Utoshelevu Wa Fasili Na Visawe Vya Vidahizo Katika Kamusi Ya Kiswahlli Sanifu
H.M. Batibo
mchapishaji
masshele
Utangulizi
Katika mkutano wa Chama cha Wanaleksikografia cha Amerika ya
Kaskazini uliofanyika Julai 1978, mada moja iliwasisimua sana wajumbe wa
mkutano. Mada hiyo ilitolewa na nwanaleksikografia mkongwe Prof. Sherman M.
Kuhn, juu ya "Mbinu za Kuandika Fasili"2 (Kuhn, 1980:115 - 121). Mada
hiyo ilieleza matatizo mengi yatokanayo na fasili za vidahizo katika kamusi.
Baadhi ya matatizo yaliyojitokeza katika mada ya Kuhn ni kutotosheleza kwa
fasili, tofauti za visawe, upana usio na mipaka halisi wa uwanja wa matumizi, na
utata wa upambanuzi.
Makala haya yatachunguza ubora wa fasili za vidahizo katika
Kamusi ya Kiswahili .Sanifu (kifupi KKS). TUKI (1981), kwa kuangalia
jinsi ilivyozingatia kanuni za fasili. Baadaye itachambua namna visawe
vilivyotumiwa katika kamusi hiyo. Mwisho, tutatoa mapendekezo ya namna ya
kuirekebisha au kuiboresha KKS. hasa pale inapohusu fasili na visawe.
Utoshelevu wa Fasihi katika KKS
Fasili ni Nini?
Swali la fasili ni nini lilianza kujitokeza tangu zama za Plato
na Aristotle. Dhana muhimu ni kutofautisha kati ya fasili ya kimantiki, ambayo
huelezea na kupambanua kitu kilivyo kiulimwengu au kisayansi, na fasili ya neno,
ambayo hulielezea na kulipambanua kufuatana na jinsi linavyoeleweka na kutumiwa
na wazungumzaji wa kawaida (Landau, 1984:120). Hivyo, fasili ya neno haina budi
kuelezea na kupambanua maana ya leksimu kwa maneno yenye maana ileile, na
yanayoeleweka zaidi katika mazingira hayo (Ogden na Richards, 1923). Fasili
katika kamusi lazima iwe dhahiri, inayolenga na inayojitosheleza (Mdee, 1993:1).
Kanuni za Fasili
Zgusta (1971) anapendekeza kanuni nne katika kutoa fasili nzuri,
nazo ni hizi zifuatazo:
a) Maneno yote katika fasili hayana budi kuelezwa.
b) Fasili isiwe na maneno magumu zaidi ya neno linaloelezwa.
c) Kidahizo, wala kinyambuo chake, visitumike kama sehemu ya fasili.
d) Fasili iwiane na aina ya neno linalofasiliwa.
Kwa ujumla, kanuni hizi zimekubalika kimsingi kwa sababu ya
mantiki yake. Isipokuwa yamependekezwa marekebisho katika (c) kuwa kinyambuo
kinaweza kutumiwa katika fasili iwapo chenyewe kimepewa hadhi ya kidahizo
(Landau, 1984:124).
Kanuni nyingine zilizopendekezwa na wanaleksikografia ni hizi
zifuatazo (Landau, 1984:124-138):
e) kutozungukazunguka kwa kufasili maana ya neno moja kwa neno jingine na neno hilohilo ukalipa fasili ya neno la kwanza.
(1) Injnia ji mtaalamu wa uhandisi3
Uhandisi ji kazi aifanyayo injinia
f) hakikisha unaeleza na kupambanua kidahizo, na siyo kuzungumza juu yake au matumizi yake. Hivyo m muhimu kuwa kila fasili ieleze aina (genus) ya neno na pia ipambanue tofauti (differentia) na maneno mengine ya aina yake.g) Maana ya msingi ipewe kipaumbele. Kwa kawaida maana ya msingi hulingana na fasili ya neno katika mawazo ya mtu wa kawaida au matumizi ya watu walio wengi.h) Fasili iwe fupi na inayolenga dhana inayoelezwa.i) Fasili iepuke maelezo marefu au yasiyo wazi kwani yanaweza kumkanganya au kumpotosha mtumiaji wa kamusi.j) Fasili ihaldkishe kuwa inamlenga mtunaiaji wa kamusi wa kawaida ambaye si mtaalamu wa nyanja zozote.
Mojawapo ya manufaa ya kanuni hizi ni kumrahisishia mtumiaji wa
kamusi ambaye:
(a) mara nyingi si mzungumzaji hodari wa lugha ile
(b) si mtaalamu wa uwanja ambao neno hutumika kitaalamu.
(c) hana muda wa kupekua maana ya maneno magumu yaliyotumiwa katika fasili.
