Monday

RIPOTI YA UTAFITI KUHUSU MBINU ZILIZOTUMIKA KATIKA UUNDAJI WA ISTILAHI ZA KISWAHILI ZILIZOINGIZWA KATIKA MIFUMO YA MAWASILIANO YA KOMPYUTA: MIFANO KUTOKA MFUMO WA KOMPYUTA WA LINUX.

0 comments

CHUO KIKUU CHA DAR ES SALAAM
 TAASISI YA TAALUMA ZA KISWAHILI
  IDARA YA LUGHA YA KISWAHILI  NA ISIMU


KI113:MBINU ZA UTAFITI  NA UANDISHI WA TASNIFU  KATIKA LUGHA NA FASIHI
RIPOTI YA UTAKUHUSU  MBINU ZILIZOTUMIKA KATIKA UUNDAJI WA ISTILAHI ZA KISWAHILI ZILIZOINGIZWA KATIKA MIFUMO YA MAWASILIANO YA KOMPYUTA: MIFANO KUTOKA MFUMO WA KOMPYUTA WA LINUX.
 KOMPYUTA WA LINUX.








JINA: MALAGIRA ARITAMBA.
NAMBA YA USAJILI: 2010-04-02466
MWALIMU WA SOMO: E. MAHENGE NA DKT. G. MRIKARIA


SHUKRANI
Utafiti huu umefanikiwa kwa jitihada kubwa za waalimu wangu wa somo.Napenda nimshukuru kwa dhati mwalimu Elizabeth Mahenge kwa kutumia muda wake mwingi  katika kunielekeza na kurekebisha mada yangu ya utafiti.Namshukuru pia Mwalimu G.Mrikaria kwa kututia moyo katika kufanikisha utafiti huu.
Vilevile nawashukuru wanafunzi wenzangu kwa kunishauri na kunitia moyo katika kuendelea na utafiti huu.Wanafunzi wafuatao wamekuwa mchango mkubwa katika kufanikisha utafiti huu;Ally Laila,Thomas Edson,Ndumbaro Eric, Ndege Busalu pamoja na Ntenga Elias.Nawashukuru pia Boniface Jacob na James Balele kwa utayari wao wa kunisaidia kuchapa utafiti huu.Na mwisho nawashukuru wote walionisaidia kwa namna moja ama nyingine,Mungu awabariki sana!

.  












                                                                          
                                               YALIYOMO
Sura ya kwanza:Utangulizi na Nadharia ya uundaji istilahi…………………. 1
1.0 Utangulizi……………………………………………………………………………………1
1.1  Tatizo la utafiti……………………………………………………………………….3
1.2  Malengo ya utafiti…………………………………………………………………....3
1.3  Umuhimu wa utafiti…………………………………………………………………4
1.4  Dhana ya istilahi,linux na nadharia ya uundaji istilahi……………………………4
Sura ya pili:Mapitio ya marejeo na mbinu za ukusanyaji data………………..8
2.1 Mapitio ya marejeo………………………………………………………………………….8
      2.2 Mbinuza ukusanyaji data ……………………………………………………………..10
Sura ya tatu:Uchambuzi wa data………………………………………………11
3.1 Utangulizi………………………………………………………………………………….11
       3.2 Mbinu zilizotumika katika uundaji wa istilahi za Kiswahili katika Linux………….11
       3.3 Ubora na udhaifu wa mbinu zilizotumika kuunda istilahi za Kiswahili katka Linux…16
             3.3.1 Ubora wa mbinu zilizotumika ……………………………………………………16
             3.3.2 Udhaifu wa mbinu zilizotumika…………………………………………………18
             3.3.3 Mbinu bora zaidi katika uundaji wa istilahi za Kiswahili…………………………19
Sura ya nne:Muhtasari na Hitimisho…………………………………………..20
4.1 Matokeo ya utafiti kwa muhtasari…………………………………………………………20
4.2 Hitimisho…………………………………………………………………………………….22
Marejeo
Viambatisho  
                                      
                                       SURA YA KWANZA
1.0   Utangulizi
Lugha ni kielelezo cha maisha ya jamii kwani huenda sambamba na mabadiliko au maendeleo katika jamii. Kila sekta ya jamii iwe  siasa,elimu,sayansi,teknolojia,utamaduni,dini,kilimo,uhandisi,sanaa,uchumi ama biashara hubadilika kila mara .Uvumbuzi mpya kila mara huzua dhana mpya ambazo zinahitaji maneno mapya kuzielezea(King’ei 2010)
King’ei(ameshatajwa) anaendelea kusema kuwa  ukuzaji wa msamiati na istilahi ni jambo la kawaida katika kurekebisha lugha ili iweze kuambatana na wakati au iwe ya kisasa. King’ei anaendelea kusema kuwa ukuzaji upya wa istilahi hufanyika kwa sababu mbalimbali.Kwanza kabisa lugha sharti iweze kuelezea dhana mpya zinazoingia katika jamii kutokana na mabadiliko katika jamii.Sababu ya pili ni kwamba maana ya maneno yanayotumika katika lugha hupanuliwa ili kuchukua maana mpya au pana kuliko ile ya awali.Sababu ya tatu ya kuwepo haja ya kustawisha istilahi mpya katika lugha ni ile haja ya kufasiri maandishi kutoka lugha moja hadi nyingine.
Msanjila na wenzake (2011) wanasema hadi wakati huu lugha ya Kiswahili imekwisha ingizwa katika mifumo miwili ya kompyuta ijulikanayo kamalinuksi na mikrosofti.Wanaendelea kusema,kuingizwa kwa Kiswahili katika mifumo hii maana yake ni kwamba mtumiaji anaweza kuvinjari mifumo hiyo ya kompyuta kwa Kiswahili akiamua kufanya hivyo.
Pia King’ei(ameshatajwa) anaelezea kuwa,kampuni ya talakirishi iitwayomicrosoft ilitekeleza hatua ya kihistoria  mwaka 2005 kwa kuanzisha kamusi maalumu inayo wawezesha watumiaji wa talakirishi kutumia lugha ya Kiswahili katika mawasiliano yao yote kwa kompyuta,anaendelea kusema,programu hii mpya inamwezesha mtumiaji kompyuta asiyefahamu lugha nyingine kama vile kiingereza kutumia kompyuta na kuwasiliana bila shida yoyote.
Katika mchakato wa kuziweka programu hizi katika Kiswahili, ilihitajika kuunda istilahi za

