watu wengine katika jamii au nchi au hali ya kadiri duniani. Hali hii pia hujulikana kama umaskini halisi au unyonge. Umaskini linganishi ni hali ya kuwa na rasilimali chache au kipato cha chini kuliko wengine kwenye jamii au nchi, au ikilinganishwa na wastani duniani kote.

Umaskini unajumlisha pia matokeo yake upande wa siasa na jamii.

Kupunguza ufukara ni kati ya malengo makuu ya taasisi nyingi za kimataifa, kama vile Umoja wa Mataifa na Benki ya Dunia. Benki hiyo imekadiria kuwa watu milioni 702.1 walikuwa wakiishi kifukara mno mwaka 2015, wakati walikuwa bilioni 1.75 mwaka 1990 (kutoka 37.1% hadi 9.6%).

Kati yao, milioni 347.1 hivi walikuwa Afrika Kusini kwa Sahara (35.2% za wakazi) na 231.3 Asia Kusini (13.5%), lakini ufukara ni changamoto kwa nchi zote duniani.

UNICEF imekadiria kwamba nusu ya watoto wote duniani wanaishi kifukara (bilioni 1.1).

Wataalamu mbalimbali wamesema sera za uliberali mpya zinazofuatwa na taasisi za kiuchumi za kimataifa (kama vile IMF na Benki ya Dunia) zinazidisha tofauti za kiuchumi kati ya binadamu.

Ipo mifano mbalimbali kutoka kwenye tamthilia ya ya Mstahiki Meya.

·         Wagojwa wanaofika zahanatini hawana pesa za kulipia huduma wanazohitaji. Siki asema “hawa watu hawana pesa” (uk.2)

·         Wagojwa wengine hata karatasi ya kunakilia udodosi wao hawana (uk.3) 

·         Wafanyakazi kama mama mwenye mtoto mgojwa zahanatini anasema amemlisha mtoto kiporo cha makombo aliyotoa kwa Mstahiki Meya. Asema chakula hicho kilikuwa kidogo hivyo yeye hakukila (uk. 4).

·         Mama anapoulizwa na daktari iwapo alikitokosa chakula anasema hakuweza kwa sababu bei ya makaa na mafuta ya taa imepanda mno. 

·         Wafanyakazi wa Mstahiki Meya hula chakula kilichopimiwa mbwa nao hukila wasidhurike (uk.5). 

·         Waridi anazungumzia umaskini wan chi (uk.3) anaposema, ‘…… nchi yenyewe maskini; ombaomba’.

·         Watoto wana utapia mlo, umaskini unawakosesha watu lishe bora. Nesi anasema; ‘Kitoto chenyewe kiriba chaongoza’ (uk. 5-6).

·         Nesi ni mkali (uk.3) na anawazungumzia wagojwa kwa dharau lakini umaskini unawafanya kumsihi ili angalau wahudumiwe kwenye zahanati hiyo kwa sababu hawana namna.

·         Umaskini wa nchi unadhihirika katika utegemezi wa mikopo kutoka nchi geni.

·          Wengi wa wakazi wa Cheneo ni maskini kiasi kwamba hawawezi kujikimu kwa chakula cha bei ya chini kama sukuma na dona. Hawawezi kugharamia elimu, aidha wanaishi mabandani. Medi anasema watoto wao anakula vya kuokota! (uk.61).

Kwa yakini umaskini umekuwa donda sugu katika jamii zetu. Madharayake yanakuwa chungu nzima.

Ripoti mbalimbali za  benki ya duniaz inasema, zaidi watu maskini duniani tayari wameumizwa na matukio yanayosababishwa na mabadiliko ya tabia nchi ikiwemo pamoja na kuongezeka kwa joto, njaa na mafuriko na kwamba hii inasababishwa na maisha ya watu hao kutegemea ardhi na kwamba wanaishi katika ukanda ambao uko katika hatari kutokana na ukosefu wa huduma za jamii."Watu masikini wapo katika hatari zaidi ya majanga yanayosababishwa na mabadiliko ya hali ya hewa ikilinganishwa na watu matajiri, kwasababu watu matajiri wanauelewa zaidi na kwamba masikini wanakosa mifumo ya kifedha na mifumo ya usalama wa kijamii ambayo ingewawezesha kujiandaa vema na kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa," zinasema sehemu ya ripoti hizo.

