FASIHI SIMULIZI INAO UKONGWE
NA PIA USASA. JADILI.
a. Ukongwe
katika fasihi simulizi.
Fasihi
simulizi ni aina ya fasihi ambayo inaaminika kuwa kongwe zaidi kuliko fasihi andishi.
Fasihi hii ilizuka tu pindi mwanadamu alipoanza kuongea. Hata hivyo upo wakati
ambapo fasihi simulizi ilidharauliwa mno. Hali hii ilitokea tangu kutawala kwa fasihi andishi
Ulaya, Asia na kutumiwa na wenye nguvu za kisiasa na kiuchumi, fasihi simulizi
ilidharauliwa ikatwezwa, ikadunishwa na kushushwa hadhi huku fasihi andishi
ikitukuzwa na kuendelezwa.
Taaluma ya fasihi simulizi hivi
leo inashughulikiwa kwa nguvu nyingi ili kuondokana na fikra duni zilizorithiwa
toka kwa wataalamu wa kigeni kuwa sanaa kongwe ya fasihi simulizi ni ya
kishenzi. Pamoja na dharau juu ya fasihi simulizi bado ukweli unabaki kuwa
sanaa hii ndiyo ghala halisi la fasihi andishi.
Hata sasa imebainika kuwa tenzi za
Kigiriki zinazodaiwa kutungwa na manju aitwaye “Home” hazikuwa zimeandikwa kwa
zaidi ya miaka mia tano (500) ndipo baadaye zikaja kuhifadhiwa katika
maandishi. Hivi majuzi pia wanateknolojia wameanza kukubali kuwa sehemu kubwa
ya Biblia ni fasihi simulizi ya Wayahudi walioishi zama mbalimbali. Wanazidi
kueleza kuwa imebainika kuwa fasihi hiyo haikutoka mbinguni bali mizizi yake ni
katika jamii ya Wasumuri (Mesopotamia), Waajemi na Wagiriki. Hoja ya msingi ni
kuwa fasihi andishi haijaibua dhamira mpya, zote ni zile zile ambazo zilijitokeza
katika masimulizi. Mfano: Mapenzi, siasa, unyonge wa wanawake, ukombozi, uchawi
na ushirikina, uzazi, ndoa na migogoro ya kitabaka. Misemo ya fasihi simulizi
haijapitwa na fasihi andishi wala fani yake haijabadilika mpaka leo.
Kwa
yakini ukongwe wa fasihi simulizi unaanzia pale sanaa hii ilikuwa ni sanaa ambayo imejengwa katika mfumo
uliozoeleka wa kufikisha ujumbe kwa hadhira, mfumo uliolenga zaidi katika kurithishana
mila, desturi na utamaduni kutoka kizazi kimoja hadi kingine.
Hii
ina maana kurithishana mila, desturi na tamaduni kutoka kizazi cha kale (babu,
bibi na wengineo wa umri wao) kwa kukifundisha kwa kukirithisha kizazi kipya
(ambacho ni watoto na wajukuu zao). Katika utoaji wa sanaa hii ni lazima pande
zote mbili ziwepo.Hili lina maana kuwa ukale na utamaduni bado umo na utazidi
kujitikeza katika fasihi simulizi.
Fasihi
hii ilirithishwa kutoka kizazi kimoja kwenda kingine kupitia katika nyimbo,
hadithi, ngoma, mashairi ya zamani (malenga), na hata michezo ya ujasiri na
majigambo.Tanzu hizi bado zipo hadi sasa ishara kuwa usuli wake wa ukongwe bado
unahimilika.
Katika
kuiwasilisha fasihi hii ni lazima kuwepo na pande mbili za mawasiliano
(majadiliano) yaani fanani (anayerithisha, msimuliaji) na Hadhira
(anayerithishwa, msimuliwaji). Fanani hujitahidi kutumia mbinu mbalimbali
kuijenga kazi yake ili iweze kuvutia hadhira.
Uhusiano
wake hujitokeza anapotumia viungo vyake vya mwili katika kujenga kazi yake.Lengo
la fanani kutumia viungo hivyo ni kuwa anataka kuyakamilisha maadili yatokanayo
na kazi yake. Msimuliaji anapochukua nafasi ya wahusika, mfano endapo kuna
wimbo ndani ya hadithi na makofi, au ishara fulani ya kutumia viungo vya mwili;
msimuliaji anapoimba na kupiga ma- kofi, hapo anakuwa msimuliaji wa wakati
huohuo pia ni mhusika mshiriki. Lazima ikumbukwe kwamba, fanani siku zote
huanzisha majadiliano au mafundisho na Hadhira lazima iwe na uwezo wa kupokea
na kuihifadhi majadiliano au mafundisho.
