Friday

FUMANIZI

0 comments

 



*FUMANIZI* (Sehemu ya III)

*©Mwafrika Merinyo*


Fatima hakuelewa chanzo cha maradhi haya yaliyomsibu Himid na hakutaka hata kujua. Alishamuuliza mumewe kama amewaona matabibu na jibu la mumewe likawa kwamba wataalam wamemweleza kuwa hana tatizo, ni hali ya kupita tu. Na sasa Fatima hakujali kuhusu hali ya Himid, kwani alikwishaona kuwa hapa ndoa haiwezi kuwepo. Alishawasiliana na bi mkubwa Salama, mke wa kwanza wa Himid, kuulizia kuhusu shida hii ya mume wao. Naye Salama akakiri kuwa kuna tatizo, ila kwa mawazo ya bi Salama Himid haelekei kujishughulisha na tiba yoyote.

Mwaka wa pili baada ya mchezo wa vidole kuanza, Fatima alichoka, akihisi kuwa anajitesa bila sababu. Kuomba talaka akahofia kuwa angeonekana mkorofi, kwa kuwa wenzake wawili walikuwa wanaendelea kuvumilia. Lakini kwa umri wake wa miaka arobaini na uzao wa mtoto mmoja tu, akajihisi mhitaji sana na asiye na msaada. Katika hali ile, na katika kuwa na maelewano ya kirafiki kati yake na Rama, mmoja wa wateja wake wa biashara ya samaki, akaanguka katika mtego wa kunusuru uhitaji wake kiwiziwizi.

Himid aliendelea kujishughulisha, bila kujua kuwa aliokuwa akiwaamsha walishapewa shughuli ya kutosha na hawakuwa na ari ya kuamka kutoka mapumzikoni kwa wakati ule. Fatima naye aliigiza kuhangaika kana kwamba shughuli ile ilimwamsha hisia, lakini hakika moyoni alijawa na kero na hata hasira kwa mambo yale aliyokuwa akifanyiwa na mumewe. Wazo la kudai talaka likamjia tena kichwani. Adai talaka, asidai? Avumilie kero na kula vya wizi pembeni kwa wasiwasi? Nani, zaidi ya wake wenzie, ajuaye adha aipitiayo? Au na wao wanajinusuru kivyao huku wakitunza picha ya ndoa  isiyokuwepo?

Maswali mengi yalimpitia kichwani Fatima ilihali akiigiza kuhangaika pale kitandani. Picha ya Ramadhani Ukeke au kwa jinale fupi Rama ikaja tena kichwani. Akaanza kukumbuka mambo yake. Shughuli yake ya kiume, si shughuli ya vidole. Hata Himid alivyokuwa yu mzima bado hakuweza kumtimizia Fatima kama alivyotimiza Rama. Lakini Rama naye ana mke, japo kwa madai yake hawako vizuri. Nao wana ugomvi wao, Rama akidai kuwa mkewe ana kisirani na hamtimizii. Fatima hakujua kama ilikuwa kweli au maneno ya kukoleza tu penzi lao, penzi alilojitahidi kumficha mumewe Himid mpaka yalipotukia haya.

Himid alihisi kuwa Fatima kahama, hana hisia tena na shughuli yake ya vidole. Akajipumzikia huku akiwaza. Labda Fatima alishamaliza mambo yake na mgoni mwenzie na alikuwa anazuga tu, aliwaza. Lakini alimkagua hamamuni na kukuta hapakuwa na ishara. Au Fatima kakereka tu na shughuli ya vidole? Himid alianza kuwaza kwa kituo sasa. Alianza kuyatafakari maisha yake ya ndoa, utadhani Fatima kampa fursa ya kutafakari kwa umakini baada ya kadhia ya siku ile.

* * *

Himid alikuwa askari wa Jeshi. Sehemu kubwa ya maisha yake akiishi Chanjali. Akiwa na nafasi nzuri kikazi na hali ya wastani kiuchumi alimuoa Bi Salama Maktum na baadaye Tatiana Haidari katika ndoa ambazo hazikupishana sana muda. Wakeze wawili walikaa nae vizuri, mkewe wa pili akamzalia binti mmoja ilhali Salama akikosa uzazi. Katika ndoa na wakeze wawili wa mwanzo hapakupata kutokea mushkeli wowote kimaelewano.

