Friday

UCHAPISHAJI NA UCHAPAJI-SEHEMU ZA KITABU: TAARIFA MUHIMU TUNAZOTARAJIA KUZIKUTA KWENYE KITABU

0 comments


MADA: *TAARIFA ZA MSINGI TUNAZOTARAJIA KUZIKUTA KWENYE KITABU*

Karibuni katika somo litakalojikita katika mada ya tatu. Tuanze kwanza kwa kuelewana kwamba somo la leo halina vigezo funge (strict parameters). Yaani mambo nitakayoyazungumzia huenda mwingine akaona si muhimu kutokana na mtazamo wake. Lakini, ukweli unabaki palepale kwamba kuna taarifa ambazo tunapotazama kitabu tunatarajia tuzikute.

Aidha, kitabu ni kipana na kukizungumzia chote si rahisi. Hivyo, somo letu liongozwe na vigezo viwili vitakavyotusaidia kubainisha taarifa hizo muhimu katika kitabu kizuri. *Mosi, tutumie kigezo cha uzito zaidi cha taarifa. Pili, tutumie kigezo cha taarifa husika kuwa katika vitabu vingi* au katika kila kitabu.

*Kwa nini tumeanza kwa kuweka vigezo vya taarifa za kitabu?*

Sababu kubwa ya kufanya hivi ni kwamba kuna aina nyingi sana za vitabu. Kwa mfano, tuna vitabu vya mkusanyo wa sala tofauti, tuna vitabu vya kuelezea historia ya watakatifu, tuna vitabu vinavyofafanua mafundisho ya Kanisa, tuna vitabu vinavyojadili changamoto za maisha ya jamii, tuna vitabu vya Kamusi, kwa kutaja aina chache tu. Kwa mazingira haya, kuna baadhi ya vitabu vina kaida ambazo ni za kipekee. Fikiria kwa mfano *Kamusi ya Liturjia ya Kanisa Katoliki* aliyotuandikia Pd. Stefano Kaombe. Mpangilio wa baadhi ya mambo hauwezi kufanana na wa kitabu cha kawaida. Ndiyo maana nikasema kwamba tuwe na kigezo ambacho, pamoja na tofauti mbalimbali za vitabu, lakini taarifa hizo walau tuzikute kwenye kila kitabu.

Kwa kuzingatia vigezo hivyo viwili, kitabu kilichokamilika kinatarajiwa kiwe na sifa zifuatazo:-

*1. Jina la kitabu*
Katika hali ha kawaida, kila kitabu kinapaswa kuwa na jina lake. Jina hilo linatakiwa kuchaguliwa kwa kuzingatia mambo makubwa matatu. Mosi, jina liakisi maudhui ya kitabu. Pili, liandikwe kwa namna ya kumvutia msomaji. Kumbuka mtu akienda maktaba au sokoni, atakutana na vitabu vingi. Hivyo, jina linalovutia humvuta pia msomaji kuchagua kitabu husika. Tatu, liandikwe kwa uwekevu. Uwekevu ni kuandika maneno machache lakini yanayobeba maana pana au yanayofikirisha. Siyo mtu aandike nusu ya jalada lote halafu aseme ni jina la kitabu.

*2. Jina la mwandishi wa kitabu*
Msomaji anaposoma jina la kitabu wakati mwingine hutamani kufahamu nani aliandika kitabu husika. Hivyo, akiona jina la mwandishi kama anamfahamu, huvutiwa kununua. Hata hivyo, hii isichukuliwe kwamba jina la mwandishi linawekwa kwa ajili ya kuwavutia wasomaji. Hapana. Jina la mwandishi ni muhimu pia hata kwa ajili ya kurejelea kitabu husika. Mtu akisoma kitabu akatamani kutumia maarifa yako, atahitaji kukunukuu kwa kukutaja majina. Sasa kama kitabu hakina jina, zoezi halitawezekana. Pia, hata katika uhifadhi wa vitabu kielekroniki, nao unahitaji jina la mwandishi. Yapo mengi kuhusu jina la mwandishi, lakini haya yanatosha kudokeza umuhimu wa taarifa za jina.

*3. Jina la Mchapishaji (ikibidi na Mchapaji pia)*
Katika uchapishaji ambao ni rasmi, Mchapishaji ana nafasi muhimu sana. Katika uchapishaji hasa wa kitaaluma, wasomi wanapochagua vitabu huangalia nani kwanza kakichapisha. Kama nilivyodokeza katika mada ya kwanza, Wachapishaji wanachukuliwa kama watu wanaoaminika kutoka na uhakiki na michakato wanayofuata katika kuchapisha kitabu.  Aidha, katika vitabu vingi, ni muhimu kupata taarifa za Mchapaji. Msomaji anaposoma kitabu, wakati mwingine hutamani kufahamu nani aliyechapa hicho kitabu. Hii inamsaidia naye kufahamu kwamba akitaka kuprinti kitabu chake aende kwa nani.