Umasikini una athari mbalimbali katika jamii zetu. Mojawapo wa athari hizi ni afya.Theluthi moja ya vifo - watu milioni 18 hivi kwa mwaka au watu 50,000 kwa siku - vinatokana na sababu zinazohusiana na umaskini. Kwa jumla, watu milioni 270, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, wamefariki kutokana na umaskini tangu 1990. Wale ambao wanaishi katika umaskini wanateseka kwa viwango visivyo sawa kutokana na njaa au hata ukosefu wa chakula na magonjwa.

Wale wanaoishi kwa umaskini huishi miaka michache zaidi. Kulingana na Shirika la Afya Duniani (WHO), njaa na ukosefu wa lishe borandilo tishio kuu zaidi kwa afya ya umma duniani na ukosefu wa lishe bora ndio unaochangia pakubwa vifo vya watoto, katika nusu ya kesi zote. Kila mwaka karibu watoto milioni 11 wanaoishi katika umaskini hufa kabla ya kufikisha miaka mitano. Watu bilioni 1.02 hulala bila chakula kila siku. Umaskini huongeza hatari ya ukosefu wa makazi. Kuna zaidi ya watoto wasio na makao milioni 100 duniani. 

 

Ongezeko la tishio la matumizi ya madawa ya kulevya pia linaweza kuhusishwa na umaskini. Kulingana na Kipimo cha Kiwango Cha Njaa Duniani, Asia ya Kusini ina kiwango kikubwa zaidi duniani cha watoto wanaokosa lishe bora. Karibu nusu ya watoto wote nchini Uhindi hawapati chakula cha kutosha, mojawapo wa viwango vikubwa zaidi duniani na ni karibu mara mbili ya kiwango cha Kusini kwa Sahara barani Afrika

Kila mwaka, zaidi ya wanawake nusu milioni wanakufa kutokana na mimba au wakati wa kujifungua. Karibu asilimia tisini za vifo vya wakina mama hutokea katika Asia na kusini kwa Sahara barani Afrika, ikilinganishwa na chini ya asilimia moja katika nchi zilizoendelea duniani.

Mbali na afya, elimu vile vile huathirika.Uchunguzi umedhihirisha ya kuwa watoto wanaotoka katika jamii zenye mapato ya chini wanakumbana na tishio kubwa la kutofanya vyema katika masomo yao. Mara nyingi, jambo hili huanza kuwadhuru watoto hawa wakiwa wangali katika kiwango cha shule ya msingi. Katika mfumo wa elimu wa Amerika, watoto hao hupata tishio kubwa zaidi, ikilinganishwa na watoto wengine, ya kutopata gredi nzuri shuleni, kuwekwa katika maeneo maalum yaliyotengwa wakati wa masomo shuleni na hata kukosa kumaliza masomo yao ya shule ya upili Kuna mambo kadhaa yanayoeleza sababu za wanafunzi kuwa na mazoea ya kuacha shule.

Kwa watoto walio na rasilimali kidogo, tishio linatokana na sababu kama vile viwango vya watoto waliovunja sheria, viwango vya juu vya watoto waliopata mimba, wakiwa wachanga na kutegemea kiuchumi mzazi au wazazi wenye mapato ya chini.

 

Waaidha umasikini umesababisha utovu wa nidhamu katika jamii kwa kuwa vijana wamejiingiza katika vitendo viovu. Baadhi ya vitendo hivi ni wizi hata wa kimabavu, ukahaba na kadhalika. Vitendo kama hivi huidhalilisha jamii kabisa kiasi kwamba huonekana kama gofu tu.

Sehemu nyingi za mabanda hapa nchini Kenya zinaimarika kwa kuwa viwango vya umaskini vinazidi kukwea ngazi kucha kutwa.

