SERIKALI imetangaza fursa ya walimu kufundisha lugha ya kiswahili nchini Afrika Kusini na watakaochaguliwa ni wenye kujua kwa ufasaha lugha ya kiswahili na kiingereza.
-
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda amesema jijini Dar es Salaam ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya kilele cha siku ya kiswahili duniani iliyopangwa kufanyika Julai 7 mwaka huu kwa mara ya kwanza.
-
Profesa Mkenda amesema katika kuhakiksha kiswahili kinakuzwa katika maeneo mbalimbali, Tanzania na Afrika ya Kusini watasaini mkataba wa makubaliano ya ufundishaji wa lugha hiyo nchini humo. Tayari Waziri wa elimu nchini humo yupo nchini akiongozana na wajumbe mbalimbali kwa ajili ya tukio hilo.
-
Amesema walimu watakao chaguliwa ni muhimu kujua kwa ufasaha lugha hizo na sio wasiojua au kuchanganya herufi katika ufundishaji.
-
"kuna watu wenye tatizo la herufi kama L na R ambapo hao watakuwa wapotoshaji wa kiswahili," amesema Mkenda na kuongeza kuwa kiswahili ni lugha muhimu kwa fursa mbalimbali.
-
Aidha amesema mbali ya Afrika Kusini pia wameongea na waziri wa elimu wa Zimbabwe ili kwa baadae kuweza kupeleka lugha hiyo katika maeneo mbalimbali.
-
Amesema serikali itapeleka timu ya wataalam kwa ajili ya kutengeneza mpango kazi wa ufundishaji nchini humo.