YALIYOMO
°maendeleo ya Tamthiliya
°maendeleo ya ushairi
°maendeleo ya riwaya
°maendeleo ya hadithi fupi
MAENDELEO YAFASIHI-ANDISHI
Kwa vile tunazingatia kwa kijumla kazi za fasihi-andishi katika kazi hii yetu, ni muhimu tuchukue nafasi ndogo tueleze jinsi kazi hizi zilivyoanza na kuendelea.
Tutazingatia katika sehemu hii maendeleo ya tanzu tatu kuu za fasihi andishi - Tamthilia, Riwaya na Ushairi - ambazo aghalabu huchukua vigezo sawa katika kuhakikiwa.
Kwa jumla, maendeleo ya tanzu hizi tatu za fasihi yamepitia vipindi mbalimbali katika historia na kila kipindi kimekuwa na athari kwa tanzu hizo, yaani mabadiliko ya kijamii kihistoria, yamedhihirika katika tanzu hizi za fasihi hususa katika fani na maudhui.
Jambo hili litadhihirika zaidi wakati tutakapokuwa twazingatia utanzu mmoja mmoja.
TAMTHILIA
UTANGULIZI:
Tamthilia ni utanzu wa fasihi- andishi ambao twaweza kusema ni zao la mabadiliko ya fasihi kama kipengee cha utamaduni wa jamii. Jina tamthilia limetokana na kitendo `mithilisha' ambacho maana yake ni kufananisha au kumithilisha hali ya maisha fulani kwa vitendo. Tamthilia basi ni maigizo ya matukio au visa fulani kwa uhalisi wake kwa ajili ya kuyasawiri maudhui au maelezo fulani.
Dhana ya tamthilia imekuwepo tangu asili na jadi hata katika jamii zetu za kiafrika kabla ya athari za kinagharibi kupitia ukoloni, kwa vile pamekuwepo sanaa mbali mbali za maonyesho ambazo humithilishwa na tamthilia. Ama kwa hakika ugeni au tofauti ya tamthilia ya fasihi - andishi na sanaa za maonyesho za hapo awali, ni katika kugawanya mchezo katika vijisehemu - matendo na maonyesho na kumpa kila mhusika sehemu maalum ya kushiriki. Mtindo huu bila shaka ni zao la mabadiliko ya kijamii. Kabla ya tamthilia tuipatayo siku hizi, maigizo kwa jumla yalihimiza ushirikishaji wa hisia kama
zinavyovutia bila shuruti. Hata wahusika walizingatia mambo papo hapo bila kupanga vile au kakariri yaliyohifadhiwa pahali fulani; yaani hapakuwa na nafasi ya kupanga na kuandika maigizo hapo awali kama ilivyo katika tamthilia ya siku hizi.
Ama kwa hakika, mtindo tunaoupata katika tamthilia ya siku hizi umekopwa kutoka kwa ule wa fasihi ya kimagharibi ambao ulitufikia kupitia kwa elimu ya kikoloni. Mfano mzuri wa kazi zilizotoa athari hii ni zile za Shakespeare anayefahamika sana kwa utunzi wa tamthilia za kiingereza. Tamthilia ya aina hii hugawika katika matendo, na kila tendo huwa na maonyesho kadha. Kila onyesho huwa na waigizaji, kila mmoja wao akiwa na sehemu yake maalum ya kuigiza ambayo ametayarishiwa namtunzi.
Tamthilia hutofautiana na tanzu nyengine za fasihi kwa kuwashirikisha wahusika wake katika mazungumzo au vitendo ambavyo hubainisha hali ilivyo mbele ya hadhira. Tamthilia huihusisha sio tu lugha ya mdomo bali pia lugha bubu inayotokana na ishara za mwili wa mhusika. Kila mtunzi wa tamthilia huwaza jinsi kazi yake ingebainishwa jukwaani na ndiposa baadhi yao husisitiza mpangilio maalum wa mapambo jukwaani, kwani yote hayo husaidia katika kuyasawiri maudhui vyema zaidi. Jambo moja la kimsingi kuhusu tamthilia zote ni kwamba wahusika wote hukutikiana katika mikinzano na matatizo fulani. Lugha wanayotumia huwa ni ya kukunzana kwa vile kila mmoja kapewa jukum lake la kutekeleza.
MAENDELEO
Maendeleo ya tamthilia ya kiswahili yanachukuana na vipindi viwili vikuu - kuja kwa wageni na baada ya uhuru. Kabla ya mwambao wa pwani ya Afrika Mashariki kuingiliwa na athari za kigeni zilizotoka ng'ambo, fasihi ya kiswahili, kama fasihi nyinginezo za Kiafrika, ilikuwa ni ya kusimuliwa tu (pasi na kuandikwa) na ilikuwa na tanzu kama vile ngano, sanaa za maonyesho, vitendawili, methali n.k. Tamthilia hivyo basi haikuwepo kama ilivyo sasa bali palikuwa na maigizo ambayo yalitolewa mbele ya hadhira kwa minajili ya kuongoa na kufundisha maadili au hata kutoa sifa kwa vitendo mwafaka vya wanajamii husika. Baada ya majilio ya wageni (Waarabu na Wakoloni) maonyesho haya yalianza kubadilika kwa kuingizwa katika maandishi na kuiga mitindo ya kimagharibi ili kuchukua mkondo wa tamthilia kwa jumla.
Kihistoria, tamthilila ilianza kwa kutongoa maudhui ya kidini ambayo aghalabu yalikuwa ni uteuzi wa visa fulani kutoka katika Bibilia ili kutoa funzo fulani. Pindi mabadiliko yalipoendelea kutokea katika maisha ya mwanadamu, hali hii ilibadilika hadi kuingia katika tamthilia zilizozingatia maudhui mengine kama vile vichekesho na hata ya huzuni. Peck na Coyle (1984:75) wanaunga mkono maoni haya hivi; "katika drama ya Kigiriki, wahusika walikabiliana na matatizo yaliyohusu uhusiano kati ya binadamu na miungu au Mungu. Katika karne ya kumi na sita hata hivyo msisitizo ulitoka katika dini na kuingilia maswala ya kijamii na tamthilia zikaanza kuzingatia maadili ya kijamii na kisiasa."
Katika Kiswahili, tamthilia ya kwanza kabisa kutungwa na kuchapishwa ni ile ya Henry Kuria (1975) kwa kichwa cha`NakupendaLakini ' ambayo ilitungwakatika
enzi ya ukoloni. Maudhui yake sawa na tungo nyengine nyingi za wakati huo, yaliegemea zaidi upande wa kufurahisha. Huu ni mchezo wa kuigiza unaotongoa maisha ya kijamii, lakini maudhui yake si mazito na hayazingatii hali ya jamii kujisaka na kujitafiti.
