Monday

FASIHI ANDISHI KF PDF

0 comments

 

FASIHI ANDISHI

__________________________________________________________________

I.                   USHAIRI

 

Kuna mitazamo ya aina mbili katika kuelezea dhana ya ushairi.kuna wanamapokeo na mamboleo. Hata hivyo kabla ya kuendelea zaidi kuwachambua tuangalie wataalam mbalimbali wanavyofasili dhana hii . Dhana ya ushairi imejadiliwa na wataalamu mbalimbali huku kila mmoja akitoa fasili yake. Baadhi ya wataalam hao ni kama ifuatavyo:

MAPOKEO

Mssamba, (2003) akimnukuu Shaban Robert,anasema; “ushairi ni sanaa ya vina inayopambanuliwa kama nyimbo, mashairi na tenzi zaidi ya kuwa na sanaa ya vina ushairi unaufasaha wa maneno machache au muhtasari.”

Mnyampala (1970)anasema kuwa “ushairi ni msingi wa maneno ya hekima tangu kale ndicho kitu kilichobora sana maongozo ya Dunia kwa kutumia maneno ya mkato na lugha nzito yenye kunata iliyopangwa kwa urari wa mizani na vina maalum.”

Amri Abeid (1954:1) anasema kuwa “ushairi au utenzi ni wimbo, hivyo kama shairi haliimbiki halina maana.”

Abdulatifu anasema kwamba ushairi ni ule ulio na sifa ya ulinganifu wa vina na mizani, lugha laini (lugha tamu) na lugha hii iweze kugusa moja kama ilivyokusudiwa.

Encyclopedia American (EA) inaeleza kuwa ushairi ni kauli zenye hisia na ubunifu, mpangilio fulani wenye urari, uwasilishaji wa tajiriba au mawazo ya mtunzi kwa maana ambayo huibua tajiriba kama hiyo katika nyayo za wasomaji au wasikilizaji na kutumia lugha ya picha yenye wizani wa sauti.

MAMBOLEO

Kezilahabi (   )anasema kuwa “ushairi ni tukio hai au wazo ambalo limeonywa kwetu kutokana na upangaji uzuri wa maneno fasaha yenye mizani Fulani ili kuonyesha ukweli”

Topan (1996) anasema kuwa “shairi ni unaoeleza hisia za ndani za binadamu kwa mpangilio Fulani wa maneno” hivyo kwa mujibu wa Topan ushairi lazima uguse hisia za ndani ya moyo wa binadamu.

Njogu na Chimerah (1999) wanasema “ ushairi ni sanaa ya lugha inayoeleza jambo kwa njia ya mkato na kwa namna inavyoteka hisia za msomaji au msikilizaji”

Mulokozi na Kahigi (1982:25) wanasema ushairi ni “sanaa inayopambanuliwa kwa mpangilio maalum na fasaha na wenye muwala, kwa lugha ya picha, sitiari au ishara katika usemi, maandishi au mahadhi ya wimbo ili kuleta wazo au mawazo, kufunza au kueleza tukio au hisia fulani kuhusu maisha au mazingira ya binadamu kwa njia inayogusa moyo.”

    Hivyo basi tunaweza kusema kuwa ushairi ni kazi ya sanaa yenye kuandikwa au kuimbwa kwa kufuata kanuni za ushairi au kutofuata kanuni za ushairi ikiwa na maana kuwa ushairi waweza kuwa wa kimapokeo au wa kisasa ilimradi ushairi huo uwe na ujumbe.

Katika ushairi FANI na MAUDHUI ni muhimu sana, mawazo fikra au sihi za ndani ni vitu muhimu sana katika ushairi

CHANZO/CHIMBUKO LA USHAIRI

 Dhana ya chimbuko inafasiliwa naTUKI (2004) kuwa ni mwazo au asili ya kitu.

    Baadhi ya wataalamu wameweza kuelezea chimbuko la ushairi wa Kiswahili kwa kuzingatia mitazamo au nadharia mbili ambazo ni kama ifuatavyo:

1.      Nadharia ya kwanza inadai kuwa; Chimbuko la ushairi wa Kiswahili ulitokana na ujio wa Waarabu.

2.      Na nadharia ya pili inasema kuwa; Chimbuko la ushairi wa Kiswahili ni zao la jamii ya waswahili wenyewe.

Hapa tunaenda kuzielezea nadharia hizi kila moja na kujaribu kuona ubora wake na udhaifu wake katika kuelezea chimbuko la ushairi

1.     CHIMBUKO LA USHAIRI INATOKANA NA UJIO WA WAARABU

Kwa kuanza naLyndon (1962) “Swahili Poetry” anatoa hoja tatu ambazo ni:

·         ushairi wa Kiswahili umetokana na Uislamu,

·         ushairi ulianzia kwenye upwa wa kaskazini mwa Kenya hususani Lamu.

·         Na maudhui ya ushairi wa Kiswahili yalitokana na ushairi wa Kiarabu. Utungo wa kwanza wa ushairi andishi wa Kiswahili ni Tambuka, Mwengo bin Athmani (1728)

 

Ubora wa Nadharia hii

·         Ubora wa nadharia hii au mtazamo wa Harries kuhusu chimbuko la ushairi wa Kiswahili ni kwamba umesaidia wengine kuendelea kuchunguza zaidi kuhusu chimbuko la ushairi wa Kiswahili.

            Udhaifu wa nadharia hii

® Udhaifu wa nadharia hii ni kuwa si kweli kwamba ushairi wa Kiswahili uliletwa na Uislamu bali ulikuwepo hata kabla ya ujio wa Uislamu, kwani ushairi hautenganishwi na jamii husika. Hivyo jamii za waswahili walitumia Nyanja mbalimbali za ushairi katika shughuli zao mbalimbali au shughuli zao za kila siku, kama vile; shughuli za kilimo na ufugaji.

® Pia ushairi wa Kiswahili ulianza karne ya 10BK na ushairi wa Kiswahili ulikuwa ukitungwa na kughanwa kwa ghibu bila kuandikwa. Wataalam wengi wanakubaliana kuwa asili ya ushairi wa Kiswahili ni tungo simulizi hasa ngoma na nyimbo.

®Udhaifu mwingine katika mtazamo wake wa kusema kuwa ushairi ulianzia pwani ya kaskazini ya Kenya si kweli kwa kuwa waswahili walikuwepo hata sehemu nyingine kama vile Kilwa na Bagamoyo ambapo ushairi wa Kiswahili ulitumika.

® Hoja ya kusema ushairi wa Kiswahili ulitokana na Kiarabu haina mashiko kwa kuwa waswahili walikuwepo hata kabla ya waarabu na walikuwa na ushairi wao isipokuwa ujio wao ulileta athari kubwa kwa kuwa ulichanganya na mambo ya dini ya kiislamu na hati.

®Knappert (1979) “Four centuries of Swahili verse” anasema;Ushairi wa Kiswahili ulichipuka kwenye upwa wa Kenya kutokana na nyimbo na ngoma za waswahili na ulianza katika karne ya 17 na pia ni ushairi wa Kiislamu wenye kuchanganya sifa za tungo za kiafrika na za kiajemi.

    Ubora wa hoja hii ni kwamba, ni kweli Knappert amekubali kuwa,ushairi wa Kiswahili ulitokana na waswahili wenyewe.