Ukongwe
wa fasihi simulizi waaidha imo katika mbinu za kuhifadhi. Hapo zama za zama fasihi
simulizi ilikuwa ikihifadhiwa kichwani. Ilihifadhiwa humo kwa muda mrefu kiasi
kwamba baada ya muda ilibidi ipatiwe kizazi kingine na kingine. Ingawaje katika
kukipatia kizazi kingine yale yaliyokuwapo sio yote ambayo yalifikishwa kwa
kizazi kipya, bali yaliyofikishwa yalikiwezesha kizazi kipya kufahamu
yaliyotokea na kutendeka hapo zamani.Hii pia ipo hadi sana ingawa kwa kiasi
fulani, maendeleo na maenezi ya sayansi na teknolojia yameivamia fasihi hii
katika viwango mbalimbali.
Urathi
vile vile eni swala ambalo lina mashiko makubwa katika fasihi simulizi. Hivyo
basi, mmiliki wa fasihi simulizi katika kipindi na wakati huo wazama alikuwa ni
mwana jamii na fasihi hii ilikuwa ni mali ya jamii. Fasihi simulizi ya zamani
ilikuwa na mvuto wa aina yake, ambapo kukosea au kwenda kinyume na maadili ya
jamii ilikuwa si rahisi kwa sababu jamii ilikuwa pamoja kwa muda mwingi.
Kupitia kwa huyo mwana jamii mmoja aneweza kufahamu mengi mno kuhusiana na
jamii husika.
Baada
ya mwingilio wa wageni toka pande mbalimbali za dunia, fasihi simulizi ilianza
kubadilika kutokana na kuingizwa kwa mila, desturi na tamaduni toka kwa wageni
hawa. Ama kwa hakika wageni hawa walifanikiwa kwa kiasi kikubwa kuathiri fasihi
simulizi na kuipa mkondo mpya. Jamii iliyapokea mafanikio ya wakoloni
yaliyodhihirika wakati wanajamii wenyewe walipoamini kwamba amali walizokuwa
nazo hazikuwa na maana kama zile walizoletewa na wageni au wakoloni hawa. Jamii
iliamini kwamba amali hizo hawakuwa nazo, na kama walikuwa nazo, basi hazikuwa
na maana kama zile walizoletewa.
Kwa
mfano wakati jamii ilifurahia kuburudishwa na kuburudika kwa kutumia simulizi
zilizotolewa jioni kwa pamoja mbele ya nuru ya mbalamwezi, kuingia kwa wageni
hawa kumesababisha kuwepo kwa fasihi simulizi nyingine ambayo kwa kiasi kikubwa
kumeadhiri starehe hiyo. Kadhalika wageni hawa wamechangia sana kuingia kwa
maendeleo ya kisayansi na teknolojia ambayo yameanza kuiingiza jamii yetu
katika fasihi ya televisheni, kompyuta redio na video ambayo kwa kiasi kikubwa
imefifisha starehe iliyokuwa ikipatikana hapo awali. Amali hizi mpya kama
televisheni, kompyuta, redio na video ndizo zinazotumika kuiwasilisha fasihi
simulizi ya kisasa na ambazo tutaziangalia uwepo wake na athari zake katika jamii.
b.
Usasa wa fasihi simulizi.
Usasa
ama uleo wa fasihi simulizi unagubikwa na swala zima la makuzi na maendeleo ya
Teknolojia. Tunapozungumzia juu ya Teknolojia ni lazima tuhusishe na Sayansi,
ambapo tunapozungumzia juu ya teknolojia tunayazungumzia maendeleo ya
Kisayansi. Kwa hivyo basi Sayansi na Teknolojia ni vitu viwili vinavyokwenda
sambamba na pamoja bila ya kuachana. Bali, teknolojia ni maendeleo ya kisayansi
katika hatua ya mwisho kabisa ambayo inaonekana. Historia inaonyesha kwamba
nchi zote ambazo zimeendelea, maendeleo yake yametokana na Sayansi na
Teknolojia.
Tunatumia
teknolojia katika maisha yetu ya kila siku; mfano nyumba, mawasiliano, mwanga n.k. Halikadhalika tunatumia
teknolojia kwa matumizi mengi ya kila siku, kupikia, kuwasilia- na,
kutembeleana na mambo mengine yanayofanana na hayo.
