Wednesday

HAKI YA KUNAKILI NA HAKIMILIKI

0 comments


MADA: *HAKI YA KUNAKILI NA HAKIMILIKI*
Wapendwa, karibuni sana katika somo letu la Nane ambalo linahusu Haki ya Kunakili na Hakimiliki. Katika vitabu na machapisho ya kitaaluma, mara nyingi kuna namna tatu ya kurejelea jambo hilo. Wengine huita *Hakimiliki,* wengine huita *Haki ya Kunakili* na wengine huita *Hatilinzi* (hasa Wakenya).

Pamoja na maneno hayo kutumika kama yenye maana moja, lakini *Hakimiliki* tofauti na hayo mengine mawili, lenyewe linasisitiza zaidi *nani mmiliki wa kitabu au chapisho husika.* Katika vitabu, Hakimiliki huwa inaoneshwa kwa alama hii 👉🏾 ©️

*Haki ya kunakili au Hatilinzi* maana yake nini hasa? Bila kutumia maneno ya kuzunguka wala maneno ya kitaalamu, hapa kinachorejelewa ni kwamba kitabu ni mali ya mtu fulani na hivyo, *Haki ya Kunakili* ni maelezo au ufafanuzi wa mmiliki wa kitabu au chapisho kwa msomaji, kuhusiana na kiasi au kiwango cha uhuru alionao msomaji katika kunufaika na kitabu husika.

Kwa hiyo, msomaji anapewa ufafanuzi mfupi kuhusiana na uhuru alionao katika kutumia kitabu husika.

Mara nyingi *Haki ya Kunakili* inakuwa na maneno yanayomtahadharisha msomaji na kumpa uhuru wa haya:

1. Kutumia kitabu atakavyo bila masharti. Mara nyingi vitabu hivi huwa huru kwa ajili ya kutoa maarifa kwa umma, na mtu anaweza kutoa nakala na kuwagawia wengine bila masharti wala kusumbuliwa na mwandishi wala mchapishaji. Aidha, kitabu chochote ambacho hakina zuio lolote la matumizi, kinaangukia katika kundi hili. *Mfano mdogo tu ni kitabu cha Godius Rweyongeza.* Kitabu hiki maana yake, kina mmiliki lakini kiko huru kwa matumizi. Changamoto hapa ni kwamba msomaji anaweza kukichukua akakiweka vizuri zaidi na kukichapisha na kuwa mali yake. Hapo kumbana inaweza kuwa ngumu.

2. Kutumia kitabu kwa ajili ya kupata maarifa na kuwafikishia wengine bila lengo la faida binafsi kibiashara. Yaani, *ikiwa mtu amesoma kitabu na kutaka kuwapa wengine basi anaruhusiwa hata kutoa nakala lakini si kwa ajili ya biashara au kujipatia faida ya fedha kupitia kitabu hicho.* Mara nyingi, vitabu vya kiroho vinaangukia kwenye kundi hili. Kwamba msomaji anufaike kupata maarifa au elimu na asitafsiri au kutoa nakala kitabu hicho kwa nia ya biashara. Lakini, ikiwa ni kwa ajili ya Uinjilishaji kitabu chaweza kutumiwa kwa uhuru.

3. Kitabu kisomwe tu na kupata maarifa. Msomaji asiruhusiwe kutoa nakala, kutafsiri, n.k. bila idhini ya mwandishi au mchapishaji.

*KWA NINI VITABU VYA KITAALUMA VINALINDWA?*

1. Ni kwa sababu ni jasho la mtu. Hivyo, mwandishi au mchapishaji hataki mtu mwingine ajipatie kipato kirahisi kupitia jasho la mwingine.

2. Kulinda uwezekano wa kukishushia hadhi kitabu. Kwa mfano, mtu anaweza kuchukua kitabu kinachopendwa sokoni na kukiongezea maarifa au kubadilisha baadhi ya maudhui ili mwandishi aonekane hana hadhi au ni mpotoshaji. Sasa ili kudhibiti, inabidi huo uhuru uminywe.

