Utangulizi
tutafasili dhana ya akronimu na uhulutishaji kwa kutumia wataalamu, katika kiini tutalinganisha na kulinganua mchakato wa akronimu na mchakato wa uhulutishaji na mwisho tutahitimisha
kwa mujibu wa TUKI (2013:7) wanaeleza kuwa akronimu ni neno linaloundwa kutokana na herufi za mwanzo za majina kama vile U.N.O United National Organisation. katika akronimu herufi au silabi za mwanzo za neno au seti ya maneno hutumika kuundia leksimu nyingine mpya. Akronimu aghalabu huandikwa kwa herufi kubwa na hizo herufi husimamia neno fulani mahususi.
Obuchi na Mukhwana (2010:109) wanasema kuwa akronimu ni utaratibu wa kuunda leksimu kwa kufupisha maneno yanayotumiwa pamoja kwa kuchukua herufi au silabi za mwanzo za maneno hayo. Sehemu za kila neno katika kishazi huchukuliwa na kuunganishwa ili kuunda leksimu moja mpya yenye kusimamia dhana moja. Mbinu hii ina sehemu ya matumizi yake hasa katika lugha ya kiingereza. Mifano ya maneno ya kiingereza ambayo yameundwa kutokana na mbinu hii ni pamoja na;
Akronimu Maana Kamili
NATO North Alliance Treaty Organization
NASA National Aeronaustic And Space Administration
UNESCO United Nations Education Scientific and cultural organisation.
UNEP United Nations Environmental Program
KANU Kenya African National Union
KARI Kenya Agricultural Research Institute
KEFRI Kenya Forestry Research Institute
KETRI Kenya Trypasonomiusis Research Institute
Kwa ujumla, akronimu ni neno linaloundwa kutokana na udondoshaji wa herufi za mwanzo za maneno, la msingi kueleweka hapa ni kwamba katika akronimu, baada ya kuunda leksimu, leksimu hiyo hutamkwa kama neno moja baada ya mazoea, na wala sio kama herufi moja moja.
Obuchi na Mkwama (2010:110) Uhulutiahaji huu ni mchakato wa kuunganisha maneno mawili yenye maana tofauti ili kuunda umbo la neno lingune lenye maana tofauti. Yaani mwanzo wa neno fulani (la kwanza) huchukuliwa na kuunganishwa na mwisho au mwanzo wa neno la pili ili kuunda leksimu mpya. Lugha nyingi huwa na maneno yaliyoundwa kwa kutumia mbinu hii ya uhulutishaji. Kwa mfano, lugha ya kiingereza ina mifano ya maneno yafuatayo.
Mfano;
Uhulutishaji Maana
Smoke + fog = smog mchanganyiko wa ukungu na moshi
Gas + alcohol = gasohol mchanganyiko wa gesi na pombe
Hotel + motor = motel msafara wa magari
Mbinu hii ya uundaji wa maneno pia inajitokeza katika lugha ya Kiswahili. Yaani yapo pia
majina ya Kiswahili ambayo yameundwa kwa mbinu hii ya uhulutishaji. Mifano ya majina haya katika lugha ya Kiswahili ni kama ifuatayo;
Mfano;
Chamcha = Chakula cha mchana
Chajio = Chakula cha jioni
Fupaja = Mfupa wa paja
Mbinu hii ya uundaji wa maneno huwa na sifa zinazokaribiana na zile za akronimu. hata hivyo hizi ni mbinu mbili tofauti za uundaji wa maneno, jinsi tumevyofafanua katika maelezo ya kila mfano wa uundaji wa maneno kwa misingi ya mbinu hizi mbili.
Kwa ujumla uhulutishaji ni mfanyiko wa kuendeleza istilahi ambapo mofimu huru mbili au zaidi huchanganywa au huungwa iii kuunda neno jipya ambalo hubeba kwa pamoja nia zote za mofimu huru husika.
Akronimu na uhulutishaji ni mojawapo ya michakato ya uundaji wa istilahi katika lugha. Kwa kutumia mifano dhahiri tunalinganisha na kulinganua michakato hii kama ifuatavyo. Kwa kuanza na ulinganishi;
Matinde (2012:110), akronimu na uhulutishaji ni michakato ambayo hutumika katika kuunda na kuongeza msamiati wa Kiswahili. Lugha hukua na kubadilika kila wakati kulingana na maendeleo ya jamii. Kigezo kimojawapo cha kukua na kubadilika kwa lugha ni kuongezeka kwa msamiati. Ili msamiati uongezeke katika lugha sharti maneno mapya yaundwe. Kwa mfano mchakato wa uhulutishaji;
Nomino na Nomino
Punda + mlia unapata Pundamilia
Bibi + Shamba unapata Bibishamba
Afisa + Elimu unapata Afisaelimu
Mwana + Siasa unapata Mwanasiasa
Bata + maji unapata Batamaji
Kuunganisha kitenzi na Nomino/Jina
Changa + moto = changamoto
Chemsha + bongo = chemshabongo
Piga + mbizi = pigambizi
Zima + moto = zimamoto
Pia kwa kutumia mchakato wa akronimu tunaweza kupata misamiati kama,
Baraza la Kiswahili Tanzania- BAKITA.
Mzaliwa wa mahali Fulani- MZAWA
Chama cha Mapinduzi- CCM.
Nyama ya mfu- NYAMAFU
Hivyo basi ni dhahiri kuwa mchakato wa akronimu na uhulutishaji ni mojawapo ya michakato inayotumika katika uundaji na uongezaji wa misamiati ya lugha ya Kiswahili.
