Mkoa wa Dar es Salaam umeshika nafasi ya kwanza kitaifa.
Dar es Salaan yatoa halmashauri nne 10 bora kitaifa.
Dar es Salaam. Kama bado unajiuliza ni mkoa gani ambao umefunika katika matokeo ya darasa la saba kwa mwaka 2021, basi fahamu kuwa mkoa huo ni Dar es Salaam ambao wanafunzi wake wamefaulu kwa asilimia 97.
Katika matokeo ya mtihani huo uliofanyika Septemba 2021, Dar es Salaam imeungana na mikoa mingine tisa kuunda orodha ya mikoa 10 bora iliyofanya vizuri kitaifa.
Katibu Mtendaji wa Baraza la Mtihani Tanzania (Necta), Dk Charles Msonde akitangaza matokeo hayo leo Oktoba 30 jijini Dar es Salaam amesema watahiniwa 1,108,023 sawa na asilimia 97.87 ya waliosajiliwa walifanya mtihani huo.
Watahiniwa 907,820 kati ya 1,107,460 waliofanya mtihani huo wamefaulu sawa na asilimia 81.97.
Dk Msonde amesema Mkoa wa Dar es Salaam ulikuwa na shule 715 na watahiniwa 81,562 walioshiriki mtihani huo ambapo waliofaulu ni 78,738 sawa na asilimia 97 ya watahiniwa wote katika mkoa huo.
Kwa ufaulu huo wa Dar es Salaam umeufanya mkoa huo kuongoza kitaifa ukifuatiwa na Iringa ambapo ufaulu wake ni asilimia 91 ya wanafunzi 28,018 waliofanya mtihani.
Mbeya imeshika nafasi ya tatu ambapo asilimia 88 ya watahiniwa 44,822 waliofanya mtihani huo wamefaulu ikifuatiwa na Arusha katika nafasi ya nne. Nafasi ya tano imeenda kwa Mkoa wa Njombe.
Njombe ilikuwa na watahiniwa 20,314 lakini waliofaulu ni 17,652 sawa na asilimia 86.9 ya watahiniwa wote katika mkoa huo.
Kilimanjaro imeshika nafasi ya sita ikifuatiwa na Mkoa wa Katavi katika nafasi ya saba kwa wanafunzi wake kufaulu kwa asilimia 87 sawa sawa na Kilimanjaro.
Wakati Katavi akishika nafasi ya saba, katika orodha hiyo, Lindi iko nafsi ya nane ikifuatiwa na Simiyu ambayo imeshika nafasi ya tisa.
10 bora imefungwa na Mkoa wa Pwani ambapo wanafunzi 32,331 kati ya 38,079 sawa na asilimia 85 katika mkoa huo wa mashariki mwaka Tanzania wamefaulu mtihani huo uliofanyika Septemba 8 na 9 mwaka huu.
Sifa za kipekee
Licha ya Dar es Salaam kushika nafasi ya kwanza kitaifa, pia imefanikiwa kuingiza Halmashauri nne katika orodha ya Halmashauri 10 bora zilizofanya vizuri kitaifa.
Halmashauri ya Jiji la Ilala ndiyo imeshika nafasi ya kwanza kitaifa. Halmashauri nyingine zilizoingia katika orodha hiyo ya dhahabu ni Kinondoni, Kigamboni na Ilala.
Pia mkoa huo umetoa wanafunzi watano ambao wamefanikiwa kuingia katika orodha ya wanafunzi 10 bora kitaifa huku ikishindwa kuingiza shule hata moja katika orodha ya shule zilizofanya vizuri.
Orodha ya halmashauri zilizofanya vizuri katika matokeo ya mwaka huu hii hapa chini.