.
Nadharia ni dhana ambayo imeweza kufasiliwa na
wataalamu mbalimbali. Mathalani, Wamitila (2003) anafasili nadharia kuwa ni
mawazo, dhana au maelezo yanayotolewa kuelezea hali fulani; chanzo chake,
muundo wake utenda kazi wake na mwingiliano wake wa ndani na nje.
Vilevile, Sengo (2009) anafasili nadharia kuwa ni
wazo kuu, fikra kuu, muongozo mkuu wa mtu, watu au jamii ya pahala fulani. Kwa
mantiki hiyo, nadharia ni dira na mwongozo wa kulikabili jambo kifalsafa,
kidini, kimantiki, kijamii na kiutamaduni.
Hivyo, kwa ujumla tunaweza kufasili dhana hii ya
nadharia kuwa ni dira inayomwongoza msomaji/mhakiki kuhusu dhana, asili au
chanzo cha jambo fulani ili kulikabili jambo hilo kifalsafa, kimantiki, kijamii
na kiutamaduni.
Dhana ya ushairi nayo imeweza kufasiliwa na
wataalamu mbalimbali kwa mikabala miwili tofauti, ambayo ni mkabala wa
kimapokeo na mkabala wa kimamboleo. Wataalamu mbalimbali wa mkabala wa
kimapokeo wameweza kufasili dhana ya ushairi kama ifuatavyo;
Amri Abeid (1954) anafasili kuwa ushairi au utenzi
ni wimbo, hivyo kama shairi haliimbiki halina maana. Katika fasili hii kinachosisitizwa zaidi ni
suala la ulinganifu au urari wa vina na mizani katika utunzi wa ushairi au
utenzi. Hivyo basi, kwa mtazamo wake anaona kuwa shairi lisipokuwa katika
muundo wa urari wa vina na mizani halina hadhi ya kuitwa shairi.
Massamba, (2002) akimnukuu Shaban Robert, anasema
kuwa ushairi ni sanaa ya vina inayopambanuliwa kama nyimbo, mashairi na tenzi
zaidi ya kuwa na sanaa ya vina ushairi unaufasaha wa maneno machache au
muhtasari. Katika fasili hii linasisitizwa suala la vina na lugha ya mkato katika
sanaa ya nyimbo, mashairi na tenzi.
Aidha, kuhusiana na mkabala wa kimamboleo pia wapo
wataalamu ambao nao wameweza kutoa fasili zao kuhusu dhana ya ushairi mfano;
Kahigi na Mulokozi (1973) wanafasili ushairi kuwa ni
sanaa inayopambanuliwa kwa mpangilio maalumu na fasaha na wenye muwala, kwa
lugha ya picha, sitiari au ishara katika usemi, maandishi au mahadhi ya wimbo
ili kuleta wazo au mawazo, kufunza au kueleza tukio au hisia fulani kuhusu
maisha au mazingira ya binadamu kwa njia inayogusa moyo.
Aidha, Njogu na Chimerah (1999) wanafasili ushairi kuwa
ni sanaa ya lugha inayoeleza jambo au wazo kwa njia ya mkato na kwa namna
inavyoteka hisia za msomaji au msikilizaji. Waendelea kuelezea kuwa maneno ya
mashairi huteuliwa kimaksudi ili yalete taswira maalumu akilini mwa msomaji au
msikilizaji. Maneno hayo hupangwa ili yatoe mdundo fulani wa shairi
linapoimbwa, linaposomwa, linapoghaniwa au linaposemwa.
Hivyo basi, kutokana na dhana hii ya ushairi
kufasiliwa na wataalamu mbalimbali wa mikabala miwili tofauti yaani mkabala wa
kimapokeo na mkabala wa kimamboleo tunaweza kutoa fasili ya ujumla ya ushairi
kuwa ni kazi ya sanaa yenye kuandikwa au
kuimbwa kwa kufuata kanuni za ushairi au kutofuata kanuni za ushairi ikiwa na
maana kuwa ushairi waweza kuwa wa kimapokeo au wa kisasa ilimradi ushairi huo
uwe na ujumbe kwa jamii fulani.
Ushairi simulizi ni
utanzu unaojumuisha tungo zote zenye mapigo ya kimziki, mawazo, hisia na hoja,
katika utanzu huu huwasilishwa kwa njia ya mdomo. Aidha, ushairi simulizi
hutumika kupitisha maarifa au mafunzo ya jamii fulani kwa mfano nyimbo za
jandoni, za harusi, za dini hutumiwa kupitisha au kuwasilisha mafunzo katika
jamii husika.
