Lahaja Na Mitindo Katika Kks
D. P. B. Massarnba
PUBLISHER MASHELE
Utangulizi
Makala haya yamegawany wa katika sehemu mbili. Katika sehemu ya
kwanza tutajaribu kutoa maelezo mafupi sana ya kinadharia kuhusu dhana
zinazovipamba vipengele vya lahaja na mitindo katika lugha kwa ujumla.
Katika kufanya hivyo tutajaribu pia kujadili umuhimu wa vipengele hivi katika
utengenezaji wa kamusi kwa ujumla. Katika sehemu ya pili tutajaribu kujadili na
kutoa tathmini ya namna vipengele vya lahaja na mitindo vinavyojitokeza
katika Kamusi ya Kiswahili Sanifu (tangu sasa K K S).
Lahaja
Wanaisimu wengi huelekea kukubali kwamba ni vigumu (na pengine
haiwezekani) kuweka mipaka bayana baina ya lugha na lahaja; na kwamba kwa
msingi huo si rahisi kutoa fasili ya lahaja inayokubalika kwa wanaisimu
wote (ling. Anttila, 1972:289 - 292; Hudson, 1980: 21 -31; Akmajian, et al.
1984:286 - 298, kwa uchache). Kauli hii inathibitika zaidi tunapojaribu
kuzichunguza fasili kadhaa zilizowahi kutolewa kuhusu dhana ya luhaja
(taz. mifano) ifuatayo hapa chini).
Crystal katika kamusi yake ya A Dictionary of Linguistics and
Phonetics (1985:92) anasema lahaja ni "mtindo bainifu wa lugha kieneo
na kijamii unaobainishwa na seti maalumu ya maneno na miundo ya kisarufi"
[tafsiri ni yangu]. Katika Kamusi Sanifu ya Isimu na Lugha (TUKI,
1990:21) tunaambiwa kuwa lahaja ni "kitarafa cha lugha kinachobainika ama
kijamii au kijiografia na kudhihirishwa na vipengee maalumu vya kisauti na
kimuundo". Pei na Gaynor katika kamuisi yao ya Dictionary of Linguistics
(1980:56) wanasema lahaja ni "namna maalumu ya lugha fulani inayotumiwa
katika mahali au eneo fulani la kijiografia. yenye kuonyesha tofauti za kutosha,
ikilinganishwa na ile [lugha] sanifu au ya kimaandishi. katika matamshi, miundo
ya kisarufi na matumizi ya nahau kwa kiwango cha kuifanya namna hiyo ijibainishe
kama kilu kinachoweza kusimama peke yake; lakini wakati huo huo isiweze knsigana
mno na lahaja nyingine za lugha ihusikayo kwa kiwango cha kuifanya ibainishwe
kama lugha tofauti" [tafsiri ni yangu].
Nayo kamusi ya Longman Dictionary of the English Language
(1984:402) inasema lahaja ni" 1. mtindo bainifu wa lugha
kieneo au kijamii... unaotofautiana na lugha sanifu; 2. yoyote mojawapo kati ya
kundi la lugha zinazohusiana; 3. mtindo wa lugha unaotumiwa na kundi la watu wa
shughuli moja". Tukizichunguza sana fasili hizi tutaona kwamha hakuna hata moja
amhayo ni rupia kwa nyingine. Fasili zote zinasigana kwa kiwango fulani. jambo
ambalo linathibitisha ugumu wa kuwepo kvva fasili moja mwafaka kwa wanaisimu
wote. Lakini pamoja na msigano unaojitokeza katika fasili hizi kuna mambo mawili
muhimu yanayojidhihirisha katika hali ya kufanana. Mambo hayo mawili ni
mazingira ya kijiografia (au kieneo) na mazingira ya kijamii.
Kutokana na sifa llizi mbili za lahaja, wanaisimu. na hasa
wanaisimujamii, wamekuwa wakizigawa lahaja katika makundi makubwa mawili:
lahaja za kijiografia na lahaja za kijamii. Katika mtazamo wa kijiografia lahaja
ni mtindo maalumu wa lugha uliohainifu na unaotumiwa katika eneo fulani la
kijiografia. Lahaja za kijamii ni mitindo maalumu wa lugha uliobainifu na
unaotumiwa na tabaka fulani la kiuchumi-kijamii. k.m. makuli, wasomi. walala
hoi. n.k. Aidha baadhi ya wanaisimu wamejaribu kupendekeza na kudai kuwa liko
pia kundi la tatu la lahaja ambalo hupewajina la lahaja za
kimbari. Mfano mmojawapo wa lahaja za namna hii ni ule mtindo wa Kiingereza
uitwao "Yiddish English" - lahaja ambayo ina chimbuko la kihistoria (kutokana na
Wayahudi wa zamani wa Ulaya Mashariki). Kwa kifupi lahaja za kimbari zina msingi
wa kihistoria.
