Saturday

Gwajima: Tusisubiri Tuokote Maiti Mitaani

0 comments


WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Dorothy Gwajima anasema kuwa, ugonjwa wa Corona unaendelea kusambaa kwa kasi nchini Tanzania, akiwataka wananchi kuchukua tahadhari badala ya kusubiri waone nchi inafikia hatua mbaya ya kuokota maiti mitaani.

 

Waziri Gwajima anasema, licha ya ugonjwa huo kudhibitiwa, wagonjwa wameendelea kujitokeza na kulazwa hospitalini.

“Kazi inayofanyika ni kufanya hali isiwe mbaya, Serikali inajitahidi na Mheshimiwa Rais (Samia Suluhu Hassan) amekuwa akikumbusha; ‘jamani ndugu zangu tuchukue tahadhari’ ili hali hii tunayodhani ipo hivi kwa sababu inashikiliwa kwa juhudi mbalimbali za kinga isije ikapitiliza,” anasema Gwajima.

 

Waziri huyo anasisitiza kuwa, wagonjwa wa corona wapo na wanaendelea kujitokeza na hiyo inamaanisha kwamba maambukizi yapo na siyo ya uongo.

 

“Ni nguvu kubwa sana inafanyika na watumishi wetu walio mstari wa mbele kuhakikisha hicho watu wanachokisubiri kitokee katika ngazi ile, kisitokee.

 

“Tunapotoa elimu tunamaanisha  kurahisisha mapambano kwa ushirikiano na nchi kwa kuchukua tahadhari,”ameongeza.

 

Anasema licha ya kutoa elimu hiyo, baadhi ya wananchi wanaitikia na wengine hawafanyi hivyo na kuwataka wafanye hivyo ili Serikali iongeze wigo ili nchi iwe salama.

 

“Kwenye msongamano wapo wanaovaa barakoa na wengine hawavai, lakini wewe uliyepona, huumwi, umebeba kimelea na unakisambaza, waokoe basi wengine.

 

“Kuna wazee, wapo wanaoumwa magonjwa mbalimbali, tunawaokoaje? Wengi tukivaa barakoa, tutaokoa wengine,”

Aidha amesema kuwa, katika kueneza elimu, wanawatumia waganga wa mikoa na halmashauri na wakuu wa wilaya na mikoa husika “Tuna tiba asili ambazo hatujazitupa, zilisaidia wengi awali na sasa zinasaidia wengi, watu watumie, wale vyakula ambavyo ni vya asili ili kuongeza kinga.

“Idadi ya wagonjwa kwa sasa siwezi kueleza kwa sababu inabadilika, wanaweza wakawa mia (100) na wakashuka wakawa 50 au wamepanda mpaka 80, kwa hiyo siwezi kusema kwa sasa kwa sababu sijaichukua, lakini itoshe kusema wagonjwa wapo,” anamalizia kusema Dkt. Gwajima

No comments:

Post a Comment