Twaweza kusema kwamba kwa muda mrefu sana kabla ya miaka ya sabini, tamthilia zilikuwa chache sana na nyingi zilikuwa ni tafsiri. Ndiposa katika fasihi ya kiswahili pana tamthilia za tafsiri kama vile Mfalme Edipode (19 ), Mabepari wa Venisi (19 ), Julias Kaizari (19 ) na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (19 ) . Yaelekea kwamba kazi za tamthilia katika kiswahili mbali na kuziba pengo lililokuwepo la kazi za tamthilia katika kiswahili, tamthilia hizi pia zilitoa athari katika mtindo wa utunzi ambapo tulipata zile zilizotungwa kishairi, na nyengive zilizotungwa katika hali yamazungumzo.
Baada ya uhuru, watunzi wa Kiafrika walijitoma katika ugwa wa maandishi ya tamthilia na hasa zenye maudhui ya kuonyesha ubovu na udhalimu wawakoloni.
Waandishi hawa walijitosa katika lindi la kuonyesha mwamko wa waafrika katika kuutetea na kuupata ukombozi wao, huku wakionyesha kila aina ya uonevu waliofanyiwa na wakoloni. Mathalani, waandishi Ebrahim Hussein katika Kinjeketile na Mugyabuso Mulokozi katika Mukwava wa Uhehe wanaonyesha hali hiyo katika utunzi wao.
Halafu pakatokea mwamko mpya miogoni mwa waandishi asilia wa kiafrika waliotanabahi kwamba kuondoka kwa mkoloni kamwe hakikuwa kitambulisho cha mwisho wa dhuluma ya ukoloni, kwani ukoloni uliacha nyuma mwenzake kwa jina
ukoloni-mamboleo. Ndiposa twapata kazi kama vile Mashetani (E. Hussein) na Kilio cha Haki (A. Mazrui) zikitongoa maudhui ya ukoloni - mamboleo, unyanayasaji wake, mifumo ya kisiasa na sera za jamii katika nchi zilizojipatia uhuru wa kisiasa.
Kwa jumla, pana mambo muhimu yanayodhihirika tunapotizama historia ya tamthilia. Maendeleo ya tamthilia kihistoria yamechukuana na mabadiliko ya kijamii. Jinsi miaka inavyopita ndivyo shughuli na mitizamo ya wanajamii inavyobadilika na mabadiliko yameratibiwa katika tamthilia. Hata ingawa tumetaja kuhusu kazi zilizozingatia historia ya ukoloni na baadaye ukoloni-mamboleo, watunzi wengine wamezingatia maswala halisi ya kijamii. Penina Mhando katika nyingi za tamthilia zake amezingatia maisha ya mwanamke katika jamii inayomtukuza mwanaume. Waandishi wengine wamepuuza maudhui yenye uzito na kuzingatia sanaa kwa ajili ya sanaa tu; yaani wakatunga kwa ajili ya kutunga tu.
Tunaporejelea tuamthilia kwa jumla, twapata kwamba inayo mambo au vipengee muhimu vinavyoikamilisha. Tamthilia kwa kawaida huwa yahusus wahusika waliopewa majukumu ambapo wanawasiliana kwa mpangilio maalum ulio na sura na katika kutungwa kwake huwa inadhamiriwa kuonyeshwa na kutendwa (kuigizwa) jukwaani na kila kipengee chake lazima kulenga jambo hilo. Tuyazingatie mambo muhimu yanayoikamilisha tamthilia yoyote ile.
Kwanza kabisa pana hadhira. Maonyesho hutokea tu kama pana hadhira, kwani madhumuni yake ni kugusa hisia za hadhira kwa njia moja au nyengine. Kwa hivyo kitendo cha kuigiza hutokea tu pale ambapo hadhiria inashuhudia maigizo. Katika tamthilia hadhira huwa ni wale wanaoitizama jukwaani wanaoisikiliza ikiigizwa redioni au hata wasomaji wake.
Pili, pana mahali pa kuonyeshewa au mandhari. Kwa kawaida, kile kitendo cha kuwasilisha mchezo wa kuigiza (tamthilia) mbele ya hadhira huhitaji mahali pa kuonyeshea pawe kando na mahali pa hadhira. Hii ndiyo ile dhana ya jukwaa na huwa ni kwa sababu mbili kuu- - kwanza, ili kuwapa hadhira fursa ya kuona maigizo, na pili ili kutoa nafasi ya kuunda jukwaa kisanaa ili kuvutia na kuwa halisi kwa kitendo kitakachoigizwa.
Tatu, pana watendaji/waigizaji. Hawa ndio uti wa mgongo katika kitendo kizima kwani ndio wanaotoa kitendo chenyewe na pia kuwafikishia hadhira kitendo hicho.
Wanaitumia miili yao, sauti zao na hisia zao ili kuwasilisha ujumbe wao. Muhimu hapa ni jinsi wanavyojitokeza na jinsi walivyosawiriwa na mtunzi kwa vile ni lazima usawiri wao (maneno, matendo na umbo) uwe wa kuchukuana na hali halisi wanayowakilisha. Kwa mfano, kama mhusika anaigiza nafasi ya mahabusi katika jela, lazima achorwe hivyo na sio vingine, lau sivyo hatakuwa mhusika wa kuaminika.
Hatimaye, ni mambo yanayoigizwa. Kwanza kabisa lazima pawe na ujumbe fulani katika maigizo hayo na lazima pawe na uwiano wa kila kitendo na chengine ili kufanikisha dhamira ya mtunzi. Huenda kitendo chenyewe kikawa ni kichekesho, tanzia, hali ya kukejeli au kuwapa watu motisho na kuwahimiza kujisaka na kujirekebisha. Hapa ndipo twapatamaudhui.
Hayo ni baadhi tu ya mambo yanayoifanikisha tamthilia kama utanzu wa fasihi lakini ni ya kimsingi na hayakosi katika tamthilia yoyote ile.