Mitindo
Ikichukuliwa katika mtazamo mpana zaidi istilahi mitindo
hujumuisha vipengele vingi ikiwa ni pamoja na lahaja sanifu, lahaja
za kimaandishi, lahaja za kijiografia, lahaja za
kihistoria, lahaja za kijamii, n.k. (ling. Crystal, 1985:292). Kwa
madhumuni ya makala haya istilahi mitindo imetumiwa kwa maana ya mitindo
kulingana na matumizi ikitatbutishwa na mitindo kulingana na watumiaji
(ling. Hudson, 1980:48) au vinginevyo. Kwa maneno mengine tunaweza kusema
istilahi mitindo, katika matumizi yetu ya sasa, ina maana ya kile ambacho
baadhi ya wataalamu wamekiita rejesta; yaani matumizi ya lugha kulingana
na muktadha. Binafsi napendelea zaidi kutumia istilahi ya mtindo
muktadha badala ya rejesta. Hivyo kuanzia sasa nitakuwa nikitumia
istilahi mtindo muktadha nitakapokuwa nikirejelea dhana hii.
Tumesema kwamba Mtindo muktudha, ambao ndio tutakaohusika
nao katika majadiliano yetu, huhusu matumizi ya lugha kulingana na muktadha. Kwa
lugha ya kawaida tunaweza kusema mtindo muktadha ni matumizi ya lugha
kulingana na mazingira mbalimbali ya mahusiano ya kijamii, k.m. mazingira ya
kidini, kisayansi, kisiasa, kibaharia, n.k. bila knjali tahaka la mtu; tofauti
na mtindo wa lahaja ya kijamii ambao huegemea zaidi matabaka ya watu
(k.m. wasumi, walala hoi, wafanyiwa kazi, n.k.) mtindo muktadha
haukukitwa kwenye matabaka ya namna hiyo.
Lahaja na Mtindo Muktadha katika Kamusi
Je kuna haja yoyote ya kuingiza maneno ya kilahaja au ya
kimtindo muktadha katika kamusi? lunaweza tu kupata jibu la swali hili kwa
kujiuliza swalijingine: je. kamusi ni nini? Kwa lugha sahili kabisa
tunaweza kusema kamusi ni kitabu cha orodha ya maneno ya lugha (ambayo
aghalabu hupangwa katika mtindo wa kialfabeti) yenye maelekezo kuhusu maana
zake, tahajia zake na matamshi yake; au orodha ya maneno ya lugha rnoja na
visawe vya maneno hayo katika lugha nyiungine. Tukizingatia fasili hiyo ya
kamusi itatudhihirikia wazi kwamba kamusi haibagui lahaja wala mtindo muktadha.
Ndiyo kusema kazi ya kamusi ni kueleza maneno yote (au baadhi tu ya maneno hayo)
ya lugha kama yanavyotumika. Ama kwa hakika maelezo hayo yanashadidiwa na ukweli
uliowahi kujitokeza katika baadhi ya lugha kama vile Kiingereza. Katika lugha ya
Kiingereza tunao ushahidi unaoonyesha kwamba mapema kabisa mnamo mwaka 1671
Skinner katika kamusi yake ya Etymologicon Lingua Anglicana
alifanyajitihada za makusudi kabisa kuingiza maneno ya kilahaja 1.
Halikadhalika Coles naye katika kamusi yake ya An English Dictionary
(1676) alifanya jitihada za makusudi za kuingiza maneno ya kilahaja.
Katika kamusi hiyo Coles alikuwa akieleza au akitoa fasili za "maneno magumu"
yaliyokuwa yakitumiwa katika nyanja mbalimbali za elimu/maarifa katika lahaja
mbalimbali za Kiingereza2
1 Katika baadhi ya maandishi kamusi ya Coles (1676) ndiyo isemekanayo kuwa ya kwanza kuingiza maneno ya kilahaja (ling. Osselton, N.E., 1958; Landau S.I. 1984).2 Hapa yaelekea "maneno magumu" ina maana ya maneno ya nyanja maalumu kulingana na lahaja.