Kiswahili ili kukamilisha shughuli hii mbinu mbalimbali za uundaji istilahi zilitumika.
Katika uundaji wa istilahi za Kiswahili kuna mbinu mbalimbali zinazotumika. Kwa mujibu wa
Kiango(2004) amebainisha mbinu za kuunda istilahi za Kiswahili kuwa ni pamoja na:Kubuni,anasema,njia hii inaweza kutumika katika kukabili mazigira ya aina mbili; kubuni msamiati ambao utataja mambo yaliyomo katika jamii ambayo hayajapata msamiati wa Kiswahili. Pili ni kubuni msamiati ambao utataja mambo kutoka nje ya jamii yenye msamiati wa kigeni, mbinu nyigine ni kukopa; kukopa kwa kutohoa msamiati wa kigeni,kukopa kwa kutafsiri msamiati wa kigeni na kukopa kwa kuingiza maneno ya kibantu na lahaja na njia nyingine ni ya kufupisha maneno.
Kahigi (2004) anasema mbinu  za kuunda istilahi ni pamoja na: unyambulishaji; unyambulishaji ni kupachika viambishi undaji ili kuunda neno lenye dhana na muafaka. Mfano, modification→ukumushaji. Mbinu nyigine ni ukopaji; ukopaji ni kuchukua neno kutoka lugha chanzi na kulitohoa ili likubaliane na taratibu za kisarufi za lugha pokezi. Mbinu zingine zilizoainishwa na Kahigi ni: tafsiri mkopo;ni aina ya tafsiri kutoka lugha chanzi ambayo ni ya moja kwa moja, mbinu nyigine ni uundaji wa maneno mapya, mbinu hii huhusisha uundaji wa maneno mapya ambayo yalikuwa hayapo kwenye lugha lengwa, mfano byte  >  baiti, uambatani; ni uwekaji wa maneno mawili au zaidi yanayowakilisha dhana moja, mfano magneticfield >ugasumaku, ufupishaji; hii ni mbinu ya kufinyanza maneno na kupata neno moja, mfano, UWT(Umoja wa Wanawake Tanzania).
Mtafiti mwingine ambaye ameelezea mbinu za uundaji istilahi ni Sewangi(2004) yeye anasema mbinu za uundaji istilahi ni pamoja na: kutohoa,kwa mfano; computer > kompyuta, program>programu, mbinu nyingine ni kubuni, kwa mujibu wa Sewangi anasema, mbinu ya kubuni inaweza kufanywa kidhahania au kwa kutumia vigezo mahususi. Kubuni istilahi   kidhahania  hutetewa kwa hoja kuwa hakuna uhusiano wa moja kwa moja baina ya istilahi na dhana inayo bebwa, hivyo neno lolote laweza kuundwa na kupewa hadhi ya istilahi ya dhana fulani. Njia mojawapo ya kuunda istilahi kidhahania ni kutumia fomula za kompyuta ambapo maneno mengi yanaweza kuzalishwa na kupachikwa dhana mahususi katika uwanja fulani wa maarifa. Njia ya kuunda istilahi kivigezo huweza kufanywa kwa kutumia vigezo mahususi kama

vile kazi, umbo au mwonekano wa kitu. Kwa mfano kwa kutumia kigezo cha kikazi kisawe cha calculator kimebuniwa kuwa ni kikokotozi (kitu kinachofanya kazi ya kukokotoa), kisawe cha data saver kimekuwa kihifadhi data (kitu kinachohifadhi data). Mbinu nyingine iliyoainishwa na Sewangi ni mbinu ya kupanua maana ya maneno yaliyopo; njia hii huchukua neno lenye maana ya jumla na kuliongezea maana ya kihistilahi katika mazingira ya kitaalamu, kwa mfano neno kifaru ambalo maana yake ya jumla ni mnyama lakini katika mazingira ya utaalamu wa kijeshi ni kisawe cha tank.
Kwa kuzingatia maelezo ya wataalamu hawa kuna mbinu tofautitofauti za kuunda istilahi. Kwa hiyo kutokana na kwaba kuna mbinu tofautitofauti za kuunda istilahi,utafiti huu hulenga kubainisha mbinu zilizotumika katika kuunda istilahi za Kiswahili zilizoingizwa katika mfumo wa kompyuta wa linux.

1.1 Tatizo la utafiti
Kulingana na tafiti za wataalamu hawa,wameelezea kuingizwa kwa Kiswahili katika mifumo ya kompyuta ya linux na Microsoft,kwa mfano, Msanjila na wenzake (2011) na King’ei (2010) wameelezea kuhusu hili. Vilevile wataalamu wengine kama vile Kiango (2004), Sewangi (2004) na Kahig i(2004) wao wameainisha mbinu mbalimbali za kuunda istilahi za Kiswahili. Kwa ujumla wataalamu hawa hawajaonyesha mbinu zilizotumika katika uundaji wa istilahi za Kiswahili zilizoingizwa katika mifumo ya mawasiliano ya kompyuta hususani mfumo wa kompyuta walinux, kwa hiyo utafiti huu hulenga kuziba pengo hili kwa kuchunguza mbinu zilizotumika katika uundaji wa istilahi za Kiswahili katika linux.
1.2 Malengo ya utafiti
Malengo ya utafiti huu yamegawanyika katika sehemu kuu mbili:
1.2.1 Lengo kuu na
1.2.2 Malengo mahususi

1.2.1 Lengo kuu
Lengo kuu la utafiti huu ni kutaka kutalii istilahi za Kiswahili zilizoingizwa katika mfumo wa mawasiliano ya kompyuta wa linux na kuainisha mbinu zilizotumika kuunda istilahi hizo.
1.2.2 Malengo mahususi
Malengo mahususi ya utafiti huu ni mawili, ambayo ni: kupambanua ubora na udhaifu wa mbinu zilizotumika katika uundaji wa istilahi za Kiswahili  katika linux na kubainisha mbinu bora zaidi inayoweza kutumika katika uundaji wa istilahi za Kiswahili.
1.3 Umuhimu wa utafiti
Umuhimu wa utafiti huu ni kwamba utasaidia kubainisha mbinu bora za uundaji wa istilahi za Kiswahili. Vilevile utafiti huu utawasaidia watumiaji wa kompyuta wanaotumia programu hii ya linux kwa Kiswahili kuelewa kwa urahisi istilahi zilizotumika baada ya kubainisha mbinu zilizotumika katika kuunda istilahi hizo.
1.4 Dhana ya istilahi, linux na nadharia ya uundaji istilahi
Istilahi ni dhana iliyofasiliwa na wataalamu mbalimbali na wote wanakubaliana kuwa, istilahi ni msamiati utumikao katika uwanja fulani maalumu wa lugha. Wataalamu wanaokubaliana na fasili hii ni pamoja na King’ei(2010), Samson(1988) na Kiango(2004). Kwa hiyo kulingana na fasili hii si kila msamiati ni istilahi bali msamiati huwa istilahi pale unapotumika katika Nyanja maalumu za kitaaluma. Kila uwanja maalumu wa kitaaluma huwa na msamiati wake ambao hauna maana nje ya taaluma hiyo wala haufahamiki kwa wazungumzaji lugha wasiokuwa wataalamu wa lugha hiyo. Kwa mfano msamiti unaotumika katika isimu,fasihi,teknolojia ya habari na mawasiliano na kadhalika ni maalumu na hutumiwa na kueleweka tu na wataalamu wahusikao na nyaja husika.
Linux kwa mujibu wa Msanjila na wenzake(2011) ni mfumo wa kompyuta huria unao ruhusu watu mbalimbali kuchangia katika marekebisho na maendeleo yake. Kimsingi linux ni mfumo endeshi wa kompyuta. Ni program katika kompyuta iayosaidia programu-tumizi na mtumiaji wa kompyuta kufikia vifaa fulani katika kompyuta ili kufanya kazi iliyokusudiwa, linux ni sawa na

