SURA YA KWANZA
UANDISHI
1.0 Uandishi maana yake nini?
Uandishi ni uwakilishaji wa lugha kwa njia ya
maandishi kwa kutumia ishara na alama - yaani
mfumo wa uandishi wa lugha husika. Lugha kwa
mujibu wa Kamusi ya Kiswahili Sanifu ni “mpangilio
wa sauti na maneno unaoleta maana ambao
hutumiwa na watu wa taifa au kundi fulani kwa ajili
ya kuwasiliana” (KKS: 201). Tafsiri ya lugha na ile
ya uandishi zikiwekwa pamoja, tunaweza kufafanua
kuwa, uandishi ni njia ya mawasiliano ambayo
wanajamii hutumia lugha ili kuwasilisha mawazo
yao kwa njia ya maandishi. Maandishi yanalenga
kumpata msomaji atakayesoma kile kilichoandikwa
na mwandishi; na kinyume chake kuna masimulizi
ambayo yanalenga kumpata msikilizaji. Kwa hiyo,
tuna msomaji kwa upande mmoja na msikilizaji kwa
upande wa pili. Yote hayo yanawezeshwa na
uwepo wa lugha.
Uandishi upo wa aina mbalimbali kama vile:
uandishi wa habari, uandishi wa kiweledi, uandishi
wa kitaaluma, na uandishi wa kubuni
(www.wikipedia.com). Uandishi utakaoelezewa kwa
kina na kwa mapani ni ule wa kubuni-yaani
unaolenga kuwaelimisha watunzi chipukizi wajue
namna ya kutunga kazi za kubuni ambazo ni
riwaya, hadithi fupi, ushairi, tamthiliya, maigizo ya
jukwaani, redioni, televisheni na filamu. Lakini
halitakuwa jambo baya kama tutaangalia aina
zingine za uandishi ili tuwe na mawanda mapana
katika uandishi wa kubuni na usio wa kubuni.
Uandishi wa habari unahusika na uchunguzaji na
utoaji taarifa za matukio, mambo, au mwelekeo wa
jamii kwa hadhira pana. Lengo la uandishi wa
habari ni kuwataarifu wananchi kuhusiana na jambo
husika (Pardue OWL, 1995 -2016). Uandishi wa
habari huhusisha fani nyinginezo kama vile: uhariri,
upigaji picha, na filamu ya makala yaani
inayoonesha hali halisi (dokyumentari).
Kwa mujibu wa Rioba, Kilimwiko, na Karashani
uandishi wa habari unachukuliwa kama taaluma ya
mawasiliano inayojihusisha na ukusanyaji, tathmini,
na usambazaji wa habari au utoaji wa maoni
kuhusiana na jambo livumalo katika jamii.
Wanaendelea kumwelezea mwandishi wa habari
kwamba, ni mtu anayejihusisha na uandaaji wa
maudhui ya vyombo vya habari kama vile
kuzikusanya habari, kuzitathmini, kuzichakata au
kuzisambaza, na kutoa maoni kuhusiana na jambo
lililopo katika jamii (2000:1 Tafsiri yangu).
Uandishi wa kiweledi ni uwanja unaoibukia; ni
uwanja unatumia mikabala ya kitaaluma katika
kutoa mafunzo ya jinsi ya kutumia lugha (ritoriki)
kwa lengo ya kushawishi hadhira-kupitia katika
uandishi. Waandishi wa kiweledi wanaweza
kuajiriwa na kufanya kazi katika kampuni za
uchapishaji, serikalini, wanahabari, maafisa
masoko, wanasheria, walimu, au katika vyombo
vya mawasiliano (Alganquin College, 2016).
Uandishi wa kitaaluma ni ule unaoelezea jambo
kiyakinifu kwa kutumia muhtasari (ikisiri). Uandishi
wa kitaaluma unatumia mtindo ambao ni wa makini
sana, na unalenga kutazama jambo kiyakinifu-ili
kuijulisha hadhira nini kinaendelea kutokana na
uchunguzi; na kujenga hoja na mawazo kuhusiana
na jambo lililochunguzwa. Mathalani, uandishi wa
kitaaluma unakusudia kuziba pengo ambalo
limekuwepo katika taaluma bila kurudia yaliyoonwa
na watafiti wengine. Uandishi huu unapatikana
katika maeneo ya kitaaluma; na unasambaa kwa
hadhira pana kwa kupitia kwa waandishi wa habari,
vitini mbalimbali, hotuba, na majarida (Pardue
OWL, 1995 - 2016).
Uandishi wa kitaaluma unapaswa kuwa na lengo la
utafiti; na umuhimu wa kufanya utafiti huo uelezwe
kinagaubaga na uwasilishwe kwa ufasaha, ili
kumwezesha mtafiti mwingine kuurudia utafiti huo
na kupata matokeo yaleyale ili kujiridhisha (Pardue
OWL, 1995 - 2016).
Uandishi wa kubuni unachukuliwa kuwa ni pamoja
na uandishi wowote ule wa kubuni au usio wa
kubuni ambao sio wa kitaaluma (yaani uandishi
ambao haufuati kaida za kitaaluma); na sio wa
kiweledi (yaani haufuati kaida za kiweledi ambazo
zinalenga kuandika kwa kushawishi wasomaji); na
sio wa kihabari (yaani haufuati kaida za uandishi
wa habari ambazo ni kukusanya taarifa,
kuzitathmini, kuzisambaza, na kutoa maoni).
Uandishi wa kubuni ni ule unaojitokeza katika
riwaya, hadithi fupi, ushairi, tamthiliya, na filamu;
vitu hivi ni miongoni mwa aina mbalimbali za
uandishi wa kubuni.
Paul Engle katika makala yake ya “The Writer on
Writing” anaelezea uandishi wa
kubuni (ashakum si
matusi) kwamba, ni sawa na kufanya mapenzi kwa
kuwa inastaajabisha kuona mtu anapagawa
(1963:3); sawasawa na uandishi wa kubuni
ambapo mtu anapagawa na kujikuta anabuni
matukio na kusimulia hadithi kwa namna akili yake
inavyomtuma. Kwa maneno mengine Engle (1963)
anastaajabu kuhusiana na ubunifu kufundishwa -
kwakuwa yeye anaona ni uwezo alionao mtu ndani
yake ambao unamfanya aandike na kubuni matukio
mbalimbali bila ya kufunzwa.
Kwa mujibu wa Semzaba (1997:75), anasema
“sanaa huanza na hisi ambazo kila mtu anazo”.
Nukuu hiyo ina maana kuwa, ubunifu wowote ule
unatokana na hisi ambazo zinamsukuma mtunzi.
Hisi hizo ni lile wazo linalomsumbua akilini ambalo
anataka aliwasilishe ili hadhira ifahamu kilichopo
moyoni mwa mwandishi. Semzaba anaendelea
kuelezea kuwa, mtunzi huchagua umbo la
kuwasilishia wazo lake kama ni hadithi fupi, riwaya,
tamthiliya, ushairi (kimapokeo au kimasivina). Yote
haya yanategemeana na uchaguzi wa mtunzi.
Mtu mwingine aliyejadili kuhusu uandishi wa kubuni
ni Khamis (1983:246). Yeye anaona kuwa, uandishi
wa kubuni ni namna mtunzi anavyoweza kuyasawiri
maisha ya mwanadamu na kuyatungia taswira
ambazo ziko mbali na mazoea ya mwanadamu;
kwakuwa, ni maisha kulingana na anavyoyaona
mwandishi katika dunia iliyomo kichwani mwake.
Naye Kezilahabi anaelezea kuwa, uandishi wa
kubuni ni sawa na ufuaji chuma; ambapo, mfua
chuma ana uwezo wa kutengeneza umbo lolote
kutokana na chuma hicho. Sawa na mwandishi
kwani yeye hutunza visa vingi kichwani mwake na
anao uwezo wa kuvifua visa hivyo na kutengeneza
kazi mbalimbali zenye kuisaidia jamii kwa njia
mbalimbali kama vile hadithi, michezo ya kuigiza na
kadhalika (Kezilahabi, 1983:237).
Tafsiri zote zilizodondolewa hapo juu, Wikipedia,
Engle, Semzaba, Khamis, na Kezilahabi
hazipishani sana katika kuelezea nini maana ya
uandishi wa kubuni. Kwa maneno mengine,
uandishi wa kubuni unaweza kuelezwa kuwa ni
mchakato ambao unatokana na kipaji au kipawa na
kujipika (kwa kusoma kazi nzuri za wengine), na
kujibidiisha ili uweze kuishi maisha yote kiubunifu -
yaani yaliyopita, yaliopo, na yajayo. Mwandishi wa
kubuni anatakiwa aweze kuchanganya maisha
halisi na ya kubuni ili aweze kutoa kazi bora.
Baada ya kupitia maana za aina mbalimbali za
uandishi, na ili kuweza kwenda sambamba katika
kozi hii ya uandishi-hatuna budi kuelewa mambo ya
msingi yakiwemo: hatua za kuandika insha,
matumizi ya alama za uandishi na uakifishi, na
makosa ya kawaida ya kiuandishi ambayo
yanafanya msomaji ashindwe kuelewa barabara
lengo la mwandishi.
1.2 Hatua za uandishi wa insha na muundo
wake
Uandishi wa kubuni ni aina mojawapo ya uandishi
wa insha. Hivyo, hatuna budi kujifunza namna ya
kuandika insha na miundo ya insha. Baadaye
tutajifunza matumizi sahihi ya alama za uandishi na
uakifishaji; na mwishowe tutaangalia makosa
mbalimbali yanayojitokeza katika uandishi wa
insha.
Katika mchakato wa uandishi, zipo hatua kadhaa
za kuzingatiwa ili insha yako au andiko lako liwe
zuri. Mahenge (2011) anabainisha hatua hizo kama
ifuatavyo:
Kwanza, ni kuchagua mada – hapa unapaswa
ujiulize swali la msingi ambalo ni: je unataka
kuandika juu ya kitu gani? Au jambo gani?
Mathalani, unataka kuandika kuhusu upishi wa
mlenda au mchunga.
Pili, ni kuiwekea mada yako mipaka – hapa inabidi
utambue kuwa mada yako itagusia mambo gani -
labda utataka kuongelea kuhusu mlenda. Je, ni
mlenda upi? Je, utatoa mifano mahsusi au ya jumla
ambayo inapatikana katika sehemu fulani? Labda
ni mazingira yapi utayachukua kama mfano wako –
je ni Kweditilibe, Kwedibangala, Kwamasukuzi, au
Kwedikwazu? Hii ni muhimu kwa sababu huwezi
kuandika katika insha moja kila kitu kilichopo
duniani kinachohusiana na mada yako.
Tatu, ni kuamua lengo la insha – je, lengo
unalolitaka ni lipi? Je unataka kushawishi?
Kuhamasisha? Kueleza na kufafanua? Au
kufundisha? Je, unataka kugusa hisia za wasomaji
wako? Chukulia mfano wa kadi za mialiko na kisha
linganisha na matini za kisayansi au hadithi na
kadhalika. Katika aina hizo za uandishi kunautofauti
wa malengo, na kwa namna hiyo hata uandishi
wake hutofautiana.
Nne, ni kuuamua mpangilio wa insha - je unataka
insha yako iwe na mpangilio gani? Je, unataka
ianzie na chanzo ambacho kitatuwezesha
kufahamu matokeo? Au utaanza na matokeo ya
jambo fulani na kisha ndipo utufahamishe kuhusu
chanzo chake au sababu za utokeaji huo?
Unaweza kufikiria kuhusu riwaya ya Mzimu wa
Watu wa Kale ambayo inaanza na
mwisho na
kurudi mwanzo au riwaya ya Nyota ya Rehema
ambayo inaanza na mwanzo na kuendelea hadi
mwisho. Ni uchaguzi wako kuamua unataka
mpangilio wa kazi yako uweje.
Tano, ni kupanga insha kividokezo - yaani
kubainisha dondoo zitakazogusiwa katika uandishi
wako. Hapa unapanga kwamba, katika utangulizi
utazungumzia nini? Katika kiini utataja hoja au
sababu gani kwa mifano madhubuti; na katika
hitimisho, utatoa maoni gani au utasema nini ili
lengo lako litimie?
Sita, ni kuandika insha kwa umbo lililopendekezwa
na Aristotle – yaani umbo la: mwanzo, kati, na
mwisho kama ulivyo muundo wa tamthiliya ya
Kigiriki. Hii ina maana kwamba, katika sehemu ya
mwanzo - unatambulisha wahusika na mada
pamoja na mahusiano waliyonayo wahusika wako
ili kuweze kujengeka migogoro. Katika sehemu ya
katikati inatakiwa uikuze migogoro iweze kukua na
kubadili mwelekeo wa mchezo. Katika hitimisho
inatakiwa litolewe suluhisho au hitimisho la
mgogoro ambapo kunatakiwa kuwe na mshuko wa
mgogoro. Huu ndio muundo wa tamthiliya au drama
kwa mujibu wa Aristotle.
Saba, ni kupitia insha na kuifanyia marekebisho. Ni
vema kuandika na kuivumbika kazi yako - yaani
kuiweka kama vile umeisahau ili muda upite na
mawazo yako yawe mapya unapoisoma. Vile vile
waweza kumpa mtu mwingine akusomee ili
kusaidia kuona makosa ambayo yatasaidia
kuiboresha kazi yako.
1.3 Matumizi ya alama za uandishi
Alama za uandishi ni alama zinazosaidia katika
mchakato wa kuandika ili uweze kueleweka.
Mathalani, hakuna mtu awezaye kuzungumza kwa
dakika moja nzima bila kuvuta pumzi au kuhema!
Vivyo hivyo kazi ya alama za uandishi ni kuweka
pumziko fupi au pumziko kamili katika insha ili
msomaji aweze kukielewa kile kisemwacho.
Alama za uandishi zipo nyingi kwa kuzitaja ni
pamoja na: kituo (.); koma (,); nukta pacha (:);
swali (?); nukta mkato (;);
mshangao (!); funga
na fungua semi (“
”); mkato wa juu ('); kimstari
au haifa (-); deshi (...); mabano ( ); mabano
ya
pande nne ([ ]); slashi (/).
Ili kujijuvya kuhusiana
na matumizi sahihi ya alama za uandishi na
uakifishi, wanafunzi wanashauriwa wasome vitabu
vifuatavyo: Uandishi wa Kiswahili cha BAKITA,
Utungaji (1) cha Steven Mrikaria, Utungaji
(2)1 cha
John Kiango na Mwenge wa Uandishi cha Wamitila
ambavyo kwa pamoja vinaelimisha juu ya matumizi
sahihi ya alama za uandishi. Vitabu hivi
vinapatikana katika duka la vitabu la TUKI
(TATAKI).
1.4 Uakifishaji
Uakifishi ni matumizi sahihi ya alama za uandishi.
Endapo mwandishi atatumia vibaya alama hizi, basi
atajikuta ameingia katika makosa na kumfanya
asieleweke. Makosa ya uakifishi hutokea kwa
kushindwa kutumia vizuri alama za uakifishi ili
kuonesha uhusiano wa neno na neno katika
sentensi au kati ya sentensi. Kama vile: kushindwa
kutumia kiusahihi kituo (.); koma (,); nukta pacha
(:); swali (?); nukta mkato (;); mshangao (!); funga
na fungua semi (“ ”); mkato wa juu ('); kimstari au
haifa (-); deshi (...); mabano ( ); mabano ya pande
nne ([ ]); slashi (/).
Vilevile, tunapoangalia suala la uakifishi pia
tunaangalia ujenzi wa aya. Aya inaundwa na wazo
moja. Aya inajengwa na sentensi mbalimbali
ambazo zinasaidiana kulikamilisha wazo husika.
Utungaji 2:Stadi za Lugha ya Kiswahili. Kiango, J.G.
TUKI. Dar es Salaam. 2009
Endapo mwandishi atachanganya mawazo mawili
kwenye aya moja, hapo atakuwa anafanya makosa
ya uakifishi kwa kuwa atamfanya msomaji
achanganyikiwe. Ni kama katika uzungumzaji, kwa
kawaida watu humaliza wazo moja kabla ya
kuingilia jingine. Na inapotokea mzungumzaji
akachanganya mawazo mawili kwenye
mazungumzo, wasikilizaji watamuuliza ‘una maana
gani’ au ‘sikuelewi’ na ndipo atagundua kuwa
amemchanganya msikilizaji. Hivyo itambidi arejee
kwenye mada husika ili aweze kwenda sambamba
na msikilizaji wake. Vivyo hivyo katika uandishi.
Ili uweze kuandika aya nzuri, inakupasa uzingatie
mambo yafuatayo:
Kwanza, kuwe na muunganiko wa mawazo kati ya
sentensi moja na nyingine; au kati ya aya na aya;
na kati ya aya zote zinazojenga wazo kuu. Ni
kanuni ya msingi katika uandishi wowote ule ambao
ni makini kwani hakupaswi kuwe na mgongano wa
hoja katika andiko husika. Ni muhimu kila sentensi,
aya, au kifungu cha maneno kihusike katika
kuifanya matini au andiko litiririke kimawazo.
Pili, usichanganye mawazo mawili au zaidi katika
aya moja – hili nalo ni tatizo linalowakumba
waandishi wengi ambao bado ni chipukizi. Kila aya
inapaswa ibebe wazo moja, na ukiona kuna wazo
tofauti linakujia – basi huna budi kulianziashia aya
yake na hivyo kuliongezea sentensi kadhaa ili
liweze kukamilika.
1.5 Makosa katika uandishi wa insha
Katika uandishi wa aina yoyote ile, matatizo
hayakosi na inabidi ufanye uhakiki mara
unapomaliza kuandika insha yako. Lengo ni
kuhakikisha kuwa wasomaji wako wanapata
ujumbe uliokusudia bila kupoteza au kuharibu,
maana kutokana na makosa ya kizembe. Miongoni
mwa matatizo au makosa haya ni pamoja na:
makosa ya kisintaksia yaani kukosekana
upatanisho wa kisarufi kati ya kiima na kiarifu;
kukosea herufi za uakifishi; makosa ya herufi;
kutonyooka kwa wazo; kukosa muunganiko wa
mawazo; kuchanganya mawazo mawili au zaidi
katika aya moja; na uwasilishaji mbaya au mbovu
(Mahenge, 2011).
Matatizo mengine ni kama vile: kutokuwa makini
katika uandikaji wa sentensi; kukosekana
usambamba wa njeo, hali, na kauli; matumizi
mabaya ya kauli ya kutenda na kutendwa;
kukosekana kwa uhusiano kati ya kichwa cha
habari na habari yenyewe; matatizo ya tafsiri;
matatizo ya finyazo; na athari ya matamshi katika
maandishi.
Makosa ya uakifishi hutokea kwa kushindwa
kutumia vizuri alama za uakifishi ili kuonesha
uhusiano wa neno na neno katika sentensi au kati
ya sentensi. Kama vile: kushindwa kutumia
kiusahihi kituo (.); koma (,); nukta pacha (:); swali
(?); nukta mkato (;); mshangao (!); funga na fungua
semi (“ ”); mkato wa juu ('); kimstari au haifa (-);
deshi (...); mabano ( ); mabano ya pande nne ([ ]);
slashi (/). Ili kujijuvya kuhusiana na matumizi sahihi
ya alama za uandishi na uakifishi, wanafunzi
wanashauriwa wasome kitabu kiitwacho Uandishi
wa Kiswahili na Utungaji (1) cha
Steven Mrikaria
na Utungaji (2) cha John Kiango ambavyo kwa
pamoja vinaelimisha juu ya matumizi sahihi ya
alama za uandishi.
Matatizo mengine ni ya herufi au makosa ya
kiherufi kwani ni vigumu kujua wakati unaandika
kazi. Ili kuepukana na tatizo hili, unashauriwa
kuangalia kwenye kamusi yale maneno usiyo na
uhakika nayo ili ujue herufi zake kama ni sahihi au
la. Unaweza kufanya kosa hili kwa kudondosha
herufi mojawapo katika neno bila kufahamu
kwamba umekosea. Mara nyingi matatizo haya
hutokea pale ambapo hutarajii kufanya kosa. Yote
haya yanachangia katika kumpotosha msomaji
(Mahenge, 2011).
Kukosekana upatanisho wa kisarufi kati ya kiima na
kiarifu nalo ni tatizo wanalokumbana nalo
waandishi wa Kiswahili. Mathalani, kama una
sentensi inayosema: “watoto zake wanalia kila
mara”. Hapa upatanisho wa
kisarufi kati ya nomino
na kitenzi haupo kwa kuwa sio sahihi kusema
‘watoto zake’ kwa kuwa kimilikishi
hicho ‘zake’
kinatumika katika ngeli nyingine na sio ngeli ya
kwanza inayohusika na viumbe hai. Kiusahihi
ilipaswa sentensi hii isomeke hivi: “watoto wake
wanalia kila mara” (Mahenge,
2011).
Kutonyooka kwa wazo ni tatizo jingine ambalo
linawakumba waandishi wengi wanaojifunza stadi
hii ya uandishi. Ili msomaji aweze kukusoma na
kukufuatilia kwa kile unachokisema – ni muhimu
uhakikishe wazo lako limenyooka. Je,utawezaje
kufikia usahihi huo? Mbinu ipo nayo ni kumpa mtu
mwingine ambaye ni tofauti na wewe ili akusomee
kazi yako na kukukosoa pale ambapo panampa
utata wa aina yoyote ile. Kwa kufanya hivyo,
itakuwezesha kuandika mawazo ambayo
yamenyooka (Mahenge, 2011).