3. Kwa sababu ya uratibu wa uchapishaji na usambazaji wa kitabu husika. Kwa mfano, kama kitabu hakilindwi, mchapishaji hawezi kujua kama wasomaji waliopata kitabu ni wengi au wachache. Unaweza kutoa nakala 5000 ukazisambaza sokoni. Mtu mwingine mitaani akichukua kitabu hicho akakitoa nakala 30,000 na kuanza kukiuza, haitakuwa rahisi kwa mchapishaji kujua mahitaji ya wasomaji baadaye. Mchapishaji anaweza kuprinti tena vitabu wakati wasomaji huko mitaani wanavyo vya kutosha kutoka kwa aliyetoa nakala au aliyegushi. Hivyo, Haki ya Kunakili, walau inaepusha usumbufu huo kibiashara.

Hizo, ni sababu chache tu zinazowasukuma waandishi na wachapishaji kuweka Haki ya Kunakili kwenye vitabu vyao.

*IKIWA VITABU VYA DINI VINA NIA YA KUINJILISHA, KWA NINI NAVYO VINAWEKEWA HAKI YA KUNAKILI?*

Kwanza ni kweli kabisa kwamba ukichukua vitabu vyetu vya kiroho navyo vinameandikwa hizo *Haki za Kunakili.* Kwa hiyo, hebu tujibu kwamba ingawa tunaandika ili kuinjilisha, kwa nini tunawazuia wasomaji kuwa huru kutumia vitabu vyetu kama watakavyo. Zifuatazo ni baadhi ya sababu:-

1. *Kutojua maana yake na kuiga tu.* Waandishi tulio wengi, hatuelewi maana ya Haki ya Kunakili. Hivyo, tukishaona wengine wameandika, *nasi tunadhani ndiyo utamaduni na hivyo nasi tunapachika maneno hayo.*

2. *Kupunguza uwezekano wa wazushi kupenyeza maarifa potofu kwa hila zao.* Kama tutakavyoona katika somo linalohusu IMPRIMATUR, Idhini hiyo ya kuchapisha inatokana na wenye mamlaka fundishi kujiridhisha kwamba kitabu hakina maudhui ya kizushi au yanayopingana na mafundisho sahihi ya Kanisa. *Sasa kama wasomaji wako huru kufanya chochote, maana yake mtu anaweza kuchukua kitabu chako akakichapisha upya, akiwa amebadilisha baadhi ya maudhui ili kupotosha watu wa imani husika.* Iwapo hilo litafanyika kwa hila, maana yake ile Imprimatur itapoteza umaana wake.

3. Kulinda maslahi ya mwandishi au mchapishaji. Hata kama tutakwepa kusema kwamba vitabu vyetu pia vinatupatia fedha kwa matumizi mbalimbali, ukweli unabaki palepale. Kwanza kuchapisha kitabu ni gharama. Sasa kurudisha hiyo gharama kupitia faida ya uuzaji, huchukua muda mrefu sana kutokana na Waafrika kutokupenda kusoma. Sasa, katika mazingira haya, wewe unahangaika kutafuta wasomaji wa kununua vitabu, halafu kuna mwingine tena mitaani naye anatumia kitabu chako ili naye afaidi kibiashara. Hapa ustaarabu unakosekana hata kama kitabu kina lengo la kuinjilisha. Huyu anayeibiwa, hatapata tena mtaji wa kuendeleza Uinjilishaji wake kwa kuprinti vitabu vingine. Mazingira haya yanamlazimisha mchapishaji au mwandishi kuweka Haki ya Kunakili.

*JE, HIZO HAKI ZA KUNAKILI TUNAZOZIANDIKA VITABUNI NI KWELI KISHERIA ZINAWEZA KUTULINDA?*

Kwa ufupi, jibu ni ndiyo na hapana. Kwa taarifa yetu, anayesimamia haki za kunakili kitaaluma huwa ni *mchapishaji.* Kisheria, mchapishaji rasmi analindwa kwa sababu:

1. Kampuni yake imesajiliwa kisheria huko BRELA. Mpaka apate usajili ya Kampuni, lazima mchapishaji atimize vigezo vingi vya kisheria. Kuna nyaraka nyingi zinahusika kulingana na taratibu za nchi ikiwemo kusaini fomu za maadili.