HITIMISHO
Katika sehemu hii tumeona jinsi ambavyo tamthilia kama tuijuavyo leo imepitia mikondo mbali mbali. Hili ni jambo la kawaida katika fasihi yoyote kwani kila fasihi na tanzu zake, hubadilika, kwa hivyo twapata mabadiliko ya tamthilia kutoka hali ya awali hadi ilivyo kwa hivi sasa. Kwa muhtasari, twaona kwamba tamthilia ilianza kama maonyesho ya kidini kunako miaka ya 1500 kule Ugiriki ambapo watu walidondoa sehemu fupi kutoka maandiko matakatifu na kuziigiza sehemu hizo ili kutoa ujumbe wa kidini. Baadaye, mkondo huu ulififia na pakaingia maudhui ya kuburudisha. Ikawa jukumu kubwa la maonyesho ya jukwaani ni kutumbuiza au pia kuhuzunisha. Katika fasihi ya Kiswahili vichekesho na kutumbuiza viligeuka na kuwa maigizo ya kuwacheka waafrika walioazimia kuwa wazungu. Hatimaye maudhui mazito ya kihalisia yakachukua nafasi ya vichekesho na watunzi wakaanza kutunga tungo zenye maudhui mazito zaidi. Hata hivyo kila kipindi cha kihistoria kina mifano mbali mbali ya kazi za tamthilia na hivyo basi hatuwezi kusema kuwa ni aina moja tu ya tamthilia inayopatikana katika kipindi maalum chahistoria.
RIWAYA UTANGULIZI:
Riwaya ni utanzu wa fasihi-andishi unaowiana sana na hadithi katika fasihi- simulizi. Wakati mwingine tunaweza kusema kwamba riwaya ni hadithi iliyohifadhiwa katika maandishi. Tofauti inatokea pale ambapo mwandishi wa riwaya, kinyume na mtamba hadithi, anakuwa na wakati na nafasi ya kusawiri visa na wahusika wake vile anavyotaka. Mtamba hadithi naye huwa hana nafasi kama hii kwa vile yeye hutoa masimulisi moja kwa moja. Lakini naye ana nafasi ya kubadili usimulizi wake kwa jinsi anavyoipima hadhira na matarajio yake.
Pametokea utata katika kujaribu kueleza riwaya ni nini. Wataalam wengi, kama walivyonukuliwa na Senkoro, F.E.M.K (1982:72) wametoa maana mbali mbali za riwaya. Mathalani, `Riwaya ni hadithi ndefu ambazo zimeandikwa - Matteru (1976);
`Riwaya inaundwa kwa njia ambayo tukio lingine lolote likiongezwa au kupunguzwa litaharibu ukamilifu wake' - Nazareth (1972); `Riwaya ni mfuatano mahsusi wa visa vilivyapangwa kufuatia wakati na kwa njia ambayo chakula cha mchana huja baada ya chamsha kinywa, Jumanne baada ya Jumatatu, kuoza baada ya kifo na kadhalika' - Forster (1949).
Kilicho dhahiri katika maelezo haya ni kwamba hapana yale yanayoweza kudai utoshelezi, kila maelezo yana dosari zake. Hata hivyo, ili kuepuka tatizo hili twaweza kusema kwamba kilicho muhimu katika kueleza chombo chochote ni sura muhimu zinazokitambulisha. Bila shaka riwaya inazo sura zake. Kwa mfano ni wazi kwamba riwaya ni utungo ulioendelezwa kinadhari na huwa na urefu wa kiasi cha kuwezesha usawiri wa whusika pamoja na matendo yao. Vile vile huwa ni kazi ya kubuni lakini ambayo imejengeka katika ploti maalum na hujaribu kuyachora maisha ya jamii inayozingatiwa. Kwa hivyo twaweza kusema kwamba riwaya ni utungo wa kinadhari uliobuniwa na ulio na urefu wa kiasi kinachowezesha usawiri wa wahusika na matendo yao ili kuwakilisha uhalisi wa maisha ya jamii husika katika ploti maalum.
Kutaja kwamba riwaya ni utungo wa kubuni na hali ni utungo unaowasilisha maswala halisi ya maisha ni jambo la kukanganya. Nia yetu katika kauli hiyo ni kuonyesha kwamba matukio na visa anavyovisawiri mtunzi huwa amevibuni lakini lazima visa vyenyewe viwe karibu na ukweli wa mambo; yaani yawe matukio halisi
ambayo huenda yakatokea katika jamii. Isiwe amebuni visa ambavyo ni dhahania ambavyo haviwezakani katika ulimwengu halisi. Hata hivyo hali ya ubunifu ndiyo inayoitambulisha kazi yoyote ya fasihi na kuitofautisha na kazi nyingine za kijamii; kama haingekuwa hivyo, basi hiyo ingekuwa kazi ya historia au ripoti ya matukio badala ya fasihi. Hata wahusika katika riwaya huwa ni watu au viumbe wa kubuniwa na mtunzi lakini hawakiuki sana mipaka ya watu katika maisha ya kila siku, na matendo yao huwa ni ya kawaida na yaliyojikita katika mantiki ya maisha ya kila siku.
Kwa hivyo neno `Riwaya' aghalabu limetuniwa kumaanisha kazi za kinadhari zilizotungwa ili kujaribu kumithilisha uhalisi wa maisha ya jamii. Huwa inajaribu kubashiri yanayoweza kuwa ya kweli kwa kutumia ploti na matendo katika usawiri wa wahusika. Riwaya basi hutambuliwa iwapo itajaribu kuchora uhalisi wa maisha hata ingawa haifungwi na kaida za maisha halisi katika kuendeleza lengo lake. Mtunzi katika riwaya kinyume na shairi au tamthilia, hutumia lugha elezi na fafanuzi zaidi kwani yeye aghalabu hufanya kutoa matukio kinadhari na kwa mfululizo unaojenga kisa au visa.
Hadithi ya riwaya huwa kamili kivyake bila kuegemea matukio, maoni, au maelezo mengine yaliyo nje ya kazi hiyo. Mambo ya nje yaweza kutumiwa kueleza zaidi matukio yaliyosawiriwa katika riwaya lakini ukamilifu wake kama kazi ya fasihi huwa hivi kwamba inatoa maudhui au hadithi inayojisimamia.
MAENDELEO
Historia ya riwaya ya Kiswahili hususa huchukuana na majilio ya wageni katika upwa wa Afrika Mashariki. Hata hivyo, riwaya hii ilianza kama hadithi zilizoandikwa kinadhari. Halmashauri ya kusanifisha lugha ya Kiswahili ilipoanzishawa mwaka 1930, ilileta mashindano ya uandishi wa hadithi fupi fupi na vitabu. Hapo ndipo palitokea vitabu vidogo vidogo kama vile Safari za Sungura, Hadithi za Mjomba Remus na Safari za Juma.
