UHAKIKI WA HADITHI YA FUMO LYONGO KWA KUTUMIA NADHARIA YA VIKALE.
Nadharia ya vikale ni
mojawapo wa nadharia critical theory.Hii ni nadharia ambayo kuchanganua
maandishi hasa visa vya kikale kwa kuelekeza makali yake kwenye ngano za
kimiujiza.Mifano ya ngano hizi za kimiujiza ni mighani.
Nadharia
hii imeelekeza mizizi yake katika miaka ya 1934 wakati Maud Bodkin
alipokichapisha kitabu chake, Archetypal Patterns in Poetry. Nadharia hii ina
Mihimili yake miwili mikuu katika vitengo viwili vya kiakademia. Vitengo hivi
ni Anthropolojia
na saikolojia
Kila mhimili huchangia nadharia hii katika njia tofauti teule. Saikolojia
hujitokeza kama tawi dogo la nadharia hii ya vikale. Nadharia
ya vikale ilitia fora mno katika miaka ya 1940 na 1950 kutokana na kazi ya
mchanganuzi wa vikale kutoka Kanada, Northrop Frye. Ingawa nadharia hii ya
vikale haijatamba na kutaratamba pakubwa, bado inashikilia nafasi kubwa muhimu
katika jamii zetu za kiutamaduni. .
Usuli wa athropolojia ya vikale unaupiku
usuli wa saikolojia kwa zaidi ya miaka thelathini(30) Maandishi The Golden
Bough (1890-1915) ya mwana-anthropojia kutoka Uskoti , Sir James George Frazer
ndiyo yaliyokuwa makala ya kwanza ambayo yaliangazia hadithi kama hizi za
kimila. Frazer alikuwa mmoja wa wanaathropolojia wachanganuzi waliokuwa katika
chuo kikuu cha Cambridge ambao walifanya kwa jino na ukucha kwenye makala : The
Golden Bough.
Frazer alipokuwa akifanya haya yupo mwenziwe Carl
Gustay Jung, na Frye. Wapo wana-lugha ambao vilevile walitoa mchango wao wa kuunga mkono wazo hili
ni pamoja na Maud Bodkin. Kutokana na maelezo ya awali basi vikale vina usuli
wa ukongwe katika jamii za wanadamu.
Ili kuthibitisha hili ,wapo watafiti wa nadharia ambao vilevile wamekita
kambi katika fani hii ya vikale.
Makumbo
yote mawili haya ya anthropolojia na kisaikolojia katika swala zima la vikale
yana umuhimu mkubwa. Katika upande wa Anthropolojia masomo ya nadharia ya
vikale huhamasisha akili zetu kuhusu vikale ambapo imani ya wasomi kama vile
Joseph Campell ni msingi wa ujumbe kwa msomi yeyote na hutupa wakati mwafaka wa
kujadili na wenzetu katika vitengo mbalimbali.
Swala
la kuwepo kwa mashujaa halina mipaka kiasi kwamba inavuka mipaka ya Utamaduni
na kiwakati kwa kuaonyesha wazi kuwa binadamu ni mmoja tu. Kwa upande wa
kisaikolojia, nadharia ya vikale huangazia maisha yetu namna yalivyo hasa
tunapochanganua maswala kuhusu mashujaa na ushujaa wao mbalimbali katika jamii.
Tunapotazama mashujaa hawa wakipambana na maisha, kwa kuanguka, kujifunza,
kuvumilia na kupitia katika hali za faraja na hofu, ni taswira kabambe
inayodhihirisha wazi hali halisi ya maisha yetu jinsi yalivyo. Hivi ni kusema
kuwa kujifunza maswala ya vikale hutuweza kujitambua na kujijua jinsi
tulivyo.Kwa hivyo tunapodadavua maswala ya nadharia ya ukale sio tu ati
tunarejeshwa kuhusu ukale wa mambo namna yalivyokuwa bali hutuwezasha Kujua
ukale wetu binafsi.
Kwa mujibu wa Wafula R.M na N. K. (2007:106),
Vikale ni picha kongwe zinazotokea mara kwa mara katika kazi za fasihi. Vikale
hivi vinaweza kuwa taswira, wahusika, miundo ya usimuliaji na fani zingine
zinazopatikana katika fasihi yoyote.
Abrahams (1971:11-12), alieleza nadharia ya
uhakiki wa vikale kwa mitazamo miwili. Alieleza kuwa chimbuko la nadharia hii
ni kutokana na kazi ya James G.Frazer katika kitabu cha “The Golden
Bough” (1890-1915) kilichotolewa na katika idara ya Antropolojia
Linganishi, Chuo Kikuu cha Cambridge. Abrahams (1971:11-12) aneleza kuwa kitabu
hiki kilifuatilia ruwaza za kimsingi za visaasili na za kitambiko ambazo alidai
hujirudiarudia katika visakale na taratibu nyingi katika tamaduni anuwai.
