![]() |
uhakiki wa riwaya |
1.0 Utangulizi
Maisha Yangu na Baada ya MiakaHamsini ni riwaya iliyoandikwa na Shaaban Robert mwaka (1936-1946) na kupigwa chapa ya mwisho mwaka (2003). Ni riwaya yenye insha na mashairi yanayoelezea mambo mbalimbali aliyopata kuyafanya tangu ujana wake hadi uzee wake, pamoja na mafanikio, changamoto alizozipitia na jinsi alivyozitatua katika maisha yake.
Kusudi la riwaya hii hasa ni kutaka kuweka kumbukumbu nzuri juu ya maisha yake kwa yale yote aliyopata kuyafanya akiwa kama mwandishi maarufu wa Afrika Mashariki na Kati, ili vizazi vijavyo ambavyo havikupata bahati ya kumwona mwandishi huyu, kwa kupitia kazi yake hii vitaweza kujifunza mambo mengi na kupata mafanikio katika maisha ya kila siku.
1.1 Nadharia ya Uhalisia kama Msingi wa Uhakiki
Nadharia ya uhalisia ndiyo itakayoongoza kuchambua kitabu hiki. Kwa mujibu wa Ntarangwi (2004) uhalisia ni humaanisha uwakilishi wa uhalisi wa mambo katika fasihi. Ni nadharia iliyozuka karne ya kumi na tisa kwa lengo la kupinga mkondo wa ulimbwende. Sababu ya kuchagua nadharia hii ni kuwa, mhakiki yeyote hupembua namna msanii anavyodhihirisha uhalisi wa mambo mbalimbali kupitia maudhui na fani. Hivyo basi, mhakiki hutizama jinsi ukweli ulivyodhihirishwa katika juhudi za mtunzi za kusawiri hali halisi ya mambo katika kipindi maalumu.
2.0 Maudhui Yanayojitokeza katika Kitabu cha Maisha Yangu na Baada ya Miaka Hamsini
Katika kipengele hiki, kuna dhamira, migogoro, ujumbe, falsafa na mtazamo wa mwandishi. Katika kuhakiki vipengele hivi vyote tutaongozwa na nadharia ya uhalisia kama ambavyo tumekwishadokeza hapo juu.
2.1 Dhamira
Dhamira mbalimbali zimejitokeza katika kitabu hiki cha Maisha Yangu na Baada ya Miaka Hamsini. Baadhi ya dhamira hizo ni kama zifuatazo;
Ubaguzi wa rangi na matabaka, enzi za ukoloni kulikuwa na ubaguzi wa rangi wa watu weupe na weusi katika mambo mbalimbali ya kijamii. Mfano; kusalimiana kwa kushikana mikono, vyombo vya usafiri vilikuwa katika madaraja, daraja la kwanza walikuwa watu weupe (Wazungu) huku daraja la tatu walikuwa watu weusi (Waafrika).
Aidha, kwenye sehemu za malazi zilikuwa katika misingi ya kiubaguzi. Shaaban Robert alilionesha hili katika Uk.50 Karibu ningalilala nje Korogwe kwa ukosefu wa malazi ya abiria Waafrika. Pia Uk.52 Huyo alikuwa ni mzungu, hakuwa tayari kushikana mikono na mimi.
Pia hata katika Insha ya Msuso Uk. 105 anasema; Mtu yeyote aliyekuwa si mweupe katika Afrika Kusini hakuwa na ustahili, thamani wala heshima ya uanadamu. Aliweza kutendewa ukatili wowote ambao haukuwezekana kujaribiwa hata kwa wanyama wa porini bila ya lawama katika nchi nyingine za ulimwengu. Mambo haya leo hii yapo hata katika jamii zetu japo yanajidhihirisha kwa namna nyingine, leo ubaguzi kati ya tajiri na masikini, wenye vyeo na wasionavyo na wenye elimu na wasio na elimu.