Tunapozungumzia
juu ya Teknolojia mpya, tunamaanisha maendeleo zaidi katika Sayansi na
Teknolojia. Na tunapozungumzia juu ya Usasa katika fasihi simulizi,
tunazungumzia jinsi ambavyo tunaweza kuitumia teknolojia mpya katika
kuihifadhi, kuiwakilisha, kuikosoa, kuburudisha na hata kuichangia mada fasihi
simulizi. Na hayo yote yanawezekana kupitia televisheni, kompyuta, mikanda ya
video, mikanda ya CD, barua pepe, simu za mkononi, setelaiti n.k. Labda hapa
niweke wazi ya kuwa nitakachokieleza manufaa ya teknolojia mpya kwa fasihi
simulizi na kwa jamii nzima kwa ujumla.
Kwanza,
katika kuiwakilisha fasihi simulizi kwa watu wengi walio mbali na fanani, kwani
hii ni fasihi ambayo uwasilishaji wake si lazima wahusika wote wawili wawepo
yaani fanani na Hadhira. Hadhira inaweza kuwepo lakini fanani asiwepo na nafasi
yake ikachukuliwa na utaalamu wa kisasa unaotokana na teknolojia mpya. Hili
hufanyika kupitia mikanda ya video na ya CD, kupitia tarakilishi, barua pepe,
radio, setelaiti,vipata-ninga n.k. Kwa ujumla hapa teknolojia mpya inatumika
kama kihifadhi cha fasihi simulizi ili kuweza kufikisha ujumbe.
Pili,
katika kuihifadhi fasihi simulizi ili vizazi vingine viweze kuirithi, nyanja
hii ya fasihi hu- tumia vyombo vya kisasa kabisa vya kuhifadhia kama mikanda ya
video, DVD, tepurekoda na utepe wake, tarakilishi,vipakatalishi,tarakiba(tab)
,rununu za kisasa(Smart phones) kadi sakima (memory card), diski mweko(flash
disk), CD mtandao wa You tube n.k. Hivi vyote vimeirahisisha shughuli nzima ya
kuhifadhi kazi mbalimbali za fasihi simulizi. Kwa kweli mbinu asilia ya
kuhifadhi fasihi simulizi inao udhaifu wake chungu nzima. Baadhi ya udhaifu huu
ni pamoja na swala la kusahau baadhi ya
sehemu za tanzu husika kwa kuwa binadamu katika kusahau si ajabu,baadhi ya
tanzu hubadilika badilika wakati hasa fanani anapowasilisha kwa kutumia maneno
mbadala na cha ajabu mno ni kule kufariki kwa aliyehifadhi fasihi hii kwa kichwa
ishara kuwa yale yote yaliyokuwa kichwani mwake nayo pia hayapo.
Tatu,
katika kuchangia mada, teknolojia mpya inatumika kama kiunganishi kati ya
fanani na hadhira, ambapo mfano mzuri katika eneo hili ni matumizi ya
setelaiti. Aidha setelaiti yaweza kutumika kuiwasilisha kazi ya fasihi simulizi
kwa hadhira iliyo mbali na fanani kama alivyofanya aliyekuwa raisi wa Marekani
Bill Clinton alipokuwa akichangia mawazo yake ili kuwezesha kupatikana kwa
suluhisho la mgogoro baina ya nchi za Rwanda na Burundi. Raisi huyu alichangia
moja kwa moja akiwa Marekani wakati mkutano wa suluhu ulikuwa ukifanyikia Arusha.
Rais huyu alionekana kwenye setelaiti akizungumzia mtazamo wake kuhusu mgogoro
huo. Vile vile vyombo vya habari huwa na sehemu fulani ambapo vituo hivi huweza
kutumia mtandao maarufu wa SKYPE kuwasiliana moja kwa moja na mtangazaji aliye
kwenye studio. Hii hujitokeza katika idhaa ya KTN, Citizen, NTV, K24 n.k.
Nne,
katika kukosoa jamii hii hufanyika
kupitia televisheni, video hasa kwenye michezo ya kuigiza (Tamthilia) kupitia
video na televisheni wasanii huikosoa jamii pale inapokuwa aidha imekosea au
imepotoka, hivyo jamii inapata mafunzo kupitia teknolojia mpya. Tamthilia
inaweza kuwa inachezwa na watu kutoka nchi nyingine kwa mfano Nigeria,Tanzania,
Uingereza lakini kwa kuwa matatizo ya kijamii hufanana basi mchezo huo unaweza
kutoa mafunzo kwa jamii mbalimbali duniani.Mifano mizuri ya idhaa hizi ni
TeleMundo, Zee World,Holly wood n.k Idhaa hizi zimeiteka jamii bakunja
kuhusiana na vipindi vyake babu-kubwa vilivyo na maudhui pana ya jamii.Hii ni
pamoja na kikosi maarufu nchini Kenya ambacho kimejitokeza kuigiza michezo
mabalimbali ikiwa pamoja na tamthilia teule zinazotahiniwa katika shule za
upili nchini.