Mifano iliyotolewa hapo juu ni michache tu kati ya mifano mingi
iliyopo inayoonyesha kwamba watungaji wa kamusi za Kiingereza walikuwa
wakizingatia sana vipengele vya kilahaja. Ama kwa hakika kuanzia miaka ya 1650
na kuendelea tunaona kamusi nyingine za Kiingereza zikiibuka na zikiwa na maneno
mengi ya kilahaja. Kwa upande wa mtindo muktadha hali ilikuwa hiyohiyo. Mmoja
kati ya mifano maarufu ni ile faharasa ya S. Pegge: Alphabet of
Kenticism (1735), na ile ya W. Pryce: Mineralogia Cornubiensis (1778)
ambayo ina maneno yaliyokuwa yakitumika katika migodi ya bati ya
Corn.3 Hii inadhihirisha kwamba kamusi hizo za zamani zitikuwa pia
zikizingatia maswala ya mitindo muktadha.
3 Kwa lugha ya kileo tunaweza kusema maneno haya yalikuwa istilahi.
Je, kila Kamusi ilizingatia Vipengele hivi?
Ingawa tumesema kwamba kamusi za zamani za Kiingereza
zilizingatia sana masuala ya lahaja na mitindo muktadha yafaa tutoe hadhari
kwamba si kila kamusi ilifanya hivyo. Ama kwa hakika kuingizwa au kutoingizwa.
kwa makusudi. kwa vipengele vya lahaja na mitindo muktadha kulitegemea madhumuni
ya kamusi iliyohusika. Kwa mfano kamusi nyingi za Kiingereza za kabla ya karne
ya kumi na saba hazikufanya jitihada za makusudi za kuviingiza vipengele vya
lahaja na mitindo muktadha. Kuhusu suala hili Wakelin (1987) anasema kwamba
wanaleksikografia wa zamani wa Kiingereza kama vile Levin (1570). Mulcaster
(1582), Coote (1596). Cawdrey (1604). Bullokar (1616), n.k. hawakutanyajitihada
zozote za makusudi za kuingiza maneno ya kilahaja katika kamusi zao (Burchfield.
1987: 156-177). Hii ni kwa sababu lengo lao kubwa lilikuwa ni kuelezea maana za
"maneno magumu".
Kwa hakika si wanaleksikografia wa karne kabla ya kumi na saba
tu ambao hawakulizingatia suala la lahaja. Hata wanaleksikografia wa baadaye pia
waliliweka kando kidogo suala hili. Mfano mzuri hapa ni wa Johnson katika kamusi
yake ya A Dictionary of the English Language (1755). Katika kamusi hii
Johnson hatilii maanani masuala ya lahaja. Lakini Johnson anafanya hivyo kwa
makusudi kabisa kutokana na haja ya wakati huo ambayo ilikuwa ni kufanya lugha
iwe bora zaidi na iwe na mfumo na rnuundo usioyumba- yumba. kujenga matanishi ya
aina moja yanayokubalika, n.k. Kwa ufupi nia yake ilikuwa imelenga zaidi katika
usanifu wa lugha. Katika mpango wa kamusi ya Johnson neno "lahaja" halitajwi
kabisa. Mpango wake unaeleza dhahiri kwamba kamusi hiyo iliegemea zaidi lugha ya
maandishi ya wale waandishi marufu wa enzi hizo.
Lahaja na Mitindo Muktadha katika kamusi sanifu
Tumekwishasema hapo juu kwamba kuingizwa na kutoingizwa kwa
lahaja na mitindo katika kamusi kunategemea sana nia na madhumuni ya kamusi
inayohusika. Kwa kuwa uingizaji wa vipengele hivi katika kamusi unategemea nia
na madhumuni ya kamusi hiyo haiwezekani kukawa na kamusi za aina moja. Lakini la
msingi zaidi na ambalo linatuhusu hapa ni kwamba kamusi ambayo imelengwa katika
usanifishaji wa lugha hujaribu, kadri iwezekanavyo, kuepuka mambo ambayo
yamemili yaani yameegemea zaidi katika upande wa lahaja au yaliyomili zaidi
katika mitindo muktadha. Hata hivyo hapa inabidi tutoe tahadhari kidogo. Yako
maneno ambayo kwa hakika yanaweza kuwa na msingi wa kilahaja au kimtindo
muktadha lakini yakawa yamekwishapenya katika lugha kwa kiasi cha kuyafanya
yasiweze kuepukwa katika kamusi ambayo madhumuni yake ni kusanifisha lugha. Hata
kamusi ya Johnson tuliyoitaja hapo juu haikufanikiwa kabisa katika kuepuka
maneno yenye asili ya kilahaja au yale ya mtindo muktadha. La muhimu kuzingatia
ni kwamba maneno ya namna hiyo huingizwa katika kamusi sanifu ya lugha kwa
kuzingatia mambo mawili. Kwanza ni kuhakikisha kwamba maneno hayo ya kilahaja
yamek wishajipenyeza katika lugha kwa kiwango cha kueleweka na kukubalika (na
pengine kutumika katika lahaja nyingine). Pili, maneno hayo huingizwa katika
kamusi sanifu inapokuwa yanavveza kueleza vizuri dhana mpya ambazo ama hazina
kabisa maneno ya kuziwakilisha au maneno yanayoziwakilisha katika lahaja sanifu
hayatoshelezi. Vinginevyo ni muhimu kuhakikisha kwamba maneno ya mitindo ambayo
ni ya kilahaja yanaepukwa kadri iwezekanavyo katika zoezi la kutunga kamusi
sanifu.
