Katika
uhakiki wa diwani ya Mapenzi Bora, utaangazia utangulizi na kiini. Ambapo
katika utangulizi utaangazia shabaha ya kitabu hiki na kiini utaangazia
vipengele vya fani na maudhui.
Utangulizi.
Mapenzi Bora
ni diwani iliyoandikwa na Shaaban Robert mwaka 1958. Diwani hii yenye beti 700,
dhumuni ni kuiadili jamii juu ya maana, faida na hasara za kukosa mapenzi bora.
Kusudi la kitabu hiki ni kuandalia mahitaji ya watu waliofikia fahamu ya kuwaza
na kuhoji neno au kitu au tendo kwa akili ingawa haitakuwa vibaya kama
kitasomwa na watu wowote ambao hawajafikia upeo kama huo wakipenda kujiweka
tayari kwa zamu yao.
Fani
na Maudhui ya kitabu hiki.
Kipengele
cha Maudhui, kipengele hiki kinahusisha dhamira, ujumbe, falsafa ya mwandishi
na msimamo wake.
DHAMIRA
Samwel
na wenzake (2013) wanaeleza kuwa dhamira ni mada, lengo, kusudi, wazo kuu
linalozungumzwa na shairi au kazi ya sanaa. Wanaongeza kuwa katika mashairi huweza
kuwa na dhamira ya kiuchumi, kijamii, kisiasa na hata kiutamaduni. Pia, katika
kazi ya fasihi kunaweza kuwa na dhamira kuu na dhamira ndogondogo.
DHAMIRA KUU
Mapenzi
yaliyo bora, katika diwani hii dhamira ya mapenzi yaliyo bora ndiyo dhamira
kuu. Katika kueleza suala hili la mapenzi bora mtunzi amefafanua kwa namna
tofautitofauti.
Mosi,
mtunzi ameonesha maana ya mapenzi bora ni yapi, mwandishi anaona kuwa mapenzi
bora ni mapenzi ya kumcha Mungu. Mungu ndiye muumba wa Ulimwengu na ndiye
anayeamua jaala za wanadamu. Hivyo basi, ni muhimu kupenda na kumjali Mungu.
Mathalani ubeti wa 122, mtunzi anasema:-
“Tusihini
walimwengu,
Mapenzi tumpe Mungu,
Naye
atatupafungu,
Katika
wake wenezi.”
Kwa
mantiki hii, inaonesha kuwa mapenzi yaliyo bora kwa wanadamu ni kumtii muumba
wa ulimwengu.
Pili, mtunzi anaona kuwa mapenzi yaliyo bora
ni yale ya kuthaminiana wenyewe kwa wenyewe bila kubaguana au kutengana na
kuangalia tofauti zetu kama vile rangi, dini, kabila na hali ya ukiuchumi. Kwa
mfano, katika ubeti wa 123, mtunzi anasema:-
“Tupendane
wenyewe,
Tofauti tuondoe,
Amani iyushukie,
Mapenzi tufanye ngazi.”
Vilevile,
mtunzi katika kuelezea suala la mapenzi bora mtunzi amebainisha sifa mbalimbali
za mapenzi bora kama ifuatavyo;
Mtunzi
anasema mapenzi bora ni kama pambo la moyo, anaona mapenzi bora ni jambo zuri linaupendezesha
moyo na haliishi uzuri wake. Kwa mfano, katika ubeti 467, mtunzi anasema;
“Mapenzi
pambo la moyo,
Nifuraha kuwa nayo,
Mapenzi
hushinda cheo,
Hata pato la ghawazi.”
Kwahiyo,
mtunzi anaona kuwa mapenzi ni muhimu kushinda hata cheo alichonacho mtu.
Pia,
mapenzi bora ni kitu cha thamani na endapo yatatoweka itakuwa gharama kubwa
sana kuyarejesha. Mathalani, katika ubeti 103- 104, mtunzi anasema;
“Wote
wapige mayowe,
Mapenzi wayalilie,
Kwa kutaka yarejee,
Na kurudi hayawezi.”
“Watayataka
kwa pesa,
Yawape tena fursa,
Kitu walichokifyosa,
Huwaje tena kipenzi!”