program-tumizi zingine kama vile windows (Linux.com).
Nadharia ya uundaji istilahihujumuisha mambo kadhaa, kwa mujibu wa Tumbo-Masabo na Mwansoko(2008) mambo hayo ni pamoja na sababu za uundaji wa istilahi, njia au mbinu za uundaji istilahi,vyombo vya uundaji istilahi na misingi ya uundaji istilahi.
Katika sababu ya uundaji istilahi Tumbo-Masabo na Mwansoko wanasema kuwa, uundji wa istilahi ni muhimu panapotokea haja ya kushughulikia nyanja ambazo zilikuwa hazishughulikiwi kwa kutumia lugha fulani. Uundaji huo aghalabu hufanywa ili kukidhi haja ya mawasiliano katika elimu ya juu, ufundi na utaalamu,na shughuli zinazohusu serikali na teknolojia. Kwa hiyo nadharia ya uundaji istilahi huambatana na sababu au haja fulani ya kufanya hivyo. Kwa mfano uundaji wa istilahi za Kiswahili katika mfumo wa kompyuta wa linux umeambatana na sababu kwamba, kuuweka mfumo huu  wa kompyuta katika Kiswahili ili kusudi watumiaji wa Kiswahili waweze kuutumia mfumo huu kwa lugha wanayo ifahamu.
Vyombo vinavyohusika katika uundaji wa istilahi.
Katika kutekeleza kazi ya kuunda istilahi vimewekwa vyombo maalumu vinavyo tekeleza suala hili, kwa mfano Tanzania chombo kilchopewa jukumu hili na serikali ni Barza la Kiswahili la Taifa (BAKITA).
Vilevile katika nadharia ya misingi ya uundaji istilahi huzingatia mambo yafuatayo:
·         Uundaji wa istilahi ni budi uanzie kwenye dhana.
·         Dhana hizo zieleweke kwa ukamilifu na uwazi.
·         Uhusiano baina ya dhana ndio uwe msingi wa uundaji wa istilahi, istilahi kopwa zichukuliwe kama zilivyo katika umbo lake la asili kwa kufanya marekebisho machache tu kulingana na sarufi na matamshi ya lugha kopaji.
·         Istilahi inafaa ziwe fupi iwezekanavyo lakini zieleweke.
·         Istilahi ziwe na muundo unaoeleweka yaani zifuate mofolojia ya lugha.
·         Uundaji wa istilahi kwa vifupisho na akronomia uepukwe hasa kama istilahi kamili si ndefu sana.
·         Istilahi zisiwe na sinonimia au homonimia.
·         Istilahi ziundwe kwa njia ambayo itakuwa rahisi kuunda istilahi nyingine kwa

mnyambuliko.
·         Istilahi zitolewe kufuatana na mfumo wa dhana yaani ziainishwe kuliko kuandikwa kwa alfabeti.
·         Muundo wa istilahi udokeze maana yake kwa watumiaji wa lugha husika. Kwa hiyo misingi hii haina budi kufuatwa katika mchakato wa uundaji istilahi.
Nadharia nyingine kama ilivyoainishwa na Tumbo-Masabo na Mwansoko(wameshatajwa) ni njia za uundaji istilahi. Katika uundaji wa istilahi kuna njia kuu mbili ambazo zinatumika zaidi, njia hizo ni pamoja na:
(i)                 Kutafsiri hasa kutoka kwenye lugha zinazojulikana kuwa ni za kimataifa kama vile Kifaransa, Kiingereza, Kihisipania.
(ii)               Kuunda istilahi kutokana na mifumo ya dhana.
Njia ya kutafsiri hutumiwa sana na vyombo vingi vya uundaji istilahi kinyume na misingi ya uundaji ambayo inasisitiza kuwa uundaji huo uanze na dhana, msingi wa njia hii ni istilahi za lugha chasili ambazo aghalabu hupangwa kwa alfabeti. Faida ya njia hii ni kwamba istilahi nyingi zinaweza kushughulikiwa  kwa muda mfupi pia istilahi za lugha lengwa huweza kutafsiriwa katika lugha za kimataifa. Hata hivyo hasara ya njia hii ni kwamba kwa vile kila istilahi hushughulikiwa peke yake, hali hii huweza kusababisha mtiririko wa mfumo wa istilahi usio na ulingano.
Kahigi (2004) anasema kuunda istilahi kutokana na mifumo ya kidhana ni kwamba istilahi huundwa kufuatana na mifumo hiyo. Kwa mfano katika hisabati kuna mifumo ya elimu-maumbo, elimu-namba, vipimo na kadhalika. Mathalani katika kuunda istilahi za dhana ya pembe itabidi dhana zifuatazo zishughulikiwe zote kwa pamoja: pembekali, pembenukta, pembetatu, pembemshabaha, pebemstari na kadhalika. Faida ya mkabala huu ni kwamba mwishowe mifumo yote ya dhana huwa na mtiririko wenye ulingano.
Katika nadharia hii ya njia za uundaji istilahi mbinu mbalimbali hutumika, mbinu hizo ni pamoja na:mwabatano;hii ninjia ya uundaji istilahi kwa kuambatanisha maneno mawili au zaidi yaliyo 
huru. Mfano ; mbwa kichaa.
Mnyambuliko;ni uundaji wa neno jipya kwa kuambatisha viambishi kewenye mzizi au shina la neno. Mfano;wekeza  >  uwekezaji.
Muungano; hii mbinu ni sawa na mwambatano isipokuwa katika muungano maneno mawili au zaidi huunganishwa ili kuunda neno moja, mfano;kiini+macho  >  kiinimacho.
Kupanua maana ya maneno; huu ni mchakato ambapo neno lililopo kwenye lugha hupewa maana pana zaidi ya maana yake ya awali. Mfano butu maana yake ya kawaida ni –sio kali,-sio kata. Maana ya kihistilahi ni pembe ambayo ni zaidi ya nyuzi 90 na ndogo kuliko nhyuzi180(hisabati).
Ufupisaji; ni mbinu ambayo inatumika kufinyanza fungu la maneno ili kuunda neno moja,mfano; BAKITA (Baraza la Kiswahili laTaifa).
Ukopaji; ni matumizi ya neno kutoka lahaja ama lugha nyingine, aghalabu neno hilo hubadilishwa ili lishabihi muundo wa lugha lengwa.
Tafsiri-sisisi; ni aina ya tafsiri kutoka lugha chasili ambayo ni ya moja kwa moja. Mfasiri habadili lolote ila anahakikisha tu tafsiri inakuwa sahihi kwa mujibu wa lugha lengwa. Kwa hiyo katika mchakato wa uundaji wa istilahi za Kiswahili mbinu hizi hutumika.








