Kitenzi
Katika kujadili dhana ya muundo wa kitenzi cha Kiswahili kwa kuzingatia viambishi awali, kati na fuatizi ni vema kuona neno lenyewe kitenzi lina maana gani, kwa kuwajelea wataalamu mbalimbali. Kihore (2000) anasema kuwa kitenzi ni “aina ya neno ambalo hutoa taarifa juu ya tendo linalofanyika au linalotendwa na kiumbe au kitu”. TUKI (1990) inasema kuwa kitenzi ni “aina ya neno ambalo huarifu aina ya tendo linalofanyika”.
Riro (2012) anasema kitenzi ni “neno linalotaoa taarifa kuhusu tendo linalofanyika , lililofanyika na litakalofanyika”.TUKI (2003) husema kuwa kitenzi ni “neno ambalo huarifu kuhusu tendo linalofanyika”.
Richard na wanzake (1985) katika Mgullu (1999) wanasema kuwa “kitenzi ni neno ambalo hutokea kama sehemu muhimu ya kiarifu na ambalo huambishwa mofu za njeo hali, nafsi, idadi na dhamira, Aidha vitenzi huelekeza juu ya tendo au hali”. Kwa ujumla twaweza kukubaliana na wataalamu hao hasa Richard na kusema kuwa kitenzi ni aina ya neno ambalo hueleza tendo lililofanyika pamoja na dhana mbalilmbali za kisarufi kama njeo, hali, nafsi na idadi kwa mofu mbalimbali zinazoambikwa.
Kiambishi
Dhana ambayo ni muhimu tena kuifasili kabla ya kuanza kujadili mada hii, ni kiambishi. Kwa mujibu wa wataalamu kadhaa wanafasili dhana kiambishi kama ifuatavyo; TUKI (1990) inasema kiambishi ni “mofimu ambayo hupachikwa kabla, kati, au baada ya mzizi wa neno”, wakati
Massamba wenzake (2003) wanasema kuwa viambishi ni “mofimu zinavyoambatanishwa kwenye mzizi wa neno ili kuwakilisha hali au dhana mabalimbali zinazofungamana na neno pamoja na mofimu”. Riro (2012) anasema kuwa “neno kiambishi hutokana na neno ambika. Kuambika ni kuweka kitu mahali kwa kukiegemeza na kingine. …Ni vineno vilivyoshikwa na mzizi wa kitenzi kabla, hata baada ya kienzi hicho”.
Mgullu (1990) anasema kiambishi ni “mofu ambazo huongezwa kwenye mzizi ya maneno na viambishi hivyo huwakilisha maana fulani. Katika lugha nyingi viambishi huwa na maana za kisarufi zaidi na havina maana ya kileksika”. Mgullu anagusia maana za kisarufi na kileksika ambazo viambishi mbalimbali huwakilisha pale zinapotokea katika mizizi ya maneno. Hivyo tunaona tayari kuwa viambishi huwa na majukumu makubwa kisarufi na kukosa au kuwa majukumu kidogo ya kileksika(Khamis, 2008)
TUKI (2013 uk.207) Hudai kiambishi ni “kipande cha neno, huwa ni silabi kinachoweza kuambatanishwa kwenye mzizi wa neno na kuunda neno jipya” Anaendelea kusema kuwa “ni mofimu inayoambatanishwa kwenye mzizi wa neno ili kuwakilisha hali au dhana”.
Muundo wa kitenzi cha Kiswahili kwa uzingativu wa viambishi
Kwa mujibu wa Massamba na wenzake (2003) wanaonesha viambishi vya Kiswahili vya aina tatu kwa kuzingatia mahali pakutokea . Na kwamba vitenzi katika Kiswahili ndio aina ya neno ambalo huathiriwa kiasi kikubwa sana na viambishi au uambishaji. Pia hoja hiyo hiyo inaungwa mkono na Riro (2012) kwa kusema kuwa “vitenzi ndio vina uwezo mkubwa wa kubeba viambishi kuliko aina zote zingine za maneno”. Na kwamba vitenzi vya Kiswahili huwa na sehemu kuu tatu pale vinapotokea na viambishi, yaani ; sehemu ya viambishi awali, sehemu ya mzizi wa kitenzi na sehemu ya viambishi tamati( Mgullu, 1990). Hivyo kwa uzingativu wa hoja hii tunaweza kusema kuwa kuna miundo mitatu mikuu ya vitenzi vya Kiswahili kwa uzingativu wa uainishaji wa viambishi kimaumbo na kiuamilifu ambayo ni
1. Muundo wa viambishi awali na vitenzi ( mziizi wa kitenzi) .
2. Muundo wa viambishi tamati na vitenzi.
3. Muundo wa viambishi awali, mizizi(vitenzi) na viambishi tamati.
Miundo hiyo ya vitenzi vya Kiswahili kwa uzingativu wa aina za viambishi huwa na majukumu yake ya kisarufi na ya kileksika katika vitenzi vya Kiswahili, ambayo hudokezwa na viambishi.Hivyo tunaweza kuonesha majukumu ambayo hufanywa na viambishi awali, viambishi fuatizi, na viambishi awali na fuatizi kwa pamoja katika mizizi ya vitenzi vya kiswahili kama ifuatavyo;
Muundo wa viambishi awali na kitenzi na majukumu yake kisarufi .
