Saturday

TAFSIRI KATIKA KAZI ZA KIFASIHI - MFALME EDIPODE

0 comments



Siku hizi tunakabiliana na changamoto kubwa sana katika mchakato wa kutafsiri vitabu kutoka lugha fulani hadi nyingine, mathalan kutoka lugha tajiri za kiulaya hadi kiswahili. Kwa jumla tunaambiwa kwamba mfasiri hana budi kutilia maanani vipengele vyote vya kiutamaduni — ingawa neno hilo utamaduni lina utata mwingi sana (soma HAPA), leo nitalichukua kama lilivyo — ambavyo aghalabu vina maana fiche katika fasihi. Kazi hiyo ni vigumu sana kwa kuwa inabidi mfasiri awe makini sana katika kazi yake, asije akaongeza au kupunguza dhana au mawazo fulani katika tafsiri zake. Katika ujumbe huu wa leo sitazumgumzia nadharia ya kiutafsiri jinsi ilivyopamba moto katika nchi za Ulaya hivi karibuni — ingawa ni hoja lililorudi katika mijadala ya wasomi, kwani wengi katika wana falsafa wa karne 18 na 19 walishalikabili swala hili —, bali nitatoa mifano miwili ambayo ilihusisha shughuli ya tafsiri ya vitabu viwili, cha kwanza tamthilia maarufu ya Sofokile (496–406 kabla Y.K.), Mfalme Edipode, iliyotafsiriwa zamani kidogo na Samuel S. Mushi na hekaya ya Saint Exupéry iliyotafsiriwa hivi karibuni na Philipp Kruse na Walter Bgoya.

Hapo sitaficha namna nilivyofurahia kusoma tena Mfalme Edipode, ambayo ni tamthilia ya misiba maarufu yenye thamani kubwa sana inayoendelea kutukuzwa na kusifiwa hadi leo tangu karne ya nne kabla ya Kristo. Hiyo tamthilia ni ya kusoma na kusoma tena, kwa maana ya kuwa na uwezo huo nadra ya kukarabati maumbile yetu na kukuza upeo wetu wa fikra. Si paukwa pakawa au hadithi fupi tunazozikuta katika magazeti ya kisasa — kwani mwandishi wa habari anajua fasihi maana yake ? — ambazo watunzi wao huzitunga kama watu wengine wanavyosiriba udongo ili kutomea kibanda chao kabla ya masika. Kusoma kwake kwa kiswahili kumenifurahisha sana kwa kuwa nimebaini kwamba tamthilia hii bado ina nguvu ya kutosha hata ikitafsiriwa katika kiswahili. Ila kuna kitu kimoja ambacho kimenitatiza kidogo katika nakala hii ya kiswahili kiasi cha kunitia wasiwasi, nacho kitu kinaambatana na neno hilo tragedyambalo lina maana mahususi. Kwa kifupi, tamthilia ya msiba ni aina ya maigizo ya huzuni ambayo si drama ya kawaida kama vile drama ya vichekesho au drama ya kiromansia (mfano V. Hugo). Hatuna budi kuainisha tamthilia hizi ili kuweka wazi fasili lililopo katika kila aina ya maigizo. Kwa mfano tunakuta katika dibaji ya Mfalme Edipode kauli ya S. Mushi inayosema kwamba tamthilia ya huzuni hukusudiwa kuwafundisha watu maadili au huambatana na mambo ya dini. Kwa maoni yangu, ufafanuzi huo hautoshi ili kupata maana kamili ya maigizo ya huzuni. Sote hapo tunaopenda tamthilia katika fani zake zote tunajua kwamba hata drama ya kawaida huwafundisha wasikilizaji maadili (licha ya riwaya ya kawaida). Isitoshe, michezo mingi katika mapokeo ya tamthilia ya Ulaya huambatana na dini, wala si maigizo ya huzuni.