Suala la mirathi, mwandishi Shaaban Robert anaonyesha namna gani suala hili linaleta ugumu hususani katika ugawaji wa mirathi. Mwandishi anasema; Choyo cha warithi mbalimbali kilifanya magawanyo kuwa magumu ajabu Uk. 48. Suala hili linahalisika katika maisha yetu ya sasa tunaona jinsi ndugu wanavyopigana na kuchukiana kwasababu ya mirathi.
Suala la uzalendo, Shaban Robert ameonyesha jinsi gani alivyokuwa mzalendo kwa nchi yake (Tanganyika) katika kupinga mifumo yote ya utawala wa kikoloni ambayo ilimdharau Mwafrika hususani katika kipengele cha siasa, kwamba Mwafrika hawezi kufanya chochote. Mfano katika Uk.75 mwandishi anaeleza; Mwafrika aliweza kufanya nini? Alikuwa mtu gani mbele ya watu? Hali hii ilimfanya Shaban Robert kujitoa muhanga kushiriki misafara mbalimbali ya kisiasa ili kuhamasisha maendeleo ya Mwafrika na gharama zote za safari zilikuwa juu yake.Hivyo basi suala hili la uzalendo linahalisika katika jamii ya sasa, kwani watu mbalimbali huingia katika siasa na kutetea maslahi ya haki zao ili kujipatia maendeleo hivyo mwandishi anaitaka jamii ya sasa kujitoa muhanga katika kupingana na utawala mbovu uliyojaa dharau kwa wanaoongozwa.
Suala la haki na uaminifu, Shaban Robert anaona kuwa uaminifu na kutenda haki ni nuru ya maisha bora kwa mwanadamu hapo baadaye. Mfano, katika insha yake ya Umri anasema; Milango ya nyuma ya kuifikia bahati ilikuwa mingi lakini haikunishawishi hata kidogo Uk.2. Hapa tunaona kwamba Shaaban Robert hakuwa tayari kupitia mlango wa pili ili kuyafikia mafanikio. Jambo hili katika jamii zetu linahalisika, kwani watu wengi hutumia mlango wa pili kuyafikia mafaniko kama vile kutoa rushwa na hongo mbalimbali au hata ufisadi.
Dhamira ya kifo na maisha, dhamira hii inajitokeza ndani ya jamii zetu. Kwa binadamu yeyote anapaswa kupokea na kukubali kukubaliana na kifo. Shaaban Robert anaeleza ugumu wa maisha ya upweke baada ya kufiwa na mke wake wa kwanza Amina, katika shairi la Amina Uk.4 anaeleza; mauti yake ya mapema yalikuwa ni msiba na hasara kubwa kwangu. Aidha katika shairi la Amina anasema;
Amina umejitenga, kufa umetangulia,
Kama ua umefunga, baada ya kuchanua,
Nakuombea mwanga, peponi kukubaliwa,
Mapenzi tuliyofunga, hakuna wa kufungua. (Ubeti. 1)
Hapa tunaoneshwa namna Shaaban Robert alivyopitia katika kipindi kigumu lakini anasema mauti yakijitenga mapenzi yatarejea. Pamoja na matatizo hayo yote jamii inapaswa kuwa na moyo wa uvumilivu kwani kifo ni sehemu ya maisha na siyo mwisho wa maisha.
Suala la dini na imani kwa Mungu, mwandishi anaamini uwepo wa Mungu ndiyo maana anamwombea mke wake dua kwa Mungu ili ayashinde maradhi. Anaamini kuwa Mungu hashindwi kitu ila kwa mapenzi yake amemchukua. Mfano, katika shairi la Amina Uk. 4 anasema;
Nilitaka unyanyuke, kwa kukuombea dua,
Sikupenda ushindike, maradhi kukuchukua,
Ila kwa rehema yake, Mungu amekuchagua,
Mapenzi tuliyogfunga, hakuna wa kufungua. (Ubeti.2)
Suala hili linahalisika katika jamii zetu ambapo jamii huamini katika Mungu na kwamba ndiye muweza kila jambo akiamua ameamua hakuna wa kupinga.