    Hata hivyo hoja yake ina udhaifu kwa kuwa ushairi wa Kiswahili ulianza kabla ya karne ya 10 BK na pia amejikita katika maudhui ya mambo mengine kama vile siasa, uchumi na kijamii. Vilevile amechanganya chimbuko la ushairi wa Kiswahili na Uarabu.

2. NADHARIA YA PILI INASEMA KUWA USHAIRI NI ZAO LA WASWAHILI WENYEWE.

Nadharia hii imejadiliwa na wataalam mbalimbali akiwemo Shaban Robert, Jumanne Mayoka (1993) na Senkoro, Mulokozi na Sengo.

Jumanne, M. Mayoka (1993) anasema ushairi umetokana na jamii ya wanadamu wenyewe na umesheheneza ukwasi mkubwa wa lugha ambayo imekuwa ikitumika katika hatua zote za kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni katika historia ambayo mwanadamu amepitia, Kwa mfano kuwa msamiati uliotumika tangu enzi za kuishi mapangoni, enzi za uwindaji, ujima, utumwa, vita vya makabila, uvamizi wa wageni, ukoloni na harakati za kupambana na ukoloni hadi kupata uhuru na maendeleo yake.

Ubora wa hoja

    Ubora wa hoja hii ni kwamba ina mashiko ndani yake kwa sababu, kila jamii ina sanaa yake na ushairi ni moja kati ya sanaa hizo ingawa inaweza ikaathiriwa na sanaa ya jamii nyingine. Pia ushairi umekuwa ukikua na kuendelea kadri jamii inavyokuwa na kuendelea.

Udhaifu wa hoja.

    Udhaifu wa hoja hii ni kwamba si kweli kuwa katika kipindi hicho ushairi ulikuwa tayari umesheheni ukwasi mkubwa wa lugha, na kama ulikuwa kweli umesheheni huu ukwasi wa lugha alipaswa kutuonesha huo utajiri wa lugha anaouzungumzia katika ushairi.

Senkoro (1988) anasema kuwa ushairi uliibuka pale lugha ilipoanza katika kipindi cha uhayawani (kipindi ambacho mwanadamu alipoanza kupambana na mazingira yake) kwenda katika kipindi cha urazini (maana) ili kumwezesha binadamu na mazingira yake kwa mfano, zana za kazi zilizotumika ziliwafanya waimbe kwa kufuata mdundo wa zana hizo.

Masamba anasema kwamba kimsingi chimbuko la ushairi wa Kiswahili ni waswahili wenyewe katika nyimbo, ngoma nk ambazo ziliimbwa katika masuala ya kilimo, jando na unyago n.k. Massamba anaendelea kusema kwamba nyimbo hizi zilikuwa zikiimbwa bila kufuata vina na mizani lakini kwa kadri muda ulivyoenda walizidi kuziendeleza na kuziboresha. Hivyo suala la vina na mizani lililetwa na wageni sio kiini cha ushairi wa kiswahili

Mulokozi fasili ya fasihi haiwezi kutenganishwa na utamaduni wa maisha ya watu. Anaelezea kuwa ushairi wa Kiswahili hutumia lugha ya Kiswahili, hivyo ili kujua chimbuko la ushairi wa Kiswahili ni lazima ujue juu ya waswahili wenyewe

    Pamoja na kuwa nadharia hii imeonesha kukubalika na wataalamu mbalimbali kama vile Senkoro, Mayoka na Shekhe Amri Abeid, lakini bado ina mapungufu. Hii ni kwa sababu imeshindwa kuonesha muda maalumu ambapo ushairi wa Kiswahili ulianza na ni wapi ulianza kutumika. Hili ni suala ambalo linaumiza vichwa vya wataalamu mbalimbali hadi hivi sasa, kwani hakuna mtaalamu yoyote aliyefanikiwa kuonesha ni wapi na ni lini ushairi wa Kiswahili ulianza.

    Hivyo basi, kutokana  na nadharia hizo mbili tunaungana na nadharia inayosema kuwa, chimbuko la ushairi wa Kiswahili ni zao la waswahili wenyewe, kwa sababu waswahili wana utamaduni wao ambao ulikuwepo kabla ya ujio wa Waarabu. Na waliutumia ushairi huo katika shughuli mbalimbali za kijamii, kwa mfano katika harusi, jando na unyago.

 

AINA ZA USHAIRI/BAHARI ZA USHAIRI

Kwa ujumla ushairi upo katika makundi mbalimbali. Uainishaji wa ushairi unategemea wataalam. Mlokozi (1996) anadai kuna bahari 13 za ushairi ambazo kwa mujibu wa tapo la wataalamu wa Mombassa

1.      Wimbo/Tathilitha

·         Shairi la aina ya wimbo lina mishororo 3 inayoweza kuwa na mikondo tofauti, unaweza kuwa na kina kimoja mwishoni

·         Mara nyingi wimbo huwa na vipande viwili

2.      Shairi/Tarbia

·         Utungo ambao una mishororo 4 katika kila beti na kila mshororo una vipande 2

·         Shairi huweza kuwa na maudhui ya namna yoyote ile

3.      Utenzi/utendi

·         Ni ushairi wenye mizani michache kuliko 12

·         Una vina vinavyobadilikabadilika isipokuwa cha mwisho

·         Kwa kawaida husimulia visa virefu vya kihistoria.mfn vita nk

4.      Zivindo

·         Ni shairi linalofafanua maana ya maneno

·         Lengo kuu ni kufunza lugha. Mfn shairi la Kihindi.

5.      Tumbuizo

·         Hauna idadi kamili ya mizani na mishororo

·         Nia yake ni kutoa hisia ambazo zimembana mtu. Mfn Mbolezi-nyimbo za misibani, nyimbo za kubembelezea watoto

6.      Hamziyya

·         Una mishororo miwili miwili na vina vyake viko mwisho tu wa beti

·         Ulitungwa na Sharif Aidarus bin Uthman

·         Ulikuwa ni wa kumsifu mtume Mohamadi S.W.A

7.      Dura Mandhuma au Inkishafi

·         Unatokana na utenzi wa mtu aliyeitwa Inkishafi

·         Una mambo ya kuonya, kufuata mambo ya kidini na kuelekeza

8.      Ukawafi

·         Una mstari mmoja wenye vipande vitatu

®Ukwapi-silabi 6

®Utao-silabi 4

®Mwandamizi 5

·         Zinahusu maudhui ya kidini

9.      Wajiwaji

·         Ni utungo ambao una mishororo 5 kila ubeti wenye mizani 5

·         Zinahusiana na mambo ya kidini, kumsifu mtu shujaa na bingwa

10.  Wawe au Vave

·         Asili yake ni kaskazini ya mwambao wa Pwani hasa sehemu za Amu na Pate

·         Unahusu kilimo, ziliimbwa wakati wa kufyeka mistu, kuchoma pori nk

11.  Kimai

·         Ni utungo unaohusu mambo ya baharini au wakati wavuvi wanapomtafuta mwenzao ambaye amepotea

·         Ni utungo unaohusu ubaharia

·         Idadi ya mizani hubadilika badilika na vina si vya lazima

12.  Ngonjera

·         ni mazungumzo au mabishano ya kishairi kuhusu mada Fulani

·         huundwa kwa kulumbana pande mbili

·         suluhisho la kile kinachojadiliwa hupatikana mwishoni

13.  Kikwamba

·         Ni utungo ambao neno moja hutumiwa kila mwanzo wa ubeti na neno hilo hufululizwa na mabadiliko mbalimbali.