                                                        
SURA YA PILI 
  Mapitio ya marejeo na mbinu za utafiti.
2.1 Mapitio ya Marejeo
Kutokana na mabadiliko yanayotokea katika jamii wataalamu wameonesha umuhimu wa lugha kuyakabili mabadiliko hayo. King’ei(2010) anasema lugha ni kielelezo cha maisha ya jamii siasa, elimu, sayansi, teknolojia, utamaduni, dini, kilimo, uhandisi, sanaa, uchumi ama biashara hubadilika kila mara, uvumbuzi mpya kila mara huzua dhana mpya ambazo zinahitaji maneno mapya ya kuzielezea.
Kulingana na kukua kwa teknolojia ya habari na mawasiliano,lugha ya Kiswahili haina budi kuyakabili mazingira haya. King’ei(ameshatajwa) anaelezea hatua ya kihistoria iliyochukuliwa na kampuni ya Microsoft mwaka 2005 kwa kuanzisha kamusi maalumu inayowawezesha watumiaji wa kompyuta kutumia lugha ya Kiswahili katika mawasiliano yao yote kwa kompyuta. Kwa maana kwamba katika programu hii mpya inamwezesha mtumiaji kompyuta asiyefahamu lugha nyingine kama vile kiingereza, kutumia kompyuta na kuwasiliana bila shida yoyote kwa Kiswahili.
Mtafiti mwingine ni Msanjila na wenzake(2011) wanasema hadi wakati huu lugha ya Kiswahili imekwisha ingizwa kwenye mifumo miwili ya kompyuta ijulikanayo kama linuksi namikrosofti. Wanaendelea kusema kuingizwa kwa Kiswahili katika mifumo hii maana yake ni kwamba mtumiaji anaweza kuvinjari mifumo hiyo ya kompyuta kwa Kiswahili akiamua kufanya hivyo.
Kimsingi hatua ya kuingiza Kiswahili katika mifumo hii ya kompyuta ni hatua muhimu sana katika maendeleo ya teknolojia ya habari na mawasiliano, katika mchakato wa kuiweka mifumo hii katika lugha ya Kiswahili ilihitajika kuundwa istilahi za Kiswahili ili mifumo hii iwekwe katika Kiswahili. Katika kuunda istilahi za Kiswahili mbinu mbalimbali hutumika, wataamu mbalimbali wamejadili kuhusu mbinu hizo:
Tumbo-Masabo na Mwansoko(2008) wanasema mbinu za uundaji istilahi ni pamoja na: Muungano wa maneno, mfano; mwanaisimu, mwambatano wa maneno, mfano; nusu kipenyo,
8
Unyambulishaji, mfano; ambisha  >  uambishaji, upanuzi wa maana za manenouhulutishji, mfano; kizigeu  >  kiziogeu, ukopaji (kukopa kutoka lugha za kigeni, lugha za kibantu au lahaja) na tafsiri-sisisi (tafsiri mkopo), mfano; measure of time  >  kipimo cha wakati.
King’ei(2010) ameainisha mbinu za uundaji wa istilahi za Kiswahili kuwa ni pamoja na uunganishaji wa maneno, ukopaji, kutafsiri maneno ya kigeni, mbinu ya ufupishajimfano;UKIMWI (Upungufu wa Kinga Mwilini) na utohozi.
Kahigi (2004) anasema mbinu za uundaji wa istilahi za Kiswahili ni pamoja na:unyambulishi, uambatani, uhulutishi, ufupishaji, utemaji, ukopaji, tafsiri mkopo na uundaji wa maneno mapya kabisa.
Vilevile Kiango (2004) ameanisha mbinu zifuatazo katika undaji wa istilahi za Kiswahili: kubuni nakukopa (kutoka lugha za kigeni, lugha za kibantu na lahaja).
Kwa hiyo kulingana na wataalamu hawa tunaweza kuanisha mbinu za uundaji wa istilahi za Kiswahili kuwa ni:
·         Unyambulishji   
·         Muungano wa maneno
·         Mwambatano wa maneno
·         Ukopaji
·         Tafsiri mkopo(tafsiri sisisi)
·         Uhulutishaji
·         Ufipishaji
·         Utemaji
·         Upanuaji wa maana ya maneno yaliyopo na
·         Kubuni
Tafiti za wataalamu hawa zina umuhimu mkubwa kwani zimesaidia kujua kuingizwa kwa Kiswahili katika mifumo ya kompyuta ya linux naMicrosoft na vilevi zimetusaidia kujua mbinu za uundji istilahi za Kiswahili. Kwa hiyo katika utafiti wetu tutabainisha mbinu zilizotumika

kuunda istilahi za Kiswahili katikalinux kati ya hizo zilizoainishwa na wataalamu hao
2.2 Mbinu za ukusanyaji data
Katika utafiti huu mbinu iliyotumika ni moja, yaani mbinu ya kusoma marejeo mbalimbali hii ni kwa kuwa utafiti huu ni wa kimakitaba. Mbinu hii imetumika katika ukusanyaji wa data zinazohusu istilahi za Kiswahili zilizoingizwa katika mfumo wa kompyuta wa linux, ambapo mbinu  hii imetumika kwa kusoma marejeo kwa njia ya wavuti na kukusanya istilahi za Kiswahili zilizokuwepo katika mfumo wa kompyuta wa linux.
Mbinu hii pia imetumika katika kukusanya data zinazohusu mbinu za uundaji istilahi za Kiswahili. Kwa kusoma marejeo mbalimbali data zinazohusu mbinu za uundaji wa istilahi za Kiswahili zilikusanywa.
Vilevile mbinu hii imetumika katika ukusanyaji wa data zinazohusu ubora na udhaifu na udhaifu wa mbinu zilizotumika katika uundaji wa istilahi za Kiswahili katika linux. Na pia mbinu hii imetumika katika ukusanyaji wa data zinazohusu kubainisha mbinu bora katika kuunda istilahi za Kiswahili.
Data katika utafiti huu zimekusanywa kutoka faharasa ya teknolojia ya habari ya KILinux(KlnX) juzuu ya kwanza. Faharasa hii inajumuisha orodha ya istilahi 700Sampuli ya utafiti huu inajumuisha istilahi 100.Sampuli hii imechukuliwa kinasibu (kiholela) yaani hakuna mpangilo au utaratibu wowote maalumu uliofutwa katika uchukuaji wa sampuli.



