Andalio la somo ni utaratibu au mpangilio wa hatua za kufundishia unaotayarishwa na mwalimu kwa kipindi husika na kwa darasa fulani.
Siku zote Andalio la Somo ndio dira ya kumuongoza mwalimu wakati wa kufundisha kwake.
UMUHIMU WA ANDALIO LA SOMO
- Huonesha wazi malemgo ambayo mwalimu anatarajia yafikiwe na mwanafunzi wake katika kipindi
- Ni muongozo wa kufuata hatua kwa hatua mwalimu anapofundisha darasani
- Humuonesha mwalimu sehemu za somo za kuuliza maswali, kutumia zana au kuhusisha wanafunzi katika vitendo.
SIFA ZA MALENGO MAHSUSI YA SOMO
A) Kipindi kimoja lazima kisiwe na malengo mengi
- Kila lengo kuu liandikwe kwa mtindo unaoonesha jambo watakaloweza kufanya wanafunzi na linaweza kuthibitishwa au kubainika.
- Malengo yahusiane na kiwango cha uwezo cha wanafunzi
- Muda wa kufikia lengo fulani utajwe waziwazi
- Kiwango cha kufikiwa kwa kila lengo kielezwe
Maneneo yafuatayo yanafaa kutumika katika kuandika malengo mahsusi ya masomo: Hii ina maanisha kuwa malengo mahsusi yawe ni yale ambayo yanapimika hata kwa kutamka tu, mfano;
- Kueleza, kusema, kusoma, kuandika
- Kujumlisha, kutoa, kuzidisha, kugawa
- Kufanya mafumbo, kupima
- Kujadili, kufupisha
- Kuchora, kutafsiri
- Kulinganisha na kutofautisha
Mwalimu anapoandika malengo ya somo asitumie maneno yasiyoweza kupimika mfano, kuelewa, kufahamu, kujua, kufurahia, kutambua, kupata vionjo nk kwani haya yanakua ni malengo ya Jumla na hayapimiki hata kwa kutamka.
VIPENGELE MUHIMU VYA ANDALIO LA SOMO
Katika kuandaa andalio la somo yampasa mwalimu azingatie vipengele muhimu vifuatavyo;
- Jina la somo
- Tarehe, darasa, muda wa kipindi, idadi ya wanafunzi
- Mada kuu na mada ndogo
- Malengo ya somo
- Vifaa vya kufundishia na kujifunzia
- Vitabu vya rejea
- Uwasilishaji wa somo hatua kwa hatua
- Kazi za mwalimu na za wanafunzi
- Maoni kuhusu mafanikio/matatizo ya ufundishaji wa kipindi
- Tathmini
- Mazoezi ya wanafunzi
Ufafanuzi wa vipengele
1) Vipengele 1,2 -3;
Vinamsaidia mwalimu kuwa na kumbukumbu ya vipindi vilivyofundishwa kwa mwaka
2) Malengo ya somo;
Yanaonesha matarajio aliyo nayo mwalimu kwa wanafunzi wake baada ya kipindi au somo. Mfano mwanafunzi aweze kutaja, kuandika au kusoma kitu Fulani kwa kiwango Fulani cha ufanisi
3) Vifaa vya kufundishia;
Hizi ni zana ambazo mwalimu anatarajia kuzitumia katika kufundisha somo husika
4) Vitabu vya rejea;
Hivi ni vitabu ambavyo mwalimu huvisoma ili kupata marifa, stadi nk. Vitabu vya rejea hujumuisha pia majarida na maandiko mengine ambayo hutumika kuandaa somo
5) Uwasilishaji wa somo hatua kwa hatua,
Hapa mwalimu anapaswa kuandika vitu viwili muhimu: kazi na hatua zote atakazofuata mwalimu wakati wa somo, pia atayarishe mawazo/maudhui makuu anayotaka yazingatiwe na wanafunzi
6) Kazi za wanafunzi,
Kazi za wanafunzi zinaweza kuwa kuchora, kueleza, kuandika, kujibu maswali ya mwalimu, kufanya maigizo, kujadiliana nk
7) Mazoezi ya wanafunzi,
Haya ni maswali ambayo mwalimuhuwapa wanafunzi kupima kama malengo ya somo yamefikiwa wakati wa kipindi
8) Tathmini,
Mwalimu aandike maelezo kama somo limefaanikiwa au la, na kwa kiwango gani.
9) Maoni, mwalimu aeleze hatua za kuchukua kutokana na tathmini ya somo lake. Kwa mfano kama somo halikufanikiwa atalirudia, atarudia baadhi ya vipengele.