Monday

PROFESA MKENDA- TUUNGE MKONO JITIHADA ZA WAANDISHI WETU WA VITABU KWA KUVINUNUA

0 comments

 


Kama alivyowahi kusema mwandishi nguli wa Afrika Mashariki, hayati Sheikh Shaaban Robert, “Mwandishi si mtu wa ajabu awezaye kuishi kwa kula hewa na kunywa ukungu. Ni mtu wa desturi ambaye, kama watu wengine wa desturi, hafarijiwi na hasara.”


Kwa muktada huo Serikali leo imesema ni wajibu wake kuwaenzi waandishi wake nchini kwa jitihada za dhati wanazofanya zinazoleta manufaa chanya kwa Taifa sambamba na kuthamini vitabu wanavyoandika kwa kuwaunga mkono katika kununua na kusoma kazi zao. 


Hayo yamebainishwa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda aliposhiriki mkusanyiko wa Elite Mjue Mtunzi lililofanyika mwishoni mwa juma ambapo sambamba na kushiriki jumuiko hilo alikabidhi Ngao ya Mtunzi ikiwa ni heshima na kutambua kazi za waandishi.


Waziri ameongeza kuwa  katika kutambua umuhimu wa waandishi wa vitabu nchini kwa mwaka huu wa fedha 2022/2023, Serikali imeunda timu inayoongozwa na Profesa Penina Mlama, ambayo itakuwa na jukumu la kuishauri Wizara namna bora ya kuendeleza waandishi wa vitabu nchini.


Waziri Mkenda amesema kuwa kwa mwaka wa fedha 2022/23 Serikali itaanza kutoa tuzo kwa waandishi bora wa vitabu kwa matumizi ya shule kwa lengo la kutoa hamasa kwa waandishi wa vitabu nchini ili kuongeza upatikanaji wa vitabu kwa ajili ya ufundishaji na ujifunzaji sambamba na kuikuza lugha ya Kiswahili.


Waziri Mkenda ametoa rai kwa waandishi kupitia umoja wa UWARIDI kupeleka mezani mapendekezo na ushauri wa namna gani bora ya kufanikisha zaidi uandishi wa vitabu kwa manufaa siyo tu ya waandishi, bali pia, taifa kwa ujumla.


“Tukiwa na machapisho mengi na mazuri, tutaweza pia kuendeleza tabia ya watu kupenda kusoma vitabu nchini.” amesema Prof. Adolf Mkenda



No comments:

Post a Comment