Kukosekana muunganiko wa mawazo kati ya
sentensi moja na nyingine; au kati ya aya na aya;
na kati ya aya zote zinazojenga wazo kuu. Ni
kanuni ya msingi katika uandishi wowote ule ambao
ni makini kwani hakupaswi kuwe na mgongano wa
hoja katika andiko husika. Ni muhimu kila sentensi,
aya, au kifungu cha maneno kihusike katika
kuifanya matini au andiko litiririke kimawazo
(Mahenge, 2011).
Kuchanganya mawazo mawili au zaidi katika aya
moja – hili nalo ni tatizo linalowakumba waandishi
wengi ambao bado ni chipukizi. Kila aya inapaswa
ibebe wazo moja, na ukiona kuna wazo tofauti
linakujia – basi huna budi kulianziashia aya yake na
hivyo kuliongezea sentensi kadhaa ili liweze
kukamilika (Mahenge, 2011).
Uwasilishaji mbaya au mbovu wa andiko lako
unaweza kumfanya msomaji ashindwe kusoma na
kuitupilia mbali kazi yako. Ni lazima kwa mwandishi
yoyote yule kuhakikisha kwamba anajua masharti,
kanuni, na miongozo mbalimbali inayomwezesha
kuandika kazi vizuri na kuipangilia kwa ustadi ili
imvutie msomaji wake (Mahenge, 2011).
Kukosekana usambamba wa njeo, hali, na kauli ni
tatizo jingine linalojitokeza katika uandishi.
Kwakuwa, wakati mwinginr utakutana na sentensi
katika magazeti ya Kiswahili zinampishano wa njeo.
Mathalani, tunasikia mara kwa mara waandishi wa
habari wakisoma habari zao kama ifuatavyo: ‘watu
200 kujeruhiwa vibaya kwenye ajali ya meli ya MV
Spice Islander’. Tatizo
lililopo la kinjeo linahusiana
na matumizi ya ‘ku’ katika kitendo cha kujeruhiwa
ambayo kiusahihi inamaanisha watu hao bado
hawajajeruhiwa na kwamba ni matarajio
watajeruhiwa – haya ni makosa kwa kuwa lengo la
habari ni kuripoti kuhusu ajali iliyotokea na kujeruhi
watu 200. Kwa hiyo, kiusahihi habari hiyo
ingesomeka kuwa ‘watu 200 wamejeruhiwa katika
ajali ya meli ya MV Spice Islander iliyotokea
Zanzibar’.
Kukosekana kwa uhusiano kati ya kichwa cha
habari na habari yenyewe – hili ni tatizo ambalo
linajitokeza sana katika habari za kwenye magazeti.
Japokuwa waandishi katika uwanja huu wanalitetea
jambo hilo kuwa ni mbinu ya kuuza magazeti –
lakini sisi tunasema wamepitiliza kwa kuwa
wangeweza kutengeneza vichwa vyenye mvuto
hata bila ya kuvipotosha. Upotoshaji huu unaweza
kuwafanya waonekane ni ‘waongo’ au ‘wambeya’.
Mathalani, utakutana na habari inayosema
“Kanumba amcharaza baba yake laivu”. Msomaji
atapata shauku ya kununua gazeti hili ili aone ni
kwa vipi kijana huyu amekosa adabu kiasi hicho –
cha kumfanya amcharaze baba yake. Kinyume
chake, ukifungua na kuisoma habari hiyo, inaelezea
mkasa tofauti; kwamba, Kanumba alihojiwa na
mwandishi wa gazeti xyz kuhusiana na ‘mahusiano’
yake na mzazi wake. Alichofanya msanii huyu nguli
ni kubainisha kwa kina kuwa mzazi huyu
alimtelekeza wakati yuko mdogo baada ya baba
huyo kuona mke mwingine. Kwa hiyo, katika habari
hiyo hakuna jambo lolote linalohusiana na
Kanumba kumcharaza baba yake.
Matatizo ya tafsiri nayo yamekuwa yakiwasumbua
waandishi wengi. Matatizo haya yanajitokeza
katika miktadha mbalimbali ya kutafsiri kisisisi bila
kuzingatia miundo ya lugha chanzi na ile ya lugha
lengwa. Kwa mfano, imekuwa ni kawaida katika
vyombo vya habari kusoma habari kama hizi:
“Zantel yatoa kumi milioni kusaidia watoto yatima”.
Hili ni kosa la kimuundo kwa kuwa muundo wa
lugha chanzi unaanza kutaja kivumishi kabla ya
nomino – yaani ‘ten million’; wakati lugha lengwa
ina muundo unaotangulizi nomino kabla ya
kivumishi – yaani ‘milioni kumi’. Kwa hiyo,
kutokuzingatia kanuni za kiisimu za lugha lengwa
na lugha chanzi ni tatizo kubwa ambalo linasumbua
waandishi wengi wa habari za magazetini hapa
nchini Tanzania (Mahenge, 2011).
Matatizo ya finyazo nayo yanajitokeza sana katika
mazungumzo ya watumiaji lugha ya Kiswahili.
Wazungumzaji wanasahau kwamba finyazo ile
inasimamia jina la kampuni, chama, au chombo
chochote kile cha serikali au binafsi; wanachofanya
ni kuipachika finyazo hiyo katika ngeli isiyohusika.
Tutatoa mifano ili tuweze kueleweka: “CHADEMA
yashinda Tarime”. Hapa
pana kosa la ngeli ambalo
limekuwepo kutokana na matumizi ya finyazo
ambayo yamemchanganya mtumiaji wa lugha na
kumfanya asahau kuwa finyazo hiyo inasimama
badala ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo
na kwamba, kipatanisho chake ni cha ngeli ya
KI/VI. Kwa usahihi kichwa hicho cha habari
kilipaswa kuandikwa hivi: “CHADEMA chapata
ushindi Tarime” (Mahenge, 2011).
Mwisho, ni athari ya matamshi katika maandishi.
Hili nalo limekuwa ni tatizo linalowasumbua
waandishi wengi katika uandishi wa Kiswahili. Kuna
baadhi ya wazungumzaji wa lugha ya Kiswahili
wanashindwa kuongea kwa ufasaha kutokana na
athari ya lugha mama – na jambo hili linajitokeza
katika uandishi wao. Kuna watu hawana ‘h’ au
mahali ambapo hapatakiwi kuwe na ‘h’ wao
wanaipachika. Kwa mfano, baadhi ya
wazungumzaji ambao asili yao ni Wahaya huwa
wanashindwa kuzingatia matumizi sahihi ya ‘h’ na
kinyume chake. Si ajabu ukamsikia mtu akisema
‘hasili ya binadamu ni sokwe mtu’ badala ya
kusema: ‘asili ya binadamu ni sokwe mtu’. Mifano
iko mingi tu kama vile ya Wachaga, Wamasai,
Wakurya, Wasukuma, Wanyamwezi na wengineo
kwa kuwataja kwa uchache. Kila mmoja katika
makabila tuliyoyataja na yale ambayo
hatukuyataka, asipozingatia matumizi sahihi ya
lugha ya Kiswahili - atajikuta akifanya makosa
ambayo hakukusudia kuyafanya (Mahenge, 2011).
1.6 Hitimisho
Baada ya kukupitisha katika nadharia ya uandishi
kwa ujumla, pamoja na matumizi ya alama za
uandishi na uakifishi; na vilevile makosa ya
kawaida ya kiuandishi na namna ya kuyaepuka,
sasa ni wakati muafaka wa kukudadavulia kwa kina
kuhusu ‘uandishi wa kubuni’ katika miktadha
mbalimbali.
Ninaposema miktadha mbalimbali ninamaanisha
uandishi katika filamu, ushairi, riwaya, tamthiliya, na
drama. Twende pamoja katika aina hizo za
uandishi. Lakini kabla ya kulifiia hilo, itakuwa vizuri
kama nitakupitisha katika hatua muhimu ya ‘namna
ya kuanza kuandika’. Kwa maneno mengine,
sehemu inayofuatia itakuwa ni mbinu na nyenzo za
kuanza kuunga na kuandika kazi yako.
SURA YA PILI
UNAANZAJE KUTUNGA KAZI YA KISANAA?
2.0 Utangulizi
Nimekuwa na kawaida ya kusikia watu wakiniuliza
‘unaanzajeanzaje kutunga na kuandika’? Leo
nitakupatia siri ya mafanikio ambayo inaniwezesha
kutunga, na huenda na watunzi wengine wana siri
zao ambazo huenda ni tofauti kabisa na siri zangu.
Jambo la msingi ni kufanyia kazi mbinu au siri
nitakazokujulisha. Kuna vitu nimeviita ‘kanuni’
navyo nitakufafanualia hapa chini:
2.1 Kanuni Zinazokuwezesha Kubuni / Kutunga
Kutokana na uzoefu wangu mdogo, kuna kanuni
tano ambazo ninaona ni muhimu ili kumwezesha
mtunzi chipukizi atunge kazi yake. Sijaona mahali
popote ambapo nimesoma na kukuta zinaitwa
‘kanuni’ ila ni mimi mwenyewe matakwa yangu
ndiyo yamenifanya niziite hivyo.
Kanuni ya kwanza: utafiti.
Mwandishi
unatakiwa ufanye utafiti ili uweze kupata taarifa
sahihi za jambo ambalo unataka kuliandikia
simulizi. Unaweza ukaniuliza utafiti nitaufanyia
wapi? Kuna sehemu kadhaa ambazo zinaweza
kukusaidia kupata tarifa unazozitaka. Mojawapo ni
kujisomea. Soma vitu mbalimbali kama ni vitabu,
magazeti, majarida, mitandao na kadhalika.
Ukikutana na maarifa yanayokuvutia yaandike. Pia
unaweza kufanya utafiti kwa kuwaulizauliza watu
kuhusu jambo husika. Unapopewa taarifa hizo
ziandike. Tatu ni kwa kufanya ziara katika maeneo
mahususi ili uweze kupata data unayoihitaji.
Tembelea sokoni ukakutane na wamachinga
ambao wamepanga bidhaa zao barabarani na mara
mgambo wanawafukuza na kuwapora mali zao, na
kuzifanya ni za kwao! Ukienda huko na kuulizauliza
utapata mengi. Yaandike na utunze kumbukumbu
kwani utayahitaji siku moja.
Kanuni ya pili: uwe
na kumbukumbu. Ili uwe
mtunzi mzuri unatakiwa upambane na tatizo la
kusahausahau. Ukiwa msahaulifu sana hata mahali
ulipoandika dondoo zako kwa ajili ya hadithi
utapasahau. Ukiona kiwango cha kusahau kinazidi
kuongezeka, tafadhali anza kula vyakula asilia.
Kula dona, kula mchemsho, punguza kula vitu vya
kiwandani. Fanya mazoezi kama vile kuruka kamba
au kukimbia n.k. Kwa namna fulani, utaifufua
kumbukumbu yako.
Kanuni ya tatu: kuza
stadi yako ya uandishi
ili uweze kujieleza kwa maandishi. Inakubidi
ujifunze namna ya kutumia alama za uandishi na
uakifishi ili unapoandika usifanye makosa. Lakini
vilevile ni kuhusu namna wenzako wanavyoandika
kazi zinazowavutia wasomaji. Hakikisha unafanya
mazoezi ya kutosha ya kuandika na kuwaomba
watu wakusomee kazi na kukushauri. Pia soma
insha zinazoelekeza namna ya kuandika vizuri.
Kanuni ya nne: kuwa
mbunifu. Kama
unataka kuwa mwandishi huna budi kuwa na mbinu
za ‘kiubunifu’ ambazo zinakuwezesha kuugeuza
uongo na kuufanya uwe ukweli. Ukweli katika
‘ulimwengu wa hadithi’. Ni ukweli ambao
unapatikana kutokana na ‘mantiki’ ya hadithi
kwamba A imesababisha B na kisha ikasababisha
C. Kwa hiyo huo ndio ‘ukweli’ ninaoumaanisha.
Ukweli ndani ya hadithi yaani kwa kimombo
(believability of what you are saying). Ni jinsi
unavyowashawishi wasomaji au watazamaji wako
na wakashawishika – ndipo huo ‘ukweli’
unapopatikana.
Kanuni ya tano: isuke
ploti yako ili iweze
kugusa hisia na hivyo kumvutia hadhira wa kazi
yako. Ploti ni ule mtiririko wa hadithi
unavyoupangilia kutoka mwanzo wa hadithi yako
hadi unapofikia mwisho. Je, ule mpangilio wako wa
visa na vituko unakupatia ucheshi? Je, msomaji
akisoma atachekeshwa? Je, ataumizwa kihisia na
atalia? Je, atakasirika? Kwa hiyo unatakiwa uweze
kuisuka ploti yako ili uibue hisia mbalimbali kwa
hadhira.
Ukishakuwa na ‘kanuni’ zako, hakikisha
unaandamana na ‘mwandani’ wako ili uweze
kunakili kila kitu muhimu ambacho kitakusaidia
kupata visa na vituko vya kuichangamsha kazi
yako. Mwandani huyu wa mtunzi ni shajara na
kalamu. Hakikisha popote unapokwenda una hivi
vitu viwili ili uweze kuandika na kunukuu dondoo
muhimu za kukusaidia.
Mara nyingi niwapo daladalani, na hasa
nikipata kiti nikakaa au nikikosa kiti na nikasimama,
ndipo hapo ninapopata visa na vituko vya
kuandikia. Wakati mwingine utasikia watu
‘wakitukanana’ au ‘wakizodoana’ kwa sababu
wamekanyagana miguuni, hapo ndipo hupata
vituko kutokana na maneno yanayowatoka
vinywani mwao. Mimi huyaandika maneno hayo na
wakati mwingine nikiumba wahusika wangu katika
hadithi huwa ninawapa maneno yaleyale
yaliosemwa na watu halisi.
Ninafurahia sana kuwa abiria ndani ya gari
kwa kuwa ninapata fursa ya kubuni hadithi au
tamthiliya. Kutokana na hili, mara nyingi ninapanda
daladala kwa kuwa ninapata fursa ya kuvinjari na
kusawiri wahusika wangu wa hadithini; tofauti na
kuendesha gari ambako kunanikosesha fursa hiyo
kwa kunitaka niwe makini. Jambo hili la kuvinjari
wahusika wangu, wakati mwingine hunilazimu
‘kujipitiliza’ kituo ilimradi tu mtiririko wangu wa
simulizi ufikie mahali pazuri. Yaani wakati mwingine
badala ya kushuka chuo kikuu huamua kupitiliza
hadi mwisho wa gari na kisha kugeuza upya na
kurudi tena chuo na hapo ndipo hushuka. Yaani
mzuka unapokujia ndipo hapohapo pa
kugangamala na kuweka mambo sawa. Kuhusu
kuwa dereva ipo siku nitarejea ulingoni!
2.2 Utaanzaje?
Anza kuchagua ‘nafsi’ ambayo utaitumia katika
kusimulia. Je, unataka kusimulia visa na mikasa
hiyo kwa kutumia nafsi ya kwanza? Nafsi ya
kwanza ni ile inayotumia ‘ni’ katika vitenzi. Kwa
mfano ni ukisema ‘nitakununulia gauni’...ile ‘ni’
iliyojitokeza hapo ndiyo hiyo nafsi ya kwanza. Nafsi
ya kwanza inaonesha simulizi iko karibu na
mwandishi na kwa namna fulani anayoyaandika
yanamhusu au amepitia uzoefu huo.
Au la unataka kusimulia kwa nafsi ya tatu? Nafsi
ya tatu ni ile inayosimulia hadithi kwa kutumia ‘a’
yaani kitenzi kinachukua kiambishi hicho cha awali.
Kwa mfano ni ukisema ‘akamnunulia gauni’
ambayo inamaanisha ni mtu mwingine. Au
unaweza ukatumia nafsi ya pili ambayo inaonesha
unamwambia msomaji ‘wewe’. Kwa mfano ni
ukisema ‘ukamnunulia gauni’. Je, umeona tofauti?
Kama hujaona tofauti, nitarudia hapa chini kama
ifuatavyo:
Nikamnunulia gauni...[mimi]
Akamnunulia gauni....[yeye]
Ukamnunulia gauni....[wewe]
Ukishachagua nafsi unayotaka kuitumia anza
kuandika sentensi yako. Kuchagua nafsi fulani ya
usimulizi hakumaanishi kuwa umebanwa usitumie
nafsi zingine, la hasha! Utazitumia kwa uhuru ila
jambo la msingi uhakikishe simulizi haipotezi
mwelekeo. Kama ulikuwa unasimulia kuwa ni tukio
linalokuhusu, {yaani mimi} msomaji atatarajia aone
hadi mwisho simulizi imekuwaje japokuwa hapa na
pale utachanganya nafsi hizo katika kusimulia.
Baada ya kuchagua nafsi ya usimulizi, anza
kuviungnisha visa vyako kimantiki. Kwa mfano,
kwenye shajara yako kuna visa mbalimbali
ambavyo uliviokota barabarani, kanisani, msikitini,
dukani, sokoni, buchani, darasani, ofisini,
daladalani na kadhalika. Visa hivi na vituko na
daiolojia huenda uliviandika katika shajara yako.
Sasa vipitie uvisome na uone ni kwa namna gani
utavipangilia na kuvifanya vilete maana kimantiki?
Baada ya kuzipitia dondoo hizo, bila shaka
umeshajikumbusha mikasa na visa mbalimbali
ulivyowahi kuvirekodi.
Kinachofuata ni kuwaumba wahusika wako
ili uweze kuwabebesha majukumu mbalimbali.
Majukumu hayo ndiyo yatakayokuongoza ili uumbe
wahusika kadhaa (idadi). Kwa mfano, katika jamii
uliona mkasa mmoja wa kijana mmoja wa kike
ambaye alikataliwa na kijana aliyempa mimba, na
kisha siku mzozo ulipotokea kulikuwa na watu
kadha wa kadha walioshuhudia n.k. Basi hapo
tayari una mhusika mvulana, msichana, mpitanjia,
n.k n.k n.k. Hapo sasa unaukuza mgogoro kuwa
itakuwaje akienda kwao (yule binti akienda kwa
wazazi wake), na ndugu n.k. Jaribu kuunganisha
visa na mikasa ili itiririke na kuvutia hisia za
wasomaji.
Mwisho ni kuanza kuipangilia hadithi yako
au filamu au drama ili mtiririko uvutie. Kwa mfano,
haitakuwa na maana kama utatuandikia hadithi
ambayo visa vyake vimekaa shaghalabaghala. Kwa
mfano, unatumbia msichana amefukuzwa na
wazazi wake baada ya kugundulika ana mimba. Ila
tulipokuwa tunasoma hadithi hatujaona hata mahali
pamoja ambapo umetuonesha kuwa binti huyo
alikuwa na mpenzi na hatimaye akaanza
mahusiano na huyo mvulana. Kwa hiyo,
kunahitajika mantiki ya hadithi yako, yaani tuone
msichana na mvulana wakianza kupendana; kisha
tuone mahusiano; kisha tutakapoambiwa binti
kapata mimba tutaelewa kwamba ilianzajeanzaje,
yaani kunakuwa na ‘mantiki’ ya kimtiririko ambayo
ndiyo inawezesha kupatikana ‘ukweli wa hadithi’.
Kinachofuata...
Anza sasa kuandika... anza....anza....anza...
(chagua umbo unalolitaka uandikie. Je, unataka
kuandika riwaya, hadithi fupi, shairi, drama ya
jukwaani, runingani, au redioni? Au je unataka
kuandika filamu? Uchaguzi ni wako. Amua na
uanze kuandika).
SURA YA TATU
UANDISHI WA MISWADA YA FILAMU
Usuli wake
3.0 Filamu ni Nini?
Filamu imeelezewa na watu mbalimbali na kwa
namna tofauti. Miongoni mwa watu hao ni Kasiga
(2013) ambaye anasema kuwa, filamu ni dhana
inayohusishwa na hadithi zinazotambwa kupitia
picha jongefu zilizorekodiwa kutoka kwenye
mazingira fulani, zikiwahusisha waigizaji, mazingira
yao, desturi zao pamoja na utamaduni uendao
sambamba na mawasilisho ya maudhui
yaliyosanwa kwenye sanaa hiyo.
Mtu mwingine ambaye anafasili filamu ni
Kileo (2012) ambaye anasema kwamba, filamu
kama kipengele cha fasihi ni utanzu wa drama
ambao una nafasi kubwa katika kufikisha ujumbe
kwa hadhira kwa njia ya maneno na matendo ya
waigizaji. Japokuwa Kasiga amejitahidi kutaja
mambo muhimu yanayohusiana na filamu, lakini
bado kuna vitu vya msingi ameviacha. Hajaelezea
sifa ya ujumuishi (maltimodo) ambayo
inaipambanua filamu na aina zingine za sanaa.