Lahaja katika KKS
Kwa bahati mbaya mpango uliotumiwa katika KKS hauonyeshi wazi ni
maneno yapi ambayo ni ya kilahaja na yapi ambayo si ya kilahaja. Kutokana na
hali kama hiyo haiwi rahisi kujua moja kwa moja ni neno lipi limetoka katika
lahaja gani. Lakini hii haina maana kwamba hakuna maneno ya Idlahaja
yanayojitokeza katika KKS; kwa hakika yako mengi sana. Swali la kujiuliza ni
kwamba tutayakabili au kuyabainisha vipi maneno kama bayo?
Kwa madhumuni ya makala haya, na kwa kuwa hatutakuwa tunarejea
kwenye labaja fulani maalumu, tutayagawa maneno yenye uelekeo wa namna hiyo
katika makundi mawili- Kundi la kwanza ni yale maneno ambayo ingawa yanapatikana
katika KKS lakini hayamo kabisa, au ni vigumu sana kuyakuta, katika matumizi ya
lugha sanifu inayotumiwa na sehemu kubwa ya wasemaji wa Kiswahili. Mengi kati ya
maneno haya yaelekea kuwa yale yenye asili ya Kiarabu ambayo" tunaweza kusema
yalilazimishwa kuingia katika Kiswahili kisha yakashindwa kupata mashiko mahali
pengi. Kundi la pili ni yale maneno ambayo katika eneo moja la Kiswahili
hutamkwa namna tofauti au hupewa neno tofauti na eneo jingine.
Ili kuweza kupata picha kamili ya suala hili yafaa tutoe mifano
michache. Tuchunguze mifano ifuatayo ambayo inahusu kundi la kwanza, (namba
zilizomo katika mabanoupinde zinaooyesha ukurasa katika KKS ambako neno
linalohusika hupatikana)
adawa =
|
uadui (2)
|
ujihi =
|
tembelea mtu aishiye mbali (4)
|
ajinabia =
|
-a kigeni, -gem (4)
|
alfeni =
|
elfu mbili (5)
|
arshi =
|
malipo kwa kuntoa mtu damu; dia; fidia (9)
|
arshi =
|
kiti cha enzi cha Mwenyezi Mungu, kiti cha enzi cha
mfalme au mtawala (9)
|
ashara =
|
kumi (9)
|
aruba =
|
nne (9)
|
arubii =
|
haraka, upesi (9)
|
atibu =
|
toa makosa; laumu (10)
|
bahaimu =
|
mnyama mwenye. tabia za ovyoovyo; mpuuzi (12)
|
bahaluli =
|
mtu mpumbavu asiyetumia akili yake (12)
|
balighisha =
|
fikisha maneno au salamu (14)
|
balwa =
|
balaa, baa (14)
|
baraste =
|
barabara iliyotengenezwa vizuri (15)
|
bariziana =
|
kabiliana katika vita (16)
|
budhara =
|
uharibifu au upotevu wa mali kwa matumizi ya fujo (22)
|
fulifuli =
|
haraka sana; mbiombio (59)
|
fulusi =
|
fedha, pesa. seti, hela (59)
|
gahamu =
|
kataa kuendelea na jambo (64)
|
gashi =
|
msichana (65)
|
gawadi =
|
mtu anayemtongozea mtu mwingine; kuwadi (65)
|
ghaidhi =
|
hasira, ghadhabu (66)
|
ghashi =
|
udanganyifu, ulaghai (66)
|
hadhirina =
|
watu walichudhuria (72)
|
jalili =
|
enye kuheshimika (88)
|
hadhongo =
|
chai; chirimiri, hongo (95)
|
kadimisha =
|
peleka mbele; tanguliza (95)
|
maujudi =
|
enye kupatikana whati wote (156)
|
msalkheri =
|
tamko linaiotumiwa kumwamkia mtu agh. wakati wa jioni au
usiku (187)
|
nusklua =
|
nakalu (218)
|
sabalkheri =
|
tamko la kumtaka mtu hali wakati wa asubuhi .....