 

 

MABADILIKO NA MAENDELEO YA USHAIRI WA KISWAHILI

MAENDELEO YA KIHISTORIA:

ü  Wataalamu ambao wanajaribu kutupa taarifa kuhusu maendeleo ya ushairi wa Kiswahili ni pamoja na M.M. Mulokozi (1996) ambaye anatuambia kwamba ulianza karne ya 10BK

ü  Katika kipindi hiki hakukuwa na ushairi ambao ulikuwa umeandikwa kwa utamaduni wa Waswahili bali kulikuwa na ushairi simulizi uliganwa kwa ghibu

ü  Kuanzia miaka ya 1000BK wakati wa ukoloni kulitokea athari kubwa katika ushairi wa Kiswahili k.v hati ya maandishi na dini ya kiislamu

ü  Ushari uliwaunganisha Waswahili na duni pana ya umma na taaluma ya uandishi kwa hati ya Kiarabu uliwapa wenyeji ujuzi wa kusoma na tabia ya kuandika

1000-1500BK

ü  Katika kipindi hiki kulikuwa na ustawi na ustaarabu wa kimji wa waswahili katika miji yote ya Pwani na biashara ilistawi  kati ya wageni na wenyeji

ü  Katika kipindi hiki fasihi pia ilistawi

ü  Mashujaa wanaosimuliwa katika tendi k.v Fumo Lyongo waliishi kipindi hiki

ü  Ushairi uliendelea kuwa simulizi

ü  Ushairi wa mwanzo uliitwa SWIFA

1500-1750BK

ü  Hiki ni kipindi cha tatu na kilikuwa kipindi cha misukosuko ya wenyeji na Wareno

ü  Kulikuwa na tungo zilizohidhiwa zilizowahusu Wareno, Migeni, Poatugei afila

ü  Tungo nyingine zilikuwa ni utendi wa Hamziyya, Siri Lasinari, Utendi wa Tambuka 1723 nyingi zilikuwa zikiwapa moyo Waswahili

ü  Waswahili walifanikiwa kuwaondoa wareno.

 

 

1750-1900

ü  Hiki kilikuwa ni kipindi cha nne, na kilikuwa ni kipindi cha utawala wa Waarabu

ü  Kulikuwa na migogoro mingi ya kivita katika utawala wa Waarabu

ü  Tabia za Mamwinyi, wafanya biashara, matajiri na wamisionari vilistawi

ü  Kipindi hiki kilitawaliwa na fasihi ya kidini ambayo ilitafakari theologia na falsafa ya maisha

ü  Kulikuwa na tendi nyingi zilizoibuka kuko Arabuni wakati wa mtume Muhamed. Mfn Shutaki, Angamia, Nakaa, Masahibu nk

ü  Pia kulikuwa na tungo za kitamaduni, mawaidha na tumbuizo. Mfn utendi wa Mwanakupona

ü  Washairi walijitokeza kuhusu mashairi ya kisiasa ambao ni Myaka bin Haji (1776-1840), huyu aliishi Mombassa.

 

KARNE YA ISHIRINI (20)

ü  Katika kipindi hiki uchapishaji wa magazeti na vitabu ulijitokeza. Kulikuwa na Asasi za kudai uhuru. Waandishi waliandika sana kuhusu kudai uhuru. Mfn Saada Kandoro

ü  Baada ya uhuru ushairi wa kisiasa ulienea zaidi kama vile Ngonjera na makue.

 

MAJARIBIO NA MABADILIKO KATIKA USHAIRI WA KISWAHILI

Senko (  ) anasema baada ya fahamu zake kufunguliwa alianza kuangalia mabadiliko katika ushairi.alidai kuwa kuwa kuwa dunia inabadilika hivyo na ushairi hauna budi kubadilika.

ü  Wangai Mwai (2008:73) fasihi hubadilika badilika katika kumbo na maudhui kwa hiyo ushairi wa Kiswahili sharti uruhusu mabadiliko yanapotokea.

 

MGOGORO WA USHAIRI WA KISWAHILI

ü  Baadhi ya washairi kama vile E.Kezilahabi, M.M Mulokozi, K.K Kahigi na wengineo walinza kuandika kazi za ushairi zisizo na urari wa vina na mizani

ü  Wengi walichukulia na kurudi nyuma kwa ushairi lakini waandishi hao waliona ni hatua ya maendeleo

ü  Hivyo mashairi yaliyotungwa kwa mfumo huo yalipata majina mbalimbali kama vile Makue, Mtiririko, Mapingiti. Nk

ü  Na hivyo watungaji wa mashairi haya waliwaita wanamapinduzi na wengine wakawaita wachochezi

ü  Ibrahim Noor Shariff (1988:183) amedai kuwa mzozo uliibuka pale wanamabadiliko  walipodai mambo matatu:

1)      Mbinu za kutunga mashairi zilikuwa chache mno

2)      Sharia za kutunga mashairi ziliwanyima uhuru wa kutunga

3)      Muundo wa tungo za kishairi uliokuwa wa Kiswahili hapo awali haukuwa na vina wala mizani, hivyo sharia si za lazima.

ü  Kauli hizi za wanamabadiliko zilipingwa sana na wanamapokeo ambao waliamini kwamba urari wa vina na mizani ndiyo roho ya ushairi, ruwaza ya vina na mizani ndizo zinazoufanya ushairi wa Kiswahili ujitambulishe.

Njogu na Chimerah (1999:113) wanadai kwamba mgogoro huu ulikuwa baina ya vijana na wazee waliokuwa wamekulia katika mazingira ya tungo za vina na mizani

MAWAZO YA WANAMABADILIKO KUHUSU USHAIRI

Mawazo yao kwa ujumla yalipingana kwa kiasi kikubwa na mawazo ya wanamapokeo japo kuna mazingira Fulani walifanana. Wanamabadiliko waliamini kuwa

v  Hakuna sheria za kutunga mashairi (Kezilahabi 1977:60), kila shairi lina njia yake ya kutunga na njia yake ya kutoa mawazo.

v  Dhamira/maudhui, mawazo, maadili na falsafa zitawale fani ya ushairi

v  Walidai kuwa mabadiliko ya umbo la ushairi yamefungamana na maendeleo ya historia ya jamii zetu, ni sehemu ya jamii yetu,hivyo kubadilika kwa ushairi wa Kiswahili si kitu cha kigeni

v  Vina na mizani ni kunga za utungaji zilizozuia ushairi wa Kiswahili kukua na kusambaa kwa mapana yake na marefu yake.

Soma Njogu na Chimerah (1999) ufundishaji wa fasihi.

 

II.                RIWAYA

Riwaya sio utanzu wa muda mrefu sana bali ni utanzu ambao umeanza kushika mashiko hivi karibuni kuanzia karne ya 19 huko Ulaya

Encloypedia hudai kuwa riwaya ni ubunilizi ya kinathari[1] inayotosha kuwa kitabu (kitabu kwa mujibu wa UNESCO ni chapisho lolote lenye kuanzia kurasa 48 na kuendelea.) bunilizi ya kifasihi ni ambapo matukio mengi yamebuniwa

Enclopedia Bratanica wanasema “riwaya ni masimulizi marefu ya kubuni ya kinathari yaliyochangamana kiasi na yenye kuzungumzia tajiriba[2] ya binadamu. Wanaendelea kusema kwamba kwa kawaida riwaya huwa na mfululizo wa matukio yanahusiana na yenye kulihusu kundi Fulani la watu kaka manthari mahususi

Mphahlele (1976) anasema kwamba riwaya fupi huwa na kati ya maneno thelathini na tano elfu (35,000) na hamsini elfu (50,000) na riwaya ndefu zaidi inaweza kuwa na maneno zaidi ya sabini na tano elfu (75,000)

Mhando na Balsidyawanadai kwamba katika riwaya lazima kuwe na mchanganyiko wa matukio na ujenzi wa wahusika naye Foaster (1949) anachangia kwa kusema kwamba riwaya lazima iwe na wakati.

