Thursday

Vigogo watakaokutana na Simba makundi Afrika

0 comments


NA AYOUB HINJO MASHELESPORT
BAADA ya safari ndefu kwa timu mbalimbali kutafuta tiketi ya kutinga katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, hatimaye klabu 16 tu zimefanikisha safari hiyo kikamilifu zaidi.
Timu hizo 16 zitatengeneza makundi manne ambayo yatakuwa na klabu nne kila kundi huku mbili za juu zikipata nafasi ya kusonga mbele kuitafuta robo fainali.
Makundi hayo yatapangwa kesho katika makao makuu ya Shirikisho la Soka Afrika, Caf, nchini Misri kwenye Mji wa Cairo huku michezo ya kwanza ikitarajiwa kupigwa Januari 11 mwakani.
Ni mataifa 11 tu ambayo yanawakilisha timu zao kwenye hatua ya makundi, nchi hizo ni Simba (Tanzania), Esperance FC na Club Africain (Tunisia), Al Ahly na Ismaily (Misri), Wydad Casablanca (Morocco), Mamelodi Sundowns na Orlando Pirates (Afrika Kusini), Lobi Stars (Nigeria), ASEC Mimosas (Ivory Coast), JS Saoura na CS Costantine (Algeria), TP Mazembe na AS Vita (DR Congo), Platinum FC (Zimbambwe) na Horoya (Guinea).
Makala haya yanakuletea jinsi timu hizo 16 zilivyofanikiwa kutinga katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu.
SIMBA
Timu pekee kutoka Ukanda wa Afrika Mashariki, Cecafa, imefanikiwa kutinga hatua hiyo baada ya kuiondosha klabu ya Nkana ya Zambia kwa jumla ya mabao 4-3.
Mchezo wa kwanza uliopigwa nchini Zambia katika Uwanja wa Nkana ulimalizika kwa wenyeji kupata ushindi wa mabao 2-1, lakini Simba walipindua matokeo kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kwa ushindi wa mabao 3-1 yaliyofungwa na Jonas Mkude, Meddie Kagere na Clatus Chama.
Kabla ya mabingwa hao wa Ligi Kuu Tanzania Bara kukutana na Nkana, walifanikiwa kuiondosha klabu ya Mbabane Swallows kwa jumla ya mabao 8-1, yaani walipata ushindi wa mabao 4-1 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kisha kushinda wa mabao 4-0 nchini Swaziland.
MAMELODI SUNDOWNS
Mabingwa wa Ligi Kuu ya Afrika Kusini ni moja ya klabu mbili zinazowakilisha taifa hilo ikiwa wamefanikiwa kutinga makundi baada ya kuiondosha klabu ya Al Ahly Benghazi ya Libya.
Mamelodi Sundowns walifanikiwa kushinda mabao 4-0 katika mchezo wa pili uliopigwa nchini Afrika Kusini baada ya ule wa kwanza kumalizika kwa suluhu nchini Libya.
Hata hivyo, Mamelodi Sundowns walianza kampeni yao kwa kuichakaza Vegetarianos ya Equatorial Guinea kwa jumla ya mabao 7-2 katika michezo miwili waliyocheza.
ORLANDO PIRATES
Timu hiyo nyingine kutoka Afrika Kusini walianza kucheza mchezo wa awali dhidi ya Light Stars ya Shelisheli, ambayo waliiondosha kwa jumla ya mabao 8-2, mechi ya kwanza walishinda mabao 3-1 na ile ya marudiano ilimalizika kwa mabao 5-1.
Baada ya ushindi huo mnono dhidi ya hao Washelisheli, Orlando Pirates walifanikiwa kupata jumla ya ushindi wa bao 1-0 dhidi ya African Stars ya Namibia.
Mchezo wa kwanza ulimalizika kwa suluhu nchini Namibia lakini wa marudiano uliopigwa Afrika Kusini ulimalizika kwa wenyeji kupata ushindi wa bao 1-0.
LOBI STARS
Timu pekee kutoka nchini Nigeria iliyofanikiwa kutinga katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu.
Lobi Stars walifanikiwa kuichapa Gor Mahia ya Kenya kwa tofauti ya bao la ugenini, mchezo wa kwanza mabingwa hao wa Kenya walishinda mabao 3-1 na ule wa marudiano timu hiyo ya Nigeria ilishinda mabao 2-0.
kabla ya mchezo huo walitupa karata yao kwa kuiondosha klabu ya UMS de Loum ya Cameroon kwa jumla ya mabao 2-1.
AL AHLY
Hii ni klabu pekee iliyofanikiwa kutwaa mataji ya Ligi ya Mabingwa Afrika mara nyingi zaidi, wamefanya hivyo mara nane.
Msimu uliopita walifungwa mchezo wa fainali na Esperance ya Tunisia kwa jumla ya mabao 4-3, lakini wametinga hatua ya makundi baada ya kuifunga mabao 2-1 klabu ya Jimma Aba Jifar ya Ethiopia.
COSTANSTINE FC
Klabu hii imefanikiwa kutinga katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mara ya kwanza ikitokea nchini Algeria.
