a). Dhana ya mtoto ni pana na ina utata katika
kuelezea maana yake kutokana na muktadha wa mtoa maana hiyo. Kwa mfano, wafuasi
wa dini mbalimbali kama vile Wakristo, Waislamu, watu wazima, wazee kwa vijana
hudai kuwa wao ni watoto wa Mungu, kwa maana hiyo mtoto hakui anabaki vilevile.
Aidha, wapo wataalamu mbalimbali ambao wamefasili dhana hii ya mtoto.
TUKI (1981) wanafasili dhana ya mtoto kuwa ni
mwanadamu au mnyama ambaye hajakomaa au ni jina analoitwa kiumbe ambaye
amezaliwa na wazazi wawili. Fasili hii ina dosari kwani si kweli kuwa kila mtu
ambaye amezaliwa na wazazi wawili ni mtoto bila kuangalia kigezo cha umri.
Ndalu na wenzake (2014) wanafasili kuwa mtoto ni
kiumbe kizaliwacho hususani na mtu. Fasili hii ina mapungufu kwani hata kiumbe
ambacho kimezaliwa na mnyama kama vile mbuzi anaweza kuwa mtoto wa mbuzi.
Kwa ujumla, mtoto ni mtu yeyote mwenye umri chini ya
miaka kumi na nane (18). Aidha, Wafula (2010) katika kusaidia kuielewa dhana
hii ya mtoto amewagawanya watu katika makundi makuu manne. Anadai kuwa rika la
utoto ni miaka 0 – 17, rika la ujana ni miaka 18 – 34, rika la wazazi/utu uzima
ni miaka 35 – 52 na rika la wazee ni miaka 53 nakuendelea. Hivyo basi, kwa
mgawanyo huo mtoto ni mtu yeyote mwenye umri wa chini ya miaka 18.
Pia, dhana hii ya fasihi ya watoto ni telezi kwani
wataalamu wamepishana katika kuifasili. Aidha, Mpesha (1995) anasema fasihi ya
watoto ni ile ambayo hulenga kuwafahamisha watoto kuhusu mambo mabaya, hisia na
matarajio ya jamii hiyo. Dosari ya fasili hii kwamba imejikita katika kuangalia
mambo mabaya tu hali ya kuwa fasihi ya watoto huweza pia kuburudisha,
kuendeleza, kukuza na kurithisha utamaduni. Lakini pia, haijaweka wazi kuhusu
hayo mambo mabaya ni yapi?
Hunt (1996), fasihi ya watoto ni ile inayolenga
kiwango cha watoto kama msomaji wa fasihi hiyo. Kwahiyo, msomaji wa vitabu vya
fasihi huwa ni watoto au mtoto aliyeandikiwa. Fasili hii pia ina dosari kwani
fasihi ya watoto huweza kusomwa hata na watu wazima.
Weche (2002), anasema kuwa fasihi ya watoto ni kioo
cha kumwongoza mtoto katika mambo yanayohusu
maadili. Pia anasema kuwa, fasihi hiyo inapaswa kukashifu tabia zisizo
kubalika na kabainika katika jamii. Dosari ya fasili hii ni kwamba imezungumzia
suala la kioo kama chombo cha kumwongoza mtoto lakini itambulike wazi kuwa kioo
hakiwezi kumwonesha mtu kila sehemu ya mwili wake na akajirekebisha. Hii ikiwa
na maana kuwa si kila maadili yanaweza kuzungumziwa katika fasihi ili
kumwongoza mtoto.
NOUN (2010), wanasema fasihi ya watoto ni dhana
ambayo inarejelea fasihi inayowalenga watoto pekee. Wanaendelea kusema, fasihi
ya watoto huweza kuwa hadithi, ushairi, visakale na drama ambazo zimetungwa kwa
ajili ya watoto wadogo. Fasili hii ina dosari kwani si kweli kuwa fasihi ya
watoto ni lazima iwahusu watoto tu kwani kuna maudhui yanayopatikana katika
kazi hizi lakini yanawahusu watu wazima.
Wamitila (2010), anasema kuwa suala la ufafanuzi wa
fasihi ya watoto linaweza kueleweka kwa kukitwa katika mitazamo mikuu miwili.