Suala la maadili mema, mwandishi Shaaban Robert anadhihirisha hili kupitia maonyo na wasaa kwa watoto wake Hati na Adili juu ya kuwa na maadili mema. Anataja mambo kama utii na adabu, umuhimu wa mwanamke kujitunza, utu wema, kujali wakati, umuhimu wa elimu, kumcha Mungu, kuheshimu wazazi, kutii mamlaka, kutunza ahadi, kuepuka fitina, kuepuka uvivu na kutunza mazingira. Mambo haya yanaelezwa katika utenzi wa Hati na Adili. Mwandishi anaeleza uvumilivu katika maisha ya ndoa. Anasema;
Na mume msishindane,
Wala msinuniane,
Jitahidi mpatane,
Ndiyo maisha ya ndoa. (Ubeti. 34)
Pia, mwandishi kuhusu anaelezea usafi na kutunza mazingira. Anasema;
Nyumba yako inadhifu,
Kwa kufagia uchafu,
Kila mdudu dhaifu,
Asipate pa kukaa. (Ubeti. 36)
Maana ya kifasihi ya ubeti huu ni kwamba, mwanamke anapaswa kutunza mwili, moyo na akili yake ili visije vikaingiliwa na fikra potofu ambazo zitadhoofisha mahusiano katika ndoa au familia yake.
Nafasi ya mwanamke katika jamii, Shaaban Robert anamchora mwanamke katika namna tofauti katika jamii. Mathalani kwenye utenzi wa Hati, anamuasa binti yake kuwa awe mtii, msafi, mpishi bora, mvumilivu katika ndoa na kujifunza elimu. Mfano, katika ubeti wa 33, Uk.10 anasema;
Upishi mwema kujua
Na mume kumridhia
Neno analokwambia,
Kwako itakuwa taa.
Hapa tunaona namna ambavyo mwanamke anapaswa kufahamu mambo mbalimbali ili kupambana na maisha ya kila siku.
Aidha, Shaaban Robert anamuona mwanamke kama pambo na faraja katika maisha ya ndoa, anaeleza katika Uk.3 Sura yake ilikuwa jamali kwa kimo cha kadirio, uso wake ulikuwa mviringo wa yai, nywele nyeusi za kushuka, paji pana, nyusi za upindi, macho mazuri yaliyokuwa na tazamo juu ya kila kitu, kope za kitana, masikio ya kindo yasiyopitwa na sauti ndogo, meno ya mwanya…
Pia, mwanamke ameoneshwa kama mtu mpole na mwenye heshima, jambo hili Shaaban Robert ameliweka wazi makusudi ili jamii iweze kuiga na kubadilika kwani wanawake wengi sasa wamepungukiwa na hilo. Mfano; Uk.37 Mke huyu wa pili alikuwa mpole, mwenye madaha na heshima, alikuwa na sura ya haya ambayo ilichuana na utawa kama uso kwa kioo. Kwa ujumla mwanamke ameonyeshwa katika nafasi tofauti.
Dhuluma na uonevu, Shaaban Robert anaeleza kuwa dhuluma na uonevu vimekuwa ni vipingamizi vikubwa katika mafanikio ya mtu ya kila siku, kwa mfano kama vile kunyimwa jambo fulani au kukandamizwa kwa sababu fulani ni ukuta katika maendeleo binafsi na ya jamii kwa ujumla. Jambo hili linajibainisha katika Uk.1 Mara kwa mara niliposimama wima kuiendea niliteleza nikaanguka chini. Nilipotaka kunyoosha mkono kuishika yalitokea mazuio ambayo sikuyatazamia au nilifungiwa milango ya mbele nisionane nayo.