(245)
|
sabatashara =
|
kumi na saba (245)
|
ubahaimu =
|
unyama; hali ya kuwa na tabia zilizo za ovyo (290)
|
wabaadu =
|
na baada ya haya (aghalabu.... katika barua) (315)
|
wahedi =
|
moja (316)
|
wahshi =
|
enye kutokuwa na maana; ovyo (316)
|
zeriba =
|
zizi au boma la ng 'ombe. (322)
|
zuumu =
|
kuwa na nia ya kufanya jambo
|
Tukiyachunguza sana maneno baya tunaona dhahiri kwamba ingawa
yamo katika kamusi ya KKS hayaelekei kuwa sanifu kwa sababu mbili kubwa. Kwanza
si maneno yanayojitokeza sana katika maandishi mengi ya Kiswahili sanifu;
achilia mbali ukweli kwamba wasemaji wengi wa Kiswahili sanifu hawayajui. Pili,
mengi kati ya maneno haya yanaelekea kuwa oa asili ya Kiarabu au lugba nyingine.
Kutokana na hali hiyo ni dhahiri kwamba watumiaji wengi wa maneno haya ni wale
ambao ama wana athari au wana msingi wa iugha ya Kiarabu. Kwa hakika haya ni
maneno ambayo aghalabu yatakuwa yanatumiwa zaidi na watu wa pwani wenye sifa
iliyotajwa hapo juu. Kwa yale maneno ambayo hayana asili ya Kiarabu au lugha
nyingine mbali na Kiswahili huenda yametokana na lahaja.
Tulisema kwamba kundi la pili ni lile lenye maneno ambayo katika
eneo moja la Kiswahili hutamkwa namna tofauri na eneo jingine. Chunguza mifano
ifuatayo:
abunuwasi > banawasi > bunuwasi > kibanawasi [jina la mhusika mjanja katika hadithi za masimulizi] (1)ahadharu > ahdhari > akhdhari [rangi ya kijani] (3)angalau > angalao > ngaa > angaa > angao [neno litumikalo kuelezea lililokuwa afadhali; japokuwa. lau] (8)bajia > badia > bagia [aina ya chakula kama andazi dogo...] (13)biringani > biringanya > biringiani [aina ya mboga jamii ya nyanya mshumaa ...] (20)blangeti > blanketi > bulangeti > burangeti [guo zito la kujifunika ili kujihifadhi na baridi] (20)bradha > bruda [mtawa mwanamume asiyekuwa kasisi au padre] (22)chakleti > chakeleti > chakuleti > chokoleti [aina ya peremende rangi ya kunde ....] (28)charahani > cherehani [mashine ya kushonea] (30)dazani > darzani > dazenu > darzeni [jumla ya vitu kumi na mbili] (42)durusu > darisi > durusi [soma kitabu kwa mazingario; pitia tena yale uliyokwishasomeshwa] (49)ebu > hebu > hembu [tamko linalotumiwa kumwita mtu atazame ..] (50)edita > editori (mtayarishaji wa makala au maandishi....] (50)epa > hepa > kwepa [jiondoa, jitoa, jihadhari usipigwe na kitu] (51)faharasa > faharisi [orodha ya vichwa mambo yaliyomo...]fazaa > fadhaa [hangaiko la moyo; wasiwasi.................] (55)goligoli > golegole > goregore [ndege aliyefanana na ... : kobozi liliokaa...] (69)halwaridi > alwaridi > lawaridi > wardi [ua mojawapo linalonukia vizuri; uturi ulio...] (74)husudu > husudi [onea kijicho; penda mno. sifu] (83)ibra > ibura [kitu au tukio la ajabu....; mafundisho,....] (83)ilimu > elimu [mafunzo, masomo au ujuzi ..; maarifa,...] (85)jamati > jamatikhana > jamatikhane [jumba la mkusanyiko wa wafuasi wa Agha Khan....] (88)karne > karni > karini [muda wa miaka mia moja] (102)legalega > regarega [kosa kuwa imara] (143)lekeza > elekeza [onyesha, basa njia, kwa maelezo au michoro] (143)nwongo > mrongo [mtu mwenye tabia ya kutosema ukweli] (206)ngeu > ng 'eu [rangi nyekundu; damu; jeraha la kichwani..](214)paaza > paza > paraza [saga kitu kama vile mbegu za mahindi, ...] (224)pachipachi > patipati [katikati ya; sehemu iliyoko katikari ya ....] (224)purutangi > patangi > pwitangi [aina ya chombo kama puto kubwa ....] (237)rejea > regea [fika tena ulipokuwa umepaondoka] (241)sombera > sombea [jisogeza kwa kutumia miguu na mikono...] (264)wehua > ehua [fanya mtu kuwa mwehu] (318)ziaka > riaka [kitu maalumu kinachotengenezwa kwa ngozi ...] (322)
