Tuesday

Serikali ya Tanzania yashusha tozo za miamala ya fedha kwa simu kwa asilimi 30

0 comments


Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Lameck Nchemba akisaini  marekebisho ya Kanuni za Tozo za Miamala ya Kielektroniki za Kutuma na Kutoa Fedha kwa Mwaka 2021, marekebisho hayo yamepunguza viwango vya tozo za miamala hiyo kwa asilimia 30, jijini Dodoma. Picha| Wizara ya Fedha na Mipango.

Watoa huduma nao wamekubali kushusha tozo wanazotoza baina ya mtandao na mtandao kwa kwa asilimia 10.Viwango vipya kutolewa Septemba Mosi, 2021.


Dar es Salaam. Huenda Watanzania watapata ahueni baada ya Serikali kufanya mabadiliko katika tozo za miamala ya fedha inayofanyika kwa njia ya simu na kupunguza kwa asilimia 30.
Viwango hivyo vimepungua baada ya Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba leo Agosti 31, 2021, ametia saini marekebisho ya Kanuni za Tozo za Miamala ya Kieletroniki za Kutuma na Kutoa Fedha za Mwaka 2021.
Msemaji wa Wizara ya Fedha na Mipango, Benny Mwaipaja amesema pia Serikali imefanya majadiliano na watoa huduma za simu ambao nao wameridhia kupunguza viwango vya tozo wanazotoza katika miamala ya kutuma na kutoa fedha kati ya mtandao na mtandao mwingine kwa asilimia 10.
“Viwango vilivyopunguzwa vitatangazwa rasmi kwa tangazo la Serikali kesho Septemba 1, 2021,” amesema Mwaipaja katika taarifa yake.
Mwaipaja amesema Serikali inaamini kuwa uamuzi huo utatoa nafuu kwa wananchi na kuiwezesha Serikali kupata fedha za kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kama ilivyokusudiwa wakati tozo hizo ziliporidhiwa na kupitishwa na Bunge la Bajeti la mwaka 2021/22.
Mabadiliko hayo yamefanyika ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Rais Samia Suluhu Hassan la  Julai 19, 2021 kwa Dk  Nchemba na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dk Faustine Ndugulile kupitia upya tozo hizo kutokana kusikia kilio cha wananchi kuhusu suala hilo.
Tangu Julai 15, kumekuwepo na malalamiko lukuki kwa watumiaji wa huduma za simu Tanzania baada ya Serikali kuanza kutoza tozo mpya kwenye miamala ya simu ambazo wengi wamesema zinawaumiza kwa kuongeza gharama za maisha. 
Fedha zinazokatwa kwenye miamala hiyo zimepangwa kutumika katika shughuli za maendeleo ikiwemo kujenga barabara za vijijini na kuendeleza miradi ya maji kwa ajili ya wananchi.
Kiasi cha Sh48.4 bilioni 48.4 zilizokusanywa hivi karibuni zimeelekezwa katika kujenga vituo vya afya 150 na ukamilishaji wa vyumba vya madarasa 560 nchi nzima.

Katika kipindi cha wiki nne tangu tozo mpya za miamala ya simu zianze kutumika, Serikali ilifanikiwa kukusanya Sh48.5 bilioni ambazo zimepelekwa kuboresha miundombinu ya kijamii ikiwemo ujenzi wa vituo vya afya.

No comments:

Post a Comment