Tano,
katika kuburudisha, hapa jamii inaburudishwa na vipindi mbalimbali vya kijamii
katika tamthilia, muziki ngoma n.k. kupitia runinga, video, tarakilishi, pata-ninga-DVD
n.k. Hapa Kenya vipo vipindi ainati vya burudani kama Kipindi cha muziki kiitwacho
“Roga roga” kwenye Radio Citizen kila wikendi na Fred Obachi Machoka, “Mseto
East Afrika” kwenye runinga ya Citizen na Mzazi Willy M. Tuva,kipindi cha
Mzooka kwenye Maisha Magic Swahili ambacho hucheza miziki hasa ya kizazi kipya
ya kuruka majoka(ngoma za rapu).
Sita,
katika kuipa jamii tumaini la maisha. Aghalabu hii hujitokeza katika vipindi
mbalimbali vya kidini (kikristo na kiislamu) ambavyo vimezagaa katika idhaa
mbalimbali ima redio runinga au setilaiti. Mifano mizuri ni vipindi chungu nzima
vya wahubiri mashuhuri hapa nchini
Kenya: James Maina ng’ang’a(Neno Everngelism Centre), Mark Kariuki(Life Celebration Centre),
Pius Muiru(Kuna Nuru Gizani), Mhubiri. Peter
Manyuru (JTM), Dr. Prophet Owuor (Ministry of Repentance and Holiness) na wengine
wengi ambapo wana vipindi chekwa katika idhaa mbalimbali za hapa nchini Kenya.
Mbali na hawa pia kuna wale wa kimataifa ambao pia jamii huwapata moja kwa moja
kupitia vitandazi tofauti tofauti. Bila kusahau kipindi maalumu cha Ukumbi wa
Kiislamu katika runinga ya KBC pamoja na idhaa maalum ya kiislamu kwenye
ving’amuzi mbalimbali.
Aidha
kwa upande mwingine mabadiliko haya ambayo yameigeuza dunia kuwa ndogo na ndogo
kila kukicha, yameonesha kwamba udogo huu wa dunia unaotokana na teknolojia
mpya ya mawasiliano, ambayo imekuwa ya kisasa zaidi. Teknolojia hii ndiyo
iliyozaa dhana mpya ya fasihi simulizi ya kileo iliyochukua nafasi ya dhana
iliyoitangulia ya fasihi simulizi
ya zamani. Kwa mtazamo wa juu zaidi twaweza kusema kuwa ni fasihi ambayo watu
wa kizazi hiki wanaiita kuwa ni fasihi inayokwenda na wakati, fasihi ya kisasa
au fasihi iliyokwenda shule.
Wataalamu
wengi wa intaneti wamefungua tovuti mama kwa nia ya kuharakisha mawasiliano
duniani. Wanafunzi wengi sana wamejifunza kutumia kompyuta na kwa kupitia
teknolojia hii wamekuwa wakipata elimu ya mbali kwa gharama nafuu. Teknolojia
ya setelaiti, intaneti imekuwa ikitumika ili kuboresha elimu ya juu na kupiga
hatua ya maendeleo ya sayansi na teknolojia. Aidha televisheni, video, mitambo
ya setelaiti na ving’amuzi vimekuwa vikitoa misaada inayojumuisha mafunzo
makini ya kuwasaidia walimu kuboresha taaluma zao. Walimu na wanafunzi
waliokuwa katika hali ya kukata tamaa juu ya namna ya kuimarisha ufundishaji,
wameanza kubaini matunda ya mpango huu wa kutoa elimu kwa kutumia teknolojia
hii. Japo kuwa katika mpango huu vifaa ni haba, shule na vyuo vinaendelea
kujitahidi kuongeza ufanisi wa ufundishaji wake pamoja na kuimarisha jamii
watokako wasomaji. Hatua hii hapana shaka itasaidia sana katika kuongeza
viwango vya wanafunzi kufaulu.