*5. Mwaka wa kuchapishwa kwa kitabu*
Mwaka wa kuchapishwa kwa kitabu una maana na umuhimu wake. Kwa mfano, unaporejelea kitabu lazima uoneshe mwaka. Watafiti wanapopitia vitabu lazima waangalie kitabu kimechapishwa lini. Zipo sababu nyingi kiutafiti kwa nini mwaka wa chapisho unahitajika. Maelezo hayo niliyotoa yatoshe tu kutujuza kwamba kitabu kinapaswa kuonesha mwaka wa kuchapishwa.

*6. Mahali kilipochapishwa kitabu*
Katika utamaduni wa uandishi, taarifa ya wapi kitabu kilichapishiwa ni muhimu. Mojawapo ya umuhimu ni kwamba wakati wa urejeleaji wa kitabu mahali kilipochapishiwa ni lazima pafahamike. Tunaposema mahali kilipochapishiwa kitabu hatumaanishi nchi hasa. Kimataifa wanahitaji jiji au mji. Kwa mazingira yetu hapa Tanzania tunaweza kusema basi jiji au mkoa. Hebu tutazame mfano wa urejeleaji hapa chini kwa mtindo wa APA.πŸ‘‡πŸΌπŸ‘‡πŸΌπŸ‘‡πŸΌ

Kaombe, S. (2016). *Kitubio: Chemchemi ya huruma ya Mungu.* Dar es Salaam: Stefano Kaombe.

Kamugisha, F. (2013). *Fadhila na sifa za Bikra Maria.* Limuru: Franciscan Kolbe Press.

Mbiku, D. H.(2007). *Bikira Maria mshiriki wa ukombozi (Co-Redemprix): Kwaresma na msamaha.* Dar es Salaam: Deogratias Hukumu Mbiku.

Bakize, L.H. (2020). *Mtu akifa leo, anakwenda wapi?* Dar es Salaam: EWCP.

Katika mifano ya urejeleaji wa kitabu hapo juu, tunaona kwamba taarifa nilizoeleza awali ni muhimu. Ukitazama mpangilio wa taarifa za urejeleaji utabaini taarifa hizi: πŸ‘‡πŸΌπŸ‘‡πŸΌπŸ‘‡πŸΌ

1. Jina la ukoo la mwandishi na herufi za majina mengine.

2. Mwaka wa uchapishaji.

3. Jina la kitabu cha mwandishi.

4. Sehemu kitabu kilipochapishiwa (jiji au mji).

5. Mchapishaji.

*7. ISBN na Bakodi*
Kama tulivyoona katika somo la pili, sote tunaweza kukubaliana kwamba uandishi wa kisasa unahitaji kuweka ISBN na Bakodi kwenye kitabu. Matumizi yake nadhani niliyafafanua kwenye somo lile.

*8. Mawasiliano ya mwandishi au mchapishaji*
Kuandika kitabu ni kuwasiliana na wasomaji wako. *Hivyo, wasomaji kama walaji wa chakula chako, wakati mwingine wanahitaji kukupatia maoni kuhusu kazi yako. Kama hakuna mawasiliano yako au ya Mchapishaji, watakupataje?* Kwa hiyo, ikiwa kitabu chako kinasambazwa na Mchapishaji, lazima kuwe na mawasiliano yake kwenye kitabu chako ili wasomaji wakitaka kumpata mwandishi iwe rahisi. Ikiwa umechapisha mwenyewe, basi wewe ndiye Mchapishaji. Hapo unapaswa kuweka mawasiliano yako kwa ajili ya kupokea maoni au mawazo ya wasomaji wako. Pamoja na changamoto zote za usalama (kwa kuweka wazi mawasiliano yako), lakini jambo hili ni muhimu sana kwa uandishi wenye tija na endelevu.

*MWISHO WA SOMO*
Kama nilivyotangulia kusema, kitabu kina mambo mengi. Hapa sijazungumzia umbo la kitabu na mjengo wa nyama (maudhui). Hayo tutayagusagusa mbele ya safari. Haya ni machache ambayo pengine nadhani ni ya muhimu katika kukamilisha taarifa za kitabu.

*KARIBUNI TUJADILI KUHUSU SOMO*

*©L.H. Bakize* (13.03.2020)
(Mwalimu wenu)
============

No comments:

Post a Comment