MADA: NAMNA YA KUENDELEZA WAZO MPAKA UPATE MSWADA WA KITABU
Karibu katika somo letu la Kumi na Tatu. Awali ya yote, *somo hili linasaidiana na lile linalohusiana na namna ya kupata kitu cha kuandikia kitabu.* Tena, somo hili linazingatia ukweli kwamba mwandishi ni msomaji mzuri. *Hivyo, matarajio ya somo hili ni kwamba una uzoefu wa kutosha katika kusoma kazi za watu.* Sasa turudi kwenye mada yetu. *Ukiwa na wazo unaliendelezaje mpaka upate mswada?* Tutaangalia majibu ya swali hili kwa kuangalia hatua mbalimbali za kufuata mpaka uwe na mswada mkononi.
1. Kuwa na wazo la kundika. Kama nilivyodokeza, hatua hii ni ya mwandishi kuwa na kitu cha kuandika. Wazo hili linaweza kuwa limetoakana na utafiti, usomaji, udadisi, semina, makongamano, na kadhalika. *Kwa hiyo, hapa jiulize kwamba una kitu cha kuandikia kitabu?* Una uhakika hakijaandikiwa na wengine?
2. Kuchagua aina ya kitabu unachoandika. Wapendwa, vitabu vinatofautiana. Kwa mfano, vitabu vya kiroho vinaweza kuwa vya sala, tafakari ya masomo ya Biblia, mada mbalimbali za kijamii, na kadhalika. *Hapa tukubaliane kwamba kila aina ya kitabu ina utamaduni wake wa kuandika.* Kwa kuwa wewe ni msomaji mzuri, tunaamini kwamba walau unafahamu utamaduni wa kuandika aina mbalimbali za vitabu. *Kwa hiyo, katika hatua hii unaulizwa swali kwamba unaandika kitabu cha namna gani?*
3. Weka data au taarifa zako pamoja na uzikague. Katika hatua ya kwanza, tuliona kwamba kama unataka kuandika lazima uwe na mada. Pia, lazima uwe umekusanya data zitakazokuwezesha kuandika. *Sasa katika hatua hii unaambiwa kwamba weka taarifa zako zote mezani ili uchambuzi uanze.*
4. Fikiria jina la kitabu au wazo litakalobeba kitabu kizima. Hatua hii ni muhimu sana kwa sababu *hapa ndipo unaweka ramani ya kitabu (sketch).* Kitabu chako kitaitwaje, kitahusu jambo gani kubwa?? Ukifanikiwa hapa, basi utaweza kuchagua data zinazofaa kukamilisha wazo hilo katika hatua inayofuata.
5. Chagua data au taarifa nzuri zaidi. Imani yetu ni kwamba baada ya kuweka data zako mezani, kama kweli wewe ni mwandishi makini, utakuwa na mambo mengi. *Katika hatua hii, unakumbushwa kwamba, si kila taarifa uliyonayo itatumika.* Hivyo, unashauriwa uchague data chache zinazofaa kuandikia kitabu chako. Taarifa nyingine zinaweza kusubiri kwa ajili ya kitabu kingine.
6. Gawanya wazo lako kuu katika sura. *Unadhani kuna mawazo gani madogomdogo ambayo yanaweza kukusaidia kulishughulikia wazo kuu?* Unapowaza kuhusu sura, zingatia kwamba zitapaswa kupokezana taarifa mpaka mwisho na kuifanya hadithi ya kitabu kizima kukamilika. Kwa hiyo, hapa unahitaji kuwa mbunifu sana. Unapaswa kufikiria majina ya sura kwa utulivu. *Ukishaweza kubashiri majina ya sura, kagua data zako kama zinaweza kuziwezesha sura zako kusimama vizuri bila kupingana.*
7. Ukishabashiri sura za kitabu chako, basi anza kuandika. Andika sura moja baada ya nyingine. *Unapotaka kuandika, hakikisha kwamba upatapo wazo jipya unalishughulikia kabla hujalisahau.* Unapoongea na watu, unapofanya kazi zako, unapozidi kusoma vitabu, una taarifa zinazolandana na unayoyaandika? Kama unapata taarifa mpya, basi ziandike haraka.
8. Ukiendelea kuandika ukafika mahala unaona una kitu mkononi, rudi nyuma ili uone kama uliyoandika yana ushirikiano. *Usipokuwa na tabia ya kujihakiki, unaweza kujikuta unafika mwisho halafu sura hazihusiani na wala haziendelezi wazo moja.* Hili likitokea, utajikuta unakata tamaa. Lakini, kama utamaliza sura mbili au tatu na kuzisoma kwanza, unaweza kuwa unajihakiki mwenyewe.
9. Endelea kuandika mpaka mswada ukamilike. *Ukishajiridhisha kwamba unakwenda vizuri, basi endelea kuandika mpaka sura zote zikamilike.* Ukifanikiwa kuandika mpaka mwisho, basi matarajio yetu ni kwamba utakuwa na mswada mkononi.