Tunaweza kusema kwamba, filamu ni utanzu
wa fasihi unaotumia picha jongefu na mbinu za
kifilamu ili kuwasilisha hadithi inayosimuliwa na
watu wengi ambao ni mwandishi, mpigapicha,
msimulizi, mhariri na mwigizaji. Wote hawa
wansaidiana ili kusimulia hadithi. Mbinu hizi za
kifilamu ni aina ya picha inayopigwa (ndogo,
kubwa, kubwa sana); mahali
inapopigiwa (juu,
chini, kawaida); mpangilio
wa vitu mbele ya kamera
(mizensini); mapigo, sauti na
midundo; mwangaza
au giza; mtazamo (POV), ploti, uhusika wa
wahusika na msimulizi (Murray, 1987). Filamu si
utanzu wa drama japokuwa inatumia waigizaji
kama inavyofanyika katika drama.
3.1 Filamu ni Fasihi?
Kuna uhusiano mkubwa sana kati ya filamu na
fasihi. Uhusiano huo unatokana na ukamilishanaji
wa pande zote mbili kama anavyoelezea Perrier
(1992) kwamba, fasihi inatoa mwangaza kuhusu
filamu, na filamu inathibitisha thamani ya fasihi. Mtu
mwingine ambaye anaonesha uhusiano huo ni
Jann (2001) anayeelezea kuwa, filamu kama ilivyo
drama na tanzu simulizi kama vile riwaya, zote
zinatumia usimulizi ili kufikisha ujumbe kwa
hadhira. Hii ina maana kuwa, fasihi (tukichukulia
mfano wa riwaya) ina mambo yanayoingiliana na
filamu.
Kazi zote zinatumia wahusika, msimulizi,
ploti, lugha na mtazamo ili kusimulia hadithi. Katika
riwaya, mwandishi anatumia sura wakati kwenye
filamu anatumia fremu. Hadhira ya kiriwaya
inatumia macho kusoma hadithi, wakati hadithi ya
kifilamu inatumia macho kutazama filamu. Kwa
hiyo, kuna mwingiliano kati ya fasihi na filamu.
Kasiga (2013) anaelezea kuwa, uhusiano wa filamu
na fasihi unatokana na kuwapo hadithi
inayotambwa, wahusika, matumizi ya hisia na
taswira mbalimbali, pamoja na daiolojia zenye
maneno kutoka katika lugha yoyote izungumzwayo
na wanadamu.
Kitu muhimu ambacho Kasiga hajakitaja
waziwazi ni aina mbili za lugha zinazotumika katika
kusimulia hadithi ya kifilamu. Lugha ya kwanza ni
hiyo aliyoitaja ambayo inatumiwa na waigizaji
kupitia daiolojia au maneno waliyopewa
kuzungumza; lakini lugha ya pili ni lugha ya kifilamu
ambayo inatumiwa na mwongozaji, mpiga picha na
mhariri ili kusimulia hadithi. Hii lugha ya kifilamu
inahusisha matumizi ya vitu kama mwangaza au
giza; maleba; midundo, milio na sauti; mpangilio wa
vitu mbele ya kamera (mizensini); rangi mbalimbali;
mahali pa kupigia picha (kamera engo) na aina ya
picha inayopigwa (kamera shoti – ni kitu kizima; ni
saizi ya pasipoti, ni ya sura tu, ni ya pua tu n.k).
Kwa hiyo, kwa kuwa fasihi ni sanaa
inayotumia lugha ili kufikisha ujumbe wake katika
jamii, basi, tunaweza kusema kuwa, filamu ni fasihi
inayotumia lugha za aina mbili ili kufikisha ujumbe
wake kwa hadhira. Hivyo, filamu si tawi la fasihi
simulizi (Kasiga, 2013) na wala si utanzu wa drama
(Kileo, 2011) ila “filamu ni fasihi ya picha jongefu
inayosimuliwa na watu wengi kwa kutumia lugha za
aina mbili” (Mahenge, pendekezo la PhD, 2014-
2016, UDSM).
Syd Field (1994:180 - 203) anadadavua
vipengele muhimu ambavyo vinatakiwa viwemo
katika mswada wa filamu; na vilevile anaelezea jinsi
wazo linavyopatikana; hadithi ya filamu
inavyosukwa; jinsi wahusika wanavyopaswa
kujengwa na hulka zao tofauti; jinsi ya kuisuka ploti
katika filamu na jinsi ya kuuandika mswada wa
filamu. Kuna vipengele muhimu ambavyo
vinatakiwa viwemo katika mswada wa filamu
ambavyo ni: kutaja namba ya onesho, mahali
onesho linapofanyikia, muda ambao onesho
linafanyika na kama ni nje au ndani. Maelekezo
mengine ni namna ya kuandika majina ya wahusika
na mazungumzo yao, na maelekezo mengine
yanayosaidia kuingia kwenye uhusika wa upande
mmoja; na kumsaidia mwongozaji kwa upande
mwingine.
3.2 Ufundi wenyewe
3.2.1 Namna ya kuanza kuandika wazo
Katika utungaji wa filamu, anaza kuandika ikisiri
(sinopsis) ambayo haizidi maneno 50. Yaani huu ni
muhtasari tu wa kazi yako inahusu nini. Haya ndiyo
yale maneno unayoyaona kwenye kasha la filamu.
Sema kwa ufupi sana filamu yako inahusu nini.
Kwa mfano: Tumiya anapendana na
kimwana mmoja huko kijijini. Tumiya anakwenda
kutoa mahari na anakuta kimwana ameshaolewa
na Njemba. Tumiya anapigana na Njemba na
anapelekwa polisi. Kesi inasomwa na Tumiya
anakosa dhamana. Tumiya anafungwa na baada
ya mizei 3 anaachiliwa. Tumiya anarudi mjini na
kukuta amefukuzwa kazi. Nini kitaendelea?
3.2.2 Kuza wazo lako
Andika kwa dondoo mawazo makuu ambayo
yatahusika katika filamu. Yaani ile hadithi yako
itakavyokuwa, mambo yatakayohusika, wahusika
watakaoshiriki, nk. Hakikisha unalipanua wazo lako
katika sentensi moja. Kila sentensi unayoiandika
ibebe wazo moja na uipe namba yake. Upanuzi huu
wa wazo usizidi kurasa tatu. Yaani hizi ni dondoo
muhimu tu bila kufafanua.
Kwa mfano ukisema: (1) Tumiya anakwenda
kijijini kuposa. (2) Binti aliyetaka kumposa
ameshaolewa na njemba moja. (3) Ugomvi
unazuka Tumiya na njemba iliyomwoa kimwana
wake (4). Njemba inampeleka Tumiya polisi
kumshitaki (5). Tumiya anawekwa lupango kwa
kusababisha vurugu (n.k n.k n.k sasa endelea hadi
mwisho wa simulizi yako).
Baada ya hapo ndio sasa unaanza
kuidadavua hadithi yako ya filamu katika kila
onesho kama tutakavyoonesha hapa chini kwenye
uandishi wake.
3.3.3 Uandishi wake:
Uandishi wa mswada wa filamu ni tofauti sana na
uandishi wa mswada wa mchezo wa redio au
mchezo wa jukwaani au runinga (tamthiliya). Kuna
vitu kadhaa vinavyoandamana na uandishi wa
mswada huu, navyo ni pamoja na:
(i) Kutaja namba ya onesho ambalo
litaonekana baada ya filamu kuwa tayari.
Katika ujengaji wa onesho hili- picha nyingi
hupigwa mpaka pale mpigapicha na
mwongozaji watakapo ridhika na picha
zilizochukuliwa. Kwa lugha ya Kiingereza
huita 'takes' ambapo ina maanisha idadi ya
picha ambazo zitapigwa ili kuja kutengeneza
hadithi nzima. Baada ya kuandika namba ya
onesho kwa herufi kubwa inafuata nukta.
(ii) Inapaswa kutajwa kuwa onesho litafanyikia
wapi? Je ni nje ya nyumba au ni ndani? Pia
inapaswa kuandika eneo hilo kwa herufi
kubwa kisha inafuatia nukta.
(iii) Kisha kitu kinachofuatia ni kutoa ufafanuzi
wa sehemu husika litakapofanyika onesho
hilo. Baada ya kusema kuwa ni ndani au nje
- yabidi kufafanua kuwa ni sehemu gani
hasa? Je ni shambani, jikoni, sebuleni au
bafuni?
(iv) Mwisho katika kukamilisha jina la onesho ni
kutaja wakati wa onesho hilo: je ni usiku,
asubuhi, jioni, au mchana? Ni lazima hali ya
asili ya maziingira isaidie kuonesha uhalisia
wa muda. Kama ni vigumu kuipata hali
halisia inawezekana kufanya ufundi na
utundu mbalimbali kupitia kompyuta ili
kupata picha zitakazoleta ukubalifu na
kuaminika kwa watazamaji. Jambo hili la
kukosa mbinu na maarifa ya kutengeneza
filamu zinazo ‘aminika’, linafanya kazi nyingi
za wasanii wa hapa nyumbani Tanzania
watengeneze filamu ambazo zinaonekana
zinadanganya, kiasi kwamba, hata mtoto
mdogo, anaweza kugundua udhaifu
unaowasilishwa katika kazi hizi. Kwa mfano,
wahusika wanajibizana kuwa ni ‘asubuhi’
wakati kwenye picha jongefu inaonesha
tayari ‘giza’ limeingia. Haifai kamwe
kudanganya namna hiyo! Kama msanii
ameamua kujikita katika uwanja huu ni
lazima ajifunze A, B, C, D’s za kazi hii ya
utengenezaji wa filamu ambapo ‘believabiliy’
ni kitu cha lazima ili ukweli wa hadithi
upatikane.
(v) Maelekezo ya matendo ya mhusika
yanaandikwa katika hati ya kawaida ambayo
sio ya mlalo. Maelekezo haya yanaandikwa
tangu pale karatasi inapoanzia na kuendelea
hadi inapoishia na kisha inawezekana
kuingia mstari wa pili na kadhalika. Aya
hazitumiki katika uandishi wa miswada ya
filamu, bali ni kuandika tu kwa mfululizo na
mwendelezo bila kuweka aya.
(vi) Mazungumzo ya wahusika yanaandikwa
katikati ya mstari chini ya jina la mhusika.
(vii) Jina la Mhusika linaandikwa kwa herufi kubwa
na chini yake linapigiwa mstari. Kisha
yanaandikwa maneno anayoyasema
mhusika huyo sambamba na jina lake.
Maandishi haya yanatakiwa yawe katika hati
ya kawaida ambayo siyo ya mlalo. Hebu
tupate mfano ambao utatuonesha namna ya
kuandika muswada wa filamu ili kupata
dhana tulilolijadili katika namba moja hadi
saba.
1. NDANI. CHUMBANI. USIKU.
Beti na Tuma wamekaa kitandani
wanatazamana. Chumba kina taa ya glopu
ambayo inatoa mwanga wa buluu.
BETI
Leo ni zamu yako ya kuzima taa.
TUMA
Zima wewe
BETI
Basi tulale hivyohivyo
TUMA
Sawa tu
Beti anajilaza na Tuma anajilaza pia. Beti
anavuta shuka na wanajifunika na wanalala.
FADE OUT.
Hivyo ndivyo skripti ya filamu inavyotakiwa
kuandikwa.
(viii) Baada ya kukamilisha yanayohitajika katika
onesho hilo, inapaswa kuandika aina ya
ifekti (effect) ambayo mtunzi atapenda
itumike katika uhariri wa kazi. Zipo aina
nyingi za ifekti kama vile: waipu (wipe),
suparimpozi (superimpose), fedi ini (fade in),
fedi auti (fade out), na kukata (cut).
Maelekezo hayo huandikwa mwishoni
mwa maelekezo ya onesho katika
upande wa kulia wa karatasi.
(ix) Wakati wa upigaji wa picha kunahitajika vitu
muhimu ambavyo vitawezesha onesho
kutokea kama alivyokusudia mwandishi.
Kuna suala la mavazi ya wahusika ambapo
kila mhusika anapaswa kuvaa kulingana na
uhusika wake. Bila shaka mtu wa mavazi
atapaswa kushughulikia jambo hili. Kwa
utaratibu, kila kazi inapaswa kufanywa na
mtu tofauti ili aweze kupata ushauri kutoka
kwa wenzake wa namna ya kuboresha kazi
yake. Mathalani mtu wa mavazi anapaswa
kufanya kazi kwa kushirikiana na
mwongozaji na vilevile na mtu wa mwanga ili
kuleta hisia iliyotarajiwa na mtunzi. Hapa
nyumbani filamu nyingi zinatobangwa kwa
kuwa unakuta kila kazi imefanywa na mtu
yuleyule - mtu anakuwa na vyeo zaidi ya
viwili- hii sio taaluma. Maadamu wasanii
wameamua kujiingiza katika fani hii, ni
lazima wafuate weledi wa taaluma yenyewe
ili kutoa kazi bora na sio bora kazi. Kama
wasanii hawatabadilika kazi zao zitazidi
kudoda kwa kuwa ni nani atakubali kuitupa
pesa yake kwa kununua kitu kilicho chini ya
kiwango? Bila shaka hakuna! Jambo hili
litaendelea kuwafanya wapenzi wa sanaa
waendelee kuvutiwa na filamu za Hollywood,
India, Japani, China, Nijeria, na kwingineko.
(x) Matumizi ya taa za mianga na riflekta
(reflector) ni muhimu ili kupata picha
inayofanania uhalisia wa maisha. Matumizi
ya reflekta yasiwe bila sababu kwani
yakifanywa bila utambuzi wa tahadhali hii -
huleteleza kazi chapya ambayo hakuna mtu
atavumilia kuitazama. Mathalani kuna kazi
moja niliwahi kuitazama ya hapa nyumbani
ambapo taa za mianga na reflekta zilitumika
vibaya na hivyo kuifanya picha nzima kuwa
nyekundu utafikiri watu wamepakwa damu,
nyumba zao zimepakwa damu, kila kitu
wanachokishika kimepakwa damu. Haifai
kufanya mambo bila kuwa na utaalamu - ni
jambo bora na la busara wasanii wakatumia
wataalamu katika maswala ya sanaa ili
waweze kutoa kazi zitakazo washika
watazamaji na hivyo kujijengea heshima
kama walivyojijengea wasanii na waongozaji
wa filamu za Kimarekani; na mahali
kwingineko ambako watu hawafanyi kazi
kwa vipaji tu - bali wameongezea na taaluma
kidogo. Kwa hiyo kunawafanya watoe kazi
bora.
(ix) Baada ya shughuli hiyo kuisha, inafuata
kazi ya studio ambayo itakuwa ni kuhariri
picha na kuingiza sauti zinazoshadidia
matukio mbalimbali pamoja na miziki ili
uundwaji wa matukio uweze kuleta hisia
na kuwashika watazamaji. Hapa zoezi la
kuhariri linafanywa na mhariri
akishirikiana na mwongozaji wa filamu ili
kuweza kufikia muafaka wa namna gani
onesho liwe. Matumizi ya efekti
mbalimbali hutawala katika hatua hii.
(x) Maswala mengine ya kiufundi
yanahusiana na mpangilio wa vitu mbele
ya kamera (katika jicho la kamera) ili
hatimaye tuweze kuona jinsi vitu
vilivyopangwa. Kwa Kiingereza jambo hili
linaitwa “mise en scene” ikimaanisha ‘kitu
gani kinawekwa wapi’, nini kinakaa
kushoto, kulia, katikati, juu, chini, na
kadhalika. Ni kama vile mwongozaji wa
michezo ya jukwaani anavyowapanga
wahusika wake na vifaa mbalimbali
vinavyomsaidia mwigizaji akiwa jukwaani.
Jambo la msingi na la kukumbuka ni
kuwa, kile kinachowekwa katikati ndicho
kinaonekana kina maana na kinawavutia
watazamaji na lazima mwongozaji wa
filamu au mchezo wa jukwaani azingatie
hilo. Kinachowekwa pembeni hakiyavutii
macho ya mtazamaji na kinaonekana
kuwa hakina umuhimu; na ikitokea, kuna
jambo linafanywa na mhusika aliye
pembezoni – ndipo hadhira itamtazama.
Pia kitu kingine ni kuzingatia ufuatiliaji wa
waigizaji wanakotazama na hadhira
itataka kutazama huko. Kwa hiyo, kama
mhusika anaonekana akielekeza macho
yake upande wa kulia – lazima kuna kitu
anakiangalia; kwa hiyo na watazamaji
tunataka kuona anachokiangalia
mwigizaji (mhusika). Kwa hiyo ikitokea
mwigizaji anatazama pembeni lakini
hakuna kitu tunachoweza kukiona, yaani
hadhira inatazama na hakuna
kitazwamacho – basi hapo sanaa
imeshindwa kufikia ubora wake
unaotakiwa. Wasanii wajifunze kwa
kuangalia kazi za wasanii wa Hollywood
na kwingineko ambako walianza
kujishughulisha na sanaa ya uigizaji kwa
karne nyingi.
(xi) Kitu kingine cha kuzingatia ni urefushaji
wa matukio bila sababu ya msingi. Katika
filamu, matukio yanapaswa kuoneshwa
kwa sekunde chache tu kama urefu wake
hauna mchango katika uendelezaji wa
hadithi. Kila urefushaji wa tukio uwe na
sababu zake katika mwendelezo wa
hadithi. Hili si tatizo kwa filamu za
wenzetu wa majuu ambao ni wabobevu
katika uwanja huu – hili ni tatizo huku
kwetu ambako watengenezaji wa filamu
wanarefusha matukio bila sababu
maalumu. Lazima kila urefu wa tukio
uhusike katika mwendelezo wa hadithi.
Mara nyingi utaona kwenye filamu zetu
mhusika anaonekana akiingia ndani ya
gari na gari lile linaondoka, tunaoneshwa
linavyokwenda zaidi ya dakika kumi – bila
kuwa na msingi wowote. Lazima kama
kuna kuoneshwa linavyokwenda kuwe na
mwendelezo wa hadithi la si kuonesha tu
ili mradi kuonesha.
(xii) Matumizi ya vifaa mbalimbali lazima
yawe na sababu. Mara nyingi katika
filamu zetu au hata michezo ya kuigiza
ya kwenye televisheni au jukwaani,
utamwona mhusika amebeba kifaa fulani,
lakini kifaa hicho hakina uhusiano
wowote na hadithi. Jambo hili halifai.
Mathalani, katika sanaa za wenzetu huko
majuu, ukimwona mhusika ameshika
kifaa labda tuseme ‘kisu’, basi kisu hicho
kinasimulizi katika hadithi. Labda
kitatumika kujeruhi mtu, au tukiona kisu
kina damu baadaye tukaoneshwa mtu
aliyechinjwa – basi hapo matumizi ya
kifaa hicho yanakuwa na mantiki. Hapa
nyumbani mambo ni tofauti, na hii bila
ubishi wowote inatokana na kutoelewa
kuwa kila kitu kishikwacho na mhusika
lazima kiwe na kazi. Mathalani tumewahi
kuona katika michezo ya televisheni,
mhusika amevaa manati kubwa shingoni,
au anaishika kila aendapo, lakini haina
matumizi. Au unaweza kuona mhusika
amebeba kikuyu na kila mahali
anakwenda nacho kakibeba tu, na hakina
matumizi. Kama mhusika huyu
angejengwa kuwa ni kichaa, ambaye
anajiokotea vitu na kuvibeba, hapo
isingeleta maswali. Lakini si mhusika
kichaa, ni mtu na akili zake timamu, lakini
anashika kifaa na kutembea nacho kila
mahali- hii haifai na siyo sahihi.
(xiii) Matumizi ya rangi za mavazi au maua na
hata vifaa mbalimbali pamoja na
mandhari nzima lazima visaidie katika
kuelezea maudhui ya kazi. Lazima fani
itumike kujenga maudhui. Kwa wenzetu
hili si tatizo kwa kuwa wanaelewa mambo
haya na hawafanyi kwa kubahatisha.
Utakuwa kuna wahusika wamebeba
dhamira ya mapenzi na wamevalishwa
mavazi meusi – hii maana yake nini?
Lazima rangi za mavazi zishadidie
maudhui. Katika sanaa, rangi zina maana
zake. Kwa mfano, rangi nyeusi
zinafungamana na maovu, dhambi, au
matendo mabaya, na ufisadi kwa ujumla.
Rangi nyeupe inafungamana na wema,
usafi wa moyo au utakatifu. Rangi ya
njano inafungamana na wivu wa
kimapenzi. Rangi nyekundu
inafungamana na mapenzi kati ya
wapendanao na ndio maana siku ya
wapendanao inatawala vazi jekundu.
Rangi ya zambarau inafungamana na
masuala yanayohuzunisha na ndio
maana katika baadhi ya makanisa – siku
ya ijumaa kuu, ambayo ni ya mateso ya
Bwana Yesu rangi za dhambarau
hutawala katika mavazi ya wachungaji,
watumishi na pia vitambaa
vinavyotandikwa altareni.