Mosi, fasihi ya watoto ni ile ambayo hadhira yake ni watoto. Pili, fasihi ya
watoto ni ile ambayo msingi wa dhamira na kimaudhui huwarejelea watoto. Dosari
ya fasili hii ni kuwa si kweli kwamba muda wote dhamira zake huwahusu watoto tu
kwani wakati mwingine huwagusa hata watu wazima.
Kwa ujumla, tunaweza kusema kuwa fasihi ya watoto ni
fasihi iliyoandikwa kwa kuwazingatia watoto kama hadhira lengwa. Hii ina maana
kuwa hata mtu mzima anaweza akaisoma fasihi hii japo kuwa hadhira
iliyozingatiwa zaidi ni watoto.
b). Kwa
kutumia kazi mbili za fasihi ya watoto ambazo ni Sababu mimi ni Mwanamke! iliyoandikwa na Ebraju (1999), pamoja na Kilio Chetu kilichoandikwa na Medical
Aid Foundation (1995) tunaweza kueleza maana ya fasihi ya watoto kwa kurejelea
kazi hizi kama ifuatavyo:
Kwa kumrejelea Mpesha (1995) anasema fasihi ya
watoto ni ile ambayo hulenga kuwafahamisha watoto kuhusu mambo mabaya, hisia na
matarajio ya jamii hiyo. Fasili hii inasawili na kile kilichozungumziwa katika
vitabu hivi viwili. Mathalani, katika kitabu cha Sababu mimi ni Mwanamke! mwandishi anasema;
“Mwanangu” alisema baba, kwa upole,
lakini bila shaka ni upole imara. “Mwanangu, wewe umekuwa mkubwa sasa. Mama
yako anakuhitaji hapa nyumbani. Hana wa kumsaidia kuteka maji wala kuchanja
kuni. Tena mtoto wa kike kutembeatembea kwenda shule si vyema sasa utabaki
nyumbani! … Nenda ukaweke mkoba wako.” (Uk.12)
Haya ni miongoni mwa mambo mabaya ambayo
yamezungumziwa kwenye fasili hii ambayo yamelenga kuwafahamisha watoto, ambapo
inaonekana mtoto wa kike akakikatizwa masomo ili amsaidie mama yake kazi za
nyumbani kwa kuwa tu yeye ni mwanamke. Vilevile, haya yanasawili kupitia kitabu
cha Kilio Chetu ambapo mwandishi
anasema;
“JUMBE:
Siyo zamani akina mama utasikia: vibaya kuangalia magazeti ya mapicha ya uchi mtaota…sinema
za “ X” ni kwa wakubwa tu siku hizi tunaangalia vyote, nani anaota?
WOTE:
Hakuna
JUMBE:
Twenzetuni tuwahi picha, senti zako tu (wanaondoka)” (Uk.20).
Hii tunaona kuwa watoto wamekuwa wakifanya mambo
mabaya ambayo hapo awali walikuwa wakikatazwa na wazazi wao.
Kwa kupitia vitabu hivi vya fasihi ya watoto tunaona
kuwa vimeweza kufanikisha kufasili fasihi ya watoto kuwa ni ile ambayo hulenga
kuwafahamisha watoto kuhusu mambo mabaya, hisia na matarajio ya jamii hiyo.
Lyimo (2016), anasema kuwa fasihi ya watoto ni
fasihi ambayo walengwa wake wakuu ni watoto. Aidha, kwa kudhihirisha hili
mwandishi wa kitabu cha Sababu mimi ni
Mwanamke! anasema;
“Sara!
Aisha! Dora! Mko wapi? mnanisikia?... wapi! Sauti yangu haifiki popote.
Inachimbuka ndani kwenye nafsi yangu. Inanitambaa ndani ya mawazo yangu. Ina nguvu
sana. Lakini wapi? Sauti ya mtoto
tena mtoto wa kike! Kwanza ni aibu kutoa sauti. Pili haifiki
popote.” (Uk. 2)
Kwa mfano huo, ni dhahiri kuwa fasili hiyo ya fasihi
ya watoto ambayo walengwa wake wakuu ni watoto ambapo tunaona hata mhusika mkuu
wa kitabu hiki ni mtoto. Vilevile, katika kitabu cha Kilio Chetu kinaonesha kuwa walengwa wake wakuu ni watoto, mwandishi
anasema;
“
ANNA: Hivi wewe unakilimbilia wapi lakini? Soma kaka yangu. Mtoto mdogo hivi
mambo haya ya nini? Mbona kutaka kujikomaza hivyo? Kisa cha kukimbilia suti na
nepi hujavaa? Mambo hayo tutayakuta wakati ukiwadia. Wewe utaoa na mimi
nitaolewa. Na nani aliyekueleza kuwa hii dunia itaisha kesho?” (Uk. 28).
