
Waziri Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa amewaagiza Wakurugenzi wa Halmsahauri zote nchini kuhakikisha wanapanga bajeti ya kufanyia matengenezo magari ya Halmashauri ili yaweze kudumu kwa muda mrefu
Akizungumza na Maafisa Elimu wa Halmashauri ya zote 184 Nchini wakati wa Uzinduzi wa zoezi la ugawaji wa Magari kwa maafisa hao yaliyonunuliwa kupitia mradi wa lipa kulingana na matokeo mapema leo katika Viwanja vya Shule ya Sekondari ya Kibasila Mkoani Dar-es-salaam amesema
‘Kuna baadhi ya Halmashauri hazitengi bajeti kwa ajili ya matengenezo ya magari yao , na kusababisha magari hayo kuharibika mapema na kuwekwa Gereji bila matengenezo ya Halmashauri zao
“Maafisa elimu wa Wilaya Mkikabidhiwa magari haya leo na tukalikuta gari limekaa na halifanyi kazi kwa kukosa matengenezo lazima Wakurugenzi wa Halmashauri watawajibishwa “ amesisitiza Majaliwa
Amesema kila Halmashauri lazima iweke mpango wa matengenezo wa magari hayo ili ziweze kufanyakazi kwa muda mrefu na kuweza kufamnya kazi iliyopangiwa ya kuhakikisha inafanya ufutiliaji wa elimu katika shule za msingi nchini.
Amefafanua kuwa magari hayo yatumike kwa ajili ya ufuatiliaji wa miradi ya ujenzi wa miundombinu ya elimu katika Halmashauri na kuhakikisha yanafuatilia ufundishaji na ujifunzaji wa elimu katika Wilaya ili malengo yaweze kufikika na kukamilika kwa wakati
Amewaagiza Wakuu wa Mikoa na Wilaya kuwachukulia hatua maafisa Elimu wote ambao watayatumia magari hayo kinyume na kazi iliyopangiwa ya ufuatiliaji wa masuala ya Elimu katika Halmashauri kwa kuwa watakuwa wameenda kinyume na matakwa ya Serikali
Hata hivyo, amewaagiza maafisa elimu wote nchini kuhakikisha wanafanyakazi kwa weledi kwa kuwa ndio msingi wa mafanikio katika maeneo yao kwa kuwa kiwango cha mafanikio ya elimu kilichofikiwa bado kinahitaji nguvu zaidi ili tuweze kufik mbali zaidi.
‘Tunatambua changamoto zinazoendelea katika Halmashauri zenu na Serikali inatambua umuhimu wa elimu niwatake muendelee kufanyakazi kwa weledi na uaminifu ili kuongeza ufaulu na Serikali itaendele kutatua changamoto zenu’amesisistiza Majaliwa
Amewataka kuhakikisha wanawatia moyo waalimu katika kutekeleza majukumu yao , watembeleeni, wasikilizeni na wahudumieni kwa kufuata sheria na taratibu za utumishi wa umma na imarisheni mahusiano katika utendaji kazi wa kila siku ili kufikia malengo yaliyowekwa na Serikali ya kuongezaufaulu kwa wanafunzi.
Aidha ametaka Maafisa Elimu Nchini kuwatumia Madiwani katika kutoa elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa elimu kwa watoto na kuhakkisha wazazi wanawajibika katika suala zima la kutimiza majukumu yake katika kuhakikisha watoto wanapata elimu bora
Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Ummy Mwalimu amesema magari hayo yamenunuliwa na Serikali kupitia Programu ya Lipa Kulingana na Matokeo kwa gharama ya shilingi bilioni 16.4.