Mifano iliyotolewa hapojuu ni sehemu kidogo tu ya maneno mengi
sana yanayojitokeza katika KKS. Uchunguzi wa makini wa mifano hii unadhihirisha
matatizo kadhaa. Baadhi ya matatizo hayo ni kama ifuatavyo:
(a) katika maneno haya kuna namna mbalimbali za matamshi ya neno
hilohilo moja. Je, ni yapi matamshi sahihi: Ni yapi matamshi sahihi:
halwaridi au alwaridi au lawaridi au wardi? Je,
tutamke chakleti au chakeleti au chakuleti au
chokoleti? Bila shaka matamshi haya yote yanakubalika na ndiyo maana
yakaingizwa katika kamusi hii. Kwa msingi huo tunaweza kusema matamshi haya yote
ni sahihi, angalau kwa mtazamo wa kiisimu. Lakini, je, matamshi haya yote ni
sanifu? Hapa ndipo tatizo linapojitokeza. Kwa mujibu wa kanuni za usanifishaji
haiwezekani kuwa na namna mbalimbali za matamshi ya neno hilo hilo moja katika
lahaja hiyo hiyo moja. Katika usanifishaji wa matamshi ya lugha inashauriwa kuwe
na namna moja tu ya utamkaji wa neno. Iwapo itakuwa hapana budi kuwa namna mbili
za utamkaji wa neno hilo hilo moja basi ihakikishwe kuwa namna hizo mbili
zinakaribiana sana. Tukichukulia kuwa msingi huu wa kinadharia ni sahihi
itadhihirika kwamba matamshi ya maneno mengi katika KKS hayakusanifishwa. Iwapo
matamshi ya maneno hayo si sanifu lakini yanakubalika kuwa matamshi sahihi
katika maeneo mbalimbali ya wazungumzaji wa Kiswahili ni dhahiri kwamba matamshi
hayo ni ya kilahaja.
(b) data yetu inadhihirisha kuwa kuna maneno mengi katika KKS
ambayo yana namna mbalimbali za kuandikwa. Hapa pia inabidi tujiulize. Ni yapi
maandishi sahihi: ahadharu au ahdhari au akhdhari?; bajia
au badia au bagia ?; biringani au biringanya au
biringiani ?; dazani au darzani au dazeni au
darzeni?; edita au editori ?; fadhaa au fazaa?. n.k. Pengine hapa
pia kwa kuzingatia namna zote hizi ambazo zimewahi kutumiwa na waandishi
mbalimbali wa Kiswahili tunaweza kusema kuwa kila namna iliyojitokeza hapa ni
sahihi kulingana na lahaja za waandishi mbalimbali. Lakini kama tulivyosema
kuhusu kipengere cha matamshi tunaweza kusema pia kwamba tukitaka kusanifisha
maandishi ya lugha basi itabidi tuwe na namna moja tu ya kuliandika neno. Ni
kweli kwamba mara moja moja katika haadhi ya kamusi za lugha nyingine tunaweza
kukuta maneno ambayo yana namna mbili tafauti za kuandikwa. Lakini ni kweli pia
kwamba kamusi hizo huwa hazidai kwamba namna zote mbili ni sanifu. Tukizingatia
kauli tuliyotoa kuhusu usanifishaji wa maandishi katika kamusi tunaweza kusema
kuwa kuna maneno mengi katika KKS ambayo maandishi yake si sanifu, ni ya
kilahaja.
(c) katika KKS kuna tatizo jingine linalojitokeza na ambalo
linahusiana sana na maandishi. Tatizo hilo ni utohoaji wa maneno.
Tunapoyachunguza maneno kadhaa yaliyotoholewa tunashindwa kupata misingi thahiti
iliyotumiwa katika kutohoa maneno hayo. Mifano michache itayadhihirisha madai
yetu. Kwa nini neno blanket liwe ama blangeti au blanketi
au bulangeti au barangeti?; kwa nini neno dozen liwe ama
dazani au darzani au dazeni au darzeni ?; na kwa
nini neno editor liwe ama edita au editori, n.k.? Laiti
kungekuwa na misingi thabiti na sanifu ya utohoaji tungekuwa na namna moja tu ya
kutohoa neno.
