MADA: *WIZI WA KAZI ZA WAANDISHI*
Wapendwa, karibuni katika somo letu kuhusu wizi wa kazi za waandishi wa vitabu. Somo hili kwa kiasi ni gumu. Pengine, njia nzuri ya kuelewa somo hili ni kupitia kwanza somo la *Hakimiliki.* Ugumu wa soma hili unasababishwa na waandishi, wasomaji na jamii nzima kutofahamu kwa kina kuhusu hakimiliki za kazi za waandishi. Pili, ni kutokana na Hakimiliki zenyewe kuonekana kutofanya kazi kwa uhalisia katika mazingira ya Kiafrika. Nikuulize swali hapa, *Umeshasikia wezi wangapi waliokamatwa kwa wizi wa kazi za waandishi?*
Aidha, tunapozungumzia wizi wa kazi za waandishi tufahamu kwamba ni neno pana na tata kidogo. Katika mazingira ya dini, utata unakuwa mkubwa zaidi. Kwa mfano, kuna vitabu ambavyo vimewekewa *Haki ya Kunakili* ambayo si funge. Kuna baadhi ya vitabu vinaweza kuandikwa kwamba kwa ajili ya Uinjilishaji basi kitabu hiki kinaweza kutumika bila ruhusa. Swali hapa linakuja kwamba *ikiwa kitabu ni cha kiroho, mipaka ya Uinjilishaji na isiyo ya Uinjilishaji tunaiwekaje?* Kwa mfano, mtu akichukua kitabu chako akakitoa nakala 1,000 akaanza kuuza kwa waamini huko mitaani, utamdhibitije? *Ukimkamata na kumshtaki, atakuonesha kipengele cha Haki ya Kunakili ulichoweka.* Atasema kwamba alivutiwa sana na kazi hiyo na alipoona wahitaji ni wengi, akatoa nakala ili ainjilishe. Akajitetea zaidi kwamba wanunuaji walikuwa wanatoa fedha ili kufidia tu gharama za kuprinti. *Je, huyo ni mwizi au Mwinjilishaji?*
Nimeanza kwa mtindo huo ili walau tuwe na picha kwamba mada ya wizi wa vitabu, hasa vya kiroho, ni ngumu. Katika muktadha mmoja mtu anaweza kuonekana kwamba ni mwizi ilihali katika muktadha mwingine akiwa anaonekana kama mtoa huduma tu wa Uinjilishaji.
*Wizi ni nini?*
Ukimuuliza mtu akuambie maana ya wizi, huenda akakuambia kwamba *Wizi ni hali ya mtu kuchakua au kumiliki kitu au mali ya mtu au watu wengine au taasisi bila ridhaa ya mmiliki halali.* Je, maana hii inatutosha? Huenda ikatusaidia mbele ya safari. Basi twende nayo kama msaada wa kuelewa mada yetu.
*Mikabala ya Kuitazama dhana ya Wizi*
Pengine yafaa tujadili wizi wa kazi za waandishi kwa kujikita katika mikabala miwili. Mkabala wa kwanza ni *wizi kwa ujumla wake* na wa pili uwe ni *wizi kwa mtazamo wa kitaaluma.*
*WIZI WA KAZI ZA WAANDISHI KWA MTAZAMO WA JUMLA*
Kwa mtazamo huu, wizi unaweza kueleweka kwa kuonesha vitendo vya wizi vinavyotarajiwa kuhusiana na vitabu au kazi za waandishi. Hapa tubainishe mifano tu:
a) Mswada au Kitabu cha mwandishi/waandishi kuchukuliwa na mtu/watu au taasisi kisha kuchapishwa bila ridhaa ya mwandishi/waandishi asilia.
b) Kitabu cha mwandishi/waandishi kutolewa nakala (kurudufiwa) na kuuzwa bila idhini kutoka kwa mmiliki/wamiliki.
c) Kitabu cha mwandishi/waandishi kuchukuliwa na mtu/watu na kubadilishwa kidogo tu kisha kuchapishwa na kuanza kuuzwa sokoni bila idhini ya mmiliki/wamiliki. Kubadilisha huku kunaweza kuwa ni kutoa jina la mwandishi na kupachika la mwizi au mtu mwingine, kubadiliki jina la kitabu wakati maudhui yakiwa ni yaleyale na kadhalika.
d) Kuchukua vitabu vya mwandishi kutoka katika hifadhi yake na kwenda kuuza sokoni bila yeye kujua. Maana hii imezoeleka na ni rahisi kuielewa.
e) Wachapishaji au Wachapaji kuprinti vitabu vya mwandishi kwa kuzidisha idadi ya vitabu ili waviuze sokoni bila mmiliki kujua. Wewe mwandishi unaweza kudhani kwamba vitabu vilivyoko sokoni ni 10,000 kumbe kuna vingine 5,000 au zaidi ambavyo huna taarifa navyo.
*WIZI WA KAZI ZA WAANDISHI KWA MTAZAMO WA KITAALUMA*
Ingawa maana na namna ambavyo wizi unaweza kufanyika inaweza kujumuisha hizo tulizoona katika kategoria ya kwanza, bado wizi wa kitaaluma unaweza kuwa katika namna yake kama:
a) Kuchukua kazi ya uandishi ya mtu/watu wengine na kuimiliki kwa kubadilisha majina, vichwa vya kazi husika, na kadhalika kisha kukusanya kazi hiyo ili upewe digrii au upandishwe daraja.
b) Kutumia maneno au sentensi za kazi ya mtu/watu bila kutaja chanzo. Yale maneno au sentensi zinakuwa zako. Hivyo, usipotaja vyanzo, basi wewe unachukuliwa kuwa mwizi wa kazi andishi. *Hii ikiwekwa kwenye vitabu vyetu vya kiroho, huenda wezi wanaweza kuwa ni wengi sana.*
3. Kuchukua kazi andishi yenye Hakimiliki na kuitafsiri bila ruhusa ya wamiliki au wachapishaji wa kazi asilia. *Hapa pia, kuna dalili za baadhi ya waandishi wa vitabu vya kiroho kukumbwa na tuhuma ya wizi.* Ukichukua kitabu au waraka ulio na Hakimiliki ukautafsiri bila ruhusa, unachukuliwa kwamba wewe ni mwizi.