(d) hukata tamaa ikiwa baadhi ya maneno ya fasili hayamo katika kamusi
(e) huwa na kiu ya kujua taarifa zote za polisemu na matumizi yote ya kidahizo ili afahamu jinsi ya kukitumia.
Utoshelevu wa KKS
KKS uneweza kutosheleza fasili kwa kiwango kikubwa, katika
sehemu zifuatazo:
Kuzingatia Aina za Maneno
Kwa ujumla fasili zimezingatia aina ya maneno ya vidahizo.
Nomino zimefasiliwa kwa nomino au vikundi nomino. Vivumishi vimeelezwa kwa
kutumia vivumishi vingine, vikundi vivumishi au vishazi rejeshi. Vitenzi
vimefasiliwa kwa vitenzi au vikundi vitenzi. Vielezi, viingizi na aina nyingine
za maneno zimeelezwa kwa maneno au vikundi vya maneno vilivyo katika aina
ileile. Utata unajitokeza katika kueleza maneno yanayotumiwa kisarufi kama vile
viunganishi, vihusishi na vihisishi. Hapa mara nyingi fasili haikupambanua ila
imeeleza dhima au matumizi ya kidahizo katika lugha.
Kutokuwa na Fasili za Mzunguko
Kwa ujumla maneno ya msingi katika fasili yameelezwa bila
mzunguko ambao ungesababisha utata kama mfano wa Landau (1984:124)
unavyoonyesha4.
(2)
(a) beauty n the state of being beautiful beautiful adj full of beauty
(b) bobcat n lynx lynx n bobcat
Fasili za mzunguko huwakatisha tamaa watumiaji wa kamusi kwa
vile hakuna anachoambulia. Bahati nzuri fasili nyingi katika KKS zimejumuisha
maelezo na visawe ili kuieleza na kuipambanua kila maana ya kidahizo.
Kutoegemea Kwenye Mawazo ya Aina Moja
KKS imejitahidi kuwatosheleza watumiaji wa aina zote na wa
mielekeo tofauti ya kijamii, kiitikadi na kitaifa. Kwa mfano neno bepari
limeelezwa kwa kuzingatia mazingira yote ya kiitikadi na kijamii
linamotumika.
(3) "bepari ji ma-
(1) mfanyabiashara mkubwa; tajiri.(2) mwenye kumiliki rasilimali na njia kuu za uchumi katika kuzalisha mali kwa faida yake mwenyewe.(3) mmojawapo katika tabaka la wanyonyaji. (TUKI, 1981:18)
Fasili zisizo na utoshelevu
Pamoja na utoshelevu uliopo katika fasili za vidahizo, zipo pia
kasoro za fasili ambazo zinajitokeza katika KKS. Zifuatazo ni baadhi ya kasoro
hizo:
Maneno Magumu katika Fasili
Watumiaji wa KKS mara nyingi, wamekumbana na maneno magumu
katika fasili kama mifano ifuatayo inavyoonyesha5
(4)
(a) "kidole ji vi-, kiungo kilicho katika ncha ya vitanga vya mikono au miguu"(b) "kelele ji 2. sauti kubwa hasa isiyokuwa na maana yoyote au ya kukirihisha"(c) "kibanda ji vi-, kijumba kidogo kitumiwacho kwa shughuli maalum, k.v. ~cha kuku ~cha kuamilia; ~cha uani.."(d) "kiganja ji vi-, sehemu ya mbele ya kitengele" (TUKI, 1981:105.f)
Katika mifano hii, maneno vitanga, kirihisha, amilia na
kitengele yatawapa shida watumiaji wa kamusi wa kawaida. Ni kweli pia kuwa
si rahisi kila mara kupata maneno rahisi kueleza dhana za kawaida kama vile
kuwa, cheka, angalia au maneno ya dbahania kama ukweli, usawa, na
kadhalika, bila kutumia maneno magumu. Vinginevyo itabidi kutumia maneno mengi
au kuwa na mzunguko wa maelezo (Landau, 1984:135).
Maneno Yasiyokuwemo katika KKS
Ni dhahiri kuwa si rahisi kila mara kuthibitisha kama kila neno
linalotumiwa katika fasili limeelezwa katika kamusi, hasa pale ambapo jopo la
wanaleksikografia limehusika kuandaa kamusi. Hali hii inajitokeza katika KKS
ambamo baadhi ya maneno yaliyo katika fasili hayamo katika kamusi. Baadhi ya
fasili hizo ni hizi zifuatazo6
(5)
a) "nahau ji 1. sarufi"
b) "konyeza kt fanya ishara kwa kuinua ushi".
c) "kikuba ji vi- pambo linalotengenezwa kwa rihani, mkadi, wandani, kilua na asumini..."
d) "kayamba ji matoazi ambayo hutengenezwa kwa matete..." (TUKI, 1981:105.f)
Kutokuwemo katika KKS kwa maneno sarufi, ushi, wandani
na toazi kutawapa shida watumiaji wake wanapotafuta fasili za
vidahizo vilivyoorodheshwa katika mfano wa 5 hapojuu, na vingine vingi vyenye
kasoro za namna hiyo. Vilevile kuna maneno yatokanayo na unyambulishaji,
nahayamo katika kamusi. Watayarishaji wa kamusi bila shaka walifikiri kuwa
mtumiaji atagundua maana yake. Ukweli ni kwamba vinyambuo hivi havijitoshelezi
na mtumiaji hupewa mzigo mkubwa wa kutambua maana yake.