 

v  Ukoloni mamboleo

Ukoloni Mamboleo ni neno linalotumiwa na wakosoaji wa ukoloni kuelekezwa kwa nchi tajiri kuendelea kuingilia masuala ya nchi zinazoendelea baada ya ukoloni wenyewe kwisha kwa ukiukaji wa azimio la Umoja wa Mataifa. Wanakosoa mataifa ya kibepari kuhusika na dhuluma katika biashara ya kisasa na yaliyokuwa makoloni.

Wakosoaji wanasisitiza kwamba wafanyabiashara binafsi na makampuni ya biashara ya kigeni huendelea kunyonya rasilimaliza mataifa baada ya enzi ya ukoloni kama ilivyotekelezwa kutoka karne ya 16 hadi karne ya 20.

Katika matumizi mapana, Ukoloni Mamboleo huweza kumaanisha ule ushiriki wa nchi zenye nguvu katika mambo ya nguvu chini ya nchi; hii ni muhimu hasa Amerika kusini.

Kwa maana hii, Ukoloni Mamboleo huweza kutaja aina ya kisasa ya ukoloni, uchumi wa ubeberu: kwamba mataifa yenye nguvu kuishi kama wakoloni, na tabia hii inafananishwa na ukoloni.

Kwa hivyo ukoloni mamboleo ni ile hali ya mataifa wafadhili au ya kigeni kudhihirisha ushawishi wake kwa mataifa ya ulimwengu wa tatu kwa kushurutisha uwepo wa masharti ya kiuchumi, kiasa, kijamii na hata kiteknolojia. Ukoloni mkongwe nao ni hali ya nchi kuidhibiti au kuikalia nchi nyingine kimabavu kwa misingi ya kisiasa na kiuchumi kama wakati mataifa machanga barani Afrika yalipotawaliwa moja kwa moja na wakoloni kutoka bara Uropa.

Wakoloni hapa walipoondoka na mataifa haya machanga kupata uhuru, bado wameendelea kuaathiri mataifa haya. Athari hizi hudhihirika kupitia masharti yanayowekewa mataifa haya machanga na mahusiano ya kiuchumi na kisiasa baina yao na waliowatawala. Huu ndio ukoloni mambo leo.

 

 

·         Dawa inaagizwa kutoka nchi za mbali. (uk.2) shehena zasemekana ziko bahari kuu.

·         Watoto wa tabaka tawala wanasomea ng’ambo na akina yakhe ndio wa kung’ang’ana na elimu inayotolewa miaka hamsini baada ya uhuru. (uk.26).

·         Meya anapotahadharisha kwamba kukaidi mipango ya mataifa ya nje kuhusu malengo ya milenia ambayo ni ya wafadhili ni hatari. (uk.14).

·          Siki kulalamikia hali ya kufuata ushauri wa nchi za kigeni ambao hawakushirikishwa ni ukoloni mamboleo.

·           Kugawana gharama za huduma ni wazo la mataifa ya kigeni ilhali wananchi hawana uwezo kifedha. (uk.3).

·           Dhana ya ubwana na utumwa inadhihirika katika mahusiano baina ya bwana Meya na wafanyakazi wake Gedi na Dida. Hii ni ishara ya ukoloni mamboleo tunaoupata katika mataifa mengi machanga miaka mingi baada ya kuondoka kwa wakoloni. Gedi kila anapoitwa na Meya anaitika ‘yes Sir’. Meya anapokosa hisani anapopewa pole na Dida katika uk. 9 inagogoteza hali hii.

·          Hali ya nchi kiuchumi ingali ileile ya ombaomba miaka hamsini baada ya uhuru. Uongozi wa Baraza unawanyonya wafanyakazi namna walivyofanya wakoloni. Kwa mfano wafanyakazi wa Baraza hawalipwi mishahara, wanapolipwa ni nusunusu na wanatozwa kodi, ilhali madiwani wanajipa nyongeza na kukwepa kulipa kodi.

·         Utegemezi wa mikopo kutoka nchi za kigeni kwa mambo ya kimsingi kama vile kulipa mishahara ya wafanyakazi. (uk.20)

·         Hali ya kupewa ufadhili kwa masharti, kwa mfano kupewa mkopo lakini kulazimishwa kupunguza idadi ya wafanyakazi. (uk.20).

