Friday

Kampuni ya Samsung yawekeza Sh50 trilioni katika teknolojia mpya za 5G, AL

0 comments

 Jinsi AI inavyoweza kusaidia kufanya kazi katika sekta mbalimbali bila usimamizi wa binadamu| Picha Mtandao.
  • Kiwango hicho cha fedha kimejikita zaidi katika tafiti mbalimbali za kuziwesha mashine zifanye kama binadamu (Artificial Intelligence) na kwenye mtandao wa 5G.
  • Mradi huo unatarajia kuajiri watafiti 1,000 duniani kote. 

Kampuni ya Samsung imepanga kuwekeza Dola za Marekani 22 bilioni kwa ajili ya kugharamia tafiti kuhusu uendelezaji wa mtandao wa 5G na teknolojia ya kuziwesha mashine kufanya kazi kama binadamu maarufu kwa Kiingereza kama Artificial Intelligence (AI) ikiwa ni moja ya mikakati yake ya kukabiliana na kasi ya ushindani ulimwenguni.
Katika teknolojia ya AI mashine inapewa uwezo wa kujifunza na kutatua matatizo kama ambavyo binadamu angefanya bila usimamizi wa mtu.
Kiwango hicho cha fedha ambacho ni sawa na zaidi ya Sh50 trilioni kitatumika kwa miaka mitatu ikiwa ni zaidi ya mara moja na nusu ya bajeti ya Serikali ya Tanzania kwa mwaka wa fedha wa 2018/19 ambayo ni Sh32.5 trilioni. 
Katika mradi huo Samsung imepanga kuajiri watafiti 1,000 kutoka pande mbalimbali ulimwenguni. Watanzania wenye ujuzi wa masuala hayo ya 5G na AI wanaweza kubahatika kuwa moja ya  watafiti hao ambao Samsung inawasaka kwa ajili ya kufanikisha mradi huo.
Tafiti za teknolojia hizo mbili ni moja ya vitu vya lazima katika maendeleo  ya utengenezaji magari yatakayojiendesha yenyewe ambayo yanategemea zaidi matumizi ya 5G na AI.
Shirika la habari la Marekani la CNN liliripoti Agosti 2018 kuwa mbali na kiasi hicho cha fedha, watatumia  jumla ya Dola za Marekani 160 bilioni kwa ajili ya maendeleo ya kampuni, kufanya tafiti mbalimbali na kufungua nyumba za ubunifu ili kupata mawazo ya kibunifu katika uwekezaji huo. Kampuni hiyo ya vifaa vya kielektroniki inatarajia kuzalisha ajira mpya 40,000 ndani ya kipindi hicho cha miaka mitatu. 
Licha ya changamoto walizokumbana nazo miaka ya hivi karibuni ikiwemo Skendo ya rushwa iliyomkuta kiongozi wao Lee Jae-yong, Samsung bado imeendelea kuongoza katika uzalishaji wa Simu Janja (Smartphones) huku ikiendelea kupata upinzani mkubwa kutoka kwa kampuni ya Huawei na Xiaomi kutoka China.

No comments:

Post a Comment