Friday

Intaneti, M-Pesa vyachangia Vodacom Tanzania kupata faida ya mabilioni

0 comments


  • Faida hiyo baada ya kodi ni ya kipindi cha miezi sita ya awali ya mwaka 2019.
  • Mapato ya M-Pesa yameongezeka kwa asilimia 15.9 kutoka yale ya mwaka jana kipindi kama hicho.
  • Usajili wa laini za simu kwa alama za vidole wazidi kuibua wasiwasi wa kupoteza wateja.

Dar es Salaam. Faida ya kampuni ya huduma za simu ya Vodacom Tanzania imeongezeka kwa asilimia 32.6 hadi Sh51.4 bilioni ndani ya miezi sita ya kwanza ya mwaka 2019 ikichagizwa zaidi na kuongezeka kwa mapato yatokanayo na huduma za kifedha na intaneti.
Matokeo hayo ya kukuza faida angalau yanaamsha matumaini zaidi kwa wawekezaji wa kampuni hiyo ya kupata gawio lililonona kidogo siku zijazo. Bei ya hisa za kampuni hiyo imekuwa na ukuaji tambalale kwa muda mrefu sasa.
Menejimenti ya kampuni hiyo iliyoorodheshwa katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) imekuwa ikipata shinikizo kutoka kwa wanahisa wake la kubana matumizi na kuongeza faida ili na wao waanze kufaidika na matunda ya uwekezaji wao.
“Faida baada ya kodi imeongezeka kwa asilimia 32.6 hadi Sh51.4 bilioni ikichagizwa zaidi na mapato imara na mpango wa kupunguza matumizi,” amesema Hisham Hendi, Mtendaji Mkuu wa kampuni hiyo kubwa ya simu nchini katika ripoti ya nusu mwaka unaoishia Septemba 30.
Hendi amesema nguzo zao kuu za ukuaji za M-pesa na intaneti zimeendelea kuonyesha mwenendo chanya licha ya kuwepo kwa ushindani mkali sokoni.
“Mapato ya M-Pesa yaliongezeka kwa asilimia 15.9 wakati yale ya intaneti yaliongezeka kwa asilimia 17.4 huku jitihada za kuimarisha mapato yatokanayo na huduma za sauti zikionekana kuzaa matunda,” amesema.
Vodacom imesema kuwa mapato yatokanayo na huduma nayo yamepaa kwa asilimia 6.5 katika kipindi hicho cha nusu mwaka huku kukiwa na fursa zaidi ya kuongezeka.

Kampuni hiyo imesema kuwa ilifanikiwa kuongeza wateja 760,000 ndani ya miezi sita ikiwa ni ongezeko la asilimia 5.5 na kufanya jumla ya idadi ya wateja wake kufikia milioni 14.8.
Kati ya wateja hao wa Vodacom, milioni 7.2 wanatumia M-Pesa na milioni 8.2 wanatumia huduma za intaneti.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya kifedha, M-Pesa iliingiza mapato ya Sh182 bilioni kutokana na kuongezeka kwa idadi ya wateja na hamasa ya watu kutumia huduma za kifedha kwenye simu za mkononi.
M-Pesa inachangia zaidi ya theluthi (asilimia 34.4) ya mapato yote ya huduma ya Vodacom Tanzania.
Hata wakati kampuni hiyo ikifurahia mafanikio hayo, Hendi amesema licha ya kuwa wanaendelea na uhamasishaji wa watumiaji wa simu kujisajili na alama za vidole bado ukomo wa kujiandikisha wa Desemba 31, 2019 ni moja ya vihatarishi katika biashara hiyo kutokana na uwezekano wa kupoteza wateja.
“Changamoto kuu inahusiana na gharama pamoja na upatikanaji mdogo wa vitambulisho vya Taifa hususan maeneo ya mikoani. Wakati tukiendelea na mikakati mbalimbali kuhusu jambo hilo, kuna wasiwasi wa kuwepo madhara makubwa iwapo wateja wasioandikishwa watazimiwa simu zao baada ya muda kufika,” amesema Hendi.
Mapema mwaka huu Serikali iliamuru watumiaji wote wa simu kuandikishwa kwa kutumia alama za vidole ikiwa ni moja ya njia imara za kukabiliana na uhalifu wa mtandaoni
.

No comments:

Post a Comment