Ukoloni mamboleo ni hali ambayo mataifa ulimwenguni hasa nchi zinazoendelea haziwezi kuepuka kamwe.Katika jamii zetu za sasa inadhihirika wazi kuwa swala la Ukoloni mamboleo limekita mizizi. Hali hii hujitokeza katika njia mbalimbali kama zifuatazo:

Ø  Mashirika ya kimataifa

Wakosoaji wa Ukoloni Mamboleo pia wanasema kuwa uwekezaji na mashirika ya kimataifa uliimarisha maendeleo duni. Katika baadhi ya nchi, ubinafsishaji wa rasilimali za kitaifa ulifuatiwa na kuongezeka kwa kiwango cha ukosefu wa ajiraumaskini, na kushuka kwa mapato. Hii ni kweli hasa katika mataifa ya Afrika Magharibi ya Guinea-BissauSenegal, na Mauritania ambapo uvuvi una historia muhimu kwa uchumi wa wenyeji. Kuanzia mwaka 1979Umoja wa Ulaya ulianza kubana haki za uvuvi katika pwani ya Afrika Magharibi kinyume cha Mkataba wa Umoja wa Mataifa juu ya bahari ambao unatambua umuhimu wa uvuvi kwa jamii. 

Ø  Taasisi za fedha za kimataifa

 

Wakosoaji wa Ukoloni Mamboleo walitaka kukataa mikopo (hasa isiyolipika) kutoka kwa taasisi za fedha za kimataifa kama vile Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na Benki ya Dunia (WB). Wao wanasema kwamba ili wapewa mikopo, na aina nyingine za misaada ya kiuchumi, mataifa dhaifu yanalazimika kuchukua hatua kwa maslahi ya kifedha ya IMF na Benki ya Dunia lakini dhidi ya uchumi wao yenyewe. Marekebisho ya miundo hayo yana athari ya kuongeza kuliko kupunguza umaskini ndani ya taifa. Watuhumiwa wa kushiriki katika ubeberu huo ni pamoja na Benki ya Dunia, Shirika la Biashara Duniani, G8 na World Economic Forum.

Wale ambao wanasema kwa hakika na ukweli kwamba Afrika leo inalipa pesa zaidi kila mwaka katika huduma ya malipo ya madeni ya IMF na Benki ya Dunia kuliko inayopata katika mikopo kutoka kwao, na hivyo mara nyingi kunyima wenyeji wa nchi hizo mahitaji halisi. Utegemezi huu unaruhusu IMF na Benki ya Dunia kulazimisha mipango yao juu ya mataifa haya. Marekebisho yanayotokana na mipango hiyo, hasa ubinafsishaji, husababisha kuzorota kwa afyaelimu, na kutoweza kuendeleza miundombinu, na maisha kwa jumla.

 

Ø  Ushawishi Mbadala

Kutokana na akiba kubwa ya fedha, serikali ya China imeanza kucheza nafasi muhimu dhidi ya ushawishi wa IMF, kwa kukopesha baadhi ya nchi, kama vile Angola mwaka 2006.  Katika miaka ya karibuni, Jamhuri ya Watu wa China imejenga sana mahusiano na Afrika,China kwa sasa ni wa pili kwa uhusiano mkubwa na Afrika, baada ya Marekani. Mnamo Agosti 2007, kulikuwa na raia 750,000 hivi wa Uchina wakifanya kazi au kuishi katika nchi mbalimbali za Afrika wakijipatia rasilimali - mafuta, madini - ili kulisha uchumi wa nchi yao na kupanua masoko ya makampuni yake. Mwaka 2006, biashara kwa njia mbili iliongezeka hadi dola bilioni 50. 

Mwaka 2007, serikali ya China na Kongo-Kinshasa ziliingia katika mkataba ambapo makampuni ya Kichina yanayomilikiwa na serikali yatatoa huduma mbalimbali (miradi ya miundombinu) katika kubadilishana na shaba ya migodi. 

Watetezi wa haki za binadamu na wapinzani wa serikali ya Sudan wanaonyesha jinsi China ilivyotoa silaha na ndege ili kupata petroli na gesi ya asili namna ya kikoloni ili kudumisha udhibiti wao wa maliasili.  Kulingana na wakosoaji wa China, China inayotolea Sudan msaada wake kutishia kutumia kura ya turufu kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kulinda Khartoum kutoka vikwazo juu  ya Darfur ili kulinda maslahi yake nchini Sudan. 

