Wednesday

Maana ya mrabaha katika uchapishaji na uandishi

0 comments


MRABAHA KATIKA UANDISHI NA UCHAPISHAJI

Wapendwa, karibuni sana katika somo hili ambalo ni mada ya saba.

Mrabaha ni nini?
Kwanza nianze kwa kusema kwamba neno hili huwa linakosewa mara kwa mara na watu wengi. Wengi hujikuta wakisema *mrahaba.* Kupitia somo la leo, sote sasa tuelewe kwamba neno sahihi ni *MRABAHA* na kwa Kiingereza ni *Commission/Royalty.*

Kwa ufupi kabisa, *Mrabaha ni asilimia za mapato ya mauzo ambazo mhusika hupewa kutokana na makubaliano na mtu mwingine au Kampuni inayojishughulisha na kazi za mtu huyo.* Mara nyingi Mrabaha huwa unahusisha masuala ya Mikataba ya kisheria. Hii ni kwa sababu anayetoa Mrabaha anaweza asitekeleze na hivyo kumnyima haki yule anayepewa. *Ndiyo maana Mrabaha mara nyingi huambatana na Mkataba ambao ni maagano kati ya pande zinazohusika.* Katika mazingira haya, kuna hatari ya watu kuahidiana Mrabaha bila maandishi yoyote ya makubaliano ambayo yanaweza kutunzwa kama kumbukumbu. Anayenufaika akifariki basi mtoaji wa Mrabaha anaweza kujikalia kimya.

*Kuna aina ngapi za Mrabaha?*
Kwa ufupi, hakuna idadi ya aina kamilli ya Marabaha. Aina itategemeana na makubaliano husika na wahusika katika makubaliano ya mgawanyo wa mapato. Pia, hutegemeana na bidhaa husika. Kwa mfano, wanamuziki hupewa Mrabaha na wasambazaji wa kazi zao, waandishi hupewa na Wachapishaji, na kadhalika. Hata hivyo, walau tuone aina chache za Mrabaha.

*1. Mrabaha wa Mwandishi kutoka kwa Mchapishaji*
Katika uandishi wa kitaaluma, yaani unaofuata kaida zote za uandishi, mwandishi huandika kitabu (mswada) na kisha humkabidhi mchapishaji kwa hatua nyingine. Mchapishaji akipitisha mswada kwenye michakato halafu akaipenda kazi na kuona kwamba ina tija, basi hugharimia kila kitu mpaka kitabu kutoka. Baada ya hapo, Mchapishaji humwita mwandishi ili wasainishane mkataba wa namna ya kugawana mapato. *Kwa hiyo, hapa mwandishi anasaini Mkataba na kukubaliana na Mchapishaji kwamba baada ya muda fulani (mara nyingi ni miezi sita au mwaka), Mchapishaji atakuwa anampatia mwandishi asilimia kadhaa za mapato ya mauzo ya kitabu chake.* Hata mwandishi akifariki, kama kitabu husika kitaendelea kuchapishwa, basi familia ya Marehemu itakuwa inachukua Mrabaha wa mwandishi.

*2. Mrabaha wa Muuzaji wa Vitabu.*
Ikumbukwe kwamba mwandishi au mchapishaji hawawezi kufanya shughuli zote ikiwamo kuuza vitabu. Ingawa watavisambaza sehemu mbalimbali, lakini watalazimika kuwaamini watu ili wauze vitabu hivyo. Wauzaji wanaweza kuwa ni maduka ya vitabu au watu binafsi. Kwa upande wa vitabu vyetu vya kiroho, wauzaji ni watu binafsi, maduka ya vitabu mitaani, Parokia na Majimbo.

Sasa hawa wanapouza vitabu hawafanyi kazi hiyo bure. Lazima kuwe na makubaliano ya asilimia ambayo muuzaji atabaki nayo baada ya kuuza kitabu husika. *Hiyo asilimia anayobaki nayo muuzaji ndiyo huitwa Mrabaha.* Kwa mfano, wauzaji wengi binafsi wanataka walau wakukate 20% ya mauzo kwa kila kitabu. Yapo maduka ya vitabu ambayo yanakata mpaka 25% ya mauzo ya kila kitabu. Parokia nyingi kwa kuwa zinatoa huduma, basi hukata 15%. Ila kuna maduka ya Kanisa pia ambayo nayo hukata 18 au 20%. Na sisi EWCP, kwa kuwa tunatoa huduma, tukiuza kitabu chako, tunakata 15% na kukutumia asilimia 75% iliyobaki.