10. Soma mswada wote na jirekebishe mwenyewe kwa kuangalia lugha, mtiririko wa mawazo na weka sawa. *Hii ni hatua muhimu sana na inapaswa kufanyika kwa makini ili kujiridhisha kwamba kwa kiwango chako, kazi ni nzuri.*
11. Vumbika mswada wako kwa muda wa kutosha (mf. mwezi au zaidi). Ukihifadhi kazi yako mahala, isahau kabisa na endelea na mambo mengine. *Baada ya muda uliojipangia kwisha, nenda kasome tena mswada wako kwa makini.* Utajishangaa kwamba baadhi ya makosa haukuyaona mwanzo. Basi rekebisha kazi mpaka wewe mwenyewe uipende.
12. Mtafute mtu unayedhani kwamba anakuzidi au anaweza kukusomea na kukupatia maoni ya kazi yako. *Usimpe mtu yeyote bila kuwa na matarajio kwamba utapata maoni ya kukuwezesha kuboresha kazi.* Kumbuka kwamba mtu huyu anayekusomea ni mtu wa majaribio ya chakula chako kabla hakijaenda mezani. Kama umeandika kitabu cha kiroho basi mpe mwenye mang'amuzi zaidi yako ili akusomee. *Katika hatua hii unashauriwa kutoogopa maoni.* Pia, maoni utakayopewa, yanahusu kazi yako. Usimchukie mtu eti kwa sababu amekupatia maoni ambayo haukuyatarajia. *Hata hivyo, unapopokea maoni kaa chini na uyatafakari. Si kila unachoambiwa kinapaswa kufanyiwa kazi.* Kuna baadhi ya maoni huwa yanaweza kupishana na wewe kwa sababu tu ya mitazamo tofauti. *Kwa hiyo, umakini unahitajika sana hapa.* Maoni yote ya kujenga, hakikisha kwamba unayafanyia kazi.
13. Tafuta mhariri unayemwamini ahariri mswada wako. *Hii ni hatua muhimu sana ingawa wengi huwa tunaipuuza kwa sababu ya gharama.* Kama tulivyoona kwenye somo la uhariri, mtu huyu anayehariri kazi yako, ataiongezea sana ubora. *Huyu pia anaweza kukushauri mambo mbalimbali ya kurekebisha kwa sababu yeye anasimama katikati ya mwandishi na msomaji.* Akishahariri mswada wako, basi ingiza marekebisho.
*SASA UNA MSWADA MKONO MWAKO. ANZA KUWAZA NAMNA YA KUUCHAPISHA.*
***************
*Epuka mambo haya utakapokuwa unaandika kazi yako.*
1. Epuka kuandika mambo ya kuhisi. Hisia zako huenda si za wengine. Jitahidi sana uandike mambo ambayo walau yanaweza kuthibitika kisayansi au kwa hoja. Hata kama mambo ya imani si yote yanaweza kuthibitika, lakini jitahidi uandike kwa kutumia lugha isiyoonesha hisia zako tu. *Mf. Mtu ukiandika kwamba kila wiki huwa unasafiri kwenda mbinguni na unapewa ujumbe na mambo mbalimbali ya kufanya au kuwaambia watu, kwa kweli wasomaji watakushangaa.*
2. Epuka kushambulia watu kwa kutumia uandishi wako. *Jitahidi kukemea tabia kuliko watu fulani halisi.* Usipokuwa makini unaweza kuibua mgogoro mkubwa kijamii au kidini. Lenga kuelimisha, kuonya, kukumbusha na mengine mengi bila kushambulia watu. *Kumbuka na wewe ni binadamu. Watu unaowashambulia, kesho wanaweza kuwa watu wazuri. Usisahau kwamba kitabu chako kitawafikia wengi na kitadumu miaka na miaka.*
3. Epuka lugha ya kuhitimisha/ya kimamlaka au ya uhakika kupitiliza (absolutism). Kuna mambo mengine unatakiwa kutumia maneno kama *huenda, yawezekana, inaelekea kwamba, inasemekana, n.k.* Mambo hayo huenesha ukweli na uungwana. Siyo kila sehemu wewe unasisitiza tu kwamba ni kweli. Usioneshe kwamba unajua kila kitu. Unapaswa kukiri kwamba nawe una mipaka ya welewa. *Kuna mambo mengine ukweli wake ni wa kimjadala.*
4. Epuka lugha ya matusi. Mwandishi lazima afahamu utamaduni wa jamii yake. *Hivyo, unashauriwa kutumia lugha ya staha na usitukane au kusema maneno ambayo hayapokelewi vizuri na jamii ya wasomaji wako.*
5. Jitahidi sana kujenga hoja kwa mifano na ushahidi. *Data ulizokusanya zikusaidie kujenga hoja kwa mifano kama ushahidi.* Ikiwezekana, kama umesoma vya kutosha, thibitisha hoja zako kwa kuwarejelea waandishi wengine walioona kama wewe. *Hii itaonesha kwamba hujakurupuka na umesoma tafiti kadhaa.* Hata hivyo, hoja hii inategemeana na aina ya kitabu unachoandika. Vitabu vingine kama vya ubunifu (creative works) havihitaji kurejelea kazi nyingine.
**************
MWISHO WA SOMO LETU. *KARIBUNI TUJADILI.*
*©️ Leonard Bakize (03.04.2020)*
eternalword2018@gmail.com
Chini ya EWCP na Ushirikishanaji Maarifa.
==============