Kwa
upande mwingine tumeona kwamba maendeleo haya ya programu za tarakilishi yameikuza
elimu ya sayansi na teknolojia kwa kiasi kwamba hata madaktari bingwa wa
upasuaji wa magonjwa ya moyo wamekiri kuwa inafaa. Aidha kwa mujibu wa maelezo
yaliyotolewa na mwandishi wa gazeti la Mtanzania la tarehe 13.06.03 ukurasa wa
9 ambapo mwandishi ambaye jina lake halikutajwa aliinukuu makala iliyochapishwa
katika gazeti la Uingereza Sunday
Times Kwa mujibu wa makala hiyo, mwandishi ametuelezea jinsi elimu ya sayansi
na teknolojia inavyotufikisha mbali akiwa anatumia mfano wa programu ya
kompyuta iliyovumbuliwa na wataalamu huko Uingereza inayoweza kuwaamba mabingwa
wa upasuaji iwapo inafaa kumfanyia upasuaji mgonjwa wa moyo.
Kwa
kuangalia maendeleo hayo ya kasi ya teknolojia ya mawasiliano na kuzingatia
ukweli uliojitokeza kwamba dunia ni mahali pa ujirani, kuna aina fulani ya
kukaribiana kwa watu kupitia hizo njia mpya na za kisasa zaidi za mawasiliano.
Kama
tulivyokwishaona, hivi sasa dunia hususan, nchi za dunia ya tatu kama Kenya,
Uganda, Tanzania na nyingine nyingi tumeikubali kwa hiari yetu wenyewe na
kuipokea aina hii mpya ya fasihi simulizi. Aidha katika kuikubali huku,
kumetokea na kumekuwepo na vituo vingi vya mitandao ya kielektroniki ambapo
vijana wanapoteza muda mwingi sana kuwasiliana na vijana wenzao duniani,
wanabadilishana mawazo na kuelimishana
mambo mengi sana yanayowahusu vijana hao.
c)
Athari hasi za teknolojia mpya katika fasihi
simulizi
Hakuna
jambo zuri linalotokea duniani bila ya kupatikana kwa ubaya wake.Hoja hii ina
mshabaha na methali isemayo: “Hakuna masika yasiyokuwa na mbu” Mafanikio haya
ya kisayansi na teknolojia mpya, yameleta athari kubwa sana katika fasihi
simulizi, hususan katika utamaduni, mila na desturi zetu. Amali hii ambayo ni
utajiri mkubwa wa taifa lolote lile ni
muhimu sana katika nchi.
Teknolojia
mpya ni utamaduni mpya kutoka nchi za Ulaya na Marekani zilizoendelea, ambazo
zina utamaduni wenye nguvu ukilinganisha na tamaduni za Kiafrika ambazo ni
dhaifu kimataifa. Kwa hivyo, kutokana na utandawazi tunalazimika kuonyesha
vipindi vingi vya Tamthilia vya nje ya nchi kuliko vya ndani ya nchi. Mfano
tamthilia nyingi za kigeni kama Egoli, The Bold & The Beautiful, Days of Our Life, La Mujer de mi Vida (Woman of My Life), Isindingo, n.k. zinaonyeshwa na
Televisheni zetu za hapa nyumbani kama KTN,CITIZEN,K24 n.k
Teknolojia
mpya inaenda sambamba na utandawazi ambao ndani yake kuna udhalilishwaji wa
nchi za ulimwengu wa tatu kama Tanzania, Uganda, Kenya na nchi nyingi nyingine
zipatikanazo hasa katika bara la Afrika. Kwa hali hiyo utakuta kuwa nafasi ya
fasihi simulizi ya nchi zinazoendelea kama Tanzania katika teknolojia ni finyu
sana katika kujitangaza.
Matumizi
ya zana za kisasa katika muziki wa dansi, hususan Bongo Flava yanachangia kwa
kiasi kikubwa kupunguza ladha halisi ya kitamaduni ambayo ingepatikana kama
ngoma, marimba, vinubi, matoazi na ala nyingine zingetumika. Aidha kwa kutumia
fasihi simulizi ya kileo kumezuka lugha za namna nyingi katika jamii zetu.
Lugha hizi zimetokana aidha na filamu jamii inazoziangalia katika vipindi vyetu
vya televisheni. Kumekuwepo na misuguano kadhaa kati ya watu wa bara na watu wa
pwani hususan wa Mombasa hapa Kenya kuhusu lugha za mitaani zinazotumika katika
televisheni zetu ambazo wakenya wenzao wa bara wanashindwa kukubali kwani
baadhi ya misamiati hiyo haipo katika misamiati ya Wakenya wenzao. Kwa mfano baadhi
ya msamiati anaoutumiwa na watangazaji kama Baya Kitsao wa Radio Rahma Mombasa:
filfi-nyange. au msamiati aliokuwa akitumia mwendazake Profesa Ahmed Sheikh
Nabahany na wengine wengi
Halikadhalika
kumekuwa na wimbi kubwa la wanajamii pamoja na mashabiki wanaoshabikia filamu
na maonyesho mengi yanayoonyeshwa katika televisheni na kumbi zetu za starehe.