Viambishi awali tofauti tofauti hudokeza au hufanya majukumu mbalimbali katika vitenzi vya Kiswahili na usarifu wa majukumu huweza kuainishwa kwa uamilifu wa mtumiaji lugha. Yafuatayo ni baadhi ya majukumu ya kisarufi ya viambishi awali katika vitenzi;
- Kudokeza nafsi ya mtenda au mtendwa jambo kama nafsi ya kwanza, ya pili na ya tatu.
Mfano a- na wa- katika maneno
{A – na – temb – e – a} – a - kiambishi awali nafsi ya tatu umoja.
{wa – na – temb – e – a} –wa – kiambishi awali nafsi ya tatu wingi.
- Kudokeza njeo au wakati ambapo tendo hufanyika. Mfano huweza kudokeza njeo iliyopo , iliyopita na ijayo.viambishi vya njeo katika lugha ya Kiswahili ni {-li-} , {-na-} na {-ta-}. mfanokatika maneno
{ni –na- lim – a}- na – kiambishi awali cha njeo iliyopo,
{ni – li – lim a} – li – kiambishi awali cha njeo iliyopita,
na {ni – ta – lim a}- kiambishi awali cha njeo ijayo.
- Kurejesha tendo kwa mtenda au mtendwa . Yaani tendo huweza kuhusika sana na mtendaji wake au mtendwaji wake. Mfano
(1) mtu aliyepigwa sana na wananchi amefariki jana au
( 2) mwalimu aliyetufundisha social ethics amefika.
{-ye-} kiambishi awali kinachodokeza urejeshi wa mtendwa.
- Kudokeza unominishaji wa kitenzi kwa kuongeza mofu ku- ya kunominisha kitenzi cha Kiswahili. Mfano omba( kitenzi) – kuomba(kitenzi jina).
- Kudokeza kudokeza hali mbalimbali za vitenzi yaweza kuwa kukamillika, kuendelea, kutokea mara kwa kmara au linatarajiwa kufanyika.
Mfano ; - nimesoma { me} – hali timilifu .
-anacheza {me} – hali ya kuendelea.
-akisoma { ki} – hali ya amasharti.
- huimba {hu} - hali ya mazoea.
- Kudokeza kujitendea au kujirejea kwa mtenda wa tendo. Mfano
-waliojisomea watafaulu. Mofu {-ji}
- aliyejichafua akanawe. Mofu {-ji}
- Kudokeza ukanushi ambapo kiambishi cha ukanushi huwekwa kwenye kitenzi kuonesha hali ya kutotenda jambo. Mofu zinazotumika ni {si-}, {ha-}, {hu-} katika mazingira ya nafsi mbalimbali. Mfano – naandika – siandiki, ninasoma – sisomi , tunasoma – hatusomi.
- Kudokeza ya mbwa ya tendo fulani . Mfano Mwalimu aliwapiga watoto, Baba aliukata mti, Juma alilipeleka gari nyumbani.
Muundo wa kiambishi tamati na kitenzi na majukumu yake kisarufi.
• Kudokeza kauli mbalimbali za vitenzi vya Kiswahili. Viambishi hufanya majukumu ya kuonesha kauli kama ya kutenda, kutendwa, kutendea, au ktindesha. Mfano
-Alipigwa {-w} – kauli ya kutendwa.
-Somea {-e} – kauli ya kutendea.
-Andikisha {- ish} – kauli ya kutendesha .
• Kudokeza rai, amrisho, kimizo kwa kutumia mofu {-e} kwenye umoja na {-ni} kwenye wingi . Mfano – kacheze, - kimbieni, -kasome, -uje, na –nipishe.
• Kudokeza mahali ambamo kitendo hutukia kwa kuonesha ukubwa na umbali wa mahali penyewe. Mfano – aingiamo {-mo), wachezeako {-ko}, afanyiapo {-po}.
• Kudokeza wakati kama ilivyo kwa kiambishi awali kiambishi tamati pia hufanya kazi hiyo. Matumizi ya mofu {-po} hufanya kazi hiyo. Mfano
– tuanzapo kusoma nitakufundisha. {-po}.
-Angurumapo samba usichezi naye.
- mwimbaji aimbapo utasikia kelele.
• Kudokeza swali kwa kutumia viambishi vya maswali kama vile {-ni}, {-pi} na {-ni}. Kwa mfano;
- wasemaje?
– yakuwashiani?
–wendapi?
• Kudokeza urejeshi wa mtenda, mtendwakulingana na ngeli za nomino katika baadhi ya vitenzi. Kwa mfano;
- akutazamaye aachi kukugeukia,
-kimsumbuacho mwanadamu ni fumbo,
-amwambiaye ukweli atamchukia.
