Mwaka 2021/22, Serikali itawekeza Sh10.6 bilioni kwa ajili ya kuongeza uzalishaji wa mbegu bora zikiwemo za mafuta ya kula.- Mbegu hizo zitaongeza uzalishaji wa mafuta ya pamba, alizeti na mawese kwa wakulima.
- Tanzania hutumia Sh474 bilioni kuagiza mafuta ya kula kutoka nje ya nchi kila mwaka.
Dar es Salaam. Huenda tatizo la uhaba wa mafuta likawa historia Tanzania baada ya Serikali kusema inaelekeza nguvu zake katika uzalishaji wa mbegu bora zikiwemo za mazao ya mafuta.
Kwa mujibu wa Wizara ya Kilimo, mahitaji ya mafuta ya kula nchini Tanzania yanakadiriwa kuwa tani 570,000 kwa mwaka huku uzalishaji unakadiriwa kufikiwa wastani wa tani 205,000.
Hali hiyo inafanya Tanzania iwe na upungufu wa wastani wa tani 365,000 na kusababisha nchi kutumia wastani wa Sh474 bilioni kuagiza mafuta ya kula kutoka nje ya nchi kila mwaka.
Naibu Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe amesema katika mwaka 2021/22, Serikali itawekeza Sh10.6 bilioni kwa ajili ya kuongeza uzalishaji wa mbegu bora za mazao zikiwemo mbegu za mafuta ya kula.
“Mbegu hizo zitasambazwa kwa wakulima wa mikoa yote inayozalisha mazao hayo ukiwemo wa Mara kupitia kwa ASA na wasambazaji binafsi,” amesema Bashe leo Mei 10, 2021 bungeni jijini Dodoma.
Uzalishaji huo utafanyika kwa kwa kuimarisha miundombinu ya umwagiliaji na kupanua mashamba ya mbegu ya Wakala wa Mbegu za Kilimo (ASA).
Aidha, Bashe ambaye pia ni Mbunge wa Nzega Mjini amesema Serikali iko tayari kufanya majadiliano na kampuni au watu wenye nia ya kuwekeza kwenye uzalishaji wa mbegu ili kuweka utaratibu wa kupunguza gharama za kuzalisha mbegu za mazao nchini.
Bashe alikuwa akijibu swali la Mbunge wa Bunda, Boniphace Getere ambaye alitaka kufahamu sababu zinazoifanya Tanzania kutokujitosheleza kwa mafuta ya kula.
“Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha mikoa yenye ardhi ya kutosha ya kuzalisha zao la alizeti hususani Mkoa wa Mara inatambuliwa rasmi na kupewa mahitaji yote ya mbegu,” amehoji Getere katika swali lake.
Kwa mujibu wa naibu waziri huyo, uhaba wa mafuta ya kula ni matokeo ya uzalishaji mdogo wa mazao ya mbegu za mafuta za alizeti, michikichi na pamba unaochangiwa na matumizi yasiyoridhisha ya teknolojia.