Costantine walifanikiwa kuingia makundi kwa kuiondosha klabu ya Vipers ya Uganda kwa jumla ya mabao 3-0 katika michezo yote miwili waliyocheza nyumbani na ugenini.
ASES MIMOSAS
Baada ya muda mrefu kupita hatimaye klabu hiyo kutoka Ivory Coast imefanikiwa kutinga katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
ASES Mimosas walifanikiwa kuifunga klabu ya Stade Malien kwa jumla ya mabao 2-0, ikiwa kabla ya kuitoa timu hiyo walifanikiwa kuiondosha Manga Sports kwa bao 1-0.
AS VITA
Ni sehemu ya klabu mbili za DR Congo zilizofanikiwa kuingia katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu.
AS Vita wameingia kwa kuiondosha klabu ya Bantu FC kwa jumla ya mabao 5-2, yaani walishinda mabao 2-1 mchezo wa kwanza na marudiano walishinda mabao 3-1.
CLUB AFRICAIN
Wababe hao wa Tunisia wametinga makundi baada ya kuiondoa klabu ya Al Hilal ya Sudan kwa jumla ya mabao 3-2, mchezo wa kwanza walishinda mabao 3-1 lakini wa pili walipigwa bao 1-0.
Pia, mchezo wa kwanza uliofanikisha wao kusonga mbele walicheza dhidi ya APR ya Rwanda na kuiondosha kwa jumla ya mabao 4-0 kwenye michezo yao miwili waliyocheza.
HOROYA FC
Klabu pekee kutoka nchini Guinea iliyofanikiwa kutinga hatua ya makundi, walipata jumla ya ushindi wa mabao 6-5 dhidi ya Al Nasr.
Lakini wababe hao wa Guinea walianza safari yao kwa kucheza dhidi ya Barrack Young Controller na kuitoa kwa jumla ya mabao 2-0.
FC PLATINUM
Timu hiyo inatokea nchini Zimbabwe ikiwa ni mara ya kwanza kutinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu.
FC Platinum wametinga kwenye hatua hiyo baada ya kuifunga timu ya Otoho d’Oyo kwa tofauti ya mabao ya ugenini, yaani mchezo wa kwanza walitoka sare ya 1-1 na ule wa marudiano uliisha kwa suluhu.
TP MAZEMBE
Timu hiyo kutoka DR Congo ni moja ya mbili ambazo zimetinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu.
TP Mazembe wametwaa taji hilo mara tano huku mwaka 2015 ikiwa mara ya mwisho kushinda ubingwa wa Afrika.
Wababe hao wa DR Congo wametinga makundi baada ya kuiondosha klabu ya Zesco ya Zambia kwa jumla ya mabao 2-1, mchezo wa kwanza ulimalizika kwa mabingwa hao wa zamani wa Afrika kushinda bao 1-0 na ule wa pili uliisha kwa sare ya bao 1-1.
EL ISMAILY
Wababe hao wa Misri wametinga katika hatua ya 16 bora baada ya kuifunga Coton Sport kwa jumla ya mabao 3-2.
El Ismaily walianza kampeni hiyo kwa kuifunga jumla ya mabao 3-1 timu ya Le Messanger Ngozi ya Burundi, huku klabu hiyo ya Misri ikiwa ya pili ambazo zinatoka nchini humo.
JS SAOURA
Hivi karibuni straika raia wa Tanzania, Thomas Ulimwengu, alijiunga na klabu hiyo kutoka nchini Algeria, mfumania nyavu huyo aliwahi kukipiga TP Mazembe na Al Hilal kwa timu za Afrika.
Saoura wamefanikiwa kuingia makundi ikiwa ni timu ya pili kutoka nchini Algeria baada ya kuifumua mabao 2-1 klabu ya IR Tanger.
Mchezo wa awali walicheza dhidi ya Sporting Gagnoa na kupata ushindi wa mabao 2-0 katika michezo miwili waliyokutana.
WYDAD CASABLANCA
Moja ya timu ambazo zilifanikiwa kutwaa taji hilo la Afrika wakitokea nchini Morocco, wamefanya hivyo mara mbili katika historia ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Wydad Casablanca walifanikiwa kuingia hatua ya makundi kwa kuitoa klabu ya Jaraaf kwa tofauti ya bao la ugenini, timu hiyo ya Morocco ilishinda mabao 2-0 mchezo wa kwanza uliopigwa nchini humo lakini walifungwa mabao 3-1 wakati wa marudiano.
ESPERANCE FC
Mabingwa wa msimu uliopita ambao walifanikiwa kuitungua mabao 4-3 timu ya Al Ahly, hawajacheza mchezo wowote wa kutafuta tiketi ya kushiriki hatua ya makundi.
Timu hiyo kutoka nchini Tunisia wameingia moja kwa moja kama mabingwa watetezi, huku hivi karibuni walitoka kucheza michezo ya Klabu Bingwa Dunia ambalo klabu ya Real Madrid wamefanikiwa kushinda kwa mara ya tatu mfululizo.