Kwa
upande mwingine alieleza kuwa, nadharia ya vikale ilitokana na maelezo ya Carl
G. Jung kuhusai na na akili-laza. Jung alikuwa mwanafunzi wa Sigmund Freud,
mtaalamu aliyeasisi taaluma ya uchanganuzi nafsia. Lakini walitofautiana
kimawazo. Wakati ambapo Freud alisisitiza akili-laza ya kibinafsi, naye Jung
alisisitiza kuhusu akili-laza jumuishi. Jung alitumia istilahi ya vikale kwenye
taswira za asili za Kumbukumbu zinazorudiwarudiwa kutokana na tajiriba katika
maisha ya tangu mababu zetu wa kale.
Alisisitiza kuwa, taswira hizi hurithiwa na
kutiwa kwenye akili-laza jumuishi ya jamii ya watu na ambazo hudhihirika katika
visaasili, ndoto, mawazo ya binadamu mathalan, katika vipengele vyote katika
maisha ya binadamu wote duniani na pia katika kazi za kifasihi. Katika uhakiki
wa kifasihi, vikale hutumiwa katika ruwaza ya aina za wahusika au taswira
ambazo zinafanana katika tungo mbalimbal za kifasihi na pia katika visasili na
mitindo anuwai ya kijamii. Kufanana katika maswala haya anuwai huchukuliwa
kuakisi seti ya ruwaza bia ambazo zimekuwepo tangu jadi. Nadharia ya uhakiki wa
vikale kwa hivyo inaeleza kuwa binadamu wote ni sawa popote walipo. Tofauti ni
kidogo za kufikirika ambazo husababishwa na tofauti za kihistoria na za
kimazingira.
Kwa mujibu wa Mutiso (1999:2). Kwa jumla,
vikale hurejelea ruwaza za kimsingi. Ruwaza za jumla au bia za aina moja au
nyingine ambazo aghalabu hudhihirika katika jamii za watu mbalimbali duniani.
Anashikilia kuwa vikale humvuta msomaji vikitumiwa vizuri katika kazi ya
fasihi.
Waitifaki wa nadharia ya vikale wanashikilia kwamba umaarufu wa kazi ya sanaa
unatokana na wahusika, maudhui na taswira zinazorudiwarudiwa katika kazi
husika. Baadhi ya wahusika wanaotumiwa kudhihirisha vikale ni kama: jaribosi au
nguli anayeandaa safari ambayo mara nyingi huanzia utotoni hadi anapofika utu
uzima ambapo safari hii inaweza kuwa ya kikweli pale nguli anajizatiti kukisaka
kitu au kujisaka mwenyewe.
Katika nadharia ya vikale, mkinzani wa nguli
huwa ni mhusika wa kikale ambaye hujifunga kibwebwe kuiharibu mipango ya nguli
kwa kujaribu kumwangamiza. Aghalabu mhusika huyu huwa mzinzi, mlafi na wakati
mwingine huwa tajiri. Hii inaafikiana na sifa za Fomo Lyongo mhusika mkuu katika
mighani ya Fumo Lyongo.
Fomo Lyongo alizaliwa katika mji wa Shanga
kwenye himaya ya ufalme wa Pate uliokuwa chini ya utawala wa Mfalme Mringwari.
Katika ubarobaro wake Fomo Lyongo
alionekana kuwa na sifa za nguvu zake, ushujaa wake katika vita, uhodari wake
katika kufuma kwa mishale, umalenga wake katika kuimba na uashairi, na umanju
wake katika kucheza ngoma na kutumbuiza watu. Kwa hakika sifa hizi zilienea
kama moto kwenye kituka kikavu swala ambalo lilimtia tumbo joto mfalme wa Pate
ambaye alianza kupinga njama ya kumwondoa uhai.
Katika vikale hutokea vishawishi chungu nzima
ambavyo hujengwa vizingiti ili nguli lengwa asiweze kutekeleza wajibu wake
kikamilifu. kwa hivyo katika hadithi ya Fumo Lyongo, wapo wengi waliodhihirisha
hili ili kumfanya Fumo Lyongo kutotimiza na kutekeleza mradi wake. Fomo Lyongo
alipohama mji wa Pate, alisakini kwenye mji wa Ozi ambao kwa wakati huo,Waozi
walikuwa wakishambuliwa na makabila mbalimbali. Kwa sababu ya nguvu zake, Fomo
Lyongo alifanywa Kiongozi wao. Hili lilimzidishia jakamoyo mfalme wa Pate.
