Friday

UHARIRI KATIKA KAZI ZA UANDISHI NA UCHAPISHAJI

0 comments


MADA: *UHARIRI KATIKA KAZI ZA UANDISHI NA UCHAPISHAJI*

Wapendwa, karibuni katika somo letu la nane. Somo linahusu uhariri wa kazi za uandishi.

Kwanza nianze kwa kusema kwamba tunaposema uhariri tuelewe kwamba hii ni dhana pana sana. Uhariri uko katika fani kama za uandishi wa vitabu, magazeti, posti za mitandaoni. Pia, kuna uhariri katika kazi za filamu, redio, picha, na kadhalika. Hivyo, kutokana na hali hii, ndiyo maana tunalazimika kusema *uhariri wa vitabu* ili tujibane kwenye kumbo moja tu. Hizo nyingine hatutazizungumzia.

*Uhariri ni nini?*
Kwa ujumla, si rahisi kutoa maana rahisi ya uhariri. Hii inatokana na ukweli kwamba uhariri unafanywa na wengi na ni kazi ya kimchakato. Uhariri unaanzia kwa mwandishi mpaka kwa mchapishaji wa kitabu.

Hata hivyo, tuseme tu kwamba uhariri *unahusisha michakato ya kupitia mswada au kazi ya msanii kwa nia ya  kuifanya kazi hiyo iwe bora zaidi, ieleweke vizuri, ionekane vizuri na pia iendane na jamii andikiwa.*

Katika mazingira haya basi uhariri unaweza kukushawishi uongeze kitu au uondoe kwa nia ya kuifanya kazi iwe nzuri kwa kuondoa makosa mbalimbali.

Hapo awali nilisema kwamba uhariri ni jambo pana sana na wengine huwa tunalichukulia katika maana ambayo ni finyu. Nilisema kwamba uhariri unaanzia kwa mwandishi mwenyewe mpaka kwa mchapishaji. Hebu tuone baadhi ya michakato ya uhariri ili tuongeze maarifa.

*1. Uhariri endelevu (developmental editing)*
Kama jina lenyewe linavyoonesha, uhariri huu unafanyika kwa mswada ambao bado unaandikwa. Uhariri huu unafanywa na mwandishi na mtu mwingine ambaye anaweza kuombwa na mwandishi ili kuona kama uandishi wa kazi fulani unaendelea katika misingi sahihi.

Kwa mfano, unaweza kuwa unaandika kitabu lakini ukatamani kumpa rafiki yako kipande cha kazi ili aone kama unakwenda vizuri. Huyu anayepitia kazi ambayo bado inaandikwa anapaswa kuwa mweledi na mbobevu ambaye anaweza kukushauri kama uandishi wako katika kazi husika unaenda sawa au la. Kwa hiyo, mtu huyu anaweza kukushauri ubadili baadhi ya vipengele au uwe makini na lugha au kitu chochote anachoona kwamba kitaathiri ubora wa andiko lako.

*2. Uhariri wa kuvumbika mswada (manuscript keeping editing)*
Aina hii haitajwi na wataalamu wengi kama mojawapo ya aina za uhariri. Hata hivyo, aina hii ni muhimu sana.

Katika mazingira ya uandishi tutakubaliana kwamba ukikamilisha mswada wako wa kitabu, halafu ukauhifadhi mahala kwa mwezi mmoja au miwili, kisha uuchukue na kuusoma tena, lazima utabaini makosa madhaa yanayohitaji marekebisho. *Huo ndio uhariri wa kuvumbika.* Kwamba unahifadhi kazi yako kwa kipindi fulani. Unaendelea kufanya mambo mengine. Baada ya muda unairudia tena kazi yako. Njia hii ni nzuri sana kwa sababu inakusaidia kuona mapungufu yako mwenyewe na kuyarekebisha kabla hujaipeleka kazi kwa mchapishaji.

