Monday

Kitabu: KURASA ZA MWANZO ZA KITABU

0 comments


MADA: *TAARIFA ZA KURASA ZA MWANZO ZA KITABU*

Wapendwa, karibuni katika somo letu la Nne ambalo linahusu taarifa au *kurasa za mwanzo katika kitabu.* Kabla sijaendelea na somo hili, ninaomba nibainishe kwanza kwamba kwa *kawaida kitabu kina sehemu kuu nne;* Sehemu ya kwanza ni *kurasa za mwanzo;* sehemu ya pili ni *kurasa za maandishi yenyewe;* sehemu ya tatu ni *kurasa za mwisho;* na sehemu ya mwisho ni *jalada.* Hivyo, somo la leo litahusu sehemu ya kwanza tu. Sehemu nyingine tutaziona baadaye. Hata hivyo, katika mtiririko wa masomo yetu, sehemu ya tatu na ya nne za kitabu zitawekwa pamoja.

Jambo la pili ambalo tunapaswa kulifahamu mapema ni kwamba taarifa hizo, wakati mwingine huwa hazina mpangilio maalumu. Kutokana na mwandishi au mchapishaji, taarifa hizo zinaweza kupangiliwa tofauti kutoka kitabu kimoja mpaka kingine. Hata hivyo, kuna mpangilio ambao kwa kiasi kikubwa tunatarajia kuuona. Lakini, nitakayoeleza yasiwe kipimo cha hukumu bali yachukuliwe tu kwamba ni mfano.

Jambo la tatu tunalopaswa kuliweka akilini mwetu mapema ni kwamba mara nyingi, kurasa za mwanzo huwekewa namba za Kirumi tofauti na zile tutakazozikuta kwenye sura za kitabu husika. *Hata hivyo, katika baadhi ya vitabu, kurasa zote za sehemu ya kwanza huwa hazina kurasa kabisa.* Lakini, inashauriwa kuweka namba japo zitapaswa kuwa tofauti na zile za maandishi ya kitabu chenyewe. Sasa tuanze kuziona kurasa za mwanzo za kitabu.

*1. Ukurasa wa kwanza*
Ukurasa huu huwa na jina la kitabu, kama linavyosomeka kwenye jalada la juu. Nia ni kwamba ikiwa jalada litachanika bado msomaji ataweza kupata jina la kitabu kwa urahisi. Ukurasa huu huwa hauwekewi namba yoyote. Ukurasa huo unakuwa na jina la kitabu tu.

*2. Ukurasa wa pili*
Kwa baadhi ya vitabu, huo ukurasa unawekwa orodha ya machapisho yanayofanana na kitabu husika. Pia, kama kitabu husika kiko katika mtiririko, basi ukurasa huo utawekwa orodha ya vitabu vingine vilivyo katika mtiririko huo. Hata hivyo, kwa vitabu vingine, ukurasa huu huwa hauna haja ya kuwa na orodha ya vitabu vingine. *Hivyo, tuseme kwamba ukurasa huu huwa na orodha ya vitabu vingine kwa baadhi tu ya vitabu.*

*3. Ukurasa wa tatu*
Ukurasa huu huwa una jina kamili la kitabu likiwa na jina la mwandishi (au mfasiri endapo kitabu ni tafsiri) chini, pamoja na nembo ya mchapishaji kama ipo na jina la mchapishaji .

*4. Ukurasa wa nne*
Ukurasa huu unatarajiwa kuwa na mwenye haki ya kumiliki maandishi (kwa alama ya ©), lazima kuwe na mwaka wa kuchapishwa,  huandikwa pia toleo au chapa ya kitabu, lazima pia kuwe na jina na anwani ya mchapishaji. Aidha, kunapaswa kuwa na taarifa za mji na nchi kitabu kilipochapishiwa na 6mwisho lazima kuwe na Haki ya kunakili. Endapo kitabu husika kiliwahi kuchapishwa miaka ya nyuma na Kampuni nyingine ni vizuri pia kuyasema kwenye ukurasa huu.

