Saturday

SIMBA HAWAJUI WALIPO , WALIPOTOKA ,NAWANAPOKWENDA : KOCHA, KAMATI YAUSAJILI ITAZIDI KUWAANGUSHA

0 comments


Na Baraka Mbolembole
WAKATI wa usajili wa dirisha kubwa katikati ya mwaka huu nilikosoa waziwazi usajili wa klabu ya Simba SC na kusema, saini za Mnyarwanda, Haruna Niyonzima, Aishi Manula, Shomari Kapombe, Erasto Nyoni, Mghana, Nicolas Gyan, Mganda, Emmanuel Okwi. Magolikipa Said Mohamed, Emmanuel Mseja, Yusuph Mlipili hazikuwa sajili zilizotokaoa na mapendekezo ya benchi la ufundi au mapungufu yaliyoonekana katika kikosi ambacho kilimaliza nafasi ya pili kwa mara ya kwanza katika ligi kuu Tanzania baada ya kusubiri kwa misimu minne.
Usajili wa kitaalam ulikuwa
Jamal Mwambeleko, Ally Shomari upande wangu ndiyo usajili ambao ulizingatia mapungufu ambayo kikosi cha Mcameroon, Joseph Omog iliyaonyesha msimu uliopita. Katika beki ya kulia ambako, Mcongoman, Javier Bukungu alikuwa akicheza palionyesha mapungufu hasa pale mchezaji huyo alipokosena kwa sababu za majeraha ama adhabu na aliyekuwa mbabadala wake,Hamad Juma alishindwa kufanya vizuri hivyo ilikuwa ni lazima Simba ifanye usajili wa nyongeza katika nafasi hiyo. Usajili huo haukupaswa kuwa wa Shomari Kapombe ambaye alisajiliwa kwa dau lisilopungua milioni 60 wakati mchezaji huyo hakuwa amecheza michezo walau 20 kwa kipindi cha mwaka mmoja akiwa Azam FC kutokana na matatizo ya majeraha.
Tatizo ni Poppe na kamati yake
Nimekuwa nikimkosoa wazi Zacharia Hans Poppe ambaye kutokana na nafasi yake ya uenyekiti wa kamati ya usajili amekuwa akiitia hasara kubwa klabu hiyo kwa kushinikiza kuachwa na kusajiliwa kwa wachezaji kila wakati wa usajili unapofika.
Poppe hana ufahamu mkubwa kuhusu soka, ndiyo maana katika kipindi cha miaka zaidi ya mitano akiwa katika nafasi hiyo Simba imesajili wachezaji wengi na wagharama kubwa kutoka ndani na nje ya Tanzania lakini wameambulia ‘patupu.’
Mwambeleko alikuwa ingizo bora na zuri katika beki ya kushoto. Huyu alisajiliwa ili kuwa msaidizi wa mchezaji bora wa klabu na ligi kuu msimu uliopita, Mohamed Hussein.
Kwa kuwa walisajili kwa ‘matakwa yao’ Ally, Kapombe, Nyoni na Mwambeleko wote walisajiliwa katika usajili uliopita na wote wanatakiwa kugombea nafasi mbili katika beki za pembeni. Huu ulikuwa ni usajili wa kocha Omog? Kama ni wake anapaswa kufukuzwa lakini kama ulikuwa usajili wa viongozi wanapaswa pia kuwajibika kwa maana tayari katika kundi hili Kapombe hatakiwi na Poppe kwa sababu tangu asajiliwe amekuwa na majeraha yaliyosababisha asicheze mchezo wowote hadi sasa.
Najiuliza, Poppe na kamati yake ya usajili hawakuwa wakifahamu lolote kuhusu majeraha ya Kapombe akiwa Azam FC? Kama walikuwa wakifahamu kwa nini sasa walimsaini kwa dau kubwa na sasa wanataka kuvunja mkataba wake hata miezi 6 haijatimia?
Kwa hakika bora kuwa nafasi ya mwisho kwa sababu unaweza kufanya juhudi na kusogea, lakini kuwa katika mwelekeo usiofahamu unapotoka, ulipo na unapokwenda ni hatari sana kwa maendeleo na hiki ndicho wanakifanya Simba hivi sasa.
Klabu hii licha ya kila mwanzo wa msimu kujinasibu watashinda ubingwa, lakini wamekuwa wakishindwa kutimiza hilo kwa sababu ya uwepo wa watu wenye madaraka mengi na wanaopenda ‘ukubwa wa kimaamuzi.’
Tazama sajili hizi za kulipwa
Sawa, tangu kina Lino Musombo, Kanu, Donald Msoti, Danny Sserunkuma,  Musa Mude, Pierre Kwizera, Simon Sserunkuma, Hamis Kiiza, Brian Majwega, Blagnon, Vicent Angban, Daniel Agyei, Bokungu, Musa Ndusha hadi sasa kina Laudit Mavugo, James Kotei, Method Mwanjale, Juuko Murshid, Niyonzima na wengineo ni dhahiri Simba imefanya usajili usio na faida chini ya kamati ya Poppe.
Hao niliowataja ni baadhi tu ya wachezaji wa kigeni ambao mwenyekiti huyo wa kamati ya ujenzi wa uwanja wa klabu (Bunju Complex) aliufanya kati ya mwaka 2013 hadi sasa. Vipi kuhusu sajili ghali alizowahi kuzifanya kwa wachezaji wa kitanzania?
Anguko zaidi
Wakati ule niliposema Kagera Sugar inapaswa kubaki na ushindi wao vs Simba, watu walipinga sana, lakini ndani ya uwanja kila mmoja aliona Simba ilivyochapwa 2-1. Niliposikia Simba wamekimbilia FIFA kwa madai ya kutotendewa haki kuhusu rufaa yao ya kadi 3 za njano za mlinzi wa Kagera Sugar, Mohamed Fakhi niliwaambia wazi kuwa uongozi wa klabu hiyo unatengeneza imani ya kuwaaminisha wanachama wao kuwa walishindwa kutwaa ubingwa kwa sababu walinyimwa ushindi na TFF, nikawaambia, ‘Barua ile haikuwa na mashiko’ wapo waliopinga, lakini miezi zaidi ya 7 sasa hakuna kitu.
Pia nilisema watafunika ‘kombe mwanaharamu apite’ wakati wa usajili wa Juni-Agosti kwa kuwasaini wachezaji wenye majina makubwa na kuwasahaulisha kuhusu barua yao ya FIFA. Nini kilitokea? Sikuacha, nikawaambia usajili wa Simba haukuwa mapendekezo ya benchi la ufundi, napo hapa wakatokea wapingaji, lakini nini kinaendelea sasa? Jicho langu la tatu huwa linaona mbali zaidi, hasa kimpira.
Sasa linaona anguko lingine la kujitakia kwa maana rundo la wachezaji waliosajiliwa kwa mbwembwe nyingi katika usajili uliopita wanaondoka katika usajili huu wa dirisha dogo ili kupisha ‘thamani mpya’ za wachezaji. Nitawaambia kwanini wanaenda kuanguka wakati ni klabu iliyofanya usajili ghali zaidi msimu huu.
Kuongoza ligi si ‘kitu’ sababu ya kuwaaminisha watu kuwa Simba inakwenda kutwaa ubingwa wao wa kwanza baada ya kupita misimu mitano, ‘la-hasha’ kwani wameshafanya sana hilo, lakini kuna tatizo kubwa ambalo linaweza kumalizika katikati ya mwaka ujao wakati klabu itakapomaliza uchaguzi wake mkuu, ama Poppe ajiuzulu sasa katika nafasi yake.