*3. Mrabaha wa Msambazaji kutoka kwa Mwandishi au Mchapishaji*
 Kwa mazingira yetu, hawa wasambazaji huenda wasituhusu sana. Aidha, huenda wasambazaji wetu wakawa ndio hao wauzaji. Hata hivyo, hawa walipaswa kusimama katika nafasi yao kwa umahususi. Hawa wanapaswa kuchukua mzigo wa vitabu na kuufikisha maeneo husika ambapo vitabu vya Kampuni vitauzwa. Mfano, wanaweza kuchukua maboksi ya vitabu kutoka Dar es Salaam kwenye kampuni fulani ya Uchapishaji na kupeleka vitabu hivyo mikoani kwa mauzaji (madukani, n.k.). *Hawa nao wanapaswa kupewa asilimia zao kutoka kwa Kampuni ya Uchapishaji au mwenye mali.* Narudia tena kusema kwamba watu hao kwa kiasi kikubwa hapa kwetu hatunao kwa sababu ya usomaji na uandishi kuwa chini. Wengi wetu tunajiuzia au tunawasafirishia wanaotuuzia mpaka walipo.

*Kwa nini Wachapishaji wengi huwa wanatuhumiwa kuwa wezi?*
Zipo sababu kadhaa ambazo hufanya mazingira na mtazamo huu kujengeka katika jamii ya waandishi. Tuone tu machache hapa.

*a) Waandishi kutojua michakato ya Uchapishaji wa kitaaluma.*
Waandishi wengi huwatuhumu Wachapishaji kuwa ni wezi kwa sababu wanaona kwamba Wachapishaji wanachukua asilimia kubwa baada ya mauzo. Huona kama vile wachapishaji wanakula jasho la mwandishi. Mathalani, utafiti wetu unaonesha kwamba *Wachapishaji wa kazi za kitaaluma huwalipa waandishi Mrabaha wa 11-13%.* Asilimia hizo kwa kuzitazama zinaonekana ndogo sana. Lakini hebu tutazame uhalisia kwa upande wa Mchapishaji.

-Akipokea mswada wako anaupeleka kwenye jopo la tathmini na lazima alilipe fedha. Kila msomaji anapewa siyo chini ya sh. 50,000/=

-Mwandishi akishapewa maoni ya kuboresha mswada na kuyafanyia kazi, lazima kazi ikikamilika apewe tena mtu ahakiki kama kweli marekebisho yamefanyiwa kazi. Huyo mhakiki hafanyi kazi bure.

-Mswada kama unahusisha picha, Mchapishaji anatakiwa atafute mchoraji atakayechora picha au vielelezo vyote na huyo lazima amlipe. *Kwa uchoraji wa kitaaluma (achana na huu wa mitaani) kila mchoro au kielelezo si chini ya 20,000/=*

-Baada ya hapo, Mchapishaji atampelekea msanifu wa kuseti mswada wako ili uwe kitabu. Huyo atatengeneza pia kava au jalada la kitabu. *Huyo naye analipwa tofauti.*

-Hatua hiyo ikimalizika basi mswada uliosetiwa humrudia mwandishi ahakiki kabla kitabu hakijaprintiwa. *Kitabu kinapoenda kuprintiwa, gharama zote za kuprinti ni za Mchapishaji*

-Kitabu kikiwa tayari, Mchapishaji anatakiwa kuandaa tukio ili kitabu kizinduliwe. Gharama za kuandaa tukio ni za Mchapishaji. Mwandishi ataalikwa tu aje walau kueleza kidogo kuhusu kitabu chake ili kuwahamasisha wasomaji.

-Kitabu kikishazinduliwa basi kitasambazwa na kuwafikia wauzaji (maduka, watu binafsi, Parokia, n.k.) *Huko nako lazima Mchapishaji awape Wauzaji Mrabaha kutokana na uuzaji wa vitabu.*

-Aidha, tukumbuke kwamba Mchapishaji naye ana ofisi, ana wafanyakazi, analipa kodi TRA, analipia leseni ya biashara serikalini na kadhalika. Vyote hivyo, vinategemea mapato yanayotokana na uuzaji wa vitabu hivyohivyo.