(6)
(a) mfahamikivu. Neno hili limetumiwa katika fasili ya kidahizo erevuka. Siyo rahisi kwa mtumiaji wa kamusi kutambua maana yake hata kama anajua maana ya fahamu au fahamivu ambayo yamo katika KKS.(b) tenganisha. Neno hili limetumiwa katika kidahizo faraka. Siyo rahisi kutambua maana yake kwa kuelewa maana ya tenga peke yake.(c) kilaji. Neno hili limetumiwa katika kidahizo peremende. Ingawa linatokana na kitenzi la lingeweza kufasiliwa kwa makosa kama 'kitu kilacho' na hivyo kuwapotosha watumiaji wa kamusi.(d) majimaji. Neno hili limetumiwa katika kidahizo povu. Maana ya neno hili katika umbo lake la uradidi hailingani na maana yake katika umbo la kawaida (Ashton, 1944).
Kushindwa kutoshelew Fasili ya Kidahizo
Kama tulivyoona hapo juu (2.2.f), fasili m lazima ikielezea kitu
na baadaye ikipambanue. Fasili nyingi katika KKS haziainishi vidahizo
kikamilifu, au kuvipambanua ili kuweza kubainika.
(7)
(a) "kipila ji aina ya ndege"
(b) "kijakazi [A] ji aina ya samaki"
(c) "kijakazi [B] ji aina ya ndizi"
(d) "katolildy ji sehemu moja ya sehemu mbili za ukristo"
(e) "kadinali ji mojawapo wa baraza kuu la Baba Mtakatifu waKatoliki" (TUKI, 1981:95.f)
Fasihi zilizoko katika mfano wa 7. hapo juu, zina kasoro katika
kufafanua maana. Fasili za mifano 7a, - 7c zimeweza tu kuainisha vidahizo lakini
zimeshindwa kuvitofautisha au kuvipambanua na vitu vingine vya aina hiyo. Aidha
mifano 7d na 7e inapambanua maana ya vidahizo bila kuviainisha kikamilifu.
Maana zote za Polisemu Kutoelezwa
Baadhi ya maana za vidahizo polisemu katikaKKS hazikuelezewa
zote.
(8)
(a) ghorofa ji sehemu ya nyumba iliyojengwa juu ya nyingine".Neno ghorofa lina maana zaidi ya moja. Maana ya pili: jengo ambalo lina vyumba katika sehemu ya chini najuu (kama katika mfano "amejenga ghorofa") ingestahili kuingizwa pia.(b) "kigezo ji vi- 1 mtu. kitu au jambo la kuigwa. 2 kielezo cha kushonea nguo. 3 fimbo au uzi wa kupimia, kipimo, rula, utepe".
Maana za neno kigezo hazina uhusiano wa karibu, hivyo
zilipaswa ziorodheshwe kama homonimu tatu. Isitoshe fasili moja muhimu
haikuorodheshwa, nayo ni jinsi au namna ya kupima kitu na thamani yake". (mfano
vigezo vinavyotumiwa kutathmini ubora wa kitu).
(c) "umbo ji ma- mkao wa kitu kilivyoumbwa au kilivyoundwa"
Fasili ya umbo haitoshelezi kwa mtumiaji wa kamusi anayetafuta
neno maumbo katika matumizi ya kisarufi (kama vile, sarufi maumbo).
(TUKI,1981:66f)
Kutumia Sifa Bainifu za kisemantiki zisizofaa au
zinazosabubisha vpotovu wa maana
Baadhi ya sifa bainifu za kisemantiki zilizotumika katika KKS
zinawapotosha watumiaji. Mfano
(9)
(a) "santuri ji chombo kinachotumiwa kutoa sauti za gramofoni".(b) "keki (TUKI, 1981:105) jl kitu kama mkate, bumunda au andazi kinachotengenezwa kwa kuchanganya unga wa ngano, mayai, sukari na hamira pamoja na siagi."(c) "kayamba ji toazi ambayo hutengenezwa kwa matete na ndani hutiwa punje kavu au changarawe na hutikiswa linapopigwa wakati wa ngoma"(d) "kitema8 ji vi- nguo iliyo mbovu".