2. Mchapishaji kisheria ni mfanyabiashara. Ndiyo maana analipa kodi TRA. Kwa hiyo, kwa sababu ya kutimiza vigezo vya kulipa kodi, bidhaa zake zinalindwa kwa namna fulani.

3. Mchapishaji pia ana leseni ya biashara ambayo hutolewa na Manispaa au mamlaka ya serikali mahali ofisi ilipo. Hivyo, kwa kuwa analipia leseni yake lazima kuna haki ya kulindwa kwa biashara zake ambazo ni vitabu.

*KUHUSU KITABU KULINDWA*
Kwa maelezo walau machache niliyotoa hapo juu, tunaweza kuona kwamba *kumbe walau mwandishi ambaye amepitia kwa mchapishaji, kitabu chake hata kama ni cha kidini, bado kuna sheria lukuki zinakigusa kama bidhaa iliyoko sokoni.* Mwandishi au mchapishaji akibaini kwamba kuna mtu karudufu kitabu sokoni, kesi ikienda mahakamani, inakuwa na mashiko zaidi kisheria.

*Kwa kuwa waandishi wengi tunafanya Uchapishaji binafsi (self publishing), hata ukimkamata mtu ukampeleka mahakamani unaweza nawe kujikuta matatani.* Utaulizwa nani mchapishaji wako ili waone kama analipa kodi na je huyo mchapishaji anatambulika kisheria? *Ukisema unajichapishia mwenyewe na kuuza, nadhani wote tunaweza kutabiri hapa kwamba nini kitafuata.*

Kwa hiyo, ingawa tunaandika hizo Haki za Kunakili kwenye vitabu vyetu, *tunaandika tu kama utamaduni au ni kama kuweka kinyago cha mtu kwenye shamba la karanga ili kuwatishia wanyama au ndege waharibifu.* Kisheria hatuko salama kwa sababu wengi tunajichapishia. Ninayo mifano kadhaa ya waandishi ambao vitabu vyao vimerudufiwa na wajanja na vinauzwa mitaani. Waandishi wanapopata taarifa huishia kusikitika tu na hawawezi kufanya lolote kisheria. Kwa sababu ya maadili sitataja hata mfano wa mwandishi mmoja. *Lakini, aminini tu kwamba huko mitaani vitabu kama vinauzika vinaibiwa na kutolewa kopi na watu kwa manufaa yao kibiashara.*

*JE, KWA MAZINGIRA YA TANZANIA VITABU VINALINDWA KWELI?*
Naomba kuwaambia ukweli kwamba kiutaratibu, hizi haki za kunakili tunaandika tu. Ukiomba ufafanuzi kule Maktaba Kuu, ambapo ndipo huwa tunapata ISBN na Bakodi, watakuambia ukweli.

*Watakuambia ukweli kwamba ili Haki ya Kunakili ifanye kazi kwa 100%, kitabu inabidi kichukuliwe kama kazi za ubunifu ambazo zinalindwa na serikali kupitia Wizara husika. Kwa wale tunaofuatilia filamu za Kitanzania, zile zilizosajiliwa na serikali, zimewekewa lebo ya utambuzi.* Ile inamaanisha kwamba kazi ile ikikamatwa imeibiwa mhusika anaweza kuchuliwa hatua kisheria. Kwa mazingira haya, kumbe hata *mwandishi anaweza kwenda kusajili kitabu chake kwenye Wizara inayolinda haki za wasanii au wabunifu ili kilindwe na sheria.* Lakini je, huo ujasiri atautoa wapi wakati si mfanyabiashara?

MWISHO WA SOMO LA LEO
*Kwa ufupi, ingawa vitabu vyetu vina maneno ya Haki ya Kunakili, lakini kisheria haviko salama. Vingi haviko salama kwa sababu tunajichapishia wenyewe kwa sababu ya Uinjilishaji.*
================

*©Leonard Bakize* (25.03.2020)

EWCP na Ushirikishanaji Maarifa.
***************

KARIBUNI TUPANUE SOMO KWA MJADALA ILI TUJIFUNZE ZAIDI

No comments:

Post a Comment