Vilevile,
mapenzi bora hayaendani na aina yoyote ya chuki na ni dawa ya kuondokana na
chuki. Kwa mfano, katika ubeti wa 471, mtunzi anasema;
“Kitu
hiki ni mithaki,
Kwa waelewa wa haki,
Mapenzi ni dawa ya chuki,
Kwa watu wavumilizi.”
Pia,
mtunzi ameonesha faida ya kuwa na mapenzi bora kwa jamii kamaifuatavyo;
Endapo
watu watakuwa na mapenzi bora wote hujiona wa namna moja pia, hawataona tofauti
zao za mambo kama ubaguzi na rangi. Kwa mfano, katika ubeti wa 147, mtunzi
anasema;
“Mapenzi
wanayo wengi,
Wanadamu kila rangi,
Lakini hayawaungi,
Kwa sera ya ubaguzi.”
Pakiwa
na mapenzi bora dhuluma itatoweka na haki itatawala katika jamii. Mtunzi anaona
kuwa haki usawiri sehemu penye mapenzi bora. Mathalani katika ubeti wa 627,
628, 630- 631, mtunzi anasema;
“Wanadamu
kwa wanyama,
Na wadudu wa kuuma,
Walisafiri salama,
Kwa imani na mapenzi.”UK.
628
Mapenzi
bora huepusha majanga mbalimbali yaliyo katika jamii kama vile, chuki na
uchoyo. Kwa mfano katika ubeti wa 66 mtunzi anasema;
“Ulimwengu kama huu,
Wenye mashaka makuu,
Kimbilio na nafuu,
Ni palipo na mapenzi.”
Aidha,
mtunzi ameonesha hasara ya kutokuwa na mapenzi bora katika jamii kama
ifuatavyo;
Mapenzi
yakisawiri na chuki husababisha kupotewa kwa amani katika jamii. Pia, anaongeza
kuwa chuki ikisawiri katika jamii ni kitu hatari kama moto. Mtunzi anasema
kwenye ubeti 333;
“Chuki
inashinda moto,
Ikisadifu
mateto,
Chuki ni kitu kizito,
Kuweka hatukiwezi.”
Kukosekana
kwa mapenzi bora katika jamii, hufanya watu wadhulumiane na wabaguane katika
jamii. Mtunzi anasema katika ubeti wa 126;
“Ubaguzi
ni husuda,
Wala
hauna faida,
Unadhuru kila muda,
Katika kila kizazi.”
DHAMIRA NDOGONDOGO
Suala
la chuki, mtunzi ameonesha kuwa chuki ni jambo mbaya sana na ina madhara pia
ameifananisha na laana, huleta maudhi na husababisha athari kwa muda mfupi.
Mfano ubeti 335, 336 na 345;
“Chuki
madhara ya dhati,
Afadhali ya mauti,
Ni
faradhi kwa umati,
Chuki inanyong’onyezi.”UK.
335
Suala
la matabaka, mtunzi amejaribu kuweka wazi namna jamii yetu ilivyo na matabaka
hasa tabaka la wenye nacho na tabaka la wale wasonacho ikiwa na maana ya
masikini. Mfano katika ubeti wa 95 mtunzi anasema;
“Masikini
na tajiri,
Watu wa kila umri,
Kulia
watakithiri,
Kama hili hubarizi.”
Suala
la uchoyo, mtunzi ameonesha kuwa uchoyo ni tatizo kubwa, humfanya mtu asiwe na
mapenzi kwa wenzake pia usababisha uhasama na upumbavu. Kwa mfano, mtunzi
anasema ubeti 378;
“Choyo
kikishika mila,
Hakimpi mtu kula,
Wala
nafasi kulala,
Hurukwa na usingizi.”
Suala
la ulevi, mtunzi amejaribu kuonesha kuwa ulevi wa pombe na mihadarati humfanya
mtu asiwe na mawazo na fikra njema, hawe bwege na akili zisimtoshe. Kwa mfano,
katika ubeti 50-52, mtunzi anasema;
“Nahofu kanywa kangara,
Kileo chenye madhara,
Na
fikra zimegura.
Kuzingatia hawezi.”