Fasili ya santuri itambabaisha msomaji kwani
hataelewa kama santuri ni kinanda chenyewe au ni sahani
inayochezwa kwenye gramofoni. Mtumiaji wa kamusi atapata shida kuunda dhana ya
keki ambayo imefananishwa na mkate na andazi, ambavyo
havifanani kwa umbo, mwonjo wala rangi. Fasili ya kayamba imetumia sifa
bainifu za kisemantiki zinazobana mno dhana ya kitu (Landau, 1984:122). Je
chombo hicho hakitakuwa kayamba iwapo badala ya matete kitatengenezwa kwa mianzi
au mbao? Au badala ya punje kavu au changarawe vikatumiwa vijiwe au hata gololi?
Fasili ya kitema, kama Mdee (1993:20) alivyoeleza, itambabaisha mtumiaji wa
kamusi. Je, ubovu wa nguo ni kwa sababu ya kuoza, kupasuka,
kuchakaa, kunuka au kuwa na kasoro ya matengenezo?
Kushindwa Kumlenga Mtumiaji wa Kawaida
Baadhi ya fasili zimeandikwa kisayansi au kitaalamu kiasi kwamba
zinamtatiza mtumiaji wa kawaida.
10) "maji ji ma- kiowevu kisicho na rangi, ladha wala harufu ambacho ni mchanganyiko wa hewa za aina ya oksijeni na haidrojeni na hugeuka mvuke wakati kikipata joto na huwa barafu wakati kikipoa sana. Huonekana kwenye bahari, mito chemichemi n.k." (TUKI,1981:149).
Ingawa ni kweli kuwa fasili inapaswa kueleza maumbile ya kitu na
siyo tu aina na tofauti zake, ni muhimu kuwa maelezo hayo yanaeleweka na
mtumiaji wa kawaida, Kwa hivyo, ufafanuzi juu ya oksijeni na haidrojeni, na
kugeuka mvuke au barafu, siyo sifa zinazoambatana na dhana ya maji kwa
mtu wa kawaida. Pendekezo la Mdee ambalo tutalitoa hapa kama mfano wa 11 ni
mfano wa fasili inayomlenga mtu wa kawaida.
mfano 11
11) "maji ji ma- uowevu unaopatikana katika mito, maziwa, chemichemi, ambao binadamu na wanyama hunywa na hutumiwa na binadamu kufulia, kuogea, kupikia n.k." Mdee 1993:23)
Kushindwa kueleza Fasili kwa Ufupi
Baadhi ya fasili ni ndefu kupita kiasi kwa sababu zimetoa
taarifa ambazo si za lazima, hasa zile zinazohusiana na mazingira, mila, desturi
au maisha yajamii. Ni bora waandaaji wa kamusi watofautishe kati ya taarifa za
lazima na zile ambazo si za lazima.
12) "akiki ji 1. sherehe inayofanywa kwa ajili ya mtoto wakati apatapo umri wa siku nane au baadaye ambapo huchinjwa mbuzi na mifupa yake hufukiwa mizima pengine hufanywa baada ya mtoto kufa iwapo hakufanyiwa". (TUKI, 1981:5)
Mtumiaji wa kamusi hana haja ya kujua maelezo marefu ambayo, kwa
kweli, yanahusiana na mila au utamaduni. Utamaduni huu unaweza kubadilika
kulingana na wakati au mabadiliko ya jamii. Kufuatana na Landau (1984:137),
fasili inaweza kufupishwa na kubakia na maana muhimu. Kwa mfano. kidahizo katika
mfano wa 12 kingeweza kufasiliwa kwa kifupi kama ifuatavyo:
mfano 13
13) akiki ji sherehe anayofanyiwa mtoto wakati apatapo umri wa siku nane au zaidi.
Utoshelevu wa visawe katika KKS
Visawe ni Nini?
Kufuatana na TUKI (1990:55) kisawe9 ni "moja kati ya
maneno mawili au zaidi, yenye maana zinazokaribiana sana". Kawaida, visawe
huongezeka katika lugha kadri lugha inavyozidi kupanuka na kuhitaji vivuli vingi
vya maana, mitindo mbalimbali katika matumizi, au maneno tofauti katika nyanja
maalumu (Landau, 1984:105, Batibo, 1987:42; Batibo, 1989:126).
14)
(a) domicile 'nyumbani' (rasmi sana)
(b) residence 'nyumbani' (rasmi)
(c) home 'nyumbani' (kawaida)
(d) abode 'nyumbani' (kishairi)
(e) shacks 'nyumbani' (kimitaani).
Kufuatana na Zgusta (1971), kuna aina mbili za visawe (i) visawe
kamili10 ambavyo hufanana ki- maana na ki- matumizi katika kila
muktadha, na (ii) visawe karibia" ambavyo hufanana ki- maana na ki-matumizi
katika baadhi tu ya muktadha. Visawe kamili huwa ni nadra sana katika lugha kwa
sababu mara nyingi tofauti hujitokeza katika mojawapo ya sehemu tatu zifuatazo.