(xiv) Matumizi ya muziki au mapigo fulani
ambayo yanaleta ridhimu lazima
yafanywe kwa uangalifu mkubwa na pia
yanapaswa yaendane na dhamira
inayoibushwa. Katika kazi za wenzetu
udhaifu huu huwezi kukutana nao; ila
katika kazi zetu udhaifu upo. Unakuta
kuna tukio la hatari, labda kuna mtu
anaviziwa ili auawe, lakini unakuta
mapigo ya hatari hayasikiki bali
yanasikika ni kama yale yanayoendana
na mahaba – yaani mapigo ya polepole,
mazuri yanayovutia na kuleta uzuri fulani,
mapigo laini – hili ni tatizo. Mapigo
yanayoashiria hatari huwa ni makali
yasiyo ya kawaida, ya haraka haraka, na
ya kushitua. Na kinyume chake unaweza
kuoneshwa wahusika wako katika
mahaba, na muziki unaopigwa ni ule usio
mwololo yaani mziki mkali unaofaa
kwenye kipindi kilichochangamka kama
cha michezo au harakati. Hili ni kosa,
muziki unaofungamana na masuala ya
mapenzi na mahaba lazima uwe mwololo
ili kushadidia dhamira hiyo. Siyo kupiga
muziki kwa ajili ya kupiga tu- hapana, kila
pigo au ridhimu lazima iwe na maana na
mchango katika kuendeleza dhamira.
(xv) Matumizi ya bakigraundi (mahali pa
nyuma kama sehemu ya picha au
sanamu panapotumika kushadidia
mandhari ya onesho) lazima yawe na
maana katika kuibua maudhui. Utakuta
picha imepigwa na kwenye bakigraundi
kuna mandhari fulani inayoonekana.
Lazima bakigraundi hiyo isadifu dhamira
inayokusudiwa. Mathalani, katika nyimbo
mbalimbali za Injili hapa Tanzania,
utakuta mwimbaji anaimba na nyuma
yake tunaiona bahari. Lakini , je, bahari
hii inayoonekana kwenye bakigraundi ina
maana yoyote katika kuibua ujumbe
unaoimbwa? Wakati mwingine, utakuta
mwimbaji ameingia ndani ya maji – labda
baharini, lakini anachokiimba hakina
uhusiano kabisa na maeneo aliyopo; au
utakuta mwimbaji anagaragara kwenye
tope akiimba kuhusiana na jambo la
furaha na sio majuto na maombolezo –
hii haifai. Lazima sanaa ifanywe kwa
viwango vinavyotakiwa. Ni bora wasanii
wetu wakajifunza kwa kuangalia kazi za
wenzao wa Hollywood na kwingineko
ambao ni wakongwe katika uwanja huu,
ili wajue nini wanapaswa kufanya na wapi
wakifanye.
(xvi) Kitu kingine cha kuzingatia ni namna ya
uchezaji na kuendana na mapigo katika
miziki ya Injili ambayo tunaiona kwenye
televisheni. Wachezaji wanaiga namna
ya uchezaji bila kufanya mazoezi ya kina
ambayo yatawawezesha kuendana na
mapigo ya muziki. Nasema hili kwa
uchungu kabisa baada ya kuangalia kazi
ya baadhi ya wasanii wa muziki wa Injili
ambao wanaiga uchezaji wa Rose
Muhando lakini wanashindwa kuendana
na mapigo ya ngoma na hivyo
kuonekana kichekesho. Haifai kuiga, ni
vema kila mwanamuziki wa Injili
akamtafuta mtaalamu wa muziki ambaye
atamshauri namna ya uchezaji kuendana
na mapigo ya wimbo na maudhui yake.
Utaweza kuona wachezaji wa nyimbo
wanaimba wimbo wa polepole lakini
wanacheza kwa haraka na kurukaruka
kama Rose Muhando; au wanaimba
harakaharaka na wanacheza kwa
mwendo wa pole. Huu ni ukiushi na
ukengeushi – haipaswi kufanya hivyo! Ni
lazima kuendana na maadili ya sanaa hii
ya vielelezo (yaani runinga na filamu)
kama ambavyo kanuni na kaida zake
zimejengwa katika nadharia hizo za
uigizaji. Kila mdundo au ridhimu iendane
na mwendo na mapigo ya muziki au
wimbo; na vilevile yaendane na uchezaji.
3.4 Hitimisho
Filamu ni sanaa inayopendwa na watu wengi
duniani. Jambo hili lina ushahidi kutokana na watu
kutazama hata filamu wasizoelewa ‘ulimi’ wake
(lugha inayotumika), lakini wanajitahidi kupata
ujumbe kupitia picha za mwendoni. Wasanii wetu
wajitahidi ili sanaa zao zibebe utamaduni wetu na
zivutie hata watu wengine ambao hawaelewi
Kiingereza wala Kiswahili, ila mvuto tu wa filamu
yenyewe inawafanya waipende na kuifuatilia.
SURA YA NNE
UANDISHI WA MISWADA YA REDIO
Usuli wake
4.0 Utangulizi:
Kwa mujibu wa Moshiro (1979:1) anaelezea
mchezo wa redio kuwa ni:
Ni igizo lifanyikalo redioni, ambalo wahusika
wake hutumia sauti zozote zilizo katika
mazingira yahusikanayo na mchezo huo ili
kutoa picha ya kile kielezwacho. Sauti hizo ni
maneno ya wahusika, zile zitokanazo na
vitendo vya wahusika na nyingine zozote za
asili zinazoyasanifu mazingira yahusikayo.
Katika michezo hii mara nyingi muziki
hutumika kama kielelezo cha ziada.
Kulingana na fasili hiyo ya Moshiro
kuhusiana na mchezo wa redio, tunaweza
kudondoa mambo ya msingi aliyoyataja ambayo ni:
igizo linalofanyika redioni - ina maana msikilizaji
atasikiliza kinachoigizwa ambacho kinapaswa
kimpe picha katika akili yake. Pili, ameelezea
wahusika hutumia sauti mbalimbali ili kukamilisha
dhana ya uhusika wao - sauti hizi zinaweza kuwa
milio ya vitu, ndege, wanyama, au sauti za
binadamu zinazoelezea hisia mbalimbali kama
kulia, kucheka, kusonya, na kadhalika au maneno
wayaongeayo.
Tatu, ametaja muziki - ambao unaweza
kutumika ili kutambulisha mandhari ya mchezo, au
wakati mwingine hutumika kusindikiza dhamira
fulani. Maana ya mchezo wa redio kama
ilivyoelezwa na Moshiro tunaikubali na hivyo
itatumika bila maboresho ya aina yoyote.
Moshiro anaendelea kuelezea hatua za
uandishi wa mchezo wa redio ambao ni pamoja na:
kwanza inatakiwa uitunge hadithi. Hadithi hii
inapaswa ichukuliwe katika maisha ya mahali fulani
na wakati fulani, kisha ifinyangwe kisanaa ili
kumwezesha msomaji au msikilizaji aione katika
fikara. Kwa mfano, hadithi kuhusu kijana wa kiume
kuchaguliwa mke wa kuoa.
Hatua ya pili ni uundaji wa migongano.
Inabidi ufikirie kisa chako kitakuwa na migongano
ya aina gani. Mathalani, tuchukulie mfano wa
msichana na mvulana wanakuwa na mahusiano ya
mapenzi kabla ya ndoa, siku moja baba wa
msichana anawafuma na kuwafungisha ndoa ya
mkeka. Sasa unda migongano kwa mkasa huu.
Hatua ya tatu ni kuupangilia mtiririko wa kisa chako
katika hadithi. Mwandishi anapaswa aamue kuwa
anataka aianze hadithi yake moja kwa moja au
atumie muundo wa kioo. Ni uamuzi wa mwandishi
mwenyewe. Hatua ya mwisho ni uandishi wa
mchezo wa redio ambao kaida zake zitaelezwa
katika sehemu ifuatayo.
4.1 Uandishi wake
Uandishi wa mchezo wa redio kwa mujibu wa
Moshiro unapaswa uwe na vitu vitano ambavyo ni:
kwanza, kuna usimulizi anauelezea kwa namna
mbili: kwanza ni msimulizi ambaye anaitambulisha
hadithi; na pili, ni mazungumzo ya wahusika
wanapowasiliana.
Pili, anazungumzia suala la uzungumzaji
kwamba, katika maisha ya kila siku, watu
wanaanza kuongea jambo moja na kisha wanarukia
jingine. Katika mchezo wa redio, sikio la msikilizaji
haliwezi kusikiliza kwa muda mrefu, hivyo inatakiwa
mazungumzo yawe haraka haraka, na ya
kueleweka kwa urahisi, licha ya kisa chenyewe
kuwa cha kusisimua.
Tatu, anazungumzia hulka kwamba, kila
binadamu ana tabia na hulka tofauti na mwingine.
Hivyo, wahusika katika mchezo wa redio hawana
budi kutofautiana hulka na tabia zao.
Nne, anazungumzia wahusika kuwa
hawatakiwi wawe wengi kwasababu
watambabaisha msikilizaji hata asijue nani ni nani
katika igizo hilo. Pia anaelezea kuwa majina ya
wahusika yatajwe mara kwa mara hasa mwanzo
wa mandhari yoyote; na pia anamzungumzia
mhusika ambaye hasemi lolote na kuwepo kwake
mahali hapo ni muhimu, mhusika huyu hana budi
kutajwa jina lake mara kwa mara ili msomaji
asimpoteze.
Mwisho ni sehemu ya mchezo, kwamba kila
mara msikilizaji anaposikia maongezi katika
mchezo, huwa kwanza anakisia mahali ambapo
wahusika wako kutokana na sauti au milio
atakayoisikia2.
Moshiro katika ukurasa wa 4-7 anaongezea
‘namna ya kuandika mchezo wa redio’ lakini
anachokifanya hakimsaidii mwandishi chipukizi kwa
sababu, anataja na kuelezea vitu muhimu
vinavyotakiwa ili uweze kuuandika mchezo wa
redio; lakini namna ya kuuandika hakuielezea.
Japokuwa ameandika mchezo wa Kusadikika
katika umbo la mchezo wa redio, lakini jambo hili
halimsaidii mwanafunzi kupata 'abc' za utunzi. Sisi
tutadokeza namna ambayo mwanafunzi wa
uandishi wa mchezo wa redio, ataitumia ili aweze
kuipangilia kazi yake, iwe ya mchezo wa redio.
Pamoja na kuzingatia vitu vitano alivyovitaja
Moshiro.
4.2 Mchezo wa redio:
Mchezo wa redio unatumia mlango wa fahamu wa
kusikia (masikio) ambao unapaswa umwezeshe
msikilizaji kuona, kuonja, kunusa, na kugusa.
Msikilizaji anapaswa akutanishwe na milango
mingine ya fahamu kupitia katika masikio yake.
2Moshiro Gervas, 1979, Michezo ya Kuigiza-10. Mchezo wa Redio
Kusadikika uk 1-7 . Tanzania Publishing House
Mchezo wa redio unatawaliwa na maneno mengi
ambayo yanakusudia kuelezea matendo mbalimbali
ili msikilizaji aweze kuona, kunusa, kuonja, kuhisi,
kupitia katika kusikia.
Kwa mfano, mazungumzo kati ya wahusika
wa mchezo wa redio yanapaswa yampatie
msikilizaji fursa ya kuona ‘akilini’ kinachoendelea;
na vilevile maelekezo ya msimulizi ambayo
yanaandikwa kwa hati ya kawaida na ambayo
msimulizi anayasema yanatakiwa pia yasaidie
kuipata picha halisi ya mandhari. Pia kuna
maelekezo ambayo yameandikwa kwa hati ya
mlazo haya yana kazi maalumu. Kazi ya maelekezo
haya ni kumwezesha mhusika (mwigizaji au
msimulizi) ili aingie kwenye uhusika wake. Ni
maelekezo ya jukwaani kama yalivyo kwenye
tamthiliya.
4.3 Ufundi wa fani:
1. Uwasilishaji wa mchezo wa redio una vipengele
vya kuzingatia ambavyo ni pamoja na:
(a) Wahusika kutofautishwa sauti zao ili ijenge
ukubalifu na kuaminika. Mathalani kusiwe na
wahusika ambao sauti zao zinafanana au
zinaelekeana. Mfano ni mchezo mmoja wa redio
ambao ulikuwa unarushwa na Redio ya Deusche
Welle huko mjini Borne
nchini Ujerumani
unaojulikana kama Tega Sikio Jenga Maisha
yako.
Ulipokuwa unaanza mchezo huu mwaka
2008, kulikuwa na wahusika wawili ambao ni mama
na mtoto, wahusika hawa walikuwa wote na sauti
nyembamba ambazo zinafanana kabisa na hakuna
namna yoyote inayomwezesha msikilizaji
kuwatofautisha na kuona ni watu wawili tofauti.
Ilikuwa ni vigumu kukubali kuwa ni wahusika wawili
au ni mmoja ambaye anatamka maneno ya
wahusika wawili (ambao ni mama na hapo hapo ni
mtoto). Huu ni udhaifu, haijalishi kuwa ukweli
ulikuwaje lakini kinachopaswa ni kuwatofautisha
wahusika ili sauti zao zisifanane na kuwawezesha
wasikilizaji kuwaona wahusika wawili wenye haiba
toifauti. Ni vema umri pia ukazingatiwa katika
kuteua wahusika. Yaani kama kuna mama na
mtoto, au mzee na kijana, au mwanamke na
mwanaume. Lazima sauti za watu hawa
zitofautiane kwa kuwa msikilizaji hawaoni kwa
macho bali ni kwa masikio, hivyo inapaswa
awezeshwe kuwaona watu hawa kupitia katika
masikio yake. Jambo hili linawezekana kwenye
usaili ambapo mkurugenzi atachagua
wahusika/waigizaji kulingana na umri, sauti n.k.
(b) Uandishi wake hautofautiani sana na ule wa
tamthiliya ila tofauti inakuja kwenye maelekezo ya
matendo mbalimbali. Katika mchezo wa redio,
maelekezo husomwa na mtu anayeitwa msimulizi
ambaye naye sauti yake lazima itofautishwe. Na
jinsi sauti yake ilivyo na anavyozungumza, laziwe
iwe katika nadharia hiyo ya kusimulia na sio
kuzungumza. Msimulizi anatakiwa asimulie na
msikilizaji aone kuwa ‘anasimulia’. Kinyume cha
maelekezo haya ya mchezo wa redio tunakiona
katika maelekezo ya tamthiliya ambako, maelekezo
haya humsaidia mhusika kuingia katika uhusika bila
maelekezo hayo kuyataja. Umeelewa?
(c) Utendekaji wa matukio mbalimbali
hutegemea sauti ambazo humwezesha msikilizaji
kuipata picha na hivyo kujiona anakiona kila kitendo
kinachofanywa na wahusika. Kwa mfano ni tukio
linalohusu mgeni kufika katika katika nyumba fulani.
Lazima isikike sauti ya mtu anayetembea, kisha
tusikie mlango ukigongwa, halafu tusikie mtu
akiitikia ‘karibu’ na kisha kusikia sauti ya mlango
unapofunguliwa, na kisha maongezi ya hao watu
wawili ambao wamekutana. Watasalimiana kwa
kutajana majina ili wasikilizaji wawaone kupitia
‘macho ya masikioni’.
(d) Msimulizi ndio kiungo cha matukio yote
yanayotendeka hasa ubadilishaji wa mandhari na
uongezekaji wa wahusika wapya. Msimulizi
anapaswa atuambie kuwa wahusika wako kwenye
mandhari gani, na mwonekano wa mandhari hiyo
ukoje. Kwa mfano, msimulizi akituambia kwamba,
tuko pwani na kuna mawimbi makali ya bahari.
Tutatarajia tusikie mvumo wa mawimbi hayo ukiwa
ni mkubwa au mdogo; na vikorombwezo vingine
vinavyofanya ukubalifu na uaminikaji wa masimulizi
yake, kuhusiana na anachotuambia. Sio atuambie
tuko katika mandhari ya ufukwe wa bichi mojawapo
halafu tuanze kusikia kelele za ng’ombe au kuku
wakiwika, hapana! Huu utakuwa ni uongo mkubwa!
(e) Kila mhusika anayezungumza hupaswa
kutaja jina la yule anayezungumza naye ili
kumfanya msikilizaji asipotezwe kwa kushindwa
kufuatilia na kujua ni nani anayezungumza. Kwa
hiyo, kuwe na namna ya kuwataja wahusika katika
mazungumzo yao; na vile vile msimulizi huifanya
kazi hii kama ni mhusika mpya anaingia katika
tukio. Yaani anaposema ‘x’ anakwenda nyumbani
kwa ‘y’ na kisha ndipo aendelee na simulizi. Au
mhusika mwenyewe anaweza kulitaja jina la
mhusika mwenzake wakati wa mazungumzo yao.
(f) Mandhari hutofautishwa na kutambulishwa
kupitia katika sauti zinazopatikana katika mandhari
hizo. Jambo hili ni kama tulivyoligusia katika
kipengele ‘d’. Lakini kutokana na umuhimu wake –
tutalijadili tena hapa kwakuwa ndio ‘moyo na uti wa
mgongo’ wa mchezo wa redioni. Tutatoa mifano
mbalimbali ili mada hii iweze kueleweka. Kwa
mfano, katika mandhari ya msituni - bila shaka sauti
za ndege hazitakosa kusikika. Au kama mandhari
ya katikati ya jiji hapa Dar es Salaam kwenye kituo
cha mabasi ya Daladala - kelele za wapiga debe na
milio ya honi na mingurumo ya magari haitakosa
kusikika na kadhalika. Mambo yote haya
humjengea msikilizaji picha ya mandhari na
kumfanya aone kila kinachoendelea.
Tutatoa mfano wa kuandika mchezo wa redio kama
ifuatavyo:
Msimulizi: Ni mchana wa jua kali siku ambayo
Tuma alikwenda kazini akiwa
amevalia suruali nyeusi, shati jeupe,
viatu vyeusi, na koti jeusi ambalo
alilivua baada ya kujihisi joto na
kulishika mkononi. Tuma anapofika
mlangoni, anagonga mlango na
kusubiri kidogo. Sauti inasikika ikiitikia
“karibu” na mlango unafunguliwa.
Beti: Karibu Tuma wangu. Pole sana kwa kazi.
Tuma: Asante Beti wangu. Habari za hapa?
Beti: Nzuri tu, habari za kazi?
Tuma: Safi tu.
Msimulizi: Baada ya Beti kumkaribisha Tuma na
kumpokea koti aliloshika mkononi, Tuma
anajitupa kochini na anachukua rimoti ya
kiyoyozi anawasha kiyoyozi. Anajifungua
vifungo vya shati lake na kisha
anajiegemeza kochini. Mara anachukua
rimoti ya runinga na anaiwasha na kutafuta
stesheni mojawapo.
Tuma: Nataka kuangalia taarifa ya habari.
Beti: (Anacheka Kidogo) He! Babu wewe, taarifa
ya habari mchana wote huu inatoka wapi?
Tuma: (Akionesha kukata tamaa) Ah! Nilidhani
kuna taarifa ya habari muda huu…
Beti: Kweli dunia imekupita. Taarifa ya habari
mchana huu?
Tuma: Nitalijulia wapi hilo bibi wewe wakati kila siku
mimi ni kiguu na njia?
Beti: Subiri saa moja au saa mbili usiku ndio kuna
taarifa.
Tuma: Basi naenda kujipumzisha kidogo. (Anapiga
mwayo) Maana nimechoka
kweli.
Beti: Nakutakia njozi njema babu wewe.
Msimulizi: Tuma anakwenda kulala (sauti ya nyayo
za mtu anayetembea harakaharaka
zinasikika na mlango unafunguliwa na
kufungwa) na Beti anaendelea
kutazama
runinga.
Muziki: (kunasikika muziki wa ala au wa taratibu
ukipigwa).
Pili, hatua inayofuata baada ya kuandika
mswada ni kuutengeneza ili uweze kurushwa
redioni. Moshiro katika ukurasa wa 9-13 anaelezea
namna ya utayarishaji wa mchezo wa redio
ambapo mwongozaji baada ya kuwasaili waigizaji
na kuwagawia husika zao, hutakiwa mwongozaji na
waigizaji wake kuusoma mswada wote na
kuuelewa. Kisha, mwigizaji mmojammoja anasoma
sehemu yake anayoiigiza na kuelewa uhusika wa
kila mmoja. Mazoezi hufuata ambayo hufanyika bila
kurekodiwa. Mwongozaji anaporidhika na mazoezi
yanayoendelea, zoezi la kurekodi onyesho moja
baada ya jingine hufuatia.
Kitu kingine alichokielezea Moshiro ni
nidhamu ya waigizaji ambayo inapaswa iwe ya hali
ya juu kwa kuwa, bila nidhamu kazi ya kuigiza
redioni itakuwa ni ngumu na sio rahisi.
4.4 Hitimisho
Sanaa ya uigizaji ina kaida na miiko yake kama
tulivyoona katika uandikaji na utengenezaji wa
mchezo wa redio. Jambo la msingi kwa mwigizaji
na mwongozaji ni kuwa na ushirikiano wa hali ya
juu ili kinachopendekezwa kufanywa, kiweze
kufanyika kwa usahihi. Kazi hii itawezekana kama
nidhamu ya kuwahi mazoezini itazingatiwa na
nidhamu kwa ujumla wake.
Jambo jingine kwa mwigizaji ni kufanya
utafiti ili aweze kuujua ‘uhusika’ anaouigiza. Kwa
kuujua uhusika kwa undani, itamwia rahisi mwigizaji
kuigiza kwa umahiri mkubwa.
SURA YA TANO
UANDISHI WA MISWADA YA TAMTHILIYA
Usuli wake
5.0 Tamthiliya
Tamthiliya ni andiko la kiuigizaji ambalo hutumia
wahusika wanaojibizana au wanaozungumza peke
yao ili kuwasilisha ujumbe wa mwandishi.