Hata hivyo, hapo awali palikuwa na aina ya riwaya ya Kiswahili ambayo ilikuwa ni insha ndefu kuhusu tajiriba za Waafrika kuhusu ukoloni au tawasifu zao (Autobiography). Abdalla Bin Hamed Bin Ali alichangia sana hali hii alipoandika Habari za Wakilindi, kazi ambayo ilichapishwa na UMCA magila Press katika miaka ya 1895 - 1907. Vile vile palikuwa Tawasifu ya Tippu Tip ya mwaka 1902. Waandishi
wengine walifuata kama vile H.M.T Kayamba aliyeandika Tulivyoona na Tulivyofanya Uingereza (1932) ambapo alisimulia safari ya Kundi la Waafrika walioalikwa na afisi ya ukoloni mwaka 1931. Naye James Mbotela (1934) aliandika Uhuru wa Watumwa ambapo alisimulia kuhusu watumwa walioachwa huru; ingawa alichukua mkondo wa kuwatukuza Wazungu na Kuwaonyesha Waafrika kama watu duni na wenye dini za Kishenzi. Kazi hii ambayo ilifanywa kitabu muhimu cha kufundishwa shuleni ilikuwa na lengo moja kuu - - kudhihirisha, kwa mtizamo wa kiafrika (japo ulikuwa wa kikoloni uliotumia jina la Mbotela tu kuupa uzito wa Kiafrika), Waswahili, Waarabu na Waislamu kama wanyama walioendeleza biashara ya watumwa na ilhali kuasawiri waingerezakama waokozi waliotumwa na mungu (Mazrui na Shariff1994:35).
Hali hiyo ya uduni wa Mwafrika katika fasihi iliendelezwa na kwa wakoloni. Hii ni kwa sababu palikuwa (kama ambavyo tumetaja) na maandishi ya kazi za Kiswahili (riwaya) kabla ya kuja kwa Wageni (Wakoloni). Hata hivyo, baada ya kuja kwa Wakoloni, Waafrika walianza kutunga kazi zao wakifuata mkondo fulani uliofanana na ule uliopatikana katika vitabu vya tafsiri. Hii ni kwa sababu Wakoloni walipoingia Afrika Mashariki, waliwaonyesha wenyeji kwamba walikuwa na hatua ndefu ya kupiga kabla ya kufikia kiwango cha ustaarabu na uhalisi (katikautunzi).
Jambo hili lilifanya vitabu vya tafsiri kuenea sana na kutumiwa kama vigezo vya kupimia ubora au ubovu wa kazi zilizotungwa na wenyeji. Ndiposa twapata ploti na usimulizi wa kazi za kwanza za mtunzi kama Shaaban Robert zilifanana na baadhi ya kazi za tafsiri zilizokuwepo. Fauka ya hilo ni kuwa hata wahusika wake walidhihiri hali hiyo. mathalani, wengi wa wahusika walionyesha hali ya unyenyekevu huku wafalme wakisawiriwa kama wenye nguvu sana na wahusika wakuu wakiwa waadilifu. Hizi zote ni athari za falsafa za Wakoloni kwa wenyeji.
Isichukuliwe kwamba twapinga kuwepo kazi za tafsiri katika fasihi ya Kiswahili. Ukweli ni kwamba sababu mojawapo ya kuenea kwa vitabu vya tafsiri kwenya fasihi ya Kiswahili ni upungufu wa vitabu vya tungo asilia ambazo zingetosheleza wadhifa wa fasihi kikamilifu. Ni dhahiri basi kwamba kuweko kwa vitabu vilivyotafsiriwa kama ziada ya vitabu vya fasihi ni jambo la maslahi na maendeleo ya fasihi kwa jumla. ndiposa twapata maudhui katika vitabu hivi vilivyotafsiriwa ni ya kuwafurahisha wasomaji walioandikiwa - kuwapatia watu fursa ya kusoma fasihi isiyohitaji uzito wa
fikra kwa kuyaelewa yanayoendelezwa vitabuni humo. Hata hivyo, baadhi ya vitabu hivi vilivyotafsiriwa siku hizo vilitongoa maudhui yanayowatukuza Wazungu, kuonyesha ustaarabu na uwezo wao, huku wakiwatweza wenyeji. Mifano ya kazi kama hizo ni Mashimo ya Mfalme Suleimani. Mkondo huu uliathiri waandishi chipukizi kama vile Shaaban Robert (Kusadikika), M.S. Farsay, (Kurwa na Doto) Ali Jamadaar (Nahodha Fikirini) Mohamed S. Abudulla (Kisima cha Giningi) hasa katika muundo na usawiri wa wahusika.
Kwa upande mwingine, hatuwezi kufikiria riwaya ya Kiswahili bila kuzingatia swala la kuja kwa Waarabu ambao waliwafunza Waafrika hati za maandishi na mbinu za kuchapisha. Kwa hivyo twaone majilio ya wageni katika upwa wa Afrika Mashariki yalileta mbinu ya maandishi na uchapishaji, hali ambayo iliathiri sana fasihi ya Kiswahili. Matokeo ya athari hizi ni kwamba hadithi na hekaya nyingi za Waarabu na Waajemi kama zile za Abunwazi, Alfu-Lela-Ulela n.k. zilitafsiriwa na kuingia katika fasihi ya Kiswahili. Vile vile pana hadithi kadha wa kadha za kizungu kama vile Hadithi za Esopo, Kisiwa chenye Hazina Mashimo ya Mfalme Suleimani n.k zilizotafsiriwa na kuingia katika uwanja wa fasihi yaKiswahili.
Licha ya kuwepo kazi hizi zilizowakilisha riwaya ya Kiswahili, utanzu huu haukupanuka sana wakati huo wa ukoloni. Hili halikuwa jambo la sadfa bali liliandamana na sababu kadhaa kwa mfano, palikuwepo ile hali ya kudunisha utamaduni wa Mwafrika na Kumfanya aabudu chochote cha wageni. Pia waingereza walihimiza mabadiliko kupitia elimu iliyosisitiza kiingereza ambapo kazi za asili ya kiingereza ziliingizwa katika sera ya elimu. Wakati huo huo Kiswahili kilipingwa sana na wakristo kwa kuhusishwa na dini ya Kiislamu. Sababu nyengine ni kuwa watafiti wengi wa kigeni (ambao ndio wangechangia katika kurutubisha riwaya ya Kiswahili) walihimiza zaidi ushairi na fasihi- simulizi. Hivyo basi utanzu wa riwayaukapuuzwa.