(a) Undani na upana wa maana (Designatum)
Ni vigumu kwa sifa bainifu za kisemantiki kuwa sawa katika
uainishaji na upambanuaji wa maana kati ya maneno mawili.
(b) maana ya kimatilaba
Kawaida kila neno lina sifa za kisemantiki za nyongeza ambazo
huhusiana na matumizi yake kijamii au kimtindo.
(c) matumizi katika muktadha mbalimbali
Kila neno huwa limejijengea mazingira yake ya kiisimu na
kitamaduni ambamo hutumika. Visawe kamili, au visawe karibia, kwa kawaida
hujitokeza kawaida katika msamiati wa kitaalamu, au kati ya maneno yenye asili
totauti.
mfano 15
15)
(a) zahanati/dispensari
(b) injinia/mhandisi
(c) falji/kiharusi
(d) irabu/vokali
(e) nasali/king'ong'o
Nafasi ya Visawe katika Kamusi
Kwa vile kamusi ni kitabu cha rejea, kuwepo kwa visawe katika
kuelezea vidahizo ni muhimu sana (Landau, 1984:110). Hii ni kwa sababu kisawe
kinatoa picha ya haraka kichwani kuliko maelezo marefu. Aidha, watumiaji wengi
wa kamusi hutafuta visawe vya neno ili kuepuka kulirudiarudia katika maandishi
au mazungumzo. Hatahivyo, ni muhimu kuwa visawe vitumike kwa uangalifu, kwa vile
vinaweza kumpotosha mtumiaji kwa sababu zifuatazo:;
(a) kutoeleza maana ya kidahizo namna ipasavyo, hasa kama kuna tofauti za kisemantiki(b) kutoeleza matumizi halisi ya kidahizo, hasa katika mitindo na nyanja mbalimbali za matumizi ya neno.(c) kutofafanua wazi muktadha wa kiisimu, hasa unaohusu nafasi ya kidahizo katika mafungu ya maneno au tungo.(d) kutoeleza matumizi ya kidahizo katika mazingira na tamaduni za wazungumzaji(e) kutoeleza nguvu au makali ya kidahizo katika hisia za wazungumzaji.
Kwa hivyo ni muhimu kuwa visawe vitumikapo katika kamusi
vifuatane na upambanuzi zaidi wa mipaka ya maana na matumizi yake.
Utoshelevu wa Visawe katika KKS
Kwa ujumla matumizi ya visawe katika KKS yameweza kutosheleza
katika sebemu zifuatazo:
Fasili kuanza na Maelezo
Waandaaji wa KKS walielewa utata wa visawe, Hivyo, waliamua
kuanza fasili na maelezo kabla ya kuongezea visawe ambavyo visingeweza kumpa
mtumiaji fasili sahihi.
16)
(a) "adhibu kt 1 tesa mtu kwa makosa aliyofanya; rudi"
(b) "bangu ji [A] mapigano baina ya watu; vita". (TUKI,1981:2f)
(c) "kinga ji [B] jambo au kitu cha kujiepusha na madhara; kago".
(d) "eropleni ji chombo kirukacho angani, agh. huwa cha kusafirisha abiria au mizigo; ndege".
Katika mifano hii maneno rudi, vita, kago na ndege
yametumiwa kama visawe vya adhibu, bangu, kinga na eropleni.
Lakini maelezo yaliyotangulia yametoa maana halisi ya vidahizo. Visawe
vimetumika kukamilisha fasili.
Kuepukana na Matumizi Visawe Holela
Kamusi ya Kiswahili Sanifu imeepukana na matumizi holela ya
visawe katika kuelezea vidahizo. Hii imesaidia kuieleza kwa uwazi zaidi maana
halisi ya vidahizo. Tukumbuke kuwa KKS ina vidahizo vipatavyo 20,000, na lugha
yenye visawe vingi kwa kawaida huwa na msamiati kati ya maneno 50,000 na 250,000
(Aitchson, 1980:6-7). Kwa hali hii ni dhahiri kuwa Kiswahili bado ni lugha
changa, kwani haijafikia kiwango chajuu katika kuupanua msamiati wake ili uweze
kulingana na matumizi na mitindo mbalimbali. Maneno mengi bado hayajaweza kuwa
na visawe kamili au vya karibu, Kwa kuzingatia hali hii hatuna budi kukubali
kuwa lilikuwa ni jambo la busara kwa waandaaji wa KKS kuthamini fasili za
maelezo zaidi kuliko.visawe.
Kasoro za visawe vya Kamusi ya Kiswahili Sanifu
Visawe vinavyofafanua vidahizo ya KKS vina kasoro zifuatazo:
Tofauti za kisemantiki za visawe hazionyeshwi
bayana
Mara nyingi visawe vimetumiwa katika kueleza vidahizo bila
kuonyesha tofauti zake za kisemantiki.