Baada ya kufasili dhana
mbalimbali zilizojitokeza katika swali hili, kuna nadharia mbalimbali
zinazoelezea kuhusu asili ya ushairi simulizi, nadharia hizo zimegawanyika
katika makundi mawili ambayo ni mtazamo wa Kiulaya na mtazamo wa Kiafrika. Kwa
kuanza na mtazamo wa kiulaya ni kama ifuatavyo.
Nadharia ya ubadilikaji
taratibu, Wamitila (2012) anaeleza kuwa mwasisi wa nadharia hii ni Charles
Darwin, huyu alikuwa mwanabaiolojia katika karne ya 19. Alifanya utafiti kuhusu
viumbe hai akaona sifa ya kufanya hivo ni kuangalia sifa ya kibaiolojia ya
viumbe hai na akaona viumbe wote wana sifa zinazofanana, kwa hiyo nadharia hii
ya kibaiolojia ikahamishiwa kwenye
fasihi, mawazo ya utafiti wa Darwin yalianza kuathiriwa na wanafunzi wake ambao
ni Edward Tylor na James George Frazer. Wanafunzi hawa waliona kuwa kuna ukoo
mmoja na jamii moja ambazo zilizagaa ulimwenguni kote. Baadae mawazo yao yalishadadiwa
na wanazuoni kama vile John Roscoe – alifanya uchunguzi katika jamii ya
Baganda, Edwin Smith na Andrew Dale walichunguza katika jamii ya Ila huko
Zambia. Wataalamu hawa walichunguza utamaduni wa binadamu katika utafiti wao
walikusanya simulizi kutoka jamii mbalimbali za Kiafrika, Asia na Amerika
ambapo baada ya kukusanya simulizi hizo ikiwemo ushairi waligundua zilikuwa na
ufanano wa kimaudhui, wanamabadiliko
wanaamini kuwa ushairi simulizi tulionao leo una asili moja isipokuwa zimekuwa
zikibadilika kutokana na mabadiliko ya wakati. Aidha, ubora wa nadharia hii ni
kwamba fasihi ya Afrika sawa na ile ya Ulaya isipokuwa hubadilika kutokana na
wakati na mazingira.
Upungufu wa nadharia hii
ni kwamba wanamabadiliko waliamini kuwa kila kitu kilichokusanywa katika fasihi
kilihesabika kama masalia ya zamani au mabaki ya fasihi iliyotangulia. Pia,
walijikita katika kuangalia kipengele cha maudhui na kusahau fani.
Nadharia ya msambao, nadharia
hii imeasisiwa na wataalamu Jacob na Wilhem Grimm ambao walitafiti fasihi
kutoka India, Afrika na nchini kwao Ujerumani, na walihitimisha kuwa kuna
kufanana kwa fasihi hizo wakatoa maamuzi kwamba fasihi za kiafrika ni chimbuko
kutoka kwa wazazi wenye asili na utamaduni wa India na Ulaya. baadae mawazo yao
yaliendeleza na Maxmuller na Stith Thompson (1946). Wataalamu hawa
walikubaliana kuwa tanzu mbili au zaidi za fasihi kutoka katika jamii mbili au
zaidi zikionyesha vipengele au sifa zinazofanana ni kwa sababu kuna kipindi
fulani huko nyuma jamii hizi ziliingiliana. Mwingiliano ambao ulisababisha
jamii moja kuchota baadhi ya vipengele vya utamaduni mwingine (Finnegan 1970). Mfano
jamii A na jamii B, jamii A ni ile ambayo imeendelea na ipo juu kiuchumi na
jamii B ni jamii ambayo ni duni hivyo, jamii hizi zikiingiliana jamii B huweza
huchota vipengele vya fasihi kutoka jamii A. Utamaduni unaenezwa kutoka jamii A
kwenda kwa jamii B. Wamitila (2012) anaeleza kuwa kiini cha nadharia hii ni fikira kuwa chochote
kinachopatikana kina chanzo chake na mahusiano ya karibu ndiyo yanaathiri
misuko, wahusiaka, visa, mada au hata matendo ya fasihi simulizi. Kutokana na
nadharia hii wanamsambao waliona kuwa asili ya ushairi simulizi ulitokana na
kuathiriana kwa jamii za Kiulaya na ukasambaa katika jamii za Kiafrika.