Katika miaka ya sitini, palitokea waandishi wengine kama vile Mohamed Saleh Abdulla Farsay aliyetunga Kurwa na Doto (1962), J.A. sipendi aliyetunga Kisa cha Germana, Monka na Shetani (1962) na Shaaban Robert katka Kufikirika (1969).
Linalodhihiri katika kazi hizi ni aina ya mambo yaliyozingatiwa mle. Waandishi hawa walitunga kazi hizo kwa kutumbuiza wasomaji wake kwa vile maswala yaliyotokea mle hayakuwa maswala ya kati katika jamii zao. Ndiposa katika kazi hizo twapata yale
mawazo ya ki-utopia ambayo yanahimiza ujenzi wa jamii mpya lakini kwa njia ambazo hazina mashiko ya kimantiki. Yaani matatizo ya binadamu yanatatuliwa kwa njia za kiholela kabisa ambazo hasipatikani katika hali halisi maishani. Hata hivyo, mwelekeo huu wa ki-utopia umeungwa mkono na wahakiki wengine wanaodai kwamba ni makosa kumnyima mtunzi au mwanadamu nafasi ya kuota kwani ni kigezo muhimu katika ubunifu wake ambacho humsaidia kwenda zaidi ya uwezo wake na kuunda picha za mambo anayoweza kujaribu kufikia katika maisha halisi.
Katika miaka ya sabini, panazuka mkondo wa waaandishi kuzingatia zaidi riwaya pevu au (riwaya nyeti) zenye mwelekeo zaidi wa kisiasa. Hizi ni riwaya ambazo twaweza kuziita riwaya za kisiasa. Ni katika kipindi hichi ambapo riwayaya
`kimapinduzi' ilijitokeza, riwaya ambayo ilitanguliwa - na hata kuchochewa kwa kiasi fulani - ushari wa kimapinduzi. Riwaya hii ni zao la hali halisi ya kihistoria ya wakati huo. Yaani katika miaka ya sabini, nchi za Afrika Mashariki zilishuhudia mabadiliko makubwa ya kisiasa na kiuchumi ambayo yaliziweka jamii katika hali ya matatizo.
Katika kipindi hiki, maisha ya jamii yalikumbana na mabadiliko mapana ya kiuchumi na hata kisiasa. Maadili ya kijumla ya kijamii pia yalibadilika huku faida na fedha zikitiliwa maanani zaidi ya utu. Kutokana na hili, twapata waandishi wakitizama swala la ujenzi wa jamii mpya inayojali maslahi ya jumuiya badala ya maslahi ya kibinafsi. Wakatongoa maswali ya kati ya kijamii kujisaka na kutafakari zaidi. Mifano ya kazi kama hizi ni Kiu, Kichwamaji, Gamba la Njoka, Nyota ya Rehema, Kasri ya Mwinyi Fuadn.k.
Vile vile palizuka riwaya ambayo twaweza kuita ya ukasuku ambayo watunzi wake huwa na tabia ya kurudia au kukariri bila ya kupima vizuri maneno na mahubiri ya viongozi wa kisiasa na wengineo. Inakuwa kazi zenyewe ni kama zimetolewa ili kutoa aina fulani ya propaganda ambapo wanaosoma kazi hizo hawahitajiki kuyapima yanayotolewa na viongozi na badala yake wanatarajiwa kuyameza moja kwa moja. Kazi kama vile Siku ya Watenzi Wote (Shaaban robert) Mtu ni Utu (Mhina G.A) na Ndoto ya Ndaria( ) ni mifano ya kazihizo.
Mkondo wa riwaya nyeti uliendelea na kuingia katika miaka ya themanini kupitia kwa kazi kama vile Mafuta (Katama Mkangi) Kiza Katika Nuru (S.A. Mohamed) Utengano (M.S. Mohamed), Dunia Mti Mkavu (S.A. Mohamed) n.k. Lakini twapata aina nyengine ya riwaya ambayo haina sura za riwaya nyeti. Ni dhahiri shabiri kwamba jinsi
miaka inavyoendelea ndiyo idadi ya watu inavyoongezeka na eneo la ardhi kupungua. Hivyo basi bidhaa zinazozalishwa ili kukidhi mahitaji ya wanajamii hazichukuani na matakwa yao na hivyo basi panatokea tofauti za kuzigawa. Hapo ndipo watu wachache wenye uwezo wa kudhibiti mali hizo chache zizalishwazo huitumia silaha ya uhaba kuchuma na kujinufaisha wenyewe. Matokeo ya hali hii ni rushwa, biashara za magendo, ulanguzi, upikaji wa pombe haramu, wizi wa nguvu, ukahaba, kushuka kwa thamani ya fedha n.k. Hii ni hali ambayo imeendelea tangu miaka ya sabini na bila shaka imeathiri sana maandishi. Kwa upande wa riwaya, pametokea waandishi ambao wameandika kama njia ya kujitatulia matatizo ya kiuchumi. Waandishi hawa wameingia katika uwanja wa riwaya-pendwa ambapo zaidi hujishughulisha na mada za mapenzi nauhalifu.
Kazi hizi zimejitokeza kwa wingi katika kipindi hiki si kwa lile lengo la hapo awali la kuziba pengo la upungufu wa maandishi ya fashihi bali kwa lengo la mwandishi kupigania na hali ngumu ya kiuchumi ya kipindi hiki. Aidha kazi hizi zimefaulu kujitosheleza kwa wingi kwa sababu mbili za kimsingi. Kwanza, ni kutokana na soko lake kubwa ambalo hasa uchapishaji. Baadhi ya kazi zinazoainishwa katika kigezo hiki ni kama vile Mpango (K.M. Kassam), Je, Kisasi? (H.A. Kimwanga), Nitakuja kwa Siri (Mbunda Msokile)n.k.
Hivyo basi katika miaka ya themanini, riwaya nyeti si nyingi tukilinganisha na miaka ya sabini. Hata hivyo, pameendelea ile hali ya kutafsiri vitabu vilivyoandikwa na Waafrika katika lugha nyngine na kuviingiza katika fashi ya Kiswahili. Mifano ya vitabu hivi ni kama vile Boi, Mshale wa Mungu, Wema Hawajazaliwa, Mwakilishi wa Watu, Shetani Msalabanin.k.
Kwa jumla, tunapotazama riwaya kama kazi ya fasihi-andishi, twapata kwamba ni utanzu wenye uwezo wa kuzingatia mambo kwa upana sana. Hivyo basi huenda mambo mengi yakazingatiwa katika riwaya moja au hata jambo moja tu likazingatiwa lakini kwa undani zaidi. Kwa kufuatia hali hii, panatokea aina mbali mbali za riwaya hasa kimuundo na kimaudhui. Ndiposa twaweza kupata aina zifuatazo za riwaya. Kwanza, pana riwaya ambayo itaratibiwa kwa kuhusishwa na wakati au kipindi halisi cha historia kinachojenga kazi hiyo. Hapa ndipo twapata riway zinazozingatia historia halisi ya jamii husika.