(d) tatizo jingine linalojitokeza ni kule kuweko kwa matumizi
badilifu ya sauti [l] na [r]. Kwa mfano kuna maneno kama: goligoli >
golegole > goregore, bulangeti > burangeti; regarega > legalega.
Ingawa ni kweli kwamba katika lugha nyingi za Kibantu kuna matumizi badilifu ya
sauti [l] na [r] si kweli kwamba kila tutakapokuta mazingira ambamo sauti moja
hutokea basi sauti nyingine pia huweza kutumiwa badala yake. Kwa mfano neno
kilimo haliwezi kuwa *kirimo wala harufu haliwi *halufu.
Kwa hiyo katika lugha sanifu kuna haja ya kuwa makini zaidi katika matumizi
ya sauti hizi mbili. Kwa maoni yetu matumizi ya sauti [l] na [r] yanayojitokeza
katika maneno hayo hapo juu yametokana na kuchukua matamshi ya neno hilo hilo
moja katika lahaja mbalimbali na kuyaingiza katika KKS bila ya kuyasanifisha.
Ama kwa hakika kuna mambo mengi sana tunayoweza kusema kutokana
na data tuliyonayo. Lakini tukiyaingilia hayo tutakuwa tunatoka nje ya mawanda
ambamo tumepewa kuogelea. Tunachoweza kusema hapa ni kwamba kwa kuangalia mifano
michache tuliyoiona ni dhahiri kwamba KKS ina maneno mengi yaliyotokana na
lahaja nyingine za Kiswahili. Ingawa maneno haya ya kilahaja yanaitajirisha
kamusi hii lakini yameingizwa kiholela bila kuzingatia kanuni za usanifishaji
zitakikanazo ili kuifanya kamusi iwe kamusi sanifu.
Mtindo Muktadha katika KKS
Mtindo muktadha ni kipengee kimojawapo kati ya vipengee vilivyo
vigumu kushughulikia katika kamusi sanifu ya lugha ya kawaida. Hii ni kwa sababu
si rahisi kupata vigezo makini sana vya kutumia katika kuamua ni maneno ya
mtindo muktadha upi yanastahili kuingizwa na ya mtindo muktadha upi hayastahili
kuingizwa katika kamusi ya namna hiyo. Je, tuingize maneno ya kidini, kibaharia,
kiteknolojia, kisayansi au yapi? Na kama tutaamua ni maneno ya mtindo muktadha
upi yaingizwe, je tutumie vigezo gani katika kuamua ni kwa kiwango gani maneno
hayo yaingizwe?
Uchunguzi kidogo tu wa maneno ya kimtindo muktadha yaliyoingizwa
katika KKS utadhihirisha kwamba takribani robotatu ya maneno hayo ni maneno ya
kidini, yakifuatiwa kwa kiasi tulani na maneno ya kibaharia. Tukizingatia
mazingira ambamo Kiswahili kilianzia na kuinukia hatutashangaa kuona hali kama
hii ikijitokeza katika kamusi hii. Lakini tukizingatia pia kwamba mawanda ya
Kiswahili yamepanuka sana siku hizi iko haja ya kujiuliza kama kweli hatuna haja
ya kuupa mtazamo tofauti kidogo utaratibu wa kukiingiza kipengele hiki katika
kamusi kama hii. Kwa mfano tunaweza kujiuliza kama kweli maneno ya kidini yana
umuhimu mkubwa zaidi kuliko yale ya kiuchumi, kisayansi au kiteknolojia; au kama
maneno ya kidini yaliyomo katika KKS yamejipenyeza zaidi katika lugha ya kawaida
kuliko maneno ya mitindo miktadha mingine.
Aidha tukiyachunguza, kwa makini maneno ya kipengele hiki
yaliyoingizwa katika KKS tutatambua kuwa hakuna vigezo makini vilivyotumiwa
katika kuchagua ni maneno yapi yaingizwe na maneno yapi yasiingizwe. Je,
yawezekana kwamba maneno yameingizwa kwa kufuata kutokea kwake mara nyingi
katika matumizi ya lugha ya kawaida? Uchunguzi kidogo wa maneno haya
utathibitisha kwamba hii si kweli. Mfano mzuri hapa ni majina kama Muhamad
na Yesu, majina ambayo yanasikika sana katika lugha ya
kila siku katika wasemaji wa Kiswahili walio wengi. La kushangaza ni kwamba
maneno haya hayamo katika KKS! Sababu ni nini? Je, inawezekana kwamba
hayakuingizwa kwa sababu ni majina matakatifu? Lakini hiyo haiwezi kuwa kweli
kwani majina hayo hayawezi kuwa matakatifu zaidi.kuzidi Allah (1)
au Mungu (199), majina ambayo yamo katika KKS. Mfano mwingine
unahusu uingizaji wa majina ya malaika. Je, ni kigezo gani kilichotumika
kuingiza majiaa ya malaika Israfili (au Sirafili),
Ibilisi na Munkari na kuacha kuingiza majina ya
Ziraili (au Israeli) na Jibrili
(au Gabrieli) ? Isitoshe, katika baadhi ya dini za
wasemaji wa Kiswahili kunatambuliwa majina mengine ya malaika kama vile
Rafaeli na Mikaeli; majina haya nayo hayamo
katika KKS. Swali linaendelea: kigezo ni nini?