Filamu hizi na maonyesho haya yanatuonyesha mila, desturi na itikadi za jamii
husika. Kwa mfano maonyesho ya Filamu za Zee Word, Telemondo,Televisa na
nyinginezo nyingi za Kimarekani, Kinaijiria, Kighana, Kikongo, Kihindi na
nyinginezo nyingi. Mapokeo ya filamu hizi kwa jamii ya Kikenya ni yale ya kupata
na kujua tamaduni za wenzetu hawa. Katika kupata na kuiga tamaduni hizo za
wenzetu, ni dhahiri kwamba kunabadilisha mwenendo na mwelekeo wa taifa kisiasa,
kijamii, kiutamaduni, kisaikolojia na kiitikadi. Mabadiliko haya yanaweza
kuibadilisha jamii hususan vijana wa marika yote katika kuiga tamaduni, mila na
desturi za mataifa mbalimbali.
Aidha
maneno yanayotumika katika nyimbo zinazoimbwa na wasanii wanaoshiriki kucheza
filamu mbalimbali hayasikiki vizuri, lugha wanayoitumia haiendani na maadili ya
mila na desturi za Kikenya. Nyimbo nyingine hazina mafunzo mazuri katika
muktadha wa jamii ya Kenya. Wengi wa wanamuziki wanajitangazia tu umaarufu wao
pasipokujua kuwa wanatakiwa kuutangaza utamaduni wa Kiafrika. Midundo
wanayoipiga na mitindo wanayoicheza haionyeshi utamaduni wa Mwafrika bali
inamdhalilisha Mwafrika kwa kuonyesha namna
jinsia moja inavyodhalilishwa.
Hii
ina maana kwamba mdhalilishwaji wa kwanza katika nyimbo, filamu au maigizo
tunayoyaonyeshwa aidha katika runinga zetu au tunazozisikia katika vipindi vya
redio daima ni mwanamke. Zaidi ya hayo, yote tusikiayo na tuonyeshwayo yanalengwa
katika utamaduni wa magharibi zaidi kuliko utamaduni wa Kikenya au wa Kiafrika
kwa ujumla. Matamasha yanayotumiwa na wasanii wetu sio yale ya kuinua vipaji
vyao kisanii bali ni ya kuiga mila na desturi za Mataifa ya wenzetu na wala sio
za kwetu. Hii imewasababisha wasanii
wengi
kudumaa na kuona kuwa hakuna haja ya kubuni na kujifunza dhana nyingine.
Fasihi
simulizi ya kileo si mali ya jamii. Hii ni mali ya wachache kwani inapotolewa
kupitia vikundi vya sanaa na utamaduni ni lazima watu walipe ili waweze
kuishuhudia. Kwa hiyo imekuwa ni biashara kuliko hali halisi.Mfano mzuri ni
kile kipindi maarufu hapa Kenya cha vichekesho cha Churchill Show ambapo lazima
watu walipe ndipo wachekeshwe. Mbali na hapo pia wapo wanamuziki chungu nzima
ambao huwa na tabia ya kuchapa muziki kwa malipo katika sehemu mbalimbali.
Ifahamike kuwa wasanii hawa wana hati-miliki ya kazi yao na iwapo yeyote
amgependa kuitumia, hana budi kupewa ruhusa nao kwa maandishi la sivyo kuna
uwezekano wake mkubwa wa kujikita taabani.
d)
Athari
chanya za teknolojia mpya katika fasihi
simulizi.
Teknolojia
mpya ni njia ya kisasa zaidi katika kuhifadhi fasihi simulizi ili kutunza
kumbukumbu. Kwa mfano historia ya zamani ya jamii kabla ya ukoloni kuhusu maisha ya mababu na
mabibi zetu inaweza ikarekodiwa kwenye mikanda na kusikilizwa na hadhira. Mfano
mzuri ni Filamu inayoonyesha juhudi za mapiganaji wa MAU MAU walipokuwa
wakitafuta kuikomboa Kenya kutoka mikononi mwa mkoloni.