Majukumu ya kileksika ya viambishi awali na tamati .
Mara nyingi katika dhana hii ya kitenzi kuwa na viambishi awali na fuatizi kwa pamoja, kitenzi huonekana kubadilika kategoria na kuwa kategoria nyingine ambayo mara nyingi ni nomino.Na uambikaji wa namna hii huonekana katika mifanyiko ya kifonolojia (mofofonolojia). Mifanyiko ya kimofofonolojia huonesha hasa katika kanuni ya kudhoofika kwa sauti ambapo tunaona viambishi vyote vya awali na vile vya fuatizi katika mchakato. Kwa mfano katika maneno ; penda, jenga, pika, na iba (Riro, 2013 uk.90) , huweza kuoneshwa jinsi vinavyoathiriwa na viambishi awali na fuatizi katika uundaji wa nomino.Kanuni ifuatayo hutawala katika mfanyiko ufuatao;
• /d/ /z/ - [i]
Penda – {mu + pend + i}
hudondoshwa Hudhoofika kuwa /z/ mpenzi
• /g/ /z/ - [i]
Loga {mu + log + i}
Hudondoshwa hudhoofishwa kuwa /z/ mlozi.
• /b/ /z/ - [i]
Iba - {mu + ib + i} /u/ /w/ -[v]-isiyo /a/
- {mw + ib + i}
Hudhoofika na kuwa /z/ mwizi
Pia athari hiyohiyo inaweza kuoneshwa kwa kutumia unyambuaji ambapo viambishi mbalimbali hupachikwa kwenye mzizi wa kitenzi ili kuunda maneno mapya. Viambishi awali na viambishi tamati huathiri mzizi wa vitenzi kuunda aina tofauti ya kategoria. Katika kuonesha mchakato huu wa kubadili kategoria, majukumu ya kileksika ya viambishi huonekana, ambayo ni kuonesha aina ya kategoria iliyoundwa tofauti na kategoria athiriwa(kama matokeo ya unyambuaji).Kwa mfano
• {u + umb + a + ji} = uumbaji kutoka kwenye kitenzi umba(nomino).
• {u + chimb + a + ji} = uchimbaji kutoka kwenye kitenzi chimba(nimino).
• {u + chor + a + ji} = uchoraji kutoka kwenye kitenzi chora(nomino).
• {u + binafs + ish + a + ji} = ubinafsishaji kutokana na kitenzi binafsisha(nomino).
Kwa kuhitimisha mjadala wetu kuhusu muundo wa vitenzi vya Kiswahili kwa kuzingatia viambishi awali, tamati na fuatizi, ni vema turejelee msimamo wetu katika mjadala huu. Miundo ya vitenzi ilijadiliwa ni mitatu yaani
- Vitenzi na viambishi awali - vitenzi na viambishi tamati na
- Vitenzi na viambishi awali na viambishi tamati kwa pamoja.
Uainishaji huu umezingatia viambishi vinavyopatikana katika lugha ya Kiswahili kwa hiyo kiambishi kati havikutiliwa mkazo kwa kuwa hakuna viambishi hivi katika lugha hii.Jambo linguine ni majukumu ya kisarufi na yale ya kileksika ambayo huonekana kama athari ya kuwepo kwa viambishi katika kitenzi.Miundo hii ya vitenzi kwa uzingativu wa viambishi haina majina maalumu na wala hakuna mtaalamu ambaye ameijadili kwa kwa ingawa ni wazi dhahiri kama unaijadili kama vile tulivyofanya. Ni nafasi ya pekee kwa wanafunzi wanaosoma Kiswahili kuandika kwa kutumia nafasi kama mjadala huu uliozuliwa na mwalimu (Mrs) Bi, Machinde Zena kuandika kama kukiendeleza Kiswahili na kupanua taaluma, ni wito wa Dr. A.D.Negussie (usemi binafsi april 18/2015) kama alivyotanguliza mhadhara ulioongozwa na mwandishi Nyangwine N. kuhusu nafasi ya Kiswahili katika muungano wa Tanzania hapa katika chuo kikuu cha Mt. Agustino Mwanza.
MAREJELEO
Khamis, A.M.(2008).Maendeleo ya Uhusika.Dar es salaam: Chuo kikuu cha Dar es salaam.
Massamba na wenzake (2009).Sarufi Maumbo ya Kiswahili Sanifu(SAMAKISA).Sekondari
na Vyuo. Dar Es salam: TUKI.
Mgullu, R.S.(1999). Mtalaa wa Isimu: fonetiki, fonolojia na mofolojia ya Kiswahili.Dar es
salaam : TUKI.
Riro, M.S. (2013). Dafina ya Lugha Isimu na Nadharia. Mwanza:Serengeti bookshop.
Distributors Ltd.
LongHorn Publishers.
TUKI (1990). Kamusi Sanifu ya Isimu na Lugha. Dar es salaam:Educational Publisher and
TUKI (2013). Kamusi ya Kiswahili Sanifu. Nairobi: East Afrika publishers.
+2555766605392