Vilevile, katika insha ya Mwandishi Shaaban Robert ameonesha ni kwa namna gani alivyodhulumiwa katika uchapaji wa kazi zake. Kwa mfano, Uk.78 anasema; Kwa kazi yangu iliyoweza kuleta sh.25000/- kwa vitabu 5000/- katika mwaka 1954 sikupewa hata pesa moja ya shaba kwa muda wa miaka kadhaa…sikupata kitu kwa kazi yangu iliyoleta karibu sh.15000/- kwa vitabu 5000/- katika mwaka 1958. Pia anaonesha ni kwa namna gani alivyozidi kudhulumiwa na hata wale ambao walichukua madaraka baadaye. Mfano; Uk.79 Nilikuwa mtumishi wa bure na mtu wa chini kuliko pembe nyeusi yoyote iliyopata kuwako katika ulimwengu huu. Kwa nani? Kwa wale waliofadhiliwa na waliotajirishwa na waliotumikiwa na waliofunzwa na kazi zangu. Katika jamii yetu ya leo hususani Tanzania tunaona mambo haya yamekithiri sana. Hivyo basi, ili jamii iweze kuondokana na hali hii ni lazima iungane pamoja na kupinga dhuluma na uonevu.
Ugumu wa soko la vitabu, mwandishi ameonesha ugumu wa suala hili pale alipofungua duka la vitabu lakini watu hawakuhamasika kununua vitabu hivyo, hali hii ilitokana watu wengi kutokujua kusoma na kutokana na utamaduni wa jamii hiyo katika suala zima la usomaji wa vitabu kwani hawakujua thamani yake, kama asemavyo; Uk.110 Walikuwa katika tarehe yaujinga wa kujua kuwa mazoea ya kusoma yalikamilisha utu wetu katika dunia. Hawakufahamu kwamba katika vitabu ndimo ghala za utamaduni wa elimu zilimopatikana. Hali hii inahalisika sana katika jamii ya leo kwani watu wengi wanajua kusoma lakini hawana utamaduni wa kusoma hivyo husababisha soko la vitabu kuwa gumu.Kufanya kazi kwa bidi, kwa kiasi kikubwa Shaaban Robert ameonesha mfano hai katika utendaji bora wa kazi akiwa kazini, kwani alikuwa ni mtu wa kujituma na vilevile alikuwa ni kiongozi mzuri na mwenye kupenda kushirikiana na wafanyakazi wenzake. Amelibainisha hili kama nyenzo kuu na muhimu sana katika kazi wakati wote, kwani kupitia nyezo hii kuna manufaa mengi sana kama vile kupendwa na watu, kupandishwa cheo na hata kuaminiwa sana ndani ya jamii. Jambo ambalo jamii ya leo yapaswa kuiga. Mfano; Uk.41 Niliaminiwa sana hata kuliko nilivyotazamia. Mapendeleo niliyotendewa yalikuwa mengi sana. Pia hata katika Uk.40 Nilitenda yote yaliyokuwa katika uwezo wangu kutimiza wajibu. Pia hata katika Insha ya Idara ya Utawala makarani walikuwa ni wachapakazi.
Kwa ujumla, riwaya hii imezungungumzia dhamira nyingi sana kama vile; suala la matabaka na ubaguzi wa rangi, ugumu wa soko la vitabu, nafasi ya mwanamke, mapenzi, kifo, imani juu ya Mungu kwa kuzitaja kwa uchache.
2. 2 Migogoro
Ni hali ya kutokuelewana baina ya pande mbili yaani mtu na mtu, mtu na kikundi au mtu mwenyewe na nafsi yake. Kuna Migogoro ya aina mbalimbali kama vile; mgogoro wa nafsi, Mgogoro wa kiuchumi, Mgogoro wa kijamii na Mgogoro wa kiuchumi.
Mgogoro wa nafsi kati ya Shaaban Robert mwenewe, huu unaonekana pale anapojiuliza juu ya maisha mazuri yakoje na je afanye nini ili awe na jina zuri duniani. Mfano; Uk.2 Ukosefu wa jina zuri ni ukiwa mkubwa duniani. Jambo hili sikulipenda. Suluhisho la mgogoro huu Shaaban Robert aliamua kufanyakazi kwa bidii na kuwa mtu mwema.
Mgogoro mwingine wa nafsi unajitokeza kwa ShabanRobert pale alipowaza ni kwa vipi angepata mke aliye na sifa kama za Amina (mke wake wa kwanza ambaye ni marehemu). Anasema Uk.37 Nilikuwa na marafiki na wenye huruma kadha wa kadha lakini, kati yao palikuwa hapana mtu niliyeweza kumwita mke. Nafasi yake ilikuwa haina mtu nyumbani. Suluhisho la mgogoro huu, alimpata mke wa pili aliyekuwa na sifa alizozihitaji.