Ø  Korea ya Kusini na ununuzi wa ardhi

Serikali tajiri na makampuni ya kimataifa yenye nguvu kutoka Korea ya Kusini zimenunua haraka mamilioni ya hekta za ardhi ya kilimo katika nchi zinazoendelea katika jitihada za kupata chakula.Hivyo, serikali ya Korea Kusini sasa hutumia rasilimali za nchi maskini kwa kununua ng'ambo nishati na chakula, ili kuwa mmoja wa uchumi unaokua kwa kasi zaidi.

Park Yong-soo wa Korea ya Kusini alisisitiza kuwa "taifa halizalishi tone moja ya mafuta yasiyosafishwa na viwanda vingine muhimu madini. Kwa nguvu ya ukuaji wa uchumi na kusaidia maisha ya watu, hatuwezi kusisitiza mno kiasi kwamba kupata rasilimali asili katika nchi za nje ni lazima kwa maisha yetu ya baadaye.

Mkuu wa Shirika la Chakula na Kilimo (FAO), Jacques Diouf, ameonya kwamba kupanda katika nchi utata mikataba inaweza kutengeneza fomu ya "ukoloni mamboleo", kwa mataifa maskini kuzalisha chakula kwa ajili ya matajiri kwa gharama zao wenyewe na njaa ya watu.

 

v  Utamaduni

Ukoloni Mamboleo unaeneza utamaduni wa kigeni ili kudhibiti mataifa mengine upande wa maadili na mitazamo kupitia vyombo vya habarilughaelimu na dini, hatimaye kwa sababu za kiuchumi. Kwa mfano, waandishi wanachapa vizuri zaidi himaya ya kikoloni katika historia ya karne ya 19.

Kuna seti ya nadharia katika falsafafilamusiasasayansi na fasihi inayoshughulika na historia ya utamaduni wa utawala wa ukoloni.

v  UFEMINISTI

Ufeministi ni istilahi inayotumiwa kueleza nadharia ambayo imewekewa misingi na msukumo mkubwa pamoja na nia ya kupigania ukombozi wa wanawake kutokana na pingu za kiutamaduni na kidini zilizomfunga kwa muda mrefu. (Malenya, 2012)

Katika Wamitila (2002:235), Ufeministi ni nadharia inayopinga asasi zote za kijamii zinazochangia katika kudhulumiwa kwa mwanamke.

Irib (2014) anasema, Ufeministi ni harakati za ukombozi zilizoanzishwa na wanawake ili kupinga mfumo dume ambao unawakandamiza wanawake katika nyanja mbalimbali

Hivyo basi, ufeministi ni harakati zinazofanywa na wanawake kujikomboa katika Nyanja mbalimbali kama; kifikra, kiuchumi, kisiasa, kijamii na kiutamaduni kutoka katika mifumo ya ukandamizwaji .

o   Historia ya Ufeministi

Dhana ya ufeministi ilianza kujitokezaa kwa mara ya kwanza baada ya Simone De Beauvoi aliyezaliwa huko Ufaransa akiwa ni mtoto wa kike na wa kipekee katika familia yao na ambaye alionekana kama muhamasishaji wa kwanza juu ya Ufeministi. Hii ilitokana na uwezo mwingi aliokuwa nao katika kufikiri, hekima na bidii katika kazi vilivyosababisha kusifiwa daima na baba yake. (Njogu & Chimera, 1999).

Hali hii ilianza kuibua mtazamo hasi dhidi ya wanawake baada ya baba yake kudai kuwa, uwezo wa akili alionao unafanana na wake na wala sio kama wa mama yake. (Njogu & Wafula, 2007). Hali hii ilimfanya Simone De Beauvoi kujenga dhana ya unyanyasaji wa wanawake na hata kumfanya asifikilie kuolewa bali ajikite na harakati za ukombozi kwa wanawake

Kupitia harakati zake aliamsha hisia na hari kwa wanawake kutaka kujikomboa. Baadhi ya nyanja zilizoonekana kumkandamiza mwanamke ni pamoja na asasi za kijamii kama vile dini, tamaduni na uandishi mbalimbali wa kazi za fasihi

o   Aina za Ufeministi:

Ufeministi wa Kiharakati; huu ni ukombozi unaotambua kuwa mwanamke ananyanyaswa na kukandamizwa na mwanaume hivyo kuona umuhimu wa kuwaelimisha wanawake kukataa unyanyaswaji na ukandamizwaji dhidi yao.