*Swali sasa ni je, hapo Mchapishaji amebaki na asilimia ngapi baada ya michakato yote?* *Je, ni kweli kwa hizo asilimia zaidi ya 80 alizobaki nazo ni mwizi?* Haya ni maswali ya mjadala.

*b) Ni kweli kuna Wachapishaji wezi*
Kiuhalisia kuna Wachapishaji wengi sana ambao ni wezi. Hawa hufanya wizi kwa namna mbalimbali. Kwa mfano, kitabu chako kinapochapishwa unatakiwa usaini mkataba wa Mrabaha na uambiwe kwamba kitabu chako kimeprintiwa nakala ngapi. Wengine inasemekana huwa wanadanganya hapa. Mchapishaji anaweza kuprinti nakala 30,000 lakini akakuambia kwamba ameprinti nakala 10,000. Kiutaratibu, nakala zikiisha utatakiwa usaini mkataba mpya ili vitabu viprintiwe vingine. Sasa katika mazingira haya, utakaa muda mrefu ukisubiri viishe sokoni, halafu haviishi. Huu ni wizi na unyonyaji. Wachapishaji wengine huiba kazi za watu binafsi, bila makubaliano na waandishi, na kuzichapisha ili wajinufaishe. Mwaka fulani, nikiwa kwenye shughuli zangu huko Nairobi, niliwahi kuona kitabu cha Prof. Mulokozi kikiwa kimechapishwa huko na kikiwa sokoni. Niliporudi Tanzania nikampasha habari, alishangaa sana, maana hakuwa na habari yoyote. Kwa Tanzania hata kama hali hii ipo, ni kwa kiasi kidogo sana.

*Hitimisho*
Katika somo hili, kama tumelielewa, tunaweza kuhitimisha kwamba:

1. Uchapishaji ni kazi nzito inayohitaji mtaji mkubwa, weledi na rasilimaliwatu ya kutosha. Ndiyo maana mpaka sasa tuna wachapishaji wachache sana wa kazi za kiroho.

2. Kwa kuwa tunajichapishia vitabu, basi tuwe makini kwenye kipengele cha Mrabaha. Wale wanaotuuzia tusiwape vitabu vingi kienyeji. Ni vizuri tukijiandalia mikataba binafsi. Bila hivyo, anayeuza kama ni mtu binafsi, anaweza kuuza na kusema tulikubaliana tugawane nusu kwa nusu (yaani 50%). Ukiwa na Mkataba utaweza walau kukwepa uwezekano wa jambo hilo kutokea. Kama unahitaji tukusaidie namna ya kuandaa Mkataba basi usisite kutuambia EWCP. Tutakusaidia bila malipo yoyote, maana tuko kihuduma zaidi.

3. Kabla ya kupeleka vitabu kwenye maduka ya kuuzia ni vizuri tufahamu Mrabaha wanachukua asilimia ngapi. Kuna wengine wanakata Mrabaha asilimia kubwa sana. Mf. Duka la UDSM liliwahi kunisaidia kuuza kitabu cha kitaaluma kwa Mrabaha wa 25%.

4. Kwa mtazamo wangu utaratibu wa Wachapishaji kuwapa waandishi Mrabaha wa 11-13% (mf. *Kitabu kikiwa kinauzwa kwa sh. 5,000 wewe mwandishi utapata sh. 550-650*) ni wa kinyonyaji. Ingawa Mchapishaji hugharimia kila kitu, lakini walau Mrabaha ungepanda mpaka 20%.

5. Ukweli unaonesha kwamba Mchapishaji mkweli anaweza kupata faida ikiwa ana vitabu vingi sokoni. Mchapishaji akiwa na vitabu tofauti kama 100 na vyote vikawa sokoni, ni rahisi kupokea miswada ya waandishi na kuichapisha kwa haraka kwa sababu mfumo wenyewe unakuwa unajiendesha. Hapo Mchapishaji ataweza kuendesha ofisi na kuwalipa waandishi Mirabaha yao. *Basi tuombeeni sana EWCP maana mpaka sasa tuna vitabu 4 tu sokoni kwenye Majimbo 10. Bado tunajikongoja, na bado tunaamini kwamba tutafika kabisa.*

KARIBUNI KWA MASWALI AU MJADALA ILI TUPANUE SOMO.
===============

*© Leonard Bakize (23.03.2020)*
eternalword2018@gmail.com

EWCP na Ushirikishanaji Maarifa
***********

No comments:

Post a Comment