                                            


SURA YA TATU
Uchambuzi wa data
2.1 Utangulizi
Utafiti huu umegawanyika katika sehemu kuu mbili, sehemu ya kwanza inahusu  uchambuzi wa data zinazohusu mbinu zilizotumika katika uundaji wa istilahi za Kiswahili katikalinux na sehemu ya pili inahusu kupambanua ubora na udhaifu wa mbinu zilizotumika kuunda istilahi za Kiswahili katika linux na kubainisha mbinu iliyo bora katika kuunda istilahi za Kiswahili. Katika uchambuzi wa data hizi tutatumia nadharia ya uundaji istilahi za Kiswahili ambayo imekwishaongelewa katika kipengele cha 1.4.    
2.2  Mbinu zilizotumika katika uundaji wa istilahi za Kiswahili zilizoingizwa katika linux.
Mbinu zilizotumika katika uundaji wa istilahi za Kiswahili katika linux ni kama zilivyobainishwa hapa chini:
Unyambulishi; katika mbinu hii kitenzi kinaweza kugeuzwa kikawa nomino au kivumishi kinaweza kugeuzwa kikawa kitenzi au au nomino. Mbinu hii imetumika kwa kiasi kikubwa, mifano ifuatayo hudhihirisha matumizi ya mbinu hii.
·         Accessing   >   ufikio ( viambishi u-i-o vimeambatiswa katika shina fika).
·         Accsess     >      fikio (viambishi i-o vimenyambulishwa katika shina  fika )
·         Allocation    >     utengaji (viambishi u-aji vimeambatishwa katika shina tenga)
·         Bookmark link   >   alamisho (viambishi ish-o vimeambatishwa katika shina alama).
·         Bookmark   >   alamisha(t) (viambishi ish-a vimeambatishwa na kuunda kitezi alamisha)
·         Deleting    >   ufutaji (viambishi u-aji vimeambatishwa katika kitenzi futa  )
·         Deletion    >    mfuto (viambishi m-o vimeambishwa katika kitenzi futa nakupata neno                                         mfuto)
·         Input   >    ingizo (kiambishi –o kimeambishwa katika shina ingiza na kuunda istilahi ingizo).

·         Interactive   >   wasilianifu ( kiambishi –ifu kimeambishwa katika shina wasiliana na kuunda neno wasilianifu).
·         Allocation(n)   >    mtengo (viambishi m-o vimeambishwa katika shina tenga na kuunda nomino mtengo ikiwa na dhana ya matokeo).
Mwabatano; hii ni njia inayotumika kwa kuambatanisha maneno mawili au zaidi. Katika linux kuna istilahi zenye mwambatano wa maneno mawili na mwambatano wa maneno matatu. Mifano ifuatayo inadhihirisha matumizi ya mbinu hii:
·         Add-on help   >   msaada nyongeza ( yameambatishwa maneno msaada na nyongeza).
·         Alphabet text character   >   kiwambo alfabeti (kiwambo + alfabeti).
·         Aperture value   >    thamani upenyo (thamani + upenyo)
·         Background colour    >   rangi usuli (rangi + usuli).
·         Block device    >     kitunza data ( (ki)tunza + data).
·         Bullet list   >    orodha tobwe (orodha + tobwe).
·         Composer    >    programu tumizi (programu+ tumizi).
·         Configuration utility   >   programu sanidi (programu + sanidi).
·         Checksum    >    namba thibitishi (namba + thibitishi).
·         Encrypted    >    msimbo fiche (msimbo + fiche).
Vilevile kuna istilahi zilizoundwa kwa kuambatanisha maneno matatu. Mfano:
·         Encrypted text   >   matini-msimbo fiche (matini + msimbo + fiche).
·         Full-screen mode   >   modi-skrini nzima (modi + skrini + nzima).
·         Small caps   >      herufi kubwa ndogo (herufi + kubwa + ndogo)
·         Column spam   >    upana-safu wima (upana + safu + wima).
·         Default search engine   >   injini tafuti-msingi (injini + tafuti + msingi).
·         Com port (communication port) >  mlango wa mawasiliano(mlango+wa+mawasiliano).
Muungano; hii ni mbinu ya kuunganisha maneno mawili au zaidi ili kupata neno moja mbinu hii pia imetumika kuunda istilahi za Kiswahili katika linux. Mifano ifuatayo inabainisha

kutumika kwa mbinu hii:
·         Anonymity   >   ufichojina (uficho + jina).
·         Arccosine   >    kosinitao (kosini + tao).
·         Backslashes   >   mkwajunyuma ( mkwaju + nyuma).
·         Data area    >    eneodata (eneo + data).
·         Data bank   >    kanzidata (kanzi + data).
·         Data base    >    kihifadhidata ( (ki)hifadhi + data).
·         Footnote    >    tiniwayo (tini + wayo).
·         Hypertext   >   matinifora (matini + fora).
·         Keybody    >    baobonye (bao + bonye).
·         Newsgroup   >   kundihabari (kundi + habari).
·         Spreadsheet   >   lahajedwari (laha + jedwari).
Ukopaji; njia hii pia imetumika kuunda isuilahi za Kiswahili katika linux. Mifano ifuatayo inaonyesha kutumika kwa mbinu hii.
·         Account    >    akaunti
·         Adapter    >   adapta  
·         Ampersand   > ampasendi
·         Applet   >    apuleti
·         Autoformat   >    fomati otomati
·         Baud   >       baudi
·         Boolean   >    buleani
·         Buffer    >     bafa
·         Cursor    >     kasa
·         Daemon    >   dimoni
·         Dial    >     dayo
·         Digit    >   dijiti
·         Icon    >    ikon
·         Kilobyte    >    kilobaiti