Aidha, mgogoro wa kijamii umetokea pale Shaaban Robert alipodharauliwa kuhusu cheo chake. Hii ilijitokeza pale ambapo Shaaban Robert hakutendewa haki kazini kwake, kwani badala ya kuwekwa wa kwanza katika orodha ya mshahara kutokana na cheo chake aliwekwa mwishoni kwa kuwa tu yeye alikuwa ni Mwaafrika. Suluhisho la mgogoro huu Shaaban Robert aliamua kuandika barua kwa mkuu lakini barua hiyo haikufanyiwa kazi na aliamua kuwa mvumilivu. Uk.55 Katika ulimwengu watu wengine walikuwa wamepatwa na madhila kuliko yaliyonipata mimi wakavumilia. Mimi nilikuwa ni nani nisivumilie?
Mgogoro wa kijamii kati ya Shaaban Robert na msimamizi wa safari, chanzo cha mgogoro huu ni ubaguzi au dharau. Hii ilijitokeza pale ambapo Shaaban Robert alipoambiwa kushuka katika lori la daraja la pili ili kuwapisha Wahindi wanne wakati yeye alistahili kuwa katika hilo gari kutokana na yeye alistahili kuwa mfanyakazi wa serikali. Suluhisho la mgogoro huu Shaaban Robert na watoto wake waliwapisha na kushuka. Msimamizi wa safari, Mhindi vilevile, hakuona mtu mwingine wa kushuka ila mimi. (Uk.50)
Katika mgogoro wa kiuchumi tunamwona Shaabani Robert akilalamika namna alivyodhulumiwa pesa za manunuzi ya vitabu vyake, Uk.78 anasema Kwa kazi yanguiliyoweza kuleta sh 25000/= kwa vitabu 5000 katika mwaka 1954 sikupewa hata pesa moja ya shaba kwa muda wa miaka kadhaa….sikupata kitu kwa kazi yangu iliyoleta karibu sh 15000/= kwa vitabu 5000 katika mwaka 1958.Suluhisho la mgogoro huu ni kwamba Shaabani Robert alizidi kuwa mvumilivu pasipo kuvunjika moyo katika kazi yake ya uandishi Uk.79anasema….sijavunjika moyo, tena ningali nayo bado furaha katika uandishi kama alivyo bi-arusi kwa mpenzi wake. Katika maisha baadhi husumbuka na wengine hucheka. Migogoro iliyojitokeza katika riwaya hii ina lengo la kuifundisha jamii kuhusu mambo tofauti katika maisha yetu ya kila siku.
2.3 Ujumbe
Mwandishi ametoa ujumbe wa aina tofauti tofauti kwa lengo la kuiasa na kuionya jamii ili iweze kubadilika na kufikia maendeleo yenye kuleta tija kwa mtu binafsi, jamii na taifa kwa ujumla. Kama vile;
Kufanya kazi kwa bidii ni msingi na kutokukata tamaa ni mzuri katika maisha. Mfano, Shaaban Robert alifanya kazi kwa bidii na ndio maana alifanikiwa katika maisha yake yote na hivyo kujijengea jina zuri na hakukata tamaa katika maisha yake yote. Ndivyo, jamii inavyopaswaa kuishi ili kila mtu ajipatie maendeleo kwa jasho lake mwenyewe.
Haki na uaminifu katika maisha humfanya mtu aheshimike na kukubalika wakati wote. Shaaban Robert alikuwa muaminifu na hivyo anaiasa jamii kuwa na uaminifu pamoja na kutenda haki katika kila jambo linalostahili haki.
Aidha, suala la malezi ni la wazazi wote wawili na sio suala la mzazi mmoja. Hivyo hakuna budi baba na mama kushiriki kikamilifu katika malezi. Vilevile, kumtegemea Mungu katika kila jambo ni muhimu, na kitu kizuri kinatoka kwa Mungu. Na uandishi ni silaha muhimu katika utunzaji wa kumbukumbu za kihistoria.
