Kwa watu wazima tatizo la kukojoa kitandani linasababisha matatizo kwenye jamii ikiwemo wachumba kuachana na baadhi ya ndoa kuvunjika kwa ajili ya kukosa uvumilivu na uelewa kuwa tatizo hili si makusudi ya muhusika na kuwa anahitaji kutiwa moyo na kusaidiwa.
Kama tatizo litaendelea baada ya miaka saba basi mzazi anaweza kuanza kutafuta tiba ya tatizo. Tiba ni pamoja na kubadili mfumo wa maisha, kumfundisha mtoto namna ya kudhibiti haja ndogo na dawa.
Dalili
Kufikia miaka mitano watoto wengi huwa tayari wana uweza wa kudhibiti haja. Kati ya miaka mitano na saba baadhi ya watoto wanakuwa na tatizo la kudhibiti haja ndogo na baada ya miaka saba wachache wanaendelea kuwa na hili tatizo.
Kukojoa kitandani inaweza kuwa ni dalili za ugonjwa mwingine ambalo linahitaji kutambuliwa na daktari. Mtakubaliana na mimi kuwa hata watoto ambao walishaweza kudhibiti haja ndogo, siku moja moja hujikuta wameshindwa kudhibiti na mara nyingi huwa ni dalili kuwa mtoto ana tatizo lingine. Pata ushauri wa daktari iwapo:
- Mtoto ataendelea kukoja akiwa na umri wa miaka zaidi ya saba
- Mtoto ameanza tena kukojoa kitandani baada ya kuacha kwa miezi kadhaa
- Iwapo kukojoa kitandani kutaambatana na maumivu, kiu isiyo ya kawaida ya maji, mkojo wenye rangi isiyo ya kawaida, choo kigumu au kukoroma
Chanzo cha kukojoa kitandani hakifahamiki vyema miongoni mwa wana sayansi ya tiba. Mambo yafuatayo yanahusishwa na kukojoa kitandani:
- Kuwa na kibofu cha mkojo kidogo. Mtoto anaweza kuwa na kibofu cha mkojo kidogo ambacho hakiwezi kuhimili kiwango na kasi ya mkojo unaotengenezwa. Hili ni jambo la kawaida kwani kumbuka mtoto bado anakua hivyo hata viungo vyake pia bado vinakua.
- Kushindwa kutambua kibofu kinapokuwa kimejaa. Mishipa ya fahamu ambayo inamsaidia mtu kutambua kuwa kibofu kimejaa inapokuwa haijakomaa vya kutosha. Katika hali hii ile hali tunayoihisi wengi wetu ya kibofu kuchoma au kuuma, baadhi ya wenye matatizo haya hawaihisi hasa wanapokuwa wamelala.
- Vichocheo hafifu. Wakati wa utoto vichocheo vinavyozuia mkojo usitengenezwe wakati wote vinakuwa hafifu hivyo kuruhusu kiwango kikubwa cha mkojo kutengenezwa hasa nyakati za usiku na kumfanya mtoto kushindwa kuhimili.
- Maambukizi ya njia ya mkojo (UTI). Kuwepo kwa hali hii kunaweza kusababisha mtoto kushindwa kudhibiti mkojo. Dalili za maambukizi haya ni pamoja na kukojoa kitandani, kukojoa mara kwa mara mkojo kidogo, mkojo kuwa na rangi ya pink au nyekundu na maumivu wakati wa kukojoa.
- Kukosa pumzi usingizini. Tatizo hili la kukosa pumzi husababisha kukatizwa katizwa kwa usingizi wa mtoto kwasababu ya kukosa pumzi, moja ya sababu zinazoweza kusababisha mtoto akakosa pumzi ni pamoja na mafindofindo (tonsillitis), kuvimba kwa tezi ndani ya pua (adenoids) ambazo humfanya mtoto kukoroma, kupumulia mdomo na anakuwa kama mwenye mafua wakati wote lakini makamasi hayatoki. Mtoto mwenye hali hii huwa na uwezekano mkubwa sana wa kushindwa kudhibiti haja ndogo.