17) "mabavu ji nguvu: Tumia ~ "(TUKI, 1981:147)
Lakini kama alivyoonyesha Mdee (1993:16), sifa bainifu za
kisemantiki kwa maneno haya (kidahizo na kisawe chake) ni tofauti. Hivyo fasili
ya mabavu kwa neno nguvu kutampotosha mtumiaji kama mfano
18 (kufuatana na Mdee, 1993:16) unavyoonyesha.
mabavu
|
nguvu
| |||
18)
|
[ + msukumo ]
|
[ + msukumo]
| ||
- nishati
|
+
|
nishati
|
Kutokana na tofauti hizi, maneno haya hutofautiana kimatumizi
kama mifano ifuatayo inavyoonyesha:
19)
a) aliingia kwa nguvu
aliingia kwa mabavub) alilia kwa nguvu
*alilia kwa mabavu12c) ?siasa ya mabavu haifai
siasa ya nguvu haifaid) nguvu za maji
* mabavu yamaji.
Matumizi ya Visawe Zaidi ya Kimoja Kufasili
Kidahizo.
Mara nyingine maana halisi ya kidahizo imekuwa ngumu kuipambanua
kutokana na matumizi ya visawe vyenye maana tofauti.
20) Hapa inakuwa vigumu kujua kama maana ya fahari inajumuisha maana ya ukuu na utukufu au baadhi tu ya sifabainifu "Fahariji [A] 2. ukuu, utukufu". (Ibid:52) za kisemantiki za maneno haya.
Kutopambanua Tofauti za Kilahaja
Mara nyingi visawe vimeelezwa bila kuonyesha tofauti zake za
kilahaja. Kwa mfano, kitabu na gauni vimeelezwa kama visawe vya
buku na kanzu. Lakini, matumizi ya maneno haya kwa maana hizo
yanatofautiana kijiografia. kitabu na gauni hutumiwa Tanzania
bara; na buku na kanzu hutumiwa katika visiwa vya Zanzibar na
Pemba.
Kutoelezea Tofauti za Muktadha
Visawe vingi vimetumiwa kueleza maana ya vidahizo. Lakini,
ingekuwa bora kama tofauti za muktadha na matumizi zingeelezwa barabara.
21) "fa (TUKI. 1981:52) kt 1. tokwa na uhai; ondoka duniani; kuwamaiti; tokaroho: fariki". (TUKI. 1981:52)
Kitomeo hiki kinatupa picha kuwa neno farild ni kisawe
halisi cha fa. Ukweli ni kwamba fa na fariki ni visawe
karibia kama muktadha wa maneno haya unavyoonyesha katika mfano wa 22
22)
(a) nimemkuta mbwa amekufa njiani
* nimemkuta mbwa amefariki njiani(b) amekufa maji
* amefariki maji(c) amefiwa na mtoto wake
* amefarikiwa na mtoto wake(d) mama yangu mzazi amefariki leo usiku
* mama yangu mzazi amekufa leo usiku,(e) mgonjwa amefariki dunia
* mgonjwa amekufa dunia
Kutoeleza Mipaka ya Usawa wa Visawe
Mara nyingi visawe vimetumiwa bila kueleza mipaka ya usawa wa
visawe hivyo. Kwa mfano, eropleni imeelezwa kama kisawe cha ndege
(TUKI, 1981:51). Lakini ndege ina maana nyingine ambayo haihusiani na
eropleni nayo ni 'nmyama arukaye anayefanana na kuku.' (TUKI, 1981:211).
Ilikuwa muhimu kwa KKS kutaarifu kuwa ni maana ya 3 tu chini ya ndege
ndiyo yenye maana sawa na eropleni 'namna ya mashine ya kusafiri hewani'.
Baadhi ya kamusi, kama vile Le Petit Robert, zinataarifu juu ya polisemu
zinazohusika kati ya visawe.
Kutotofautisha Matumizi ya Mitindo kati ya Visawe
Baadhi ya visawe vimetumiwa kueleza dhana ya kidahizo bila
kuonyesha tofauti za mtindo.
23) "hela ji [A] pesa, fedha" (TUKI, 1981:78)
Hela hutumika katika mazingira yasiyo rasmi kama mifano
inayofuata inavyoonyesha,
24)
(a) *Hela nyingi zimetengwa na serikali kwa ajili ya mradi huo.Fedha nyingi zimetengwa na serikali kwa ajili ya mradi huo.(b) Yakhe, nipe hela yangu! (mitaani)Yakhe, nipe fedha zangu! (mitaani)
Hitimisho
Mapendekezo ya Jumla
Katika makala hii tumeona jinsi KKS ilivyoweza kutosheleza na
pia kutotosheleza katika kueleza maana ya vidahizo kwa njia ya fasili na visawe.
