Saturday

Ripoti: nusu ya wanawake katika nchi zinazoendelea hawana uhuru na miili yao

0 comments

 




  • Wananyimwa haki ya kuamua kuhusu miili yao ikiwemo tendo la ndoa, uzazi wa mpango au kutafuta huduma za afya.
  • Ni asilimia 55 pekee ya wanawake katika nchi hizo wamepewa na uwezo wa kusema ndiyo au hapana kwenye tendo la ndoa. 
  • UNFPA yasisitiza kuimarishwa kwa mifumo ya kisheria na afya kuwapa uhuru wanawake. 

Dar es Salaam. Ripoti mpya ya Shirika la Umoja wa Mataifa la idadi ya Watu (UNFPA) imeeleza kuwa takribani nusu ya wanawake wote katika nchi zinazoendelea duniani wananyimwa haki ya kuamua kuhusu miili yao ikiwemo tendo la ndoa, uzazi wa mpango au kutafuta huduma za afya.

Pia imebaini kuwa wanawake walazimishwa kufunga vizazi, kupimwa bikira na kufanyiwa ukeketaji.

Ripoti hiyo ya hali ya idadi ya watu duniani iliyotolewa mapema mwaka huu/2021 imejikita kupima nguvu za wanawake kufanya  maamuzi yao wenyewe kuhusu miili yao na kiwango ambacho sheria za nchi zinaunga mkono au zinaingilia haki ya mwanamke kufanya maamuzi. 

Ripoti hiyo inaonyesha kuwa katika nchi ambazo taarifa zinapatikana asilimia 55 pekee ya wanawake wamepewa uwezo kamili wa kufanya uchaguzi juu ya huduma za afya, uzazi wa mpango na uwezo wa kusema ndiyo au hapana kwenye tendo la ndoa. 

“Ni asilimia 71 tu ya nchi zinahakikisha upatikanaji wa huduma ya uzazi kwa kwa ujumla na ni asilimia 75 tu ya nchi ambazo kisheria zinahakikisha upatikanaji kamili, ulio sawa wa uzazi wa mpango,” imeeleza taarifa ya UNFPA kuhusu ripoti yake.  




    UNFPA imeeleza kuwa ukosefu huo wa uhuru wa mwili una athari kubwa kwa  wanawake na wasichana kwani inaenda mbali zaidi kuvuruga uzalishaji wa uchumi, kupunguza ujuzi, na kusababisha gharama za ziada kwa huduma za afya  na mifumo ya kimahakama.

    "Ukweli kwamba karibu nusu ya wanawake bado hawawezi kufanya maamuzi yao kuhusu ikiwa watafanya tendo la ndoa au la, kutumia uzazi wa mpango au kutafuta huduma ya afya inapaswa kutukasirisha sisi sote. 

    “Kimsingi, mamia ya mamilioni ya wanawake na wasichana hawamiliki miili yao wenyewe. Maisha yao yanatawaliwa na wengine,” amesema Mkurugenzi Mtendaji wa UNFPA, Dk Natalia Kanem.

    Dk Kanem ameshauri mifumo ya sheria na elimu ya uzazi na jinsia iimarishwe na kusisitizwa kwenye nchi zinazoendelea ili kuwapa uhuru wanawake ambao ni haki zao za msingi.
     

    No comments:

    Post a Comment