Tamthiliya ina mpangilio wake katika msuko wa
matukio ambao una sehemu tatu: mwanzo, kati, na
mwisho. Msuko huu ni muhimu kwa kuwa
unawezesha kujua kisa kilivyoanza, kinavyokua, na
kinavyohitimishwa. Katika sehemu ya mwanzo
ndipo utambulisho wa wahusika hufanyika na ni
sehemu ambayo wahusika huanza kukutana na
kuhusiana ili kujenga migogoro inayoaminika.
Katika sehemu ya kati, hapo ndipo kuna
kuwa na mgogoro au kutofautiana kwa mielekeo
ambako kunasababisha malumbano na hatimaye
mchezo unabadili mwelekeo, hicho kinaitwa kilele
au taharuki.
Sehemu ya mwisho wa mchezo ni pale
penye mshuko wa matukio. Katika sehemu
migogoro iliyokuwa ikifukuta inatatuliwa na
kuhitimishwa. Huo ni msuko wa kawaida ambao
unapatikana katika tanzu zote tatu za tamthiliya,
filamu, na michezo ya redio. (Aristotle; Semzaba).
5.1 Uandikaji wake:
Uandishi wa mswada wa tamthiliya una namna
yake inaoutofautisha na mswada wa filamu na
redio. Tutachunguza vipengele kadhaa vifuatavyo:
a) Kuna maelekezo kwa mwongozaji au
msomaji yanayomsaidia kuipata picha halisi ya
tukio linaloandamana na majibizano ya wahusika.
Maelekezo haya (stage directions) yanatakiwa
yawe katika hati ya mlalo na kwenye mabano.
Maelekezo haya yanatakiwa kuonekana mwanzoni
kabla ya kitendo husika hakijafanyika na sio baada
ya hapo. Mathalani unataka mhusika wako acheke
kabla hajaongea neno, itakubidi maelekezo hayo ya
kucheka yaje mwanzoni na ndipo acheke. Mfano
ukisema (Beti anacheka na kisha anamtazama
Tuma na kusema) Nakupenda
laazizi!
b) Maneno ya wahusika yanapaswa kuwa
katika hati ya kawaida ambayo siyo ya mlalo.
Majibizano haya yanafuata baada ya kutaja jina la
mhusika.
c) Majina ya wahusika yanaandikwa upande
wa kushoto wa karatasi (au tuseme mwanzo wa
ukurasa) na kisha maneno ya mhusika yatafuata
mbele ya jina lake.
d) Nukta pacha - hizi hutumika katika
kutenganisha jina la mhusika na maneno yake
anayoyatamka.
e) Majibizano ya wahusika yanapaswa kufuata
mara tu baada ya kuandika nukta pacha.
f) Onesho linaweza kuwa na sehemu au lisiwe
nazo. Likiwa na sehemu inabidi sehemu hizi
zijengwe kwa mfuatano unaoleta mantiki katika
ujenzi wa kisa au tukio. Wakati mwingine,
baadhi ya wasanii huliita onesho - kitendo; vilevile
kitendo kinaweza kuwa na sehemu au la. Kikiwa na
sehemu kifuate utaratibu kama tulivyoeleza hapo
juu. Kwa hiyo, unaweza kuwa na onesho la kwanza
lenye sehemu tatu ambazo ni: sehemu ya kwanza;
sehemu ya pilil; na sehemu ya tatu. Tutatoa
mfano wa kuandika mswada wa tamthiliya katika
ukurasa unaofuata.
5.2 Ufundi kuhusu fani
Ufundi huu hujumuisha mambo mengi pamoja na
mambo muhimu ya kumalizia shughuli nzima ya
kuubadili mswada ili uwe kitabu.
a) Jalada la tamthiliya litakuwa na jina la kitabu
ambalo linapaswa libuniwe kisanaa ili liweze
kujenga hamu ya msomaji kukinunua na kukisoma.
Jina lazima liwe na mvuto.
b) Rangi za jalada lazima zielekeane na
dhamira kuu inayojengwa katika kitabu. Rangi hizi
zinapaswa kutumika kwa malengo maalumu na sio
kinyume chake. Japokuwa wakati mwingine
mwandishi huchagua rangi kutokana na mvuto
wake na siyo maudhui! Mathalani katika uwanja wa
sanaa, rangi zina maana yake na matumizi yake
yanapaswa kutiliwa maanani. Rangi ya njano
inabeba dhamira ya wivu na ndio maana hata
katika filamu kukiwa na mhusika ana wivu kwa
mpenzi wake anaweza kumpa ua la rangi ya
manjano au anaweza kuvalia nguo za rangi hiyo.
Rangi nyekundu inafungamana na mapenzi
na ndio maana kuna kupeana maua mekundu au
kuvalia nguo nyekundu. Rangi nyeupe
inafungamana na utakatifu, usafi wa moyo, na
tabia. Rangi nyeusi inafungamana na uovu na
uchafu wa moyo na uasi. Haya yote ni katika
muktadha wa sana aza maonesho
Rangi ya buluu hasa ikiwa inatumika katika
chumba huleta mandhari ya kimahaba katika
chumba husika. Kwa hiyo, kila rangi ina maana
yake katika uwanja wa sanaa na haipaswi
kuzitumia mchafukoge. Kwa mfano, kama
tamthiliya inahusu maasi, uovu, na uchafu wa moyo
- rangi za jalida hazipaswi kuwa nyeupe kwani kwa
kufanya hivyo, itatathminiwa kuwa msanii
ameshindwa kutumia weledi wake. Au kama ni kwa
makusudi maalumu ya kuonesha ukinyume - ni
lazima isemwe tangu mwanzoni ili kazi itathminiwe
kwa haki.
(c) Kuna maelezo ya ndani kabla ya kufikia penye
tamthiliya yenyewe. Maelezo haya ni pamoja na:
ukurasa wa haki miliki ya mwandishi au
mchapishaji ikiambatana na mwaka
kilipochapishwa kitabu na kampuni ya uchapishaji
iliyohusika. Vilevile kuna ukurasa wa dibaji,
shukrani, utangulizi, na yaliyomo. Kipengele hiki
kinaweza kuandikwa mwisho mara baada ya
kuikamilisha tamthiliya yako.
d) Nyuma ya kitabu kunakuwa na blabu. Blabu ni
maelezo mafupi kuhusiana na wasifu wa mwandishi
na muhtasari wa kazi yake ambao utamfanya
mnunuaji wa kitabu avutiwe na kukinunua. Watu
wengine huweka maoni ya baadhi ya wasomaji
kuhusiana na kazi hiyo ambayo kwa pamoja
huongeza mvuto kwa mnunuaji wa kitabu, na
kupata hamu ya kukisoma.
5.3 Uwasilishaji wake:
Tamthiliya ni kazi inayokusudiwa kutendwa
jukwaani kwa hiyo maneno au majibizano ya
wahusika yalenge utendekaji na sio mahubiri.
(a) Tamthiliya haihitaji maneno mengi kama
mchezo wa redio kwa kuwa watu wanatazama kwa
macho yao na wanasikia maneno ya waigizaji. Kwa
hiyo hapo tunapata tofauti ya kazi hizi mbili. Kwa
mfano una wahusika wawili ambao ni wapenzi -
hebu tuangalie uwasilishaji huu:
(i) Beti: (Tuma anafungua mlango na mkononi
ameshika kofia lake, anaingia sebuleni.
Anamkuta Beti anaangalia runinga. Beti
ananyanyuka anampokea kofia Tuma na
analiweka mezani) Karibu
laazizi.
Tuma: Asante asali wangu. (Anaketi.
Wanatazamana). Habari
za hapa?
Beti: Nzuri tu, za kazi?
Tuma: Safi.
Hebu angalia uwasilishaji mwingine huu hapa chini
kati ya Beti na Tuma.
(ii)Beti:(Tuma anafungua mlango, mkononi
ameshika kofia lake, anaingia sebuleni.
Anamkuta Beti anaangalia runinga. Beti
ananyanyuka na kumpokea kofia Tuma na
kuliweka mezani). Hebu
nikupokee hili kofia
lako na niliweke hapa mezani. Karibu laazizi.
Tuma: Asante asali wangu. (Anaketi). Hebu nikae
kwanza. (Wanatazamana). Habari za hapa?
Beti: Nzuri tu, za kazi?
Tuma: Safi.
Mfano huo mmoja unatosha kuonesha kuwa
utanzu wa tamthiliya haupaswi kuwa na maneno
yote hayo. Matendo yaonekane kupitia vitendo na
sio kusimulia vitendo hivyo. Maneno yote hayo
yangefaa kama ingelikuwa ni katika utanzu wa
mchezo wa redio. Kwa hiyo, ukiangalia majibizano
ya wahusika Beti na Tuma katika (i) na (ii) yaliyopo
hapo juu, yale yaliyopo katika (i) ndiyo bora; na yale
yaliyomo katika (ii) ni uwasilishaji mbovu wa
tamthiliya.
(b) Kila sehemu ya tukio inapobadilika hapo
tayari kuna matukio mawili na sio moja. Kama
onesho lilikuwa linafanyikia sebuleni, mhusika
akinyanyuka na kuingia jikoni - tayari hayo ni
maonesho tofauti na yanapaswa kutochanganywa.
Jambo hili pia linatofautisha tamthiliya na igizo la
runinga au mchezo wa redio.
5.4 Historia ya Tamthiliya ya Kiswahili
Kwa mujibu wa Edwin Semzaba, tamthiliya ya
Kiswahili ilianzia kwenye sanaa za maonesho za
jadi ambazo zililenga kusaidia jamii katika mambo
mbalimbali. Sanaa hizi za maonesho za jadi ni
kama vile ngoma, maigizo simulizi ya (watoto, au
watani wakati wa misiba); sherehe za kuzaliwa
watoto na kutoa majina; sherehe za jando na
unyago; majigambo, na utani; na kadhalika.
Matendo haya yalikuwa ni ya dhati kutokana na
jukumu lililokuwepo katika jamii.
Baadaye matendo haya ya dhati
yaliondolewa kutoka katika udhati wake na
kufanywa kuwa maigizo ya matendo hayo (yakiwa
ni maigizo ujue kuna masihara ndani yake); ni
kama vile waigizaji wanafanya sherehe za jando na
unyago jukwaani, au kwenye mchezo wa redio,
runinga, au kwenye filamu. Yale wayafanyayo siyo
ukweli wenyewe bali ni mwigo wa ukweli huo.
Chanzo kingine kilichofanya tamthiliya ya
Kiswahili ichipuke ilikuwa ni wakati wa ukoloni
ambapo Waingereza walikuja na drama zao
(tamthiliya za William Shakespeare ambazo
ziliingizwa mashuleni). Wanafunzi walitakiwa
kuigiza tamthiliya hiyo katika siku ya kufungua
shule; siku ya wazazi; au wakati wa mashindano
ambapo shule mbalimbali za sekondari
zilishindanishwa na mshindi alipewa zawadi.
Baadaye Watanzania waling'amua kuwa
michezo hiyo ya kuigiza haikuyahusu maisha yao
na hata kilichokuwa kikiongelewa hawakukielewa.
Kutokana na matumizi ya lugha ya Kiingereza;
kilichowavutia ilikuwa ni uigizaji, uvaaji wa mavazi
maalumu; matumizi ya taa; majukwaa maalumu ya
kuigizia; na utamkaji wa maneno ya Kiingereza.
Watanzania wakaanza kutengeneza sanaa
zao zenye mwelekeo wa kidrama. Wakatumia
vichekesho ili kuwacheka washamba mbalimbali
ambao walikuwa hawajua tamaduni mpya za
Kizungu ambazo zilikuwepo katika jamii.
Vichekesho kama Mshamba wa Kioo vilishika kasi
katika jamii yetu. Vichekesho vililenga kuwacheka
Waafrika ambao bado walikuwa ni washamba
kutokana na vitu vya kigeni ambavyo vilikuwepo
katika jamii na waliojua kuvitumia ni wale werevu
(wasomi) waliosoma katika shule za Wazungu.
Baadaye dhima ya vichekesho ilibadilika
kwa wasanii kutunga vichekesho vinavyowacheka
Wazungu weusi ambao walionekana ni
malimbukeni. Huu ulikuwa ni wakati wa kujitambua
na kudai ukombozi wa Bara la Afrika na Tanzania
ikiwemo. Vichekesho vikaacha kuwadhihaki
Watanzania ambao hawajui mila na tamaduni za
Kizungu - na vikaanza kuwacheka Waafrika ambao
walijifanya Wazungu-weusi.
Baada ya baadhi ya wahitimu kumaliza
shahada ya chuo kikuu cha Dar es Salaam,
wakaanza kuandika tamthiliya zenye mwelekeo wa
drama za Wazungu. Tamthiliya za Penina Muhando
kama vile Hatia, Heshima Yangu; na za Ibrahim
Hussein kama vile Wakati Ukuta na Kwenye Ukingo
wa Thim; tamthiliya za Semzaba
Ngoswe Penzi
Kitovu cha Uzembe na
Tendehogo (kwa kuzitaja
kwa uchache) zikafuata mwelekeo wa drama za
Kizungu. Tamthiliya hizi zilizingatia vipengele vya
tamthiliya kama vilivyotajwa na Aristotle yaani:
maudhui; ploti; uteuzi wa lugha; wahusika; kionwa;
na muziki vikatiliwa maanani sana.
Kisha, wasomi hawa kwenye miaka ya 1980
na kuendelea, wakaanza kubadili mawazo yao na
kutaka kutunga Tamthiliya za Kitanzania ambazo
zitajumuisha sanaa za maonesho za Kiafrika
(sanaa za jadi) katika utunzi wa drama hizo. Ndipo
mabadiliko haya yakatupeleka kwenye tamthiliya
kama: Lina Ubani na Nguzo Mama (Penina
Mlama); Mkutano wa Pili wa Ndege (Amandina
Lihamba); Jogoo Kijijini na Ngao ya Jadi (Ebrahim
Hussein); Kija (Shani Kitogo); Safari ya Chinga
(Shani Omari), na Changamoto (Elizabeth Godwin
Mahenge) kwa kuzitaja kwa uchache tu. Tamthiliya
hizi zilichanganya miundo ya tamthiliya za Kizungu
na vipengele vya sanaa za maonesho za Kiafrika
katika kutunga tamthiliya ambazo tunajivunia
kusema kuwa ni 'Tamthiliya za Kitanzania
barabara'.
Watunzi hawa wa tamthiliya walipoanza
kutunga kazi zenye mwelekeo wa Kiafrika, kukawa
na mwamko katika kumbo zingine za fasihi andishi
ambayo ni ushairi wa Kiswahili. Ni kipindi hiki ndipo
mgogoro wa ushairi ulipozuka, ukipambanisha
washairi wa kimapokeo na washairi wa kisasa.
Mgogoro wao ulijikita katika hoja ya uasili wa
ushairi kwamba, mwingine ndio ulikuwa na asili ya
Kiafrika na mwingine ulikuwa ni mwigo wa tungo za
Kimagharibi. Si hivyo tu, bali kipindi hiki ndipo
tunapoona fasihi ya majaribio ikijichomoza. Ni
majaribio ambayo pia yalijitokeza katika kumbo ya
tamthiliya.
Hivyo, kwa mujibu wa Semzaba, tamthiliya
ya Kiswahili inaweza kuwekwa katika vipindi vinne:
Kabla ya ukoloni (sanaa za maonesho za jadi);
wakati wa ukoloni (vichekesho na drama za
Kizungu); baada ya ukoloni na wakati wa Azimio la
Arusha (1960's-1990's); wakati wa vyama vingi vya
siasa (1995 na kuendelea).
5.5 Vipengele 6 vya Tamthiliya
Tamthilia ni utanzu wa sanaa za maonesho ambao
uliletwa na wakoloni wakati wa ukoloni. Kabla ya
ukoloni, jamii yetu ilikuwa na tamthiliya ambazo ni
za ufaraguzi (yaani ambazo zilitungwa bila
kuandikwa) na waigizaji walichukua husika
mbalimbali. Wakati wa ukoloni, mambo yalibadilika
kidogo ambapo, wakoloni wa Kiingereza walitafuta
namna ya kujiburudisha na kukumbuka nyumbani
kwao Ulaya. Katika kutimiza hilo, wakaleta
tamthiliya za Shakespear ambazo ziliigizwa na
Watu wa Afrika Mashariki.
Baadaye, tamthiliya ya Kiswahili ilitumia
tafsiri kwa kuwa baadhi ya tamthiliya za
Shakespear zilitafsiriwa kama vile Juliasi Kaisari
(Mwalimu Nyerere) na Mfalme Edipode (Mushi).
Tamthiliya hizi kwa Kiswahili zilileta changamoto
kwa wasomi na waandishi wa Kiafrika na hapo
wakaanza kutunga tamthiliya zao kwa kutumia
muundo wa tamthiliya za Ulaya. Hadi kufikia hatua
hiyo, tamthiliya ya Kiswahili ilikuwa imeshazaliwa.
Kwa mujibu wa Aristotle ambaye ni gwiji
katika fani hizi za sanaa za uigizaji alitaja vitu sita
muhimu ambavyo vinatakiwa viwepo ili utanzu
uweze kupewa hadhi ya kuitwa tamthiliya (drama).
Vipengele hivi ni pamoja na: muziki, kionwa,
maneno/dayolojia, wahusika na uhusika, dhamira,
na msuko wa matukio. Tutaangalia kipengele
kimoja baada ya kingine ili tuweze kuelewa vizuri.
5.5.1 Msuko wa Matukio/Ploti
Ploti au msuko wa matukio ni ile namna ya
mpangilio wa kisa katika simulio. Msuko huu
unaweza kuwa wa moja kwa moja au unaweza
kuwa wa urejeshi. Jambo la msingi kwa
mwongozaji wa mchezo wa kuigiza ni kuelewa
msuko huo ili aweze kuwaelekeza waigizaji wake
waweze kuiwasilisha dhamira ya mwandishi kwa
ufanisi.
Msuko wa matukio/ploti (au kisa) ni lazima uwe
na mwanzo, kati, na mwisho; lakini si lazima kwa
mchezo kufuata huo mpangilio, na ndio maana
tumetaja kuna namna mbili za kuwasilisha hadithi
(ama moja kwa moja au kwa mrejesho). Ploti ina
mwanzo, kati na mwisho.
MWANZO
Katika sehemu hii ya mwanzo, mwandishi anajaribu
kutambulisha mahusiano kati ya wahusika ili
ikitokea mtazamaji anaona hawapatani – swali hilo
liweze kujijibu kutokana na mwanzoni ilivyoonesha
wasifu wa kila mhusika. Mathalani tunaoneshwa
kuna wahusika ambao ni ndugu wa kuzaliwa (yaani
kaka wawili ambao wamezaliwa na baba mmoja na
mama mmoja, kaka hawa wanapendana sana na
haiwezi kufikiriwa kuwa wanaweza kugombana).
Pia katika sehemu hii ndipo tunapotambulishwa
mandhari ya mchezo husika ni wapi; na vilevile
tunaweza kujua mwelekeo wa kazi husika kama ni
ya huzuni, majonzi, mapenzi, au vita.
KATI
Sehemu hii ya kati ndio ile inayokuza mgogoro.
Mgogoro huu unakuzwa kwa kuonesha mielekeo
tofauti ya wahusika na hata yale mambo
wanayoyasimamia. Tuchukulie mfano wa hao kaka
wawili ambao wanaelewana sana na kupatana;
kwamba, itokee wanachangia mwanamke (yaani
mmoja awe na rafiki yake wa kike halafu yule
ndugu wa pili naye aingie hapohapo). Hebu fikiria
hawa ndugu watakuwa katika hali gani? Je, kule
kupendana kwao kutaendelea vilevile? Jibu ni
hapana, na katika jibu hili ndipo tunapoweza kuona
mgogoro ukikua na hata kaka hawa kudiriki
kufanyia matukio mabaya.
Inawezekana mmojawapo akapanga kumwua
mwenziwe. Katika harakati hizi za kuuana ndipo
mchezo unapofikia kwenye kilele chake na
mwelekeo wa mchezo utabadilika – tukikumbuka
ulianza vizuri kwa akina kaka hawa kupendana –
sasa tunaona ni maadui wa kutupwa.
MWISHO
Sehemu hii sio lazima iwe suluhisho kwani kuna
matatizo ambayo ni magumu na mwandishi
huyaepuka kutoa suluhisho ambalo linaweza
kuonekana ni la uongo. Tunaweza kusema kuwa,
sehemu hii ni ya hitimisho la kisa. Kama mkasa au
kisa kilisababisha ndugu hawa kuuana – je, ikitokea
kweli mmoja akafanikiwa kumuua nduguye, je
mahusiano yake na yule msichana yatakuwaje; na
mahusiano yake muuaji na familia, au marafiki zake
yatakuwaje? Katika kupata majibu ya maswali
haya, ndipo tunapoweza kuona mshuko wa mkasa
na inaweza kuwa ndio mwisho wa mchezo.