Kwa kuzingatia kuwa maana ya kidahizo ndiyo kipengee muhimu ambacho watumiaji
wengi wa kamusi hutafuta (Bejoint, 1981; Quirk, 1973), ni muhimu kwamba maana
zinazotolewa ni sahihi, kamili, wazi na zinazojitosheleza. Ili kupunguza kasoro
na utata ulio katika fasili na visawe vya kamusi, wanaleksikografia wengi
wamechukua hatua zifuatazo:
Kutumia Mifano ya Matumizi
Ili kuonyesha matumizi sahihi ya vidahizo katika lugha
inashauriwa pawe na mifano mingi inayoonyesha muktadha, mazingira ya kiisimu na
utamaduni, matumizi ya mitindo, nahau na misemo. Vidahizo vingi katika KKS
havina mifano ya kuridhisha.
Kutumia Picha Kujaliza Fasili
Kamusi nyingi kama vile Oxford Advanced Learners Dictionary
of Current English na A Concise English-Swahili Dictionary hutumia
picha kuonyesha vitu, hasa vya kiteknolojia au utamaduni, ambavyo si rahisi
kuvieleza kwa maneno matupu. KKS haikutumia mbinu hii.
Kudondoa Maandishi ya Watu Maarufu
Baadhi ya wanaleksikografia hutumia madondoo kutoka maandishi ya
watunzi maarufu ili kuonyesha muktadha halisi wa maneno. Kwa mfano, Le Petit
Robert imetumia mifano ya waandishi mashuhuri kama vile Balzac, Bernanos,
Zola, Stendhal na Barbe. KKS imetumia mifano ya kubuni au kuambatanisha nahau,
misemo au methali ambamo maneno hayo yametumiwa.
Kueleza Mazingira ya Maneno
Baadhi ya wanaleksikografia wametumia nyenzo za kiteknolojia
kama vile kompyuta ili kukusanya na kurekodi maandishi mengi, kama vile
magazeti, vitabu, makala na ripoti kwa madhumuni ya kuchambua mazingira ya kila
neno.13 Hii inasaidia sana katika kuelezea mazingira yote ya neno
kiisimu, kimtindo na kitamaduni. Mbmu hii hupunguza manung'uniko ya baadhi ya
wazungumzaji wa lugha kuwa wanaleksikografia hubuni tu maana na matumizi ya
maneno bila kutumia data za wazungumzaji. Aidha, kama mbinu hii ingekuwa
imetumiwa, KKS isingeyasahau maneno muhimu kama vilesarufi. Labda, ni
mapema mno kufikiria jinsi mradi wa namna hii ungeweza kuiboresha KKS.
Majopo ya Kuhariri na Kutathmini Kamusi
Ni muhimu kuwa majopo ya kuhariri na kutathmini kamusi yawepo
mara tu wanaleksikografia wanapomaliza kazi yao. Mara nyingi kazi ya uchapishaji
huanza kabla ya kukamilisha kazi muhimu ya uhariri na tathmini.
Mapendekezo yanayohusu KKS
Kwa ujumla, KKS imetosheleza katika sehemu muhimu ya kuainisha
na kupambanua maana ya vidahizo. Ni sehemu chache ambazo vidahizo havikufasiliwa
inavyofaa. Mapendekezo yafuatayo yanafaa kuzingatiwa.
Kila Neno Lililotumiwa katika Fasili liingizwe kama
Kidahizo
Maneno yaliyotumiwa katika fasili ambayo hayakuingizwa kama
vidahizo (kama vile sarufi, dhifa, ushi, wandani, toazi n.k.) ni lazima
yaingizwe katika kamusi na kufasiliwa.
Vinyambuo Viingizwe kama Vidahizo
Katika baadhi ya kamusi za Kiswahili (kama vile Johnson, 1939),
vinyambuo havikuingizwa katika kamusi kama vidahizo. Ui kutowapa shida watumiaji
wa kamusi, ni muhimu vinyambuo (hasa vikiwa na maana maaium, kama vile,
endea, endesha, endelea n.k.) viorodheshwe pia kama vidahizo.
Uainishaji na Upambanuaji wa Sifa Bainifu
Itakuwa bora kama vitu (hasa viumbe kama wanyama, ndege, nyoka,
wadudu na samaki) vitaelezwa kwa ukamilifu zaidi kwa kuelezea aina yake na sifa
zake maalum kama vile rangi, ukubwa, umbo. mlio, masikani, malisho, ukali, sumu
na kadhalika.
Ufafanuzi wa Maana
Kwa vile baadhi ya vidahizo ni vigumu kuvieleza kwa maelezo au
visawe, litakuwa jambo la busara iwapo mbinu zingine, kama vile nufano ya
matumizi au picha vitatumika pale inapobidi.