SIFA ZA RIWAYA

v  Ni masimulizi ya kubuni

v  Ni hadithi ya nathari katika masimulizi

v  Ni ya mpangilio au hakuna mpangilio

v  Inafungamana na wakati (yaani yale yanayotendeka katika jamii hiyo)

v  Ina sifa ya urefu kama tulivyoona hapo juu

v  Ina mawanda mapana (yaani inaweza kuzungumzia mambo kwa upana sana)

v  Lazima kuwe na mchangamano wa visa mfano; katika riwaya ya Janga Sugu la Wazawa ina visa kama, ushirikina, vifo, mapenzi ya kweli na ya uongo,ndoa, mila nk

v  Ina wahusika wengi

 

CHIMBUKO LA RIWAYA

Riwaya imejazwa na mambo makubwa mawili:

1)      Fani za kijadi za fasihi

2)      Mazingira ya kijamii

 

1.      FANI ZA KIJADI ZA KIFASIHI

 

a)      Ngano-hadithi za kubuni zinazohusu wanyama, watunzi wengi wameathiriwa na ngano kw wasababu wanachota visa, mbinu za kifani , dhamira katika ngano (zinaonekana kwamba ni za kingano zaidi)

b)      Visasili-masimulizi ya kubuni ambayo yanaeleza juu ya maisha, asili, ya vitu na hatima yake. Kwa kawaida visasili huaminiwa kuwa ni hadithi za kweli

c)      Visakale-ni hadithi za kale zinazohusu kabila la kale, udini nk. M.M.Mulokozi anasema kuwa kila kabila lina visakale vyake. Katika riwaya visakale vinajitokeza katika riwaya ya Kisima cha Giningi

d)     Hekaya-ni hadithi za kusisimua kuhusu masaibu na matukio ya ajabu yasiyo ya kawaida, mara nyingi masaibu yanasababishwa na mapenzi, huwa ni ndefu kuliko hadithi nyingine lakini si ndefu kuliko riwaya. Katika taaluma ya Kiswahili ni riwaya ya Adili na Nduguze-Shaaban Robert, Riwaya ya Ubeberu Umeshindwa ya KIIMBILA( 1971)

e)      Tendi-ni hadithi ya kishairi kuhusu mashujaa wa kihistoria na wakubuni wa jamii au taifa.mfano Utendi wa Fumo Lyongo, kuna baadhi ya riwaya zimeiga mbinu za kiutendi. Mfano huko Ulaya Illiad Odyssey, Don Tuliv 1928, Toistoi (1828-1910). Mfano katika Afrika ni riwaya ya Ngugi wa Thiong’o ya Matigali.

f)       Masimulizi ya wasafiri-ilihusu masaibu waliyopata wasafiri mbalimbali. Mfano Riwaya ya kiingereza ya kwanza ni Robinson Kruso ilihusu habari ya mhusika mkuu ambaye alikuwamo katika merikebu iliyozama na akaokoka na kuamua kuiishi katika kisiwa peke yake. Katika Kiswahili kuna riwaya kama vile “utumwa”  “Kwa Heri Iselamagazi” hizi zote ziko katika muundo huu.

 

2.      MAZINGIRA YA KIJAMII

Katika karne ya 16 fani nyingi ziliendelea. Na mojawapo ya sababu ya kuendelea kwa riwaya ilikuwa ni:

1)      Ukuaji mkubwa wa shughuli za kiuchumi huko Ulaya baada mapinduzi ya kiviwanda

2)      Mageuzi ya kijamii na kisiasa yaliyofungamana na mabadiliko ya kiuchumi

3)      Ugunduzi wa teknolojia ya upigaji chapa

AINA ZA RIWAYA

Mpaka sasa hakuna vigezo maalumu vya uainishaji wa riwaya, kila mtaalamu huangalia kwa jinsi anavyoona yeye. Wengine wanaangalia muundo, mtindo, umbo, lengo/shabaha/historia.Madumula (2009:61 anasema “riwaya inaweza kuainishwa kifani, kidhamira, kihistoria na kiitikadi

Naye Mulokozi M.M (1996) anaonyesha michepuo miwili ya riwaya:

1)      Riwaya ya dhati(zinahusu masuala ya kijamii)

2)      Riwaya pendwa

Katika mhadhara huu tutaangalia riwaya kama alivyoainisha Madumula

1)      RIWAYA YA KITAWASIFU

v  Inahusu maisha ya mtu binafsi, yaani mwandishi mwenyewe, tatizo hapa ni uaminifu wa mwandishi, si rahisi kuandika kweli yote.

v  Mfano katika Kiswahili ni Riwaya “Maisha yangu baada ya miaka 50” ya Shaaban Robert

2)      RIWAYA YA KIWASIFU

v  Inahusu mtu mwingine na siyo mwandishi mwenyewe

v  Pia inahusu maisha ya mtu binafsi lakini ni maisha ya mtu mwingine na siyo ya mwandishi mwenyewe

v  Ni matukio ya kusisimua ambayo hayajawatokea watu wengine

v  Lengo kuu ni kueleza ugumu wa maisha ya maisha ya mhusika mkuu jinsi anavyopambana na maisha. Mfano Wasifu wa Siti Binti Saadi ya Shaaban Robert

3)      RIWAYA YA KIMAADILI

v  Ina lengo la kufundisha maadili mema ambayo ndiyo msingi katika maisha

v  Inahusu: mateso na uvumilivu, majuto baada ya kutambua kosa. Mfano katia Kiswahili ni Adili na Nduguze, Kusadikika, Kufikirika-zote za Shaaban Robert

4)      RIWAYA YA KIHISTORIA

v  Huchanganya historia halisi na sanaa ili kuleta maudhui Fulani

v  Hazielezi matukio yote ya kihistoria bali yale ya muhimu tu, yaliyoathiri mwelekeo na mwenendo wa jamii Fulani

v  Maudhui yake ni kumbukumbu ya mambo yaliyopita na dhamira zake huwagusa watu wengi. Mfano katika Kiswahili ni Riwaya ya Uhuru wa Watumwa ya J. Botela, Kwa Heri Iselamagazi ya J Mapalala, Zawadi ya Ushindi ya Beni Mtobwa, na Njozi iliyopotea ya Mung’ong’o

5)      RIWAYA YA KISOSHOLOJIA

v  Inahusu maisha ya watu na msisitizo wake ni katika mila, desturi na mabadiliko ya kijamii

v  Dhamira huanzia ngazi ya familia hadi kitaifa na hata kiulimwengu

v  Husawiri matatizo yaliyo katika jamii kwa kuonyesha chanzo chake. Mfano katika Kiswahili ni Dunia Uwanja wa Fujo ya Kezilahabi, Siku ya Watenzi Wote ya  Shaaban Robert na Harusi ya J.Safari

