SIKU chache baada ya kurejea uwanjani, mshambuliaji wa Yanga, Amissi Tambwe, amewatahadharisha mabeki wa timu pinzani kuwa atarejea na kasi kuisaidia timu yake kutetea ubingwa wake msimu huu.
Tambwe ambaye alikuwa nje kwa muda mrefu, wiki hii alianza mazoezi na kucheza kwenye mchezo wa kirafiki dhidi ya Polisi Tanzania ambapo timu hizo zilimaliza dakika 90 bila kufungana.
Akizungumza na mwandishi wetu baada ya mazoezi ya jana asubuhi, yanayofanyika kwenye Uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam, Tambwe, alisema kuwa kwa sasa yupo fiti na shauku yake kubwa ni kufunga katika kila mchezo.
"Nimekaa sana nje, na nilikuwa nasononeka kukosa kucheza, kwa sasa mashabiki wasiwe na hofu, nimerejea kwa kazi moja tu, kufunga na kusaidia timu yangu kupata ushindi," alisema Tambwe.
Aidha, alisema kuwa anafahamu ushindani wa namba utakuwa mkali hasa kutokana na kuwapo kwa washambuliaji wengine kama Ibrahim Ajibu na Yohana Nkomolwa, lakini atamshawishi Kocha George Lwandamina kwenye mazoezi ya timu hiyo.
Lwandamina kwa sasa ana wigo mpana wa kupanga kikosi chake kwenye safu ya ushambuliaji kufuatia kurejea kwa Tambwe na mshambuliaji raia wa Zimbabwe, Donald Ngoma, ambaye naye alianza mazoezi wiki hii.
Kwenye michezo iliyopita ya Ligi Kuu, Lwandamina, alikuwa akiwategemea zaidi Ajibu na Obrey Chirwa kwenye safu ya ushambuliaji na wachezaji hao walionyesha uwezo na ushirikiano mkubwa.
Ajibu na Chirwa wamechangia kupatikana kwa mabao 17 katika michezo 11 waliyocheza huku wawili hao kwa pamoja wakiifungia Yanga inayodhaminiwa na Kampuni ya Kubashiri Matokeo Michezoni ya SportPesa mabao 11.