*5. Ukurasa wa tano*
Kwa baadhi ya vitabu, ukurasa huu huwa na maneno machache ya kuonyesha heshima kwa mtu au kikundi cha watu. Mtu au watu hao wanaweza kuwa hai au wakawa ni marehemu. Ikumbukwe kwamba ukurasa huu si wa lazima sana. Itategemeana na maamuzi ya mwandishi wa kitabu husika. Ukurasa huu hupewa jina la Tabaruku.

*6. Ukurasa wa sita*
Ukurasa huu unaweza kuwa wa vifupisho vyote vilivyotumika katika kitabu. Nia ni kumsaidia msomaji kwamba atakapoona vifupisho hivyo ndani ya kitabu asijiulize maswali. Waandishi wengi huwa wanapuuza taarifa hizi. Lakini, kama vifupisho vipo kitabuni, ni vizuri vikafahamika mapema.

*7. Ukurasa wa saba*
Ukurasa huu mara nyingi huwa ndio unaoonesha yaliyomo kwenye kitabu. Hapa waandishi wanashauriwa kujifunza namna nzuri ya kuandika yaliyomo kwenye kitabu. Ikiwa mwandishi ndiye anayechapa kitabu chake basi ukurasa huu unatakiwa kuandikwa kwa mfumo wa Kompyuta unaojiendesha wenyewe (automatic). Ushauri huu unatolewa ili walau kumsaidia mwandishi kukwepa usumbufu. Ikiwa yaliyomo itaandikwa kwa namna ya kawaida (manual) mabadiliko yanapotokea ndani ya mswada itakuwa vigumu sana kuyabaini na kuyafanyia mabadiliko. Lakini, yaliyomo ikiandikwa kwa namna inayojiendesha yenyewe, basi mabadiliko yakitokea ndani ya kitabu, mwandishi atakuwa anahuisha (update) tu kipengele cha yaliyomo.

Katika ukurasa huu, mwandishi anashauriwa kwamba yaliyomo ioneshe sura za kitabu na vipengele vyake vidogo. Aidha, yaliyomo yasisahau kujumuisha vipengele muhimu vya awali kama Dibaji, Utangulizi, vifupisho, na kadhalika.

*8. Ukurasa wa nane*
Katika baadhi ya vitabu, ukurasa huu unaweza kuwa na aidha utangulizi au Dibaji. Basi, kwa sasa tuchukulie kwamba mambo hayo mawili yatatenganishwa. Hapa tuzungumzie Dibaji kwanza.

Kama tulivyowahi kudokeza kwenye mijadala, utangulizi na Dibaji huwa viko kwenye kapu moja la kutangulia maandishi ya sura za kitabu. Kuna baadhi ya vitabu huwa na kimojawapo tu kati ya Dibaji na Utangulizi.

Hata hivyo, ikiwa tunataka kuandika kitaalamu, basi tusifuate mazoea bali tufuate taratibu na sababu za msingi. *Inasisitizwa kwamba Dibaji isiandikwe na mwandishi mwenyewe.* Nia ya Dibaji ni mtu mwingine mwenye utaalamu wa eneo husika au mwenye mamlaka zaidi, kuelezea kile kilichoandikwa na mwandishi. Hii inalenga kuwahakikishia wasomaji kwamba kilichoandikwa kina viwango stahiki na kuna maarifa kedekede. *Kwa hiyo, Dibaji inalenga kumsemea mwandishi. Sasa kama mwandishi atajisemea na kukipigia upatu kitabu alichoandika mwenyewe, kwa kweli haitapendeza.*

Katika mazingira ya kawaida, inatarajiwa kwamba Mlei akiandika kitabu cha kiroho basi Dibaji yake itaandikwa na Padre au Askofu. Kama ni Padre aliyeandika kitabu basi Dibaji yake itaandikwa na Padre mwingine mwenye uzoefu au ubobevu kumzidi au Askofu. Ikiwa kitabu kimeandikwa na Askofu basi Dibaji itaandikwa na Askofu mwingine. Hata hivyo, ikiwa Askofu au Padre ameandika kitu ambacho ni cha kitaalamu zaidi na mwenye uzoefu na maarifa ya kubobea ni Mlei basi halitakuwa jambo la ajabu kuona Mlei akiwa ameandika Dibaji ya kitabu hicho. Haya ni mawazo tu. *Lakini, hoja muhimu hapa ni kwamba Dibaji inaandikwa na mtu mwingine na siyo mwandishi. Tena mtu huyo anatarajiwa kuwa na uzoefu au weledi zaidi katika eneo lililoandikiwa.* Katika baadhi ya vitabu vya kitaaluma, sehemu hii pia yaweza kuandikwa na Mhariri. Hii ni kwa sababu Mhariri ni mtaalamu na inatarajiwa kwamba anaipitia kazi husika kwa kina na anao uwezo wa kukisemea kile alichokihariri ili kukipa uzito kitabu mbele ya wasomaji na kuwahakikishia kwamba mwandishi amefaulu na anao uwezo wa ujuzi wa yale aliyoandika. Ukijiandikia mwenyewe Dibaji ni kama vile unajisifia mwenyewe