Ufeministi wa Kiutamaduni; ni aina ya ufeministi unaotoa wito kwa kila mwanamke kuona umuhimu na wajibu wa kushiriki katika ukombozi wa mwanamke.

Ufeministi wa Kidhahania; ni aina ya ufeministi ambao unamwonesha mwanamke kama kiumbe huru mwenye uwezo wa kuteua, kujilinda na kujitazama atakavyo mwenyewe. Aidha, mwanamke anaona kuwa hakuna haja ya mawazo yake kuamuliwa na mwanaume au mtu yeyote katika jamii. Kutokana na dhana hii, jamii imeanza kuwapata wanawake wanajeshi, wazalishaji mali, walimu na matabibu.

Ufeministi wa kiutamaduni; hii ni aina ya ufeministi ambayo inautizama utamaduni kama nyenzo kubwa katika kumdhalilisha na kumfanya mwanamke aamini kuwa anapaswa kuwa na hali aliyonayo mfano; kukandamizwa, kudhalilishwa na kukosa uhuru wa kutoa maoni. 

Maudhui ya nafasi ya mwanamke yanahusu masuala ya kijinsia hasa vile ambavyo
mhusika wa kike amesawiriwa katika kazi ya kifasihi. Wanawake huwa wanakweza au kutwezwa katika kazi za kifasihi.Mwandishi wa tamthilia ya Mstahiki Meya amewatumia wahusika wachache katika mchezo huu. Hata hivyo, nafasi alizowapa hawa wachache katika mchezo hii. Hata hivyo, nafasi alizowapa hawa wachache zinadhihirisha kwamba, mwanamke hajaachwa nyuma katika shughuli za mapambano katika jamii. Yeye (mwanamke) amejifungata masombo kuhakikisha kwamba haki na usawa vinadumishwa katika jamii kwa minajili ya manufaa ya vizazi vijavyo.

Mmojawapo wa wahusika wa kike ambaye nafasi yake inajitokeza vizuri zaidi ni
Waridi. Waridi na Nesi katika hospitali ya Baraza la Cheneo. Wanafanya kazi na wenzake katika hospitali hiyo pamoja na Daktari Siki. Waridi ni mhusika ambaye anaweza kudaiwa kwamba hajapevuka kamwe kuhusu matatizo yanayokumba nchi yake. Kwake, ukosefu wa dawa pale hospitalini ni jambo linalosababishwa na hali ya nchi yake kuwa changa na maskini (uk.3). Haya si madai wala imani ya kweli kwa kuwa Baraza la Cheneo lina utajiri mkubwa ila tu limeachwa

kuongozwa na viongozi walafi.

Ingawa ni mwanamke, ni kinaya kwamba mhusika huyu anamlazimisha mama
mwenye mtoto mgojwa kupiga foleni bila kujali kuwa mtoto yuko katika hali mbaya
kiafya. Kwa hiyo, tunaweza kudai kwamba hana utu wala huruma (uk.3). Je, adui wa
mwanamke ni mwanamke mwenzake katika jamii? Vilevile, anasisitiza kuwa wagojwa
wazidi kusubiri dawa na kwamba wanaotaka kulazwa walipie gharama hiyo (uk.7).
Hiki ni kinyume na Siki (mwanamume) ambaye anawahurumia wagojwa hao ambao ni
mafukara.
Waridi pia anakata tamaa kutokana na hali mbaya ya mambo pale hospitalini. Dawa
walizokuwa wakisubiri hazikuletwa. Wagojwa waliendelea kufariki pale hospitalini
kutokana na ukosefu wa dawa. Mambo haya yanamfanya kutamauka na kujiuzulu
(uk.35). Kwa hivyo, ni mhusika asiyekuwa mvumilivu wala hana stahamala.
Hata hivyo, tukigeuza upande wa pili wa sarafu, kuna mwanamke mwenzake ambaye
anapambana bega kwa bega na wanaume katika kukabiliana na dhuluma
zinazoikumba jamii. Huyu ni Tatu ambaye sawa na Medi na Beka ni viongozi na
wafanyakazi. Wao ndio waliotumwa na wafanyakazi kwenda kuwakilisha mbele ya
Meya na kuwasilisha malalamiko yao. Kwa hiyo, katika kiwango hiki, mwandishi
amemsawiri mwanamke kama mshirika mwenza wa mwenzake mwanaume katika
jitihada za kupigania ukombozi.