Pili, pana aina ya riwaya iliyo na misingi ya mkondo wa ulimbwende. Utapata katika riwaya kama hiyo, nguli hutokea na kusifika sana huku akihusishwa na visa vya kusisimua na vinavyomwathiri kwa njia moja au nyengine. riwaya nyingi zenye nia ya kufurahisha na kusisimua wasomaji wake hupatikana hapa. Watu wengine wameziita riwaya - pendwa.
Tatu, pana riwaya ambazo huzingatia kwa undani sana fikra azma na hisia za mhusika au wahusika. Hivyo basi riwaya kama hii zaidi hujikita katika kuingilia kwa kindani maisha ya ndani ya mhusika mmoja au ya wahusika wachache ndipo twapata ile inayoitwa riwaya ya kisaikolojia.
Vile vile utapata riwaya iliyojengeka katika nguzo halisi za kijamii ambapo mtunzi wake hujaribu kusawiri jamii nzima au hata kijisehemu kikubwa cha jamii hiyo kinavyotenda mambo. Aghalabu riwaya kama hii itajaribu kusawiri hali halisi ya maisha ya jamii husika huku ikidhihirisha shida zake, matamanio yake, na hata kutoa pendekezo la suluhisho kwa shida hizo.
Hivyo basi utapata katika utanzu wa riwaya peke yake pana aina mbali mbali za utunzi ambazo zaweza kuainika. Hata hivyo sio lazima riwaya iweze kuratibiwa katika vigezo hivyo au vingineyo kwa vile wakati mwingine huenda riwaya moja ikazingatia vigezo viwili au zaidi.
MASHAIRI UTANGULIZI
Ushairi ndio utanzu mkongwe kabisa katika fasihi na yamkinika ulianza tangu binadanu alipoanza kutumia lugha wakati wa kazi na mapumziko. Ushairi umechipuka kutoka katika nyimbo zilizoundwa na binadamu kutoa hisi zake alipoanza kushirikiana na kuwasiliana na wenzake. Ndiposa Senkoro, F.E.M.K. (1988:17) anasema;
Baada ya kuzuka kwa lugha, fasihi ya Mwanzo ilifuatia. Fasihi hii ilitokana na kazi alizofanya mtu katika kupambana na mazingira Polepole alianza kutunga maneno na sauti Zilizofuatia mapigo ya zana za kazi. Baada ya mudaalizitumia
sauti hizi hizi za mapigo ya zana zake za kazi kujiimbia nyimbo wakati alipokuwa akifanya kazi. Wimbo wa kazi, basi ukawa ndiyo fasihi ya mwanzo.
Hivyo basi nyimbo zilitumiwa katika harakati za binadamu za kuzalisha mali ambapo mwimbaji aliathirika kihisia na hivyo kumsukuma kufanya kazi kwa dhati zaidi na kumsahaulisha ugumu wa kazi ile. Kufuatia hili, twaweza kusema kwamba ushairi asilia ulifungamana na nyimbo na ulitungwa kwa njia ambayo iliweza kuufanya ufuatie mapigo ya zana za kazi na kuweza kukumbukwa kwa urahisi. Kwa uzi huo huo twaweza kusema kuwa ushairi kama utanzu katika fasihi-andishi ulianza pindi taaluma ya kuandika na kupiga chapa ilipoanza Afrika Mashariki.
Tungependa kutaja hapa kwamba neno shairi si sawa na ushairi kwa vile shairi ni mojawapo ya tanzu katika ushairi. Kwa hivyo katika ushairi twazingatia dhana ya namna ya kutunga shairi/mashairi na twapata tungo kama vile tenzi, nyimbo, wajiwaji, hamziya, tumbuizo, shairi n.k.
Katika sehemu hii tutazingatia shairi kama utungo wa kisanaa ulioandikwa kwa matumizi ya lugha ya mkato na yenye mpangilio maalum unaoonyesha uzingatifu wa utaratibu wa urari na muwala maalum unaoheshimu kanuni za utunzi wa ushairi unaohusika. Kwa ujumla wake ushairi huwasilisha fikra na taswira mbali mbali ili kugusa hisia za hadhira.
MAENDELEO
Historia ya ushairi wa kiswahili haiwezi kuelezwa bila kurejelea swala la kuja kwa wageni katika Afrika Mashariki. Hii ni kwa sababu kuja kwa wageni hao kulisababisha mabadiliko katika umbo la shairi la kiswahili. Kama ambavyo tayari tumetaja, ushairi wa Kiswahili asili yake ni nyimbo; na kabla ya kuja kwa wageni, nyimbo hizi hazikufuata sheria za vina na mizani kama ilivyo leo. Aidha nyimbo hizo zilisimuliwa tu na watunzi hawakuwa na muda wa kukaa na kupanga nashairi yao kama ilivyo na waandishi wa siku hizi.
Wageni (hasa waarabu na wazungu) walipoingia Afrika Mashariki waliwaletea wenyeji mbinu ya maandishi (waarabu) na uchapishaji (wazungu) na kuwafanya wawe na
uwezo wa kuandika na kuhifadhi mashairi yao. Wakati huo huo waarabu walikuwa na nyimbo zao za dini (kasida) ambazo zilitungwa kwa mpango maalum wa silabi zilizoishia kwa mapigo sawa ya sauti. Mpangilio huu uliendelezwa kwa`nyimbo' za kiswahili.
Wenyeji nao walivutiwa na ufundi huo wa kuwa na mistari iliyoishilia kwa silabi sawa. Kwa vile kasida za waarabu zilikuwa katika mstari mmoja, ilikuwa vigumu kuandika mstari mmoja uliojitosheleza katika kiswahili. Ndiposa palizuka tungo zenye zaidi ya mstari mmoja. Tungo kama vile tarbia, tathlitha na takhimisa zilitokea zikionyesha tofauti katika idadi ya mishororo katika kila ubeti. Hata hivyo twaweza kusema kuwa mashairi aina ya takhimisa na hamziya yana asili ya kiarabu na tathlitha au utatu umetokana na nyimbo za kiswahili. Athari ya wageni haikuishia hapa, kwani Waajemi nao walichangia ushairi wa Kiswahili kimuundo kwa kusisitiza vina vya mwisho viwiane.
