
Da es Salaam. Kama ulipuuzia kujiorodhesha kwenye kanzidata, hii ni habari njema kwa watalaamu wa lugha ya Kiswahili nchini ambao walitii wito huo. Serikali imesema itayasambaza kwenye ofisi mbalimbali za ubalozi majina yaliyoorodheshwa kwenye kanzidata ya Baraza la Kiswahili la Taifa (Bakita).
Akizungumza hivi karibu wakati akizindua Mpango wa Kutahmini Uwezo wa Wakalimani katika ukumbi wa Bakita, Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe alisema tayari kuna wataalamu wa Kiswahili zaidi ya 1,000 ambao Bakita imewatambua kwenye kanzidata yake.
Pia,ameliagiza Baraza hilo lianze kuwaingiza kwenye kanzi data wakalimani ambao watakidhi vigezo kwenye kanzidata ya taifa ili watumike watakapohitajika na ikibidi waendelezwe zaidi.
Alisema suala la kuwapeleka walimu wa Kiswahili kwenye nchi ambazo zimeomba wataalamu linafanyiwa kazi kwa umakini na shughuli hiyo inakwenda vyema.
Alisisitiza kwamba Watanzania watambue kwamba sio rahisi kama watu wengi wanavyodhani kuwapeleka walimu wa kiswahili mara wanapoombwa. Alitolea mfano Afrika Kusini baada ya kutangaza kufundisha Kiswahili kwenye shule zake, wao upande wa serikali wameandaa andiko ikiwa ni hatua ya awali. Pia upande wa Afrika Kusini nao wanalazimika kubadilisha mtaalaa ambao mabadiliko hayo yanaratibiwa kisheria.
Dk Mwakyembe alisema ipo kasumba kwa baadhi ya Watanzania inapotolewa wito wao wanaanza kubeza na kujivutavuta. Mathalan alisema majirani zetu Kenya inakadiriwa tayari imeshaandaa zaidi ya watalaamu wa Kiswahili 40,000 wamejiandikisha kuchangamkia fursa ya kufundisha Kiswahili.
Akizungumzia kuhusu kazi ya kukusanya taarifa kwenye kanzi data, Katibu Mtendaji wa Bakita, alisema shughuli hiyo ni endelevu.
“Tumeweka utaratibu kuwafikia watu mbalimbali katika mikoa yote hapa nchini. Kazi nyingine ambayo inaendelea kwa sasa ni kuwafanyia tathmini wale wote wenye vipaji vya ukalimani kubaini uwezo wao iwe wamesoma taaluma ya ukalimani au hawajasomea.