6)      RIWAYA YA KISAIKOLOJIA

v  Aina hii inaweka mkazo juu ya mikinzano ya ndani ya binadamu, kiakili, kinafsi na kijinsia

v  Huonyesha uwezo na udhaifu wa binadamu katika kuzikabili hali ngumu za maisha

v  Mhusika mkuu husukumwa katika ukingo wa aidha kufa ili ayaepuke matatizo au aishi na hayo matatizo. Mfano katika Kiswahili ni riwaya yaKIU ya Muhamedi S.Abdalah, Nyota ya Rehema ya huyu huyu Muhamed, Rosa Misitika ya Kezilahabi na Kichwa Maji ya Kezilahabi

7)      RIWAYA YA KIMAPINDUZI

v  Ni riwaya ambayo inajadili matatizo ya kisiasa

v  Inalenga kuleta mabadiliko ya kisiasa na kijamii

v  Mara nyingi riwaya za kimapinduzi zina mwelekeo wa kisosholisti ambapo mlengwa mkuu ni umma kushika hatamu

v  Mkazo upo katika ITIKADI kama msingi na dira ya kuongoza jamii

v  Wahusika wake wanatoka katika matabaka mbalimbali

v  Mfano katika Kiswahili ni riwaya ya KULI ya Adamu Shafi, Utengano ya Saidi A Mohamed, Dunia Mti Mkavu ya S.A.Muhamedina KASRI MWINYIFUAD ya Shafi A Shafi

8)      RIWAYA YA FALSAFA

v  Inajadili migogoro na maisha ya binadamu kwa kutafakari kwa mantiki na kwa kina kuhusu mambo yanayohusu maisha

v  Inajadili maswali kama vile: maana ya maisha nini? Hatima ya binadamu nini? Uhusiano wa binadamu na malaika ukoje?

v  Mifano ya riwaya ya kifalsafa ni: Mzingire, dunia uwanja wa fujo, Nagona, babu alivyokumbuka ya S.A Muhamedi, Riwaya ya Binadamu-ya K.w Wamitila. Riwaya hizi ni ngumu sana kuelewa zinaelezea, hata wahusika wake ni wa kufikirika zaidi, mfn wanyama nk

9. RIWAYA PENDWA

v  Ni riwaya ambazo hujishughulisha na masuala ya upelelezi, mapenzi na ujasusi, mara nyingine zinahusisha mapigano ya kimwili na ya kiakili kati ya mtu mmoja na watu wengi. Na mara nyingi huyu mtu mmoja huwashinda watu wengi

v  Riwaya hii inakuwa na mhusika mkuu mkweli (ambaye anapewa sifa ambazo zinazidi uwezo wa mwanadamu wa kawaida-yaani huwezi kumshinda kuanzia mwanzo hadi mwisho). Riwaya za namna hii zina chumvi nyingi. Mfano Riwaya ya “Kifo ni haki yangu” mhusika wake mkuu Camila anayekata nyeti za wanaume. Mfano mwingine ni  Simu ya kifa ya Faraji Katambula, Kikosi cha Kisasi ya E.Musiba. Mzimu wa watu wa kale, Kosa la Bwana Msa-vya Muhamedi S.Abdula-mhusika wake mkuu ni Msa

HISTORIA YA RIWAYA YA KISWAHILI

v  Utanzu wa riwaya umekuja baada ya utanzu wa ushairi na tamthiliya lakini ukuaji wake umekuwa kwa kasi kubwa. Inasemekana kwamba riwaya ya Kiswahili ilianza kujitokeza katika mwisho mwa karne ya kumi na tisa. Kwa nini ilichelewa sana hapa Afrika? Sababu yake ni kwamba

1.   Hadhira kubwa ya watu haikujua kusoma na kuandika

2.   Hadhira kubwa ya watu haikuweza kununua vitabu

3.   Jamii ya waswahili haikuwa na mitambo ya kupigia chapa na pia haikuwa na mfumo mzuri wa usambazaji vitabu(hapakuwa na printers nk)

Hivyo tunaona kwamba wakati wa ujio wa wakoloni ulisababisha kuanzishwa kwa baadhi ya vituo vya kupigia chapa, kwa mujibu wa Mulokozi ( ) anasema ukoloni uliweka mazingira ambayo yameweza kuilea riwaya. Mfano: hati ya maandishi ya Kirumi, mfumo wa usambaji wa vitabu

Mwanzo riwaya ya Kiswahili ilianza kujitokeza kwanza kama tafsiri ya kazi za nje, hivyo tafsiri nayo ilisaidia sana kuchipuka kwa riwaya. Kwa kadri tafsiri zilivyokuwa zikifanywa, waswahili walianza kuiga vitabu hivyo.

1930 KULIANZISHWA KAMATI YA LUGHA YA AFRIKA MASHARIKI

Kamati hii ilihimiza uandishi katika lugha ya Kiswahili kwa njia ya kushindana. Hivyo ilianzisha mashindano ya uandishi wa Kiswahili. Riwaya ya kwanza ya Kiswahili ilikuwa Uhuru wa Watumwa ya MBOTELA Ilichapwa mwaka 1934, riwaya nyingine ni riwaya ya “Mzimu wa watu wa kale”na “Simu ya Kifo”

MWAKA 1940 hadi 1960

Kulijitokeza riwaya ambazo zilikuwa zikifuata mkondo wa kingano.Njogu na Chimerah (2008) wanaeleza kuwa”kimaudhui riwaya nyingi zilikuwa na mambo ya kimila na tabia kama njia ya kutunza maadili. Miongoni mwa riwaya hizo ni Utu bora mkulima, Kufikirika, Kusaidikika, Adili na Nduguze na Siku za watenzi wote zote za Shaaban Roberti.

Kulikuwa na mambo yafuatayo:

Ukombozi wa bara la Afrika na ujenzi wa jamii mpya, hivyo maudhui yake yalikuwa ni ujenzi wa jamii mpya na:

     Kusuta ubinafsi na ukandamizaji

     Zilikuwa zikihakiki unyama wa maisha ya kimiji

     Zilikuwa zikiielekeza jamii katika mkondo wa kibinadamu katika usawa na ustawi. Mfano riwaya hizo ni LILA NA FILA, KABURI BILA MSALABA-iliandikwa na KAREITHI

Katika kipindi hiki pia kulijitokeza kundi la Riwaya Pendwa zilizohusu upelelezi na uharifu mfano Mzimu wa watu wa kale, Kisima cha Giningi, Simu ya Kifo

Zile za uharifu niMTAKA YOTE HUKOSA YOTE ya Leo Odera Omera, Tatizo Kisauni ya CHADHORO

MIAKA YA 1970 HADI 2000

v  Ni kipindi cha kupevuka na kushamiri kwa riwaya ya Kiswahili, katika kipindi hiki riwaya nyingi zilianza kujishughulisha na uongozi na usaliti wa kisiasa.

v  Njogu na Chimerah (2008) wanadai wasanii walianza kutafakari jinsi ukoloni ulivyoanza kufungua milango kwa watu wachache na kutumia mali kwa manufaa yao wenyewe

v  Katika kipindi hiki kuliibuka riwaya za kihistoria kwa mfano KWA HERI ISELAMAGAZI iliyoandikwa na Mapalala. Miradi Babu ya wazalendo.

v  Katika kipindi hiki kulizuka riwaya ya kifalsafa na ya majaribio. Mfano Nagona 1987, Mzingile(1991)-Kezilahabi. Riwaya ya Zilahiri na Zirani ya William

v  Katika kipindi hiki kulikuwa na ongezeko la riwaya ya vijana na watoto. Mfano wa riwaya hizo ni Mashujaa wa Kaza kamba-ya Shija (1980) wimbo wa Sokomoko (1990), Ngome ya Mianzi (1990), Ngoma ya Mianzi(1991) Moto wa Mianzi (1995) zote hizi ni za Mulokozi.