Kauli nyingine husema kwamba mchezo huo wa huzuni lazima uwe na misiba. Na kweli katika michezo mingi ya aina hii, tunakuta mauaji mengi kama vile mwanamke anayeua mumewe, mama ya watoto anayeua wanawe, au mwanamme anayegundua kwamba amemwoa mamake baada ya kumwua babake. Lakini mauaji haya na misiba hii, pamoja na kwamba ni vigezo vikubwa vinavyotakiwa viwepo katika tamthilia ya aina hii, pia havitimizi malengo ya tamthilia ya huzuni kama havijachongwa na udrama unaozingatia majaaliwa ya binadamu. Kwa mfano, Edipode amemwoa mamake baada ya kumwua babake. Sawa, lakini kwa nini ? Ikiwa tunataka kupata jawabu sahihi hapo, hatuwezi kusema kwamba Edipode alitenda hivyo kwa sababu yote yanamhusisha yeye tu. Hapo tutakuwa tumekosa lengo kubwa la tamthilia hii. Mchezo huu si mchezo wa kawaida inayotuelezea mikasa na visa vya mtu fulani aliyeishi katika jamii fulani wakati fulani. Hapana. Matokeo yote yanayomkumba yanatuhusu pia kwa sababu Edipode si myunani tu, bali ni binadamu (kama sisi) ambaye hawezi kuepukana na mapatilizo — iwe adhabu au takdiri — aliyojaaliwa kukumbwa nayo.

Ndiyo maana tamthilia ya huzuni lazima iongezwe na kipengele kingine ambacho kikikosekana kinaweza kuathiri maudhui ya tamthilia husika, nacho ni majaaliwa. Hata hivyo, pamoja na kwamba kigezo hiki kinaelekea ni cha lazima katika michezo ya huzuni, tunakuta kuwa si katika michezo yote (hasa tukichambua ile ya Eoripide, 480– c.406 kabla ya Y.K.). Majaaliwa ni jambo linalotakiwa katika tamthilia hiyo lakini pia huendana na bahati, agano, ramli, na ajali. Kikubwa hapo ni kusisitiza kwamba hakuna tragedyisiyokuwa na binadamu (licha ya utamaduni wake, yaani mila na desturi zake) ambaye nadhari yake imezidiwa na nguvu — Zeo, miungu, daimoni, n.k . — ambazo si katika uwezo wake kuzipinga. Siyo kusema kwamba mhusika katika maigizo hayo hana hiari wala matakwa. Hata kama Edipode amenaswa katika maapizo mabaya, kitu ambacho kinatutosa katika udrama wa huzuni, tusisahau kwamba drama, katika lugha ya kiyunani, ni neno linalomaanisha kitendo. Edipode ni shujaa ambaye hakubali aliyotazamiwa, hupigania yale yale yanayomkusa ajitoboe macho yake, kwa kifupi ni mtu mwenye akili yake timamu ambaye ana uwezo wakuchagua, yaani kukiri au kukanusha, kupuuza au kusifu, kupenda au kuchukia, n.k. Ni mtu mwenye wajibu wake kamili, na ndiyo sababu ni mhusika anayeibua sura na taswira yakinifu katika mchezo mwenyewe.

Mushkeli niliyo nayo wakati wa kusoma tafsiri ya Samuel Mushi imenivaa hasa wakati wa kuelekeza mapitio yangu kwenye sehemu muhimu ya mchezo huo. Nitatoa madondoo kadhaa ili kuleta baadhi ya hoja muhimu ambazo zinanitia mashaka. Katika tafsiri ya Samuel Mushi, tunakuta :

- uk.4 Edipode anasema : « … nyote mna huzuni ziliwazidi binafsi nyoyoni, lakini moyo wangu walemewa na huzuni hiyo yenu, yangu, na ya jumuia nzima… »

Hapo mfasiri ametumia neno hilohuzuni ambalo si sahihi kwa kuwa mchezo chanzo unashadidia tukio la maajaliwa. Huzuni aghalabu ni aina ya majonzi inayosababishwa na jambo linalojulikana, kinyume na hapo ambapo Edipode anajiuliza kuhusu malalamiko ya raia wake na janga linaloukabili mji wa Thebe.