Ubora wa nadharia hii
kwa mujibu wa Finnegan (1970) wanamsambao waliipa hadhi fasihi simulizi kwa
kuchunguza muktadha kwa undani. Vilevile, nadharia hii ilionekana kuwa ya
kisayansi zaidi, hivyo inaweza kuchunguzika tofauti na wanamabadiliko kwa akili
ya mtu haiwezi kuchunguzika. Aidha, Udhaifu wa nadharia hii ni kwamba imepuuza
fasihi ya Afrika. Kwamba fasihi ilisambaa kutoka nchi zilizostaarabika (ulaya)
kwenda nchi zisizostaarabika (Afrika).
Nadharia ya uamilifu, kwa
mujibu wa Walles na Wolf (1980) nadharia ya Uamilifu iliasisiwa karne ya 20 na
Bronslav Malinowski. Malinowski alizingatia fasihi simulizi kwa mujibu wa
uamilifu au utenda kazi wake. Nadharia ya uamilifu huzingatia kuwa fasihi
simulizi ina utenda kazi katika mfumo wa jamii ambapo huwa imo. Hali hii ni
sawa kwa vitanzu vyake vyote zikiwemo nyimbo. Kwamba, ijapokuwa mwanafasihi hujihusisha
na usanifu wa kazi fulani ya fasihi, sambamba na hilo hujaribu kubainisha
utenda kazi wa utanzu katika jamii anayoifanyia uchunguzi. Kutokana na nadharia
hii tunaona kwamba kila jamii ina utamaduni wake wa kuwaongoza katika maisha
yao ya kila siku mfano; jando na unyago, matambiko, harusi, mazishi na kusalia miungu kuwa ndio chanzo cha fasihi.
Ubora wa nadharia ni kwamba umesaidia kuondoa mawazo
kuwa chimbuko la fasihi mbalimbali ikiwemo ushairi ni mahali fulani bali ni
kila jamii imekuwa na simulizi ambazo zina sawiri uzoefu wao wa kila siku
katika nyanja mbalimbali kama vile kiuchumi, kisiasa, kiutamaduni na kijamii.
Pia, nadharia hii inatusaidia kujielewa na kuzielewa jamii zetu vizuri kwa
kuyaelewa mazingira ya mila na desturi zetu katika jamii.
Baada ya kuangalia nadharia ya asili ya ushairi
simulizi kwa mtazamo wa Kiulaya, zifuatazo ni nadharia za ushairi simulizi kwa
mtazamo wa Kiafrika
Nadharia ya Uhulutishi, hii ni nadharia ambayo iliasisiwa
na wanazuoni wa Kiafrika wenye mtazamo kuwa hata wageni wamechangia sana katika
ukuzi wa fasihi simulizi ya Kiafrika. Miongoni mwa waasisi na wafuasi hawa ni
pamoja na Mulokozi, Johson na Ngugi wa Thiongo. Nadharia ya uhulutishi inaleta
uwiano wa kitaaluma na kuona kwamba ingawa kwa kiwango kikubwa mawazo ya
wanazuoni wa kigeni yalitawaliwa na
dosari kadhaa, si kila walichokinena kuhusu Afrika, hususani utamaduni wa
fasihi ya Kiafrika si kibaya. Pia, kwa mujibu wa wanazuoni wa nadharia hii, yaliyosemwa
na wageni yanahitaji kuchambuliwa na kufanyiwa ufafanuzi wa kina. Hii ni kwa
sababu ndani mwake kuna uzuri na dosari ya namna fulani, hayapaswi kupuuzwa
kabisa. Nadharia hii inasisitiza kuwa mbinu ya kupata nadharia bora ni kuchanganya
nadharia zote mbili ya Kiafrika na Kiulaya.
Ubora wa nadharia hii ni kwamba, ilichunguza na
nadharia mbalimbali mfano nadharia kwa mtazamo wa Kiulaya wakaona sio kila
walichokinena kuhusu Afrika kilikuwa kibaya au kupuuzwa. Pia, Udhaifu wa
nadharia hii ni kuwa hawakuelezea asili ya ushairi simulizi.
Nadharia ya Kitaifa, nadharia hii iliasisiwa na
Adebayo Babalola, Daniel Kunene na Clark. Nadharia hii ilizuka katika vuguvugu
la kudai uhuru barani Afrika. Mfano Adebayo Babalola katika kitabu chake cha The Content and Form of Yoruba Ijala (1966).