Kwa
utashi huo ina maana kuwa teknolojia mpya ni utaalamu wa hali ya juu, hivyo
kazi zimekuwa za ubora wa hali ya juu. Teknolojia mpya ina faida nyingine
nyingi katika kukuza fasihi simulizi ya Kiswahili. Mfano katika jamii ya leo hasa taifa la Kenya kwa ujumla kuna vituo
vingi vya redio na televisheni ambavyo hurusha matangazo yake sehemu mbalimbali
hapa nchini Kenya na nje ya mipaka yake.
Kwa
kupitia vituo hivyo fasihi simulizi imeweza kuwafikia watu wengi ambao wako
mbali ambako matangazo hayo ya redio na
televisheni yanafika. Katika vituo mbalimbali vya runinga hapa nchini kuna vipindi mbalimbali vya watoto
ambapo hadithi, vitendawili, methali, mafumbo husimuliwa kwa watoto walioko
pale studio na wengineo ambao huyapata matangazo hayo kupitia sehemu walizopo.
Katika idhaa ya redio ya Radio Salaam kuna kipindi cha watoto kila siku ya Jumamosi
saa tatu asubuhi.
Kule
nchini Tanzania siku ya Jumapili saa
tisa alasiri kuna kipindi cha mgongano wa mawazo ambapo fasihi ya Kiswahili
husimuliwa kwa jamii hasa fasihi ya vitabu ambapo huwa kuna mjadala kuhusu mada
mbalimbali za kifasihi na huendeshwa na wanafunzi chini ya usimamizi wa walimu wao.
Hapa
nchini Kenya kulikuwa na kipindi cha Kamusi ya Changamka kwenye NTV kikiongozwa
na Nuhu Bakari na Mnene Nyaga, katika runinga ya KBC kuna kipindi cha
mashindano ya mijadala kwa shule za upili ambacho hukuza vipawa vya ulumbi kati
ya wanafunzi wa shue za upili.
Kwa
upande wa redio nchini Tanzania vipo vipindi kadhaa katika Radio One Stereo,
ambapo baadhi yake ni kile cha watoto ambacho hurushwa kila siku ya Jumamosi
asubuhi, na kimekwishadumu kwa muda mrefu kikiwa kikiendeshwa na mtangazaji wa muda
mrefu wa redio nchini Tanzania, Julius Nyaisanga, ambaye katika kipindi hicho
cha watoto hujulikana kama Babu wa Kimanzichana. Kimanzichana ni moja ya sehemu
maarufu katika mkoa wa Pwani ambayo ipo kijijini. Radio Tanzania na Televisheni
ya Taifa nao hawako nyuma katika hilo. Nao pia wana vipindi mbalimbali kama
zilivyo redio na televisheni nyingine. Mfano mzuri redio Tanzania wana vipindi
kama “cheichei Shangazi” na “mama na mwana”, ambapo hadithi mbalimbali zenye
semi, mafumbo, methali na vitendawili husimuliwa.
Hapa
nchini Kenya idhaa mbalimbali za redio nazo zina vipindi mbalimbali ambavyo
huangazia maswala ya Kiswahili.Radio Maisha kuna kipindi cha Bahari ya Lugha
chini ya nahodha wake Hassan Mwana wa Ali (Mtoto wa Nyumbani) kila Jumamosi
asubuhi ambaye huwashirikisha wataalam mbalimbali wa Kiswahili wakiwa pamoja na
Ustadhi Guru Wallah bin Wallah, mwalimu Tsalwa na wengine wengi. Kwenye kipindi
hiki Mashairi hughaniwa, wanafunzi wakahojiwa na uchambuzi mbalimbali ukafanywa
pamoja na chemshabongo mbalimbali hasa kutoka kwa Guru Ustadh Wallah bin Wallah
ambaye pia huwa na hadithi za kuibua hisia za kutafakari ambazo huionya,
kuisifu na kuielekeza jamii ifaavyo.
Waaidha jijini Mombasa kuna idhaa ya Radio Rahma
ambayo huangazia kipindi cha Ndimi za Malenga kila Jumamosi saa nane hadi saa
kumi alasiri. Kipindi hiki huongozwa na Baya Kitsao pamoja na mwalimu Newton
Omukabe. Kwenye kipindi hiki, mambo mbalimbali huangaziwa yakiwa pamoja na ughani
na uchambuzi wa mashairi, uchambuzi wa vitabu mbalimbali vinavyotahiniwa katika
kidato cha nne na mengine mengi.Radio
rahma kwa upande wake jijini Mombasa, ina kipindi cha Ukwasi wa Lugha ambacho
pia huangazia fani mbalimbali za lugha huku wakishirikisha wataalamu mbalimbali
kutoka mwambao.
e)
Hitimisho
Fasihi
simulizi hapo zamani ilikuwa imekitwa
katika misingi mikuu miwili; moja, mila na de- sturi. Mbili, fasihi simulizi ya
kale ililenga kutoa huduma zaidi na si biashara. Fasihi hii inafikisha ujumbe
katika jamii ikiwa na lengo la kuelimisha, kuonya, kuburudisha na kukosoa.