Kwa hiyo, ni jambo la msingi kabisa kwa watunzi
wa kazi za kiubunifu wazingatie msuko wa matuki
na sio kukurupuka na kuandika visa visivyo na
mzizi. Mathalani, hapa nyumbani kuna baadhi ya
drama au filamu ambazo zikichezwa hadi
unashangaa kuwa hawa watu wanajua watendalo
au wamedandia gari kwa mbele. Utakuta kunaibuka
tu mgogoro ambao chanzo chake hakiko bayana na
hivyo kuondoa ukubalifu na uaminikaji wa jambo
husika mbele ya macho ya hadhira (believability).
5.5.2 Wahusika na Uhusika
Wahusika ni nyenzo inayomwezesha mwandishi
kufikisha ujumbe wake kwa hadhira aliyoilenga.
Kuna wataalamu wamejadili kuhusiana na dhana hii
ya wahusika. Tutawadondoa hapa chini ili tuweze
kueleweka.
Kwa mujibu wa Kamusi ya Fasihi, Istilahi, na
Nadharia, mhusika ni:
Kiumbe anayepatikana katika kazi ya kifasihi na
ambaye anafanana na binadamu kwa kiasi fulani.
Wasifu wa mhusika unategemea mkabala uliopo.
Kazi zinazoegemezwa katika mitazamo ya kihalisia
zinamsawiri mhusika kwa namna inayokaribiana sana
na binadamu katika ulimwengu wa kawaida
(Wamitila, 2003 uk.123).
Brockett (1964) kwa upande wake anaelezea kuwa
mhusika ni kitu muhimu sana katika msuko wa
matukio ya hadithi. Msuko huu huweza kuelezwa
kupitia migogoro na matamanio tofauti tofauti ya
wahusika, ambao kwa kutumia mazungumzo na
tabia zao tofauti huwezesha kuukuza mgogoro.
Brockett anaeleza sifa za aina nne za mhusika
kuwa ni: za kimaumbile, za hali ya kisaiolojia, za
nafasi yake katika jamii, na za kimaadili.
Kimaumbile – tunaangalia: je,
mhusika
anaonekanaje kiumbo ? Je, ni mnene au
mwembamba? Je, ni mweupe au mweusi ? Je, ni
mfupi au mrefu. Kisaikolojia mhusika anatazamwa
hali yake ya kiakili – je anapenda nini na hapendi
nini? Kijamii mhusika anatazamwa kuwa anafanya
kazi gani – je ni mkulima, mwalimu,
mfanyabiashara, mchungaji na kadhalika.
Kimaadili - mhusika
anachunguzwa namna
anavyoweza kufanya uchaguzi au uamuzi wa
jambo moja kati ya mawili ambayo yako mbele
yake (Brocckett, 1964 uk.30).
Kutokana na maelezo hayo hapo juu,
inaonekana kuwa dhana ya uhusika na dhana ya
uigizaji haitofautishwi. Wamitila (2003) na Brockett
(1964) wanamjadili mhusika kuwa ni kiumbe (mtu)
lakini hawaongelei lolote kuhusu mhusika kama
mashini, mnyama, mawe, na viwakilishi vingine
ambavyo si binadamu. Hata hivyo, dhana ya
uhusika ni ya jumla na dhahania zaidi
ikilinganishwa na dhana ya uigizaji ambayo ni
mahususi. Mwigizaji ni lazima awe binadamu, lakini
mhusika si lazima awe binadamu. Dhana hii na
utofauti uliopo ni mambo muhimu katika
kuchambua wahusika wa kazi za kimaandishi kama
tamthilia ; na waigizaji ni muhimu katika kazi za
utendaji kama drama na filamu. Maana na tofauti
hizi za wahusika na waigizaji zimefafanuliwa wazi
katika nadharia ya usimulizi
Scholes na Kellogg (1966) wanaelezea
dhana ya uhusika katika nadharia ya usimulizi kuwa
haiwezi kutenganishwa na usimuliaji wa tukio katika
hadithi. Mhusika ni nyenzo anayoitumia mwandishi
ili kusimulia tukio au jambo fulani. Scholes na
Kellogg (1966 :160) wanasema:
Mhusika ni kitu gani kama sio kiwakilishi cha tukio?
Tukio ni kitu gani kama hakitafafanuliwa kupitia
mhusika? Je picha ni kitu gani au novela (riwaya) ni
nini pasipo kuwepo mhusika? Je ni kitu gani tutakuwa
tunakitafuta kwenye riwaya au picha kama
hatutatumia au kuwahusisha wahusika?...
Hoja inayowasilishwa na (Scholes na Kellogg,
1966) inadhihirisha kuwa si rahisi kuelezea dhana
ya uhusika pasipo kuelezea tukio linalotendwa; si
rahisi kutenganisha tukio na mhusika katika
simulizi, vitu hivi vinajengana na kutegemeana.
Wahusika na tukio ni kama pande mbili za sarafu
moja ambazo haviwezi kutenganishwa.
Kwa mujibu wa (Bal, 1985), uhusika na
uigizaji ni dhana mbili ambazo hazina budi
kutofautishwa. Dhana moja inajikita katika kueleza
ujumla wa mambo, ikihusishwa na matendo (au
tukio); na nyingine ikieleza jambo mahsusi.
Mhusika ni wakala ambaye anafanya matendo
fulani. Mhusika si lazima awe binadamu, lakini
lazima awe mtendaji (Bal, 1985, uk5).
Uhusika ni istilahi inayojumuisha wigo
mpana (au wa jumla) kuliko ilivyo kwa istilahi finyu
ya uigizaji. Kwa maneno mengine, mbwa, mashini,
na kitu chochote kisicho binadamu kinaweza kuwa
mhusika na sio kinyume chake. Kwa upande
mwingine, mwigizaji anafafanuliwa katika nadharia
hii kama kiumbe ambacho kinasimama badala ya
kitu kingine katika usimulizi. Kiumbe hiki awe ni
binadamu au la, hupewa sifa za binadamu ili
kukamilisha usimulizi. Mwandishi anawezesha
kumpa mwigizaji sifa (wasifu) kwa kutumia
ufafanuzi ambao unamfanya mwigizaji aweze
kuvaa sura ambayo inamfanya afanane na
binadamu halisi kwa kuwa na haiba, saikolojia, na
itikadi (Bal, 1985 uk. 115).
Kwa hiyo, mhusika hupewa wasifu wa aina
mbalimbali ili dhana ya uigizaji iweze kupatikana.
Jambo hili linafanywa na mwandishi kwa uteuzi
maalumu ili jambo analotaka kuliongelea liweze
kuiwakilisha jamii anayoisemea. Na kwa hiyo hapa
tunaona hatua tatu muhimu ambazo ni: mwandishi,
wahusika wake na jamii, hatua hizi zinatokeza
uigizaji anaoufanya mwandishi kupitia katika kazi
yake.
“Dhima za wahusika kinadharia si za mtunzi
binafsi bali ni miundo inayopatikana katika jamii
kwa ujumla” (Wafula na Njogu, 2007 uk.16). Ukweli
huu unadhihirisha mambo mawili katika nadharia ya
naratolojia. Kwamba, mtunzi anajiondoa yeye na
kuwafanya wahusika kusema kwa niaba yake; na
pili ni kuwa, wahusika wenyewe hawajisemei wao
kama wao, bali pia wao kama wawakilishi wa jamii
wanamotokea. Upekee wa lengo la mwandishi
unajitokeza kwa jinsi anavyochagua mhusika wa
kumsemea na kuisemea jamii na kumpa mhusika
huyo lugha inayoendana na dhima yake.
Wakiandika kuhusu “Freud, Ndoto na Fasihi”
Wafula na Njogu (kama ilivyotajwa hapo kabla)
wanasema:
Nao wahusika wanaopatikana katika fasihi ni
wanadamu wanaoishi katika ndoto na njozi za
mwandishi. Hawa ni kama vile wanadamu wa kweli
wanaoshirikiana na mwandishi katika matatizo na
matarajio yake” (Wafula na Njogu, 2007 uk 79).
5.5.3 DHAMIRA
Dhamira ni yale yazungumzwayo katika kazi ya
sanaa; ni lile wazo; au hoja; au jambo ambalo
linajadiliwa na mwandishi. Mathalani, katika
tamthiliya ya Machozi ya Mwanamke iliyotungwa na
Ibrahimu Ngozi (1977), inahusu ukombozi wa
mwanamke kutoka katika uonevu wa mwanaume.
Tutathibitisha jambo hili kupitia katika sehemu ya
utangulizi ambayo aliiandika mwandishi
mwenyewe. Mwandishi anasema:
Mwaka 1975, ulitangazwa na Umoja wa
Mataifa kuwa ni mwaka wa kina mama.
Wanawake wapate haki zaidi na usawa kati
yao na wanaume. Kwetu sisi Watanzania
wanawake walio wengi wako vijijini. Hivyo
basi itakuwa ni kujidanganya iwapo kama
tutapiga kelele juu ya ukombozi wa
mwanamke tukimfikiria mwanamke afanyaye
kazi mjini tu, kwamba apate madaraka zaidi
na nafasi zaidi za kuonesha uwezo wake, hali
tukimsahau kabisa, mwanamke aliye kijijini,
akigandamizwa, kunyanyaswa, na kuonewa
na mwanaume miaka nenda rudi!
(Ngozi, 1977uk. iii).
Kutokana na nukuu hiyo hapo juu,
tunaweza kuiona dhamira ya mwandishi ambayo
inaweza ikawa na vijidhamira vidogodogo ambavyo
vinasaidia katika kuijenga. Kila kazi ni lazima iwe
na ujumbe,dhamira, wazo, hoja, au jambo ambalo
linaongelewa. Bado hakujawahi kuwa na ‘sanaa
kwa ajili ya sanaa tu’ (art for art sake) – kila sanaa
inao ujumbe au inayo dhamira inayoongelewa na
mwandishi.
5.5.4 MANENO/DAIOLOJIA
Maneno au daiolojia ndio roho ya mchezo wa
kuigiza. Mchezo wa kuigiza wa redioni unahitaji
maneno mengi kwa kuwa lengo ni kuwafanya
wasikilizaji waone yale yanayoigizwa kulingana na
muktadha huo; kwa hiyo kuna uzungumzaji mwingi
katika michezo ya kuigiza ya redioni.
Michezo ya kuigiza ya jukwaani inapaswa
iwe na daiolojia inayosaidia kusukuma mchezo
mbele. Hakupaswi kuwa na mahubiri ambayo
yatalenga kuelezea au kusimulia jinsi matendo
yanavyofanyika – hapana! Mchezo wa kuigiza wa
runinga au jukwaani hauhitaji maneno mengi- bali
unahitaji maneno machache ambayo yatakuwa
yanausukuma mchezo na hivyo kuendelea mbele
na sio ‘gari kukwama kwenye mchanga’.
Kwenye filamu ndio kabisa haitaki maneno
mengi- kinachotakiwa ni matendo (picha) ieleze
hadithi na sio maneno. Kwa ujumla, maneno ni
muhimu katika fani hii ya uigizaji ila inategemea
kinachoigizwa ni kwa ajili ya nini – je ni kwa ajili ya
redio? Runinga? Au filamu?
5.5.5 MUZIKI
Muziki kwa mujibu wa Kamusi ya Kiswahili Sanifu
(2000:268) ni mpangilio wa sauti za ala, uimbaji au
vyote viwili, unaoleta athari fulani kwa kiumbe;
wimbo. Muziki katika dhana nzima ya uigizaji sio tu
zile sauti ziimbwazo pamoja na mapigo ya vyombo
(ala za muziki) - hapana! Muziki unajumuisha
mpando na mshuko wa sauti za waigizaji pale
wanapojibizana katika kuifanya drama isonge
mbele.
Vilevile ule utofauti wa sauti za waigizaji
kama vile: sauti kali, ya juu, nzito; na kwa upande
mwingine sauti ya upole, nyororo, na nyembamba
hufanya mazungumzo yanoge katika igizo. Hali hii
inathibitisha umuziki uliopo katika uigizaji. Kwa hiyo
katika uigizaji, dhana ya muziki ni pana zaidi kuliko
ilivyo finyu katika muktadha wa uimbaji.
5.5.6 KIONWA
Kionwa ni dhana inayojumuisha vile vitu vyote
vinavyoonekana jukwaani vikimsaidia mhusika
kuutoa ujumbe unaotakiwa. Ni kila kitu kilichopo
jukwaani ambacho kinawezesha igizo kutendeka.
Tunaweza kujumuisha mavazi, vifaa vya kushikwa
au kutumiwa na waigizaji katika husika zao, na hata
maleba; vyote kwa pamoja vinaunda dhana hii ya
kionwa.
Kionwa au vionwa vinapaswa vitumike
kulingana na sababu husika kwa maana kuwa,
mhusika hapaswi kubeba au kushika kifaa
ambacho hakitamsaidia kuuvaa uhusika wake na
kutoa ujumbe uliotarajiwa. Kama mhusika
anaonekana akibeba kibuyu – lazima kuwe na
sababu ya yeye kubeba kibuyu hicho; na sio kama
inavyotokea katika sanaa zetu za hapa nyumbani –
ambazo utamwona mhusika katika kila onesho
amebeba manati au ameshika kibuyu ambacho
hakitumiki katika onesho. Mambo haya yanafanyika
isivyo – hakuna budi kubadilisha na kufanya kama
taaluma ya uigizaji inavyotaka na kuelekeza.
5.5.7 Hitimisho
Vipengele sita vya tamthiliya ni muhimu sana katika
sanaa yoyote ya maonesho. Hivyo mwanasanaa
hana budi kuvielewa vipengele hivi kwa undani na
kuvizingatia atungapo kazi yake; au aingiapo
kwenye uhusika wakati wa kuigiza.
5.6 Aina za Tamthiliya
Tamthiliya ni mtu akiwa kitendoni (Semzaba, 1997);
au kwa maneno mengine, tamthiliya ni umithilishaji
wa maisha ya binadamu katika jukwaa. Tamthiliya
ni pale msomaji anapofungua ukurasa wa kitabu na
kuisoma – inapokuwa inachezwa, sio tamthiliya
tena, bali ni drama. Drama hii inaweza kuwa katika
maumbo mbalimbali kama vile: mchezo wa
jukwaani, mchezo wa kwenye runinga, mchezo wa
kwenye redio, au filamu.
Tamthiliya iko katika makundi mawili ambayo ni
ramsa na tanzia. Tutatumia maarifa tuliyoyapata
darasani wakati Mwalimu Edwin Semzaba (wa
Idara ya Sanaa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam) na
Daktari Aldin Mutembei (wa Idara ya FAMU Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam) walipokuwa
wakifundisha mada ya tanzia na ramsa. Kwa kiasi
kikubwa, mada hizi zimechukua maarifa yao kwa
kuwa nilikuwa mwanafunzi wao na hivyo nikajifunza
kutoka kwao.
5.6.1 TAMTHILIYA YA KIRAMSA
Tamthiliya ya kiramsa au kikomedia inatakiwa
onesho lake liivutie akili. Yaani onesho hilo lisivutie
hisia au mihemko. Chukulia mfano wa tamthiliya ya
AMEZIDI, ambayo inavutia
akili na kujiuliza
‘mantiki’ ya mambo wafanyayo wahusika.
Sifa nyingine ya ramsa ni lazima kuwe na
matendo yanayotendwa bila ya kufikiria. Lengo la
kufanya matendo bila kufikiria ni kwa ajili ya
kumcheka mhusika kutokana na upumbavu
wakewake.
Sifa ya tatu ya komedia ni kuwepo na desturi au
mila ambazo hadhira inazifahamu kutoka katika
jamii yake ambazo zinazodokezwa katika onesho.
Kwa mfano ni katika onesho la Mizengwe la
Jumapili, ambapo Mjumbe wa Nyumba kumi
(kiongozi wa watu) anavyoshikwa kwa ugoni na
wake za watu ambao anawatongoza kwa nyakati
tofauti. Kwa hiyo, mila na desturi za jamii husika
zinaona uzinzi kuwa ni kitendo kiovu. Kwa hiyo
kuna ucheshi kwa watakaokamatwa na tukio hili.
Anapokamatwa na kupigwa, hadhira haimwonei
huruma bali itamcheka.
Sifa ya nne ni kuwa, mazingira ya onesho na
vipengele vyake visiwiane au kupatana. Hii ina
maanisha kuwa, ile ploti haina nafasi katika ramsa.
Na ndio maana kila juma kuna mkasa tofauti katika
vipindi hivi vya ramsa za runingani ambazo hazitoi
mwendelezo wa visa. Tazama Ze Comedy au
Origino Comedí, Mizengwe, na Futuhi.
Sifa ya tano ni kutokuwaogopesha hadhira.
Inatakiwa kuwa, hadhira inapoangalia isiogope au
kupata uchungu bali icheke kwa kejeli kutokana na
ama tabia mbaya au matendo mabaya ambayo
mhusika anayatenda (Mwalimu Edwin Semzaba,
Idara ya Sanaa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam;
Prof. Aldin Mutembei wa Idara ya FAMU Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam)
5.6.2 Sifa za Shujaa wa Kimramsa
Sifa za shujaa wa kiramsa ni pamoja na:
- Asiwe mtu maarufu katika jamii. Anaweza kuwa ni
kichaa au mwendawazimu fulani ambaye yuko
katika jamii.
- Awe ni mtu duni katika jamii lakini matendo yake
ni ya kiucheshi-ucheshi. Mtu huyu historia humlea
na kumkuza hata akatokea kuwa “fulani” katika
jamii na akaishi raha mustarehe.
- Anatakiwa awe mhusika wa kufurahiwa na
watazamaji kutokana na mafanikio yake. Mhusika
ambaye akifanikiwa kila mtu atafurahia na baada ya
igizo atakuwa ameridhishwa na mwisho huo mzuri
wa kuishi raha mustarehe. Lengo ni kuwafanya
hadhira watue mioo yao baada ya kumwona
mhusika anafanikiwa na kuishi raha mustarehe.
Katika ramsa haitakiwa kuwachosha hadhira kwa
kuwatwisha huzuni katika nyoyo zao (Mwalimu
Edwin Semzaba, Idara ya Sanaa Chuo Kikuu cha
Dar es Salaam; Prof. Aldin Mutembei wa Idara ya
FAMU Chuo Kikuu cha Dar es Salaam).
5.6.3 Uhusika wa Wahusika wa Kiramsa
- Wahusika wanaotakiwa kuonekana katika kazi ya
kiramsa ni watu wa kawaida ambao wana kipato
cha kati na chini kama vile: washona viatu, wauza
mitumba, wakata nyama, wachoma mishikaki,
wanafunzi, walimu, wasukuma mikokoteni, n.k.
Tamthiliya ya kiramsa haihusu watu wa juu ambao
ni wafalme, au malkia, au viongozi. Kwa ujumla,
ramsa haihusu watu wote wa nasaba BORA badala
yake ni wale wa nasaba DUNI (Mwalimu Edwin
Semzaba, Idara ya Sanaa Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam; Prof. Aldin Mutembei wa Idara ya FAMU
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam).
5.6.4 Dhamira za Kiramsa
Tamthiliya za kiramsa zinahusu mambo ya kawaida
ya watu duni katika jamii. Miongoni mwa dhamira
hizo ni: kufanikiwa kimaisha, kupata marafiki wapya
au kurudisha wa zamani, kupanda cheo n.k.
Tazama komedia zinazooneshwa kwenye runinga
utapata dhamira za kutosha za ramsa. Kwa hiyo
kinachoangaliwa katika ramsa ni mafanikio ya
mhusika ambaye alikuwa hafanikiwi; na mwishilizo
mzuri wenye furaha na kicheko (Mwalimu Edwin
Semzaba, Idara ya Sanaa Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam; Prof. Aldin Mutembei wa Idara ya FAMU
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam).
5.6.5. Aina za Ramsa
1) UTANI/ VICHEKESHO
Utani ni aina mojawapo ya ramsa ambayo inalenga
kuchekesha kwa kugeuza mambo ili yawe kinyume;
kuvaa vinyago ili kuchekesha watazamaji. Lengo ni
kuchekesha na maana hupatikana humohumo.
2) MAHABA/ MAPENZI
Aina hii ya ramsa inahusu mapenzi au mahaba.
Kinachofanyika hapa ni kuwawekea vikwazo
wahusika ili wasifanikiwe. Vikwazo vinaweza kuwa
ni pamoja na umaskini, utajiri, ulemavu, ukabila,
udini nk. Lakini wapendanao hawa hufanya mambo
ya kuchekesha ambayo hatimaye huwawezesha
kufanikiwa kutimiza malengo yao.
3) TASHTITI/ DHIHAKARamsa
ya kitashititi ni zile kazi zinazolenga
kuwadhihaki viongozi wa kisiasa, au kidini kutokana
na matendo yao. Kwa mfano zamani Original
Comedy (akina Joti) ilipokuwa ikirusha vipindi
vyake kupitia East Africa Television (EATV).
- Pia tashititi huhusisha hudhihaki wahalifu,
matapeli, wanafiki, wala rushwa, wafanya
magendo, waongo n.k. Kwa hiyo, katika aina hii ya
ramsa, kiongozi ambaye ni mhusika mkuu mwenye
tabia hizo mbaya, anadhihakiwa ili aache. Kwa
mfano, kama kiongozi anapenda ‘dogodogo’ yaani
watoto wa shule, anadhihakiwa ili aache tabia hii.