Ijala ina maana ya ushairi wa
wawindaji katika jamii ya Wayoruba, alibainisha mbinu za kimtindo katika Ijala (ladha ya kishairi) pia matini ya
mashairi ya Ijala katika lugha ya
Kiyoruba na tafsiri ya mashairi katika lugha ya Kiingereza. Wanautaifa wanadai
kuwa wananadharia waliopita hawakuwa na uelewa wa kutosha kuhusu lugha za
Kiafrika, kwa kiwango kikubwa waliathiriwa na dhana ya ukoloni na upendeleo wa
kibepari kuwa Afrika ni bara la giza na la washenzi wasiokuwa na aina yoyote ya
ustaarabu na walistahili kustaarabishwa na Wazungu kupitia mlango wa ukoloni. Katika
nadharia hii wamejaribu kuondoa dosari ambazo nadharia zilizopita zimeshindwa
kuondoa. Kutokana na kwamba wananadharia waliopita mara baada ya kutafiti
hawakuwa tayari kuchapisha matokeo yao halisi ya utafiti bali kuyahariri
matokeo yao. Na wanaona ni kosa kubwa kufanya utafiti bila kuwahusisha wahusika
wa eneo la utafiti. Hivyo, ili kufahamu vyema historia ya fasihi simulizi ya
kiafrika ni lazima kuhusisha wataalamu na wanazuoni wa taifa au jamii hiyo.
Ubora wa nadharia hii ni kwamba wanazuoni wenyeji
walifanikiwa kueleza na kufafanua ufanisi wa mbinu mbalimbali za kimtindo
katika fasihi hasa katika ushairi simulizi. Pia, walirekodi hali na muktadha
wote wa utendwaji wa fasihi simulizi.
Hivyo basi, baada ya kuangalia nadharia mbalimbali zinazoelezea
ushairi simulizi kwa mtazamo wetu tunaona kuwa nadharia ya Kitaifa ndio
nadharia iliyo bora na faafu. Hii kwa sababu kila jamii ina utamaduni wake na
jamii ya Waafrika ina utamaduni wao ambao ulikuwepo hata kabla ya ujio wa
wageni. Kupitia utamaduni wao huo, waliweza kuwa na ushairi simulizi wao ambao waliutumia
katika shughuli mbalimbali za kijamii, kama vile katika harusi, jando na unyago.
Aidha, ushairi huo ulikuwa unafungamana na muktadha na utendaji wa jamii hiyo
katika kuwasilisha kazi iliyokusudiwa kwa jamii fulani.
Kwa ujumla, ushairi simulizi umekua na kuenea kwa
kasi katika jamii za Waafrika kutokana na fani hii ya ushairi kutumika katika
nyanja mbalimbali kama vile katika nyanja za kiuchumi, kisiasa na kijamii. Ushairi
unadhima mbalimbali kwa jamii, mathalani kuburudisha, kuelimisha, kuomboleza,
kubembelezea watoto na kuhamasisha watu kutenda jambo fulani, hivyo basi, fani
hii haiwezi kutenganishwa na maendeleo ya jamii husika kwani kila jamii
inapobadilika na utanzu huu pia hubadilika kulingana na jamii hiyo.
MAREJELEO
Abedi, K. A.
(1954) Sheria za Kutunga Mashairi na
Diwani ya Amri. Nairobi: Kenya Literature
Bureau.
Finnegan, R. (1970)
Oral Literrature in Africa. Nairobi:
Oxford University Press.
Kahigi, K.K na Mulokozi,
M. M. (1973) Mashairi ya Kisasa. Dar
es Salaam: Tanzania Publishing House.
Massamba, D. P.
B. (2002) Historia ya Kiswahili: 50 BK
Hadi 1500 BK. Nairobi: The Jomo
Kenyatta Foundation.
Mulokozi, M.M.
na Sengo T. S. Y. M (1995) History of
Kiswahili Poetry A.D. 1000-2000. Dar es Salaam: Institute of Kiswahili
Research.
Njogu, K. na Chimerah, R. (1999) Ufundishaji
wa Fasihi: Nadharia na Mbinu. Nairobi: Jomo Kenyatta Foundation.
Sengo, T. S. Y.
M. (2009) Sengo na Fasihi za Kinchi.
Dar es Salaam: AKADEMIYA.
Walles, R. A. na
Wolf, A. (1987) The Contemporary Socialogy Theory. New York: Prentice Hall
Publishers.
Wamitila, K. W.
(2003) Kamusi ya Fasihi, Istilahi na
Nadharia. Nairobi: Focus Publication Ltd.
______________(2010)
Kichocheo cha Fasihi Simulizi na Andishi.
Nairobi: English Press.