2.4 Falsafa ya Mwandishi
Falsafa ya mwandishi Shaaban Robert anaamini kuwa mtu hupendwa na kukubalika kwa watu kutokana na matendo yake mazuri kama vile, kauli njema, ufanyaji kazi kwa bidii, utii na unyenyekevu, msamaha, uvumilivu na kuwa na moyo wa kujitoa.
2.5 Msimamo wa Mwandishi
Mwandishi ameonesha msimamo wa aina mbili, kwanza msimamo wa kidhanifu ambao umetokana na imani yake aliyoishikilia kwamba Mungu ndiye tegemeo. Na anatudhihirishia kwamba mtu akimtegemea Mungu atafanikiwa. Pili ameonesha msimamo wa kiuyakinifu kwani anaeleze kuwa, mtu anayefanya kazi kwa bidii na mwenye ushirikiano na maadili mema ndiye hujitengenezea jina zuri katika jamii. Na hii inajidhihirisha wazi katika maisha yake ya kabla na baada ya miaka hamsini na ndiyo maana mpaka leo anakumbukwa.
3.0 Vipengele vya Fani katika kitabu cha Maisha Yangu na Baada ya Miaka Hamsini.
Katika kipengele cha fani kuna; muundo, mtindo, matumizi ya lugha, wahusika, kufaulu na kutofaulu kwa mwandishi, mandhari na jina la kitabu. Katika uchambuzi wa vipengele vyote hivi tutaongozwa na nadharia ya Umuundo.Kwa mujibu wa Mulokozi (2017), hii ni nadharia iliyohusishwa na Ferdinand de Saussure ikijikita zaidi katika kusisitiza kuwa maana inaweza kubadilika kulingana na miktadha husika, katika dhana zake za langue(lugha) na parole(utendaji). Hivyo, mhakiki wa nadharia hii huzingatia; vipengele vya muundo wa kazi ya fasihi (visa, matukio na vitushi), mundo wa lugha (sarufi), muundo wa sauti za lugha, arudhi katika ushairi, vina na mizani nakadhalika. Kwakuwa nadharia hii inazingatia matumizi ya vipengele hivi vyote, basi itatuongoza kuchambua vipengele vya fani.
3.1 Mtindo
Senkoro (2011) anaeleza kuwa,mtindo katika kazi ya fasihi ni ile namna ambavyo msanii hutunga kazi yake na huipa sura ambayo kifani na kimaudhui huainisha kanuni zilizofuatwa kama niza kimapokeo au ni za kipekee. Mwandishi ametumia mtindo wa kipekee kabisa kwani ameweza kuchanganya insha,mashairi pamoja na tenzi ambazo kwa ujumla huelezea maisha yake Shaaban Robert hususani katika insha, na katika mashairi na tenzi kuna majonzi, mawaidha, maonyo na maadili.
Aidha, mwandishi ametumia mtindo wa kimapokeo katika mashairi yake, kwani amezingatia urari wa vina na mizani, urari wa mishororo, kibwagizo na utoshelevu katika kila beti. Mfano, ubeti wa 1katika shairi la Amina anasema;
Amina umejitenga, kufa umetangulia,
Kama ua umefunga, baada ya kuchanua,
Nakuombea mwanga, peponi kukubaliwa,
Mapenzi tuliyofunga, hakuna wa kufungua. (Uk. 4)
Katika mfano wa shairi hili lina idadi ya mishororo minne na kila mshororo una urari wa vina na mizani. Hivyo, mwandishi ametumia mtindo wa kimapokeo.
3.2 Muundo
Kwa mujibu Senkoro (kashatajwa), muundo hutokana na umbo na mpango wa kazi ya fasihi. Katika Utenzi wa Hati na Utenzi wa Adili, mwandishi ametumia muundo wa tarbia (mistari minne). Mfano;
KIJANA lete kalamu,
Nina habari muhimu,
Napenda uifahamu,
Dadayo kisha zamuye. (Uk.)
Aidha, muundo uliyotumika katika mashairi yote na tenzi zote ni muundo wa tarbia yaani mistari minne katika kila beti. Mfano, shairi la Amina ubeti.1
Anima umejitenga, kufa umetangulia,
Kama ua umefunga, baada ya kuchanua,
Nakuombea mwanga peponi kukubaliwa,
Mapenzi tuliyofunga hapana wa kufungua.(Uk.4)
3.3 Matumizi ya Lugha
Mwandishi ametumia lugha fasaha na inayoeleweka na wote hasa katika upande wa insha, lakini katika upande wa ushairi kwa kiasi fulani ametumia msamiati wa lugha ya Kiarabu. Mfano, katika shairi la Namshukuru kuna maneno kama vile, Illahi, Alhamdulillahi, Latifu, rakadha na Ashrafu. Vilevile, mwandishi ametumia tamathali za semi kama vile;
Takriri, ni urudiaji wa neno, sentensi au kifungu cha maneo ili kusisitiza jambo. Mfano ubeti wa 1 na 4 Nakuombea mwanga, peponi kukubaliwa pia ubeti wa 4:3 Nawe wangu penzi,peponiutaingia. Neno peponilimerudiwa ili kuonesha msisitizo kwamba baada ya maisha haya kuna maisha mengine peponi (mbinguni). Vilevile katika Utenzi wa Hati neno hati limejitokeza mara nyingi mfano, ubeti wa 1, 2, 5, 6, 7, 8, 9, 10, 17…….
Tashbiha, shairi la “Amina” ubeti wa 1:2 uk.4 “Kama ua umefunga baada ya kuchanua”. Neno “kama” ni tashbiha inayotumika kulinganisha vitu viwili.
Vilevile hata katika “Utenzi wa Hati na Adili Uk.7 ubeti wa 7:4 tunaona tashbiha zikijitokeza. Anasema, “Nakupenda kama Hidaya” na ubeti wa 6:3 anasema, “Tunza kama sahibu”
Tashihisi, kukipa kitu kisicho hai uwezo wa kutenda. Mfano; ubeti wa 6:2;3 uk.5 anasema,
Vumbi tena likiunga, roho likirudishiwa,
Mauti yakijitenga, mapenzi yatarejea. (Uk. 5)
Pia katika Utenzi wa Hati na Adili Uk.7 ubeti wa 6:1 anasema, Dunia ina aibu. Hapa dunia inapewa sifa ya ubinadamu ya kuona aibu. Vilevile uk.8 ubeti wa 17:3 anasema,Sauti yendavyo mbio. Hapa napo sauti inapewa uwezo wa kukimbia kama kitu chenye uhai. Pia Uk.27 ubeti wa 43:2 Viungo vyake husema. Viungo mbalimbali vya mwili vinapewa uwezo wa kusema kama binadamu.
Sitiari: kitu kupewa jina la kitu kingine. Hii ni katika Utenzi wa Hati na AdiliUk.13 ubeti wa 50:3 anasema, Mtu mwongo ni msongo. Mtu mwongo anafananishwa na mtu asiyechezwa unyago/asiyefundwa. Pa Uk.15 ubeti wa 64:1 mama anafananishwa na kitu cheupe, kitu safi. Anasema “Mke ni nguo nyeupe”.
Misemo, ni kauli fupifupi zenye ujumbe mzito. Kwa mfano: uk.9 ubeti wa 20:1 “Dunia ni Mvurugo” yaani inamaanisha kuwa duniani kuna mabaya na mazuri, hivyo tunapawa kuwa waangalifu. Pia uk.6 ubeti wa 5:1, “Ulimwengu una adha” pia uk.13 ubeti wa 54:1 “Ulimi wa pilipili”
Methali, Uk. 9 ubeti wa 22:2 Cheche huzaa moto yaani kitu kidogo chaweza kuleta madhara makubwa. Pia uk10 ubeti wa 28:1 Dunia mali ya roho pia katika shairi la “Ujane” uk. 82 ubeti wa 4:1 Ujane neno la feli, kugombana watu wema.