MAJARIBIO NA MABADILIKO KATIKA RIWAYA YA KISWAHILI

®Fasihi huithamini jamii kihistoria, kiitikadi, kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni na kijamii, na kwa kuwa jamii imekuwa ikibadilika badilika kimtazamo, fasihi nayo imekuwa ikibadilika kwa sababu jamii inabadilia. Na hivyo fasihi nayo inahitaji kupokea mabadiliko hayo ili kwendana na jamii husika.

®Mabadiliko katika riwaya (fasihi) yanatokea kwa sababu ya wasanii kutumia vionjo vipya katika kuziumba kazi zao. Kama anavyosema Khamisi (2007) anasema,mara moja tunaona neno kionjo linajisemea lenyewe kimya kimya juu ya mabadiliko ya utanzu wa fasihi. Lengo la mabadiliko hayo ni kwamba “chenye mwanzo hakikosi kuwa na mwisho”

®Utanzu wa riwaya ya Kiswahili haukuepuka mabadiliko. Sababu zilizobadilisha mabadiliko haya ni makali ya wembe wa kisiasa, mfano nchini Kenya makali ya kisiasa yalikuwa dhidi ya Masosholisti. Mfano wa riwaya ni Gamba la Nyoka,

®Majaribio na mabadiliko ya riwaya ya Kiswahili yalianza pale ambapo waandishi wengi wa Kenya na Tanzania walipoanza kukataa kukubali kila kitu walichokisikia. Walipoanzaa kukataa kanuni za jamii za ughunaji, hivyo wakaanza kuandika riwaya tofauti na za mwanzo.

®Madumula anawanukuu SCHOLES na APLLOE riwaya huweza kubadiliko kutokana na utanzu wenyewe kuwa hauna mashiko legelege na tepetepe, hubadilika badilika

®Hivyo kutokana na majaribio na mabadiliko katika riwaya ya Kiswahili tunaona upywa katika kazi za riwaya katika fani na maudhui yake. Kisanaa riwaya hizi zinachanganya uhalisia na falsafia. Mfano wa riwaya ya Kufikirika. Mfano mwingine ni UKIUSHI-Mtiririko haueleweki, na riwaya hizi zinakuwa na mwingiliano matini yaani kuchanganya kazi nyingi katika kazi moja.kisanaa pia zina wahusika wa kidhani

®Pia riwaya hizi zina mazingaombwe sana, kwa mfano katika Nagona lugha yake ni ya mafumbo, visasili, pia ni lugha inayoelekeza, haifafanui sana.kimaudhui riwaya hizi za majaribio inatazama matatizo kwa mtazamo wa ndani. Inashughulikia masuala ya ulimwengu wote, riwaya hizi pia kimaudhui zinaitetea dunia dhidi ya maangamizi ya uovu mkubwa.

 

3.      TAMTHILIYA NA DRAMA

Kumekuwa na mkanganyiko kati ya dhana hizi mbili, watu wamekuwa wakizichanganya sana.

·         Tamthiliya  ni drama na kinyume chake

·         Tamthiliya ni drama lakini si drama zote ni tamthiliya

 

A.    TAMTHILIYA

·         Mulokozi (1999:88) tamthiliya ni kazi iliyokusudiwa kutendwa jukwaani kwa ajili ya hadhira fulani

·         Tamthiliya huitwa mchezo wa kuigiza. Istilahi hii tamthiliya imetokana na neno methali lenye maana ya mfano/ishara ya kitu

·         Wamitila (2003)tamthiliya ni kazi ya kidrama na ya kimaongezi ambayo huigizwa mbele ya hadhira/kazi iliyoandikwa ili kusomwa

·         Kimuundo tamthiliya hudhihilika katika:

®matendo na maonyesho, mazungumzo huchukua sehemu kubwa katika uwasilishwaji wake wa maudhui (huwa katika diolojia)

®haiweki msisitizo mkubwa katika uwasilishwaji wake jukwaani wakati drama inaweka msisitizo mkubwa katika uwasilishwaji wake

®Penina Mhando anadai kuwa “Tamthiliya ni ule utungo unaoweza kuwa umeandikwa au haukuandikwa ambao ambao unaliweka wazo linalotaka kuwasilishwa katika umbo la tukio la kiliwezesha kutendeka mbele ya hadhira”

·         Kutokana na sifa hii ya kutendeka jukwaani tamthiliya inawekwa kwenye kundi la sanaa za maonyesho(Mulokozi)

 

SANAA ZA MAONYESHO

Mohamedi na Balysidya wanasema kuwa sanaa za maonyesho ni kitendo chochote chenye sifa 4

a)      Mchezo

b)      Mchezaji

c)      Uwanja wa kutendea

d)     Watazamaji

©tamthiliya ni andiko la kiuigizaji linalotoa simulio kwa kuonyesha maneno na matendo

B.     DRAMA

Wamitila (2003) anasema “ ni aina ya utanzu wa fasihi ambao kimsingi hudhamiriwa kuigizwa mbele ya hadhira” inaweza kuwa imeandikwa au haikuandikwa lakini msisitizo wake ni kuigizwa

·         Msingi mkuu wa drama ni utendaji na utanzu huu umebuniwa kwa ajili ya thieta

·         Wahusika hupewa majina ya kuigiza mbele ya hadhira

Iwochukuu (2000) anasema “drama ni mabadiliko, ubunifu na usawiri wa uhalisi jukwaani. Msingi mkuu wa drama ni matendo. Hoja hii imeungwa mkono naAristotle anayeifafanua drama kama uigaji wa matendo

·         Bretcht anasisitiza kuwa drama si uigaji wa matendo pekee pia ni chombo cha ufafanuzi wa hali za kijamii, chombo cha mabadiliko ya kisiasa na kiuchumi

·         Kitendo huitwa drama endapo kitendo hicho ni mwigo wa kitendo cha kilichokwishatangulia.

DRAMA ZA KIJADI

Jamii ya waafrika ikiwemo ambayo utamaduni wake ulikuwa haujaingiliwa na wakoloni ilikuwa na sanaa ya maonyesho zilizogawanyika katika makundi mbalimbali. Balisdya na Mhando walianisha aina mbalimbali za drama hizo

1.      SHEREHE

·         Zilihusishwa na kundi moja kwenda kundi jingine mfano. Jando na unyago, jina kwa mtoto, kuota meno nk

·         Ziliambatana na madaraka kwa mwanajamaii ya mwanajamii aliyeingia katika kundi jipya. sherehe ziliwekwa katika katika umbo la vitendo na vikapewa uzuri wa kisanaa

2.      NGOMA

·         Mhando na Balisdya wanasema ni chombo, sherehe au uchezeshaji wa viungo vya mwili. Malengo yake ni kuburudisha

3.      MASIMULIZI YA HADITHI

·         Katika usimuliaji wa hadithi kuna vipengele vya kidrama vinavyojitokeza. Yaani:

v  Usimuliaji

v  Uigizaji

v  Uimbaji

v  Muziki

4.      KUSALIA MIUNGU

·         Jamii fulani inapopata mafanikio au matatizo fulani ndipo huenda kutambikia miungu yao kwa kushukuru au kuomba kutatuliwa matatizo yao

5.      MAJIGAMBO

·         Masimulizi ya kujigamba ya mtu kuhusu mambo ya kishujaa aliyopata kuyatenda maishani mwake

·         Kwa kawaida hutumia lugha ya kishairi na masimulizi huambatana na vitendo vya majigambo yenyewe.