Wizi wa kazi kitaaluma unaitwa *Plagiarism* kwa lugha ya Kiingereza.
KATIKA TAALUMA
Kuna njia mbalimbali za kubaini wizi wa kazi za kitaaluma. *Njia ya kwanza ni kusoma kazi fulani na kuisikia sauti ya kazi ya mwandishi mwingine bila huyo mwandishi mwingine kutajwa.* Kwa mfano, unaweza kuwa unasoma kazi ya Mwl. Bakize halafu ukawa unapata mwangwi wa kazi nyingine unayoifahamu. Hii ni kwa wale ambao ni wasomaji wazuri tu, ambao wanakuwa wamesoma kazi za watu wengi. Huwezi ukasoma kazi moja ukabaini wizi huu kwa urahisi. Njia ya pili ni ile ya kutumia programu maalumu ya Kompyuta inayoitwa *Antiplagiarism software.* Hii ndiyo njia ya kisasa ya kukamata wezi wa kazi za kitaaluma. *Hata hivyo, njia hii ina udhaifu mkubwa kwa sababu ina uwezo tu wa kubaini kazi zilizoko mtandaoni na kuzifananisha na kazi nyingine tena zilizoko mtandaoni. Sasa hapa, maana yake ni kwamba kama kazi iliyoibiwa haijawekwa mtandani, basi mwizi hatakamatwa.* Lakini, kwa wenzetu walioendelea kiteknolojia, ambao kazi zao huwekwa mtandaoni, njia hii huwasaidia sana.
Katika vyuo vikuu vingi duniani, *mwanafunzi wa Umahiri (Masters) au Uzamivu (PhD) hawezi kukusanya kazi yake ya utafiti bila kuambatisha ripoti ya kiwango cha wizi kilichofanyika.* Mfumo wa kukagua huweka matokeo ya wizi katika asilimia. Kila chuo kina asilimia zake zinazokubalika kwa sababu ya tofauti za teknolojia na programu wanayoitumia katika kubaini wizi.
Huwa kuna adhabu kwa mwizi wa kazi za kitaaluma endapo atabainika kabla, wakati au baada ya kumaliza masomo. Kwa mfano.
1. Kama mwanafunzi amebainika kabla ya kumaliza masomo, anaweza kuambiwa arudie utafiti ili aje na kazi yake mwenyewe.
2. Kama alikuwa anatetea kazi yake, anaweza kuambiwa arudie utafiti au akafukuzwa masomo moja kwa moja.
3. Kama kazi ya utafiti ilikuwa imekusanywa na mhusika akapewa digrii, basi chuo kinayo mamlaka ya kumnyang'anya digrii *(degree revocation)* hata kama ni baada ya muda mrefu. Hili siku hizi linatokea sana duniani.
*HALI YA WIZI WA VITABU AFRIKA YA MASHARIKI*
Kwa kuangalia namna na aina za wizi wa vitabu, utabaini kwamba huenda wizi unafanyika kila siku kwa namna moja ama nyingi hapa kwetu Afrika ya Mashariki.
Katika mazingira ya vitabu vya kiroho huenda wizi ni wa kiwango cha juu kwa sababu ya baadhi ya vitabu kuuzika zaidi. Aidha, tukivitazama vitabu vya kiroho kwa mtazamo wa kitaaluma, basi vingi vitakuwa vimeibiwa sana.
Kuna vitabu vingi sana ambavyo ukivisoma unasikia maneno na sentensi za vitabu vingine vya lugha hiyo au ya Kiingereza.
Pia, ukivitazama vitabu vingi vya kiroho vilivyoko sokoni, utabaini kwamba kuna baadhi ya waandishi wanatumia mwanya wa wasomaji wengi kutojua lugha ya Kiingereza au lugha nyingine. *Mwandishi anaweza kuchukua kitabu cha Kiingereza akakitafsiri sura zake kwa Kiswahili na kukimiliki.* Wanaoweza kubaini wizi huo ni wale wasomaji ambao wanamudu lugha zote mbili na ni wafuatiliaji wa vitabu na vyanzo vingine vya mtandaoni.
Lakini, kuna swali ambalo linabaki bila kujibiwa. *Ikiwa hawa wanaotafsiri au kuiba kazi zetu wanazifikisha kwa wasomaji na wasomaji wananufaika kiroho, je waliofikisha hizo kazi ni wezi?* Je, ikiwa waandishi wa vitabu vya kiroho *wanaandika kwa ajili ya kuinjilisha, wanao ujasiri wa kuwakamata wezi hao na kuwawajibisha kisheria?* Wakifanya hivyo, jamii itawaonaje? Je, wataeleweka kweli kwamba waliandika kwa nia ya kuinjilisha?
NAWAACHIENI NANYI MTAFAKARI. *TUNAKARIBIA MWISHO WA DARASA. ANZA KUHIFADHI MASOMO VIZIRI.*
Karibuni kwa mjadala.
*©️Leonard Bakize* (30.03.2020)
eternalword2018@gmail.com
EWCP na Ushirikishanaji Maarifa
=============