*3. Uhariri wa mjengo wa mawazo na mantiki (Line editing)*
Uhariri huu unaweza kufanywa na mwandishi pamoja na mtu mwingine ambaye ameombwa amsomee mwandishi na kumpa maoni. Hii huwa wengi tunaifanya. Mwandishi anampatia labda rafiki yake au mtu mwenye ubobevu katika eneo husika na kuomba maoni kuhusiana na kazi. *Huyu msomaji kwa kiasi kikubwa hataangalia kila kitu.* Huyu ataangalia mjengo wa sentensi unaotokana na matumizi ya maneno ili kuleta maana. Hapa mhariri huyu ataangalia mawazo ya jumla na mantiki ya maudhui. Ndiyo maana huyu anaweza kusoma kazi haraka na akakuambia kwamba kazi ni nzuri lakini inapaswa iende kwa mhariri wa kitaaluma (tutamuona baadaye huyo mhariri).

*4. Uhariri wa kitathmini (Evaluation editing)*
Huu ni uhariri ambao unafanywa na kampuni au watu wenye mamlaka kwa kufuata vigezo fulani ili kuona kama kazi husika inakidhi viwango au la. Lengo ni kutoa ushauri ili kazi irekebishwe au kuboreshwa kwa nia ya kuifanya iwe bora zuri.

Kama tulielewa vizuri wakati wa somo la uchapaji na uchapishaji, tulisema kwamba mchapishaji anapopokea kazi ya mwandishi huipeleka kwenye kamati yake ili kuipima kazi hiyo kama ni bora au la. *Wapitiaji hawa ndio ambao wanafanya tathmini.* Tukumbuke kwamba tathmini hii ni sehemu ya uhariri kwa sababu wasomaji wanasoma kazi na kuandika ripoti inayoonesha ubora na udhaifu wa kazi husika. Wapitiaji hawa kwenye ripoti hueleza pia namna gani mwandishi anaweza kuboresho mswada ili uwe mzuri zaidi. Zoezi hilo nalo linaingizwa kwenye michakato ya uhariri. Tena kazi haisomwi na mtu mmoja. Aidha, watu kama watatu wanaweza kusoma mswada mmoja tena bila kufahamiana. Nia ni kuona kama maoni ya ripoti zao hayatakuwa na upendeleo. *Ndiyo maana kazi ambayo imepitia kwa mchapishaji inaaminiwa zaidi.*

*4. Uhariri wa kina wa mswada (copy-editing)*
Huu ni uhariri wa kina ambao huwa unafanywa na wahariri waliobobea au wenye taaluma za uhariri. Wengi wetu huwa hatuwapelekei kazi zetu kwa sababu ya gharama. Kwa mfano, TATAKI (UDSM) wanatoa huduma za uhariri. BAKITA, nao wanatoa huduma za uhariri. *Gharana ya kuhariri ukurasa mmoja ni sh. 5,000/=* Maana yake kama mswada wako una kurasa 100 inabidi uandae *sh. 500,000/=* kwa ajili tu ya uhariri.

Uhariri huu kama hujausomea au huna uzoefu mpana wa kazi za uandishi si rahisi kuufanya. Wahariri hawa wanapopitia mswada wako wanaangalia karibu kila kitu ili kuufanya mswada wako uwe mzuri zaidi. Kwa mfano, wataangalia kama umetumia kweli lugha andishi, kama herufi ziko sawa, wataangalia uteuzi wa maneno na sentensi, wataangalia matumizi ya nyakati, wataangalia kama mtiririko wa mawazo uko sawa, wataangalia kama kila aya imebeba wazo lake, wataangalia sura zako kama zinapokezana taarifa, wataangalia kama umetumia vyema alama za uandishi kama vituo, mikato, viulizo, mabano, na mengine mengi. *Ndiyo maana kazi ambayo imepitiwa na mhariri lazima iwe na mambo ya kurekebisha.* Kutokana na weledi wa mwandishi, kazi inayotoka kwa mhariri inaweza ikaja na marekebisho mengi au machache.