·         Pia yaliambatana na matumizi ya maleba

 

AINA ZA TAMTHILIYA

1.      TANZIA

·         Ni tamthiliya yenye huzuni inayogusa hisia za wasomaji kiasi cha kuogopesha na kumuonea huruma mhusika mkuu ambaye hupatwa na masahibu/matatizo/majanga hayo

·         Msingi mkuu inalenga msomaji kupata hisia

·         Mhusika mkuu huwa ni maarufu

·         Aristotle anasema kuwa “ mhusika mkuu lazima atoke katika familia yenye nasaba bora/tabaka la juu”

·         Si tanzia zote mhusika anatoka tabaka la juu. Mfano KIFO KISIMANI-mhusika mkuu hapa anatokea katika tabaka la chini kabisa

 

Misingi ya utokeaji wa tanzia

·         Iamushe hisia za woga na huruma miongoni mwa hadhira

·         Shujaa lazima awe mtu mwema, sura nzuri,umbo zuri, ili yanayomtokea yasitarajiwe

·         Mhusika huonyesha kuumia kadri mtu anavyoonekana kuwa ni mwema na ana umbo zuri.

·         Anguko la shujaa huja kutokana na uamuzi wake ama kosa lake mwenyewe

·         Katika tanzia ya kirasimi shujaa hutoka katika nasaba bora

2.      RAMSA/KOMEDI

·         Ni tamthiliya ambayo inachangamsha na huishia kwa kufurahisha/ni tamthiliya ya vichekesho, hii haina maana kwamba haina maudhui mazito ndani yake.

·         Inashughulikia mambo yale yale yanayoweza kushughulikiwa na tanzia. Mfano masuala ya unafiki,uzembe, wivu nk, hata hivyo inayashughulikia kwa namna tofauti na tanzia

·         Kwa kawaida wahusika wa Ramsa huumbwa vibaya kuliko walivyo

·         Udhati wa ramsa si kwamba usanii humalizika katika kicheko/furaha zaidi ni kuishia mhusika mkuu kufanikiwa

 

shujaa wa kiramsa

·         Si lazima awe mtu maalum/mbabe au shujaa, anaweza kuwa mtu wa kawaida

·         Kwa mujibu wa Aristotle anasema mhusika wa ramsa lazima awe mtu wa wastani chini ya wastani, awe ni mtu ambaye hatarajiwi kujitokeza na mtu wa nasaba duni na matendo yake yawe ya ucheshi

·         Ni lazima awe mtu ambaye akifanikiwa wasomaji au watazamaji watafurahi

 

uhusika wa wahusika wa ramsa

·         Ramsa inawahusu watu wa kawaida kuliko ilivyo tanzia

·         Inawahusu watu wa kipato cha kati na cha chini

·         Na dhamira zote huelekezwa kwa watu wa kipato cha chini na duni. Mfano walalahoi

AINA ZA RAMSA

 

a)      UTANI

·         Ni aina ya ramsa ambayo mambo inayozungumzia yanaokana kuwa ya kipuuzi

·         Mambo hugeuzwa kuwa kinyume kabisa na jinsi yalivyo

·         Kwa kawaida sura za wahusika hubadilishwa kuwa kama vinyago

·         Lengo kuu ni kuchekesha-ambalo ndilo haswaa, lengo la tamthiliya ya ramsa

 

b)      RAMSA ZA MAPENZI/MAHABA

·         Hizi zinahusu mapenzi ambapo wapendanao huwekewa vikwazo kama vile fedha, elimu, din, kabila nk

·         Wahusika hawa hushinda vikwazo hivyo

c)      TASHTITI/DHIHAKA

·         Zinalenga kwa viongozi wa kisiasa au dini

·         Zinawahusu matapeli, wanafiki, wala rushwa, ni

·         Mhusika mkuu anakuwa na sifa za utapeli nk

·         Lengo kuu ni kumdhihaki huyu kiongozi ili aachane na tabia hizo

·         ni njia ya walalahoi kupeleka malalamiko yao kwa viongozi

SIFA ZA RAMSA

·         Shartiivutie akili na siyo hisia

·         Ni lazima kuwa na matendo bila kufikiria hii itapelekea msomaji au mtazamaji kujua kwamba wahusika hawa hawana akili

·         lazima iwe na hali ya utu (ikitukumbusha ubinadamu wetu)

·          sharti iwe na mila na desturi ambazo hadhira inazifahamu toka katika jamii yake

·         Hadhira isiogope au kupata uchungu kwa sababu hii sio lengo lengo la ramsa

·         Wahusika wa ramsa hujaribu kuepuka vikwazo ambavyo vimewekwa

·         Inaonyeshahaja ya  kuikomboa nafsi

Mfano wa ramsa ni kama vile MFALME JUHA

d)     TANZIA-RAMSA

·         Hii ni tamthiliya ambayo inaonyesha mabaliko ya aina fulani yanayogeuza matukio ya tanzia kuwa ya ramsa

·         Ni tamthiliya inayochanganya vipengele vya tanzia na ramsa

·         Hutumiwa sawa na tamthiliya ya kibwege-hii ni tamthiliya ambayo inaonyesha kwamba kicheko au furaha ndiyo jibu pekee la maisha kwa watu ambao hawana imani na maisha ambao kwao misingi dhabiti ya maisha imeondoleo. Mfano tamthiliya ya AMEZIDI ya S.A Mohamedi

e)      MELO-DRAMA

 

CHIMBUKO , MABADILIKO NA MAENDELEO YA TAMTHILIYA YA KISWAHILI

CHIMBUKO LA TAMTHILIYA

 Tamthiliya chimbuko lake duniani kote linashahibiana/zinapatikana duniani kote na kuonekana katika maumbo tofauti tofauti. Tamthiliya inahusishwa sana na visakale na matendo ya kidini. Katika bara la Ulaya tamthiliya inahusishwa na miviga ya kidini katika jamii ya Wayunani/Wagiriki wa zamani/ancient Greek. Miviga hii katika jamii ya wayunani iliambatana na dua ya kuzaliwa..mpaka kufa na kuoza na kuwa binadamu tena

 

1.      Huko India

tamthiliya zilitokana na tenzi zilizoitwa Mahabharata na ………pia zilitokana na miviga zilizoendana na utendi wa tendi hizo kutika mahekalu ya kidini

2.      Kule Japani na China-drama inatokana na dansi na miviga ya kidini baadaye miviga hii ilijitenga na dini na kuanza kujishughulisha na sanaa

3.      Katika Afrika-maigizo ya tamthiliya yalikuwa yanapatikana huko Misiri na maigizo haya yalikuwa yanahusu kufa na kufufuka kwa mungu wa wamisiri aliyeitwa osiais. Miviga hii ilikuwa inaigizwa kila mwaka kwa miaka kama elfu mbili. Pia katika Afrika kulikuwa na maigizo ambayo hayakuwa yameandikwa lakini yalikuwa ni sehemu ya matendo ya kijamii yaani miviga na ngoma. Kulikuwa na tamthiliya bubu, maigizo ya watoto na maigizo ya watani. Drama hizi zilikuwa zikifungamanishwa na fasihi simulizi