·         Pixels    >     pisel
·         Printer   >  printa
Mbinu hii ya ukopaji imetumika kwa kiasi kikubwa katika uundaji wa istilahi za Kiswahili zilizopo katikalinux.
Mbinu nyingine iliyotumika kwa kiasi kikubwa katika uundaji wa istilahi za Kiswahili katika linux ni mbinu ya tafsiri mkopo (tafsiri sisisi). Tafsiri mkopo nitafsiri ya moja kwa moja kutoka lugha chanzi. Mifano ifuatayo inathibitisha matumizi ya mbinu hii katika uundaji wa istilahi za Kiswahili katika linux.
·         Actions menu   >   menyu vitendo.
·         Address book   >   kitabu cha anwani.
·         Alert me    >     nitahadharishe.
·         Auto complete     > kamilisha kiotomati.
·         Boolean operations     >     matendo buleani.
·         Certificate manager    >    meneja ithibati.
·         Certificate viewer      >     kionyeshi hati.
·         Chat group    >     kundi sogozi.
·         Colour capability    >     uwezo kirangi.
·         Connection failure     >     unganisho shinde.
·         Control panel     >    paneli dhibiti.
·         Country code    >     msimbo nchi.
·         Device manager    >    meneja vifaa.
·         Dialogue box     >     kisanduku cha mawasiliano.
·         Drag and drop   >    kokota na dondosha.
·         Eject     >       fyatua.
·         Flow control     >     udhibiti wa mtiririko.
·         Word processor    >    kichakata matini.
·         Web master    >     mtawala tovuti.

Mbinu nyingine ni mbinu ya kuunda maneno mapya kabisa mbinu hii imetawaliwa na maneno ya mkopo. Mfano:
·         Icon   >     ikoni
·         Italic    >   italiki
·         Label    >   lebo
·         Megabyte(MB)   >    megabaiti(MB)
·         Menu proxies    >    menyu proksi
·         Manager   >    meneja
·         Pixels   >     piseli
·         Program    >   programu
·         Scan    >    skani.
·         Scanner    >  skana
·         Tab    >    tabo
·         Tag    >  tagi
Mbinu ya ufupishaji pia imetumika katika kuunda istilahi za Kiswahili katika linux; hii ni mbinu inayotumika kufinyanza fungu la maneno na kupata neno moja. Mifano ifuatayo huonyesha matumizi ya mbinu hii:
·         Alt(alternate)    >    Kbdl (kibadala)
·         BSS (Bulletin Board Service)     >     HUM (Huduma za Ubao wa Matngazo)
·         Ctrl (ontrol)     >   Kdbt (kidhibiti)
·         ESC (escape)   >    Epa (epuka)
·         FAQ (frequently asked quetions)   >    MYM (Maswali Yaulizwayo Mara kwa mara)
·         FTP (file transfer protocol)    >      IKF (Itifaki ya Kuhawalisha Faili)
·         FYI (For Your Information)    >    KTY (Kwa Taarifa Yako)
·         Megabyte (MB)       >      megabaiti (MB)
·         Ref:           >       Yah:
·         Re:             >        Jb:
·         TCP (Transfer Control Protocol)      >     IKU (Itifaki ya Kudhibiti Urushaji)

·         URL (Uniform Resource Location)   >   KISARA (Kioneshi Sanifu Rasilimali)
·         WWW (World Wide Web)      >    WWW (Wavu Wa Walimwengu)
Uhulutishi ni mbinu pia liyotumika katika uundaji wa istilahi za Kiswahili katika linux, mbinu hii hutumika katika uundaji wa istilahi kwa kuunganisha sehemu za maneno na kuunda neno moja. Mbinu hii imetumika kwa kiasi kidogo sana, rejea mifano ifuatayo:
·         Bitmap    >   taswidoti ( (taswi)ra + doti)
·         Multimedia    >   medianuwai ((medi)a + anuwai)
Mbinu nyingine iliyotumika katika uundaji wa istilahi za kiswahili katikalinux lakini kwa kiasi kidogo sana ni ilembinu ya upanuzi wa maana za maneno, upanuzi wa maana za maneno ni kuongezea maana maalumu za kihistilahi katika maneno ya Kiswahili. Mfano:
·         Mouse      >       puku
Puku kwa maana ya kawaida ni panya pori lakini hapa limepewa dhana mahususi katika kompyuta kwa maana ya kifaa kinachotumika katika utumiaji wa kompyuta.
Utemaji (clipping) ni mbinu pia iliyojitokeza kwa kiasi kidogo sana, kwa kutumia mbinu hii istilahi huundwa kwa kukata sehemu ya neno na sehemu ya neno itakayobaki hutumika kama istilahi. Mfano: key (on keyboard)     >    kibonye ( kutoka neno bonyeza na kuongeza kiambishi cha ngeli ya saba ki-).
Kwa hiyo hizi ndizo mbinu zilizobainika kutumika katika uundaji wa istilahi za Kiswahili zilizoingizwa katika mfumo wa kompyuta wa linux.
2.3 Ubora na udhaifu wa mbinu zilizotumika kuunda istilahi za Kiswahili katika linux.
2.3.1 Ubora wa mbinu zilizotumika.
Kwa kiwango kikubwa mbinu zilizotumika zimezingatia misingi na kanuni za uundaji istilahi. Kwa mujibu wa Tumbo-Masabo na Mwansoko (2008) wanabainisha kuwa misingi mahususi

katika uundaji wa istilahi ni pamoja na: Uangavu wa wa istilahi iliyoundwa yaani istilahi ziakisi sifa bainifu za dhana zinazoziwakilisha. Mbinu zilizotumika katika uundaji wa istilahi za Kiswahili katika linux kwa kiasi kikubwa zimezingatia msingi huu. Kwa mfano:
Ufikio     >    accessing,         ingizo    >     input,   alamisha     >     bookmark.
Istilahi hizi zinaonyesha wazi dhana zinazowakilishwa, kwa mfano, alamisha inabeba dhana ya   kitendo cha kuweka alama hivyo kwa msingi huu inadhihirisha mbinu zilzotumika ni bora. Vilevile mbinu zilizotumika zimezingatia msingi wa uundaji istilahi unaosema, istilahi sharti ziwe na uwezo mkubwa wa kunyambuliwa na kuunda istilahi nyingine za kikoa au ukanda unaohusika. Msingi huu umefuatwa katika kuunda istilahi za kwenye linux, kwani istilahi nyingi zilizoundwa zina uwezo wa kunyambulishwa. Mfano:
·         Add   >    ongeza
·         Add-on    >    nyongeza
·         Alert(n)    >    thadhari
·         Alert(v)     >    tahadharisha
Pia uundaji wa istilahi za kwenye linuxumezingatia msingi wa uundaji istilahi unaosema,uwakilishi wa istilahi moja kwa dhana moja. Msingi huu umezingatiwa kwa kiasi kikubwa kwani istilahi takribani zote huwakilisha dhana moja isipokuwa zile zilizoundwa kwa kupanua maana ambazo ni chache sana.
Mfano: configuration    >  usanidi
             Configuration file   >   faili sanidi
Vilevile mbinu zilizotumika ni bora kwani hazijatumia kwa kiasi kikubwa mbinu za uhulutishi na mbinu ya kupanua maana ya maneno yaliyopo, hii ni kwa sababu misingi ya uundaji wa istilahi za Kiswahili husisitiza kuepuka matumizi ya mbinu hizi; hii ni kwa kuwa istilahi zinazo uundwa kwa mbinu ya uhulutishi huwa na uvulivuli wa maana na kufanya kuwa ngumu kukumbukwa na kutumiwa. Pia uundaji wa istilahi kwa kupanua maana ya maneno yaliyopo husababisha watumiaji wa istilahi hizi kushindwa kutofautisha maana zake za kawaida na zile za

kihistilahi.
Mbinu za uundaji istilahi za Kiswahili katika linux, pia zimezingatia msingi wa uundaji wa istilahi za Kiswahili unaosema, istilahi sharti ziwe fupi na zenye kueleweka. Istilahi nyingi zimeundwa kwa kuzingatia msingi huu.