Maswala ya Kuzingatia
Hakuna kamusi ambayo fasili za vidahizo ni sawa na kamili katika
hali zote. Hii ni kwa sababu maana na matumizi ya maneno hukubalika kulingana na
wakati, mitindo. aina ya jamii na lahaja. Vidahizo vingi katika kamusi sanifu
hubadilika haraka zaidi kufuatana na matokeo ya usanifishaji na upanuzi wa lugha
ili kukidhi mahitaji mbalimbali. Hivyo, hata baada ya marekebisho, KKS bado
itapitwa na wakati. Aidha KKS haitegemei kukidhi mahitaji ya watumiaji wote au
kukubalika kwa wazungumzaji wote wa Kiswahili. Itakuwa ni mafanikio makubwa kama
itawaridhisha au kuwasaidia wengi, wakiwemo wasomi na watu wa kawaida.
Tanbihi
1. Napenda kumshukuru Dr. J.S. Mdee kwa kunipa maandishi mengi, yakiwemo yake mwenyewe, ambayo yamekuwa nyenzo muhimu katika uandaaji wa makala hii.2. Kwa lugha ya awali (Kiingereza) mada hii iliitwa "The Art of Writing a Definition that Does not Define"3. Mfano huu ni wa kubuni, haukuchukuliwa kutoka KKS.4. Tafsiri yake:
a) uzuri = hali ya kuwa mzuri -zuri= iliyojaa uzuri
b) linkisi = ni mnyama kama pakabobu pakabobu = ni mnyama kama linkisi.
5. Baadhi ya mifano ni ile iliyotumiwa na Mdee (1993:3)6. Baadhi ya mifano ni ile iliyotumiwa na Mdee (1993:6)7. Baadhi ya mifano hii imechukuliwa kutoka Mdee (1993:21)8. Mfano huu umetumiwa na Mdee (1993:20)9. Kwa maana ya 'Synonym' katika kiingereza10. Istilahi ya visawe kamili na visawe karibia imetumiwa kwa maana ya 'absolute synonym' na 'near synonym' au 'quasi-synonym.'11. Hapa nimetafsiri sifa bainifu za Mdee (1993:16), [force] na [power] kama [msukumo] na [nishati]. Tafsiri hizi siyo halisi.12. Alama ya [*] inaonyesha kuwa tungo hiyo haikubaliki katika Kiswahili. Alama ya kuuliza (?) inamaanisha tungo inayokubalika kwa shida au na baadhi tu ya wazungumzaji.13. Kwa mfano mradi wa kitaifa unaoendeshwa katika Idara ya Leksikografia katika Chuo Kikuu cha Leiden Uholanzi.
MAREJEO
Aitchison, J. 1987. Words in the Mind. Basil Blackwell:
Ashton, E.O. 1944. Swahili Grammar. Singapore; Longoman.
Batibo, H.M. 1987, "The Challenge of Linguistics m Language
Develoment. The Case of Kiswahili in Tanzania" Pongweni, A.J. C. and J.
Thondhalane (Wah.) LASU Conference Proceedings. Harare, uk. 39-46.
Batibo, H.M. 1989, "Usahihi na Upotovu katika Tafsiri za
Kiswahili" katika WAFASIRI (Mh), Makala za Kongamano la
Kimataifa kuhusu matatizo ya Tafsiri Barani Afrika, Dar es Salaam uk.
120-130.
Benjoint, H. 1983 "On Field-work in Lexicography" katika R.R.K.
Hartmann, (Mh) Lexicography: Principles and Pracfice. Academic Press,
Inc.
Hornby, A.S. 1974, Oxford Advanced Learner's Dictionary of
Current English. Oxford University Press.
Johnson, F. 1939, A Standard Swahili-EngUsh Dictionary,
Oxford University Press.
Kuhn, S, 1980. "The Art of Writing a Definition That Does Not
Define", katika L: Zgusta (Mh.) Theory and Method of lexicography.
Hornbean Press, uk. 115-121.
Landau, S.I. 1984 Dictionaries, The Art and Craft of
Lexicography.
Mdee, J.S. 1990. Theories and Methods of Lexicography in the
Standard Swahili Dictionary, Ph.D Thesis
Mdee, J.S. 1993," Writing Definitions that Do Not Define: An
Appraisal of Kamusi ya Kiswahili Sanifu (KKS)". Kiswahili Juzuu 58, 1991
uk 68-81
Ogden, C.K. and I.A. Richard, 1923. The Meaning of Meaning,
London.Art Paperbacks Edition.
Quirk, R., 1973 "The Social Impact of Dictionaries in the UK",
katika McDavid, R.I. na A.R. Duckert (Wah.) Lexicography in English.
Juzuu 211. New York: Academic of Science Annuals.
Rey-Debove et al (Wah.) 1972, Le Petit Robert.
Snoxall, R.A. 1958. A Concise English-Swahili Dictionary.
Oxford University Press.
Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili (TUKI). 1981, Kamusi ya
Kiswahili Sanifu. Nairobi, DSM: Oxford University Press.
Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili (TUKI) 1990. Kamusi Sanifu
ya Isimu na Lugha. Chuo Kikuu, Dar es Salaam.
Zgusta, L. 1971. Manual of Lexicography. Praha
academia