Tatu ni mtetezi wa haki za wafanyakazi wenzao. Yeye na wenzake wanapofika mbele ya Mstahiki Meya, wanawasilisha matatizo ya wenzao jinsi walivyotumwa (uk.66-72).Katika kutekeleza hili, wanaonyesha ujasiri na hawachelei kumkosoa Meya. Hawatereki kamwe katika kuutafuta ukweli na wanamwambia Meya ukweli wa mambo yalivyo katika himaya anayoiongoza. Kwa mfano, wanamwambia bayana ukweli kuhusu tofauti za maisha kati ya viongozi (matajiri) ambao ni watawala na maskini (watawaliwa) (uk.69). Maswala kuwahusu Wanawake yamekuwa yakiangaziwa katika jamii zetu tangu jadi.

Hata kwa sasa kila jamii inajaribu Kuhakikisha kuwa wanawake wanapewa nafasi yao kama inavyostahili. Mfano katiba ya Kenya inapendekeza thuluthi ya uwakilishi wa wanawake kudhihirika wazi katika nyanja mbalimbali. Ukitazama utagundua kuwa upo wadhifa maalum ambao umetengwa hasa kwa wanawake ambao ni Wawakilishi wa wanawake(Women Rep) ambacho hicho ni kiti maalum kwa kina mama.

Mbali na hapo Tumeona wanawake wa Kenya wakitambulika hata kwenye kiwango cha kitaifa na kimataifa. Hii nikwa sababu ya juhudi zao mbalimbali za kumkomboa mwanamke na kumpa hadhi yake kama inavyofaa.Waaidha hawa wanawake ni wale wenye ushawishi mkubwa zaidi kulingana na Ripoti ya www.ureport.co.ke  iliyotolewa  09th Mar 2017

Hawani pamoja na Martha Karua ambaye ni mwanasiasa mtajika nchini  Kenya na ambaye amekuwa mbuge wa eneo bunge la Gichugu kwa muda mrefu. Mbali na hapo alikuwa baadhi ya wanawake wenye ushawishi mkubwa serikalini wakati wa serikali ya aliyekuwa rais wakati huo, Mwai Kibaki. Ikumbukwe kuwa yeye pia alikuwa miongoni mwa wajumbe walioteuliwa na serikali kutafuta uwiano wa taifa hili na upinzani baada ya uchaguzi wa 2007 ulioleta maafa na utata nchini kati ya serikali na upinzani. 

Lupita Nyong’o ambaye aliingia katika kioo cha ulimwengu katika mwaka wa 2014 alipocheza mchezo wa kuigiza kama Patsey katika Steve McQueen 12 years a slave.  Shughuli hiyo ilimfanya kupokea tuzo 25 kuanzia mwaka wa 2013 hadi 2014 pamoja na ile tuzo bora zaidi ya Oscar. Kwa sasa ni mwanamke mtajika na balozi wa Afrika.

Marehemu  Wangari Maathai naye pia atakumbukwa na wengi kitaifa na kimataifa katika utetezi wa mazingira. Mwaka wa 1977 aliannzisha Green Belt Movement ambayo ilikuwa na lengo la kuhifadhi misitu. Katika mwaka wa 2004 alikuwa mwanamke wa kwanza mwafrika kupokea tuzo ya Nobeli.