2.3.2 Udhaifu wa mbinu zilizotumika
Katika uundaji wa istilahi za Kiswahili za kwenye linux, kuna baadhi ya mbinu zilizotumika zinazoonyesha kuvunja kanuni na misingi ya uundaji istilahi. Kwa mfano kuna istilahi zilizoundwa kwa kukiuka msingi wa uundaji istilahi unaosema, istilahi sharti ziwe fupi na zenye kueleweka. Kuna baadhi ya istilahi ambazo ni ndefu na hivyo kukiuka huu msingi. Mfano:
·         Allow popup from this site    >    ruhusu udukizi kutoka tovuti hii
·         Com port      >        mlango wa mawasiliano
Istilahi hizi zimeonekana kuwa ndefu kwa sababu mbinu iliyotumika ni ya mwambatano wa maneno, na kwa mujibu wa Tumbo-Masabo na Mwansoko wanasema, “iwapo istilahi zitaundwa kwa kutumia mbinu za muungano na mwambatano wa maneno basi mambo yafuatayo itabidi yazingatiwe”:
                  i.             Idadi ya maneno yanayounganishwa au yanayoambatanishwa yafaa yasizidi mawili.
                ii.            Vistari visitumike kutenga istilahi ambatani kwani katika Kiswahili istilahi za namna hii hutamkwa kama neno moja lenye mkazo mkuu kwenye silabi moja tu.
              iii.            Istilahi za namna hii yafaa zisiwe na silabi zaidi ya nane kwani kwa kawaida maneno ya Kiswahili yanawastani kati ya silabi moja na tano tu. Kwa msingi huu mifano ya itilahi zilizotolewa hapo juu zimeundwa na maneno zaidi ya mawili na silabi zaidi ya nane. Mfano ; mlango wa mawasiliano (silabi 10), ruhusu udukizi kutoka tovuti hii (silabi 15) na hivyo huu ni udhaifu uliojitokeza.
Vilevile matumizi ya mbinu za uhulutishi na upanuzi wa maana ya maneno yaliyopo zimetumika, huu ni udhaifu kwani misingi ya uundaji wa istilahi za Kiswahili inasema, mbinu ya

uhulutishaji iepukwe kwani etimolojia yake ina uvulivuli na uundaji wa istilahi kwa kupanua maana ya maneno yaliyopo yafaa uepukwe kwani istilahi za namna hii zinawakanganya wengi hasa zinapotumika nje ya muktadha au kwenye taaluma zenye mahusiano ya karibu.
Mifano ya istilahi zilizoundwa kwa uhulutishaji ni:
·         Taswidoti    >      bitmap
·         Medianuwai     >    multimedia
Na mfano wa istilahi iliyoundwa kwa upanuzi wa maana ya neno ni:
Puku    >    mouse. Puku ni istilahi iliyopanuliwa maana ambapo maana yake ya kawaida ni panya pori lakini maana yake maalumu ni kifaa kinachotumika katika utumiaji wa kompyuta.
Kwa hiyo huu ndio udhaifu wa istilahi zilizotumika katika uundaji wa istilahi za Kiswahili katika linux.

2.3.3 Mbinu bora zaidi katika uundaji wa istilahi za Kiswahili.
Kulingana na utafiti huu mbinu zilizoonekana kuwa bora zaidi na ambazo zinatumika sana katika uundaji wa istilahi za Kiswahili ni pamoja na, unyambulishaji, ukopaji, mwambatano, muunganiko pamoja na tafsiri mkopo. Mbinu hizi zimeonekana kuwa bora katika uundaji wa istilahi za Kiswahili kwa sababu zinaruhusu uundaji istilahi kwa wingi iwezekanavyo na mbinu hizi huzingatia misingi ya uundaji istilahi za Kiswahili. Misingi hiyo ni pamoja na ufaavu wa kiisimu, uwekevu wa kiisimu, unyambulifu , uwakilishi wa istilahi moja kwa dhana moja, udhahiri na utoshelevu pamoja na uangavu. Mbinu hizi huakisi kwa kiasi kikubwa misingi hii na hivyo kupendekezwa na waunda istilahi katika uundaji wa istilahi za Kiswahili.


                                            

                                             SURA YA NNE
   Muhtasri na Hitimisho
4.1 Matokeo ya utafiti kwa muhtasari
Utafiti huu umeongelea malengo matatu. Kwanza utafiti huu umebainisha mbinu za uundaji istilahi zilizotumika katika linux. Pili utafiti umepambanua ubora na udhaifu wa mbinu za uundaji istilahi za Kiswahili zilizotumika katika linux. Tatu umebainisha mbinu bora zaidi katika uundaji wa istilahi za Kiswahili.
Utafiti huu umeonyesha kuwa mbinu kumi za uundaji istilahi za Kiswahili zimetumika katika istilahi za linux. Mbinu hizo ni pamoja na:
Unyambulishi; mifano ya istilahi zilizoundwa kwa mbinu hii ni kama vile:
·         Ufikio   >    accessing
·         Utengaji   >   allocation
·         Alamisho   >    bookmark link
·         Ingizo   >    input
Muungano wa maneno; mifano ya istilahi zilizoundwa kwa mbinu hii ni pamoja na:
·         Ufichojina   >   anonymity
·         Mkwajunyuma   >   backslashes
·         Kanzidata     >      databank
Ukopaji; mbinu hii pia imetumika katika kuunda istilahi za kwenye linux. Mfano:
·         Akaunti    >   account
·         Apuleti      >   applet
·         Dayo      >      dial
Tafsiri mkopo (tafsiri sisisi); mifano ya istilahi zilizoundwa kwa kutumia mbinu hii ni:
·         Menyu vitendo    >    actions menu

