Sunday

MAREKANI KUISAIDIA UKRAINE NDEGE ZA KIVITA

0 comments

 

Marekani imesema itawaruhusu washirika wake wa Magharibi kuipatia Ukraine ndege za kivita za hali ya juu, zikiwemo za F-16 zilizotengenezwa Marekani, katika kuimarisha zaidi Kyiv.

Mshauri wa Usalama wa Kitaifa Jake Sullivan alisema Rais Joe Biden “aliwajulisha wenzake wa G7” juu ya uamuzi huo katika mkutano wa kilele wa umoja huo huko Japan siku ya Ijumaa.

Wanajeshi wa Marekani pia watawapa mafunzo marubani wa Ukraine kutumia ndege hizo, Bw Sullivan alisema.

Ukraine kwa muda mrefu imekuwa ikitafuta ndege za teknolojia ya juu na Rais Volodymyr Zelensky alipongeza hatua hiyo kama “uamuzi wa kihistoria”.

Marekani inapaswa kuidhinisha kisheria uuzaji upya wa vifaa vilivyonunuliwa na washirika na hatua hiyo itasafisha njia kwa mataifa mengine kutuma hifadhi zao zilizopo za F-16 kwa Ukraine.

“Katika kipindi cha miezi michache iliyopita, sisi na washirika wetu tumezingatia sana kuipa Ukraine silaha zenye kutumia mifumo na mafunzo inayohitaji kufanya operesheni za kushambulia msimu huu,” Bw Sullivan aliwaambia waandishi wa habari huko Hiroshima. “Tumetimiza kile tulichoahidi.”

“Sasa tumegeukia mijadala kuhusu kuboresha jeshi la anga la Ukraine kama sehemu ya dhamira yetu ya muda mrefu ya kujilinda kwa Ukraine. Mafunzo yanapoendelea katika miezi ijayo, tutashirikiana na washirika wetu kubainisha ni lini ndege zitawasilishwa, ” nani ataziwasilisha, na zitakuwa ngapi.”

Ukraine imerudia mara kadhaa kushawishi washirika wake wa Magharibi kutoa ndege za kusaidia katika mapambano yake dhidi ya Urusi.

Kabla ya tangazo rasmi la Jumamosi, Rais Zelensky alisema ndege hizo “zitaboresha sana jeshi letu angani”, akiongeza kwamba anatazamia “kujadili utekelezaji wa vitendo” wa mpango huo kwenye mkutano wa kilele wa G7 huko Hiroshima, ambapo atakapowasili Jumapili.

Marekani ilikuwa na shaka kuhusu kuipatia Ukraine ndege za kisasa za kivita – angalau katika muda mfupi ujao.

Mtazamo wake badala yake umekuwa katika kutoa msaada wa kijeshi kwenye ardhi.

No comments:

Post a Comment