Baadaye alikwenda kikazi Tulizanafasi, akakutana na Fatima katika mgahawa wa mama yake Fatima, Mwasiti Mangungu katika mgahawa uliokuwa maarufu 'Kwa Bi Siti' ambapo Fatima akimsaidia mamake kazi ya kupika na kuuza chakula. Hii ilikuwa baada ya Fatima kuhitimu elimu ya sekondari muda mrefu bila matarajio ya kuendelea zaidi kielimu wala kupata ajira yoyote. Baadae katika pitapita zake akakutana na Abuu aliyempa mimba ya kushtukiza, akamzaa binti ambaye kwa sehemu kubwa alilelewa na bibi yake, Mwasiti Mangungu almaarufu Bi Siti. Abuu hakuwa na mpango wa kuoa wala kuishi na Fatima.

 Macho yao yalipogongana, Himid na Fatima wakamaizi kuwa pana mwito wa mahaba kati yao. Himid alirusha ndoana, na baada ya kufika kula Kwa Bi Siti mara tatu, chambo kikamnasa Fatima, akimwona Himid kama mtu mstaarabu na mwenye utulivu wa aina fulani. Asiye na makeke. Mama Fatima aliyamaizi mapema, na akamshauri bintiye kuwa ni vema kama amempenda Himid amweleze alete posa. Hakuwa tayari kubeba shughuli ya malezi ya mwana na mjukuu mwingine. Himid hakufanya hiyana, kwani moyo wake ulisharidhia kwa Fatima, tamaa ya kuoa bado ilikuwepo moyoni na nafasi ilikuwepo katika mfumo wake wa maisha na imani yake.

Baada ya ndoa, Himid alimpeleka Fatima kumtambulisha kwa wakeze wawili huko Chanjali na kisha kumrudisha akaishi Tulizanafsi, jambo ambalo Himid aliamini lingepunguza misuguano ambayo ingeweza kutokea kama angewaweka wote watatu pamoja. Maisha yakaenda vema, akihudumia na kuridhisha nyumba zake zote tatu.

Alipata changamoto moja tu kutoka kwa mkewe mpya, Fatima. Bi mdogo hakuisha kulalamika kuwa anaachwa muda mrefu bila kupewa haki yake ya ndoa. Ikabidi Himid ajenge utaratibu wa kuvuka bahari kwenda Tulizanafsi walau mara moja katika wiki mbili; jambo ambalo kiasi liliyanyamazisha malalamiko ya Fatima. Pia mara kwa mara Himid alitumwa kikazi makao makuu ya jeshi kwenye jiji kuu la nchi, Ngomeni, lililokuwa jirani na Tulizanafsi. Akatumia mwanya huo kwenda Tulizanafsi kumtia moyo mkewe kuwa hamtelekezi. Maisha yakaendelea. 

Ikatokea ile siku ya balaa katika maisha ya Himid ambayo hataisahau. Ilikuwa katika sherehe za miaka hamsini ya jeshi, naye Himid akawa katika safu ya watoa huduma kwa wageni waalikwa na maafisa wakuu wa jeshi katika tafrija iliyokuwa ikifanyika kwenye bwalo kuu la maafisa.

Katika kuzunguka ukumbini kuhakikisha usalama upo na mambo yanakwenda vizuri ndipo alipomwona mwanamke aliyemsababisha akakodoa macho kama zuzu aliyeona lori lililosheheni mzigo wa noti mpya.

“Afande unatafuta kufa?” Alimsukuma kwa kiwiko mbavuni Adolf, askari wa cheo cha chini yake lakini waliyezoeana sana. Himid akaruka kama aliyeshtuliwa kutoka ndotoni.

“Nini wewe?” Akahoji Himid.

“Kifaa cha Mkuu wa Majeshi hicho afande, ohoo!” Alicheka Adolf. “Asipokufunga atakuroga Mfipa yule kaka!” Wote wakajikuta wakicheka.