·         Meneja ithibati    >    certificate manager
·         Paneli dhibiti     >       control panel
Mwambatano;  mbinu hii vilevile imebainishwa kutumika katka uundaji wa istilahi za Kiswahili  katika linux:
Mifano:   Rangi usuli    >     background color
                Orodha tobwe    >    bullet list
                Thamani upenyo   >    aperture value
Kuunda maneno mapya kabisa;mbinu hii pia imetumika. Mfano.
·         Ikoni    >   icon
·         Italiki    >    italic
·         Menyu proksi   >   menu proxies
Ufupishaji; katika utafiti huu mbinu hii pia imetumika. Mfano:
·         Kbdl (kibadala)   >   Alt (alternative)
·         Kdbt (kidhibiti)   >    Ctrl (control)
·         Epa (epuka)     >     Esc (escape)
·         KISARA (Kioneshi Sanifu Rasilimali )   >    URL (Uniform Resource Location)
Uhulutishi; mbinu hii pia imetumika. Mfano:
·         Taswidoti   >   bitmap
·         Medianuwai   >   multimedia
Upanuzi wa maana; mfano, puku (panya pori)   >   mouse.
Utemaji (clipping); mbinu hii pia imetumika. Mfano, kibonye   >   key (on keybody).
Kwahiyo hizi ndizo jumla ya mbinu zilizo tumika kuunda istilahi za Kiswahili katika linux.

Matokeo ya utafiti huu yanaonyesha mbinu zilizotumika ni bora kwa kiasi kikubwa hii ni kutokana na sababu kwamba, mbinu zilizotumika zimezingatia misingi na kanuni za uundaji istilahi kwa kiasi kikubwa. Lakini vilevile baadhi ya mbinu za uundaji istilahi zimetumika
 ambazo kwa mujibu wa misingi ya uundaji istilahi hazifai kutumiwa katika mchakato wa uundaji wa istilahi za Kiswahili. Mbinu hizi ni pamoja na uhulutishi na upanuzi wa maana ya maneno yaliyopo.
Pia utafiti huu umebainisha mbinu bora katika uundaji wa istilahi za Kiswahili kuwa ni unyambulishaji, muungano wa maneno, uambatishi, mkopo pamoja na tafsiri mkopo. Hii ni kwa sababu mbinu hizi huzingatia misingi ya uundaji wa istilahi za Kiswahili kwa kiwango kikubwa.

3.2 Hitimisho
Katika mchakato wa uundaji wa istilahi za Kiswahili kuna misingi ambayo hainabudi kufuatwa. Ili kuunda istilahi zilizobora mwanahistilahi hanabudi kuzingatia misingi hii.
Kwa mujibu wa Tumbo-Masabo na Mwansoko (2008) wanasema kuwa ili kuinua ubora wa istilahi za Kiswahili waundaji istilahi wanasisitizwa kuzingatia mambo matatu muhimu. Kwanza wanasisitizwa kwa kadri iwezekanavyo wafuate kwa makini kanuni na taratibu za uundaji istilahi za Kiswahili. Kwa kufanya hivi itawezesha kwa kiwango kikubwa kuundwa istilahi za Kiswahili zenye kulandana vizuri kisarufi.
Pili waundaji istilahi wanahimizwa kuachana na mtindo wa kuunda istilahi moja moja kukidhi mahitaji yao ya istilahi ya papo kwa papo kwani mtindo huu unasababisha uundaji wa istilahi zisizo na mtiririko na  utimilifu wa kuridhisha. Kwa kuwa dhana zinazo wakilishwa na istilahi kwa kawaida huwa hazikai pweke pweke bali hukaa kama seti au mifumo maalumu, basi ni vema uundaji istilahi ufuate vilevile mifumo hiyo ya kidhana. Kulingana na maelezo haya kinachosisitizwa ni uundaji wa istilahi kwa kuzingatia mifumo ya kidhana. Kwa mujibu wa Tumbo-Masabo na Mwansoko (wameshatajwa) wakimnukuu Mkude (1989:34) wanasema,

uundaji wa istilahi kwa kuzingatia mfumo wa kidhana unafaida kuu nne:
(i)     Utawasaidia waunda istilahi kuonyesha wazi mantiki ya uhusiano baina ya istilahi za ukanda mmoja.
(ii)   Utawahimiza waunda istilahi kubainisha vizuri zaidi tofauti ndogondogo lakini muhimu baina ya istilahi zinazokaribiana.
(iii) Utawasaidia kutambua haraka mapengo katika nasaba au upungufu katika maelezo.
(iv) Utawasaidia waunda istilahi kuona haraka ni istilahi zipi zitaweza kuathiriwa upesi iwapo  kutatokea mabadiliko katika istilahi moja wapo.
Hivyo utaratibu wa uundaji istilahi kinasaba ukitumiwa utaepusha uundaji wa istilahi zinazogongana na zisizo na mtiririko wenye mantiki.
Jambo la tatu kama ilvyoainishwa na Tumbo-Masabo na Mwansoko ni kwamba uundaji wa istilahi haunabudi kuzingatia tofauti za watumiaji, mathalani viwango vyao vya elimu, mazingira yao na kadhalika. Kwa hali hii ili kuhakikisha istilahi bora za Kiswahili zinaundwa ni muhimu hadhira mahususi za watumiaji istilahi ziainishwe na istilahi ziundwe kufuatana na viwango vya elimu ya watumiaji lengwa. Ni kwa kufanya hivyo dhana kama vile istilahi angavu au istilahi zenye uvulivuli zitakuwa na maana halisi kwani zitahusishwa na vikundi mahususi vya watumiaji istilahi.

Na Aritamba Malagira.
Haki zote zimehifadhiwa. 








                                                 MAREJEO

Kahigi,K.K (2004).Ujanibishaji wa office na windows xp kwa Kiswahili sanifukatika
                 http//ajol.info.
Kiango,J.G (2004). Uundaji wa msamiti mpya katika Kiswahili: Zoezi lenye njia mbalimbali
                 katika Kiango.htm.
King’ei, K (2010). Misingi ya isimujamii. Dar es salaam. Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili.
Msanjila,Y.P, Kihore,Y.M na D.P.B Massamba (2011). Isimujamii sekondari na vyuo.
                    Dar es salaam. Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili.
Samson, H.R (1988). Ufundi wa magari, mfano wa ukuzaji wa istilahi za Kiswahili katika
                     Mulika na.21. Dar es salaam. Taasisi ya uchunguzi wa Kiswahili.
Sewangi,S.S (2004). Maana katika uundaji wa istilahi katika Sewangi,pdf.
Tumb-Masabo,Z.N.Z na Mwansoko,H.J.M (2008). Kiongozi cha uundaji istilahi za Kiswahili.
                       Dar es salaam. Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili.