Monday

TUACHE KUCHEKESHANA KWAKUTUMIA NENO NGOMA, TAMBWE WANGEKUWEPO !!!

0 comments



NA SALEH ALLY
MECHI ya watani wa jadi, Yanga na Simba haijawahi kwenda kimyakimya, yaani baada ya mechi watu wamalize siku hiyohiyo na kuendelea na mengine.

Hata baada ya siku mbili, tatu au nne, bado mjadala huendelea kuwa motomoto kwa kuwa unahusisha furaha na maumivu katika makundi karibu yote ya wadau wa soka.

Waandishi wangependa kuzungumzia mechi hiyo na inakuwa rahisi kupishana kulingana na mtazamo wa kila mtu katika jambo moja au tofauti.

Lakini kwa mashabiki nao, ikiwezekana kwa matakwa binafsi kwa kuwa hapa kunakuwa hakuna tena taaluma, kila mmoja anaweza kueleza kivyake.

Ubaya au raha zaidi, dunia inabadilika kwa kasi na kila mmoja anaweza kuanika anachoamini kulingana na hamu ya moyo wake na baada ya hapo akaeleza kuwa ni mchambuzi.

Uchambuzi wa jambo kama ni wa kitaalamu ni vizuri pia kuangalia miiko badala ya ushabiki kama ambavyo umeona mashabiki wengi wa Simba wameumia kwa kuwa waliingia uwanjani wakiwa na matokeo yao mfukoni.

Ukiachana na hayo, zaidi nilitaka kulenga mjadala ambao kwangu niliuona unazungumzwa lakini wengi wanaojadili hawakuwa wameangalia jambo la msingi na vizuri kujifunza kupitia kilichotokea kabla hakijayayuka.

Baada ya sare ya watani Yanga na Simba ambao wamemaliza kwa sare ya bao 1-1, wengi wamekuwa wakisema Yanga imetoka sare huku ikiwa na wachezaji wake watatu nyota nje na kama wangekuwepo, ingekuwa ni wakati mgumu kwa Simba.

Kwamba Yanga ilikuwa inawakosa kiungo Thabani Kamusoko na mshambuliaji Donaldo Ngoma raia wa Zambabwe, lakini pia Amissi Tambwe kutoka Burundi. Wengi wanaamini wangekuwepo, ingekuwa ni hatari zaidi.

Ukisikiliza maneno ya mashabiki wengi wakiwemo wale niliowasiliana nao kupitia mtandao niliona hawakuwa wanaelewa hili na huenda walilizungumza kishabiki sana, kuwasaidia linapaswa kuwa jukumu langu kama sehemu ya wadau.

Nianze na Kamusoko, huenda huyu ungeweza kumuita pengo katika mechi lakini bado si kubwa sana kwa kuwa Yanga imeshinda mechi mbili za Kanda ya Ziwa kwa kuichapa Kagera Sugar kwa mabao 2-1 na baadaye Stand United kwa mabao 4-0 bila ya kuwa na Kamusoko.

Kama unakumbuka katika mechi dhidi ya Mtibwa Sugar kabla ya Yanga kwenda Kanda ya Ziwa, matokeo yalikuwa 0-0 na Kamusoko alikuwemo. Mechi mbili, pointi sita na mabao sita, hakuwemo. Unawezaje kusema angekuwemo dhidi ya Simba ingekuwa hatari zaidi?

Hii inakwenda moja kwa moja kwa Donald Ngoma, naye hakuwemo katika mechi hizo, Yanga ikafunga mabao sita na pointi sita. Vipi ionekane angekuwemo dhidi ya Simba ingekuwa hatari zaidi.

Huenda inaweza kuchekesha zaidi kama Yanga wangesema wanamtegemea zaidi Tambwe kuliko Chirwa ambaye katika mechi tatu sasa mfululizo amefunga mabao matatu akiwa anafunga kila mechi. Alianza dhidi ya Kagera, akafuatia dhidi ya Stand na juzi dhidi ya Simba. Hapa Tambwe na Chirwa nani ni mchezaji wa kutegemewa Yanga kwa sasa?

Kama Ngoma unasema wa kutegemewa, unaweza kumuweka Ajibu nje katika namba 10 kwa sasa kwa kuwa katika mechi tatu amefunga mabao matatu pia, akifunga moja dhidi ya Kagera na mawili dhidi ya Stand, lakini akianzisha kutengeneza bao dhidi ya Simba?

Kuna haja ya kujifunza kwamba, mchezaji tegemeo katika kikosi ni yule aliye fiti. Anayekuwa majeruhi hawezi kuwa tegemeo katika kikosi na kama ni hivyo itakuwa ni kichekesho. 

Hata kwa mashabiki wa Yanga wanaoamini wangekuwa na Tambwe au Ngoma ndiyo wangeshinda wakati wamewahi kuwa nao dhidi ya Simba na hawakushinda.


Vizuri kuwategemea walio fiti na kuamini mchango wao. Epuka kuwakatisha tamaa kwa kuonyesha wao si tegemeo na wangekuwepo wengine wangekuwa zaidi wakati Yanga iliingia uwanjani ikiwategemea wao.