Mkewe rais Margaret Kenyatta anapendwa na wengi kwa kuanzisha Miradi mbalimbali ambayo inagusa afya ya watu.Baadhi ya Miradi hiyo ni kupunguza vifo vya watoto na kina mama hata wanapojifungua. Mradi wake umepewa jina, Beyond Zero Campaign. Oktoba 2014 alitajwa kuwa mwanamke wa mwaka na Umoja wa Mataifa.

Mifano ya wanawake kama hawa hapa nchini Kenya ni mingi mno ikiwa pamoja na  Njoki Ndungu ambaye ni hakimu katika mahakama ya rufaa nchini,Gina Din ambaye ni mwanzilishi wa kampuni ya Public Relations Afrika Mashariki na pia balozi wa Msalaba mwekundu. Waidha yupo Catherine Kasavuli ambaye amekuwa maarufu katika uga wa uanahabari,

Hitimisho

Kama inavyodhihirika katika makala haya ni kuwa mwandishi yeyote wa kazi ya fasihi huyapata na kuyajenga maudhui yake kutokana na hali halisi ya jamii. Kwa kupitia tamthilia ya Mstahiki Meya imekubalika kuwa mtuzi huyu ameyapachua maudhui yake katika jamii anamoishi au ufahamu wake kutokana na mazingira mbalimbali ambyo amekumbana nayo.

Maudhui makuu ambayo yamejadiliwa yamefungamana na mengine madogo ambayo kwayo yanaathiriwa moja kwa moja na yale makuu. Haya ni pamoja na: udhalimu/unyanyasaji ,utabaka ,ubarakala/ukaragosi,utu na uadilifu ,matatizo ya uchumi ,usaliti,nafasi ya sheria,haki,uwajibikaji na mapuuza ,ubinafsi na umangimeza ,unafiki na huduma za kijamii. Kwa hivyo kwa kuichukua jamii kama kioo cha kumwongoza mwandishi yeyote yule basi atainasa jamii moja kwa moja.

Marejeleo

a)      T.M. Arege(2013) Mstahiki Meya,Vide Muwa, Nairobi Kenya.

b)      C- Brooks na R.P. Warren, Understanding Fiction, F.S. Crofts & Co., Inc. 1943.

c)      .B. Deutsch, Poetry Handbook, Jonathan Cape, Thirty Bedford Square, 1965.

d)     W. Blair (na wenzake), Literature, Scott, Foresman and Company, New York: 1966.

e)      C.H. Holman, A Handbook to Literature, The Odysey Press, New York, 1936.

f)       R. Wellek na A. Warren, Theory of Literature, A Harvest/HBJ Book London 1975.

g)      F-V. Nkwera, Sarufi na Fasihi: Vyuo na Sekondari, TPH, 1978

h)      S.D- Kiango na T.S.Y. Sengo, Hisi Zetu - I . TUKI, 1973.

i)        P. Muhando na N. Balisidya, Fasihi na Sanaa za Maonyesho, TPH, 1976

j)        H. Arvon, Marxist Aesthetics Cornell University Pres, 1973.

k)      A. Zis, Foundations of Marxist Aesthetics, Progress Publishers, Moscow, 1977.

l)        M.Mulokozi, na K-K- Kahigi, Kunga. za Ushairi na Diwani Yetu", TPH, Dar es Salaam: 1979.

m)    F.E.M.K Senkoro, Fasihi, Press and Publicity Centre, Dares Salaam: 1979.

n)      Irib world Service (march 14, 2014) Matatizo ya Wanawake katika Ulimwengu wa Magharib.www.kiswahili.irib.ir/38823   

o)      Malenya, M. M.(2012), Matumizi ya  Lugha katika Fasihi Simulizi. Mwanza: Inland Press.

p)      Wamitila, K. M. (2002), Uhakiki wa Fasihi, Misingi na Vipengele vyake. Nairobi: Phoenix.

q)      Njogu, K. & Chimera, R. (1999). Ufundishaji wa Fasihi. Nairobi. Jomo Kenyatta Foundation.

r)       Njogu, K & Wafula, R.M (2007). Nadharia za Uhakiki wa Fasihi. Nairobi. Jomo Kenyatta Foundation

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

No comments:

Post a Comment