Friday

Marekani yaichokoza tena Korea Kaskazini, yafyatua kombora jipya

0 comments
Katika wakati huu ambapo hali si hali huko Korea, dola la kibeberu la Marekani limefanya uchokozi mpya kwa kufanyia majaribio kombora lake la "Minuteman III" lenye uwezo wa kupiga umbali wa karibu kilomita elfu sita na 760. Hatua hiyo ya Marekani imechukuliwa huku dunia ikiwa bado haijasahau makelele mengi yaliyopigwa kufuatia Korea Kaskazini kufanyia majaribio kombora lake jipya la balestiki.
Jeshi la Anga la Marekani limetangaza kuwa, kombora hilo limefanyiwa majaribio bila ya kuwa na silaha zinazoambatanishwa nalo. Majaribio hayo yamefanyika katika kituo cha jeshi la anga cha Vandenberg, California, na baada ya kuvuka masafa ya meli elfu nne na 200 takriban kilomita elfu 6 na 760, limepiga shabaha iliyokusudiwa.
Wiki iliyopita pia jeshi la Marekani lilifanyia majaribio kombora kama hilo yaani tarehe 26 mwezi uliopita wa Aprili na duru za kijeshi za nchi hiyo zikadai kuwa lilipiga shabaha iliyokusudiwa.
Kombora la "Minuteman III" la Marekani

Katikati ya mwezi Aprili pia, Jeshi la Anga la Marekani lilifanya majaribio mengine ya anga katika jangwa la Nevada na kudai kuwa lengo la majaribio hayo ni kufanyia majaribio uwezo wa ndege zake za F-16 wa kubeba na kufyatua mabomu aina ya B-61.
Si hayo tu, lakini pia juzi Jumanne ndege za kivita za Marekani zilipaa kwa ajili ya kushiriki kwenye mazoezi ya anga yaliyozishirikisha pia Korea Kusini na Japan.
Uchokozi wa namna hii unaipa kisingizio Korea Kaskazini cha kujiimarisha kijeshi na kufanyia majaribio silaha zake zikiwemo za nyuklia.
Cha kushangaza ni kuwa, Marekani inafanya kwa uhuru majaribio ya makombora yake na silaha zake nyingine nzito na za maangamizi, lakini huwa inalalamika mno inapoona nchi nyingine nazo zinafanyia majaribio silaha zao za kujilinda na ubeberu wake.

No comments:

Post a Comment