“Aaa, unadhani mtu akishakuwa Mfipa basi ndio atakuwa mchawi? Mnawaonea bure Wafipa bwana.” Alisema Himid, akijaribu kuiondoa taswira ya yule mwanamke kichwani mwake bila kufanikiwa. “E bwana, kwani huyu demu wa wapi?”

“Yuko kitengo cha kilimo Jeshini, ni kepteni yule.” Alitoa taarifa Adolf. “Yuko kwenye ofisi yao hapa Mapambano kambini. Pale unapoona matrekta ukipita barabarani unapoelekea Tulizanafsi.” Sherehe zilikuwa zikifanyika kwenye kambi kuu ya Mapambano jijini Ngomeni. Wakati Adolf akimpa taarifa Himid kuhusu yule askari mwanamke aliyeziteka fahamu zake, Himid alikuwa akisikia nusu ya maelezo ilhali nusu ya fahamu zake ilimfuatilia mwanamke yule ambaye sasa alikuwa ametoka eneo alilokaa akielekea maliwatoni.

Himid alichomoka kama risasi kuelekea eneo la maliwato, akimwacha Adolf ameachama mdomo. Baadae, walipokuwa wamekaa nje ya ukumbi wakiteta, Adolf akawa anamsikiliza Himid, akimshangaa.

“Demu kameza chambo.” Himid alitamba. Tutaonana kabla sijarudi Chanjali." Alizidi kumweleza Adolf kwamba yule kepteni hajaolewa, kwani hiyo ndiyo habari ya kwanza aliyotaka kuipata kutoka kwake alipojitambulisha kule eneo la maliwato. Himid alifanya kijeshi na kidharura alipokutana na kepteni akitoka upande wa wanawake wa maliwato: alijitambulisha na kumweleza kwamba angependa waonane nje ya pale, akamuuliza jina na kutaka kujua kama ameolewa. Akajibiwa maswali yake na kujibu kuwa yuko radhi kuonana nae Himid atakapohitaji. 

Yakachipuka mahaba kati ya Himid na Paulina, askari wa kike aliyefahamika kuwa hawara wa Mkuu wa Majeshi, Jenerali Nguvu Kayanza. Waashiki wale wawili wakaashikizana huria, tena maashikiano ya hatari, bila kujali habari za hatari zilizovuma kuhusu Jenerali Kayanza. Mkuu wa Majeshi yule alihofiwa na takriban jeshi zima kwa cheo chake na ukali aliojivika kama taji. Iliaminiwa pia kwamba cheo chake hakikupatikana hivihivi, bali alirudi kwao Ufipa alipojua kwamba jenerali mwingine alikuwa akitajwatajwa kupewa cheo hicho baada ya mkuu aliyetangulia kustaafu kwa mujibu wa sheria. Wenye umbea wao wakadai kuwa huko kwao Jenerali Nguvu Kayanza akatengeneza mambo na kuivuta nyota ile kumwangazia yeye. Hivyo hapana yeyote aliyethubutu kukatiza mbele ya Kayanza kwa jambo lolote, sembuse kumchukulia mwanamke wake!

Mahaba yakamzoa Himid mzimamzima, asisikie la mwadhini wala mnadi swala, akala asali mzingani kwa Jenerali kama vile yuko shambani mwake. Rafiki yake Adolf alimuonya mara kadhaa, lakini Himid akaziba masikio kwa nta iliyobakia mzingani kila alipopakua asali.

“Naona wataka kuingia katika orodha afande!” Sauti ya luteni Adolf limshtua meja Himid. Walikuwa wamekaa katika mgahawa wa Strikers maeneo ya Uswazini jijini Ngomeni. Hapa ndipo walipozoea kuweka ‘RV’ au makutano Himid na kepteni Paulina kabla ya kuingia ‘chimbo’ kama walivyoita nyumba ya wageni. Siku hii Himid alikutana na Adolf kwa mazungumzo pale Strikers wakati Himid akimsubiri mpenzi wake Paulina.

-ITAENDELEA-

No comments:

Post a Comment