- uk. 12 Edipode anasema : « …kwa kuwa nimeshika nafsi yake (ya Laio), kitanda chake na mkewe halisi, ambaye kama ajali ‘ngeridhia, wanawe utu uzima kufikia, wangeleta uhusiano mwingine, na kati yetu kwa damu tuungane : naye, maskini, kapata msiba… »

Hapo sioni sababu ya kutumia msibawakati matini ya asili inatumia neno kama ajali. Katika mchezo husika tunasoma sentensi kama hiyo : ajali imeniangukia kichwani, badala ya naye maskini kapata msiba, wakati nenoajali linamaanisha kwa bahati mbaya, tofauti na majaaliwa ambalo linasisitiza mtiririko wa matukio ambao umesukwa na miungu (au nguvu zisizojulikana) na usioepukika.

- uk. 19, Teresia anamwambia Edipode : « … na pinga maneno yangu upendavyo, utatwezwa vibaya nchini humo, asivyopata kutwezwa binadamu… »
Hapo nakataa katakata. Kitenzi hikokutwezwa kina maana ya kuaibisha au kumvunjia mtu heshima, maana ambayo haipo katika mchezo chanzo unaotilia mkazo juu ya ajali. Sentensi asiliya husema kitu kama hicho :utaangamizwa na mapigo ya kiajali.

- uk. 33 : Edipode anasema : « …badala ya jibu linafurahisha, napewa kisa kinachosikitisha… ».

Hapo pia sikubali tafsiri hiyo kwa kuwa inapotosha maana halisi iliyomo katika tamthilia husika, kwa sababu Edipode hapo anaambiwa kwamba atakumbwa na balaa kubwa (sicho kisa) ambayo itatokezea kwa mujibu ya majaaliwa mabaya ambayo binadamu hushindwa kupambana nayo.

- uk. 36 : wazee wanasema : « Kitu niombacho ni kuishi, nitimize amri itokayo mbinguni kwa imani… ».

Pia mfasiri amekosea hapo kwa kukosa maana halisi ya tamthilia husika. Maneno ya wazee hapo yamepangwa hivi : laiti ningalijaaliwa kupata msaada kusudi nijitakasishe katika kutunga sentensi na vitendo vyangu vyote…

uk. 40 : Jokasta anasema : « Kuogopa ? Mwanamume awezaje kuogopa ?Maisha yetu ni bahati nasibu, hatujui mbele yatakayosibu… »

Hapo mfasiri amepoteza maana halisi ya matini chanzo ambayo inasema, kwa kufuatisha sentensi na maneno yale yale, « yupo mikononi mwa majaaliwa, kwa hivyo hatujui… »Bahati nasibu si majaaliwa (wala si ajali).


- uk. 53 : Edipode anasema pia : « …nimeangukiwa na ajali gani ? »

Hapo si ajali, bali majaaliwa.

Vigezo vyote tulivyogusia kwa juujuu ili kueleza manaa ya tragedyhaviridhishi kwa kuwa huzuni, misiba, huruma, tishio, mauaji, n.k. ni vipengele vinavyodhihirika katika tanzu nyingine zaidi ya tamthilia ya huzuni. Lakini tragedy ni tragedy, na Sofokile, Racine, Shakespeare waliotunga michezo mingi ya huzuni walijua maana halisi ya fani hii katika tamthilia. Endapo tutasoma zaidi michezo ya wasanii hawa, tutagundua kwamba tragedy hutusaidia kuelewa kwamba masaibu makubwa ambayo tunakabiliwa nayo katika maisha yetu hayana suluhisho wala utibabu — wala kusema hivyo si muono hasi kwani binadamu hufariki — ila tunapaswa kupambana nayo kwa ukakamavu, ushujaa na moyo wa kiuthabiti. Hiyo ndiyo maana na uzito wa tamthilia ya aina hii. Hiyo ndiyo dhima kuu ya tragedy.


Inaendelea.

No comments:

Post a Comment