5.7 TAMTHILIYA YA KITANZIA
- Tamthiliya ya tanzia hutumika kuonesha
kuanguka na kushindwa kwa mhusika maarufu,
mhusika mbabe, au shujaa. Tamthiliya hizi
hutumia mhusika atokaye katika tabaka la juu,
yaani ni mtu mwenye nasaba bora kwa maana
amezaliwa katika nyumba ya kifalme au
kimalkia. Tanzia ilianzia kwenye miviga ya kidini
katika Ugiriki ya kale ikihusishwa na sherehe za
Dionisius.
Lengo la tanzia ni kuwaingizia watazamaji
hisia za woga kutokana na yanayompata
mhusika mkuu, ambayo yanasababisha anguko
lake (Mwalimu Edwin Semzaba, Idara ya
Sanaa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam; Prof.
Aldin Mutembei wa Idara ya FAMU Chuo Kikuu
cha Dar es Salaam).
5.7.1 Utokeaji wa Tanzia
Tanzia inatakiwa iwe na uwezo wa kuamsha hisia
za woga na huruma miongoni mwa hadhira. Hisia
za woga na huruma zinatokana na mikasa
inayompata mhusika wa kitanzia ambaye ni
mwema, mzuri kwa sura na umbo, ambaye kila mtu
anampenda na hatakiwi kupata baya lolote. Mfano
mzuri wa mhusika wa aina hii ni wa filamu ya
Second Chance – aliyeitwa Salvado
Solenza.
- Mhusika mkuu anatakiwa apate anguko
linalotokana na uamuzi wake mbaya au kosa
analolifanya. Lengo ni yeyé mwenyewe kujiona ana
hatia na hakwepi hatia hiyo. Mhusika wa tanzia
anaikabili hatia iliyopo mbele yake. Kama ni
kunyongwa basi atakwenda kwa hiari kukikabili
kinyongeo na wala hatoroki (Mwalimu Edwin
Semzaba, Idara ya Sanaa Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam; Prof. Aldin Mutembei wa Idara ya FAMU
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam).
5.7.2 ISTILAHI KATIKA TANZIA
HAMARTIA
Ni kosa kubwa sana ambalo mhusika mbabe
analifanya na kosa hili humtumbukiza katika kifo
(Mwalimu Edwin Semzaba, Idara ya Sanaa Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam; Prof. Aldin Mutembei wa
Idara ya FAMU Chuo Kikuu cha Dar es Salaam).
HUBRISI
Hii ndiyo dhambi yenyewe. Ni kule kutenda kosa
kwenyewe. Mfano, Mfalme Edipode kulala na
mama yake mzazi. Kitendo hiki ndicho
kinachomwingiza katika hamartia (Mwalimu Edwin
Semzaba, Idara ya Sanaa Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam; Prof. Aldin Mutembei wa Idara ya FAMU
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam).
ANAGNORISIS
Huu ni utambuzi wa ndani ya nafsi ya mkosaji.
Hapa anakuwa ameshalifahamu kosa lake ambalo
limeshamwingiza katika anguko (Mwalimu Edwin
Semzaba, Idara ya Sanaa Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam; Prof. Aldin Mutembei wa Idara ya FAMU
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam).
PERIPATEA
Haya ni matendo muhimu ambayo humtoa shujaa
katika hali iliyoonekana kuwa afadhali kumdidimiza
katika hali mbaya kabisa. Kwa mfano, baada ya
Mfalme Edipode kutambua kosa lake, anaamua
kujitoboa macho (Mwalimu Edwin Semzaba, Idara
ya Sanaa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam; Prof.
Aldin Mutembei wa Idara ya FAMU Chuo Kikuu cha
Dar es Salaam).
NEMESIS
Hii ni adhabu ambayo haina budi kutendeka
kutokana na kuwapo kwa matendo ya Hubrisi
(Mwalimu Edwin Semzaba, Idara ya Sanaa Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam; Prof. Aldin Mutembei wa
Idara ya FAMU Chuo Kikuu cha Dar es Salaam).
5.8 Hitimisho:
Tamthiliya ni utanzu wa muhimu sana wa sanaa
tendaji ambayo inakusudiwa kutendwa jukwaani.
Kwa mtengenezaji au mtunzi wa drama za runingni,
jukwaani, redioni na filamu, hana budi kuzingatia
maudhui haya yanayoihusu tamthiliya kwa kuwa ni
pande mbili za sarafu moja. Ninamaana kuwa, hiyo
drama ni tathiliya iliyotendwa tayari ambayo
inaonekana mbele ya watazamaji. Kwa upande
mwingine tathiliya ni lile andiko lenyewe la kiuigizaji
ambalo lina wahusika na majibizano yao
yanakuwepo, lakini inakuwa vado haijawekwa
vitendoni.
SURA YA SITA
UANDISHI WA MISWADA YA USHAIRI
6.0 Utangulizi
Ushairi kwa mujibu wa Mulokozi (1996) ni:
Sanaa iliyopambanuliwa kwa mpangilio
maalumu wa maneno fasaha na yenye
muwala, kwa lugha ya mkato, picha, sitiari au
ishara, katika usemi, maandishi au mahadhi
ya wimbo, ili kuleta wazo au mawazo, kufunza
au kuelezea tukio au hisi fulani kuhusu
maisha au mazingira ya binadamu kwa njia
inayogusa moyo. Mulokozi na Kahigi,
(1982:25) kama walivyonukuliwa katika
(Mulokozi 1996:96).
Mtu mwingine aliyeelezea maana ya ushairi ni
Mathias Mnyampala (1965) yeye anasema kuwa:
Ushairi ni msingi wa maneno ya hekima tangu
kale. Ndicho kitu kilicho bora sana katika
maongozi ya dunia kwa kutumia maneno ya
mkato na lugha nzito yenye kunata
iliyopangwa kwa urari wa mizani na vina
maalumu kwa shairi” (Mnyampala,1965:vii).
Mnyampala anaendelea kusisitiza kipengele cha
kutosheleza shida ama haja za shairi
akitahadharisha wale wenye mtazamo kuwa shairi
linapaswa liwe fupi na kwamba shairi refu ni bayalahasha;
kila shairi linapaswa lijitosheleze haja yake
kama ni fupi au refu. Haipaswi kulazimisha shairi
fupi liwe refu, na refu liwe fupi. Kila moja
litategemeana na kile akisemacho mwandishi kama
kimejitosheleza ama la.
Mtu mwingine aliyezungumzia kuhusu ushairi ni
Shabaan Robert yeye anasema:
Ushairi ni sanaa ya vina inayopambanuliwa
kama nyimbo, mashairi, na tenzi zaidi ya
kuwa sanaa ya vina ushairi una ufasaha wa
maneno machache au muhutasari. Mwauliza
wimbo, shairi , na tenzi ni nini? Wimbo ni
shairi dogo, shairi ni wimbo mkubwa, na
utenzi ni upeo wa ushairi. Mwauliza tena kina
na ufasaha huweza kuwa nini? Kina ni
mlingano wa Sauti na herufi. Kwa maneno
mengine huitwa mizani ya sauti; na ufasaha
ni uzuri wa lugha. Mawazo, maoni, na fikira
za ndani zinapoelezwa kwa muhutasari wa
ushairi huvuta moyo kwa namna ya ajabu
(Robert, 1968:61).
Abdilatifu Abdala (1973) anaelezea kuwa ushairi ni:
... na utungo ufaao kupewa jina la ‘ushairi’ si
utungo katika kila ubeti wake kuna ulinganifu
wa vina vitukufu vilivyopangwa kimoja baada
ya chenziye; wenye vipande vilivyo na
ulinganifu na mizani zisizopungua wala
zilizozidi; na vipande hivyo viwe vimetandwa
na maneno ya mkato maalumu na yenye
lugha nyofu, tamu, na laini, lugha ambayo ina
uzito wa fikira, tamu kwa mdomo wa kuisema,
tumbuizi kwa masikio ya kusikia na yenye
kuathiri moyo uliokusudiwa na kama
ulivyokusudiwa...
Tatizo la fasili za Robert (1968), Mnyampala
(1965), na Abdala (1973) ni kule kuona kwamba
shairi linapaswa lipambanuliwe kwa vina na mizani.
Wachambuzi hawa wanaona kuwa vina na miziani
ni uti wa mgongo wa Ushairi wa Kiswahili.
Kwa upande mwingine, fasili ya Mulokozi na
Kahigi (1982) ndiyo yenye mawanda mapana
ambayo inaelezea ushairi ni nini kwa kuzingatia
kanuni na misingi ya utanzu huu. Fasili yao ndiyo
tunayoiunga mkono na inashadidiwa na Massamba
(1983) anapoelezea tanzu za ushairi wa Kiswahili
kuwa ni pamoja na: tumbuzi, nyimbo, shairi, tenzi,
mashairi, na ngonjera (ukurasa wa 60-94).
Anaendelea kuelezea aina za mashairi, mitindo, na
miundo ya mashairi. Pia amegusia sifa za mtunzi
wa ushairi kwamba anapaswa awe na kitu
kinachomsukuma na sio kuwa na vina tu bila wazo.
Vilevile ameongelea kitu muhimu kwa mtunzi ni
kuelewa falsafa za maisha za watu wengine na
kuona anatofautianaje nao au anafanananao vipi.
Pia mtunzi huyu anapaswa kujua hisia za watu
wengine kuhusu falsafa yake na wanapingana naye
kwa vipi na kwa nini (Massamba, 1983:81).
7.1 AINA ZA USHAIRI
Aina za ushairi katika Kiswahili ni pamoja na:
• Tumbuizo
• Nyimbo
• Shairi
• Utenzi – khamziya & takhamisa
• Ngonjera
Mwanafunzi anashauriwa asome makala hii ya
Massamba katika kitabu cha FASIHI III
kilichochapisha na TUKI (1981). Massamba
anadadavua aina hizo za ushairi kwa mapana na
marefu. Vilevile, mwanafunzi anashauriwa atafute
vitabu vinginevyo ambavyo pia vimejadili aina za
ushairi ili aweze kujijuvya kwa kina kuhusu utanzu
huu. Kwa kufanya hivyo, itamwezesha mwanafunzi
kuchagua anataka kuwa mshairi wa ushairi upi?
7.2 VIPENGELE VYA FANI KATIKA USHAIRI
• Vipengele vya fani katika ushairi ni pamoja
na:
• Jina / anwani
• Mandhari
• Wahusika
• Muundo –tathnia, tathlitha, tarbia, tathamisa,
sabilia (soma makala ya Massamba, 1981)
• Mtindo – pindu, msisitizo, beti kubadilishana
vina, kurudiwa kipande kizima cha mstari wa
mwisho kikiwa ni chanzo cha ubeti
unaofuatia (Massamba, 1981) katika TUKI,
FASIHI III.
7.3 MAUDHUI YA USHAIRI
Maudhui ni nini? Maudhui ni yale mawazo ambayo
mtunzi anayawasilisha katika kazi yake ya ubunifu.
Kuna vipengele vya maudhui ni pamoja na:
migogoro, ujumbe, falsafa, msimamo, mtazamo, na
dhamira za mwandishi. Ushairi unaweza kuwa na
matumizi mengi kama: kuomboleza, kubembeleza,
kuliwaza, kufundisha, kuburudisha, kukosoa, na
kadharika
7.4 Hitimisho
Kila mtu ameumbwa kwa majaliwa
mbalimbali jambo ambalo linafanya tuwe tofauti
katika utunzi. Kuna mtu ni mwepesi sana kupata
mawazo ya kutunga shairi, mwingine ni mwepesi
sana kupata vina na mizani, lakini mwingine ni
mzito sana na anaweza kuchukua hata wiki moja ili
kutunga ubeti mmoja wa shairi. Wakati kuna
mwingine ambaye dakika moja ni kubwa sana
kuweza kukutungia ubeti. Kila mtu na majaliwa
yake.
SURA YA SABA
UANDISHI WA MISWADA YA HADITHI FUPI
7.0 Utangulizi
Hadithi fupi ni nini?
Alex Ngure (2003:2) anasema kuwa:
...ni masimulizi yanayojikita katika kisa kimoja
chenye uzito kimaana. Inambidi mwandishi
wa hadithi fupi achague tu yale mambo ya
lazima kuyaelezea”. Hadithi fupi aghalabu
huwa na mhusika mkuu anayehusishwa na
matukio makuu katika hadithi nzima.
Hadithi ni habari za mambo yaliyotukia; ni
mtungo wa habari unaosimulia mambo yaliyotukia.
Hadithi fupi ni mtungo wa habari za kubuni ambao
si mrefu sana – ni kama kurasa kumi hivi na
kunakuwa na wahusika wachache na hata kisa
kinakuwa ni kimoja na ndipo suala la ufupi wa
utanzu huu linapokuja.
Uandishi wa miswada ya hadithi fupi
inatakiwa uegemezwe katika masimulizi ya nini
kilitokea; wapi; lini; nani alihusika; na kwa nini. Ni
utanzu ambao unataarifu kuhusu jambo fulani lakini
taarifa hii inapaswa iwasilishwe kiubunifu kwa
mtindo wa nathari. Nathari ni maandishi ya moja
kwa moja, maandishi ya kawaida ambayo
hayajaandikwa kwa mpangilio wa kishairi.
7.2 NAMNA YA KUANDIKA HADITHI FUPI
Hadithi fupi zinaweza kuandikwa kwa kutumia
mianzo mbalimbali. Kwa mujibu wa Free advice
“The 7 types of short story opening/ and how to
decide which is right for your story
www.http://109.com/5814687 wanaeleza
kama
ifuatavyo:
i) Unaweza kuanza kwa kutambulisha
mandhari. Hii inafanyika katika aya ya
kwanza ili msomaji aweze kuwajua wahusika
na mandhari.
ii) Kuanza na mgongano – hii inawezekana
kwa kuanza simulizi wakati wahusika
wanakwaruzana kuhusiana na jambo fulani.
iii) Kuelezea jambo la kidhahania. Unampeleka
msomaji katika mambo ambayo hawezi
kuyaona wala kuyahisi. Mathalani,
unazungumzia namna mhusika alivyokuwa
akipanda ngazi za kuenda mbinguni.
iv) Kutumia msimulizi wa nje. Hii ni nafsi ya tatu
inapotumika katika simulizi inamfanya
msimulizi awe huru kuingia ndani ya simulizi
na kutoka. Usimulizi huu una mawanda
mapana.
v) Kutumia usimulizi wa nafsi ya kwanza. Hapa
msimulizi anabanwa na wakati, mazingira,
na muktadha. Msimulizi anasimulia vile vitu
alivyokutana navyo tu.
vi) Kuanza na nukuu. Katika uandishi wa habari
ndiko mtindo huu wa kiuandishi
hupendelewa. Huu sio mtindo mzuri kwa
mwandishi wa kubuni hadithi. Hivyo, uepuke.
vii) Taharuki. Unaweza kuanza hadithi yako na
migongano kati ya wahusika wako na
kumfanya msomaji awe na taharuki kwamba
nini kitatokea.
7.3 VIPENGELE VYA KIFANI VYA HADITHI FUPI
Vipengele hivi ni kama vilivyoelezewa katika
sehemu ya tamthiliya. Japokuwa huu ni utanzu
tofauti, dhana ni ileile.
• Matumizi ya lugha
• Muundo
• Mtindo
• Wahusika
• Mandhari
• Jina/anwani
7.4 MAUDHUI YA HADITHI FUPI
• Dhamira
• Migogoro
• Falsafa
• Mtazamo na msimamo
• Ujumbe
7.5 Hitimisho
Katika maisha ya utunzi, kanuni za jumla hutumika
katika utunzi mahsusi. Ninapotaja kanuni za jumla
ninarejelea mambo ya msingi ambayo
yanakuwezesha kutunga kazi yako. Kanuni
hizohizo unaweza kuzitumia ili kutunga kazi ya
kumbo yoyote ile. Vivyo hivyo mtunzi wa hadithi
fupi, nakushauri usome sehemu ya mwanzoni mwa
kitabu hiki ili ujue kanuni za jumla za utunzi ili
zikuwezeshe kutunga kazi yako.
SURA YA NANE
UANDISHI WA MISWADA YA RIWAYA
8.0 Utangulizi
Riwaya kwa mujibu wa Said Mohamed Abdula
imepata tafsiri nyingi katika nadharia ya fasihi.
Wapo waliozingatia kigezo cha urefu na kuonekana
kuna mapungufu katika kigezo hiki, kwa sababu je
ni urefu wa kimuundo, kimaudhui, kilugha, au yote
kwa pamoja? (Abdula, 1995:66).
Abdula anaendelea kufafanua kuwa, katika
riwaya kuna hadithi, yaani, kuna simulio
linalokwenda hatua kwa hatua katika mfunguko wa
matukio, visa, na mikasa inayojengwa katika
matendo fulani yanayofanywa na wahusika ambao
hutenda au kutendana kuisukuma mbele hadithi
kiwakati na kipahala, huku wakiibua humo au kile
kinachoitwa taharuki kwa hadhira. Pia anaendelea
kufafanua kuwa, riwaya inatakiwa ijibu maswali
matano ambayo ni pamoja na: nani anafanya nini;
wapi anafanyia; wakati gani anafanya; afanye nini
na nani; na kwa vipi? (Abdula, 1995:66).
Mtu mwingine anayetafsiri riwaya ni Njogu
na Chimerah (1999) wanafafanua kuwa ni: “utungo
mrefu wa kubuni, na wenye ploti, uliotumia lugha ya
nathari” (1999:35). Maelezo ya Abdula
tunakubaliana nayo bila shaka yoyote kuhusiana na
maana ya riwaya. Ila fasili ya riwaya kwa mujibu wa
Njogu na Chimerah ina kasoro kuhusiana na
kipengele cha ‘urefu’ kwa kuwa kigezo hicho tu
hakiwezi kuifanya riwaya iwe na sifa ya kuwa
riwaya. Lakini kwa upande mwingine tunakubaliana
nao kuwa riwaya inahitaji ploti (yaani msuko wa
matukio), na lugha ya nathari.
Mulokozi (1996) anaelezea kuwa wataalamu
katika Lugha ya Kiswahili wameelezea maana ya
riwaya kwa namna tofauti. Wataalamu hawa ni
pamoja na Muhando na Balisidya (1976:63); na
Mlacha na Madumulla (1991:1) ambao walizingatia
kigezo cha urefu. Mulokozi anaendelea kukiri
kwamba, fasili zao zina walakini lakini anaiona fasili
ya Senkoro ndiyo inayoelezea kwa uzuri maana ya
riwaya. Senkoro kama alivyonukuliwa katika
Mulokozi (1996:139) anasema kuwa riwaya ni:
Sifa ya uchangamano ni nzuri zaidi kuelezea
maana ya riwaya. Twaweza kusema kwamba
riwaya ni kisa mchangamano ambacho
huweza kuchambuliwa na kupimwa kwa
mapana na marefu kifani na kimaudhui.
Riwaya ni kisa ambacho urefu wake
unakiruhusu kitambe na kutambaa vizingiti
vingi vya maisha kama apendavyo mwandishi
wake. Riwaya basi, ni hadithi ndefu ya kubuni,
yenye visa vingi, wahusika zaidi ya mmoja, na
yenye mazungumzo na maelezo
yanayozingatia kwa undani na upana, maisha
ya jamii (Mulokozi, 1996:139).
8.1 UANDISHI WA MISWADA YA RIWAYA
Uandishi wa miswada ya riwaya inatakiwa
uegemezwe katika masimulizi ya nini kilitokea;
wapi; lini; nani alihusika; na kwa nini. Ni utanzu
ambao unataarifu kuhusu jambo fulani lakini taarifa
hii inapaswa iwasilishwe kiubunifu na kwa mtindo
wa nathari. Nathari ni maandishi ya moja kwa moja,
yaani maandishi ya kawaida ambayo
hayajaandikwa kwa mpangilio wa kishairi.
Riwaya ni hadithi ndefu ya kubuni
iliyoandikwa kwa maelezo ya kubuni aghalabu
inaelezea ukweli fulani wa maisha. Kuna
mchangamano wa visa na matukio na vilevile
kunakuwa na wahusika wengi ambao kila mmoja
ana matamanio yake tofauti na mwingine. Katika
kutofautiana huko kwa matamanio ndiko
kunakotupa hadithi ndefu kwa sababau kutakuwa
na visa na mikasa mingi ambayo inasimuliwa katika
hadithi.
Ili mtunzi aweze kutunga riwaya hana budi
kuwa na visa vingi ambavyo anataka kuvisimulia
katika hadithi yake. Baada ya kuvipata visa hivyo –
inatakiwa afikirie na apangilie kuhusu mtiririko wa
visa na matukio katika simulizi yake, ili kuleta mvuto
utakaomfanya msomaji asikiweke chini kitabu mara
tu atakapoanza kukisoma. Hapa kinachoongelewa
ni msuko wa matukio – jinsi utakavyoyapangilia
tangu mwanzo hadi mwisho; ili katika upangiliaji
huo kuweze kuwa na taharuki za kumvuta msomaji
asome au hata kama imetengenezwa filamu –
aiangalie bila kuudhika na kuzima televisheni yake.
Jambo jingine ni mtunzi kufanya utafiti wa
kina ili ajue undani na ukweli ulivyo kuhusiana na
mambo anayotaka kuyaandikia. Kwa kufanya hivyo,
atajiweka katika mazingira mazuri ambayo
yatawafanya wasomaji au watazamaji wa kazi yake
waamini yale anayowaambia ‘kuwa yana ukweli’
(believability).