*9. Ukurasa wa tisa*
Ikiwa Dibaji na Utangulizi vitatenganishwa, basi ukurasa huu utakuwa na utangulizi. Utangulizi unapaswa kuandikwa na mwandishi mwenyewe. Kutokana na kuandika kimazoea basi kuna vitabu ambavyo utangulizi wake umeandikwa na watu wengine. Nia ya utangulizi ni kueleza shabaha ya kitabu, walengwa wa kitabu (wasomaji), maelezo mafupi kuhusiana na yaliyoandikwa na jinsi yalivyopangwa kitabuni. Hapa mwandishi anaweza kutoa ufupisho sana wa maudhui ya kitabu kwa kuelezea kwa kifupi yale yanayopatikana katika kila sura. Sehemu hii ikiandikwa vizuri huwasaidia sana wale wanaosoma vitabu kwa ajili ya utafiti. Mtafiti akisoma tu utangulizi walau atajua kwamba kitabu kinamfaa au la. Kwa hiyo, sehemu hii sasa inapaswa kuandika vizuri ili kumpa hamu msomaji kuhusiana na kilichomo ndani.

Aidha, kwa baadhi ya vitabu, sehemu hii humalizika kwa kuwataja watu wachache waliomsaidia mwandishi kwa namna mbalimbali. Kama watu hawa ni wengi sana, basi inashauriwa kuwe na ukurasa maalumu wa shukurani.

*10. Ukurasa wa kumi*
Kama orodha ya waliomsaidia mwandishi ni ndefu au mwandishi anatamani kueleza namna alivyosaidiwa, basi ukurasa wa kumi utakuwa ni kwa ajili ya kutoa Shukurani. Sehemu hii siyo ya kuorodhesha ukoo wote wa mwandishi. Waandishi wengi sana huorodhesha wake/waume zao, watoto, marafiki, wazazi, na kadhalika. Ikiwa watu hao kweli wana mchango kwa kilichoandikwa basi haina shida. Lakini, nia ya ukurasa huu ni kuwashukuru kweli wale waliowezesha kitabu kukamilika. Watu hao wanaweza kuwa wahakiki au wasomaji wa mswada, mwandishi wa dibaji, watoa data (kama kitabu ni cha utafiti), Wapiga chapa, Wachapishaji, na kadhalika. Hivyo, hapa uhuru unabaki kwa mwandishi mwenyewe kwamba kwa hakika ni akina nani wanapaswa kushukuriwa. *Lakini ni jambo la kushangaza kuona kitabu ambacho mwandishi hamshukuru yeyote. Hii huchukuliwa kwamba mwandishi ni mbinafsi na hatambui michango ya wengine katika zake.* Kutokana na michakato ya uandishi haitarajiwi kwamba mwandishi atafanya kila kitu. Hivyo, hakuna sababu ya kutoshukuru waliokusaidia.

*Hitimisho*
Baada ya kurasa za utangulizi, basi kurasa zitakazofuata ni za maandishi yenyewe ya kitabu (yaani yale yanayobeba kitabu). Ikumbukwe kwamba mpangilio wa kurasa za utangulizi si sheria. Ndiyo maana vitabu vinatofautiana kuhusiana na vipengele vya utangulizi. Mpangilio nilioupendekeza unaweza ukafuatwa au usifuatwe kutokana na utashi wa mwandishi mwenyewe.
****************

*© Leonard Bakize (16.03.2020)*
eternalword2018@gmail.com

*KARIBUNI KWA MJADALA*
===========

No comments:

Post a Comment