Mfalme Mringwari alifanya njama ya kumuua
Fumo Lyongo akitumia mashujaa wakali wa kabila la Wagala.Wagala walifululiza
hadi mji wa Ozi wakiwa na nia ya kumwangamiza Fumo Lyongo ingawa walipowasili
walifahamishwa kuwa hakuwepo wakati huo kwa vile huwa yeye huenda mawindoni na
kurudi siku ya pili baadaye. Hata hivyo mashujaa wa Wagala walitulia na
kumsubiri hadi wampate na kumwangamiza. Kwa kweli vikale huwa na nguli mbao
huyatenda mambo yasiyo ya kawaida.Fumo Lyongo alipotoka mawindoni, alipuliza
panda yake.Kwa mshangao Wagala hao walitanabahi kuwa zile panda zote mbili
alizozipulizwa, zilipasuka.Hali hii iliwaingiza mugma wa hali ya juu kwa kuhofu
namna Fumo Lyongo alivyokuwa na nguvu kiasi hicho. Hofu iliwaingia na kuondoka
bila kwaheri jinsi walivyoingia bila hodi wala karibu.
Kwa kweli vikale kwa ujenzi wake huwa na
mhusika mmoja ambaye huiongoza njama ya kuyawekea mitego na viunzi matendo ya
wahusika wakuu ambao huwa nguli. Kwa hivyo mfalme wa Pate hakufa
moyo.Aliwakabidhi Wasanye na Wadahalo wanamoishi msituni kumwuua pindi aendapo kuwinda.
Njama yao iliteguka. Mahasidi hawa walimwita
Fumo Lyongo kwenye karamu ya kikao. Kila
mmoja alihitajika kuchuma makoma ambayo
yataliwa kwenye kikoa. Mtego wao ulikuwa
eti pindi tu Fumo Lyongo apandapo kuchuma makoma, ndipo wangemwangamiza.
Hata hivyo Fumo Lyongo kwa weledi na uhodari wake, kwa kutumia weledi wake wa
kufuma, alifuma na kuangusha fungu zima la makoma. Hilo liliwafanya Wasanye
kuwa na hofu na kukosa tumaini la kumwangamiza.
Ila za mfalme wa Pate hazikukoma kama koma
zilizokoma kurudi kwenye mkoma.Aliwaarifu Wasenye wamwalike Fumo Lyongo kwenye ngoma ya mdundo wa gungu ambayo aliipenda sana. Hii ndiyo hila
iliyofaulu kwa kuwa Fumo Lyongo hakuweza kustahimili mawimbi ya mdundo huo. Hii
ilikuwa nafasi murua na mwafaka ya
kutekeleza unyama wao ambapo walimtia nguvuni kwa Kufungwa kwa pingu na
silisili hadi gerezani Pate.
Katika nadharia hii ya vikale , hutokea
mhusika mmoja mwenye hekima ambaye hutumiwa kumwasa nguli.Katika hadithi hii,
kuna binti mjakazi kwa jina Saada ambaye
kila mara alitayarishiwa mkate na kumpelekea Fumo Lyongo akiwa gerezani.
Alipopata habari kuwa angeuawa ingawa kabla ya hapo aombe lolote ambalo
angetaka.Kwake aliomba apewe nafasi ya kuwatumbuiza wageni katika harusi ya
nduguye.
Kwa ujanja wake, Fumo Lyongo alimpa mjakazi
ujumbe kwa wimbo wa kuandaliwa mkate kisha awekewe ndani tupa ya kukerezea
minyororo. Alipofanya hivyo akiwa kwenye gungu watu walishangaa kuona kuwa Fumo
Lyongo akiwa huru Huria. Alitoroka kutoka hapo hadi akafika Ozi.
Katika nadharia ya vikale hutokea mhusika
mmoja ambaye huwa na ukuruba wa karibu na nguli na yuyo huyo ndiye atumiwaye
kumwangamiza. Mhusika huyu huwa mwenye wingi wa ubinafsi wa kujitakia makuu.
Hata hivyo wanaomhadaa huelekea kwenye mtindo wake wa maisha huku wakimpa ahadi
chungu nzima kwa kutekeleza maangamizi ya nguli.
Kwenye hadithi hii mwanawe Fumo Lyongo
aliyekuwa na usuhuba na binti mmoja kutoka Pate ndiye aliyetumiwa kutia babaye
hatarini. Alipewa ahadi kuwa iwapo angemwua babaye basi angeozwa yule binti
kutoka Pate ambaye alimtaka. Kijana huyo aliwatobolea siri ya ushujaa wa Fumo
Lyongo kuwa akitiwa tu sindano kwenye kitovu, basi huo huwa mwisho wake wa
kuishi.