Vilevile mchakato wa akronimu na uhulutishaji hubadilisha muundo au miundo ya maneno. Obuchi na Sangali(2016) wanasema kuwa michakato hii huathiri mofolojia ya maneno kwani huusisha udondoshaji wa baadhi ya mofu katika maneno na kuunganishwa pamoja mfano, Taasisi ya Taaluma za Kiswahili, mofu za mwanzo hudondoshwa na kuwekwa pamoja na kuunda neno TATAKI, vilevile katika katika Uhulutishaji huhusu kuchuliwa kwa baadhi ya sehemu za maneno na kuunganishwa pamoja. Mfano Chakula cha jioni , huhulutishwa na kuwa chajio.
Hivyo basi miundo ya maneno hubadilika pale michakato hii inapofanyika katika uundaji wa maneno.
Michakato yote miwili akronimu na uhulutishaji hujishughulisha na ufupishaji wa maneno katika lugha ya Kiswahili. Mwansoko (1990:56) anaeleza kuwa uhulutishaji ni mchakato wa uundaji wa istilahi mahuluti ambazo huundwa kutokana na sehemu za maneno mawili au zaidi ambapo hakuna uchambuzi angavu katika mofu. Istilahi mahuluti katika jamii huundwa kutokana na mahitaji ya watumiaji wa lugha. Kwa mfano katika lugha ya Kiswahili;
Siunganishi kutokana na isiyo na viunganishi
Chajio kutokana na chakula cha jioni.
Vilevile katika akronimu Obuchi na Sangili (2016) wanasema kuwa mchakato wa akronimu huusisha udondoshaji wa herufi na uunganishaji wa herufi hizo, kwa mfano
UKIMWI Udhaifu wa Kinga Mwilini
TUKI Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili.
WWW Wavu wa Walimwengu.
Hivyo michakato hii yote miwili wa akronimu na uhulutishaji hutumika kufupisha maneno au tungo katika lugha ya Kiswahili na hivyo husaidia na kurahisisha mawasiliano katika jamii husika.
Pia michakato hii ya akronimu na uhulutishaji hutofautiana kama ifuatavyo;
Mchakato wa akronimu huweza kuunda maneno yenye maana zaidi ya moja katika lugha tofauti lakini uhulutishaji huunda maneno yenye maana moja peke yake. Maneno yaliyo undwa kutokana na akronimu ambayo huhusisha udondoshaji wa herufi za mwanzo za maneno na kuwekwa pamoja, maneno hayo huweza kuwa namaana tofauti katika lugha nyingine mfano neno W. W. W, lenye maana ya Wavu Wa Watu , katika kingereza akronimu hii W. W.W linamaana ya World Wide Web. Pia akronimu C.A katika muktadha wa darasani ambapo inamaana ya Class assigment na akronimu hii katika muktadha wa hospitali linamaanisha canser. Lakini katika mchakato wa uhulutishaji maneno yanayoundwa katika mchakato huo hayawezi kuwa na maana tofauti katika lugha nyingine mfano Bata+Mzinga =Bata mzinga. Katika lugha nyingine litakuwa lina kiwakilishi chake chenye maana hiyo hiyo.
Vilevile, katika mchakato wa akronimu leksimu huandikwa kwa herufi kubwa, kwa mfano K.I.A Kilimanjaro International Airpot. BAMITA Barasa la Mitihani Taifa, BASATA Baraza la Sanaa Taifa. Lakini katika mchakato wa uhulutishaji maneno huandikwa kwa herufi ndogo isipokuwa kama zinaanza mwanzo wa tungo na kushikanishwa na maneno au mofu nyingine.
Mchakato wa uhulutishaji ni wa kiholela lakini mchakato wa akronimu hufuata masharti katika uundaji wa istilahi, hivyo istilahi zinazoundwa kwa mchakato wa uhulutishaji ni ngumu kueleweka ukilinganisha na zile zilizo undwa kwa mchakato wa akronimu. Tumbo na Mwansoko(1992:36) wanasema kwamba istilahi mahuluti huungwaungwa kiholela kufuatana na mapenzi ya wale wanaoziunda. Hivyo basi mchakato wa uhulutishaji huweza kufanywa kulingana na matakwa ya waundaji wa istilahi lakini katika mchakato wa akronimu sharti muundaji wa istilahi kutumia mofu za mwanzo katika kuunda maneno mengine.
Kwaujumla, mchakato wa akronimu na uhulutishaji husaidia katika uundaji wa misamiati na istilahi zinazotumika katika lugha. Pia huweza kurahisisha mawasiliano ya pande mbili zenye uhusiano hivyo, hukuza lugha kwa kuongeza istilahi na misamiati na kuifanya lugha kujitosheleza kwa watumiaji wake.
MAREJELEO
Matinde, R. S. (2012). Dafina ya Lugha Isimu na Natharia. Kwa Sekondari, Vyuo Vya Kati na
Vyuo Vikuu. Mwanza: Serengeti Educational Publishers.
Mwansoko, H.J.M. (1990). "The Modernization of Swahili Technical Terminologies: An Investigation of the Linguistics and Literature Terminologies," Tasnifu ya Ph.D. Chuo Kikuu cha York. (Haijachapwa)
Obuchi, S. M. na A. Mukhwana (2010), Muundo wa Kiswahili; Ngazi na Vipengele. Nairobi: Frame publishers.
Obuchi, S. M na Sangili, N. K. N. (2016). Taaluma ya Maana: Semantinki na Pragmatiki. Nairobi: Jomo Kenyatta Foundation.
TUKI (2013). Kamusi ya Kingereza- Kiswahili:3rd Edition: University of Dar es Salaam. Dar es Salaam: University press.
Tumbo-Masabo, Z.N.Z. na H.J.M. Mwansoko (1992). Kiongozi cha Uundaji wa Istilahi za Kiswahili. Dar es Salaain: TUKI.