- Kwa watoto ambao walishaweza kudhibiti haja ndogo muda mrefu lakini wakaanza kukojoa tena kitandani basi hii inaweza kuwa dalili kuwa mtoto ana kisukari. Kama tunavyofahamu kuwa kisukari ambacho hakijapata tiba husababisha kukojoa mkojo mwingi na mara kwa mara, kusikia kiu kuliko kawaida, kupungua uzito licha ya kula chakula kama kawaida na kuchoka kusikokuwa na maelezo.
- Tatizo sugu la kupata choo kigumu. Misuli inayosaidia kudhibiti haja kubwa ndiyo hiyo hiyo inatumika kudhibiti haja ndogo. Tatizo la kupata choo kigumu linapokuwa la muda mrefu,baada ya muda misuli inayohusika huchoka na kushindwa kufanya kazi yake kama inavyotakiwa hivyo kusababisha kushindwa kudhibiti haja ndogo.
- Matatizo ya uumbaji. Baadhi ya watoto huzaliwa na matatizo yanayohusiana na baadhi ya mifumo na viuongo vinavyohusika na udhibiti wa mkojo kutokamilika, mifumo hii inaweza kuwa ya fahamu au mfumo wa njia ya mkojo ambapo sehemu mojawapo kati ya figo, mirijia inayoleta mkojo kwenye kibofu au kibofu chenyewe.
Kukojoa kitandani kunaweza kumpata yeyote katika maisha yake hata kama hukuwahi kuwa na hilo tatizo. Kuna mambo mengine yanayoweza kuchangia na kumfanya mtoto awe kwenye uwezekano wa kukoja kitandani nayo ni:
- Msongo na wasiwasi (Stress). Mabadiliko ya mwili yanayohusiana na kubalehe huwa ni changamoto kwa baadhi ya watoto, kuanza shule mpya, au kulala ugenini vinaweza kumfanya mtoto kukojoa kitandani. Baadhi ya wazazi wameshakumbana na tatizo hili wanaposafiri na watoto, utawasikia wakisema “Nashangaa kwanini kakojoa huku, nyumbani huwa hana hili tatizo”
- Wazazi ambao walikuwa wanakojoa kitandani wakiwa wadogo wana uwezekano mkubwa wa kuwa na watoto wanaokojoa kitandani. Aina hii ya wazazi huwa hawana hofu sana ya mustakabali wa watoto wao kwani huwa wanajipa moyo kwa kusema “Hata mimi nilikuwa hivyo lakini niliacha baadae”.
- Baadhi ya wahusika huhusi kama kawaida kuwa kibofu kimejaa mkojo wakiwa ndotoni, na huota kuwa wameenda msalani au kajificha kichakani na kuanza kukojoa kumbe lahaula…!
Hakuna athari zozote za kiafya anazoweza kupata mtoto kwa kukojoa kitandani zaidi ya kukosa kujiamini na kuhisi anadhalilika. Pamoja na haya kukojoa kitandani kunaweza kuleta mambo yafuatayo:
- Kukosa kujiamini mbele ya wenzake
- Kushindwa kujichanganya na wenzake nje ya nyumbani. Watoto wenye tatizo hili hukataa kwenda safari za kimafunzo ambazo zitamsababisha alale nje ya nyumbani kwa kuhofia kukojoa kitandani kisha kuchekwa nk.
- Kupata harara (vipele) sehemu za mwili zinazokuwa zimeloana na mkojo. Kuzuia tatizo hili kabla ya kwenda kulala mtoto anaweza kupakwa mafuta ya mgando sehemu zote zinazogusana na mkojo.
Kama nilivyoeleza awali, ili mtoto aweze kutibiwa tatizo lake, ni vyema kwanza akapimwa ili kujua kama ana tatizo linalosababisha akojoe kitandani. Hivyo daktari atatumia utaalamu wake kumpima mtoto.
Matibabu
Watoto wengi huacha kukojoa kitandani wenyewe baada ya kukua. Baadhi ya wazazi hufanya juhudi mbalimbali zikiwemo zisizofaa za kumfanya mtoto aache kukoja kitandani. Nakumbuka zamani kulikuwa na kindumbwendumbwe ambapo mtoto kikojozi hupitishwa mtaani na nyimbo mbalimbali za kumfedhehesha ili aache, lakini wengi watakubaliana na mimi kuwa mbinu hizo ikiwemo kuchapa na kugombeza watoto hazikuwahi kusaidia chochote.
- Kubadili mfumo wa maisha kunaweza kusaidia pia kuondokana na tatizo hili, mfano kunywa kiwango kidogo cha kinywaji muda wa jioni. Kunywa maji kwa wingi ni vizuri kwa afya, hivyo basi tumia muda wa asubuhi na mchana kunywa maji mengi ili kuzuia usipate kiu jioni. Kwa watoto wanaopenda michezo wasizuiwe sana kutumia maji kwani huwa wamepoteza kiwango kikubwa cha maji michezoni.
- Kwa watu wazima waache matumizi ya vinywaji vyenye caffeine. Kwa mazingira yetu vinywaji hivi vinajulikana kama energy drinks.
- Watoto wanashauirwa kukojoa mara mbili muda wa jioni karibu na muda wa kulala.
- Kutibu kikamilifu tatizo lililotambuliwa na daktari. Kama ni uambukizo wa mkojo, kisukari au mafindofindo yanayomfanya mtoto kukosa pumzi nyakati za usiku basi yatibiwe.
- Kengele ya unyevunyevu (Moisture Alarm). Njia hii siyo maarufu sana miongoni mwetu. Hiki ni kifaa maalum ambacho kina sehemu mbili; ya kwanza ni sehemu ambayo inaweza kutambua unyevunyevu na sehemu ya pili inaweza kuwa kengele au kifaa chenye kutikisika au vyote kengele na kutikisika kama zilivyo simu za viganjani. Sehemu inayotambua unyevunvyevu hupachikwa kwenye nguo yake ya ndani ya mtoto sehemu ya mbele na kengele hupachikwa mkononi kati ya kiwiko na bega. Pale ambapo mtoto atakojoa tu kengele italia au mtikisiko utatokea au vyote kulingana na mtengenezaji. Hii itamfanya mtoto aamke na mara moja atadhibiti mkojo na kwenda msalani. Kifaa hiki lengo lake ni kumfundisha mtoto kudhibiti mkojo, zoezi hili huchukua muda wa miezi mitatu au zaidi kuweza kupata matokeo. 30% – 60% ya watoto wanaweza kusaidiwa kwa kutumia kifaa hiki. Kwa watoto wenye usingizi mzito sana inatakiwa awepo mtu mwingine ambae atasadia kumuamsha mtoto mara kengele inapolia. Matumizi ya kifaa hiki ni salama zadi kuliko dawa, hakuna maudhi au athari tokezi (side effects), mtoto akipona uwezekano wa kurudia kukojoa kitandani ni mdogo.
Pale ambapo mbinu zote zimeshindikana ndipo tunashauri mtoto apewe dawa. Dawa hizi zipo kwenye makundi mbalimbali kulingana na ufanyaji kazi wake.
- Zipo ambazo zinamfanya mtoto asilale kiasi cha kushindwa kujua kibofu cha mkojo kinapokuwa kimejaa. Dawa hizi hupewa mtoto saa 1 kabla ya kwenda kulala. Namaanisha dakika sitini kabla ya kwenda kulala na si saa moja jioni.
- Zipo ambazo zinapunguza uzalishwaji wa mkojo nyakati za usiku hivyo kufanya kibofu kuchukua muda kujaa.
- Zipo ambazo zinaongeza uwezo wa kibofu kuhimili mkojo mwingi (kutanuka zaidi) hasa kwa wale wenye vibofu vidogo.