“Nahisi
kalewa mbege,
Na sawa na mtu bwege,
Mapenzi tunda za ndege,
Wanyama na sisimizi.”
UJUMBE
Samwel
na wenzake (2013) wanasema ujumbe ni yale mambo ambayo mshairi angependa
hadhira yake ijifunze ili kuweza kufanikisha misimamo iliyojengwa na mshairi
huyo.
Mtunzi
amebainisha ujumbe wa aina mbalimbali katika diwani hii kama ifuatavyo;
Mosi,
Binadamu wote bila kujali tajiri ama masikini anahitaji mapenzi ya dhati na
yaliyo bora, kwa sababu mapenzi yanatija kwa matabaka yote. Kwa mfano katika
ubeti 95.
Pili,
mapenzi ya kweli ni muhimu katika mzungumzo wa maisha, kwa kuwa mapenzi ni
uguzo kwa wagonjwa na ni faraja kwa yatima. Mfano, ubeti 251- 252
FALSAFA
Wamitila
(2003) anasema falsafa ya mwandishi ni mawazo au wazo alilo nalo juu ya kile
anachokiamini kuwa kina msingi unaotawala maisha.
Mtunzi
wa diwani hii, anaamini kuwa dunia au nchi itakuwa na utulivu na amani endapo
jamii bila kujali kabila, dini, rangi na matabaka watakapo na mapenzi bora
wenyewe kwa wenyewe na mapenzi kwa mwenyezi Mungu muumba wa ulimwengu na Mungu
atatupatia thawabu.
MSIMAMO WA MTUNZI
Mtunzi
anaamini kuwa mapenzi ya kweli ni muhimu kwa maendeleo ya Nyanja zote za maisha
ya binadamu.
FANI
Katika
kipengele cha fani kinahusisha muundo na mtindo wa mtunzi.
MUUNDO
Senkoro
(2011) anasema muundo wa kazi ya fasihi ni mpangilio na mtiririko wa kazi hiyo
kwa upande wa visa na matukio. Kwahiyo,
mtunzi ana namna yake ya kusuka, kufuma, kuunda na kuunganisha tukio moja na
lingine.
Mtunzi
ametumia muundo wa tarbia ambao kila ubeti wa shairi una mishororo mine. Na
mshororo wane ni kituo.
MTINDO
Njogu
na chimerah (1999) wanasema kuwa hakuna njia moja ya kuelezea mtindo. Lakini
kwa ujumla twaweza kusema kwamba mtindo ni tabia ya utungaji inayopambanua
mtunzi mmoja na mwingine.
Katika
diwani hii mtunzi ametumia mtindo
unaofuata kanuni za ushairi wa kamapokeo, yenye vina, ulinganifu wa mizani na
mpangilio wa beti. Kila ubeti una vina vya mwisho ambavyo ni “nzi” na “zi” na
kila mstari una mizani 8.
MATUMIZI YA LUGHA
Tamathali
za semi
Senkoro
(k. h. j) anasema ni maneno, nahau au sentensi ambazo hutumiwa na wasanii wa
fasihi ili kutia nguvu katika maana, mtindo na hata sauti katika maandishi ama
usemi. Wakati mwingine hutumiwa kama njia ya kuipamba kazi ya fasihi na
kuongeza utamu wa lugha. Katika diwani hii tamathali za semi zilizojitokeza ni
kama zifuatazo;
Sitiari,
Senkoro (2011) anasema sitiari ni kama tashibiha hulinganisha vitu ama watu
bila kutumia viunganishi-linganishi.
Sitiari
zilizoibuka ni mapenzi ua la moyo, mfano ubeti 161. Kwahiyo, mtunzi alimaanisha
kuwa mapenzi hufurahisha na kupendezesha moyo kwa mwenye nayo.
Pia,
sitiari nyingine ni chuki mwanawe ni kondo.
Ubeti 280
Maisha
ni utelezi, katika ubeti 641. Mtunzi akiwa na maana maisha muda wowote yanaweza
kukatika.
