Tuesday

Mambo ambayo huwezi kuyakwepa unapoanzisha ‘startup

0 comments



  • Baadhi ya mambo ni kuwa kamwe wateja wako hawataridhika na bidhaa zako na utalazimika kufanya kazi muda mwingi kuliko utakavyo. 
  • Utapoteza marafiki na ushindani utaongezeka zaidi. 

Kampuni zinazochipukia maarufu kama ‘startups’ zilizojikita katika ujasiriamali wa teknolojia imekuwa kimbilio la vijana wabunifu kutekeleza mawazo yao ili kuboresha maisha ya watu wanaowazunguka kwenye jamii. 
Huenda una ndoto ya kuanzisha au tayari una startup yako, ni muhimu kufahamu baadhi ya mambo ambayo hujaambiwa na watu wengine katika safari uliyoanza. Utakutana na mambo haya: 
Wateja wako hawataridhika kamwe
Haijalishi unatoa huduma nzuri kiasi gani, wateja wako wataendelea kukusumbua ili wapate huduma bora zaidi ya unazotoa sasa. Hiyo ni kwa sababu teknolojia inakua kwa haraka na kila siku zinavumbuliwa njia rahisi na bora za kutoa huduma. 
Ni jukumu lako kuisasisha (Update) teknolojia unayotumia kutoa huduma kwa kuzingatia mahitaji ya wateja wako ili kuhakikisha unaendelea kuwepo katika soko la ushindani. 
Dunia inaenda kasi ina watu wadadisi wa bidhaa na huduma, na wewe jitahidi kuwa mbunifu na kuwapa kile wanachikitaka kwa wakati muafaka. 
Wateja wako watakusumbua kila wakati ili tu kuwapa huduma na bidhaa wanazozitaka. Picha|Mtandao. 
 Utalazimika kufanya kazi kwa saa nyingi
Kutokana na umuhimu wa bidhaa na huduma unazotoa, wakati mwingine utalazimika kufanya kazi kwa saa nyingi. Jiandae kwa hilo! Wakati unaotaka kupumzika na familia yako mwishoni mwa wiki, zinaibuka kazi nyingi ambazo unatakiwa uzikamilishe ili usonge mbele. 
Kipindi hicho unaweza kuchukiwa na watu wako wa karibu, lakini unahitaji kujenga msingi ili biashara yako isimame na kuendelea kuwepo katika ulimwengu wa ushindani. 

Soma zaidi:

Hautakuwa na fedha za kukutosha
Haijalishi unapata pesa nyingi kiasi gani na kampuni yako inastawi kila siku, bado utajikuta katika hali ya kutaka pesa zingine. Kila siku utakuwa unawaza kufikia kilele cha mafanikio yako. 
Utawaza kuwekeza zaidi katika miradi na teknolojia mbalimbali ili tu uwe na vyanzo vingi vya mapato. 
Hata hivyo, pesa ni sehemu muhimu ya uwekezaji wowote unaoufanya. Endelea kuitafuta kadiri uwezavyo lakini fahamu hautaipata inayoweza kukutosha na kukidhi kile unachokitaka kwa asilimia 100. 
Utapoteza marafiki
Unapoanzisha startup, akili na fikra zinabadilika. Utajikuta unapenda kukaa na kujichanganya na watu wenye mawazo sawa na wewe. 
Hatua hiyo inaweza kukutenga na hata kukupotezea baadhi ya marafiki wasio wachapa kazi ambao umekaa nao kwa muda mrefu. Hiyo ni kawaida kwa sababu hakuna rafiki wa kudumu. 
Endelea kushikamana na marafiki wabunifu wenye ndoto za kufanikiwa katika maisha. Kupoteza marafiki inaweza kuwa njia kukufanya upate muda zaidi wa kutimiza malengo yako kwa wakati. 
Marafiki wengine watakurudisha nyuma kwa kile unachokifanya lakini usiwatazame, baki kwenye mstari wako. Picha|Mtandao. 
Ushindani utaongezeka
Kila hatua ya mafanikio katika biashara yako unayopiga utakutana na ushindani. Washindani wako hawatakuacha salama watafanya kila mbinu kuhakikisha wanateka soko la bidhaa au huduma unazotoa. 
Usitishwe! Ni kipindi cha kujiimarisha zaidi kwa kuwa karibu na wateja wako. Lakini ongeza ubunifu na fanya mambo tofauti na washindani wako. 
Wasome washindani wako ni maeneo gani hawafanyi vizuri ili utumie udhaifu wao kupanda juu zaidi. Biashara ni ushindani, hakuna atakayekuonea huruma unapoanguka. 
Wakati wote simamia kile unachokiamini kuhakikisha unakitekeleza kwa viwango vya ubora wa juu. Tambua bado una kazi kubwa ya kufanya kuifanya biashara yako kuwa endelevu.
 

No comments:

Post a Comment