Kimaudhui twapata athari za waarabu (hasa dini ya Kiislamu) na Wazungu (unyenyekevu kwa watawala) zikijitokeza sana katika mashairi yaliyotungwa na wanyeji katika kipindi cha kuwepo wageni hao. Ndiposa twapata mahairi ya zamani kama vile Utendi wa Mwanakupona, Hamziyya na utenzi wa Al-Inkishafi yanakita zaidi katika maudhui ya dini ya unyenyekevu. Mbali na athari hii, tutaongeza kwamba kwa vile wageni hawa ndio waliotamalaki nyenzo za uandishi na uchapishi, bila shaka hawangekubali kutoa kazi ambazo zilikiuka kaida na matarajio yao.
Baadaye yalitungwa na kuchapishwa mashairi yaliyokuwa na maudhui mbali mbali yaliyolenga nyanja zote za maisha ya mwanadamu. Mfano wa mashairi kama hayo yaliyotungwa enzi hizo ni kama vile ya Muyaka bin Haji. Katika kipindi kilichofuatia, hasa baada ya nchi za Afrika Mashariki kupata uhuru wa kisiasa, mashairi yalitungwa yaliyoegemea maudhui mbali mbali. Pana yale yaliyozingatia vita vya uhuru, Mengine yakazingatia wakati wa na baada ya uhuru. Mashairi kama vile Sikate Tamaa (S.A. Mohamed) na Sauti ya Dhiki (A. Abdalla) yanatoa mifano mizuri ya maudhui ya mambo tofauti yakumbayo jamii kila mara. Mbali na kutokea mkondo wa kukiuka utunzi uliozingatia maudhui ya kidini, palizuka waandishi chipukizi (katika miaka ya sabini) ambao walipinga matumizi ya vina na mizani kama kigezo cha kutunga mashairi ya Kiswahili. Walitaja kwamba kila kitu duniani hukumbwa na mabadiliko. Walishikilia kwamba maudhui ndicho kitivo cha ushairi wa Kiswahili. Baadhi ya waitifaki wa
mkondo huu ni kama vile S.A. Mohamed na E.Kezilahabi ambao wamedhihirisha msimamo wao katika tungo zao. Hata hivyo mpaka wa leo haijakubaliwa ni mkondo upi wafaa kufuatwa. Pengine yategemea mtunzi husika, nia yake, na itikadi yake kuhusu utunzi.
Lakini hata wanamapokeo wanaoshikilia kwamba uketo wa ushairi wa Kiswahili ni ufuasi wa sheria za utunzi hawapingi kabisa umuhimu wa maudhui (yanayosisitiwa na wanamapinduzi). Ama kwa hakika Kaluta Amri Abedi katika kitabu chake Sheria za kutunga mashairi na Diwani ya Amri, na ambaye ni mfuasi mkuu wa mkondo wa wanamapokeo, anakanganya hali hii asemapo katika utangulizi kwamba;
Neno moja tukumbuke katika utungaji, maudhui Yazue vina, siovinakuzua mawazo. Ndiyo kusema, baadhi ya watungaji, hasa wale wanaojifunza, hukusudia kitu kingine lakinitaratibu ya vina kawalazimisha waingiekatika jambo jingine wasilokusudia, ili tu wapatanishe vina.
Jambo linalodihirika kutokana na mawazo haya ya amri Abedi ni kwamba bado pana utata katika kuamua ni lipi la muhimu katika utunzi wa shairi la Kiswahili - ni maudhui au fani. Mzozo bado upo lakini hauwezi kusuia utunzi wala uhakiki wa kazi za kishairi.
Hata hivyo bila kuunga mkono upande wowote ule, ni dhahiri kwamba pana mambo kadhaa yanayofanya shairi kuwa bora. Kwanza, shairi liwe na mpangilio mzuri wa mistari katika ubeti, na habari zinazozungumziwa ziungane tangu mwanzo hadi mwisho ili kuzua mitiririko maalum. Kila ubeti ujitosheleze kiujumbe ili kueleweka kivyake. Hivyo basi shairi liwe na maana. Mbali na hayo, utamu wa shairi upo katika jinsi ya kuficha maana katika mafumbo ili lisiwe rahisi sana kueleweka. Twaweza kuona shairi kama mchezo kati ya mtunzi na hadhira ambapo pana masharti na kaida wanazozielewa wote ili kuweza kuzhiriki katika mchezo huo. Kufahamu lugha iliyotumiwa, muktadha wa maudhui, na maana fiche ya maneno ni baadhi ya masharti anayopaswa kufahamu mpokezi wa shairi.
Kwa kuhitimisha twaweza kusema kwa jumla kuwa pana miundo mingi ya mashairi katika Kiswahili na aghalabu huratibiwa kutegemea idadi ya mizani, idadi ya mishororo, mkarara wa maneno, majibizano, maudhuni na urari wake.
HITIMISHO
Maendeleo ya kazi za fasihi-andishi ya Kiswahili ni swala ambalo haliwezi kujadiliwa kivyake bila kuhusishwa na maendeleo na historia ya jamii husika. Hii ni kwa sababu mabadiliko ya mtindo na maudhui ya kazi hizo yalikuwa ni zao la mabadiliko ya ujuzi, maadili, mielekeo, na urazini wa wanajamii husika. Ndiposa twapata vipindi vitatu maalum vya maendeleo hayo. Vipindi hivi tutavizingatia kama ifuatayo; kipindi cha kwanza ambacho chasimamia hatua ya mwanzo katika fasihi-andishi, kipindi cha pili kinachosimamia miaka kadhaa baada ya mwanzo lakini kabla ya uhuru na kipindi cha tatu kinachosimamia enzi baada ya uhuru hadi leo. Tutazingatia kila hatua mojamoja.
HATUA YA MWANZO
Hiki ni kipindi ambacho twaweza kukiona kama kilichokuwa na utasa wa namna fulani kwa ukosefu wa nyenzo za maandishi na uchapishi. Hata hivyo kazi za mwanzo kabisa zilikuwa katika utanzu wa ushairi kwa namna ya nyimbo zilizoimbwa na wanajamii husika. Hapana ithibati zozote zinazoonyesha palikuwepo na maandishi (fasihi-andishi) kabla ya kuja kwa wageni toka magharibi na mashariki. Kwa wakati huo jamii ilikuwa inashirikiana sana, fasihi (ambayo ilikuwa simulizi wakati huo). ilikuwa chombo cha kuunganisha wanajamii pamoja na kuyajumulisha matukio yote ya utamaduni wao. Pia fasihi ilikuwa ni chombo cha kuhusisha kila mwanajamii hata hadhira yake. Twaweza kupendekeza kwamba imani za dini na falsafa ya unyenyekevu kwa dini za kigeni na himaya zake haikuwa imeingilia maudhui ya fasihi hiyo. Hatuwezi kukanusha kuwepo kwa utunzi ulioonyesha ubinafsi wa mtunzi na ubunifu wake. Tungo zenye sifa kwa shujaa, viongozi, mazingira, na maisha kama yalivyoeleweka enzi hizo lazima pia zilikuwepo. Ni baada ya kuja kwa taaluma ya kuandika na kupiga chapa ndipo tungo zilipoingizwa katikafasihi-andishi.
