Maana ya falsafa ya kiafrika kwa mujibu wa Placide Tempels, Falsafa ya
kiafrika ni ile falsafa inayowashughulisha waafrika wenyewe na watu
wengine ambao sio waafrika lakini wanakubaliana na mila, tamaduni za
waafrika na fasihi simulizi za kiafrika.Hivyo falsafa ya kiafrika ni ile
falsafa ambayo imejikita katika mifumo ya kijamii, mila na desturi na
fasihi simulizi za kiafrika.
Placide Tempels alizaliwa tarehe
18/02/1906 katika mji wa Barcal huko Ubelgiji na alikufa tarehe
09/10/1977 akiwa na umri wa miaka sabini na moja huko huko Ubelgiji.
Aliishi Kongo kwa miaka ishirini na tisa mpaka pale aliporejea kwao
ubelgiji. Kwa kipindi chote alipokuwa Kongo alifanya kazi kuu mbili,
kazi ya umishenari na uandishi.Katika kipindi chote hicho alichokaa
Kongo alisoma tabia ya waafrika wanaoishi Kongo hususani kabila la
Waruba, na akabaini kuwa waafrika wana tamaduni zao zilizojikita katika
fasihi simulizi. Hivyo akaandika kitabu chake kiitwacho “The Bantu
philosophy” (1945), katika kitabu hicho anapinga mawazo ya wazungu kwa
kusema kuwa waafrika wanafalsafa yao na hivyo Tempels akatumia hoja
kadhaa kutetea mawazo yake hayo, kama imani ya uchawi, hofu ya uhai na
kifo, nguvu hai, suala la ndoa na dhana ya uduara.
Katika kujibu
swali hili riwaya ya “Mirathi ya Hatari” ndio inayotumika. “Mirathi ya
Hatari” ni riwaya ilioandikwa na C. G. Mung’ong’o (1977). Riwaya hii
inajaribu kuelezea visa na mikasa ya kisihiri iliojitokeza katika jamii
za kiafrika hususani katika jamii ya Njombe (Kiterevadzi) na maeneo
mengine. Hivyo msanii amemtumia mhusika Gusto ambaye ndiye
anayerithishwa mirathi ya hatari kutoka kwa baba yake Mzee Kazembe,
mirathi hiyo ndiyo inayopelekea vifo vingi kutokea ikiwemo visasi mfano
kifo cha mama yake Gusto na dada yake Nandi, pia inapelekea kifo cha
mjomba ake Gusto Kapedzile. Ukiachana na vifo hivyo pia inapelekea
kutokea kwa matukio mengi ya kiuchawi.
Ufuatao ni uhakiki wa
riwaya ya “Mirathi ya hatari” kwa kuzingatia misingi ya kisalsafa kama
ilivyoainishwa na Placide Tempels katika kitabu cha “The Bantu
Philosophy” na kuonyesha uhalisia wake na faida na hasara ya falsafa
hiyo katika jamii ya kitanzania.
Imani ya uchawi, Katika falsafa
ya imani ya uchawi Tempels anaamini kwamba waafrika wanategemea sana
nguvu za kichawi, katika kuelezea suala hilo Tempels anajaribu kuangalia
jamii ya Ulaya kwamba wengi wapatapo matatizo hurudi kwa Kristo lakini
jamii nyingi za Afrika pindi wapatapo matatizo hutegemea uchawi kama
suluhisho la matatizo yao wanayarudisha kwenye imani za kishirikina.
Falsafa hii ya imani ya uchawi imejitokeza kwa kiasi kikubwa sana katika
riwaya ya “Mirathi ya Hatari” kwani kuna matukio mengi ambayo
yanadhihirisha hilo. Mfano, kitendo cha Gusto kukabidhiwa mirathi ya
uchawi kutoka kwa baba yake. Mfano uk. 15 Mzee Kazembe anamwambia Gusto
“Mwanangu nakuachia kazi kubwa. Ni urithi mkubwa ukiutumia vyema, bali
pia ni mirathi ya hatari usipojihadhari nayo, nakuachia dawa zote za
milki yangu katika mizungu ya sihiri”. Pia uwepo wa kiapo cha uchawi,
unadhihilika pale ambapo Gusto anaapishwa kama ni uaminifu wa kuingia
katika uchawi kiapo hicho kila mtu anahitaji kiapo ndipo awe mchawi;
mfano katika ukurasa wa 21 anaonekana akiapa kwa kutamka maneno, “Enyi
Mahoka na Mababu...”. Pia mazingira ya vifo vyote, vinatokea katika
mazingira ya utatanishi ambayo ni mazingira ya kichawi. Mfano, kifo cha
Kapedzile, ambaye aliuliwa na Gusto, kifo cha Dina ambaye aliuliwa
katika mazingira ya kichawi na baba yake, kifo cha mama yake Gusto
Nyamidze na Nandi ambao walikuwa na Malipula kwa kutaka kulipa kisasi na
kifo cha Malipula aliyeuliwa na Gusto pamoja na Mavengi katika
mazingira ya Kichawi.
Katika jamii yetu ya kitanzania imani ya
uchawi inajitokeza sana kwani kuna matukio mengi yanayojitokeza na
yanaonekana kiuhalisia mfano watu kugandishwa katika nyumba za watu na
pia kila kukicha wanaonekana wakianguka usiku na Nyungo zao, pia suala
la uwepo wa misukule katika nyumba za watu. Pia baadhi ya watu kutumia
hirizi kama kinga. Falsafa ya imani ya kichawi haina nafasi katika jamii
kwani inasababisha migogoro mingi, maafa pamoja na kurudisha maendeleo
nyuma. Hivyo wanajamii wa leo wanaaswa kuachana na imani za kichawi.
Hofu ya uhai na kifo. Hii ni hoja nyingine ya Tempels kwani anaamini
kuwa Waafrika wana hofu ya uhai na kifo. Kwa kudhihilisha hili anaweza
kuangalia salamu zao, na pia mtu anapopatwa na ugonjwa anaamini hawezi
kupona na kifo kinamsogelea. Wazo hili limejitokeza pia katika riwaya ya
“Mirathi ya Hatari” mfano pale Mzee Kazembe anapomueleza mwanae kuwa
hali yake ni mbaya na kifo kinamkaribia uk. 15 “Siku zangu zimekwisha
sidhani kama nitaishi zaidi”. Pia mama yake Gusto alikuwa na hofu na
uhai wa Gusto na ndio maana akamuusia aachane na mirathi aliyokabidhiwa
na baba yake kwani anaweza akapoteza maisha. uk 38 “Sipendi nimpoteze
tena hata mmoja wenu kabla sijafa”.Pia suala la salamu na kujua hali ya
mtu inaonesha hofu ya kifo, mfano ni pale Malipula alipokwenda nyumbani
kwa kina Gusto walianza kujuliana hali uk. 57,......Nikawauliza.....,
“Habari za nyumbani wazee wangu”, “Nyumbani kwema tu” alijibu mzee
Kindimba “Lakini hatujui ya huko nyuma”
Suala la hofu ya uhai na
kifo linajitokeza sana katika jamii ya kitanzania mfano, Watanzania
asubuhi wakiamka au wasipoonana muda mrefu basi hutoleana salamu na
kujuliana hali, pia pale mtu anapoamua watu huwa na wasiwasi sana na
uhai wake hivyo hujikithirisha kumuombea dua ili aweze kupona. Falsafa
ya uhai na kifo ina nafasi katika jamii kwani inawafanya wanajamii
kuchukuwa tahadhari ili kuzuia kifo, pia inaendeleza dhana ya kustawisha
zaidi uhai. Kwa upande mwingine falsafa hii in hasara kwani hurudisha
nyuma maendeleo kwa sababu mtu ataogopa kufanya suala la maendeleo kwa
kuhofia kifo ambacho kitamfanya kuacha mali zote alizochuma pia
kutotimiza malengo yake.
Waafrika wanaamini katika suala la ndoa,
pia hili ni wazo la Placide Tempels ambae anasema kuwa waafrika
wanaamini sana katika ndoa zao na ndoa hizo hudumishwa ili kupata
watoto. Uhai wa binadamu unaanzia kwenye mimba ambayo ni matokeo ya
Ndoa. Wazo hili linaonekana sana katika riwaya ya “Mirathi ya Hatari”
mfano ndoa ya Kazembe na Nyamidze watoto wanaopatikana ni nane na
wanaokufa ni watoto watano ambapo uk. 5 unaonyesha hilo. Pia familia ya
Malipula na mkewe pia wana watoto. Pia mjomba wake Dina alikuwa na ndoa
iliyompeleka kupata watoto katika uk.78.
Suala hili la ndoa
linasawiri maisha halisi ya kila siku ya Tanzania mfano kuna ndoa za
kanisani, msikitini ndoa za serikali na ndoa za kijadi. Suala la ndoa
lina nafasi kubwa katika jamii kwani inaendeleza nguvu kazi inayotokana
na watoto wanaozaliwa ambao wanatumika katika ujenzi wa taifa kwa sababu
hujishughulisha na shughulu mbalimbali za ujenzi wa taifa. Pia falsafa
hii huunganisha jamii, vile vile inaleta heshima katika jamii. Kwa
upande wa hasara ni pale inapotokea ndoa za kulazimishwa au umri mdogo,
kwani kuna wazazi wanawazoesha watoto wao wakiwa bado wanafunzi.
Waafrika wanaamini katika nguvu hai, hili ni wazo jingine la Tempels
kwani anasema kwamba waafrika wanaamini sana katika nguvu hai na
wanaamini kwamba chanzo kikuu cha nguvu hai ni Mungu mwenyewe, nguvu hii
hupitia kwa wahenga nao hupeleka kwa mizimu ambao hupeleka kwa binadamu
na binadamu hupeleka kwa wanyama na mimea. Tempels anasema waafrika
wanaamini nguvu ya waganga na hivyo mganga ana uwezo mkubwa wa kupunguza
au wakuongeza nguvu hai kwa binadamu. Tempels anajiuliza maswali kadhaa
kuhusiana na suala la waganga mfano, Dawa zawezaje kuponya?, Dawa
inawezaje kuua mtu aliye mbali?, ni vipi mtu aliyekufa anaweza kuzaliwa
upya?,na anasema kitendo cha kupungukiwa nguvu huitwa “Kufwa” na
“Kufudwilika” katika ukurasa wa 22. Hivyo Tempels anasema kuwa majibu ya
maswali yote matatu, ili uweze kujibu maswali hayo ni lazima uwe
mshirika wa mambo hayo. Dhana hii inajitokeza katika riwaya ya “Mirathi
ya Hatari” mfano baada ya kufa Mzee Kazembe mke wake Nyamidze alikwenda
kwa mganga kuthibitisha nini hasa chanzo cha kifo hicho uk.37.
“Mwanangu leo asubuhi nilikwenda kwa mama Tamwene kuulizia kifo cha baba
yako. Mganga anasema kuwa kifo chake kimetokea si kwa mapenzi ya Mungu
ila kwa michezo ya binadamu wafaidio kuwaona watu wakifa” Mama Gusto
alimwambia mwanawe Gusto. Pia Malipula alitaka ampeleke Gusto kwa
Chikanga (Mganga) ili kubaini kama amehusika na mauaji ya Kapedzile
katika uk.60.
Jambo hili katika jamii ya sasa bado linaendelea,
kwani Watanzania wengi huenda kwa waganga ili kukamilisha mambo yao,
mfano kwenye masuala ya siasa, elimu, biashara, kilimo, mauaji ya
albino, upigaji wa nondo, uchunaji wa ngozi yote haya yanahusishwa na
waganga. Falsafa hii ina nafasi katika jamii kwani inaendeleza uhai pale
mwanadamu anapojihangaisha na kutafuta tiba ya maradhi yake na hatimae
anaweza kupona na kuendelea kuishi. Pia imani hii ya ya nguvu hai
inaweza kupelekea migogoro katika jamii hasa waganga wa jadi
wanaposhirikishwa katika kuongeza nguvu hata pamoja na kupiga ramli
huzusha mgogoro katika jamii.
Dhana ya uduara, katika wazo hili
Tempels anasema kuwa waafrika hupenda vitu vya umbo la uduara kwani
wanaamini kuwa hivyo ndivyo vitu vizuri. Mfano katika riwaya ya “Mirathi
ya Hatari” dhana hii inaonekana sehemu nyingi. Mfano, pale Gusto
alipoingizwa kwenye pango na kukalishwa katika kigoda chenye umbo la
duara katika ukurasa wa 33. Pia Gusto anapomsifia Dina kuwa ana uso wa
mviringo katika ukurasa wa 30. Vile vile Mavengi anapoupitisha mgwisho
wake na kuwazungushia Dina na Gusto katika umbo la duara uk.73. Hata
meza ya Gusto ilikuwa ni ya mviringo.
Dhana hii inajitokeza
katika jamii ya leo mfano nyumba za msonge katika kanda ya ziwa, Mikao
ya kula huwa katika duara pia vyombo vingi huwa na umbo la duara kama
sufuria ,Vyungu, Vinu, Nyungo za kupepetea na Ngoma. Falsafa ya uduara
ina nafasi katika jamii kwani hudumisha na kuendeleza utamaduni wa
mwafrika, kwani tangu zamani inaaminika kuwa kila kitu chenye uduara ni
kizuri, pia kuna jamii nyingine zinazoendeleza kujenga nyumba za msonge.
Hasara ya falsafa hii hushirikisha imani hii ya uduara kama ndiyo kitu
pekee kizuri, kwani kuna vitu vingine ambavyo si duara na ni vizuri.
Kwa ujumla Placide Tempels ametoa mchango mkubwa sana juu ya falsafa ya
kiafrika, ambaye anakubali kabisa kuwa waafrika wana falsafa yao.
Mawazo yake yanapelekea kuibuka kwa wanafalsafa wengine wanaoizungumzia
falsafa ya kiafrika kama vile Kwame Nkurumah, J. K. Nyerere, Kenneth
Kaunda. Hivyo basi mawazo yake yana uhalisia pia yana umuhimu katika
jamii ya kiafrika. jiunge na MASSHELE BLOG _0766605392