Tuesday

Vigogo 10 Wafyekwa, Siku 17 Za Rais Samia

0 comments

 


 


SIKU 17 za Rais Samia Suluhu madarakani, zimefyeka vigogo 10 kutoka Taasisi  na Idara za serikali.


Ikiwa ni mwendelezo wa kuunda safu yake ya uongozi katika uteuzi alioufanya jana Jumapili Aprili 4,  2021, amefyeka vigogo tisa huku wengine wakibadilishwa maeneo ya kazi.


Awali siku saba zilizopita alitangaza kumsimamisha Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA), Deusdedit Kakoko, na kumteua Erick Benedict Hamis kuongoza mamlaka hiyo.


Hadi anasimamishwa, Kakoko alikuwa ameongoza mamlaka hiyo kwa miaka minne na miezi tisa, kuanzia Juni 25, 2016  hadi Machi 28 i 2021, Rais Samia alipomsimamisha ili kupisha uchunguzi wa tuhuma mbalimbali zinazoikabili mamlaka hiyo ikiwemo ubadhilifu wa fedha zaidi ya Sh bilioni tatu.


Miongoni mwa vigogo waliofyekwa na panga la Rais Samia, ni pamoja na William Erio ambaye alikuwa Mkurugenzi Mkuu wa  Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), na nafasi yake kuchukuliwa na  Masha John Mshomba.


Erio alianza kuongoza taasisi hiyo 14 Julai 14, 2018, akichukua nafasi ya Profesa Godius Kahyarara ambaye uteuzi wake ulitenguliwa na Hayati Magufuli.


Kabla ya uteuzi huo, Erio alikuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Pensheni (PPF).


Mwingine ni Dk. Edwin Mhede ambaye alikuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), ambapo nafasi yake imechukuliwa na Alphayo Kidata.


Dk Mhede aliongoza mamlaka hiyo kwa mwaka mmoja na miezi tisa, kuanzia Juni 8, 2019, akichukua nafasi ya Charles Kichere, ambaye aliteuliwa kuwa Katibu Tawala, Mkoa wa Njombe na baadaye Mkaguzi Mkuu na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).


Kabla ya uteuzi huo, Dk Mhede alikuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara.


James Kaji aliyekuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya, ametupwa nje na nafasi yake ikichukuliwa na Gerald Kusaya. Kabla ya uteuzi huo, Kusaya alikuwa Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo.


Kaji alianza kwa kukaimu nafasi hiyo, baada ya aliyekuwa bosi wa mamlaka hiyo, Rogers Sianga kustaafu mwaka 2019. Hayati Rais John Magufuli alimthibitisha kuwa Kamishna kuanzia Julai 6, 2020.


Mwingine aliyewekwa kando ni James Kilaba, aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), nafasi yake ameteuliwa Dk Jabir Bakari Kuwe. Kabla ya uteuzi huo, Dk Kuwe alikuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao.


Mwingine aliyefekwa ni Emmanuel Ndomba, aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Shirika la  Meli Tanzania (TASAC), ambapo nafasi yake ameteuliwa Abdi Mkeyenge.  Ndomba aliteuliwa na Hayati Magufuli kuwa mkurugenzi mkuu Aprili 23, 2019.


Dk Mabula Mchembe ambaye alikuwa Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto amewekwa pembeni na nafasi yake kuchukuliwa na  Dk Abel Makubi. Dk Mchembe  aliapishwa kuwa Katibu Mkuu Aprili 22, 2020.


Mwingine aliyewekwa kando ni aliyekuwa Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Elius Mwakalinga na nafasi yake imechukuliwa na Joseph Malongo.

Aloyce Nzuki aliyekuwa Katibu Mkuu Wizara ya Mali Asili na Utalii, nafasi yake imechukuliwa na Ludovick Nduhiye.


Joseph Nyamhanga aliyekuwa Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali amefyekwa na nafasi yake kuchukuliwa na Profesa Riziki Shemdoe


No comments:

Post a Comment