Baada ya kuiandika kazi yako (kama ni
riwaya, hadithi fupi, tamthiliya, shairi, au filamu),
huna budi kumpatia mtu mwingine ayasome
maandishi yako kiyakinifu ili aweze kukushauri pale
penye tatizo na kwa kufanya hivyo utaiboresha kazi
yako na kujijengea heshima ya kuandika vizuri!
8.2 AINA ZA RIWAYA
Kuna aina kuu mbili za riwaya ambazo ni dhati na
pendwa. Lakini ndani ya riwaya hizi kuna aina
ndogondogo za riwaya ambazo ni pamoja na:
mahaba, uhalifu, upepelezi, ujasusi, kihistoria,
kijamii, kisaikolojia, vijana, majaribio, barua na
kadhalika.
8.3 VIPENGELE VYA KIFANI VYA RIWAYA
2) Matumizi ya lugha
3) Muundo
4) Mtindo
5) Mandhari
6) Jina/anwani
7) Wahusika
8.4 VIPENGELE VYA KIMAUDHUI VYA RIWAYA
• Dhamira
• Migogoro
• Falsafa
• Mtazamo na msimamo
• Ujumbe
8.5 Hitimisho
Mtunzi chipukizi unapaswa uzingatie mambo
mbalimbali uliyofundishwa kuhusu hadithi fupi,
kwani kwa namna fulani yanaingiliana na utanzu wa
riwaya. Kitu cha kuzingatia ni kujikumbusha kanuni
za utunzi na maelekezo mahususi yanayohusu
riwaya; kisha anza kutunga kazi yako.
Jambo la kukushauri ni kuwa, unatakiwa
uwe msomaji mzuri wa kazi za wenzako ili uone
wanaandikaje. Ukiwa msomaji mzuri na ndivyo
utakavyokuwa mwandishi mzuri. Zingatia jambo
hilo!
SURA YA TISA: UANDISHI WA KUBUNI:
NADHARIA
9.0 Uandishi wa kubuni unatakiwa uweje?
Uandishi wa kubuni ni taaluma kama zilivyo
taaluma nyinginezo. Ubunifu ni kazi kama zilivyo
kazi zingine ambazo zina kaida na kanuni zake –
vivyo hivyo uandishi wa kubuni una kaida na
kanuni.
Mwandishi wa kubuni ni yule ambaye
anatumia uzoefu wake pamoja na utafiti ambao
anaufanya kuhusiana na uzoefu mbalimbali ili
kuweza kutoa simulio kwa njia mbalimbali. Utoaji
simulio unaweza kuwa kwa njia ya utunzi wa
hadithi, riwaya, shairi, tamthiliya, mchezo wa redio,
mchezo wa televisheni, au filamu. Vilevile, anaweza
kutoa simulio kwa njia ya uigizaji, uchezaji ngoma,
uimbaji, au uchezaji muziki. Zote hizo ni njia
ambazo mwandishi wa kazi za kubuni anaweza
kuzitumia ili kusimulia kisa alichokuwa nacho katika
mawazo yake.
Uandishi wa kubuni unamtaka mwandishi
atumie milango yake ya fahamu ambayo ni: kuona,
kusikia, kunusa, kuonja, na kugusa katika kusimulia
hadithi au mkasa wowote ambao ama umempata
au umempata mtu mwingine. Mtu huyo anaweza
kuwa ni wa karibu au mbali – haijalishi kwa kuwa
mwandishi wa kubuni anatumia utafiti katika kupata
kitu cha kusimulia.
Katika usimulizi huo, mwandishi wa kubuni
ana uhuru wa kutumia nafsi zote tatu ili kuweza
kugusa hisia za msomaji au mtazamaji wa kazi ya
sanaa. Mtunzi huyu anaweza kutumia nafsi ya
kwanza ambayo inataja kitu kinachokuhusu mtu
binafsi kama vile 'mimi nina...' katika umoja au 'sisi
tuna...' katika wingi.
Akitumia nafsi ya kwanza inaonesha simulio
inamuhusu (kama ndiye au amejifanyisha kuwa
ndiye). Nafsi nyingine ni ya pili ambayo katika
umoja ni 'wewe una...' na katika wingi ni 'ninyi
mna...'. Hii pia inaonesha
angalau mwandishi
hayuko mbali sana na simulio japokuwa nafsi hii
haitumiki sana katika uandishi wa kubuni –
hutumika katika uandishi usio wa kubuni ambao
unalenga kumwelimisha msomaji. Lakini si jambo la
ajabu kama utakutana na kazi ya sanaa ambayo
inatumia nafsi ya pili – huu ndio uhuru wa kuchagua
namna ya kusema jambo unalotaka kulisema.
Matumizi ya nafsi ya tatu yanaonesha kuwa
simulio liko mbali na mwandishi – inaonesha sio
yeye wala wakala wake, bali ni mtu mwingine ndiye
yamemkuta hayo anayotueleza. Faida ya kutumia
nafsi ya tatu ni kubwa kwa kuwa inakuwezesha
mwandishi kuogelea popote pale na kusimulia
mambo mengi yanayotokea mahali popote katika
wakati huohuo. Hii inawezekani kwa kuwa nafsi ya
mwandishi haipo hapo – iliyopo ni nafsi ya
msimulizi ambaye anatusimulia kilichotokea. Nafsi
hii ya tatu ni ile ya kusema 'yeye ana...' katika
umoja; na 'wao wana...' katika wingi.
Kwa hiyo, uandishi wa kubuni sio lelemama.
Ili mwandishi aweze kuandika au kubuni kazi
ambazo zinawashika hadhira kikwelikweli, hana
budi kuwa mtafiti na kujielimisha vya kutosha ili
ajue mbinu mpya zinazotumika katika uwanja wa
sanaa ili sanaa yake isipwaye kwa kuonekana
imepitwa na wakati.
9.2 Mchakato wa ubunifu
9.2.1 Mwandishi na zana zake
Uandishi ni nini?
Uandishi ni kazi ya kuandika (KKS, 2000:418).
Kuandika ni kitendo cha kuweka alama au michoro
kwa kutumia herufi ili kuwakilisha sauti.
Ubunifu ni dhana inayotokana na tendo la kubuni.
Kubuni ni kutengeneza kitu kwa mara ya kwanza;
kugundua. Vilevile, tunaweza kusema kuwa, kubuni
ni kuzua au kutunga jambo (KKS, 2000).
Zana ni nini?
Zana ni chombo au kifaa kinachohitajika ili kufanyia
kazi fulani. Katika muktadha wa uandishi wa
kubuni, zana ni pamoja na kalamu, karatasi, na
shajara. Kwa upande mwingine, zana ni lugha
ambayo inamwezesha mwandishi kueleza kile
kilichomo moyoni mwake.
Lugha ni nini?
Lugha ni sauti za nasibu ambazo zinatumiwa na
jamii fulani ili kuwasiliana.
Kuwasiliana au kupashana habari kunawezekana
kupitia njia tatu ambazo ni: sauti, maandishi, na
alama.
Mwandishi wa kubuni anatumia maandishi ili aweze
kuwasiliana. Katika njia hii ya mawasiliano,
anahitaji nyenzo zitakazomwezesha aeleweke kwa
hadhira yake. Nyenzo hizi ni alama za uandishi na
uakifishi.
Alama za uandishi
Alama za uandishi ni nini? Ili uweze kujua vema
jambo hili, huna budi kusoma kitabu cha Mwongozo
wa Wandishi wa Kiswahili cha
BAKITA, 1994).
Alama hizi za uandishi ni pamoja na: nukta, nukta
pacha, nukta mkato, koma, kistari, kwa kuzitaja kwa
uchache.
Uakifishaji
Uakifishi ni nini? (Soma vitabu vya Wamitila,
Mwenge wa Uandishi (2009); na Mrikaria Utungaji
(1) cha mwaka (2009) na
Kiango Utungaji (2) cha
mwaka (2009).
9.2.2 Mwandishi na mazingira yanayomzunguka
Mazingira ni nini?
Mazingira ni hali au mambo yanayomzunguka
kiumbe katika sehemu anapoishi au maisha yake
(KKS, 2000:238).
Mwandishi huzungukwa na mazingira mbalimbali
kama vile: nyumbani, shuleni, mtaani, kiibada,
kijamii, na kadharika.
Nyumbani:
Nyumbani – je katika familia yako mahusiano
yakoje kati ya wenza na watoto au wanandugu
wengine?
Je, wewe ni yatima? Uyatima wako ulitokana na
nini. Je, uyatima ulitokana na milipuko ya mabomu
ya Mbagala au Gongo la Mboto? Je, ni ajali ya MV
Bukoba au MV Spice Islander? Au je, uyatima
wako ulitokana na mashambulizi ya kigaidi
yaliyochoma Balozi za Marekani nchini Tanzania au
Kenya? Je, wewe ni yatima kutokana na ajali za
barabari au ajali ya ndege? Elezea mkasa wako
kinagaubaga ili uweze kuishika hadhira na
wasomaji wako.
Mahusiano ya wanandugu yakoje?
Je, baada ya wazazi kufariki - mali za marehemu
zilileta ugomvi baina ya ndugu? Je, mashemeji na
mawifi walivamia na kukwapua mali za marehemu?
Je kama kuna watoto wa marehemu – je wanapata
shida yoyote baada ya wazazi kufariki? Majibu ya
maswali haya yatakuwezesha kujua namna ya
kukuza migogoro na migongano katika tamthiliya
au drama
Shuleni – mazingira yakoje kuhusiana na
masomo au shule yako? Je, unakutana na
unyanyasaji wa kijinsia kutoka kwa walimu? Je,
wewe ni mlemavu na unakutana na vikwazo gani
katika mazingira ya shule? Je kama wewe ni
mlemavu unabaguliwa? Majibu ya maswali haya
yatakuwezesha kujua namna ya kukuza migogoro
na migongano katika tamthiliya au drama
Mazingira ya kiimani:
Je, wewe ni Mkristu, Mwislamu, Myahudi? Mhindu,
Mbuddha? Au unaamini katika Uafrika na mizimu?
Je imani uliyonayo inajitokeza katika uandishi wako
- kwa namna unavyotatua migogoro?
Je, imani yako unayoifuata uliipataje: je uliirithi
kutoka kwa wazazi au umebadili dini? Kama
umebadili dini je ni sababu gani zilizokufanya uache
dini x na kuingia katika dini y? Majibu ya maswali
haya yatakuwezesha kujua namna ya kukuza
migogoro na migongano katika tamthiliya au drama
Mazingira ya kijamii:
Unakaa wapi kijiografia: je uko sehemu gani ya nchi
ya Tanzania?
Je, jamii inayokuzunguka ina sifa gani? Je, sifa hizo
zinakuathiri kwa namna yoyote? Je, unaishi katika
jamii ya waliosoma au wasiosoma? Wewe una
kiwango gani cha elimu ukijilinganisha na
wanaokuzunguuka? Je, kiwango chako kinaleta
tatizo lolote la kimahusiano na jamii
inayokuzunguka?
9.2.3 Welewa wa mwandishi kuhusu uhalisi,
uhalisi sambamba, na uzoevu
Uhalisi:
Uhalisi ni nini?
Kwa mujibu wa Wamitila, ni dhana inayotumiwa
katika fasihi kuelezea hali ilivyo katika jamii
kiuchumi, kijamii, kisiasa na kiutamaduni (272)
Uhalisia ni mkondo unaosisitiza usawirii wa matukio
au maisha katika fasihi kama yalivyo katika maisha
ya kila siku. Mkabala huu unahusishwa na mfuasi
wa Karl Mark kutoka Hungary anaitwa Georg Lukas
Uhalisi sambamba:
Katika fasihi ni namna ya kuliandika jambo katika
mizania na ridhimu. Kwa kuzingatia hilo, ndipo
tunapopata umbo la kazi na mtiririko wake.
Usambamba huu unahusiana na matumizi ya
maneno yenye uzito sawa na ridhimu ili kuliweka
jambo husika katika mizania. Usambamba wa
'huzuni' ni ridhimu ya 'taratibu inayoonesha
majonzi'. Lakini usambamba wa 'mapambano au
harakati za kuondokana na udhalimu' ni ridhimu ya
'harakaharaka, ya kustua ambayo imechangamka.
Uzoevu au uzoefu:
Uzoefu ni hali ya kukaa au kujishughulisha na
jambo au kitu kwa muda mrefu (KKS, 2000:451).
Mwandishi ana uzoefu (uzoevu) wa kukabiliana na
maisha kwa kiasi gani? Je, ni matatizo gani
ambayo umekutana nayo katika maisha yako? Je,
ni mafanikio gani umekutana nayo katika maisha
yako? Kwa mfano, katika ajali ya MV Spice (2011)
kuna baadhi ya watu waliokolewa na magodoro ya
Tanzania? Magodoro haya yana nailoni na je kama
yasingekuwa na nailoni? Uzoefu wako ukoje katika
tukio fulani?
9.2.4 Uchunguzi sambamba dhidi ya mambo ya
kufikirika
Uchunguzi sambamba wa mambo ya kufikirika
maana yake ni nini?
Uchunguzi unapaswa ufanywe na mwandishi ili
aweze kuandika jambo au tukio bila kuongopa. Kwa
kufanya udanganyifu, mwandishi atapoteza imani
yake kwa wasomaji wa kazi zake.
Uchunguzi ili ufahamu au ujue mtu,
mnyama, mdudu na kadharika – anatembeaje,
anakulaje, analalaje, anaishije, anachekaje,
analiaje, anazaaje, anahusianaje na wenzane na
mazingira yake? Haya ni maswali muhimu katika
kumwezesha mtunzi kufanya utafiti wa kina ili ajue
kitu anachotaka kukiandika akiandikaje na
akiwasilishaje ili aweze kuikamata hadhira yake.
9.2.5 Mwandishi na jadi
Jadi ni nini?
Jadi ni asili ya mtu anakotoka; kizazi cha mtu;
nasaba; ukoo (KKS, 2000:126).
Mwandishi ni mtu wa kabila au mkoa gani?
Je, ni mtu wa nasaba bora au nasaba duni?
Je, ni mtu kutoka ukoo wa kichifu au kitemi au ukoo
wa kawaida?
MWANDISHI NA RASILIMALI ZAKE: RASILIMALI
ZA KIJADI NA KIUTAMADUNI
Rasilimali ni nini?
Rasilimali ni jumla ya mali aliyonayo mtu au nchi.
Mwandishi ana rasilimali nyingi ambazo ni za kijadi
na kiutamaduni; na kwa upande mwingine, ana
rasilimali za kiisimu na lugha.
Rasilimali za kijadi na kitamaduni – ni kuhusu mila,
asili, jadi na desturi za kundi la jamii fulani (KKS,
2000:445).
9.2.6 Rasilimali za kiisimu na za lugha alizonazo
mwandishi
Katika rasilimali za kiisimu: tunaangalia mwandishi
ana umahiri kiasi gani katika isimu ya lugha
anayoitumia kujieleza.
Je, kama anatumia Kiingereza anakimudu
barabara? Je, kama anatumia Kiswahili anakimudu
barabara? Au mwandishi anaandika Kiingereza au
Kiswahili chenye makengeza na matege?
Lugha za mwandishi: je yeye ni mlumbi au ni mtu
anayejua lugha mama peke yake?
9. 3 Hitimisho
Mwandishi chipukizi anapaswa aisome nadharia ya
uandishi wa kubuni ili aweze kujijengea msingi wa
kuifanya kazi hii. Kuandika si jambo rahisi, ndio
maana si kila mtu ni mwandishi bora; mwandishi
nguli; mwandishi maarufu. Kuandika ni kipaji au
tuseme karama ambayo Mwenyezi Mungu
amemjalia amtakaye kwa ajili ya sifa na utukufu
wake. Hivyo cha msingi ni kujitahidi kuzingatia
mambo tuliyokuelekeza ili uweze kuandika kazi na
wewe ujulikane katika ulimwengu wa fasihi kuwa
upo.
SURA YA KUMI NA MOJA: UANDISHI WA KUBUNI:
VITENDO
10.1 Utangulizi
Uandishi wa kubuni ni ule unaojitokeza katika riwaya,
hadithi fupi, ushairi, tamthiliya, na filamu; vitu hivi ni
miongoni mwa aina mbalimbali za uandishi wa kubuni.
Unaweza kujiuliza kwa nini nimerudia sehemu hii? Hii ni
kutokana na umuhimu wake, hivyo nakushauri usome
kwa furaha.
Semzaba (1997:75), anasema “sanaa huanza na
hisi ambazo kila mtu anazo”. Semzaba anaendelea
kuelezea kuwa, mtunzi huchagua umbo la kuwasilishia
wazo lake kama ni hadithi fupi, riwaya, tamthiliya,
ushairi (kimapokeo au kimasivina)-yote yanategemeana
na uchaguzi wa mtunzi.
Khamis (1983:246) yeye anaona kuwa uandishi
wa kubuni ni namna mtunzi anavyoweza kuyasawiri
maisha ya mwanadamu na kuyatungia taswira ambazo
ziko mbali na mazoea ya mwanadamu-kwakuwa ni
maisha kulingana na anavyoyaona mwandishi katika
dunia iliyomo kichwani mwake.
Uandishi wa kubuni unamtaka mtunzi atumie
milango yake ya fahamu kinagaubaga. Kuna milango ya
fahamu mitano ambayo ni pamoja na: kuona, kunusa,
kusikia, kuhisi, na kuonja.
• Kuona: je, mhusika unayemfikiria kichwani
mwako unamwonaje? Umbo lake ni la kuvutia au
kuchusha? Je, macho yake yakoje – je ni ya
golori au la? Ni makubwa au madogo? Je, ni
mlemavu wa macho?
• Kunusa: pua zako zinakufanya usikie harufu
gani? Je, ni harufu mbaya au nzuri? Je, ni
uvundo au marashi? Je, mhusika wako ananuka
kikwapa au uturi? Je, ananuka mdomo?
• Kuhisi: je, unapokaa karibu naye unajihisi nini?
Je, unapata mhemko wowote au huhisi
chochote? Je, akikupapasa mwilini mwako
unajisikia nini? Akikugusa bega unajisikia nini?
• Kuonja: je, ukiweka kitu hicho mdomoni
unaonjaje – ni chungu au tamu? Je, ina pilipili au
masala? Je, kuna chumvi au sukari? Je, kitu
hicho kina ukakasi au uchachu?
• Kusikia: je, sauti unayoisikia ikoje? Inamtoa
nyoka pangoni? Inakufanya ukose usingizi? Je,
ni sauti nzuri au mbaya? Ni nyororo au nzito?
• Kama ni sauti ya muziki – je, iko chini au juu
(kelele)?
Mahenge (2011) anasema uandishi wa kubuni ni
ule unatokana na hisia ambazo zinamsukuma mtunzi ili
atunge kazi yake. Hisia zinaungana na wazo ambapo
vitu hivyo vinamsumbua akilini na kumkosesha raha.
Mahenge anaendelea kufafanua kuwa, mwandishi wa
kubuni anataka aliwasilishe wazo lake ili hadhira
ifahamu kilichopo moyoni mwake. Mwandishi hukosa
usingizi na hivyo hulazimika kuamka na kuandika kile
kinachomsukuma akilini mwake.
10.2 Hitimisho
Uandishi wa kubuni unahitaji ufanywe kwa vitendo na
sio maneno matupu. Mwandishi ninakuhimiza ufanyie
kazi maelekezo yote niliyokupatia katika uandishi wa
kumbo za fasihi na kasha uanze kuandika mara moja.
Anza kwa kupitia zile kanuni za uandishi na kisha nenda
kwenye kipengele cha ‘utaanzaje kuandika’. Ukisoma na
kuelewa sehemu hizo, weka katika matendo yale
mambo unayoelezwa ili uanze kuingia vitendoni.
MAREJEO
BAKITA.Mwongozo wa Waandishi wa
Kiswahili Sanifu. Dar
es Salaam.1994.
Free advice “The 7 types of short story opening/
and how to decide which is right for your
story www.http://109.com/5814687/the 7
types-of-short-story-opening-and-how-todecide-
which-is-right- for-your-story
Mahenge, E. Uandishi katika
Kiswahili.www.lulu.com 2011
Mahenge, E. Sanaa ya Uigizaji: Mwongozo kwa
Waongozaji na Waigizaji wa Michezo ya
Kuigiza ya Jukwaani, Redioni, kwenye
Televisheni, na Filamu. Www.lulu.com
2011
Moshiro Gervas, Michezo ya Kuigiza-10. Mchezo wa Redio
Kusadikika. Tanzania Publishing
House. 1979
Kiango, J.G. Utungaji 2:Stadi za Lugha ya
Kiswahili. TUKI. Dar es
Salaam. 2009
Mrikaria, S.Utungaji 1: Stadi za Lugha ya
Kiswahili. TUKI. Dar es Salaam.
2009
Paul, E. Writer on Writing. 1963
Semzaba, E. Tamthiliya ya Kiswahili. OUT.1997
Syd Field katika kitabu chake cha Screenplay:
The Foundations of Screenwriting – A step by
Step Guide from Concept to Finished
Script. 1994
www.wikipedia.com
TUKI. Kamusi ya Kiswahili Sanifu. Dar es
Salaam.
2000.