Tashihisi,
Senkoro (k. h. j) anasema kuwa tamathali hii wakati mwingine huitwa fasili ya
binadamu, kuvipa sifa ya kibinadamu vitu visivyo na si hizo. Tashihisi
zilizojitokeza katika diwani hii kama vile;
Tunachekwa
na wadudu wajinga wa kuabudu, kwa mfano, ubeti 201. Mtunzi anawapa sifa ya
kucheka wadudu kama binadamu. Pia, chuki ilie kwa wivu, mfano ubeti 583. Kondoo na mbwa mwitu
hawakuteta kwa kitu, mfano ubeti 630.
Tashibiha,
Gibbe (1980) anasema kuwa ni tamathali ambayo hulinganisha vitu viwili kwa
kutumia viunganishi linganishi mbalimbali kama vile, mithili ya na kama kwamba.
Tashibiha zilizoibuka katika diwani hii ni;
Mapenzi
kwa mwanadamu, kama mshipa na damu, mfano ubeti 86. Akiwa na maana ya utegemezi
wa vitu hivi viwili.
Twanuka
kama kutuzi, mfano ubeti 298. Mtunzi anaona wasio na mapenzi bora wananuka kama
kutuzi.
Mubaalagha,
Mulokozi na Kahigi (1979) wnasema kuwa dhima ya mubaalagha ni kuongeza utamu na
kuleta athari fulani. Kwa mfano katika diwani hii mubaalagha kadhaa
imejitokeza;
Nyuso
zikifanya mito, ya machozi ya fukuto, katika ubeti 94
Nyuso
zete zitatota kwa bahari ya machozi, katika ubeti wa 93
MBINU NYINGINE ZA KISANAA.
Takriri,
Msokile (1993 ) anasema takriri ni moja kati ya vipengele vya matumizi ya lugha
katika kazi ya fasihi ambapo kuna kuwa na marudirudio ya herufi, silabi, neno
kirai, sentensi na wakati mwingine hata aya nzima. Katika diwani hii takriri
zilizoibuka ni kama zifuatavyo;
“Chuki”
katika beti ya 330- 336, kuna “choyo” katika ubeti wa 364- 385, kuna “tata na
tatizi” katika ubeti wa 296-297.
Mazida,
ni mbinu ya kisanaa ambayo mtunzi hurefusha neno kwa lengo la kupata vina ama
idadi ya mizani, kwa mfano;
Neno,
“zamani” katika mshororo usemao “watu wa zamani hizi” akimaanisha “zama hizi” ubeti wa 98. Pia,
“wataalumuzi” katika ubeti wa 648 akimaanisha “wataalamu”
KUFAULU KWA MTUNZI
KIFANI
Mtunzi
ametumia Kiswahili fasaha kilichojaa tamathali za semi kama vile, tashihisi,
sitiari mbaalagha, tashibiha na mbinu nyingine za kisanaa kwa lengo la kuipamba
kazi yake na kuongeza utamu wa lugha.
KIMAUDHUI
Mtunzi
ameonesha umuhimu wa kudumisha mapenzi bora kwa jamii, pia ameonesha mapenzi
bora ni yapi na kujaribu kuonesha mambo ambayo jamii inaweza kukumbananayo
wasipo zingatia kuwa na mapenzi bora. Wamitila, K. W. (2003). Kichocheo cha
Fasihi: Simulizi na Andishi. Nairobi: focus publications Ltd.
MAREJELEO
Gibbe,
A. G. ( 1980). Shaaban Robert: Mashairi.
Dar es Salaam, Tanzania Publishing House.
Mulokozi,
M. M. na Kahigi, K. K. (1979). Kunga ya
Ushairi na Diwani Yetu. Dar es Salaam.
Tanzania Publishing House.
Njogu,
K. na R. Chimerah (1999). Ufundishaji wa
Fasihi: Nadharia na Mbinu. Nairobi.
Kiswahili Tertiary
Publishing Project.
Robert, S, (1958). Mapenzi Bora. Dar es Salaam. Mkuki na Nyota publishers Limited.
Samwel,
M na wenzake, (2013). Ushairi wa
Kiswahili, Mwongozo kwa Walimu wa Kiswahili na
diwani ya MEA. Dar es Salaam. Mevelli Publishers.
Senkoro,
F. E. M. K.(2011). Fasihi. Dar es
Salaam, KAUTU Limited.