Tunachojaribu kusema hapa ni kwamba utaratibu uliotumiwa katika
kushughulikia kipengele cha mtindo muktadha katika KKS haukukitwa kwenye vigezo
tbabiti, na hivyo kukifanya kipengele hiki kuwa na sura iliyokaa kombo.
Pamoja na vigezo vingine vinavyoweza kutumiwa katika
kushughulikia kipengele hiki katika kamusi ya namna hii kuna vigezo muhimu
viwili ambavyo vinapaswa kuzingatiwa. Kwanza maneno ya kimtindo muktadba ambayo
yameelemea zaidi katika taaluma maalumu yafaa yasiingizwe katika kamusi ya namna
hii. Kwa msingi huo maneno kama adaa (2), allahuma
(6), altare (6). istiskaa (86),
katekista (103), pengine yasingestahili kuingizwa katika KKS.
Pili, kama tulivyodokeza hapo awali maneno ya kimtindo muktadba yanayostahili
kuingizwa katika kamusi kama KKS shurti kwanza yawe yamekwishajipenyeza katika
lugha ya kawaida kwa kiwango cha kuyafanya yaonekane ya kawaida na yenye
kukubalika katika matumizi yasiyo ya kitaalamu. Kwa mfano, ingawa maneno kama
Ramadhani, maulidi, kusilimu, kuhiji, msikiti, mfungo mosi, Krismasi,
Pasaka, Kwarezima, ubatizo, kanisa, Muhamad, Yesu na Mungu
ni maneno ya mtindo muktadha wa dini yanastahili kuingizwa katika KKS, kwa
sababu takribani watumiaji wote wa Kiswahili wanayajua na wameyazoea.
Hitimisho
Makala haya yamejaribu kushughulikia mambo mawili muhimu kuhusu
vipengele vya lahaja na mitindo katika kamusi. Kwanza tumejaribu kutoa maelezo
mafupi ya kinadharia kuhusu uingizaji wa vipengele hivi katika kamusi na hasa
kamusi sanifu ya lugha yoyote ile. Pili, tumejaribu kuonyesha jinsi gani
vipengele hivi viwili vimeshughulikiwa katika KKS. Katika kuchunguza mamna
vipengele hivi vilivyoshughulikiwa katika KKS tumeona matatizo kadhaa
yakijitokeza. Kutokana na matatizo hayo tukahitimisha kuwa maneno ya kilahaja na
mitindo yaimeingizwa katika KKS bila kuzingatia utaratibu wa usanifishaji wa
lugha. Tumejaribu pia kuonyesha jinsi gani matatizo hayo yaliyojitokeza
yangeweza kuepukwa. Ni matarajio yetu kwamba mchaago wetu utaweza kusaidia
kidogo katika zoezi la kuiduruso kamusi ya KKS.
MAREJEO
Akmajian, A. et. al 1984. Linguistics: An Introduction to
Language and Comunication: Second Edition. Massachusetts: MIT Press.
Anttila, R. 1972. An Inroduction to Historical and
Comparative Linguistics. New York: Macmillan Publishing Co., Inc.
Bwenge, C.M.T. 1992. "Uteuzi wa Msamiati na Uingizaji wa
Vidahizo katika Kamusi Ukarii wa KKS." Makala yasiyochapishwa.
Crystal, D. 1985. A Dictionary of Linguistics and
Phonetics.
Homby. A. (Ed.) 1974. Oxford Advanced Leamers Dictionary of
Current English. Oxford: Oxford University Press.
Hudson, R.A. 1980. Sociolinguistics. Cambridge: Cambridge
University Press.
Pei, Mario A. and Frank Gaynor 1975. Dictionary of
Linguistics. Littlefield, Adams & Co.
TUKI. 1981. Kamusi ya Kiswahili Sanifu. Nairobi, Dar es
Salaam: OUP.
Wakelin. Martyn F. 1987. "The Treatment of Dialect in English
Dictionories" in Burchfield, R. (Ed.) Studies in Lexicogrophy.
Clarendon.