Taswira, katika Utenzi wa Hati Uk.26 kuna taswira ya hereni. Hapa mwandishi anamfananisha hati na pambo la sikioni, anaona kuwa binti yake akizingatia hayo atafanikiwa maishani. Pia kuna taswira ya pilipili (kitu kichungu) ubeti wa 54. Utenzi wa Hati na Adili anamuasa mwanaye asiwe na ulimi kama wa pilipili bali awe na kauli ya upole na faraja siku zote.
4.0 Mandhari
Mandhari mbalimbali yamejitokeza katika riwaya hii, mwandishi ametumia mandhariya Kitanzania ambapo amezungumzia mandhari ya mjini wa Tanga, Dar es Salaam, Dodoma na mandhari mbalimbali kama vile; mandhari ya nyumbani, forodhani, ofisini nakadhalika. Mandhari katika riwaya hii imesaidia sana kufikifisha kile alichokusudia mwandishi kiwafikie wananchi.
5.0 Jina la Kitabu
Jina la kitabu Maisha Yangu na Baada ya Miaka Hamsini, linasadifu kabisa yaliyomo katika kitabu. Kwani kazi yake yote mwandishi ameigawa katika sehemu kuu mbili sehemu ya kwanza ni Maisha yangu na sehemu ya pili ni Baada ya Miaka Hamsini. Vilevile katika kuelezea maisha yake ameelezea kwa mtindo wa insha, mashairi na utenzi. Na katika kila kichwa cha insha, shairi na utenzi vimesadifu kabisa yaliyomo ndani yake.
6.0 Wahusika
Maisha Yangu na Baada ya Miaka Hamsiniimetumia wahusika halisikabisa. Ambapo wametumiwa na mwandishi kueleza historia ya maisha ya mhusika mkuu ambaye ni Shaaban Robert. Wahusika wengine ni hawa wafuatao; Amina, Hati, Adili, Waafrika, Wazungu, Mudir, na wahusika wengine waliyotumiwa na mwandishi ili kufikisha ujumbe kwa jamii.
7.0 Kufaulu na Kutofaulu kwa Mwandishi
Mwandishi amefanikiwa kwa kiasi kikubwa sana, kwani mambo aliyoyandika yana halisika katika maisha yetu ya kila siku. Kutokufaulu kwa mwandishi kunaonekana ambapo mwandishi ameelezea mambo mengi kwa kufuata imani ya dini ya Kiislamu na kusahau kwamba anaowaandikia ni mchanganyiko wa imani tofauti tofauti. Pia amejikita zaidi katika mambo dhahania kama vile Mungu. Vilevile, hata lugha aliyoitumia kwa kiasi fulani ina msamiati wa Kiarabu hasa katika ushairi, hivyo inawawia vigumu kuelewa wale wasiojua lugha ya Kiarabu.
Kwa ujumla, sisi kama wachambuzi wa kazi hii tunaweza kusema kwamba Shaaban Robert ni kivuli kinachoishi, kwani mambo mengi aliyoyaeleza bado yapo katika jamii ya leo na kazi yake bado inamashiko na itaendelea kuwa na mashiko hata kwa vizazi vijavyo. Aidha, kipengele cha mandhari, wahusika pamoja na vipengele vingine vyote tulivyovijadili na ambavyo hatujavijadili vimetumika kuonyesha mambo yalivyo katika jamii.
MAREJELEO
Mulokozi, M.M (2017). Utangulizi wa Fasihi ya Kiswahili, Kozi ya Fasihi Vyuoni na Vyuo Vikuu.
Moccony Printing Press: Dar es Salaam.
Ntarangwi, M. (2004). Uhakiki wa Kazi za Fasihi. Augustana College, Rock Island, IL 61201
Robert, S. (1991).Maisha Yangu na Baada ya Miaka Hamsini. Mkuki na Nyota Publishers. Dar
es Salaam.
Senkoro, F.E.M. K (2011).Fasihi. KAUTTU Limited: Dar es Salaam.