HATUA YA PILI
Katika kipindi hiki twapata mataifa ya kimagharibi yalikuwa yakigawa Afrika kwa minajili ya kuendeleza utawala. Hiki ni kipindi ambapo pia twapata aina mbalimbali za vita - vita vya dunia na vita kutaka uhuru miongoni mwa nchi za Afrika. Kuja kwa wageni kulitoa athari zenye mashiko kwa fasihi ya kiswahili. Kuja kwa wageni wa mashariki (waarabu) kulileta mbinu ya maandishi na pia dini ya kiislamu. Hivyo basi wenyeji wakapata mbinu ya kuwasaidia kutunga kazi zao - vile vile umbo la mashairi ya kiswahili liliathiriwa na utunzi wa kiislamu (kasida) uliozingatia maudhui ya kusifu mtume Mohammed. Pia palitokea athari kwa maudhui ya fasihi ya kiswahili (hasa mashairi) kwa kuzingatia maudhui yaliyotoa fikira za Mungu mmoja na kuzingatia unyenyekevu kwa kuogopa kuangamia baadaye.
Kwa upande mwingine, kuja kwa wageni wa Magharibi ambao walizua ukoloni wa kizungu, pia ulitoa athari kwa fasihi ya kiswahili. Wageni hawa waliwaletea wenyeji mbinu ya uchapishaji wa vitabu na kuvisambaza. Hivyo, basi wakapata njia ya kuhifadhi maandishi yao. Lakini wageni hawa walikuja kwa nia yao ya kutawala na kujiendeleza kiuchumi, hivyo basi kukawa iwapo wangeendeleza fasihi, basi lazima iwe na sura zitakazochukuana na nia yao. Ndiposa palitokea hali ya kulazimisha tafsiri za kazi za kigeni na pia kazi zinazotoa maudhui ya kidini na unyenyekevu. Hapa twapata watunzi kama vile Mwana Kupona (japo pana maoni kwamba kazi yake yapaswa kusomwa kama iliyokuwa ikidhihaki misingi ya kijamii iliyozingatiwa), Aidarus, na Shaaban Robert wakithibiti hali hiyo.
Hata hivyo mkondo huo haukudumu sana kwa vile palitokea watunzi wengine walioanza kujiuliza maswali na kuanza kutunga kazi zilizoegemea maudhui ya matukio mahsusi katika jamii. Kazi kama vile Utenzi wa vita vya Maji Maji, Utenzi wa vita vya uhuru, Kusadikika n.k. zilizingatia maudhui ya mambo halisi katika jamii husika.
Palitokea pia kazi za kuwahimiza waafrika katika vita vya uhuru huku pakidhihirishwa hadaa na hila za wageni hao. Hata hivyo bado palikuwa na shehena la vitabu vya tafsiri katika fasihi ya kiswahili kwani wenyeji bado hawakuwa wamehimili nguvu za kupiga chapa na kuandika.
HATUA YA TATU
Baada ya utunzi kushika mizizi miongoni mwa waafrika, palitokea kazi nyingi ambazo ziliwafahamisha wasomaji kuhusu maswala ya kitawala na kijamii ya wakati huo. Fasihi ikatumiwa kama chombo cha kuibua na kuhamasisha urazini mpya miongoni mwa Waafrika. Hapa ndipo palikuwa kilele cha vita vya uhuru katika nchi za Afrika Mashariki (hasa miaka ya mwanzo ya sitini) na palitungwa kazi za kuonyesha dhuluma ya ukoloni. Baada ya uhuru palitokea mabadiliko ya mtizamo katika utunzi ambapo badala ya kukashifu dhuluma ya ukoloni - mamboleo, baadhi ya watunzi waliwapongeza viongozi na wapigania uhuru. Lakini ilidhihirika kwamba matamanio na matarajio ya uhuru yaligeuka na kuwa kinyume ndiposa Abdalla, A (1983:ix)alisema;
Tangu nchi zetu zipate uhuru, yajapo mambo yahusianayo na siasa, fasihi ya kiswahili imebaki kuzungumzia na kujishughulisha zaidi na uchambuzi wa yaliyokuwa yakitendwa na
wakoloni walipokuwa wametutawala na imekuwa ikiyafumbia macho yale maovu na makosa tuyatendayo sisi wenyewe.
Kwa hivyo tukawa na kazi za fasihi za kikasuku ambazo silijaa sifa na propaganda kemkemu za wanasiasa na viongozi wengine huku maswala muhimu ya wananchi yakipuuzwa. Mara nyingi kazi hizi zilitungwa huku watunzi wakitaka kupata kutambuliwa na viongozi na hivyo basi kutunukiwa au ilikuwa viongozi wetu hawawezi kukubali kazi zichapishwe amabzo zilikashifu uongozi wao. Wengi wa watunzi waliotiwa kizuizini walikiuka matarajio hayo ya viongozi. Hata hivyo palikuwa na kazi zilizopinga hali hii baada ya watunzi kuona hatari ya mkondo huo wa kikasuku. Hapa ndipo twapata kazi nyingi za kimapinduzi.
Kwa jumla twaweza kusema kwamba jinsi miaka ilivyopita, ndivyo wanajamii walivyobadilika katika mitizamo yao kuhusu maisha huku ubinafsi ukishika nafasi ya kwanza maishani. Mabadiliko haya yalijitokeza katika fasihi hasa ambapo watunzi walisawiri undani wa wahusika. Hapo ndipo twapata riwaya na tamthilia za kisaikolojia ambazo uketo wake upo katika matarajio na hisia za ndani za mhusika/wahusika na
zinazohitaji upembuzi na kujisaka kwingi. Mashetani (E. Hussein) na Shetani Msalabani
(Ngugi wa Thiong'o) ni mifano ya kazi sampuli hiyo.
info.masshele@gmail.com