Kijana huyo kwa ujanja na hila zake alimdunga
Fumo Lyongo kitovuni. Fumo Lyongo aliondoka na maumivu hadi mtoni ambapo
alifia. Kikawa kilio mjini Ozi
huku mfalme wa Pate akiwa na sherehe kisirisiri.
Katika
kazi hii nitatumia mtazamo wa mtaalamu Gustav Jung kwa kumuonyesha hadithi hii anavyomsawiri Fumo Lyongo katika safari ya
kuijenga jamii adilifu kuonyesha maudhui ya wema na uovu na jinsi mhusika huyu
anavyopambana na vipingamizi kutoka kwa wakinzani wake, Mfalme Mringwari wa Pate. Haya yote ni katika kudhihirisha
kuwa fasihi simulizi ni picha kongwe za fasihi zinazotokea mara kwa mara katika
jamii zetu.
Hitimisho
Kazi hii inatalii kwa muhtasari maisha na wasifu Fumo Lyongo wa
Ozi. Ni muhimu kutaja kuwa makala haya yametuwezesha kumulika na kuelewa wasifu
wa Kiongozi huyu aliyekuwa mashuhuri. Kupitia kazi hii, tumedhihirisha kwamba vikale
ni tukio la kihistoria. Hadithi ya Fumo
Lyongo ni dhihirisho tosha kuwa nguli na majagina ni wahusika ambao kwa njia
moja ama nyingine hupimana nguvu, maarifa na uwezo katika jamii zetu.Waaidha
makala haya yanadhihirisha kuwa ni
muhali kuitenga jamii na historia.
Kwa hivyo ili kuyaelewa haya fika si jingine ilakuzama katika
nadharia ya vikale inayotupa mwongozo na kioo thabiti cha kuyachanganua haya
yote.
Marejeleo
Kiswahili kwa kidato cha pili(Toleo
Jipya)-2005-Uk.60-64, KLB, Nairobi
Aristotle(1965).“Poetics”,Classical
Literary Criticism. Harmondsworth:
Penguin.
Bakhtin, Mikhail (1989). The Dialogic Imagination. Austin: University of Texas Press.
Blamires, Harry (1995).A
History of Literary Criticism.London: Macmillan.
Cuddon, J.A. (1977). A
Dictionary of Literary Terms.Oxford: Blackwell.
Daiches, David (1981). Critical
Approaches to Literature.London: Longman..
Dundes, Alan (1965). The Study of Folklore. NJ: Prentice Hall, Inc.
Eagleton, Terry (1983). Literary Theory: An Introduction. Oxford: Blackwell.
Esslin, Martin. The Theatre of the Absurd. London: Methuen.
Feud, Sigmund (1950). The Interpretation of Dreams.
Harland, Richard (1999). Literary Theory: From Plato to Barthes. New York: St. Martins.
Kimani Njogu et.al.
(1999). Ufundishaji wa Fasihi:
Nadharia na Mbinu. Nairobi: Jomo
Kenyatta.
Lord, Albert (1960). The Singer of Tales. Cambridge: Harvard University Press.
Murfin, Ross ed. (1991). The Case Studies in Contemporary Criticism. New York: St. Martins Press.
Musau, Paul (1985). Kezilahabi: Mwandishi Aliyekata Tamaa. Tasnifu, M.A.
Chuo Kikuu cha Nairobi.
Ngugi wa Thiong’o (1986). Decolonising The Mind. London: HEB.
Scholes, Robert (1974). Structuralism in Literature. New Haven: Yale University Press.
Wafula, R.M.& Kimani Njogu
(2007). Nadharia za Uhakiki wa Fasihi. Nairobi: Jomo Kenyatta Foundation.
Wafula, R.M. (1999). Uhakiki wa Tamthilia: Historia na
Maendeleo Yake. Nairobi: Jomo Kenyatta Foundation.
Wamitila, K.W. (2003). Kamusi ya Fasihi: Istilahi na Nadharia. Nairobi: Focus Books.
Wamitila, K.W. (2002).
Uhakiki wa Fasihi.
Nairobi: Phoenix.
Zirimu, Pio ed.(1971). Black Aesthetics. Nairobi: Kenya Literature Bureau.
Abrams, M.H. "Archetypal Criticism. (1999)" A
Glossary of Literary Terms. 7th ed. Fort Worth: Harcourt Brace College
Publishers.
Biddle,
Arthur W., and Toby Fulwiler(1989). Reading, Writing, and the Study of
Literature. NY: Random House.
Lynn, Steven(1998). Texts and Contexts:
Writing About Literature with Critical Theory. 2nd ed. NY: Longman.
Murfin, Ross, and Supryia M. Ray.(1997) The
Bedford Glossary of Critical and Literary Terms. Boston: Bedford Books.
Walker, Steven F. Jung and the Jungians
on Myth. NY(2002): Routledge.