Tuesday

ONTOROJIA YA KIBANTU- NADHARIA YA ONTOROJIA YA KIBANTU

0 comments


NADHARIA YA  ONTOLOJIA YA KIBANTU.


Nadharia ya Ontolojia ya Kibantu. Kuna wataalamu mbalimbali waliozungumzia nadharia hii. Kwa jumla, wataalamu hawa wameeleza maana ya Ontolojia kuwa ni mtazamo unaohusu kuwepo kwa kitu katika dunia na kuangalia vitu katika uhasilia wake (Nicholaus 2011).
Ontolojia inaweza kutazamwa kwa namna tatu: kama taaluma, kama falsafa na kama nadharia. Hivyo kwa kuwa utafiti huu ulichunguza “Mabadiliko ya kiuandishi kutoka kanuni za Ki-Aristotle kwenda kanuni za jadi ya Ki-Afrika”, kipengele cha Ontolojia ya Kibantu kinachoweza kutumika katika kazi za fasihi, tuliona ni vyema kutumia Ontolojia kama nadharia katika utafiti huu, kwani imewezesha utafiti huu kufikia malengo yake, pia ilihusiana na mada iliyoshugulikiwa.
Kimsingi kuna mitazamo minne kuhusu Ontolojia ya Kibantu. Mitazamo hiyo ni, ule wa falsafa ya kisiasa (Itikadi ya kisiasa), mtazamo au falsafa ya Kihikimati (Sagacty), wanafalsafa waliojikita katika kurekodi imani katika utamaduni wa mwafrika (Ethnofilosofia), na falsafa ya Kiuweledi.
Wanaitikadi wa kisiasa walichunguza masuala ya undugu wa kifamilia, ujamaa na kujitegemea ndani ya Afrika. Wanasiasa hao ni Julius Nyerere, Leopold Senghor na Kwame Nkurumah. Lengo lao lilikuwa ni kutaka kutafuta uhuru wa kweli kwa waafrika ili kurudisha heshima kwa mwafrika kama ingewezekana.
Mtazamo wa Kihikimati umejikita katika masuala ya uhuru, hekima na desturi za watu. Waanzilishi wa mtazamo huu wameshawishika kwamba falsafa ya kiafrika haiangalii vitu vyote vinavyohusu kazi. Lengo lao walitaka kuonesha kwamba ujinga sio hali ya kifalsafa na ujinga upo kwa kila jamii, ujinga wa mwenzako waweza kuwa uhuru kwake. Waanzilishi wa falsafa hii ni Odera H. Oruka na Marcel Griaule’s.Marcel Griaule’s alifanya mazungumzo na Oyotemmeli kiongozi wa kabila la Wadogoni na matokeo yake walipata falsafa ya kidini ya wadogoni.
Ethnofilosofia hujishughulisha na ukusanyaji wa mitazamo ya kiulimwengu kutoka katika tamaduni mbalimbali za waafrika. Hii imejikita katika masuala ya imani, masimulizi na misemo ya watu. Muunganiko huo umeunganishwa na Paulin Hountondji.  Wengine waliojihusisha na falsafa ya kiafrika katika mtazamo huu ni Placid Tempels, Leopald Senghor, John Mbiti na Alex Kagame. Hivyo, mtazamo huu umejikita zaidi katika masuala ya mila, desturi na imani za jamii.
Falsafa ya Kiuweledi imejikita katika uchambuzi na ufafanuzi wa ukweli. Zaidi inajihusisha na uhakiki, na hoja ndizo sifa za msingi kwao. Waanzilishi wa falsafa hii ni Paulina Hountondji, Kwasi Waredu, Odera Oruka na Peter Bodunrin. Wanasema kuwa falsafa ya kibantu kwa sasa inaitwa Metafilosofia, na imejikita katika kuangalia maudhui ya msingi. Wao wanahoji kwamba falsafa ya Afrika ni ipi?
Roberto (1996) anasema Ontolojiani nadharia inayohusu kuwapo, yaani ni nadharia inayoangalia yaliyokuwepo na yale ambayo hayakuwepo, halisi na yasiyo halisi, tegemezi na vinavyojitegemea.
Parrinder (1969) anasema kuwa nadharia ya kibantu inahusisha mwafrika na imani yake. Hujumuisha maisha, mazingira pamoja na fikra zake. Pia anasema kuwa mawazo ya mwafrika hujengwa katika misingi ya nguvu mbalimbali ambazoni Mungu, binadamu, wanyama, mimea na kadhalika.
Wataalamu wengine waliozungumzia nadharia ya Ontolojioa ni: Husserl (1913), Tugendhat (1928), Wolff (1928), Gruber’s (1993), Bolzano (1996), Guariono (1998), Wamitila (2008) na Cocchiarella (2007).
Kwa jumla, wataalamu hawa wameeleza mengi juu ya nadharia hii, jambo lililosisitizwa sanana wataalamu wengi waliojadili nadharia hii ni kuhusu uchaguzi wa Ontolojia nzuri na namna ya kutumia nadharia hii. Wanasema Ontolojia nzuri ni ile inayohusisha njia za Kisayansi na kutupatia njia chache na rahisi ambazo zitaelezea mambo mbalimbali katika ulimwengu. Pia nadharia hii inatukuza sana Ubantu na kumuona mwafrika kama kiumbe bora mwenye uwezo wa kubuni na kusimamia mambo yake kwa usahihi. Mbali na kutumia Ubantu (U-Afrika), nadharia hii inaeleza mambo kadhaa ambayo ni sehemu ya ufahari kwa waafrika, mambo hayo ni pamoja na dhana ya familia pana, kuamini uzazi kuwa ndio njia ya uzima wa milele, yenye kuhashiria umuhimu wa binadamu, na Ugumba ni laana na utupu kwa binadamu, kuabudu katika Mungu na miungu na kuheshimu Wahenga. Pia huhusisha na imani kuhusu uchawi, na sihiri, na ndani yake kuna masuala ya uganga. Pia umri kwa waafrika una nafasi kubwa sana katika jamii na unabeba hekima za mtu.




No comments:

Post a Comment