Teknolojia
mpya katika fasihi simulizi ina faida na hasara kama tulivyobainisha. Fasihi
simulizi hii imekitwa katika misingi mikuu miwili. Moja, sayansi na teknolojia;
mbili, ni biashara. Fasihi hii inaua utamaduni wa jamii. Mfano watoto na vijana
wengi hivi sasa wanafurahia na kufahamu mambo mengi ya Ulaya, Amerika na
tamaduni zao kuliko tamaduni za jamii zetu za kiasili. Haya wanayafahamu
kupitia televisheni, video na intaneti. Fasihi simulizi ya kileo imekuwa ni
biashara zaidi kuliko kutoa elimu kwa jamii kama huduma ya kawaida. Hivyo kwa
kadri tunavyozidi kuwa karibu zaidi utandawazi na matumizi ya teknolojia mpya katika
maisha yetu ya kila siku, nchi za Kiafrika ni lazima ziwe bunifu kwa tamaduni
zao wenyewe ili kuepukana na hasara zinazopatikana kutokana na kuwepo kwa
teknolojia mpya.
Aidha
kwa upande wa vifaa, nchi nyingi za Kiafrika zimeshindwa kuagiza vifaa na
kutumia teknolojia mpya kutokana na sababu kwamba ni ghali sana. Hii
inahatarisha uchumi wa nchi hizi kwa kuzifanya ziwe tegemezi katika kuipata
teknolojia mpya. Teknolojia mpya ni nguzo muhimu sana katika maendeleo ya
fasihi simulizi si katika jamii ya Wakenya tu, bali ulimwenguni kwa ujumla. Hii ni kwa sababu
inawawezesha watu wengi zaidi kupata matangazo ya moja kwa na wakati mwingine
wao kushiriki kwa kupiga simu na kuchangia wanachopaswa kama ni kusimulia
hadithi, vitendawili, nyimbo, ngonjera n.k.
Lakini
wengi wanaofaidi huduma hii ni wale walioko mijini na katika vijiji vichache
ambapo matangazo ya redio na runinga yanafika na kwa bahati nzuri katika
dunia ya leo sehemu nyingi sana za
mijini na vijijini wanapata matangazo ya redio mbalimbali zilizopo nchini. Kwa
upande wa runinga zaidi ni mijini kuliko vijijini ndio wanaofaidi huduma hii
kwa kiwango kikubwa. Teknolojia mpya ina faida nyingine nyingi katika kukuza
fasihi simulizi ya Kiswahili. Mfano katika jamii hasa hapa nchini Kenya tuna
vituo vingi vya redio na televisheni ambavyo hurusha matangazo yake sehemu
mbalimbali nchini. Kupitia vituo hivi fasihi simulizi imeweza kuwafikia watu
wengi ambao wako mbali ambako matangazo hayo ya redio na televisheni yanawafikia.
Marejeleo
·
Gazeti la Mtanzania la tarehe 13.06.03.
·
Kimani N. 2006. Fasihi Simulizi na
Nadharia ya Fasihi ya Kiafrika, katika Fasihi ya Kiswahili. Nairo- bi: Twaweza
Communications. Uk. 1 – 10.
·
Kirumbi, P. S. 1975. Misingi ya Fasihi
Simulizi. Nairobi: Shungwaya Publishers.
·
Matteru, M. D. 1983. Fasihi Simulizi na
Uandishi wa Kiswahili, katika Fasihi: Makala za Semina ya Kimataifa ya
Waandishi wa Kiswahili. Dar es Salaam: TUKI. Uk. 26 – 37.
·
Mlacha, S. A. K. 1995. Fasihi Simulizi
na Usuli wa Historia ya Pemba. Katika: Lugha, Utamaduni na Fasihi Simulizi ya
Kiswahili. Dar es Salaam: TUKI/ITAA. Uk. 16-26.
·
Msokile, M. 1992. Kunga za Fasihi na
Lugha. Kibaha: EPD.
·
Wamitila K. W. 2003. Kamusi ya Fasihi:
Istilahi na Nadharia. Nairobi, Kenya: Focus Publications. Wamitila, K. W. 2003.
Kichocheo cha Fasihi: Simulizi na Fasihi. Nairobi, Kenya: Focus Publications.