*5. Uhariri wa prufu (proofreading/editing)*
Ikumbukwe kwamba baada ya kazi kutoka kwa mhariri utatakiwa kuingiza marekebisho na kuituma tena kwa mchapishaji. Mchapishaji atapeleka kazi yako kwa msanifu ili aweke picha au vielelezo kama vinahusika. Kazi ikitoka hapo itamwendea mtaalamu wa kuseti kitabu. Kumbuka hapo awali uliandika kwa mfumo wa kawaida kwenye Kompyuta na kazi yako ilikuwa kwenye mwonekano wa karatasi ya A4. Sasa vitabu huwa vinasetiwa kwa ukubwa tofauti na katika programu tofauti. Baada ya kitabu kusetiwa, mwandishi atarudishiwa mswada uliosetiwa ili ahakiki kama kila kitu kiko sawa na hakuna uharibifu uliofanyika katika kupanga maneno, sentensi, picha na kadhalika. *Usomaji huu wa kazi ambayo imeshasetiwa ndio huitwa uhariri wa prufu.* Baada ya uhariri huu basi kitabu kinaingizwa kwenye mashine kwa ajili ya kuprintiwa.

*6. Uchungaji au Uratibu wa michakato ya uzalishaji wa vitabu (Book-shepherding)*
Wataalamu wengi wa mambo ya vitabu wanamtambua mchapishaji kama msimamizi pia wa zoezi la uhariri na kumpa aina inayojitegemea. Katika kusimamia ubora wa vitabu vyake, Mchapishaji huwa ana vigezo vya kazi bora. Hivyo, vigezo hivyo vinamfanya na yeye awe na aina yake ya uhariri. *Ndiyo maana unaweza kupeleka mswada wako kwa mchapishaji, halafu baada ya tathmini ukaambiwa kwamba samahani kazi yako haikukidhi viwango vyetu.* Maana yake naye ni msimamizi wa ubora wa vitabu katika nafasi tu ya uratibu. Hii ni aina ambayo ni ya kimjadala kwa sababu wengine hawaoni sababu ya kuitenga kama aina.

Kwa ufupi, hizo ni aina chache za uhariri na nina imani kama mmesoma mtakubaliana na mimi kwamba kumbe kazi zetu huwa hazihaririwi ipasavyo. *Hata hivyo, sinamaanishi kwamba kazi zetu si bora.*

*USHAURI WANGU KUHUSIANA NA UHARIRI WA KAZI ZA KIROHO, HASA ZA KIKATOLIKI* Kwa uzoefu wangu wa miaka 9 katika mambo ya uandishi, waandishi wengi huwa hatumjali mhariri. Hivyo, kazi zetu zinakuwa na makosa lukuki ya lugha za mazungumzo, ukiukaji wa alama za uandishi na kadhalika. Huwa tunajiaminisha tu. *Huwa nikisoma miswada mingine najikuta nawaonea huruma wanaohusika katika kutoa IMPRIMATUR. Nahisi kama wanakutana na kazi nyingine za ajabu.*

Unakuta mtu amemaliza kuchapa kazi yake, hajaipitia tena ili kuondoa makosa madogomadogo halafu anakwambia nina haraka nataka nichapishe.

Mazingira haya huwa yananiwazisha kwamba ikiwa tunawapelekea Maaskofu wetu miswada ikiwa katika namna niliyoieleza, basi tunawatwisha mizigo mizito. *Kwa mtazamo wangu, kazi inayoenda kupitiwa ili ipate Imprimatur, inapaswa kuwa imesomwa tena na tena ili isiwe na makosa ya kawaida.* Hii itawasaidia wapitiaji wamakinike zaidi kwenye kipengele cha maudhui kwa sababu ndicho kinachowahusu zaidi. *Lakini kazi ikiwa na makosa mengi, basi huwachosha sana au wanaweza kujikuta wanahangaika na makosa ya uandishi na kusahau maudhui.*

Hivyo, kazi zetu zihaririwe vizuri ili ziwe bora na kuwawezesha wasomaji kupata maudhui kirahisi.
============

KARIBUNI KAMA KUNA MASWALI ILI TUPANUE SOMO.

*© Leonard Bakize (27.03.2020)*

*****************

No comments:

Post a Comment