Kutokana na mifano hii kutoka katika kazi hizi mbili
tunaona kuwa inaenda sambamba na ile fasili inayosema kuwa fasihi ya watoto ni
fasihi ambayo walengwa wake wakuu ni watoto.
Pia, Weche (2002), anasema kuwa fasihi ya watoto ni
kioo cha kumwongoza mtoto katika mambo yanayohusu maadili. Fasili hii inaendana
na kitabu cha Kilio Chetu pale ambapo
mwandishi anasema;
“BABA
ANNA: Haya wenzangu kurupushani za nini?
MJOMBA:
Dada kakuta vidonge vya majira kwenye nguo za Suzi. Sasa kamdunda wee, mie
nikamwambia hilo sio jibu la kumwokoa mtoto. Vyema basi aelimishwe madhara
makubwa ya kufanya ngono kabla ya wakati wake. Akielimishwa kwa kina hawezi
kuthubutu. Sasa nimekumbana na upinzani. Na jirani hapa alivyokuja ndio
kabisaa.
BABA
ANNA: Una maana kupewa elimu ya jinsia kama inavyoshauriwa?
MJOMBA:
Hasaa.
BABA
ANNA: Hilo ndilo mie nililofanikiwa mwenzenu. Nimemwambia mama Anna akae na
mabinti zake nami nikae na vijana wangu wa kiume. Tumefanya kazi hiyo kwa
makini sana. Tumewaelimisha juu ya madhara ya tabia hiyo kwao binafsi na kwetu
sote. Hatukubakiza kitu. Dunia imeharika sasa bwana. Mzazi usipomfunza,
walimwengu watamfundisha; Tena sasa si maadili bali ni njia potofu.
MJOMBA:
Mzazi ndie mwalimu wa kwanza.” (Uk.
12 – 13)
Hapa tunaona kuwa katika mfano huu umeweza kuangazia
suala zima la maadili hususani kwa watoto wadogo.
Kwa kuhitimisha tuaweza kusema kuwa fasihi ya watoto
ina dhima mbalimbali katika jamii, dhima hizo ni kama vile kupata maarifa
mapya, kuelimisha jamii, kufikirisha hadhira, kuedeleza, kukuza na kurithisha
utamaduni pamoja na kusaidia kujielewa na kuwaelewa wengine.
MAREJELEO
Ebraju, P. B.
(1999). Sababu mimi ni Mwanamke!.
Educational Books Publishers Ltd. Dar es Salaam.
Hunt, P. (ed.).
(1999). Understanding Children’s
Literature: Key Essays from the International Companion Encyclopidia of
Children’s Literature. New York: Routledge.
Lyimo, E. B.
(2016). Dhima na Mianzo na Miisho katika Nathari za Kiswahili na Fasihi ya
Watoto: Mifano kutoka Riwaya na Hadithi za Watoto nchini Tanzania.
Medical Aid Foundation.
(1995). Kilio Chetu. Tanzania
Publishing House Limited. Dar es Salaam – Tanzania.
Mpesha,
N. (1995). “Children’s Literature in Tanzania: A Literary Appreciation of its
Growth and Development.” Tasnifu ya PhD.
Chuo Kikuu cha Kenyetta. (Haijachapishwa).
Ndalu, A. E,
Babusa, H, na Suleiman, A. M. (2014).
Kamusi Teule ya Kiswahili Kilele cha Lugha. East African Educational
Publisher Ltd: Nairobi – Kenya.
NOUN (2010). Children’s Literature. Lagos: National
Open University of Nigeria.
TUKI
(1981). Kamusi ya Kiswahili Sanifu.
Oxford University Press. Dar es salaam - Tanzania.
Wamitila, K. W.
(2010). Kichocheo cha Fasihi: Simulizi na
Andishi. Nairobi: Focus Books.
Weche, M. O.
(2002). “Children’s Literature an Image Force. A Case Study of Ezekiel Alembi’s
Books.” Tasnifu ya M. A, Chuo Kikuu cha Kenyetta. (Haijachapishwa).