 

Hivyo tamthiliya inatokana na mambo makuu matatu

a.       Miviga na viviga vya kijamii, na dini pamoja na tendi

b.      Usawilishaji wa maisha ya kawaida kwa ajili ya burudani, elimu nk

c.       Sanaa za maonyesho za kijadi; ngoma na dansi

 

MAENDELEO YA TAMTHILIYA YA KISWAHILI  9/1

Maendeleo ya tamthiliya yamegawanywa katika vipindi vitatu

1.      KABLA YA UKOLONI:

Ø  Kulikuwa na tamthiliya ambazo hazikuandikwa lakini zilikuwa zikionyeshwa katika matukio mbalimbali kama vile jando na unyago, arusi nk

Ø  Hazikuwa na muundo wa Kiaristotle: mwanzo, kati na kilele

2.      KIPINDI CHA UKOLONI

Ø  Kilianza mwaka 1860-1960

Ø  Kipindi hiki kilikuwa na aina mbili mpya ya tamthiliya

a.       Kizungu —zililetwa mwanzoni mwa utawala wa wazungu. Zilikuwa na malengo mawili: 1. Kuwaburudisha wazungu  2. Kufunza imani ya kikristo.

®    Huko Kenya ilianza kuonyeshwa/kuigizwa Nairobi na mombassa kabla ya vita ya kwanza

®    Tanzania zilianza kuigizwa mashuleni mwaka 1920

®    Katika kipindi hiki kulianzishwa vikundi mbalimbali za kuigiza tamthiliya ya kizungu. Mfano hapaTanzania kundi lilianzishwa ni Dar es salaam player 1947. Na kundi lingine ni Arusha Little Theater

®    Na huko Kenya kulikuwa na kundi la National Theater 1952

Makundi haya yalitawaliwa na michezo ya wageni

b.      Vichekesho: --zilikuwa ni tamthiliya gezwa.

®    Zilianza mwaka 1920 kwa ajili ya kuwaburudisha wenyeji

®    Miongoni mwa vichekesho maarufu ni kile cha KIOO

c.       Mwisho ilijitokeza aina ya tatu: TAMTHILIYA ANDISHI ZA KISWAHILI

®    Zilianza kujitokeza mwaka 1950

®    Zilianza kutungwa mwaka 1952

®    Shughuli za tamthiliya zilikuwa zikisimamiwa na Gramah Gyslop-huyu alikuwa ni mkoloni huko Kenya aliyepewa kusimamia tamthiliya..mwaka 1954 yeye mwenyewe alianza kuandika. Mfano ni tamthiliya ya kuigizwa ya AFADHALI MCHAWI

®    Henry Huria aliandika tamthiliya iliyoitwa: NAKUPENDA LAKINI nayo iliigizwa mwaka 1954 na kuchapwa 1957

®    Baada ya Henry motisha ya kutunga tamthiliya iliongezeka. Kulijitokesha watu wengi wa kutunga. Mfano GERSHOM NGUGI, tamthiliya ya NIMELOGWA NISIWE NA MPENZI

®    NYOIKE aliandika tamthiliya ya MAISHA NINI iliigizwa mwaka 1955

3.      KIPINDI CHA UHURU

Vile vile kuna aina tatu

1.      Tamthiliya za kizungu-ziliendelea kuigizwa hata baada ya uhuru lakini umaarufu wake ulipungua sana kwa upande wa tamthimini

®    Katika kipindi hiki tamthiliya za kizungu zilianza kutafsiriwa mfano, JULIUS KAIZA na  ‘MABEPARI WA VENIS- Ilifasiriwa na mwl Nyerere.

®    Nyingine ni MAKBETH iliyotafsiriwa na S.S.MUSHI

®    MKAGUZI MKUU WA SERIKALI iliyotafsiriwa na  C.MWAKASAKA

***Tammthiliya zilizowahusu waafrika ni Tamthiliya ya Ngugi wa Thiong ya THE BLACK HERMIT-MTAWA MWEUSI

***MASAHIBU YA NDUGU JERRO

***I WILL MARRY WHEN I WANT-na  Ngugi

2.      Vichekesho

®    Vilikuwa vikizungumzia matatizo ya watu wa kawaida. Mf. Ukosefu wa kazi, uhalifu

®    Vilikuwepo pia vichekesho vya kisiasa.mf siasa ya ujamaa

®    Vilikuwepo baadhi zilianzishwa na wanasiasa

3.      Tamthiliya andishi ya Kiswahili

®    Baada ya uhuru kulitokea mashindano yaliyosimamiwa na Youth Dramma ambayo yalikuwa mashindano ya uandishi wa drama.

®    Ibrahimu Husein katika kazi yake ya WAKATI UKUTA ni matokeo ya mashindano hayo.

®    1970-1994 Kulichapishwa kazi nyingi za tamthiliya ya Kiswahili. Mfano wa kazi hizo ni KINJEKITILE, MASHETANI 1971, JOGOO KIJIJINI NA….1989, ARUSI 1980, KWENYE UKINGO WA THIM 1989

®    Zingine za Penina Mhando: HATIA, 1972. TAMBUENI HAKI ZENU 1984 NGUZO MAMA 1982

®    Mwingine. E.mbogo: GIZA LIMEINGIA 1980, TONE LA MWISHO 1981, NGOMA YA NG’WANAMALUNDI 1988, MORANI 1983, SUNDIATA 1985

HUKO KENYA:

THOMAS M,---BAHATI NASIBU 1971

C.N CHACHA---MKE MWENZA 1981

JAY KITHO------MALIMWENGU ULIMWENGUNI 1983

                            BIBI ARUSI 1985

 

MAJARIBIO KATIKA TAMTHILIYA YA KISWAHILI

Tunapozungumzia majaribio katika tamthiliya ya Kiswahili tunazungumzia upya wa kazi ya tamthiliya. Waandishi waliokuwa wakiandika kipindi kile walikuwa wakiongozwa na mwongozo wa Kiaristotle. Ni vigumu sana kuona tofauti yoyote unapozingalia kazi hizi labda kwa upande wa maudhui.

Kuanzia mwaka 1970 watunzi wa tamthiliya ya Kiswahili hawakuridhika kabisa na utunzi wa mbinu ya kiaristotle, hivyo walianza kuchota mbinu kutoka katika sanaa za kijadi. Ukiangalia tamthiliya kama vile za Penina Mhando, mfano Nguzo Mama, ina muundo tofauti kabisa-ni mtindo wa ngano, hivyo hii nayo ni tamthiliya ya majaribio

Pia kuna mbinu ya majigambo, mfano ya Penina Mhando ya HARAKATI ZA UKOMBOZI, lakini pia SUNDIATA imetumia majigambo. Pia tamthiliya ya KIVULI KINAISHI imetumia majigombo

Kuna matumizi ya TENZI SIMULIZI katika baadhi ya tamthiliya za majaribio. Mfano ni MKWAVA WA UHEHE

Kuna matumizi ya uganga. Mfano NGOMA YA NG’WANAMALUNDI



[1]nadhari-ni maelezo ya kina yanayoelezea jambo kwa mapana (hii inafanya itofautiane na ushairi na tamthiliya

[2] Tajiriba ni uzoefu alio nao mtu. Uwe mbaya au mzuri

No comments:

Post a Comment